Showing posts with label Udikteta. Show all posts
Showing posts with label Udikteta. Show all posts

7 Jan 2011













PICHA KWA HISANI YA VYANZO MBALIMBALI MTANDAONI.
INTELIJENSIA YA KUBASHIRI KUWA MAANDAMANO YA AMANI YATAISHIA KUVUNJA AMANI-IPO.INTELIJENSIA YA KUMJUA MMILIKI WA KAGODA HAIPO.INTELIJENSIA YA KUMTAMBULISHA MMILIKI WA DOWANS HAIPO!

BINAFSI NACHUKULIA AMRI YA KIKWETE ILIYOPELEKEA MAUAJI YA WATANZANIA WASIO NA HATIA ILITOKANA NA HASIRA YA YEYE KUTAJWA KUWA NI MMILIKI WA KAMPUNI YA KIJAMBAZI YA DOWANS.

LAKINI KWA VILE KIKWETE-NA DOLA YAKE ANAYOJIVUNIA KUWADHIBITI WANAOMTAKA AWAJIBIKE- AMEINGILIA JUKUMU LA MWENYEZI MUNGU KWA KUKATISHA UHAI WA WATANZANIA WASIO NA HATIA HUKO ARUSHA (HATUWEZI KUJUA KWA HAKIKA NI WANGAPI WAMEUAWA KWA VILE WATOA TAARIFA NI POLISI HAOHAO WALIOUA) BASI AMIN NAWAAMBIA MUNGU MTOA HAKI YA KWELI ATATENDA HAKI.HAKUNA MAHAKAMA YA TANZANIA INAYOWEZA KUMHUKUMU KIKWETE AU SAID MWEMA LAKINI TAYARI MAHAKAMA YA UMMA (COURT OF PUBLIC OPINION) IMESHATOA HUKUMU,NA TUNACHUSUBIRI NI HUKUMU KUBWA ZAIDI KUTOKA KWA MUUMBA WETU (MAANA KIKWETE KALEWA MADARAKA MPAKA KUINGILIA KAZI ZA MUNGU ALIYEMUUMBA).

KWA WAZALENDO WALIOUAWA-"KOSA" LAO LIKIWA KUTUMIA HAKI YAO YA KIKATIBA KUANDAMANA KWA AMANI-DAMU YENU HAIJAMWAGIKA BURE.KIKWETE NA WAPAMBE WAKE WATAJITAHIDI KUWAPACHIKA KILA MAJINA ILI KUHALALISHA KUWA MLISTAHILI KUUAWA.HATUWEZI KUMZUWIA KWA SASA.LAKINI KAMA DOLA ZA KIKOMUNISTI ZA ULAYA YA MASHARIKI ZILISAMBARATIKA LICHA YA MATUMIZI MAKUBWA YA NGUVU ZA DOLA,BASI IPO SIKU UBABE,UNYAMA,UUAJI NA USHENZI WA CCM UTAFIKA KIKOMO.

TUNAKUOMBA MUNGU MWENYE HURUMA NA UPENDO UZIREHEMU ROHO ZA MASHUJAA WETU WALIONYANG'ANYWA UHAI NA SERIKALI YA KIKWETE,NA TUNAKUOMBA UTOE ADHABU KALI KWA WAHUSIKA,HUSUSAN RAIS JAKAYA KIKWETE NA VYOMBO VYAKE VYA DOLA.KWA MUNGU YOTE YANAWEZEKANA. 

22 May 2010



Katika siku za hivi karibuni,Rais Jakaya Kikwete amekuwa akitoa kauli ambazo kwa namna flani zinaweza kupelekea uvunjifu wa amani.Sote tunakumbuka hotuba yake kali aliyotoa mbele ya walioitwa 'wazee wa jiji la Dar es Salaam' ambapo baadhi ya maneno yake yanaweza kabisa kuwatia jeuri wanadola wanapoagizwa kudhibiti wananchi.Kwa ujumla hotuba hiyo ilitawalia zaidi na kauli za ubabe na vitisho badala ya kuelimishana kistaarabu.Mbona ukali huo haukutumika kwenye hotuba yake ya Agosti 2008,ambapo pamoja na mambo mengine na kinyume na matarajio ya wengi,aliongea kwa upole na kukumbushia haki za binadamu kwa mafisadi.Nadhani msomaji unakumbuka kijembe alichotoa Spika Samuel Sitta kwa JK kwamba haki za wananchi ni za muhimu pia (tena zaidi ya za mafisadi).

Majuzi akarejea tena kauli ambazo kwa hakika zinapaswa kukemewa vikali.Kwanza, 'aliwapa jeuri' vijana wake wa UVCCM kwamba wasikubali kufanyiwa vurugu kipindi cha uchaguzi.Huku akitambua wazi kuwa yeye ni Amiri Jeshi Mkuu,na mwanajeshi mstaafu,bado alitoa uhuru kwa vijana hao 'kukabiliana na vurugu kama zile za katika baadhi ya chaguzi ndogo zilizopita'.Hivi Rais wetu anajifanya hajui kuwa wenye jukumu la kukabiliana na vurugu ni jeshi la polisi na sio UVCCM?Hivi kiongozi wetu huyu haelewi kwamba kuna uwezekano wa wahuni kujichanganya na vijana hao wa CCM kisha katika 'kukabiliana na vurugu za wapinzani' wakapelekea maafa,na halafu wakajitetea kuwa waliamriwa na Rais 'kudili na vurugu kwa namna hiyo'?

JK anapaswa kufahamu kuwa si yeye wala hao vijana wake wa UVCCM wako juu ya sheria au wana mamlaka ya kujichukulia sheria mkononi.Kwa kuruhusu hilo,Rais anaweza kuyapa changamoto makundi mengine katika jamii 'kufuata busara zake' na kuchukua sheria mkononi badala ya kuviachia vyombo vya dola vitimize wajibu huo.

Lakini ukidhani hiyo ndio kauli pekee ya kutisha kutoka kwa JK,basi hujaiskia hii.Akiwa ziarani huko Mtwara,Rais aliagiza msako wa nyumba hadi nyumba kusaka wanafunzi waliofaulu na kuchaaguliwa kujiunga elimu ya sekondari lakini hawajafanya hivyo kutokana na sababu moja au nyingine.Kwa mujibu wa gazeti moja,Rais alisema "ikibidi hata nguvu itumike" katika utekelezaji wa agizo hilo.Hivi JK anaweza kutueleza ni nguvu ya namna na kiasi gani itakuwa halali katika utekelezaji wa agizo hilo?Je Rais hadhani kuwa agizo lake linaweza kupelekea ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu kwa wanafunzi hao na wazazi wao?Kwanini badala ya msako uliopewa baraka za kutumia nguvu kusifanyike vikao kati ya wazazi wa wanafunzi hao na serikali ngazi ya mtaa,kata,au wilaya?Hivi Rais haelewi kuwa hata kama amri yake haitopelekea balaa kwa wanafunzi hao na wazazi wao (si unajua mgambo wanavyonyanyasa watu),na wanafunzi hao kupelekwa mzobe mzobe mashuleni,bado wanaweza kabisa kugoma kusoma wakiwa mashuleni?Shule sio sawa na baa ambapo unaweza kumpeleka mtu kibabe na kumshikia mtutu anywe pombe na akainywa kwa kuchelea matokeo.Kwa shule,hakuna namna unaweza kumlazimisha mtu asome na kuelewa.hata kama utampeleka shuleni kwa kikosi cha mizinga.

Je inawezekana kauli hizi za JK zinazobeba (au kuruhusu) matumizi ya nguvu zinatokana na ukweli kuwa yeye ni mwanajeshi mstaafu?Nauliza hivyo kwa vile kuna imani kwamba mentality anayojengwa askari jeshi huweza kudumu kwa mjeshi huyo kwa takriban muda wake wote wa uhai wake hata anapostaafu.

Kuna watakaotafsiri makala hii kama alarmist,yaani yenyebkubeba wasiwasi usio na msingi.Yote kheri,lakini tukumbuke kuwa pindi amani yetu ikivurugika kwa sababu ya matumizi mabovu ya nguvu ya uongozi wa umma,hakutakuwa na nafasi ya kuzuia uvunjifu wa amani.Kadhalika,ni vema kidhibiti dalili za udikteta kabla hazijaota mizizi na kushamiri.

Kwa bahati mbaya,au makusudi,ni kama watu wako usingizini (na usingizi wenyewe ni ule wa kupuliziwa dawa ya kulala bila kushtuka hata ukiangukiwa na paa).Namna mambo yalivyo ni kama watu 'wamekubali matokeo kabla ya kipenga cha mwisho'.Jeuri za watawala wanaopuuza haki za binadamu za wanyonge huimarishwa zaidi na 'usingizi huo wa pono'.Kama mtu anakufinya na wewe unazubaa tu,hutoi japo yowe,basi ni dhahiri kuwa sio tu mtu huyo atakubana zaidi bali pia ataamini kuwa huumii.

Amkeni!

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.