Showing posts with label Ushushushu. Show all posts
Showing posts with label Ushushushu. Show all posts

12 Oct 2016

Moja ya kazi ambayo inapendwa na kutamaniwa na watu wengi mno DUNIANI ni Uafisa Usalama wa Taifa, kwa jina jingine USHUSHUSHU.

Kuipenda au kuitamani fani hiyo kunachangiwa na ukweli kwamba, kwa upande mmoja ni eneo ambalo limekuwa maarufu mno kwenye filamu, na kwa hakika watu wengi wanapenda filamu za kishushushu.Ni nani asiyependa filamu za James Bond? Au series kama 24 na Homeland zinazohusu fani ya ushushushu?

Lakini licha ya filamu, kuna lundo la vitabu vya riwaya za kuhusu matukio halisi (non- fiction) au ya kutunga (fiction), na vingi ya vitabu hivyo ni 'vitamu' ukivisoma. Na sote twafahamu kuwa moja ya vitabu vilivyokuwa na bado vina umaarufu mkubwa mno nchini Tanzania ni vya Willy Gamba, shushushu mhusika katika vitabu vya Marehemu Eristablus Musiba.

Binafsi nilitamani kuwa shushushu nilipokuwa mtoto mdogo tu. Marehemu baba alikuwa na tabia ya kutusimulia kuhusu vitabu alivyosoma. Na kitabu cha kwanza hakikuwa cha kishushushu, bali story tu, kilichoandikwa na James Hadley Chase, "Come Easy Go Easy."

Baadaye alitusimulia kuhusu kitabu kimoja na James Bond, japo sikikumbuki jina. Kwa mara ya kwanza ndio nikafahamu kuwa kuwa watu wanaitwa 'ma-spy' na wanafanya kazi hiyo ya ushushushu. Fast forward miaka kadhaa baadaye, nikakutana na vitabu vya Willy Gamba, kuanzia "Njama," "Kikomo," "Kikosi cha Kisasi" na kadhalika.Kwa kweli kusoma vitabu hivyo vilikuwa kama kuangalia filamu. Tangu wakati huo nikatamani kuwa Willy Gamba.

Anyway, japo ushushushu kama tunavyoufahamu ni kwa ajili ya masuala ya usalama wa taifa, mbinu zinazotumiwa na mashushushu kusaka habari zinatumika katika maeneo mengine pia. Eneo linalotumia mbinu zinazoshibihiana zaidi na ushushushu ni uandishi wa habari.

Lakini eneo ambalo linanufaika na mbinu mbalimbali za kishushushu ni maisha yetu ya kila siku. Kwamba kuna mbinu mbalimbali za kishushushu ambazo zinaweza kumsaidia mtu wa kuwaida kufanikisha azma kama vile pale inapotokea mwenza mmoja kuhisi kuwa mwenzio anamsaliti au kupima uaminifu wa mwenza wako, kufahamu yanayoendelea 'behind the scene' katika masuala mbalimbali ya kimaisha,nk.

Je unahisi kuwa girlfirend/ boyfriend wako anaku-cheat? Je wahisi kuwa mumeo/mke 'anachepuka? Je unahisi kuwa binti yenu ameanza 'michezo michafu'? Je unahisi kuwa mtoto wenu wa kiume kaanza kujihusisha na makundi yasiyofaa? Je mshirika wako wa kibiashara ana ajenda ya siri dhidi yako? 

Ili uweze kupata majibu ya uhakika au yanayokaribiana na uhakika inabidi uwe shushushu, sio kwa ajili ya usalama wa taifa bali kwa ajili yako wewe mwenyewe au na mwenza wako au familia yako, nk.

Anza safari ya kujifunza ushushushu kwa kununua kitabu changu kuhusu taaluma ya Uafisa Usalama wa Taifa, kitabu pekee katika historia ya Tanzania, kinachoeleza kwa undani kuhusu taaluma hiyo. Ukifuatilia 'comments' za waliokwishasoma kitabu hicho utabaini kuwa wengi wamejifunza kutumia mbinu za kishushushu katika maisha yao binafsi.

Kwa wakazi wa Dar, unaweza kununua kitabu hicho na kuletewa hadi nyumbani, kazini, sehemu ya biashara, shuleni/chuoni, au hata kijiweni au pub.

Maduka ya vitabu jijini Dar na mikoani yanayouza kitabu hicho ni kama ifuatavyo


KARIBUNI SANA



11 Aug 2016

Makala hii maalum ya sauti inazungumzia kitabu changu kuhusu taaluma ya uafisa usalama wa taifa (ushushushu) ambacho sasa kinapatikana katika nakala dhahiri (hard copy). Makala hii inaeleza kuhusu nini kilichonisukuma kuandika kitabu hiki na pia inaeleza kwa undani yaliyomo kitabuni.




Check this out on Chirbit

5 Aug 2016


Kitabu kuhusu taaluma ya uafisa usalama wa taifa (ushushushu) kinapatikana kwenye maduka ya vitabu sehemu mbalimbali nchini Tanzania.

Kwa wanunuzi wa rejareja, kitabu hiki kinapatikana katika maduka ya vitabu yafuatayo


 Bei ya rejareja ni sh 15,000. 

Pia fursa hii ni kwa wenye vibanda vya kuuza magazeti au wachuuzi wa bidhaa za mkononi. Bei ya jumla kwa kila kitabu ni sh 8,400.

           KARIBUNI SANA


17 May 2016


"Hello world!" ndio ilikuwa tweet ya kwanza baada ya Idara ya ushushushu ya Uingereza inayohusika na kunasa mawasiliano, GCHQ (Government Communications Headquarters)  kujiunga na mtandao huo wa kijamii. 

Hawa jamaa, ambao makao yao makuu ni hayo pichani juu, ndio wenye jukumu la kusoma barua-pepe zetu, kusikia simu zetu na kutegesha vinasa sauti pale inapobidi, wamebobea kwenye hacking...kwa kifupi ukitaka kuwaelewa vema, m-Google yule jamaa anaitwa Edward Snowden..amewazungumzia vya kutosha, wao na washirika wao wa Marekani, wanaoitwa NSA.

Sasa hawa jamaa wameingia rasmi katika mtandao wa kijamii wa Twitter.



Hiyo tweet yao ya kwanza ya "Hello world" iliyoambatana na picha ya ndani ya ofisi yao, ina umuhimu wa aina yake kwa sababu ni programu ya kwanza kujifunza kuandika wakati mtu anapojifunza kundika kwa lugha ya ku - code katika  vile Java, Python, C, PHP, na Ruby.

"Kwa kujiunga na mitandao ya kijamii, GCHQ inaweza kutumia sauti yake yenyewe kuongea  kuhusu kazi muhimu tunayofanya kuiweka Uingereza salama," alisema Andrew Pike, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa taasisi hiyo ya kishushushu.

Taasisi hiyo ya kishushushu imeeleza kuwa inataka kufikika (accessible) na kuufahamisha umma kuhusu shughuli zake. Kadhalika, inataka majadiliano na watu wenye ufahamu wa teknolojia hususan katika maeneo ya teknolojia, hisabati, usalama mtandaoni na mada nyinginezo.




23 Jun 2015

Polisi jijini London hapa Uingereza wamemkamata Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa ya Rwanda, Jenerali Karenzi Karake, kutokana na maombi ya Hispania ambako anahitajika kwa makosa ya uhalifu wa kivita.

Jenerali Karake, Mkurugenzi Mkuu wa National Intelligence and Security Services alikamatwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Heathrow, Jumamosi iliyopita, kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na polisi wa hapa jana.

"Karenzi Karake, mwenye umri wa miaka 54, raia wa Rwanda, alifikishwa mbele ya mahakama ya Westminster, (jijini London)...baada ya kukamatwa kwa kutumia hati ya Ulaya ya kusaka watuhumiwa (European Arrest Warrant) kwa niaba ya mamlaka za Hispania, ambako anatafutwa kuhusiana na uhalifu wa kivita dhidi ya raia," ilieleza taarifa iliyotolewa kwa barua-pepe.

Jenerali huyo alirudishwa rumande hadi Alhamisi.

Haikuwezekana mara moja kuwasiliana na familia ya mkuu huyu wa ushushushu au mwanasheria wake nje wa muda wa kazi jijini London. Ubalozi wa Rwanda hapa Uingereza nao haujatoa maelezo yoyote.

Mwaka 2008, jaji wa mahakama kuu ya Hisania, Fernando Andreu, aliwatuhumu viongozi 40 wa kijeshi na kisiasa wa Rwanda, ikiwa ni pamoja na Jenerali Karake, kujihusisha na mauaji ya kisasi kufuatia mauaji ya kimbari yaliyoikumba nchi hiyo mwaka 1994.

Jaji huyo aliwaona watuhumiwa hao na hatia ya mauaji ya kimbari, ualifu dhidi ya binadamu na ugaidi, makosa yaliyopelekea vifo vya mamia ya maelfu ya watu ikiwa ni pamoja na Wahispania.

CHANZO: imetafsiriwa kutoka Matthewaid.com


12 Oct 2014

Kama mtu mwenye uelewa kiasi kuhusu utendaji kazi wa Idara yetu ya Usalama wa Taifa, nimekuwa 'nikipiga kelele' mara kwa mara kuhusu haja ya mageuzi ndani ya taasisi hiyo nyeti. Kwa bahati mbaya sio tu kelele hizo ni vigumu kueleweka kwa Watanzania wengi, uwezekano wa kusikilizwa ni mdogo hasa ikizingatiwa kuwa asili ya taasisi hiyo ni kutekeleza majukumu yake kwa siri, na kama hiyo haitoshi, mara nyingi wahusika wa taaluma hiyo inayopaswa kuhusisha matumizi ya hali ya juu ya akili, hawapendi kusikia ushauri wa 'walio nje' kama akina sie.

Mageuzi ninayoyapigia kelele ni ya kimfumo. Kubwa zaidi ni haja ya uwepo wa mazingira ya uwajibikaji pale watu wanapoboronga. Moja ya dhana zinazotawala fani ya ushushushu ni ile isemayo 'kushamiri kwa matishio ya usalama katika nchi husika ni dalili kuwa taasisi ya ushushushu katika nchi husika ina mapungufu.' Sasa huhitaji uelewa wa fani hiyo kutambua kushamiri kwa matishio kadhaa ya usalama katika Tanzania yetu, kubwa zaidi likiwa ufisadi. 

Labda waweza kujiuliza, iweje ufisadi uwe tishio la usalama? Jibu jepesi ni kwamba ufisadi unatoa fursa kwa maadui wa ndani na nje wa taifa kutimiza azma zao kwa urahisi. Kwa mfano, laiti kukiwa na ufisadi kwenye mipaka ambapo wahusika wanaruhusu kirahisi tu wageni kuingia nchini pasi kuzingatia taratibu zilizopo, ni rahisi kwa magaidi kutumia mwanya huo. 

Ufisadi unaweza kutuletea tapeli la kimataifa kuwekeza kwenye maeneo yanayofahamika kiusalama kama 'vituo muhimu' (vital installations) kama vile viwanja vya ndege na bandarini.

Sasa tukichukulia mfano wa ufisadi, sio tu umeshamiri vya kutosha lakini ndo wazidi kuongezeka. Kuna wanaojiuliza je TISS (Idara yetu ya Usalama wa Taifa) ipo likizo ndefu, wahusika wapo katika usingizi fofofo au kazi imewashinda? Mie sina jibu la moja kwa moja lakini nadhani tatizo la TISS ni la kimfumo zaidi kuliko kiutendaji, japo utendaji wao nao una walakini.

Lakini kabla ya kuingia kwa undani katika mada hii, nirejee kwenye kichwa cha habari. Majuzi, mkuu wa taasisi yenye jukumu la ulinzi wa viongozi wakuu wa Marekani, Secret Service, Bi Julia Pierson alilazimika kujiuzulu wadhifa huo baada ya mtu mmoja kuingia uzio wa Ikulu ya nchi hiyo na kutishia usalama wa Rais Barack Obama. Kwa wenzetu tukio hilo lilikuwa na uzito mkubwa sana, na lilitawala sana katika vyombo vya habari.


Hata hivyo, kwa vile wenzetu wanaendesha mambo kwa uwazi, mwanamama huyo aliitwa mbele ya kamati moja ya bunge la juu la nchi hiyo na kupewa fursa ya kuieleza, ambapo watunga sheria waliafikiana kwamba anapaswa kujiuzulu.
Tukirejea huko nyumbani, ukweli usiopingika ni kwamba licha ya vikwazo vya kimfumo vinavyoikabili TISS, ksingizio  cha 'taasisi hii yafanya kazi kwa siri na hakuna anayepaswa kuhoji' kinatoa fursa kwa wazembe kupata kinga katika utendaji wao mbovu. Ndio, kazi za TISS ni za siri lakini so far usiri huo haujafanikiwa kuwawezesha kukabiliana ipasavyo na matishio ya kiusalama, la wazi likiwa ni ufisadi.

Miongoni mwa mapendekezo yangu (yapo mengi) kuhusu haja ya mageuzi ni kama ifuatavyo.

Kwanza, uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu unapaswa kufanywa kwa uwazi zaidi, ikiwezekana kuidhinishwa na Bunge. Hiyo itazuia uwezekano wa Rais kumpatia wadhifa huo mtu yeyote yule bila kuzingatia uadilifu na uwezo wake kikazi. Kwa kumpa Rais 'blank cheque' ni rahisi kwake kumchagua mtu wake, au mshkaji wake kwa minajili ya kumlinda au kuwa kibaraka wake badala ya kulitumikia taifa kiufanisi.
Pili, ni muhimu TISS kama taasisi iwajibike kwa umma, na si kwa Rais pekee (maana huyo Waziri Katika Ofisi ya Rais mwenye jukumu la kuisimamia TISS anakwazwa na mazingira yalivyo, sambamba na 'uoga' wa kawaida). Ifike mahali, watendaji wakuu wa TISS waweze kuitwa Bungeni, kwa mfano, kuhojiwa kuhusu masuala mbalimbali yanayoihusu taasisi hiyo.

Kiutendaji, ni muhimu kwa taasisi hiyo kupewa uhuru wa kioperesheni utakaoiwezesha kuondokana na hali iliyopo sasa ambapo kwa kiasi kikubwa imekuwa kama tawi la usalama la chama tawala. Sambamba na hilo ni haja ya kuitengenezea mazingira yatayoiwezesha kuhakikisha mapendekezo yake kwa Rais yanafanyiwa kazi hata pale Rais anapoyapuuza. Ikumbukwe kuwa licha ya Rais kuwa 'mkuu halisi wa TISS,' yeye bado ni mwananchi kama wananchi wengine ambao TISS inawajibika kuhakikisha sio tu usalama wao bali hawawi tishio kwa usalama huo. Rais anapopuuza ushauri unaotishia usalama wa taifa basi TISS ijengewe mazingira ya kuhakikisha kuwa ushauri wake unafanyiwa kazi.

Nimalizie kwa kutumaini kuwa 'kelele' hizi zitasikika kwa wahusika. Tujifunze kwa wenzetu waliotatutangulia na wahusika wasione aibu kusikia ushauri wa wenye uelewa hata kama wapo nje ya 'uwanja wa mapambano.'

Endelea kutembelea blogu hii kwa habari mbalimbali, ikiwa ni pamoja na hizi za ushushushu (bonyeza hapo kwenye menu ya INTELIJENSIA upelekwe moja kwa moja)





Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.