Showing posts with label VITA DHIDI YA UFISADI. Show all posts
Showing posts with label VITA DHIDI YA UFISADI. Show all posts

28 Mar 2012

Humiliation: Jose Gonzales has to stand carrying this sign on a street corner after his father caught him stealing $100 from his cousin
Pengine badala ya kuwabebesha mzigo walipa kodi kwa kuwapeleka gerezani mafisadi (ndoto isiyowezekana)-ambako watakula na kulala bure- adhabu mwafaka kwao ingekuwa kuwatembeza mitaani wakiwa wametundikwa mabango yenye kueleza makosa yao.Na hapa chini tunapewa darasa mwafaka la namna ya kutekeleza adhabu hiyo ya kudhalilisha.

Mzazi mmoja huko Denver nchini Marekani aliamua kumpa mwanae adhabu ya kutembea na bango linalotamka bayana kuwa "Mie ni mwizi, nimeiibia familia yangu." Angalia picha hapo juu pamoja na video hapo chini, kisha bonyeza kiungo kusoma habari kamili



CHANZO na kwa habari kamili: Daily Mail

12 Mar 2010

 Habari zilizotawala vyombo vya habari vya hapa Uingereza ni kufikishwa mahakamani kwa wabunge watatu wa chama tawala (Labour) na mbunge wa bunge la mabwanyenye kutoka chama cha Conservatives.Kwa pamoja wabunge hao wanatuhumiwa kufuja fedha .Wabunge hao, Elliot Morley, David Chaytor na Jim Devine wa Labour na Lord Hanningfield wa Conservatives wanashtakiwa kwa ubadhirifu wa jumla ya takriban pauni 60,000 za mafao ya wabunge.Wakati hayo yakitokea hapa katika nchi ambayo ni wafadhili wetu wakubwa,hadi muda huu sie tumeendelea kuwekwa kizani kuhusu mdudu aitwaye Kagoda,huku mtuhumiwa wa ufisadi wa rada na wale wa ujambazi wa Richmond wakiendelea "kupeta". Ni dhahiri kwamba watawala wetu hawako serious na mapambano dhidi ya uhalifu wa vigogo.Hebu angalia mfano mwepesi wa ishu ya mtangazaji wa TBC,Jerry Muro.Japo blogu hii si mahakama ya kuamua kama mtangazaji huyo hana hatia au,kasi ya vyombo vya dola katika kushughulikia 'tuhuma' dhidi yake zilikuwa kubwa sana tofauti na namna vyombo vya dola vinavyojiumauma hadi leo kuhusu majambazi wa kampuni ya Kagoda waliokwiba shilingi bilioni 40 katika utapeli wa EPA.Watawala wetu wameendelea kuweka pamba masikioni na kupuuza kilio cha umma kuhusu haja ya angalau kutajiwa wamiliki wa kampuni hiyo ya kijambazi.

Ndio maana blogu hii imeendelea kuiona sheria mpya ya kudhibiti rushwa katika chaguzi kuwa ni mwendelezo wa ahadi lukuki za kunoresha ustawi wa taifa letu lakini ahadi hizo zimeendelea kuwa viinimacho visivyotekelezeka.Sheria hii inaweza kupelekea waheshimiwa wawili watatu kutiwa nguvuni (kama TAKUKURU watashikiwa silaha kuwezesha hilo), vichwa vya habari vitasomeka kwa herufi kubwa kwamba sheria imeanza kufanya kazi.Lakini kana kwamba wana ugonjwa wa kusahau historia,baadhi ya wanahabari wetu watazembea kurejea matukio ya nyuma ambapo kesi kama za akini Profesa Mahalu,na hizi za karibuni za Mramba na Yona zinaendelea kusuasua mahakamani pasipo dalili za haki kutendeka-kwa watuhumiwa na walipakodi wa Tanzania.

Watakaonaswa baada ya sheria hiyo 'kuanza kutumika' watakuwa mithili ya 'muzi wa kafara',na 'changa la macho' kuonyesha umma kuwa sheria inafanya kazi lakini mwisho wa siku itaishia kuwa 'flani kafikishwa mahakamani',and that's it.Suala sio kumfikisha mtuhumiwa mahakamani bali haki itendeke,na sio itendeke tu bali ionekane imetendeka.

Yayumkinika kusema kuwa kesi za EPA zinazoendelea kwa mwendo wa kinyonga hazikidhi haja ya umma hasa kwa vile japo wote ni watuhumiwa lakini wale wa Kagoda waliiba fedha nyingi zaidi.Cha kushangaza ni kwamba hadi leo wameendelea kuhifadhiwa.Sasa tukisema ufisadi ni sera ya CCM tutaambiwa tumekosa nidhamu?

Tukio la kufikishwa mahakamani kwa wabunge hawa wa Uingereza kunapaswa kutufumbua macho kwa vile kama nchi inayotufadhili iko hailei wabadhirifu iweje sie tunaotegemea misaada tunakuwa na 'sintofahamu' katika kuwachukulia hatua mafisadi?Hivi kuna sababu za msingi kwanini hadi leo Mzee wa Vijisenti Andrew Chenge hajafikishwa mahakamani kuhusu vijibilioni vyake huko visiwani Jersey?Basi hata kama wanamwonea aibu,yaani CCM wanashindwa hata kuona haya kwa mtuhumiwa huyo kuwa mwenyekiti wa kamati yake ya maadili?Au ufisadi ni sehemu ya maadili katika chama hicho?

Wakati tukiendelea kuaminishwa kuwa sheria hiyo ya kudhibiti rushwa kwenye chaguzi itakuwa 'kiboko' ya rushwa,toleo la wiki hii la gazeti la Raia Mwema lina habari kuwa rushwa inamwagwa katika majimbo kadhaa kama wahusika hawana akili nzuri.Sijui huko ni kumkejeli Rais Kikwete aliyetamka bayana kuwa atasaini sheria hiyo kwa mbwembwe au ni kuujulisha umma kuwa CCM na rushwa ni damu damu!Kilicho wazi ni kuwa hakuna mgombea wa CCM atakayefanikiwa kupitishwa na chama hicho pasipo kutoa rushwa.Hilo halihitaji mjadala.Na kama Rais Kikwete anaamini kuwa sheria anayoipigia jaramba itakomesha rushwa kwenye chaguzi,basi ni vema naye akatafakari upya kama kuna umuhimu wa kuendelea kuwa kiongozi wa watu wasioafikiana na mtizamo wake.

Kinachosikitisha zaidi ni namna jamii isivyoonekana kukoseshwa usingizi na namna nchi yetu inavyozidi kutafunwa na mafisadi.Angalia mwitikio wa wananchi kuhusu 'makamanda wa vijana' wa CCM.Hivi watu hawajiulizi hawa makamanda walikuwa wapi siku zote kiasi cha kukurupuka ghafla kufishana makoti na joto lote hilo kwa kifuniko cha 'ukamanda wa vijana'?Na huo ukamanda unawasaidiaje vijana husika?Kwanini makamanda hao wasielekeze nguvu zao katika kupambana na ufisadi? Kwa asiyefahamu 'siri ya ukamanda wa vijana' basi aelewe kuwa kila anayevikwa wadhifa huo ni 'mgombea mtarajiwa'.Ni namna ya kujiweka karibu na wapiga kura.

Lakini sina tatizo sana na makamanda hao bali hao wanaoaminishwa kuwa ili waendelee wanahitaji makamanda wa vijana.Mie ni muumini mkubwa wa wazo kwamba UFISADI ni kikwazo nambari wani cha maendeleo yetu,au sababu kubwa ya kwanini tumeendelea kuwa masikini wa kutupwa licha ya utajiri lukuki wa maliasili tulionao.Logic yangu ni simple.Huwezi kujaza maji kwenye ndoo yenye matobo au kujaza upepo kwenye mpira uliotoboka.Paipo kudhibiti ufisadi na mafisadi,maendeleo yataendelea kuwa ndoto inayogeuka ukweli mchungu kila kukicha.

Na tukitegemea kwamba wanufaika wa ufisadi watajumuika nasi katika kukomesha kilekile kinachowawezesha 'kutanua' na ma-vogue,mahekalu ya bei mbaya na nyumba ndogo zisizohesabika basi tutaendelea kusubiri milele,au kwa lugha nyingine,TUANDIKE TUMEUMIA.

FUNGUKA MACHO,WAKATI NI SASA!.

10 Feb 2010


Baada ya danadana za muda mrefu ndani na nje ya bunge,hatimaye mjadala wa ujambazi wa Richmond umefungwa rasmi.Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana kutoka Dodoma,bunge limeridhia taarifa ya utekelezaji wa Azimio lake kuhusu suala la Richmond.Kwa lugha nyepesi,wawakilishi wetu wameridhia ujambazi uliofanywa na wahusika wa mradi huo wa kitapeli.

Kama ilivyo ada,CCM imeendelea kutumia wingi wa wabunge wake kuhakikisha kuwa matakwa yake yanatimia hata kama ni kinyume na matarajio ya Watanzania walio wengi.Wingi wa wabunge wa CCM umeendelea kuwa nyenzo muhimu kupunguza/kuondoa umuhimu wa wabunge kutoka vyama vya upinzani

Inasemekana kwamba msimamo wa pamoja wa wabunge wa CCM ulifikiwa katika kikao chake cha "kuwekana sawa",utaratibu uliiota miziz ndani ya chama hicho kila linapojiri jambo linaloashiria upinzani kwa ajili ya maslahi ya wananchi.

Wabunge wote walioamua kuzika mjadala wa Richmond ni sawa na wasaliti kwa vile nafsini na akilini mwao wanafahamu bayana kuwa namna pekee ya kumaliza suala hilo ilikuwa kwa wahusika kuwajibishwa.Madhara ya muda mrefu ya usaliti huo ni uwezekano wa kusambaa kwa virusi vya ufisadi ambavyo vinatambua bayana kuwa vina ulinzi wa kutosha kutoka chama tawala.

Kulikuwa na ugumu gani kuagiza suala hilo lipelekwe mahakamani ili kama wahusika walionewa basi iwe hivyo,na kama waliliingiza "mkenge" taifa basi wavune walichopanda?Hizi siasa za kulindana zitaendelea mpaka lini?CCM wanasahau kwamba hiki ni kipindi cha mpito tu,watafanya maamuzi ya kulindana mpaka wachoke,lakini siku ya siku watajilaumu kwa uzembe wao katika maamuzi.

Na kama kuna wa kusutwa basi na wale waliokuwa wakipata huku na kule wakijitambulisha kuwa ni "makamanda wa vita ya ufisadi".Nimeshaandika mara kadhaa kuhusu tunavyodanganyika kirahisi kila tunapowasikia akina Sitta wakidai "wanahujumiwa kwa vile wamesimama kidete kwenye mapambano dhidi ya ufisadi".Kwanini mapambano hayo yabaki ya kihisia/kufikirika zaidi kuliko vitendo?I just hope kwamba uamuzi wa kuzika hoja ya Richmond utajumuisha pia kuzikwa kwa kundi la wanafiki wajiitao "makamanda wa vita ya ufisadi".Kama ni makamanda basi ni wa mbao (wooden soldiers).

Lakini wenye uchungu wa dhati na nchi yetu bado wana fursa kubwa tu ya kutoa hukumu yao hapo Oktoba mwaka huu.Naendelea kuamini kuwa njia pekee ya kuikomboa Tanzania kutoka kwenye lindi na umasikini na bahari ya ufisadi ni kwa kuiondoa CCM madarakani.Tusitarajie lolote jipya kutoka kwa chama hicho kilichochoka kimawazo na kilichoishiwa na uwezo wa kutawala.Kuendelea kukiweka madarakani ni kukionea tu kwa vile kimeshatuthibitishia vipaumbele vyake.

Akina Muro wakituhumiwa rushwa basi hata kichanga kilichozaliwa jioni hii kitatambua namna dola "inavyowajibika".Yakija masuala ya akina Lowassa,Chenge,Kamragi,Msabaha na watuhumiwa wengine basi zinaanza ngonjera moja baada ya nyingine.Sasa kama walikuwa wanajua hatma ya mazingaombwe haya ni hii basi kulikuwa na haja gani ya kutuzingua kila kilipojiri kikao cha bunge?Na kama kawaida ya mengi ya magazeti yetu,danganya toto kuwa "bungeni hapatakalika kwa mjadala wa Richmond,Kiwira,TICTS,nk" ziliendelea kutawala vichwa vya habari.

Sababu nyingine ya ziada ya kuinyima CCM kura yako hapo Oktoba.

28 Oct 2009


SERIKALI imeshutumiwa kwa kuibua hoja ya 'posho mbili' kwa wabunge ili kuzima kashfa ya Kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond Development (LLC) iliyobuni mkataba wa kifisadi kati yake na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Shutuma hizo zinakuja baada ya vyombo vya habari mbalimbali kutangaza jana msuguano uliojitokeza kati ya Spika wa Bunge, Samuel Sitta aliyetoa hoja kusitishwa kwa wabunge kuhojiwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kusisitiza kuwa zoezi hilo litaendelea kwa sababu ni agizo kutoka katika Ofisi ya Rais, Ikulu.

Takukuru imekuwa ikiwahoji baadhi ya wabunge, wengi wao wakitajwa kuwa ni miongoni mwa wanaojipambanua katika kupiga vita ufisadi, kwa madai ya kupokea posho mara mbili, kufuatia malalamiko ya baadhi ya idara na taasisi kuwa kamati za Bunge zinadai posho mara mbili.

Sambamba na hoja ya 'posho mbili' za wabunge kwa kazi moja, kuendelea kujadiliwa katika nyanja mbalimbali za kijamii, pia mjadala mkali umekuwa ukiendelea katika mtandao maarufu wa 'wanajamii'.

Mchangiaji mmoja, Richard Mabala alisema anashangaa kuona serikali imeamua kuchagua kupambana na baadhi ya wabunge wakati suala la 'posho mbili' ni utamaduni wa miaka mingi bungeni.

"Mwaka juzi nilipotumwa kazi na wafadhili kuonana na kamati moja ya Bunge, vivyo hivyo walitengewa vijisenti vyao, wakiwemo mawaziri na mawaziri wastaafu ndani ya Bunge, mashirika ya jamii na wafadhili," ameandika.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge iliyochunguza kashfa hiyo ya Richmond, juzi alizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma na kusema kuwa kitendo hicho cha Takukuru ni cha kisasi na kuwa kamwe hatokubali kuhojiwa.

Jana Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Juma Haji Duni alisema serikali inaogopa matokeo ya sakata la Richmond na inataka kutumia suala la wabunge kupokea posho mara mbili kama njia ya kutokea, baada ya kukwama kutekeleza maazimio ya Bunge kwa zaidi ya miezi sita sasa.

"Waziri Mkuu Mizengo Pinda na serikali yake anaogopa Richmond, anakazania wabunge wahojiwe kwa kuwa anaona hapo ndio mahali pa kutokea, wanajaribu kukwepa hoja ya msingi," alisema.

Alisema ikiwa serikali ina sura mbili moja ikiwa ya ufisadi na ndio sababu inachelea kuchukua hatua za wazi zilizopendekezwa na kamati ya Bunge kuhusu watendaji wake.

"Kama serikali ina sura mbili, moja ya kifisadi; ingekuwa makini ingewachukulia hatua wote kama ilivyopendekezwa na Bunge. Sasa inashangaza kwa kushupalia posho za wabunge na kuwahoji ikitafuta pa kutokea," alisema Duni na kuongeza:

"Kama serikali ipo makini kwa nini haijasema wazi ni nani waliorejesha fedha za EPA? Si kweli kama posho za wabunge ndiyo suala kubwa kwa sasa. Serikali iache unafiki kwani, kama posho si wabunge pekee hata watendaji wa serikali wanakula mara mbili."

Alisema, Pinda anajipapatua, huo ni unafiki wa serikali kutaka kufunika hoja ya Richmond na kwamba, kama wana umakini mbona waliorejesha fedha za EPA hawatajwi mpaka leo. Kama Takukuru wapo 'serious' (makini) kwa nini hawakulisemea hilo mwanzo wanasubiri wakati huu wa mkutano wa Bunge."

Aliongeza kuwa lililo mbele ni Bunge kuachiwa lifanye kazi yake na wabunge wafanye kazi yao na iwapo serikali kupitia Takukuru inahitaji kuwahoji basi isubiri kumalizika kwa mkutano wa Bunge.

Kauli hiyo ya Naibu Katibu Mkuu wa CUF iliungwa mkono na Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Hamad Rashid Mohamed (Wawi-CUF) aliyesema kuwa ingawa hana tatizo na Takukuru kutekeleza wajibu wake, lakini hofu yake ni wakati gani inatekeleza wajibu huo na kama Bunge ambalo pia lina kanuni zinazoweza kufanyia kazi madai hayo limeshindwa kufanya hivyo.

"Ingawa sheria za nchi hazikatazi mtu kuhojiwa wakati wowote, lakini kila jambo lina wakati wake. Kama Takukuru imefanya hivyo ili kudhoofisha nguvu za wabunge kutetea maslahi ya taifa, basi wajue hakuna mtu yeyote anayeweza kulizuia Bunge kufanya kazi yake," alisema Hamad na kuongeza:

"Bunge lisizuiwe kufanya kazi yake. Hata kama litawavuruga wachache bado tutasimamia haki kwani waliobaki pia ni nguvu ya umma, kwa kuwa ni wawakilishi wa wananchi na wana nguvu na uwezo ule ule".

Kwa upande wake Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe amewasihi wabunge wenzake kukubali kuhojiwa na Takukuru kama njia pekee ya kujisafisha mbele ya umma kuhusu tuhuma za kulipwa posho mara mbili kwa kazi moja.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi ofisini kwake bungeni mjini Dodoma jana, alihadharisha kuwa endapo umakini na busara haitatumika katika suala hilo, kashfa hiyo inaweza kuliondolea Bunge heshima ambayo chombo hicho kimejijengea kwa wananchi.

“Sisi wabunge tunapopinga kuhojiwa na chombo cha dola tunatoa taswira mbaya kwa jamii…tunaweza kuharibu hii sifa tuonekane kuna mambo tunayafanya halafu tunajificha na kinga ya Bunge…kinga inatulinda kutoa maoni na michango yetu ndani ya Bunge tusishtakiwe,”alisema Zitto.

Katika mtazamo tofauti Mwenyekiti wa Taifa wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema anayachukulia mabishano hayo sawa na ya vibaka wawili wanaogombana kila mmoja akitaka kumuwahi mwenzake.

“Takukuru ni questionable (wanatuhumiwa) na wabunge nao pia ni ‘questionable’. Sasa imekuwa ni sawa na vibaka wawili ambao wanapambana na sasa inategemea ni kibaka yupi atamuwahi mwenzake.” alisema Mbatia.

Alifafanua kuwa katika mazingira ya sasa wabunge, wanatuhuma na wanapaswa kuchunguzwa na suala la Richmond nalo linapaswa kuchukua nafasi yake, hivyo Takukuru wasizuiwe kufanya kazi zao kama Bunge nalo lisivyotakiwa kuingiliwa.

Naye Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ambaye pia ni kijana aliyeinukia kwa kasi kisiasa nchini katika miaka ya karibuni, Nape Nnauye, alisema anatilia shaka uhalali wa Takukuru kutekeleza kazi yao wakati huu wa Mkutano wa Bunge, hasa ikizingatiwa hoja nzito zinazotarajiwa kujadiliwa.

"Mazingira ya sasa tuna sakata la Richmond na bado halijaisha na mmoja wa wanaotuhumiwa ni Mkurugenzi wa Takukuru. Hata kama operesheni yao ni 'genuine' (halali) tunaweza tukafikiri ni kuzuia wabunge wasitekeleze wajibu wao," alisema Nnauye.

Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Usu Malya alielezea kitendo hicho cha Takukuru kuwa ni cha kuwadhalilisha wabunge na kuongeza kama ni suala la kutolewa posho mara mbili kwa wabunge, Bunge kupitia kamati yake ya maadili lingeweza kujadili na kutoa ripoti.

"Tunaamini wabunge wetu wamekuwa wakijadili kwa uwazi mambo yote kwa maslahi ya umma. Suala hilo pia wangeweza kulifanyia kazi. Kitendo cha Takukuru kwenda kuwafuatilia mimi naona ni cha kuwashushia hadhi," alionya Usu.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Dk Edward Hosea, ametia ngumu akitaka uchunguzi dhidi ya wabunge uendelee akisema : "Hakuna mtu aliye juu ya sheria."

Kauli hiyo ya kwanza ya Dk Hosea tangu kuanza uchunguzi huo ambao sasa umefikia hatua ya juu zaidi, inakuja kipindi ambacho tayari kumeibuka msuguano kati ya mihimili miwili ya dola, ambayo ni Bunge na Serikali.

"No one is above the Law..., no matter who are you (Hakuna aliye juu ya sheria, bila kujali wewe ni nani)," alisema Hosea na kuongeza:

"Sisi tunafanya kazi kwa mujibu wa sheria na katiba, kwa hiyo hatuangalii nani ni nani zaidi ya sheria na katiba".

Mapema mwaka huu Dk Hosea alionya wabunge kwamba, wakianza mchezo wa kuumbuana hawatasalimika, kwani kumekuwa na taarifa na ushahidi wa kutosha kuhusu ufisadi wao wa kuchukua posho mara mbili.

Akionyesha kutimiza azma hiyo, Hosea alisema hapendi malumbano na wanasiasa kwani yeye si mwanasiasa mwenye jukwaa kama Bunge, ila atasimamia sheria.

"Wanaweza kusema mambo mengi, mimi si mwanasiasa sipendi malumbano na wanasiasa, wao wana audience (hadhara) mimi sina, wana Bunge na wanaweza kukaa bungeni na kuzungumza chochote," alifafanua Hosea na kusisitiza:

"Lakini kwa kifupi ni kwamba, msimamo wa Takukuru uko wazi, ni kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na katiba basi, hakuna jambo jingine".

Alipoulizwa endapo uchunguzi huo una msukumo na nguvu za aina yoyote nje ya sheria na utendaji kazi wa kawaida wa Takukuru, alijibu: "Nasisitiza, sipendi malumbano na wanasiasa, wanaweza kusema mengi, lakini tunasimamia sheria tu".

Msuguano huo unaondelea kati ya mihimili hiyo miwili ya dola, pamoja na mambo mengine unaweza kuliingiza Bunge la Tanzania katika kashfa mbaya ya matumizi mabaya ya fedha za umma kama ilivyokuwa kwa Bunge la Uingereza.

Tayari hadi sasa, wabunge wengi wakiwa ni kutoka Kamati ya Nishati na Madini wakiongozwa na Shellukindo mwenyewe, wamekwishahojiwa kutokana na tuhuma hizo.

Kwa mujibu wa habari ambazo gazeti hili imezipata, karibu wajumbe wote 21 kutoka Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma wamekwishaitwa kuhojiwa huku mwenyekiti wao Zitto akiwa njiani.

Baadhi ya wabunge kama James Lembeli wa Kahama na Dk Mwakyembe, walikwishaitwa kuhojiwa lakini hadi sasa hawajafanyiwa hivyo, huku mbunge huyo wa Kyela akiweka bayana kwamba, hayuko tayari kuhojiwa na Takukuru vinginevyo apelekwe mahakamani.

Baadhi ya wananchi waliliambia gazeti hili kwamba, hawaoni sababu ya wabunge kulalamikia kitendo cha Takukuru.

"Mjadala wa bunge hauwezi kuzuia mambo mengine yasifanyike... kama wabunge watashindwa kwa sababu tu ya kuhojiwa basi kazi yao watakuwa hawaijui. Na pengine hili litakuwa ni changamoto kwao," alisema Hamis Athuman.

Imeandaliwa na Exuper Kachenje, Leon Bahati na Ramadhan Semtawa

SOURCE: Mwananchi

21 Oct 2009


DANADANA KUHUSU SUALA LA RICHMOND IMEZIDI KUENDELEA.BINAFSI SIDHANI KAMA SUALA HILI LITAPATIWA UFUMBUZI UNAOSUBIRIWA NA WATANZANIA WENGI.KUPATA UFUMBUZI,KWA MAANA YA KUWEKWA BAYANA UKWELI WA UTAPELI NA UJAMBAZI HUO UTAMAANISHA WATU MUHIMU KUPOTEZA NYADHIFA ZAO.SIO KWAMBA HILO NI BAYA BALI HALIWEZEKANI KATIKA MAZINGIRA YA SIASA ZETU ZA KUJIKOMBA,KUOGOPANA NA BORA LIENDE.


PENGINE HII NI SABABU NYINGINE MUHIMU KWA WAPIGAKURA KUIHOJI CCM COME THE 2010 ELECTION.HEBU SOMA KWANZA HAPA CHINI:


Mazingaombwe tupu Richmond


• Shellukindo anuna, akataa kuulizwa maswali

na Deogratius Temba

KWA mara nyingine tena, serikali jana ilishindwa kuwasilisha maelezo ya utekelezaji wa maazimio 23 ya Bunge kuhusu hatma ya kashfa ya Kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

Licha ya kauli thabiti iliyotolewa na Mwenyekiti wa kamati hiyo, William Shellukindo mwanzoni mwa wiki kwa waandishi wa habari kuwa, serikali ingetoa maelezo hayo kwa kamati yake jana, hali ilikuwa tofauti baada ya Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja kutotokea katika ofisi ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam, ambako kamati mbalimbali za Bunge zinaendelea na vikao vyake.

Kwa mujibu wa ratiba mpya ya vikao vya kamati hiyo vinavyoendelea katika ofisi hizo, jana kamati ilipanga kupokea taarifa hiyo na kuanza kuijadili kwa muda wa siku mbili, baada ya wiki iliyopita kuahirishwa kwa kile kilichoelezwa kuwa Waziri Ngeleja alikuwa nje ya nchi.

Habari ambazo Tanzania Daima Jumatano lilizipata kutoka kwa baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini zilieleza kuwa, walipokea ombi la serikali la kuahirishwa kwa mjadala huo ili ijipange sawasawa.

Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo alieleza kuwa, serikali katika ombi lake kwa kamati, iliitaka kuliweka suala hilo pembeni hadi baadaye itakapoarifiwa, na ilitaka kuendelea na ratiba zake nyingine kama zilivyopangwa.

“Ni kweli leo (jana) tulikuwa tuipokee taarifa ya serikali kuhusu utekelezaji wa maazimio ya Bunge, lakini haya ni masuala yanayoihusu serikali zaidi, wameomba tuendelee na kazi nyingine, wanaweza kuiwasilisha kesho (leo) au keshokutwa (kesho),” alisema mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo aliyeomba jina lake lisitajwe kwa sababu si msemaji.

Alieleza zaidi maelezo kamili ya kuahirishwa kwa upokeaji maelezo ya serikali yanaweza kutolewa na mwenyekiti wa kamati hiyo, Shellukindo, ambaye ndiye aliyepokea ombi hilo la serikali.

Shellukindo alipoulizwa kuhusu hali hiyo, aligeuka mbogo kwa waandishi wa habari kwa kuwataka wasimuulize maswali kuhusu Richmond. Kwa ukali aliwataka waulize maswali yanayohusiana na kampuni ya kuzalisha umeme wa gesi ya Songas, ambayo ilikuwa ikijadiliwa na kamati yake jana.

“Nataka kuwaeleza tulichozungumza na watu wa Songas, lakini nikimaliza nitakaribisha maswali ambayo yatahusiana tu na suala hili la Songas, nje ya hapo sitajibu,” alisema Shellukindo.

Msimamo huo wa Shellukindo uliwafanya waandishi wa habari waliokuwa na shauku ya kutaka kujua sababu za serikali kushindwa kuwasilisha taarifa ya utekelezaji maazimio ya Bunge ambayo imekuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa na watu wengi, kushikwa na butwaa na kushindwa kuuliza maswali kwa muda.

Baada ya dakika chake, Shellukindo ambaye alionekana kutokuwa katika hali ya kawaida, alieleza kuwa kamati yake imezungumza na uongozi wa Kampuni ya Songas kuhusu utengenezaji wa mashine ya kuzalisha umeme wa megawati 20 iliyoharibika wiki iliyopita na upatikanaji wa gesi nchini.

Hata hivyo katika hali ambayo haikutarajiwa na waandishi wa habari, wakati Shellukindo akiendelea kutoa maelezo, wajumbe wa kamati walianza kusimama mmoja mmoja na kuondoka na walipoulizwa sababu ya kuondoka katika kikao hicho, walidai kuwa wana majukumu mengi ya kufanya.

Kabla ya Shellukindo kuanza kuongea na waandishi wa habari, Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe ambaye ni kinara wa kashfa hiyo, alisimama na kutoka nje. Mwakyembe amekuwa hazungumzi lolote na waandishi tangu kuanza kwa vikao vya kamati hiyo.

Awali Tanzania Daima Jumatano lilielezwa kuwa, taarifa hiyo haitawasilishwa kwa kamati hiyo ikiwa jijini Dar es Salaam kwa sababu za kiusalama na badala yake itawasilishwa mjini Dodoma.

Taarifa hizo zilieleza kuwa, wajumbe wa kamati ya Shellukindo watapata nafasi ya kuijadili wakiwa Dodoma na endapo watairidhia wataruhusu serikali iiwasilishe bungeni katika mkutano wa 17, utakaokuwa ukiendelea. Mkutano huo unatarajiwa kuanza Oktoba 27.

Taarifa nyingine zilizolifikia gazeti hili zilieleza kuwa, serikali ina hofu kuwa, iwapo itaitoa taarifa hiyo kwa kamati ya Shellukindo mapema, inaweza kuvuja na kutoa mwanya kwa baadhi ya watuhumiwa wa Richmond kujipanga namna ya kujisafisha au kupoteza baadhi ya vielelezo.

Mmoja wa viongozi wa serikali aliyezungumza na gazeti hili katika eneo la ofisi ndogo za Bunge jana, alisema serikali imekuwa ikisita kuiwasilisha taarifa yake kwa kamati hiyo kwa sababu inaweza kuvuja na kuvuruga mwenendo wa mambo.

“Hofu yetu ni kwamba, serikali ikiwasilisha taarifa hii mapema, hadi kufikia siku ya kuijadili bungeni itakuwa imezagaa mno, taarifa kuenea si jambo jema, watuhumiwa wanaweza kujipanga, inatakiwa iwe ya kushtukizia,” alisema ofisa huyo.

Katika mjadala huo uliokamiwa na baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo, wajumbe pamoja na mambo mengine wataangalia kama serikali imejibu maswali na maagizo ambayo Bunge liliipa serikali.

Wakati Bunge likitaka watu zaidi waliohusika wawajibishwe, tayari mmoja wa wawakilishi wa Kampuni ya Richmond, Naeem Adam Gire, ameshafikishwa katika Mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam Januari 13, mwaka huu na kusomewa mashtaka matano ya makosa ya jinai.

CHANZO: Tanzania Daima

MAAMUZI YA KUIPA TENDA RICHMOND HAYAKUFANYIKA KWENYE KIJIWE CHA KAHAWA BALI KWENYE OFISI NYETI.SASA KWANINI KILA ALIYEHUSIKA KWENYE MAAMUZI HAYO ASIWEKWE HADHARANI?JIBU JEPESI NI KWAMBA KUFANYA HIVYO KUNAWEZA KUPELEKEA "KUISOGEZA 2010 KABLA YA MUDA WAKE" (READ BETWEEN THE LINES,PLZ).

15 Jul 2009


na Charles Mullinda

IMEBAINIKA kuwa, Ofisi ya Bunge imetumia vibaya mamilioni ya shilingi yaliyotolewa na serikali kwa ajili ya uendeshaji wa ofisi hiyo katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2007/2008.

Hayo yamebainishwa na baadhi ya wabunge wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) katika mahojiano yao na Tanzania Daima Jumatano yaliyofanyika wiki iliyopita mjini Dodoma kwa wakati tofauti.

Wakizungumza kwa sharti la majina yao kutoandikwa gazetini, kwa kile walichoeleza kuwa ni kuogopa kuandamwa na baadhi ya wabunge wenzao, walisema ushahidi wa maelezo yao umo katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CGA) ya mwaka wa fedha wa 2007/2008.

Mmoja wa wabunge hao alieleza kuwa licha ya ripoti ya CGA kubainisha matumizi mabaya ya mamilioni ya fedha katika Ofisi ya Bunge, Mwenyekiti wa PAC, John Cheyo, alizuia kujadiliwa kwa ripoti hiyo baada ya kushauriana na baadhi ya vigogo wa Ofisi ya Bunge, jambo ambalo linazuia kuchukuliwa hatua zozote za kisheria au kurekebisha hali hiyo hadi sasa.

Alisema Ofisi ya Bunge imekuwa ikifanya jitihada za makusudi kuhakikisha ripoti hiyo haijadiliwi na PAC, kwa hofu kwamba inaweza kusababisha baadhi ya watendaji kuwajibishwa na baadhi ya wanasiasa kuchafuka majina yao.

Cheyo, Mwenyekiti wa PAC na Mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP), alipoulizwa na gazeti hili kuhusu madai hayo, alisema ni kweli ripoti ya CAG kuhusu matumizi ya fedha za serikali katika Ofisi ya Bunge si nzuri, kwa sababu inaonyesha upungufu mkubwa wa urejeshaji masufuru pamoja na matumuzi mengine mabaya ya fedha za ofisi hiyo.

Hata hivyo, alikana kuikalia ripoti hiyo kwa namna yoyote na kueleza kuwa, aliamua kuiweka pembeni baada ya kushauriana na kukubaliana na wajumbe wote wa kamati hiyo kuwa hawawezi kuijadili, kwa sababu walishindwa kumhoji Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, ambaye wakati kamati hiyo akikutana kujadili ripoti mbalimbali za CGA kuhusu hesabu za taasisi za serikali, alikuwa hajaapishwa na rais kushika wadhifa huo.

“Ni kweli ripoti ya CAG kuhusu matumuzi ya fedha katika Ofisi ya Bunge si nzuri, inaonyesha upungufu mkubwa katika urejeshaji wa masurufu, na ripoti zote ambazo zinaonyesha hivyo kihasibu huwa ni mbaya. Sasa kwa Spika hii si nzuri, inamtia doa, anaweza asiaminike tena iwapo itawekwa wazi, kwa sababu ataonekana hafanani na kauli zake.

“Siyasemi haya kwa sababu nina kisasi na Spika, bali ni kwa sababu umeniuliza. Unajua Spika amenijeruhi hivi karibuni, sasa sitaki nionekana kama ninalipa kisasi. Lakini ukweli unabaki pale pale kwa sababu umeandikwa vitabuni kuwa kuna kasoro katika Ofisi ya Bunge ambayo inasimamiwa na Spika,” alisema Cheyo.

Spika Sitta alipoulizwa kuhusu kauli hiyo ya Cheyo, alisema hahusiki kwa namna yoyote na uchukuaji wa masurufu, hivyo hapaswi kunyooshewa kidole iwapo imebainika kuwapo kwa kasoro zozote za matumuzi mabaya ya fedha za serikali katika ofisi yake.

Spika alisema taratibu ziko wazi kuwa wanaochukua masufuru kwa ajili yake ni wasaidizi wake wanaohusika kumuandalia safari zake zote, ndani na nje ya nchi.

“Mimi sihusiki kuchukua masurufu, wanaohusika ni wasaidizi wangu, sasa kama kuna kasoro, wao ndio wanajua. Nina ofisi yangu binafsi kama viongozi wengine wakuu wa kitaifa, sitembei na fedha mfukoni, wasaidizi wangu wa ofisi hiyo ndio wanaoniandalia safari na ziara zangu zote. Wao ndio wanaonilipia kila kitu, walinzi, maradhi, kila kitu, ndio wanaochukua fedha za masurufu kwa niaba yangu,” alisema Spika Sitta.

Alipoulizwa kuhusu madai kuwa alitumia fedha nyingi za Ofisi ya Bunge kugharamia vikao na tafrija zilizokuwa zikifanyikia nyumbani kwake wakati mkewe, Margaret Sitta, ambaye pia ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, akiwania nafasi ya kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC), alisema madai hayo inabidi yafafanuliwe.

“Ninachokijua mimi kuhusu hili, ni kweli kulikuwa na vitu vya aina hiyo wakati huo, lakini ninachokumbuka ni kwamba gharama nyingi za mikusanyiko hiyo nilikuwa ninatumia fedha zangu za mfukoni, nilikuwa nalipa mwenyewe. Lakini hili ili nilielewe vizuri, inabidi lifafanuliwe,” alisema.

Naye Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah alipoulizwa kuhusu hali hiyo, alisema hawezi kuzungumza jambo hilo, kwa sababu alipoingia katika wadhifa huo alikuta hali hiyo imeshatokea.

Alibainisha kuwa ni kweli hakuhojiwa na Kamati ya PAC kwa sababu alikuwa hajaapishwa na rais, lakini kwa sasa kamati hiyo inaweza kuendelea na kazi zake kama kawaida, bila kupata kipingamizi kutoka kwa mtu yeyote.

“Mimi nilipoingia katika ofisi hii, hali hiyo niliikuta, hivyo siwezi kusema kitu, kwa sababu sikuwapo, siwezi kuizungumzia. Ninachoweza kukitolea maelezo ni kile ambacho kimefanyika wakati wa kipindi changu.

“Lakini suala la ripoti hiyo kukaliwa halipo, PAC ikitaka kukaa kuijadili hata kesho ni sawa tu, hakuna tatizo, waje wakae, wao wana ratiba zao za vikao, kuna ripoti nyingi tu hazijajadiliwa, hizi hazijakaliwa, naomba kwa sababu linahusu Ofisi ya Spika, isichukuliwe kuwa linazimwa,” alisema Dk. Kashililah.

Ripoti ya CAG, ambayo Tanzania Daima Jumatano imeiona, katika ukurasa wake wa 43, fungu la 42, inaitaja Ofisi ya Bunge katika orodha ya taasisi za serikali zilizopewa hati zenye shaka, kwa kukiuka taratibu za kihasibu.

Ripoti hiyo inabainisha kuwa Ofisi ya Bunge ilifanya malipo ya matibabu nje ya nchi ya zaidi ya sh milioni 101 bila kuidhinishwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, uhamisho wa fedha wa zaidi ya sh milioni 63 kutoka kifungu kimoja kwenda kingine bila kibali na malipo yenye thamani ya sh milioni 7.8 yalifanyika bila kibali.

Upungufu mwingine uliotajwa katika ripoti hiyo ni malipo yenye nyaraka pungufu ya sh milioni 526, malipo yasiyo halali ya sh milioni 102.5, malipo yenye shaka ya sh milioni 63.9, mishahara isiyolipwa na ambayo haikurejeshwa Hazina sh milioni 17.1, sh milioni 3.4 za mishahara ya watumishi walioachishwa kazi inayoendelea kulipwa kwenye akaunti zao benki na usuluhisho wa tofauti ya sh milioni 1.1 kati ya bakaa ya benki na bakaa inayoonyeshwa katika daftari la mapato na matumizi haukufanyika.

Marekebisho yasiyostahili yaliyojumuishwa kwenye hundi ambazo hazijawasilishwa benki ni sh milioni tano, masurufu maalumu ya sh milioni 50.2


KINACHOKWAMISHA VITA DHIDI YA UFISADI NI HUU MTINDO WA KUENDESHA MAMBO KISHKAJI.UKITAFAKARI KAULI YA CHEYO KUHOFIA KUHUSISHA HABARI ZA UFISADI HUO NA HATUA YA SPIKA KUMTOA NJE YA BUNGE HIVI KARIBUNI UTAGUNDUA KUWA BADALA YA MBUNGE HUYO KUSHUGHULIKIA SUALA HILO KAMA MWENYEKITI WA KAMATI HUSIKA,YEYE ANAJIONA KAMA JOHN MOMOSE CHEYO ALIYETOLEWA NJE NA SAMUEL SITTA,BADALA YA OFISI YA BUNGE ILIYO CHINI YA SPIKA NA WATENDAJI KADHAA.

NA UNAFIKI MWINGINE NI WA HAO WABUNGE WALIONUKULIWA KATIKA HABARI HII AMBAYO HAWATAKI KUTAJWA MAJINA KISA WANAOGOPA KUANDAMWA NA WABUNGE WENZAO.KWANI WALIINGIZWA BUNGENI NA HAO WABUNGE WENZAO WANAOWAOGOPA AU WANANCHI HUKO MAJIMBONI?

WIZI MTUPU!


25 Apr 2009



MZALENDO MMOJA AMENITUMIA UJUMBE UFUATO KWENYE E-MAIL,NAMI NAOMBA KUUWASILISHA KAMA ULIVYO:


Kuna habari kwamba mmoja wa wafanyabiashara aliyetajwa na Mkurugenzi wa IPP Bwana Reginald Mengi amenunua hisa nyingi za umiliki wa kituo cha kurusha matangazo ya Television.

Mfanya biashara huyo inasemekana ni yule aliyetumia mtindo huohuo kununua hisa za kampuni iliyokuwa inatoa gazeti lilikuwa maarufu kabla ya mwaka 2005 na sasa si maarufu tena.

Mfanyabiashara huyo ambaye ana hisa kwenye kampuni moja ya simu za mikononi inasemekana ana mpango wa kutumia minara ya kampuni hiyo ya simu ili kusambaza matangazo ya kituo hicho nchi nzima kwa urahisi na bila gharama kubwa.

Kwa vile kampuni yake ndiyo yenye mtandao mkubwa hapa nchini basi itakuwa ni rahisi kwake kusikika nchi nzima kuzidi vyombo vyote vya habari.

Iwapo mpango huo utatekelezwa basi mfanyabiashara huyo atakuwa anaongoza kusikika eneo kubwa nchini.

Bwana Mengi ina ITV na Redio zake tabidi avute bidii ya kasi kwa sababu yeye hataweza kuwa na mtandao mkubwa kama hiyo TV.

Wenu mtafuta habari

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.