9 Dec 2014

Wakati Tanzania Bara inatimiza miaka 53 ya uhuru, leo pia ni siku yangu ya kuzaliwa. Naitakia nchi yangu kila la heri na fanaka, na Mweneyzi Mungu aiongoze nchi yetu kwenye njia njema, sambamba na kuiepusha na mabalaa. Kwa mujibu wa mambo yalivyo huko nyumbani, hali si ya kuridhisha sana. Basi ni muhimu tuitumie siku hii muhimu kuiombea nchi yetu kwa kila jema.

Kwangu, siku hii ya kuzaliwa ni fursa nyingine ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia kuongeza mwaka mwingine katika maisha yangu. Nawashukuru sana wazazi wangu Baba Mzee Philemon Chahali na mama yangu mpendwa, marehemu Adelina Mapango (we all miss you so much mom). Pia nawashukuru wanafamilia wenzangu, ndugu, jamaa na marafiki kwa mema yote waliyonifanyia. Natumaini mtaendeleo kuwa nami siku zote za uhai wangu.

Nwashukuru nanyi wasomaji wa blogu hii, marafiki zangu wapendwa ambao nawafahamu kwa kuangalia idadi ya wanaotembelea blogu hii. Japo pengine wengi wenu hatufahamiani personally, lakini mnapochukua muda wetu muhimu kunitembelea hapa, kuvumilia makelele yangu na 'upuuzi' wmingine ninaoandika, ni faraja kubwa mno kwangu. Nawashukuru kwa kuwa sehemu ya familia yangu kiuandishi.

Nimalizie kwa kumwomba Mwenyezi Mungu azidi kunijalia afya njema, maisha marefu, afya njema kwangu, familia, yangu, ndugu, jamaa na marafiki, na niwe na mafanikio katika kila jambo. Amen

5 Dec 2014


NIANZE kwa kuelezea kuhusu hatua mbili zilizochukuliwa na mamlaka za hapa Uingereza na jinsi zilivyobadili maisha kwa wakazi wengi wa nchi hii.
Lengo la kuelezea hatua hizo ni kuhusisha na tatizo kubwa linalokwaza utekelezaji wa sera na mipango mbalimbali huko nyumbani: ukosefu wa dhamira.
Hatua ya kwanza ilihusu dhamira ya serikali kuhamasisha wavuta sigara kuachana na tabia hiyo ambayo si tu ina gharama kifedha bali pia kiafya.
Kwa hapa Scotland, mwaka 2006 serikali ilipiga marufuku uvutaji sigara hadharani. Hatua hiyo, sambamba na mikakati mbalimbali ya kuwasaidia watu wanaotaka kuacha uvutaji wa sigara, imekuwa na mafanikio makubwa.
Mwaka jana, serikali ilitangaza sheria ya kuyataka maduka makubwa (supermarkets) yote kutuonyesha sigara katika maeneo yaliyotengwa kwa uuzaji wa bidhaa hiyo. Sambamba na hatua hiyo ni kutuonyesha bei za pakti za sigara hadharani.
Sheria hiyo itaanza kutekelezwa na maduka yote kuanzia Aprili mwakani. Hatua zote hizo ni utekelezaji wa mkakati wenye lengo la kuifanya Scotland kuwa ‘smoke-free’ kufikia mwaka 2034.
Hatua nyingine ya hivi karibuni ni ile ilivyoanza kutekelezwa Oktoba mwaka huu, ambapo kila biashara ya bidhaa imeagizwa kutoza ushuru wa pence 5 (takriban shilingi 136) kwa kila mteja atakayetaka mfuko wa kubebea bidhaa alizonunua.
Lengo la hatua hii ni kuhamasisha utumiaji tena wa mifuko iliyokwishatumika (re-use) na kupunguza takataka. Hatua hii imekuwa na mafanikio makubwa mno, kwani wateja wengi sasa wanakwenda madukani wakiwa na mifuko yao wenyewe ili kuepuka ushuru huo.
Kama nilivyotanabahisha mwanzoni, lengo la kuelezea kuhusu hatua hizo mbili ni kuzihusisha na tatizo linaloikabili nchi yetu la kukosa dhamira katika hatua mbalimbali tunazozichukua kwa manufaa ya jamii au Taifa kwa ujumla.
Wiki iliyopita tumeshuhudia sokomoko kubwa kuhusiana na skandali ya ‘Tegeta Escrow.’ Kwa kifupi, skandali hii ilihusu uchotwaji wa mabilioni ya shilingi katika akaunti ya Escrow ndani ya Benki Kuu ya Tanzania, katika mazingira yanayoashiria ufisadi.
Kamati husika ya Bunge chini ya uongozi wa Mbunge Zitto Kabwe ilifanya kazi kubwa ya kufuatilia suala hilo, na hatimaye kuwasilisha ripoti iliyotokana na uchunguzi wa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Serikali (CAG) na Taasisi ya Kupambana na Kuzuwia Rushwa (Takukuru).
Tarehe 26 ya mwezi uliopita yaweza kuingia katika historia ya taifa letu, ambapo kwa sisi tunaofuatilia masuala mbalimbali ya huko nyumbani kwa kutumia mitandao ya kijamii tulishuhudia kiu kubwa ya Watanzania kuhusu undani wa skandali hiyo ya Escrow hususan majina ya wahusika na hatua pendekezwa dhidi yao.
Kwa siku nne mfululizo, wengi wa Watanzania walionekana ‘kusahau takriban kila kitu’ ikiwa ni pamoja na ‘vipaumbele vyetu vya kawaida’ kama vile maendeleo ya ligi za soka barani Ulaya, na kuwekeza nguvu zao kufuatilia mjadala wa skandali hiyo huko Bungeni, Dodoma.
Hatimaye, Jumamosi iliyopita, ripoti hiyo iliridhiwa na wabunge wetu japokuwa wananchi wengi (angalau katika mitandao hiyo ya kijamii) wakibaki na kinyongo kidogo kutokana na Waziri Mkuu Mizengo Pinda ‘kuokolewa.’ Hata hivyo, kwa kiasi kikubwa, wengi wa waliokuwa wakifuatilia tukio hilo walionekana kuridhishwa na maamuzi yanayotaka mamlaka husika kufanya uchunguzi wa haraka na kuchukua hatua stahili dhidi ya wahusika.
Nisingependa kurejea yote yaliyojiri wakati wa mjadala huo mkali, lakini masuala muhimu yaliyojitokeza waziwazi ni pamoja na, kwanza, kuwapo baadhi ya wawakilishi wa wananchi ambao hawataki kabisa kusikia vilio vya wanaowawakilisha, na badala yake kutetea misimamo na maslahi yao binafsi.
Baadhi ya wabunge wa CCM, hususan wa kuteuliwa, walionekana kama ‘wametoka sayari nyingine’ kwa jinsi walivyosimama kidete kuwatetea watuhumiwa katika skandali hiyo.
Pili, na pengine hili ni la muhimu zaidi, ni jinsi tofauti za kiitikadi zilivyowekwa kando kwa kiasi kikubwa na wengi wa wabunge kuhakikisha kuwa maslahi ya umma na Taifa yanawekwa mbele, na hatimaye kufikiwa mwafaka wa ‘pande tatu,’ kwa maana ya CCM, Ukawa na Kamati husika ya Bunge. Tukio hili sio tu ni la kihistoria bali lina umuhimu wa kipekee.
Iwapo wanasiasa wetu wataendeleza ari hiyo ya kuweka mbele maslahi ya Taifa badala ya maslahi yao binafsi, au ya vyama vyao, basi kwa hakika twaweza kupiga hatua kubwa katika kukabili changamoto mbalimbali zinazoikabili Tanzania.
Hata hivyo, ukweli mchungu kuhusu hitimisho la suala hilo ni kwamba baadhi ya watuhumiwa ‘wameokolewa.’ Ikumbukwe kuwa taarifa zilizopatikana awali, na hatimaye kuwekwa hadharani na Mbunge Tundu Lissu ni uhusika wa IKulu, ambayo inaelezwa iliidhinisha malipo hayo kutoka katika akaunti ya Escrow huko Benki Kuu. Sambamba na hilo ni kauli za mara kwa mara za Waziri Mkuu Pinda kuwa fedha hizo si za umma.
Na kama kutonesha ‘kidonda kibichi,’ wakati anaahirisha kikao cha Bunge hilo, ambacho pamoja na mambo mengine, kilisomewa na kujadili ripoti kuhusu skandali hiyo ya Escrow, Pinda aligusia tena swali ambalo limeonekana kama ‘utetezi’ na ‘tuhuma’ kuhusu utoaji wa fedha hizo, yaani “je fedha hizo ni za umma?”
Watuhumiwa wanadai si za umma ilhali watuhumu, ikiwa pamoja na wananchi wengi, wanaamini kuwa fedha hizo ni za umma, na kitendo cha kuzitoa Benki Kuu ni cha kifisadi.
Na hapa ndipo maelezo niliyoyatoa hapo awali kuhusu hatua mbili zilizochukuliwa hapa Scotland yanapokuwa na umuhimu  kwa hali ya huko nyumbani. Kama kweli tungekuwa na dhamira ya dhati ya kupambana na ufisadi, hakukuwa na haja ya ‘kuchuja’ wahusika. Je, kwanini hoja iliyotolewa na Mbunge Lissu kuhusu kuhusika kwa Ikulu ilitelekezwa?
Japo wakati anarejea nyumbani kutoka Marekani kwa matibabu, Rais alieleza kuwa “hafahamu kwa undani kuhusu kilichokuwa kikiendelea Dodoma (kwa maana ya mjadala huo wa skandali ya Escrow), ukweli ni kwamba taasisi ya urais si mtu aitwaye Jakaya Kikwete pekee bali wasaidizi na taasisi mbalimbali kama vile Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Idara ya Usalama wa Taifa, nk.
Licha ya ukweli kwamba Rais alikwenda Marekani kwa matibabu, sitaki kabisa kuamini kuwa alikuwa hafuatilii kinachoendelea kuhusu skandali ya Escrow. Kama aliweza kusoma ‘meseji’ mbalimbali alizotumiwa na Watanzania kumtakia afya njema, ninaamini alipata muda pia wa kufahamishwa kinachoendelea huko nyumbani kuhusu sakata la Escrow.
Mbunge Lissu pia aligusia kuhusu utendaji kazi mbovu wa Idara yetu ya Usalama wa Taifa. Aliishutumu vikali huku akihoji ilikuwa wapi wakati ‘ufisadi wa Escrow’ ukitendeka.
Licha ya mchango wa mbunge huyo machachari kuhusu taasisi hiyo kutopewa uzito kabisa katika maazimio ya Bunge juu ya skandali ya Escrow, Kamati ya Zitto, kwa sababu ambazo si vigumu kwa sisi wengine kuzielewa, ilikwepa kuitwisha lawama Idara ya Usalama wa Taifa.
Licha ya kutoafikiana na hatua hiyo ya Kamati ya Zitto kutomgusa Rais Kikwete wala Idara ya Usalama wa Taifa, binafsi ninaamini kuwa hatua hiyo ilikuwa ya kiufundi zaidi kwa maana kwamba ya kuepusha kuwaunganisha CCM, ambayo ndio iliyotoa wengi wa wajumbe wa Kamati hiyo, kuipinga ripoti nzima.
Kama ambavyo CCM imefanikiwa kumwokoa Pinda, laiti Kamati hiyo ingemtuhumu Rais Kikwete na Idara ya Usalama wa Taifa basi huenda isingemudu japo kufikia hatua ya kujadiliwa.
Sasa matokeo yake tumefanya kile Waingereza wanaita to settle for less yaani angalau tumepata chochote kitu. Lakini msemo huo wa Kiingereza unaonya kuwa ‘when you settle for less, you end up getting even lesser than what you deserved’ (unapokubali kupewa kitu pungufu ili mradi upate tu, waishia kupata pungufu zaidi ya unachostahili).
Pengine Rais Kikwete atatekeleza maazimio yote ya Bunge. Pengine utekelezaji huo utafanyika mapema iwezekanavyo. Lakini ukweli utabaki kuwa licha ya skandali ya Escrow kuwa moja tu ya skandali nyingine kadhaa ambazo bado zinaitesa Tanzania yetu, na nyinginezo zinazoweza kuibuka huko mbele, hatujafanikiwa kukata mzizi wa tatizo la ufisadi ambalo kwa kiasi kikubwa limegubika utawala wa Rais Kikwete. Na kama nilivyotanabaisha katika makala iliyopita, Rais wetu ni mgumu katika kuchukua hatua stahili, na matokeo yake twajikuta kila mara tukirejea kulekule tulikotoka. Tunapiga hatua 50 mbele, baadaye twarejeshwa hatua 100 nyuma.
Kinachosababisha haya ni kile ambacho wenzetu hapa Scotland wamefanikiwa: si tu kuwa na sera au mipango mizuri, bali pia kuitafsiri katika vitendo.
Japo ningetamani sana kuona skandali ya Escrow kuwa ya mwisho angalau hadi Rais Kikwete atakapomaliza muda wake, ukweli kwamba kuna mabilioni ya fedha tuliyoibiwa na kufichwa kwenye akaunti za Benki huko Uswisi, sambamba na ‘uhalifu uliozoeleka’ wa biashara haramu ya madawa ya kulevya na ujangili, sintoshangaa tukikumbana na ‘Escrow nyingine’ hivi karibuni.
Nihitimishe makala hii kwa kukumbushia mambo haya: wenye ufahamu wanaelewa ukaribu uliopo kati ya Rais Kikwete na Waziri Muhongo (inaelezwa kuwa ndiye aliyemshawishi kutoka kwenye taaluma na kuingia kwenye siasa kwa uteuzi) wanaona ni mtihani mkubwa mno kwa Rais Kikwete kumtimua waziri huyo ambaye siku zote amesimama kidete kuwaaminisha Watanzania kuwa fedha za Escrow si za umma.
Kwa upande mwingine, kumwajibisha Mwanasheria Mkuu Werema kutamaanisha ‘kumweka huru’ mtu mwenye uelewa mkubwa wa ‘mambo mengi’ yaliyotokea, yanayotokea na yatakayotokea katika utawala wa Rais Kikwete.
Katika mazingira ya kawaida tu, si rahisi mtu ‘kujitenga’ na ‘mwandani’ wake, hasa ikizingatiwa kuwa ‘hasira za kutimuliwa’ zaweza kumshawishi kuweka hadharani mengi ya tusiyoyajua (kwa mfano majina ya walioficha fedha zetu kwenye mabenki ya Uswisi.)
La mwisho kabisa ni Singasinga. Bila haja ya kudadisi nani aliyemleta wala kujua washiriki wake wa kibiashara nchini Tanzania, ni muhimu mapendekezo ya kuchukua hatua kali za kisheria dhidi yake yakatekelezwa haraka pengine kabla ya hatua dhidi ya watendaji wa serikali waliohusishwa na skandali hiyo.
Ushauri wangu mwepesi ni kuwa huyo mtu atangazwe kuwa ‘persona non grata’ (mtu asiyetakiwa kuwapo katika nchi husika) mara moja.
Idara ya Usalama wa Taifa inafahamu bayana tishio la kiusalama linalosababishwa na kuwapo kwake, na huenda CCM pia yatambua madhara aliyosababisha mtu huyo kwa kilichokuwa chama tawala nchini Kenya, KANU. Atimuliwe.
Tanzania yetu ni kama nyumba zilizojengwa bonde la Jangwani (Dar), msimu wa kiangazi tupo salama, msimu wa mvua ukiwasili inakuwa tabu. Ikumbukwe kuwa hata Nabii Nuhu alijenga safina kabla gharika haijaanza. Tujipange kupambana na ‘Escrow nyingine’ sasa badala ya kusubiri hadi ziibuke.
INAWEZEKANA, TUKITIMIZA WAJIBU WETU IPASAVYO


Waingereza wana msemo ambao unatafsirika kwa Kiswahili kama "chuki ya pamoja ni mwanzo wa urafiki mkubwa." Kimahesabu kama A hapatani na B, na A anamchukia C kama ambavyo B anamchukia pia C, basi chuki ya A na B kwa C yaweza kuwa mwanzo wa wawili hao A na B kuwa marafiki wenye lengo la kumwangamiza C.

Binafsi, naomba kukiri kuwa kwa muda sasa nimekuwa siafikiani na mitizamo na mwenendo wa mwanasiasa mahiri wa upinzani, Zitto Kabwe. Siwezi kusema nina chuki dhidi yake bali mie sio miongoni mwa supporters wake.Pamoja na sababu nyingine, kubwa ni kile ninachokitafsiri kama mwanasiasa huyo kutanguliza mbele maslahi yake binafsi badala ya chama chake yaani Chadema. Kwa mtizamo wangu, mgogoro uliopelekea hatua ya Chadema kumvua madaraka Zitto ni matokeo ya 'imani potofu' kuwa kuna mwanasiasa anayeweza kuwa maarufu kuliko chama chake, Si kwamba haiwezekani kabisa kwa hilo kutokea lakini si kwa hatua waliyofikia Chadema hivi sasa.

Lakini lengo la makala hii si kumjadili Zitto wala ugomvi kati yake na Chadema. Ila nimegusia suala hilo kwa sababu nililazimika 'kurejesha urafiki' na mwanasiasa huyo, angalau kinadharia, wakati akifanya jitihada kubwa binafsi na kama mwenyekiti wa PAC kushughulikia ufisadi wa Tegeta Escrow. Kwa kutumia mfano huo hapo juu wa chuki za A kwa C na za B kwa C, na A ni Zitto, na B ni mie, huko C wakiwa mafisadi wa Escrow, basi 'urafiki' usingeepukika.

Hakuna Mtanzania atakayeshindwa kumpongeza Zitto na Kafulila pamoja na PAC kwa ujumla walivyofanya kazi kubwa na nzuri katika kushughulikia skandali hiyo. Nina imani hata wahusika wa ufisadi huo wa Escrow wanamkubali kwa jinsi alivyowakalia kooni...ALMOST.

Hata hivyo, mara baada ya kumalizika kwa 'timbwili' hilo la Escrow bungeni, nilitumiwa meseji na 'mjuzi mmoja wa mambo ya huko nyumbani' ambaye alidai kuwa pamoja na kazi nzuri iliyofanywa na PAC, kuna 'mchezo mchafu' uliofanyika katika kufikia mwafaka miongoni mwa wajumbe, hususan wale wa kutoka CCM. Alidai kuwa kilichowezesha mwafaka huo kufikiwa ni pamoja na 'kumnusuru' Rais Jakaya Kikwete, ambaye kama Mbunge Tundu Lissu alivyobainisha bungeni, anatajwa kuhusika katika skandali hiyo. Kimsingi, hoja ya Lissu, ambaye pia aliilaumu Idara ya Usalama wa Taifa kwa kutowajibika ipasavyo katika mlolongo wa skandali mbalimbali zinazougubika utawala wa Rais Kikwet, iliuawa kimyakimya licha ya umuhimu wake mkubwa.

Hata hivyo, kwa uelewa wangu, jaribio lolote la kumhusisha Rais Kikwete na skandali hiyo hata kama ushahidi upo lingepelekea mparaganyiko mkubwa katika kamati hiyo ya Zitto. Na kama tulivyoshuhudia 'makada' wa CCM huko bungeni walivyopigana kufa na kupona hadi Waziri Mkuu Mizengo Pinda akanusuriwa, kwa hakika ishu ya Kikwete kuhusishwa na Escrow ingepelekea bunge hilo kuvunjika pasi kufikia hitimisho.

Lakini what if mkakati huo wa 'kumnusuru Rais Kikwete' unabeba mengi zaidi ya tunavyodhani? 


Kwa kifupi, tume-settle for less. Na Waingereza wana msemo unaotahadharisha kuhusu ku-settle for less, ambapo wanasema 'pindi ukikubali kupokea pungufu ya unachostahilki basi hatimaye utaishia kupokea pungufu zaidi ya kile ulichostahili awali.' Japo ni mapema kuhitimisha kwamba 'tumeingizwa mkenge,' lakini ukimya wa Rais Kikwete katika kutekeleza maazimio ya Bunge kuhusu Escrow umeanza kuzua wasiwasi.

Na 'kigugugmizi' kinachomkabili Rais Kikwete kina sababu kadhaa za wazi. Kwa mfano, kumtimua Mwanasheria Mkuu Jaji Werema kunaweza kupelekea kuzuka kwa skandali nyingine iwapo Jaji huyo ataamua 'mmemwaga mboga, na mie namwaga ugali' kwa maana anajua mengi yaliyojiri na yanayojiri katika utawala wa Rais Kikwete. Japo si kwamba haiwezekani kumtimua na kisha kumfunga mdomo, lakini historia ya wanasheria wakuu huko nyuma inapaswa kutukumbusha jinsi 'wanavyobebwa' kwa minajili ya 'kutotengeneza uadui na mtu anayejua siri nyingi.'

Kwa upande wmingine, ni muhimu kukumbuka kuwa kimsingi Rais Kikwete ndo aliyemleta Profesa Muhongo katika frontline politics. Hawa ni marafiki wa karibu. Na hadi sasa Muhongo ameendeleza jeuri yake ya kisomi na kusisitiza kuwa fedha za Escrow si za umma. Msimamo huo pia washikiliwa na Waziri Mkuu Pinda. Je kuna anayefahamu msimamo wa Rais Kikwete? Maelezo yanaonyesha kuwa yeye aliridhia malipo ya Escrow kufanyika. Je amebadili mawazo na kutambua kuwa hilo lilikuwa kosa?

Lakini wakati tayari tunafahamu majina mengi ya walionufaika na mgao wa Escrow kupitia Benki ya Mkombozi, inadaiwa kuwa mgao mkubwa zaidi uliopitia Benki ya Stanbic ulihusisha vigogo kadhaa lakini hadi muda huu hakuna jina hata moja lililowekwa hadharani. So far, gazeti la Raia Mwema limeripoti kuwa mke wa kigogo momja mwandamizi huko Ikulu alikatiwa shilingi bilioni 5. Sasa huhitaji kujua hesabati vizuri kubashiri kwamba kama mke wa kigogo alikatiwa mbilioni tano, mumewe alipewa kiasi gani? 

Hayo yote tisa, kumi ni kauli niliyokumbana nayo muda mfupi uliopita, na ambayo kwa hakika ndio iliyonisukuma kuandika makala hii. Kauli hiyo ni ya Jaji Mkuu Chande ambayo kimsingi inaharibu mwenendo wa kesi yoyote itakayofunguliwa dhidi ya wahusika wa ufisadi wa Escrow. Nimeinukuu kwa picha hapa chini.


Je Jaji Mkuu alikuwa anatoa tu tahadhari au alikuwa akifikisha ujumbe mahsusi kwamba hata tukiwapeleka mahakamani wahusika wa Escrow, utetezi wao upo bayana...kwamba walishahukumiwa bungeni. Na kama Jaji Mkuu 'hakutumwa' basi kwa hakika amewapatiwa washtakiwa-watarajiwa ushauri mzuri wa bure kisheria kuhusu jinsi ya kupambana na kesi yoyote watakayofunguliwa kuhusisna na suala hilo: wajitetee kuwa walishahukumiwa na bunge, na mawakili waoa waweza kutumia kauli hiyo ya Jaji Mkuu kama supporting evidence.

Anyway, pengine ni mapema mno kuhukumu lakini kama ambavyo Mzee Warioba alivyoonyesha mapungufu ya taarifa ya PAC na maazimio ya bunge kuhusu skandali ya Escrow, sintomshangaa mtu yeyote atakayeanza kupatwa na wasiwasi kuwa tumeingizwa mkenge...TENA.


Sijui msomaji mepndwa unaonaje. 





1 Dec 2014

Kwanza niombe samahani kwa ku-update blogu hii kitambo. Nilitingwa na majukumu. Pili, makala hii chini ilichapishwa katika gazeti la RAIA MWEMA toleo la Jumatano Novemba 26, 2014, lakini kwa sbabau nisizofahamu tovuti ya gazeti hilo haikuwa up-dated hadi asubuhi hii. Licha ya kuwa na nakala halisi ya makala hii, nilionelea ni vema kusubiri 'edited version' ya makala hii pindi ikichapishwa kwenye tovuti ya RAIA MWEMA. Endelea kuisoma
KWANZA, nianze makala hii kwa kuomba samahani kwa ‘kutoonekana’ kwa takriban mwezi mzima sasa. Hali hiyo ilitokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wangu. Ninapenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa wasomaji mbalimbali walionitumia barua-pepe kuulizia kuhusu ‘ukimya’ huo.
Wiki iliyopita, Rais wa Marekani, Barack Obama, aliandika historia kwa kuweka hadharani mpango kabambe kuhusu hatma ya takribani wakazi milioni 12 wanaoishi isivyo halali nchini humo.
Ujasiri wa Obama katika suala hilo unatokana na ukweli kwamba licha ya jitihada za muda mrefu, uhasama wa kisiasa kati ya vyama vikuu vya siasa nchini humo, Democrats na Republicans, ulikuwa kikwazo kikubwa katika kufikia mwafaka na ufumbuzi.
Wakati vyama vyote viwili vinaafikiana kuhusu uwepo wa wakazi hao wasio halali milioni 12, wahafidhina wa Republicans wamekuwa wapinzani wakubwa kuhusu ‘ufumbuzi rahisi’ wa kutoa msamaha (amnesty) kwa wahamiaji hao na kisha kuimarisha udhibiti katika mianya inayotumiwa na ‘wahamiaji haramu.’
Lakini suala hilo limekuwa mzigo mkubwa kwa Obama ambaye hata kabla hajaingia madarakani aliahidi kutafuta ufumbuzi hasa ikizingatiwa kwamba licha ya utajiri wa Marekani, hakuna uwezekano wa kuwatumia wahamiaji hao wote.
Kadhalika, mara kadhaa Obama alikuwa akieleza kwamba kulipuuza tatizo hilo hakutolifanya lipotee lenyewe, bali litazidi kuwa kubwa na gumu kulitatua.
Hatimaye Obama aliwatahadharisha Republicans kuwa atalazimika kutumia ‘Nguvu ya Kirais’ (Executive Order) ambayo haihitaji kuridhiwa na Bunge la nchi hiyo, iwapo wanasiasa wataendeleza malumbano pasipo kuja na ufumbuzi.
Hata hivyo, Republicans walitoa vitisho mbalimbali kwa Obama dhidi ya kutumia ‘executive order,’ huku baadhi wakitishia kumburuza mahakamani ili kumng’oa madarakani kwa madai ya ‘kukiuka katiba.’
Licha ya vitisho hivyo, na upinzani wa wengi wa wananchi wa kawaida (ambao kura za maoni zilionyesha wananchi wengi kutoafiki Rais kutumia ‘executive order’ katika suala hilo), hatimaye Obama aliweka hadharani mpango huo kabambe utakaowapatia ahueni ya kimakazi takriban wahamiaji milioni tano.
Matokeo ya uamuzi huo ni bayana: Republicans wamekasirishwa mno na hatua hiyo, huku chama cha Democrats ambacho kwa kiwango kikubwa kimekuwa mstari wa mbele kuwanusuru wahamiaji hao, kikinufaika kwa sapoti kutoka kundi muhimu katika siasa za chaguzi za Marekani, Walatino.
Kundi hili linatajwa kuwa muhimu mno kwa vyama vyote viwili, kwa Democrats kubaki madarakani baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2016, na Republicans kukamata Ikulu baada ya miaka 10 ya Obama. Kidemografia, idadi ya Walatino inaongezeka kwa kasi kuliko kundi lolote lile la ‘asili ya watu’ kwa maana ya Wamarekani Weupe na Wamarekani Weusi, na makundi mengine madogo.
Sasa ni wazi kuwa ili mgombea wa chama chochote kile afanikiwe kuingia Ikulu, ni lazima apate sapoti na kura za kutosha kutoka kwa Walatino.
Uamuzi huo wa Obama umekuwa kama mtego kwa Republicans. Laiti chama hicho kikiendeleza upinzani dhidi ya suala hilo, si tu kitajipunguzia umaarufu wake kwa Walatino na hivyo kuathiri nafasi yao katika uchaguzi mkuu ujao, lakini pia kitawatenga Wamarekani wasio Walatino lakini wanaotaka ‘wahamiaji haramu’ kupatiwa makazi ya kudumu nchi humo.
Lakini kwa upande mwingine, chama hicho kinatambua kuwa kwa kiasi kikubwa ‘Wamarekani hao wapya’ (kwa maana ya ‘wahamiaji haramu’ watakaopewa makazi ya kudumu) wataisapoti Democrats kama kulipa fadhila kwa kushughulikia tatizo lao.
Nitaendelea kuwaletea maendeleo ya suala hili katika makala zijazo hasa kwa vile uamuzi huo wa Obama ni kama umeanzisha ‘vita’ ya kisiasa kati yake binafsi (na chama chake) dhidi ya Republicans ambao mapema mwezi huu walifanikiwa kukamata uongozi wa mabunge yote mawili ya nchi hiyo, yaani Seneti na Congress.
Lengo hasa la kuzungumzia tukio hilo la nchini Marekani ni hali ilivyo huko nyumbani hivi sasa. Hadi wakati ninaandaa makala hii, ‘mshikemshike’ unaotokana na skandali ya ufisadi wa ESCROW sio tu unazidi kukua lakini pia unaleta dalili za uwezekano wa Rais Kikwete kulazimika kufanya mabadiliko kwenye Baraza lake la mawaziri kwa mara nyingine.
Kwa vile takribani kila Mtanzania anafahamu kinachoendelea kuhusu skandali hiyo ya ESCROW, sioni haja ya kuizungumzia kiundani. Hata hivyo, pasi haya, na huku nikitambua kuwa Rais wetu Jakaya Kikwete yupo katika matibabu nchini Marekani, ukweli unabaki kuwa yeye ndiye chanzo cha yote haya.
Nikirejea uamuzi wa Obama kutumia ‘nguvu ya kirais’ kupata ufumbuzi katika tatizo la ‘wahamiaji haramu,’ Kikwete alipaswa kuchukua hatua kama hiyo muda mrefu uliopita. Hapa ninamaanisha Rais kutumia nguvu alizopewa na Katiba kupambana na uhalifu.
Ninaandika hivyo kwa sababu Kikwete ana uelewa wa kutosha kuhusu ‘mgogoro wa IPTL’ ikizingatiwa kuwa huko nyuma alishawahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini. Lakini wakati miaka yake 10 ikielekea ukingoni, hakuna jitihada yoyote ya maana iliyofanywa nae kulipatia ufumbuzi tatizo hilo.
Lakini hata tukiweka kando uzoefu wake katika suala hilo, utawala wake utakumbukwa zaidi kwa kuandamwa na mlolongo wa matukio ya ufisadi ambayo hatma yake imekuwa kuwashawishi mafisadi wengine ‘kujaribu bahati zao’.
Naam, kama Kikwete alidiriki ‘kukumbushia haki za binadamu’ za mafisadi wa EPA, na kuwapa deadline ya kurejesha mabilioni waliyoiba, kwanini mafisadi watarajiwa waogope kufanya uhalifu?
Yayumkinika kuhitimisha kwamba laiti idadi ya safari alizokwishafanya nchi za nje ingelingana na hatua dhidi ya ufisadi/ mafisadi, huenda leo hii tungekuwa tunazungumzia ‘mafanikio ya kihistoria ya uchumi wa Tanzania’.
Badala yake, tumekuwa tukiandamwa na vyombo vya habari vya kimataifa kuhusu taifa letu lilivyoukumbatia ufisadi kiasi cha kuruhusu ndege ya msafara wa Rais wa China kuondoka na vipusa, sambamba na taarifa mpya kuwa kuna mpango wa serikali kuwatimua wafugaji wa Kimasai katika makazi yao ili kukabidhi eneo hilo kwa familia ya kifalme ya mojawapo ya nchi za Kiarabu.
Sasa badala ya viongozi wetu kushughulikia changamoto mbalimbali zinazolikabili taifa letu, wamekuwa ‘bize’ kupambana na vyombo vya habari vya kimataifa kukanusha tuhuma hizo. Hivi wazembe hawa hawaoni haya na kujiuliza “kwa kipi hasa cha kuvifanya vyombo vya habari vya kimataifa vituandame bila sababu?”
Kwa upande mwingine, skandali hii ya ESCROW ni uthibitisho mwingine kuwa Idara yetu ya Usalama wa Taifa (TISS) imepoteza mwelekeo, haitimizi wajibu wake, na ni kama ipo likizo ya muda mrefu.
Hivi inawezekana vipi huyo ‘Singasinga’ anayetajwa kuwa mhusika mkuu katika skandali hiyo aliruhusiwa kuishi Tanzania huko rekodi yake ikionyesha bayana kuwa ni mtu hatari kwa usalama wa taifa letu?
Hii haikuhitaji hata operesheni maalum kwa Idara yetu ya Usalama wa Taifa kwani habari za mtu huyo zipo wazi kwenye mtandao. Hivi Idara hiyo imejaa uzembe kiasi cha kushindwa japo ku-Google taarifa za mtu huyo?
Lakini kama ambavyo lawama nyingi katika skandali hii zinaelekezwa kwa Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo na Katibu na Katibu Mkuu wake, Eliachim Maswi, sambamba na Mwanasheria Mkuu, Frederick Werema, huku Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, akishutumiwa kwa kushindwa kusimamia vema watendaji walio chini yake, wenye kustahili kubeba lawama kubwa zaidi ni Rais Kikwete na idara yetu ya Usalama wa Taifa.
Ninaandika makala hii kabla ya taarifa za uchunguzi za CAG na TAKUKURU kusomwa hadharani na ‘Kamati ya Zitto’ (PAC), kwahiyo ni vigumu kubashiri hatma ya suala hili. Hata hivyo, uzoefu wa skandali zilizopita, kuanzia Richmond, EPA, Mabilioni  yaliyofichwa Uswisi, Meremeta, Tangold, nk, si ajabu iwapo wahusika wakuu watalindwa na Watanzania kuachwa ‘wanang’aa macho tu.’
Muda mfupi uliopita, zimepatikana taarifa kwamba ripoti hiyo ya PAC imeonekana mitaani huku kurasa zenye majina ya wahusika zikiwa zimenyofolewa. Binafsi ninaamini huo ni ‘uhuni’ tu unaofanywa kuwachanganya Watanzania.
Lakini ukijumlisha na tukio linalodaiwa la kunyweshwa sumu Mbunge Nimrod Mkono, ni muhimu kutodharau nia, sababu na uwezo wa mafisadi kupambana na ukweli kuhusu skandali hii.
Nihitimishe makala hii kwa kumkumbusha Rais Kikwete- kwa mara nyingine - kuwa chini ya mwaka mmoja kutoka sasa atarejea ‘uraiani.’ Ni muhimu kwake kutumia miezi hii michache iliyobaki kurejea ahadi aliyotoa mara baada ya kuapishwa kuwa Rais wetu mwaka 2005 kuwa hatowaonea aibu mafisadi. Tungependa tumkumbuke kwa mema lakini sio rekodi ya kuliingiza taifa kwenye korongo refu la ufisadi.
Kwa ndugu zangu wa Idara ya Usalama wa Taifa, ninawasihi mtambue mzigo mkubwa mnaowabebesha Watanzania masikini kumudu gharama za operesheni zenu. Kwanini msijiskie aibu  kuwasaliti wanyonge hawa –wengi wakiwa ni ndugu, jamaa na marafiki zenu – kwa kutotimiza majukumu yenu ipasavyo?
TUSIPOZIBA UFA TUTAJENGA UKUTA

World AIDS Day 2014 Theme

UKIMWI ulikuwepo na bado upo, na hadi sasa dalili za kuutokomeza ugonjwa huo bado ni ndogo kwani hakuna kinga wala tiba.

Una na fasi ya kuchangia mapambano dhidi ya ugonjwa huu

ACHA ZINAA

KUWA MWAMINIFU

IKISHINDIKANA, TUMIA KINGA

Lakini badala ya kuamini tu kuwa upo salama, ni muhimu pia kufanya vipimo vya ugonjwa huo ili kutambua kama upo salama au umeathirika. Ukiwa salama, Mshukuru Mungu na endelea kuwa makini. Ikitokea bahati mbaya kuwa umeathirika, usikate tamaa kwani kuna matibabu mbalimbali na ya uhakika ya kumwezesha mwathirika wa ugonjwa huu kuishi maisha marefu (japo si tiba kamili).

Iwapo ndugu, jamaa au rafiki yako ameathirika, usimtenge. Mpatie kila aina ya sapoti ikiwa ni pamoja na kum-treat kama binadamu mwenzio. 

Sikiliza wimbo huu wa 'Mshikaji Mmoja' wa msanii wa Kitanzania JOSLIN ambao una mafunzo mengi kuhusu UKIMWI (isipokuwa hitimisho kuwa "ukiupata ni kifo") 

9 Nov 2014

Watafiti wamefanikiwa kubaini kwani aina mbaulimbali za viumbe hai vina sehemu za siri za aina tofauti. Katika nyoka na viumbe wanaotambaa, sehemu zao za siri zimeumbika katika namna zinashabihiana na miguu, na hivyo kutengeneza sehemu za siri mapacha. Katika binadamu, sehemu za siri zimeundwa kwa namna ya mkia/ kiishio cha uti wa mgongo, na hivyo kuwa na sehemu ya siri moja tu.

Soma zaidi kuhusu matokeo ya uchunguzi huo kwa kubonyeza HAPA

Embedded image permalink
Gazeti la The Citizen la Tanzania linamwita 'lulu iliyofichika' (hidden gem, kwa kimombo). Huyu ni Leo Mkamia, msanii wa Kitanzania na mwanzilishi wa aina ya muziki ujulikanao kama 'Swahili Blues.'

Siku chache zilizopita, Leo alirekodi wimbo wake mpya uitwao 'Pamoja.' Miongoni mwa yatakayoonekana katika video ya wimbo huo ni performance ya kihistoria ya msanii huyo katika moja ya vyuo vikuu vikubwa hapa Uingereza, Nottingham University, ambapo Leo alifanikiwa kuwaimbisha Kiswahili baadhi ya wahadhiri na wanafunzi wa chuo hicho kikuu. Katika shughuli hiyo, Leo aliimba na kwaya ya Nottingham Academy.

Kinachomfanya Leo kuwa msanii wa kipekee kutoka Tanzania kuwa na fursa kubwa ya kutawala anga za muziki kimataifa ni ukweli kwamba amefanikiwa kuanzisha kitu kipya- muziki aina ya Swahili Blues- na ambao tayari umeanza kukubalika kimataifa.

Mtaji mkubwa wa Leo ni ukweli kwamba anatoka familia ya muziki.Unamkumbuka mkongwe wa gitaa Henry Mkanyika? Basi huyo ni baba mzazi wa Leo, ambaye alianza kucharaza gitaa akiwa na umri wa miaka minane tu.

 

Kwa sasa Leo ni miongoni mwa wasanii wachache mno, sio tu wa Tanzania, bali Afrika nzima kwa ujumla, ambao sura na sauti zao sasa 'zimezoeleka kwenye vituo vya radio na televisheni vya kimataifa kama BBC. Na katika kuthibitisha hjilo, Leo alihojiwa na BBC mara baadha ya performance hiyo ya kihistoria huko Nottingham.



Pamoja na kufanya vizuri kimataifa, Leo bado anathamini asili yake. Kama video ya pili inavyoonyesha, Leo alifanya mahojiano na mtandao mkubwa na maarufu wa burudani Tanzania na Afrika kwa ujumla wa Bongo5. Kadhalika, msanii huyo anapata sapoti kubwa kutoka kwa mmoja wa waasisi wa muziki wa Hip-Hop nchini Tanzania, lejendari @XamiaSiku4Saa4 wa kundi maarufu kabisa la Kwanza Unit. Ieleweke kwamba katika shughuli za muziki, kupata 'endorsement' ya mkongwe wa muziki ni uthibitisho kuwa msanii husika anafanya kazi nzuri mno.

Kama Watanzania, tuna wajibu na kila sababu ya kumuunga mkono Leo, kwani sio tu anaitangza Tanzania yetu bali pia anautambulisha utamaduni wetu-kwa maana ya lugha ya Kiswahili- kupitia muziki wake wa Swahili Blues.

Unaweza kufuatilia maendeleo yake ya kimuziki kwa akaunti zake mbalimbali za mitandao ya kijamii: Twitter na Facebook  na katika tovuti yake sambamba na ukurasa wake wa YouTube









5 Nov 2014


Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.