30 Jan 2015

l


Angalia dakika ya 3,14  hadi dakika ya 3,19, baadhi ya waandamanaji wanasema "TUUENI..."
Angalia pia kuanzia dakika ya 3.21 ambapo polisi wanaanza kurusha risasi (sina hakika kama ni risasi za moto au bandia) lakini kitu cha kukiangalia kwa makini ni ukweli kwamba ukiacha watu wachache wanaoonekana kutishwa na milio hiyo ya risasi, idadi kubwa tu ya watu inaonekana kutotishika. Hali hiyo inaendelea hata baada ya 'king'oling'oli' cha polisi kinapooanza kulia na hatimaye polisi kutembeza kipigo cha kinyama.

Licha ya kuumia mno kuona Polisi wakitumia nguvu kubwa katika tukio ambalo lingeweza kabisa kumalizwa kwa amani pasipo haja ya kurusha risasi japo moja au kuwapiga na hatimaye kuwakamata waandamanaji akiwemo Mwenyekiti wa CUF Prof Lipumba, kilichonipa hofu ni jinsi taratibu wananchi wanavyoanza kuota 'usugu' dhidi ya unyanyasaji wa polisi. 

Inapofika mahala wananchi wanaashiria bayana kuwa wapo radhi kuuawa, na kuwaambia polisi waziwazi kuwa TUUENI, basi kwa haki tumeshafika mahala pabaya. Na kama nilivyobainisha hapo juu, na kama inavyoonekana kwenye video hiyo, imefika mahala wananchi wameanza kuzowea sauti za risasi sambamba na mabomu ya machozi.

Hii ina maana gani? Wakati tayari wananchi wameshaonyesha kuzowea unyanyasaji na unyama wa polisi wetu na kuwa tayari kwa lolote lile, yayumkinika kubashiri kuwa kuna siku sio tu wananchi wataweka kando uoga na kuendeleza 'usugu' huo nilioueleza hapo juu bali pia wanaweza kujibi mashambulizi.

Uchambuzi mwepesi ni kwamba wakati polisi hawana njia nyingine zaidi ya hizi wanazotumia kila siku: kutumia nguvu kuvunja maandamano ya amani, wananchi wanapata nguvu mpya kwa kuondoa uoga na kuwaacha polisi wafanye watakalo. Upo uwezekano wa wananchi hao kutoishia hapo tu bali badala ya kuwaachia polisi wawaonee, WANAWEZA KUJIBU MASHAMBULIZI. Na kwa mwenendo ulivyo, hatuko mbali na hali hiyo.

Ni vigumu kubashiri ni lini polisi wetu watathamini haki za binadamu na uhai wa wananchi wasio na hatia. Ni vigumu zaidi kutarajia mabadiliko kutoka kwa mwana-CCM yoyote yule atakayemrithi Kikwete baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.Na ndio maana hujaskia yeyote kati ya waliotangaza nia ya kuwania Urais kupitia CCM akilaani unyama huo wa polisi. Walaani kwanini ilhali wao wana kinga ya kudumu dhidi ya polisi? Japo Rais kutoka chama cha upinzani anaweza kutugeuka, lakini katika mazingira ya kawaida ya kibinadamu angalau yeye naye atakuwa ameshaonja unyama wa polisi wetu na ni rahisi kwake kuchukua hatua kuliko hao wasioguswa na polisi.

Kwako msomaji, nakusihi uiangalie video hii kwa makini zaidi ya hayo niliyotanabaisha hapo juu. Jiulize, kama wanaweza kumfanyia LIPUMBA hivyo, watashindwa kukufanyia wewe, familia yako, nduguzo au jamaa zako? Sikiliza malalamiko ya huyo mwanamama katika dakika ya  6.24 na uyafanyie kazi.

TANZANIA ISIYO NA UNYAMA WA POLISI INAWEZEKANA

29 Jan 2015

AlexanderLitvinenko.jpg
Ushushushu unaendelea kuwa ni moja ya taaluma hatari kabisa kwa maana ya kutembea na roho mkononi pindi mambo yakienda mrama. Tatizo kubwa la ushushushu sio kutoka kwa maadui wa nje (kwa maana ya taifa la nje au maadui wasio wa kitaifa- non-state actors) bali pia hata maadui wa ndani. Kiasili, migogoro au kukosana ni sehemu ya 'kawaida' katika maisha yetu wanadamu.

Mie katika familia yetu tumejaaliwa kuwa na mapacha. Vitinda mimba katika familia yetu ni Kulwa na Doto. Hawa walipishana kuzaliwa kwa dakika chache tu, na wamefanana mno kiasi kwamba ninapokutana nao baada ya kupotean kidogo tu inabidi niwaulize yupi ni Kulwa na yupi ni Doto. Pamoja na hali hiyo, kuna nyakati hutofautiana na hata kugombana. 

Kwa mantiki hiyo, si suala la ajabu kwa mwajiriwa kukosana na mwajiriwa wake. Wakati kukosana na mwajiri wako katika taaluma nyingine kwaweza kupelekea kushushwa cheo, kuhamishwa au kupoteza ajira, kwa ushushushu hali ni tofauti kabisa. Kutibuana na mwajiri kwaweza kupelekea kifo, kama stori hii hapa chini inavyotanabaisha.

Ukisoma au kusikia balaa lililomwandama Alexander Litvinenko (pichani juu) hadi kifo chake, waweza kudhani ni simulizi kutoka kwenye filamu au riwaya flani. Litvinenko aliwa shushushu wa shirika la ushushushu la Russia, FSB, katika kitendo cha kubaliana na uhalifu mkubwa (organised crime). Kabla ya kuwa shushushu, Litvinenko alikuwa mwanajeshi ambapo alipanda cheo hadi kufikia ngazi ya ukamanda wa platuni.

Mwaka 1986, Litvinenko alianza kuingia kwenye taaluma ya ushushushu baada ya kuwa 'recruited' kuwa mtoa habari (informant) Shirika la zamani la ushushushu la Russia KGB, katika kitengo cha kupambana na ujasusi (counterintelligence). Miaka miwili baadaye, Litvinenko alihamishiwa rasmi KGB kwenye Kurugenzi Kuu ya Tatu iliyokuwa inahusika na military counterintelligence. Mwaka huohuo, baada ya kuhudhuria mafunzo ya ushushushu, Litvinenko akawa shushushu kamili katika eneo la kupambana na ujasusi hadi mwaka 1991, ambapo alipandishwa cheo na kuingia katika Federal Counterintelligence Service, shirika la ushushushu baada ya KGB, ambalo lilidumu kutoka mwaka 1991 hadi 1995lilipoundwa upya kuwa shirika la sasa la ushushushu la Russia yaani FSB. Shushushu huyo alipangiwa kitengo kilichohusika na kukabiliana na ugaidi sambamba na kujipenyeza (infiltration) kwenye makundi ya uhalifu mkubwa. Kadhalika, alikuwa na jukumu la kufuatilia 'maeneo ya moto' (hot spots), yaani maeneo nyeti ndani ya Russia na katika nchi znyingine zilizokuwa ndani ya USSR. Wakati wa vita ya Chechnya, Litvinenko alifanikiwa kupandikiza mashushushu kadhaa ndani ya Chechnya.

Mwaka 1994, Litvitenko alikutana na mmoja wa waliokuwa matajiri wakubwa nchini Russia, Boris Berezovsky (pichani chini) alipokuwa anafuatilia jaribio la mauaji dhidi ya tajiri huyo.


 Hatimaye akaanza kufanya kazi za pembeni kwa ajili ya Boris, na baadaye akawa msimamizi mkuu wa ulinzi wa kibopa huyo. Ofkoz 'ajira' hiyo ya Litvitenko kwa tajiri huyo ilikuwa sio halali lakini dola iliwavumilia hasa ikizingatiwa kuwa mishahara ya mashushushu kama yeye ilikuwa kiduchu.

Mwaka 1997 shushushu huyo alipandishwa cheo na kuingia Kurugenzi ya Uchambuzi na Ukandamizaji wa makundi ya uhalifu mkubwa, akiwa na wadhifa wa mtendaji mwandamizi na naibu mkuu wa Idara ya Saba.

Mwishoni mwa mwaka huo, shushushu huyo alitoa tuhuma nzito kuwa alipewa amri ya kumuua Boris.Mwaka uliofuata, Boris alimtambulisha Litvinenko kwa Vladmir Putin, rais wa sasa wa Russia lakini wakati huo akiwa shushushu mwandamizi wa FSB.
Putin akiwa amezungukwa na walinzi wake

Tatizo ni kwamba Litvinenko alikuwa akipeleleza ufisadi ambao Putin anadaiwa kuwa mhusika. Mwaka huohuo, shushushu huyo na baadhi ya wenzake wallijitokeza hadharani kueleza kuhusu njama za kutaka kumuuwa tajiri Boris.Baada ya tukio hilo, shushushu huyo alitimuliwa FSB na Putin alitanabaisha kuwa ndiye aliyetoa uamuzi huo.

Oktoba 2000, Litvinenko alitoroka Russia na familia yake na kwend Uturuki ambako aliomba hifadhi ya ukimbizi katika Ubalozi wa Marekani jijini Ankara lakini maombi yake yalikataliwa. Inaaminika kuwa kukataliwa huko kulitokana na hofu kuwa kuyakubali maombi hayo kungezua matatizo kati ya Marekani na Russia. Mwaka huohuo,shushushu huyo alinunua tiketi ya kusafiri kwa ndege kutoka Ankara kwenda Moscow kupitia London, Uingereza. Alipofika uwanja wa ndege wa Heatrhow kusbiri ndege ya kwenda Moscow, shushushu huyo aliomba hifadhi ya ukimbizi wa kisiasa, ambapo maombi yake yalikubaliwa mwaka mmoja baadaye, si kwa sababu ya uelewa wake wa mambo ya ushushushu bali kwa sababu za kibinaadamu (humanitarian grounds).

Wakati akiwa London, Litivnenko alijihusisha na uandishi wa habari, sambamba na kumsapoti tajiri Boris (aliyekimbilia Uingereza) katika mapambano ya kiharakati dhidi ya utawala wa Putin. Oktoba 2006, shushushu huyo alipatiwa uraia wa Uingereza.

Wakati huohuo, gazeti la Independent la hapa, liliripoti kuwa Litvinenko alikuwa akitumia na shirika la ujasusi la Uingereza, MI6 kutokana na ushahidi wa malipo yaliyokuwa yakifanywa na shirika hilo kwa shushushu huyo.

Makao makuu ya shirika la ujasusi la Uingereza MI6 kwenye kingo za Mto Thames, eneo la Vauxhall, jijini London


Mwaka 2007, gazeti moja la Poland lilidai kuwa picha ya Litvinenko ilikuwa ikitumika kwenye mazoezi ya kulenga shabaha (kama huelewi, hiyo ni ishara ya kuwindwa kuuawa). Kabla ya hapo, mwaka 2002, shushushu mmoja wa FSB, Mikhail Trepashkin, alimwonya Litvinenko kuwa kulikuwa na mpango wa kumuuwa uliokuwa ukiandaliwa na FSB. Mwaka huohuo, shushushu huyo alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela kwa tuhuma za rushwa, japo alikuwa nje ya Russia.
50pxx50pxpx
Nembo ya Shirika la Ushushushu la Russia FSB

Hata hivyo, wakati flani, wasifu wa shushushu huyo ulichafuka baada ya kupatikana taarifa kuwa alikuwa akiwatishia kuwaumbua matajiri kadhaa wa Russia kuhusu uhusika wao kwenye uhalifu mkubwa, na kudai pauni 10,000 kila mara ili asiwaumbue.

Wakati wa uhai wake, shushushu huyo alitoa tuhuma kadhaa dhidi ya Putin, Russia na mwajiri wake wa zamani FSB. Miongoni mwa tuhuma hjizo ni Russia kuhusika na mashambulizi katika bunge la Armenia yaliyopelekea kifo cha Waziri Mkuu wa nchi hiyo Vazgen Sargsyan, FSB kufanya mauaji nchi Russia na kuwalaumu magaidi wa nje ili kupata uhalali wa kufanya ubabe nje ya nchi hiyo, mdai ya uhusiano kati ya Russia na Al-Qaeda, nk.

Novemba 2006, Litvinenko aliugua ghafla na kulazwa. Baadaye, vipimo vilibaini kuwa alidhuriwa kwa kemikali ya sumu ya Radionuclide Polonium-210. 

Litvinenko akiwa hospitalini jijini London baada ya kudhuriwa na sumu

Katika mahojiano, shushushu huyo alieleza kuwa alikutana na mashushushu wawili wa FSB Dmitry Kovtun na Andrei Lugovoi.Japo wote wawili walikanusha kumdhuru shushushu mwenzao, nyaraka zilizovuja za Ubalozi wa Marekani zinaeleza kuwa chembechembe za kemikali iliyomdhuru Litvinenko zilikutwa kwenye gari alilotumia Kovtun huko Ujerumani.

Dmitry Kovtun, right, with Andrei Lugovoi in 2007. Both deny murdering Alexander Litvinenko
Andrei Lugovoy (kushoto) na Dmitr Kovtun 

Baadaye mwezi huo, Litvinenko alifariki baada ya moyo wake kushindwa kufanya kazi kutokana na sumu iliyomdhuru. Kabla ya kifo chake, shushushu huyo aliandika taarifa iliyoeleza ameuawa.

Juzi, taarifa ya uchunguzi wa kifo chake ilieleza kuwa njia iliyotumika kumuuwa ilikuwa ni ya hatari zaidi kutokea katika Nchi za Magharibi.

Dokta Nathaniel Cary alieleza kuwa kifo cha shushushu huyo mwili wake ulidhurika vibaya mno kabla ya kifo chake kiasi kwamba ililazimu awekwe katika wodi maalum amapo wagonjwa hutengwa kwa ajili ya uchunguzi wa hali ya juu. Alisema kuwa shushushu huyo aliuawa kwa mionzi ya sumu. Kifo chake kilitokea takriban wiki tatu baada ya kunywa chai ambayo baadaye ilifahamika kuwa ilinyunyiziwa sumu ya Polonium.

Dokta Cary alieleza kuwa yye na timu yake walilazimika kuvaa suti mbili za kujikinga (kama zile za matabibu wa Ebola) ambazo ziliwekwa hewa ndanikupitia mirija maalum ili kukwepa athari za sumu husika. Alisema, "uchunguzi huo wa maiti ulikuwa ni usio wa kawaida kabisa katika historia ya nchi za Magharibi"

Natumaini habari hii imekusaidia msomaji kutambua hatari zinazowakabili mashushushu katika utendaji kazi wao, na hasa pale 'wanapotibuana' na aidha waajiri wao au watawala.





Enzi hizo: Rais Kikwete akiwa na James Rugemalira

RAIS Jakaya Kikwete anapaswa kuwajibika binafsi katika kashfa ya ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi katika Akaunti ya Tegeta Escrow. Saed Kubenea anaandika…(endelea)

Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mabere Marando amesema, Rais Kikwete, ndiye aliyeruhusu kiasi cha Sh. 321 bilioni kuchotwa katika mazingira yaliyosheheni udanganyifu.

“Fedha zile zimechukuliwa kwa maelekezo ya Rais Kikwete ili kumuwezesha chama chake kufanikishe kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka huu,” ameeleza Marando.

Hata hivyo, Marando anasema, “Tumeambiwa na watu waliokaribu na chama hicho, kuwa ni sehemu ndogo sana ya fedha iliyoibwa zilizofikishwa CCM. Nyingi ya fedha hizo zimechukuliwa na familia ya rais mwenyewe.”

Taarifa zinasema, familia ya Rais Kikwete imepata zaidi ya Sh. 9 bilioni, kutoka katika mgawo wa fedha zilizohifadhiwa katika akaunti ya Escrow.


“Kikwete anajua kila kitu. Yule singasinga – Harbinder Singh Sethi – alitokea Ikulu. Mpango wa uchotaji wa fedha za umma ulipangwa Ikulu na ulitekelezwa kwa maelekezo ya rais,” ameeleza.


Taarifa zinasema, anayejiita na kuitwa na serikali kuwa ni “mmiliki mpya wa IPTL/PAP,” Harbinder Singh Sethi, alichotewa fedha hizo baada ya kufikishwa Ikulu na baadaye akakutanishwa na gavana wa BoT, Prof. Benno Ndullu; na kutoka hapo alikwenda kukwapua mabilioni hayo ya shilingi hata bila kumfahamisha James Rugemalira – mbia mwenzake.

Sakata la ukwapuaji wa fedha katika akaunti ya Escrow ndilo lililomtupa nje ya ofisi, aliyekuwa waziri wa nishati, Prof. Sospeter Muhongo.

Taarifa zinasema, Prof. Muhongo, ni miongoni mwa wanaotajwa kunufaika na fedha za Escrow zilizopitia benki ya Stanbic. Mwingine ambaye jina lake lilitajwa bungeni na mmoja wa wabunge wa upinzani, ni Albert Marwa.

Marando anasema, “Pamoja na kujiuzulu kwa Prof. Muhongo, bado haitoshi bila kuhojiwa au kuwajibishwa kwa gavana Ndullu, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, Katibu Mkuu wizara ya Fedha, Dk. Servacius Likwalile na maofisa wa ikulu na hata rais mwenyewe ambaye ndiye aliyeruhusu fedha hizo kutolewa.”

Akiongea kwa kujiamini, Marando anasema, “Wizi huu ulianzia Ikulu na umefanyika kwa baraka za Ikulu na mbele ya macho ya rais. Umewashirikisha baadhi ya maofisa wake na hata familia yake.”

Dk. Likwalile ndiye aliyewasilisha kwa gavana wa BoT kwa ajili ya utekelezaji, maagizo ya Rais Kikwete kuwa fedha katika akaunti ya Escrow zilipwe kwa PAP.

Alikuwa akirejea maagizo kutoka kwa Rais Kikwete kwa kunukuu barua ya tarehe 13 Novemba 2013, ambayo ilisainiwa na Katibu wa Rais, Bw. Prosper Mbena.


25 Jan 2015

24 Jan 2015

Whatsapp kwa sasa ni chaguo la wengi linapokuja suala la mawasiliano yasiyohitaji malipo. Awali ilikuwa sio tu haiwezekani kutumia app hiyo katika kompyuta yako bali pia haikuwezekana kuitumia katika 'devices' mbili tofauti kwa namba moja ya simu. Kwa upande mmoja app hiyo haikuwezekana kutumika katika kompyuta, kwa upande mwingine, ili kuitumia katika Tablet yako, ililazimu utumia namba tofauti za simu wakati wa kujisajili, kwani ukitumia namba uliyojisajili kwa simu kwenye Tablet, app hiyo haifanyi kazi tena kwenye simu.

Habari njema ni kwamba sasa waweza kutumia Whatsapp sio tu kwenye Kompyuta bali pia kwenye Tablet yako.

Tuanze na Whatsapp kwenye kompyuta:

1. Kwa kutumia browser ya Chrome, fungua tovuti hii https://web.whatsapp.com/
2. Utakutana na QR code hii


3. Nenda kwenye Whatsapp yako kwenye simu
4. Bonyeza 'menu' (duara ya kijani - kutegemea na aina ya simu yako) kisha nenda 'Whatsapp Web' kama ilivyo pichani chini 


5. Ukibonyeza 'Whatsap Web' itafungua QR Scan kama hapa chini (inabidi simu yako iwe na app hiyo ambayo inapatikana Google Play  )


6. Elekeza QR Scanner hiyo kwenye ukurasa huu https://web.whatsapp.com/
7. Kazi imekwisha. Browser yako sasa itakuwa imeunganishwa na Whatsapp yako ya kwenye simu

Kwenye Tablet.

Hatua zote ni kama hapo juu ila tofauti tu badala ya Kompyuta, utakuwa unatumia Tablet. Kumbuka kuwa kwa sasa browser pekee inayoweza kutumika ni Chrome. Pia waweza kutumia.

Ukikwama, nifahamishe kwa comment katika post hii. Karibuni sana.

ANGALIZO: Maelezo haya ni kwa Android devices ambazo ndo nazitumia. Sijafanya uchunguzi kuhusu iOS devices kama iPad au Mac computers.

Share is caring, ukishasoma na kuelewa, mfahamishe na mwenzako


Siku ya mwaka mpya nilitangaza huko Twitter kuhusu dhamira yangu ya #ProBono yaani kuwahamasisha watu wenye uwezo, vipaji au nafasi mbalimbali kuisadia jamii bure. Kimsingi, huku nchi za Magharibi, sekta ya kujitolea pasi malipo imekuwa na msaada sana kwa jamii. Ninaamini kwamba nasi tukijaribu, itakuwa na msaada mkubwa sana hasa tukizingatia jinsi umasikini unavyowakwaza wanajamii wengi.

 So far, mwitikio umekuwa wa kuridhisha. Tayari, mwanasheria mmoja mahiri huko nyumbani anashughulikia bure kesi ya mwanajamii mmoja huku akiridhia kupelekewa kesi nyingine inayohusu mirathi. Pia gwiji mmoja wa fani ya PR na Marketing amekubali kumsaidia mwanajamii mmoja kuingia kwenye fani hiyo. Vilevile, designer mmoja wa kimataifa huko nyumbani amekubali kumsaidia desgner mchanga aliyekuwa anahitaji mwongozo katika fani hiyo.Kadhalika, dada mmoja mtaalam wa mambo ya fedha amekubali kutoa msaada wa ushauri wa kifedha bure, sambamba na wasanii wawili maarufu wa huko nyumbani, mmoja wa Bongoflava na mwingine wa Bongo Movies.


Lengo la makala hii sio kuzungumzia kuhusu #ProBono bali muda mfupi uliopita, nilikutana na habari ambayo kwa namna flani inahusiana na suala hilo la #ProBono. Hivi unawakumbuka TLC? Ni kikundi cha akinadada watatu wa Marekani ambao walivuma sana miaka ya nyuma katika fani ya R&B.

Labda kabla ya kwenda mbali, niamshe kumbukumbu yako kwa mmoja wa nyimbo zao maarufu, Red Light Special (TAHADHARI: Hii ni 'dirty version.')




Kwa bahati mbaya, Aprili 25, 2002 kundi hili la akinadada watatu lilipatwa na mkosi wa kuondokea na mwenzao aliyekuwa maarufu zaidi, Lisa Lopez au maarufu kama 'Left Eye, (pichani chini) aliyefariki kwa ajali ya gari akiwa mapumzikoni nchini  Honduras.


Kifo cha mwenzao huyo kililiathiri sana kundi hilo, kwa sababu zilizo wazi.

Hata hivyo, katika jitihada zake za kurejea tena katika anga za muziki, wasanii wawili waliobaki katika kundi hilo, Rozonda 'Chilli' Thomas na Tionne 'T-Boz' Watkins, waligeukia wazo la ujasiriamali linalotamba sasa katika nchi za Magharibi hasa Marekani, linalofahamika kama 'crowdfunding' (kuomba jamii ikuchangie fedha) kupitia jukwaa la kufanya hivyo linalojulikana kama KICKSTARTER

T-Boz (kushoto) na Chilli

Habari njema ni kwamba siku nne tu baada ya kuanzisha kampeni yao ya Kickstarter kuwapatia dola za kimarekani 150000 kwa ajili ya kutengeneza albamu yao mpya, na ya kwanza baada ya miaka 10 ya ukimya, wamefanikiwa kupata michango zaidi ya kiwango walichokusudia.Hadi kufikia juzi, walikuwa wameshachangiwa Dola za kimarekani 180000, ikiwa ni Dola 30000 zaidi ya kiwango walichokusudia.

Kilichowapa moyo zaidi ni pale walipotembelea ukurasa wao wa Kickstarter


na kubaini kuwa msanii mahiri wa Pop, Katy Perry (pichani chini), ameahidi kuwachangia dola 5000. Kadhalika, kundi maarufu la zamani la New Kids on the Block limeahidi kuwachangia wanadada hao dola 20,000

Baada ya kusoma habari hiyo nikakumbuka wazo langu la #ProBono na kujiuliza, hivi haiwezekani kuwasaidia wanajamii mbalimbali, kwa mfano wasanii wetu, katika namna hiyo kundi la TLC linasaidiwa na jamii kutimiza lengo lao la kutengeneza album mpya?

Jibu ni kwamba inawezekana, japo si rahisi sana kuwashawishi watu wachangie fedha kwa ajili ya mafanikio ya mtu mwingine. Hata hivyo, cha muhimu hapa ni moyo wa kujitolea. Kwahiyo basi, ushauri wangu, hasa kwa kuanzia na wasanii, mfanye moja kati ya haya mawili:

Kwanza, aidha mjaribu bahati zenu huko Kickstarter, kama wanavyofanya TLC japo yaweza kuwa vigumu kwa msanii asiye maarufu

Au pili, tumieni mpango wa #ProBono kama nilivyoueleza ambapo kwa pamoja tutahamasisha upatikanaji wa mahitaji mbalimbali kwa ajili ya utengenezaji na uzinduzi wa kazi ya msanii husika. 

Sharing is always caring!



15 Jan 2015



 

30 Dec 2014



Nesi mmoja aliyekwenda Sierra Leone kusaidia harakati za kukabiliana na janga la ugonjwa wa Ebola, amerudi Uingereza akiwa ameambukizwa ugonjwa huo, na hivi sasa amelazwa kwenye kituo cha maradhi ya kuambukiza cha Browlee katika Hospitali Kuu ya Gartnavel, hapa Glasgow.

Nesi huyo anatarajiwa kuhamishiwa London kwenye hospitali maalum ya Royal Free Hospital.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu wa Uskochi, Nicola Sturgeon, amewahakikishia wakazi wa Glasgow na Uskochi kwa ujumla kuwa uwezekano wa kusambaa kwa ugonjwa huo kutokana na maambukizi ya nesi huyo ni 'sawa na sifuri.'

Hata hivyo, bado kuna maswali ilikuwaje nesi huyo aliyepimwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Heathrow, London, kabla ya kuunganisha ndege na kuja Glasgow, hakugundulika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo hatari usio na kinga wala tiba.

Profesa Jonathan Ball, mtaalam wa 'molecular virology' katika Chuo Kikuu cha Nottingham, ameeleza kuwa kesi hiyo inaashiria ugumu wa mkakati wa kupima wasafiri kutoka nchi zilzoathirika na Ebola wanapoingia Uingereza.

Chini ni baadhi ya picha zinazohusiana na habari hii ambayo waweza kuisoma kwa kirefu HAPA

A female health worker who returned from Sierra Leone last night is being treated for Ebola at Glasgow's Gartnavel Hospital (pictured), the Scottish Government confirmed
Hospitali ya Gartnavel

Safari ya nesi aliyeambukizwa Ebola, kutoka Sieera Leone hadi Glasgow.



The health worker was admitted to hospital early yesterday morning after feeling unwell and was placed in isolation 

The ebola patient is being treated at the specialist Brownlee Unit for Infectious Diseases at Gartnavel Hospital
Kituo cha maradhi ya kuambukiza cha Brownlee

24 Dec 2014

Awali,kupitia akaunti yake ya Twitter, Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC Swahili) iliripoti ifuatavyo



Hata hivyo, baada ya kuzongwa na baadhi ya WANAHARAKATI huko Twitter walioonyesha kukerwa na hatua hiyo ya nchi wahisani, Mwenyekiti wa nchi wahisani, Balozi wa Finland nchini Tanzania Sinikka Antila (@SinikkaAntila) alifafanua kwa tweet ifuatayo 


Kwa lugha ya taifa, Balozi huyo anaeleza kwamba "vyombo vya habari havipo sahihi. Asilimia 15 ya msaada ulioahidiwa kwa bajeti ya mwaka 2014/15 ilitolewa kabla ya hotuba ya Rais (Kikwete)."

Hata hivyo, licha ya kauli hiyo ya Balozi Antila kutanabaisha kuwa BBC Swahili waliripoti ndivyo sivyo kuwa wafadhili wameamua kutofa fedha hizo baada ya kuridhishwa na hotuba ya Rais Kikwete, bado kuna swali gumu kuhusu suala hilo, nalo ni JE NCHI WAFADHILI ZILITUHADAA ZILIPODAI KUWA ZIMESITISHA MISAADA HADI HATUA ZITAKAPOCHUKULIWA KUHUSU SUALA LA ESCROW?

Swali hilo linatokana na kauli ya Balozi huyo wa Finland kuwa fedha hizo zilishatolewa hata kabla ya hotuba ya Rais Kikwete, ikimaanisha aidha nchi hizo wahisani zilikuwa zina hakika kuwa Rais Kikwete angechukua 'hatua hizo za kuwaridhisha wafadhili' au 'walituzuga tu' kuhusu kusitishwa misaada hiyo.

Kadhalika, kauli ya Balozi Antila haikanushi kuridhishwa kwa wafadhili na hotuba ya Rais Kikwete, ambayo Watanzania wengi wanaamini kuwa imewalinda mafisadi hasa ikizingatiwa mzigo mkubwa wanaoubeba kutokana na sakata la muda mrefu la IPTL. Kwa Rais Kikwete kushindwa kumaliza sakata hilo, na kuridhia kuwa pesa za Tegeta Escrow ni za IPTL/ PAP, ina maana Watanzania wataendelea kulipa mamilioni ya shilingi kila siku kwa huduma ya umeme ambayo kimsingi ni hewa.

Binafsi ninaguswa na uamuzi wa nchi wahisani kwa sababu kama mkazi wa Uingereza, ninalipa kodi mbalimbali, ambazo sehemu ya kodi hiyo ipo katika misaada inayotolewa na nchi hii kwa Tanzania. Wakati sina kipingamizi kwa nchi hizo kuisaidia Tanzania, siungi mkono kabisa kuendelea kutoa fedha zinazoishia kuwaneemesha mafisadi kwa kunenepesha akaunti zao, kuongeza idadi za mahekalu na magari yao ya thamani na kukuza idadi ya nyumba zao ndogo.

Ufadhili usiozingatia maslahi ya nchi fadhiliwa sio tu ni upuuzi bali pia ni ku-abuse fedha za walipakodi katika nchi wafadhili.

18 Dec 2014

Desemba 9, ilikuwa siku yangu ya kuzaliwa. Niliadhimisha sikukuu hiyo kwa sala, kumshukuru Mungu kwa kunijaalia kuongeza mwaka mwingine katika umri wangu sambamba na kuomba baraka zaidi.
Kadhalika, kama zilivyokuwa sikukuu zangu za kuzaliwa huko nyuma, niliadhimisha siku hiyo kwa kufanya tafakuri ya nilipotoka, nilipo na niendako.
Siku ya kuzaliwa ina pande mbili, moja ya furaha kwa maana ya kutimiza mwaka mwingine katika maisha, na ya pili ni kutambua kwamba umri unakwenda mbele, na hivyo kupitia malengo mbalimbali kuona kama yametimia, na kwa kiwango gani, na wapi panahitaji jitihada zaidi, sambamba na kuweka malengo mapya inapobidi.
Kadhalika, wakati kwa vijana wenye umri mdogo, sikukuu ya siku ya kuzaliwa ni furaha tupu, ambapo kwa mfano, sheria mbalimbali zinatoa ruhusa fulani kwa kutimiza umri fulani, kwa wenye umri mkubwa, sikukuu hiyo huambatana na ukweli mchungu kuwa ‘dakika zinayoyoma.’
Kwa kijana wa miaka 17, kutimiza miaka 18 kunamaanisha fursa ya kupiga kura, kwa mfano. Kwa hapa Uingereza, kutimiza miaka 18 kunamaanisha ruhusa kisheria kutumia kilevi.
Lengo la makala hii si kuzungumzia sikukuu yangu ya kuzaliwa. Ukweli kwamba sikukuu yangu ya kuzaliwa inalingana na sikukuu ya kusherehekea uhuru wa Tanganyika huzua tafakuri nyingine mpya kuhusu nchi yetu.
Wakati sikukuu ya kuzaliwa kwangu ni suala langu binafsi, sikukuu ya uhuru wa Tanganyika ni suala linalomgusa kila mmoja wetu.
Japo hujiskia fahari kuchangia sikukuu ya kuzaliwa na Tanganyika, ukweli mchungu ni kwamba ninalazimika pia kujiuliza nchi yangu imetoka wapi, ipo wapi, na inaelekea wapi, na mara nyingi tafakuri hiyo huvuruga kabisa sikukuu yangu ya kuzaliwa.
Kama nilivyotimiza miaka kadhaa tangu nizaliwe, jana Tanganyika yetu imetimiza miaka 53 tangu ipate Uhuru. Wakati binafsi ninaweza kuhitimisha kuwa angalau nimepiga hatua fulani kimaisha, huku malengo kadhaa niliyojiwekea huko nyuma yakitimia au yakielekea kutimia, kwa mwenzangu Tanganyika hali si nzuri.
Tumefika mahala, baadhi ya Watanganyika wamefikia hatua ya kutamani mkoloni asingeondoka.
Nitakuwa mwenye roho mbaya iwapo nitazungumzia mabaya tu yaliyoiandama na yanayoendelea kuiandama nchi. Lakini kwa vile tafakuri katika siku muhimu kama hiyo inalenga zaidi kuangalia maeneo yanayoifanya isiwe timilifu, basi inakuwa vigumu kutoyapa uzito matatizo badala ya mafanikio.
Kadhalika, siku hiyo ni ya kupima mzani wa mafanikio na kufeli, na pindi mzani ukielemea upande wa kufeli, basi lazima taa ya tahadhari iwashwe kwani hali hiyo yaweza kuashiria matatizo zaidi huko mbele.
Kati ya sababu za kudai Uhuru kutoka kwa mkoloni ni kutaka kujitawala wenyewe, sambamba na kuondokana na mfumo wa kibaguzi uliotufanya tuwe mithili ya wageni katika nchi yetu wenyewe.
Miaka kadhaa baada ya Uhuru, jitihada zilizoongozwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, zilionyesha matunda ya uhuru na si tu tulifanikiwa kwa kiasi kikubwa kujenga jamii yenye usawa lakini pia tulimudu kujitegemea wenyewe.
Matatizo yalianza kujichomoza baada ya Mwalimu kuondoka madarakani na hatimaye kufariki kwake. Kimsingi, nchi yetu ilikuwa kama ipo mikononi mwa Nyerere, na ilikuwa inasubiri aondoke tu ili irejee mahala pabaya pengine zaidi ya ilivyokuwa kabla ya Uhuru.
Ieleweke kwamba wakati mkoloni alikuwa na ‘excuse’ (japo isiyokubalika) ya kuiba raslimali zetu kwa ajili ya matumizi ya viwanda vyao huku Ulaya, wakoloni weusi kwa maana ya Watanganyika wenzetu waliosomeshwa na Watanganyika wenzao waliojinyima ili wapate viongozi, hawana sababu moja hata ya kutusaliti.
Yaani angalau mkoloni angeweza kujitetea kwamba acha niibe kwa sababu hii nchi si yangu. Lakini kwa wakoloni weusi, Watangayika wenzetu wanaoendekeza ufisadi hawawezi kudiriki kujitetea kwa namna yoyote ile, hasa ikizingatiwa kwamba kihistoria, takriban sote ni ndugu kwa kuzingatia asili yetu.
Kwa maana hiyo, kiongozi anayekabidhiwa dhamana kisha akafanya ufisadi, anajiathiri yeye mwenyewe pia kwa sababu mahala fulani, kuna mtu wake wa karibu atakayekuwa mhanga wa ufisadi huo.
Tusiende mbali. Angalia skandali ya ufisadi wa hivi karibuni wa Tegeta Escrow. Baadhi ya wabunge walikuwa wakitokwa na mapovu kutetea kuwa fedha fedha hizo si za umma ilhali nao ni sehemu ya umma wanaoukana. Takriban wote waliojivika kilemba cha itikadi, mdudu anayeiangamiza Tanganyika yetu kwa kasi kubwa.
Si kwamba watu hawa wamekunywa maji ya bendera kiasi cha kutoelewa kitu kingine chochote zaidi ya maslahi ya chama chao bali itikadi yatumika tu kama kilemba cha kufika nia zao mbaya.
Lakini pia suala la Tegeta Escrow limeibua tena tatizo moja linalotukwaza kama Taifa. Hili ni utegemezi wetu kwa wanasiasa na taasisi kama vyama vya siasa na watu, kwa maana ya wanasiasa.
Ukiweka kando kelele ndogo kwenye mitandao ya kijamii kudai wananchi watendewe haki kwa kurejeshewa fedha zilizokwapuliwa katika akaunti ya Tegeta Escrow na wahusika wawajibishwe, kwa kiasi kikubwa suala hilo liliachwa mikononi mwa wanasiasa.
Katika hili, ninaweza kumlaumu Mwalimu Nyerere kidogo. Pengine kwa vile tulikuwa tukihangaika kujenga Taifa lenye kujali usawa wa binadamu, na hivyo kuleta umuhimu wa wateule wachache wa kusimamia mambo, zama hizo zilikuwa za viongozi kama miungu-watu.
Mfumo wa siasa enzi hizo uliwapa madaraka wateule wachache ambao kila walichosema kilikuwa sahihi hata kama si sahihi, na ukaribu wao na watawaliwa ulikuwa mdogo mno.
Miongoni mwa madhara ya mfumo huo ndio hii hali tuliyonayo sasa ambapo wananchi wamekuwa wategemezi wa kupindukia kwa taasisi kama serikali au vyama vya siasa, na watu, hususan, wanasiasa.
Sasa angalau katika zama hizo za Mwalimu, kwa kiasi kikubwa sote tulikuwa na maslahi yanayolingana, yaani ujenzi wa Taifa kwa faida ya wote. Hivi sasa tuna wahuni wengi tu waliojiingiza kwenye siasa kwa maslahi yao binafsi. Na kama nilivyotanabahisha awali, maslahi ya chama yamekuwa kama kitu cha kuficha tu maslahi binafsi.
Ni muhimu kutambua udhaifu wa taasisi zetu na wanasiasa wetu. Lakini hata taasisi hizo zingekuwa timilifu na wanasiasa wetu kuwa imara, ukweli unabaki kuwa wao ni sehemu ya tabaka tawala, na kwa kiasi kikubwa wanatetea maslahi ya tabaka hilo, ilhali wananchi wengi wapo tabaka la chini.
Na kwa vile hatuna tabaka la kati la kueleweka, utegemezi kwa vyama vya siasa/ serikali au wanasiasa utaendelea kuwa kikwazo kikubwa kwa wananchi.
Wakati jana Tanganyika yetu imetimiza miaka 53, hivi kuna anayeweza angalau kubashiri hali itakuwaje miaka 20 kutoka sasa?
Kwa kasi hii ya mafisadi kushindana kuifilisi nchi, Tanganyika ya mwaka 2050, kwa mfano, itakuwa na tembo hata mmoja? Je, madini tuliyonayo ambayo yanawanufaisha zaidi wawekezaji na watawala wetu yatadumu kwa muda gani? Na hata hayo mafuta na gesi ambayo tunanyimwa haki ya kuona mikataba yake, yatakuwa neema au laana  kwetu?
Hadi wakati ninaandika makala hii, maazimio ya Bunge kuhusu skandali ya Tegeta Escrow hayajajibiwa. Ukimya wa Rais Jakaya Kikwete unaanza kuwafanya baadhi ya wananchi kuhisi kuwa tumeliwa.
Wananchi wanaishia kuonyesha masikitiko tu pasipo dalili ya kushinikiza wapatiwe haki yao kwa njia za amani.
Tumeona nguvu ya umma inavyoweza kuzaa matunda. Watanzania walihamasishana hadi msanii Diamond akashinda tuzo tatu kwenye Tuzo za Video za Kituo cha Televisheni cha Channel O (CHOAMVA). Tumeshuhudia pia nguvu ya umma ilivyomwezesha mwakilishi wa Tanzania katika Big Brother 2014 kuwa mshindi na kujinyakulia dola za Kimarekani 300,000. Kwanini basi nguvu hiyohiyo isitumike kushinikiza sio tu maazimio ya bunge kuhusu Tegeta Escrow yafanyiwe kazi bali pia kudai mabilioni yetu yaliyoibiwa na kufichwa katika mabenki nchi Uswisi yarejeshwe?
Nihitimishe makala hii kwa kumtakia mwenzangu Tanganyika heri na baraka ya kutimiza miaka 53. Lakini ninaomba pia kutumia fursa hiyo kumkumbusha (kwa maana ya wananchi wenzangu) kuwa tulipotoka kulikuwa na matumaini, tulipo si kuzuri na tuendako hakueleweki.
Ni wajibu wetu kubadili mwelekeo huu. Hili si suala la hiari bali la lazima iwapo twataka kuiona Tanganyika yetu ikiishi maisha marefu ya furaha na amani.


Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.