11 Dec 2015

‘HAPPY birthday Tanzania…happy birthday me.” Naam, leo ni sikukuu ya Uhuru na Jamhuri, siku ya kuzaliwa kwa Tanganyika (sasa Tanzania Bara), siku ambayo pia ni ya kuzaliwa kwangu.

Nilizaliwa Desemba 9, miaka kadhaa baada ya uhuru wa nchi yetu, na kila ninapoadhimisha siku ya kuzaliwa, ninaadhimisha pia siku ya kuzaliwa kwa nchi yetu.

Kwa kawaida, maadhimisho yangu ya siku ya kuzaliwa huwa sio sherehe bali hutumia siku hiyo kumshukuru Mungu, sambamba na kufanya tafakuri ya nilipotoka, nilipo na niendapo. Sherehe pekee ilikuwa kuimbiwa wimbo wa ‘Happy Birthday’ na marehemu baba, ambaye kwa bahati mbaya hayupo nasi sasa. Kwa hiyo hii itakuwa birthday yangu ya kwanza kukosa ‘sherehe’ hiyo iliyoambatana na sala za kumshukuru Mungu na kuniombea mafanikio.

Lakini wakati wa kusherehekea siku ya kuzaliwa pamoja na ‘birthday-mate’ (mtu mliyezaliwa naye siku moja) Tanzania imekuwa kama tukio la kihistoria na la kujivunia, kwa upande mwingine kila ninapofanya tafakuri kuhusu ‘mwenzangu’ huyo alipotoka, alipo na aendako huishia kupatwa na maumivu.

Si kwamba nimefanikiwa sana kuliko ‘mwenzangu’ huyo bali angalau kwa upande wangu kila nikiangalia nilipotoka, nilipo na niendako, nimekuwa naona mwanga zaidi. Kwa ‘mwenzangu’ Tanzania, wakati huko alikotoka kulileta matumaini, alipo na aendako (kwa miaka ya hivi karibuni) kulinipa shaka.

-Lengo la kupata uhuru halikuwa kumwondoa tu mkoloni bali pia kujenga jamii yenye amani na usawa, pamoja na mambo mengine. Japo katika miaka 54 ya uhuru wetu, Tanzania imeendelea kuwa nchi ya amani kwa maana ya kutokuwepo vita, lakini katika miaka ya hivi karibuni amani kwa maana ya kuwa na uhakika wa mlo wa kesho, au wanafunzi kuwa na hakika ya ajira wanapomaliza masomo au wakulima kuwa na uhakika wa mauzo ya mazao yao, au wagonjwa kuwa na uhakika wa huduma wanayostahili katika vituo vya afya na uhakika katika maeneo mengine, vimekuwa ni mgogoro.

Kadhalika, amani yetu imeonekana kuwanufaisha zaidi ‘mchwa’ wachache walioigeuza Tanzania yetu kuwa shamba la bibi, wenzetu ambao miaka michache iliyopita tuliwaita kupe, wanaovuna wasichopanda, wanaoneemeka kwa jasho la wengine.

Mara kadhaa, maadhimisho ya sikukuu ya uhuru wetu yameambatana na swali gumu, je kweli tupo huru? hasa ikizingatiwa kuwa kwa kiasi kikubwa nchi yetu imeendelea kuwa tegemezi kwa wafadhili, miongoni mwao wakiwa watu walewale tuliowafukuza mwaka 1961.

Kuna wenzetu wengi tu wanaodhani kuwa uhuru wetu ulifanikiwa kumtimua mtu mweupe lakini miaka kadhaa baadaye huku tukiwa huru tumeshuhudia ukoloni mpya unaofanywa na mtu mweusi. Na japo wakoloni hawawezi kuwa na kisingizio cha kututawala, lakini walipoinyonya nchi yetu walikuwa na malengo ya kunufaisha nchi zao na sio watu binafsi. Kadhalika, hawakuwa na uchungu na nchi yetu kwa vile sio yao.

Kinyume chake, wakoloni weusi sio tu ni wenzetu bali wengi wao aidha walisomeshwa bure au kwa fedha za Watanzania wenzao, lakini badala ya kurejesha fadhila kwa kulitumikia taifa kwa uadilifu, wameishia kuwa wanyonyaji wasio na huruma. Tofauti na wakoloni weupe, wenzetu hawa hawana kisingizio japo kimoja kwani wanainyonya nchi yao wenyewe.

Moja ya vikwazo vya kutuwezesha kufaidi matunda ya uhuru ni ukosefu wa uzalendo. Licha ya jitihada kubwa za Mwalimu Nyerere kuhamasisha mapenzi na uchungu kwa nchi yetu – uzalendo- tawala zilizofuatia baada ya yeye kung’atuka zikawekeza katika kuboresha maslahi binafsi badala ya maslahi ya taifa. Japo mabadiliko yaliyoikumba dunia wakati Mwalimu anataka madaraka yalisababisha haja ya mageuzi katika itikadi ya ujamaa, lakini kilichofanyika si mageuzi tu bali kuua kabisa mfumo wa ujamaa.

Kuna wanaodai kuwa isingewezekana kufanya mageuzi ya kisiasa na uchumi huku tukikumbatia mfumo wa ujamaa. Hilo sio sahihi, kwani tunashuhudia taifa kubwa kama China ambalo limefikia hatua ya juu kabisa ya ujamaa yaani ukomunisti, likimudu kuendelea kuwa taifa la kijamaa huku likijihusisha pia na sera za uchumi wa kibepari kama vile uwekezaji.

Nikirejea kwenye siku ya kuzaliwa Tanzania Bara, na yangu, Ninaomba kukiri kuwa baada ya muda mrefu, mwaka huu sikukuu yetu ya kuzaliwa mie na ‘mwenzangu’ inaleta furaha na matumaini.

Na yote hayo ni matokeo ya ninachokitafsiri kama kusikilizwa kwa dua/sala zetu kwa Mwenyezi Mungu kuturejeshea Nyerere na (Waziri Mkuu wa zamani marehemu Edward) Sokoine wengine. Tumejaaliwa kumpata Rais mpya, Dk. John Magufuli, ambaye mwezi mmoja tu tangu aingie madarakani ameweza kwa kiasi kikubwa kurejesha matumaini yaliyopotea.

Na pengine kuashiria kuwa Nyerere amerudi kupitia Dkt Magufuli, mwaka huu tunaadhimisha siku ya uhuru na Jamhuri kwa shughuli za usafi wa mazingira, na hii inakumbusha dhana ya Mwalimu ya Uhuru na Kazi. Na kwa hakika hatuwezi kuwa huru kwa kuwafanyia kazi wenzetu wanaotuibia kila kukicha.

Majuzi akiwahutubia wafanyabiashara wakubwa huko nyumbani (Tanzania), Rais Dk. Magufuli alieleza bayana jinsi tunavyoweza kutoka kundi la nchi masikini na ombaomba na kuwa miongoni mwa nchi wafadhili iwapo tutatumia raslimali zetu vizuri, sambamba na kupambana na ufisadi. Uhuru wa bendera pekee, wa kumwondoa mkoloni mweupe huku tukisumbuliwa na mkoloni mweusi ni tatizo kwani suala si rangi ya mkoloni bali ukoloni wenyewe. Tukimudu kuboresha uchumi wetu na kuweza kujitegemea, tutakuwa na uhuru kamili.

Kadhalika, kama Mwalimu alivyotufundisha, uhuru bila nidhamu ni uwendawazimu. Hatuwezi kuwa na uhuru kamili kama hatuna nidhamu ya matumizi na tuliowapa dhamana ya kutuongoza hawana nidhamu kwa maadili ya taifa.

Ni matumaini yetu wengi kuwa maadhimisho haya ya siku ya uhuru na Jamhuri kwa njia ya uhuru na kazi, sambamba na kasi kubwa ya Dk. Magufuli kutumbua majipu ni ishara njema kuwa Tanzania tuliyoitarajia Desemba 9, 1961 na kufaidika nayo zama za Mwalimu, ipo mbioni kurejea.

Nimalizie makala hii kwa kusema tena ‘Happy birthday Tanzania, happy birthday to me.’

Mungu Ibariki Tanzania.
Mungu mbariki Rais wetu Dk. John Magufuli.

Mungu tubariki Watanzania. 

9 Dec 2015

Siku ya leo ninaadhimisha birthday tatu kwa mfululizo, mbili zangu binafsi na moja pamoja na Watanzania wenzangu. Wakati Tanzania inatimiza miaka 54 tangu ipate uhuru, nami ninatimiza miaka kadhaa tangu nizaliwe, nikiwa mtoto wa tano wa familia ya watoto wanane ya marehemu baba yangu mpendwa Philemon Chahali na marehemu mama yangu mpendwa Adelina Mapango.

Lakini leo pia ni siku ambayo kampuni yangu ya huduma za ushauri wa kitaalamu (consulting services) inazaliwa rasmi, Kampuni hii ni matokeo ya uamuzi wangu wa kutafsiri ujuzi na uzoefu wangu wa muda mrefu katika maeneo kadhaa na kuufanya kuwa kazi rasmi. 

Jina la kampuni, yaani AdelPhil, ni kumbukumbu ya marehemu mama ADELina na marehemu baba PHILemon,. Imesajiliwa hapa Uingereza lakini itatoa huduma za kimataifa katika maeneo ya Intelijensia na Usalama, mikakati ya siasa (political strategies), na masoko kupitia mitandao ya kijamii (social media marketing). Lengo hasa la kampuni hii ni kuliunganisha eneo la Maziwa Makuu (Great Lakes region) yaani Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Zaire na Jamhuri ya KidemOkrasia ya Watu wa Kongo (DRC) na dunia kwa ujumla. Awali, msisitizo utakuwa kati ya Tanzania na Uingereza. 

Pamoja na sababu nyingine, kuanzishwa kwa kampuni hii ni katika kuunga mkono jitihada za serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi uliotukuka wa Rais Dkt John Magufuli, ambaye tangu aingie madarakani amekuwa akifanya jitihada kubwa kuipeleka Tanzania yetu mahali inapostahili. AdelPhil itawasaidia Watanzania - kwa maana ya taasisi za umma na binafsi na watu binafsi - kulifikia soko la huduma na bidhaa hapa Uingereza (kwa kuanzia) na wakati huohuo kuwezesha wateja wa hapa Uingereza kulifikia soko la hudma na bidhaa nchini Tanzania. Baadaye wigo utatanuliwa ili kufikisha huduma hizo kwa nchi zote za Maziwa Makubwa na dunia kwa ujumla (hususan Ulaya Magharibi).

Basi nitumie fursa hii kumshukuru Mungu kwa kunijaalia mwaka mwingine. Japo mwaka huu ninaomaliza ulikuwa mgumu kwangu kutokana na kumpoteza baba yangu mpendwa, Marehemu Philemon Chahali, miaka 7 baada ya kumpoteza mama yangu mpendwa, Marehemu Adelina Mapngo, na sasa kubaki yatima.

Hata hivyo, japo nusu ya pili ya mwaka huu ilianza kwa kifo cha baba, hatimaye nilipata nguvu na kushiriki kikamilifu katika kampeni za uchaguzi mkuu huko nyumbani ambapo hatimaye Rais Dkt Magufuli aliibuka mshindi. Ushiriki huo umechangia sana wazo la kuanzishwa kwa kampuni ya AdelPhil baada ya kupata ushauri kutoka kwa watu kadhaa.

Uchungu mkubwa katika siku hii ni kutokana na ukweli kwamba kila mwaka, siku yangu ya kuzaliwa iliambatana na Marehemu baba kuniimbia happy birthday, kwa simu niwapo mbali na nyumbani, lakini hii ni birthday ya kwanza ambapo nitakosa upendo huo mkubwa wa baba kwa mwanae. Lakini yote ni mipango ya Mungu, na ninaamini wazazi wangu wapendwa huko walipo wanapata faraja kuona mtoto wao naanzisha kampuni ambayo nime-dedicate jina lake kwao.

Kwa Watanzania wenzangu, wito wangu mkubwa kwenu ni kuendelea kuunga mkono jithada za Rais Dkt Magufuli kwa sababu tuna malima mrefu wa kupanda na anahitaji kila aina ya ushirikiano wetu. Mie ndo mchango wangu wa kwanza ni huo wa AdelPhil Consultancy, kampuni ambayo japo inafanya biashara lakini pia ni ya kuwatumikia Watanzania wenzangu na nchi yetu kwa ujumla. Katika siku zijazo nitaelezea kwa undani ni jinsi gani waweza kunufaika na huduma za kampuni hii.

Nimalizie kwa kusema HAPPY BIRTHDAY TANZANIA, HAPPY BIRTHDAY ME, na HAPPY BIRTHDAY ADELPHIL CONSULTANCY

4 Dec 2015


KWA wanaofuatilia safu hii, watakumbuka kuwa mara baada ya CCM kumpitisha Dk. John Magufuli kuwa mgombea wake wa kiti cha urais katika Uchaguzi Mkuu uliopita, niliandika makala iliyoonyesha kukata tamaa na kutotegemea lolote jipya. Licha ya kutojutia kuwa na mtizamo huo ambao ulitokana na mwenendo wa chama hicho tawala kwa miaka kadhaa sasa, pia wakati huo nilikuwa na matumaini makubwa kuwa vyama vya upinzani, hususan Chadema vingetupatia mbadala wa CCM.

Hata hivyo, baada ya Chadema na vyama vingine vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kumpokea Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa, na baadaye kumteua kuwa mgombea wao, sambamba na ‘kumpa kisogo’ mwanasiasa aliyeifanyia makubwa Chadema, Dk. Willbrord Slaa, ambaye pia alikuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, nilitafakari upya msimamo wangu.


Awali, nilielekeza nguvu zangu katika kupingana na uamuzi wa Chadema/Ukawa kumpokea Lowassa na kumfanya kuwa mgombea wao wa kiti cha urais. Lakini kwa vile kwa vyovyote vile, ilikuwa lazima Rais wa Tano wa Tanzania angetoka aidha CCM au Ukawa na tayari nilishatafsiri kuwa uamuzi wa Lowassa kupokelewa na Upinzani na kufanywa mgombea wao ni usaliti, hatimaye nililazimika kumwangalia mgombea wa CCM, Dk. Magufuli, kwa jicho la tatu.


Baada ya kusikiliza hotuba yake siku ya uzinduzi wa kampeni za CCM na hotuba zilizofuatia alipozunguka sehemu mbalimbali za nchi yetu kuomba kura, niliamua kumuunga mkono kwa asilimia 100. Japo uamuzi huo haukuwa mgumu kwa vile kadri siku zilivyoenda ilionyesha bayana kuwa Dk. Magufuli angekuwa kiongozi mwafaka kwa Tanzania yetu, hofu yangu kuu haikuwa endapo angeshindwa bali iwapo angeshinda na kuendeleza yale yale yaliyonifanya kuwa miongoni mwa wakosoaji wakubwa wa CCM. Kadhalika, uamuzi huo, ulisababisha kurushiwa maneno makali na tuhuma mbalimbali ikiwa ni pamoja na madai kuwa nimenunuliwa na CCM.


Urahisi wa kumuunga mkono Dk. Magufuli ulichangiwa zaidi na kiburi kilichowapata wafuasi wa Lowassa ambao kwa kiasi kikubwa walikataa katakata kuweka mantiki mbele ya hisia. Wimbo uliotawala kwao ulikuwa ni mabadiliko tu, na kila aliyejaribu kuhoji kuhusu mabadiliko hayo alirushiwa maneno makali, na wakati mwingine kutukanwa. Kwa hiyo ilifikia wakati wa kuamua liwalo na liwe. Waingereza wana msemo ‘the end justifies the means,’ yaani, kwa tafsiri isiyo rasmi, matokeo huhalalisha njia iliyotumika kuyafikia.


Kwa hiyo, nilijipa matumaini kuwa iwapo Dk. Magufuli angeshinda na kutimiza ahadi zake basi sio tu itamaliza kelele za waliotuona wasaliti dhidi ya mabadiliko yaliyoahidiwa na Lowassa bali pia itatimiza ndoto ya kila Mtanzania kuiona nchi yetu ikipata kiongozi wa kutufikisha mahala tunapostahili kuwepo.


Bahati nzuri, sio tu kuwa Dk. Magufuli alishinda bali muda mfupi tu tangu aingie madarakani ameweza kufanya mambo makubwa zaidi ya matarajio ya wengi kwake. Kwa hiyo, tuliomuunga mkono sio tu tuna furaha ya ushindi wake lakini pia tuna furaha kubwa zaidi ya kupata mtu wa watu, anayetambua matatizo yanayoikabili nchi yetu, mwenye uamuzi stahili, na anayetupa matumaini kwamba hatimaye nchi yetu itaweza kuangamiza janga la kitaifa la rushwa na ufisadi, hatua itakayosaidia kutuondoa kwenye umasikini mkubwa licha ya rasilimali lukuki tulizonazo, na hatimaye kuwa na Tanzania tunayoweza kujivunia.


Binafsi, nimejijengea utaratibu wa kuanza siku yangu kwa kuangalia kilichojiri huko nyumbani, kwa kupitia vyombo mbalimbali vya habari mtandaoni. Mara nyingi utaratibu huo wa kila siku uliishia tu kutibua siku yangu kwani kila kukicha ilikuwa ni mlolongo wa habari mbaya baada ya habari mbaya. Ilikuwa nadra kwa wiki kupita bila kukumbana na habari za ufisadi, ujangili, ahadi za porojo, na kadhalika.


Lakini hali sasa ni tofauti tangu Magufuli aingie madarakani. Yaani ni raha mtindo mmoja, kwani kila siku ni habari njema juu ya habari njema. Na si vigumu kuwa na matumaini makubwa ikizingatiwa kuwa hadi wakati ninaandika makala hii, Rais Magufuli amekuwa madarakani kwa takriban wiki tatu tu. Yayumkinika kubashiri kuwa siku 100 za kwanza za urais wake zitashuhudia Tanzania ikiwa nchi ya mfano wa kuigwa.


Na hilo limeshaanza kutokea. Tayari vyombo mbalimbali vya habari, hususan barani Afrika, vimekuwa vikiripoti kwa wingi kuhusu hatua mbalimbali anazochukua Rais Magufuli. Lakini kivutio zaidi ni jinsi baadhi ya wananchi katika nchi kama Kenya, Uganda, Malawi, Afrika Kusini, Nigeria na kwingineko walivyofikia hatua ya kutamani Magufuli awe Rais wao. Hii inatukumbusha zama za Baba wa Taifa ambaye alionekana machoni mwa Waafrika wengi kama mmoja wachache wa bara zima.


Taratibu, hisia kuwa kasi ya Magufuli ni nguvu ya soda zinaanza kufutika huku wananchi wengi wakiahidi kumpa ushirikiano katika jitihada zake za kuikomboa Tanzania yetu. Hata baadhi ya wafuasi wa vyama vya upinzani sasa wanamkubali baada ya kuridhishwa na uchapakazi wake.


Hata hivyo, kuna takriban makundi matatu ya wapinzani wa Dk. Magufuli. Kundi la kwanza ni la wapinzani wa asili, linalojumusiha wenzetu waliojitoa ufahamu na kuamini iwe isiwe lazima Lowassa angekuwa rais. Hawa hawashangazi na huenda baada ya muda ndoto ya urais wa Lowassa itawatoka na watakubaliana na hali halisi. Lakini kwa vile upinzani si uadui, na kimsingi upinzani wa kisiasa waweza kuwa chachu nzuri ya kumsaidia Rais wetu na chama chake kuibua uovu dhidi ya taifa letu, basi kundi hili si tatizo sana.


Kundi la pili ni la watu walioigeuza Tanzania yetu kuwa shamba la bibi, waliozoea kuvuna wasichopanda, watu ambao zama za Ujamaa tuliwaita kupe. Kundi hili lajumuisha mafisadi na wanufaika wa ufisadi, wahalifu (kwa mfano wauza dawa za kulevya, majangili). Hawa wanatambua kuwa arobaini za mwizi zimewadia. Kundi hili ni hatari kwani miongoni mwao kuna wenye tabia za kimafia. Hawa si wa kufumbiwa macho hata kidogo, na ni muhimu kwa taasisi za usalama kuwabaini na kuwadhibiti mapema. Si rahisi kwa kundi hili kumkubali Magufuli au kuunga mkono jitihada zake kwa sababu kimsingi jeuri yao mtaani inafikishwa kikomo.


Kundi la tatu ni la wenzetu waliozowea kupata wasichostahili. Kuna ugonjwa mmoja unaitwa Stockholm Syndrome, ambao kwa kifupi ni hali inayomfanya mtu anayenyanyaswa au kuteswa kuyakubali manyanyaso/mateso hayo na kuyaona kama stahili yake. Mara kadhaa tunashuhudia mwanandoa anayeteswa na mwenza wake akitokea kuwa mtetezi wake mkuu. Katika kundi hili kuna wenzetu wanaoamini kuwa mapambano dhidi ya rushwa au ufisadi hayawezi kufanikiwa kwa vile, kwa mtizamo wao, ni hatima (destiny) ya taifa letu. Uzuri ni kwamba kadri jitihada za Magufuli zitakavyozidi kuzaa matunda, taratibu watu wa aina hii wataanza kutambua kuwa imani yao ni fyongo.


Nimalizie makala kwa kukumbushia kuwa hakuna safari isiyo na kona au milima na mabonde. Jitihada za Magufuli kuikomboa Tanzania yetu hazitokuwa nyepesi lakini la muhimu ni imani kuwa zitafanikiwa. Hata hivyo, ili jitihada hizo zifanikiwe ni wajibu wetu sio tu kumuunga mkono au kumsifia tu bali nasi wenyewe tunapaswa kubadilika kwa kuchukia ufisadi, rushwa, uzembe na vitu vingine vinavyolikwaza taifa letu.


INAWEZEKANA, TIMIZA WAJIBU WAKO

- Se

28 Nov 2015


Makala hii imechapishwa katika jarida la Raia Mwema toleo la wiki hii lililotoka tarehe 25/11/2015, lakini kwa sababu nisizoelewa tovuti ya jarida hilo haijawa-updated kwa wiki kadhaa sasa. Kwa vile makala ninazotuma gazetini hufanyiwa uhariri kabla ya kuchapishwa, yawezekana makala iliyopo gazetini ikawa na tofauti kidogo na hii.

MAKALA YA RAIA MWEMA TOLEO LA NOVEMBA 25, 2015

Hotuba hii ya Rais Magufuli ni moja ya hotuba bora kabisa katika historia ya siasa za Tanzania.” Hili lilikuwa hitimisho langu katika mtandao wa kijamii wa Twitter mara baada ya Rais John Magufuli kumaliza kulihutubia Bunge wiki iliyopita, huko Dodoma.

Na kwa hakika watu kadhaa waliafikiana na hitimisho hilo.  Kilichovutia wengi waliosikia hotuba hiyo, katika shughuli ya ufunguzi wa Bunge la 11, sio tu mpangilio wa hotuba yenyewe bali pia jinsi kila alilotamka lilivyoonyesha bayana kuwa lilitoka moyoni mwake kwa dhati kabisa.

Rais alianza hotuba yake hiyo kwa kuorodhesha matatizo mbalimbali aliyobaini wakati wa kampeni zake Urais ambapo alizunguka takriban Tanzania nzima. Alitoa uchambuzi wa kina wa matatizo hayo kabla ya kuelezea kwa undani ni kwa jinsi gani serikali yake itayashughulikia. Ilikuwa ni zaidi ya hotuba ya kisiasa, na pengine ingeweza kabisa kuwa mhadhara wa kitaaluma uliofanyika katika lugha nyepesi na ya kueleweka.

Moja ya vitu vilivyonivutia sana katika hotuba hiyo ni jinsi Rais Magufuli alivyoweza kutupatia jibu la swali ambalo kwa miaka kadhaa lilionekana kuwatatiza viongozi wetu mbalimbali: “Kwanini Tanzania ni masikini licha ya utajiri lukuki wa raslimali ilionao.” Alieleza bayana na kwa kirefu jinsi ufisadi, rushwa na uhalifu vinavyochangia kukwamisha maendeleo ya taifa letu. Kadhalika, alifafanua, kwa kutumia takwimu halisi, jinsi mabilioni ya fedha yalivyotumika visivyo kwa matumizi yasiyo muhimu na yaliyo nje ya uwezo wa taifa letu masikini.

Kwa hakika ilikuwa hotuba ya kihistoria iliyofunika kabisa utovu wa nidhamu wa hali ya juu ulioonyeshwa awali na wabunge wa upinzani ambao walitumia muda mwingi kabla ya hotuba hiyo kuzomea na baadaye kuamiriwa  kutoka nje ya ukumbi huo.

Lakini kwa vile sio rahisi kumridhisha kila mtu, baadhi ya wenzetu waliosikiliza  hotuba hiyo walidai kuwa eti “haina tofauti na hotuba nyingine kadhaa zilizokuwa nzuri kuzisikiliza lakini zikaishia kuwa maneno matamu tu.” Wengine walikwenda mbali zaidi na kudai kuwa hata mtangulizi wa Rais Magufuli, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete naye pia alianza urais wake kwa hotuba za kutia moyo kama hizo lakini mengi ya aliyoahidi, hususan lile la ‘Maisha Bora kwa Kila Mtanzania,’ yaliishia kuwa ahadi tu.

Sikubaliani kabisa na wakosoaji hao, japo hoja zao zinaweza kuwa na mantiki kidogo. Ni kweli kwamba ukosefu wa hotuba za kuvutia si moja ya matatizo yanayoikabili nchi yetu. Wengi wa wanasiasa na viongozi wetu ni mahiri sana wa maneno lakini tatizo huwa katika kutafsiri maneno yao kuwa vitendo.
Wakosoaji hao hawapo sahihi kwa sababu, kama nilivyoeleza awali, hotuba hiyo ilikuwa ya kutoka moyoni.Ilikuwa hotuba ya kiongozi anayeguswa na yanayoisibu nchi yake, kiongozi mwenye uelewa wa changamoto zinazoukabili uongozi wake, na mwenye dhamira thabiti ya kukabiliana na changamoto hizo.

Kuna mbinu moja muhimu ya kubaini iwapo mtu anaongea ukweli au anahadaa, nayo ni kumwangalia usoni. Tangu kuanza kwa kampeni zake za urais na hadi wakati wa hotuba hiyo ya wiki iliyopita, uso wa Rais Magufuli wakati anaongea unaonyesha bayana kuwa kila neno linalotoka mdomoni mwake ni la dhati, linatoka moyoni na si sehemu ya porojo tulilozowea kutoka kwa wengi wa wanasiasa na viongozi wetu. Mtaalam yeyote wa kubaini ukweli na uongo hatoshindwa kuafikiana nami kuwa uthabiti wa kauli za Magufuli upo wazi kwa yeyete anayemwangalia usoni wakati anaongea.

Lakini pia, hotuba hiyo ilikuwa mwendelezo wa ishara nzuri zilizoanza kujitokeza siku moja tu tangu Rais Magufuli aingie ofisini, ambapo alifanya ziara ya kushtukiza Wizara ya Fedha, kabla ya kufanya ziara nyingine kama hiyo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Na siku ya uzinduzi wa Bunge, alitukumbusha enzi za (Waziri Mkuu wa zamani) hayati Edward Sokoine, aliyesifika kwa uchungu wa mali za umma, baada ya kuamuru zaidi ya shilingi milioni 200 zilizochangwa kwa ajili ya hafla ya mchapalo ya sherehe za uzinduzi wa Bunge jipya zielekezwe kwenye ununuzi wa vitanda katika hospitali ya Muhimbili, na kiasi kidogo tu kitumike kwa ajili ya hafla hiyo.

Kimahesabu, chini ya wiki tatu tangu aingie madarakani, Rais Magufuli ameshaokoa jumla ya shilingi milioni 900 kutokana na hatua alizochukua dhidi ya matumizi yasiyo ya lazima. Kwa kasi hii, tuna kila sababu ya kutarajiwa kuiona nchi yetu ikipaa kiuchumi, na hatimaye Watanzania kunufaika na neema lukuki ambayo nchi yetu imejaaliwa kuwa nayo.

Sina shaka kuhusu uwezekano wa mafanikio ya hatua za Rais Magufuli huko serikalini. Licha ya kuwa na Waziri Mkuu mchapakazi mzoefu, Majaliwa Kassim Majaliwa, kuna kila dalili kuwa baraza la mawaziri ambalo hadi wakati ninaandaa makala hii lilikuwa halijatangazwa, litasheheni wachapakazi kama yeye. Kwahiyo, kazi ya kurejesha nidhamu serikalini, kupunguza matumizi yasiyoendana na umasikini wetu na kupambana na ufisadi ina dalili kubwa za mafanikio.

Eneo ambalo Rais Magufuli hawezi kufanikiwa peke yake pasipo ushirikiano wa Watanzania wote ni nje ya serikalini na huko ‘mtaani.’ Mara kadhaa nimekuwa nikisisitiza umuhimu wa wananchi kujenga kasumba ya kudai haki na stahili zao badala ya kuona haki/stahili hizo ni kama fadhila au upendeleo flani. Wenzetu huku Ughaibuni wamejenga desturi ya kutokubali huduma au bidhaa inayotolewa chini ya kiwango wanachostahili. Haki na stahili za mpokea huduma ni miongoni mwa vitu vinavyopewa umuhimu mkubwa huku tulipo.

Haitokuwa rahisi kwa Rais Magufuli au wasaidizi wake kwenda kila sehemu kuwezesha au kuharakiasha upatikanaji wa huduma. Jukumu hilo linapaswa kusaidiwa na wananchi wenyewe ambao mara nyingi ndio wahanga wakubwa wa huduma mbovu. Kadhalika, watoa huduma nje ya serikali wanapaswa kutambua kuwa hizi ni zama mpya, na asiyeweza kuendana na kasi ya Rais Magufuli na ajiweke kando.

Lakini mchango mkubwa zaidi wa wananchi wote unahitajika zaidi katika kupambana na ufisadi, rushwa na uhalifu mwingine nje ya serikali. Wakati Rais ameahidi kukabiliana na ‘mapapa’ wa uhalifu kama kwenye biashara hatari ya madawa ya kulevya, pasipo wananchi kumsaidia kwa kuwatenga wahusika na kuwaripoti -  badala ya kuwasujudia na kuwapa majina ya heshima kama ‘wazungu wa unga’ au ‘mapedejee’ – basi tutamkwamisha, na nchi yetu itaendelea kuumizwa na vitendo hivyo viovu.

Kadhalika, ili kauli-mbiu ya ‘Hapa Ni Kazi Tu’ iweze kuleta matokeo kusudiwa na kuwa ya ufanisi ni muhimu kwa kila Mtanzania kuachana na dhana fyongo ya kusaka mafanikio kwa njia za mkato, turejee zama za Ujamaa na Kujitegemea ambapo waliokula bila kuvuja jasho tuliwaita ‘kupe.’ Sote tuchape kazi, tuache kufanya ‘ujanja ujanja,’ tuone fahari kuwa na shughuli halali badala ya kuamini kuwa ufisadi, rushwa, uhalifu,nk ndio njia rahisi na sahihi za kufikia mafanikio kwa haraka.

Baada ya kumpoteza Baba wa Taifa Marehemu Mwalimu Julius Nyerere aliyetujengea misingi imara ya taifa letu, japo sasa inamong’onyoka kwa kasi, na mzalendo wa daraja la kwanza, Marehemu Sokoine, sala/dua zetu katika wimbo wetu wa taifa katika maneno “Mungu Ibariki Tanzania…” zimesikika, na Mwenyezi Mungu ametuletea ‘Nyerere na Sokoine mpya’ kupitia kwa Rais wetu mpya Dkt Magufuli. Tusijiangushe wenyewe kwa kutotumia ipasavyo fursa hii adimu.

Nimalizie makala hii kwa wito ‘wa kitaalamu’ kwa ndugu zangu wa Idara ya Usalama wa Taifa, ambao pamoja na majukumu mengine, wana dhamana ya ulinzi wa Rais wetu na viongozi wengine wakuu kitaifa. Kama alivyosema mwenyewe, vita aliyoanzisha dhidi ya kila vitendo na kasumba zinazolikwaza taifa letu ni nzito na inawagusa watu wazito. Kwa vile yayumkinika kusema kuwa vitendo vya rushwa,ufisadi na uhalifu vimefikia hatua ya ‘kimafia,’ basi ni muhimu kuimarisha ulinzi wa Rais wetu (na viongozi wengine wanaopatiwa ulinzi) kwa sababu ‘tupo vitani.’

Simaanishi kuwa ulinzi uliopo una mapungufu lakini angalizo hili linazingatia ukweli kwamba ‘vita’ hiyo inagusa maslahi ya wengi, maslahi ya ‘kupe’ lukuki walioigeuza Tanzania yetu kuwa ni ‘shamba la bibi,’ la kuvuna wasichopanda, sambamba na wahalifu wanaoingiza, kuuza na kusafirisha madawa ya kulevya kana kwamba ni bidhaa iliyoidhinishwa na Shirika la Viwango la Taifa (TSB), majangili wanaoshindana kuua wanyamapori wetu na kusafirisha nyara za serikali, na wahalifu wengineo.

Rais Magufuli ameahidi kutotuangusha, basi nasi tusimwangushe.

Hapa Ni Kazi Tu!

Barua-pepe: [email protected] Tovuti: www.chahali.com Twitter: @chahali



28 Oct 2015





Bonyeza hapo juu kusikiliza mahojiano hayo kuhusu Uchaguzi Mkuu nchini Tanzania, na bonyeza link chini ya picha ifuatayo kusoma mahojiano kati yangu na BBC Swahili


BONYEZA HAPA kusoma mahojiano kamili


21 Oct 2015




OKTOBA 25 mwaka huu, Tanzania itafanya Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani. Mchuano mkali zaidi unatarajiwa kuwa katika nafasi ya urais, ambapo licha ya vyama vinane kusimamisha wagombea wao katika nafasi hiyo, ushindani mkali ni kati ya mgombea wa chama tawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, na yule wa umoja wa vyama vinne vya upinzani (Ukawa), Edward Lowassa.
Ushindani huo unatokana na unachangiwa zaidi na ukweli kwamba mgombea urais kwa tiketi ya Ukawa, Lowassa, awali alijaribu kuwania nafasi hiyo akiwa mwanachama wa CCM, lakini jina lake halikupitishwa, na hatimaye alijiunga na moja ya vyama vinavyounda Ukawa, Chadema, na kupitishwa kuwa mgombea urais kwa tiketi ya umoja huo unaojumuisha pia chama cha National League for Democracy (NLD), NCCR- Mageuzi na Chama cha Wananchi (CUF).
Yayumkinika kuhitimisha kuwa Rais wa Tano wa Tanzania, atakayemrithi Rais wa sasa, Jakaya Kikwete, atakuwa kati ya Dk. Magufuli au Lowassa, huku mgombea urais kwa tiketi ya chama kipya cha Alliance for Change and Transparency (ACT- Wazalendo), Anna Mghwira akitarajiwa kushika nafasi ya tatu.
Dalili kuwa uchaguzi huo ungekuwa na ushindani mkubwa zilianza kujitokeza katika mchakato wa CCM kumpata mgombea wake, ambapo licha ya baadhi ya wanasiasa wa chama hicho waliokuwa na nia ya kuwania urais kujitokeza kutangaza nia takriban mwaka mzima kabla ya kuanza rasmi kwa mchakato huo, jumla ya makada 43 walichukua fomu za kuwania kuteuliwa kuwa wagombea urais, huku 38 kati yao wakifanikiwa kurejesha fomu.
Kwa upande wa Lowassa, jina lake lilianza kusikika katika duru za siasa za Tanzania kuhusu mrithi wa Rais Kikwete, mara baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010. Ikumbukwe pia kuwa Lowassa alikuwa na mchango mkubwa katika kampeni za urais mwaka 2005, ambapo hatimaye Rais Kikwete alishinda. Kadri Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu ulivyozidi kujongea, ndivyo jina la Lowassa lilivyozidi kuvuma. Kimsingi, mchakato wa CCM kupata mgombea wake uligubikwa zaidi na shauku ya Watanzania iwapo Lowassa angepitishwa au la.
Hata hivyo, hatimaye jina la Lowassa halikupitishwa, na badala yake akapitishwa Magufuli, hatua ambayo pia ilihitimisha tetesi za muda mrefu kuwa urafiki kati ya Lowassa na Rais Kikwete ulikuwa umefikia kikomo, hasa ikizingatiwa kuwa hoja iliyokuwa na nguvu katika harakati za Lowassa kuwania urais kupitia CCM ni hisia kuwa huenda Kikwete angemsaidia Lowassa kuwa mrithi wake.

Kwa upande wa Ukawa, umoja wa vyama vinne vya upinzani ulioundwa katika Bunge Maalumu la Katiba mwaka jana kwa lengo la kushinikiza matakwa ya wananchi yaheshimiwe katika mchakato wa kupata Katiba mpya, mchakato wa kumpata mgombea wao wa urais ulitawaliwa na ukimya kwa muda mrefu, kabla ya Lowassa kujiunga na Chadema na hatimaye kupitishwa kuwa mgombea urais kwa tiketi ya umoja huo. Ujio wa Lowassa uliamsha hamasa kubwa miongoni mwa wafuasi wa vyama vinavyounda umoja huo, sambamba na kuleta ushindani mkubwa dhidi ya CCM.
Hata hivyo, uamuzi wa Chadema kumpokea Lowassa, mwanasiasa ambaye chama hicho kilimwandama na tuhuma za ufisadi kwa muda mrefu, ulipokelewa kwa hisia tofauti na Watanzania wengi, huku baadhi wakiuona umaarufu wake kama mtaji muhimu kuwezesha kuishinda CCM, huku wengine wakidhani kitendo hicho ni cha usaliti, hususan kwa Chadema ambayo ajenda yake kuu ilikuwa kupambana na ufisadi.
Licha ya uamuzi wa Lowassa kujiunga na umoja huo wa wapinzani, ukweli kwamba kwa mara ya kwanza, vyama vya upinzani nchini humo vimeweza kushirikiana kwa kusimamisha wagombea mbalimbali katika nafasi ya urais, ubunge na udiwani, imeufanya uchaguzi huo kuwa wa kwanza katika historia ya Tanzania ambapo nafasi ya ushindi kati ya chama tawala na upinzani zinakaribiana.
Takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa idadi kubwa ya Watanzania sio wanachama wa chama chochote cha siasa. Na kundi hili licha ya kutarajiwa kuwa muhimu katika kuwezesha ushindi katika uchaguzi huo, pia linajumuisha wapiga kura wanaokabiliwa na uamuzi mgumu kujiunga mkono CCM na mgombea wake licha ya chama hicho kutuhumiwa kuwa kumechangia matatizo mengi yanayoikabili nchi hiyo, au kujiunga mkono Ukawa ambayo mgombea wake wa urais, Lowassa, licha ya kuhubiri kuhusu mabadiliko, anaonekana kama hana tofauti na chama hicho tawala, hasa ikizingatiwa alikuwa huko kwa muda mrefu.
Kwa tathmini hadi wiki hii ya mwisho kabla ya uchaguzi huo, chama tawala CCM 

kinatarajiwa kufanya vizuri zaidi ya vyama vya upinzani katika nafasi zote, yaani urais, ubunge na udiwani. Kwa upande wa urais, nguvu za CCM zimekuwa katika maeneo kadhaa ikiwa ni pamoja na kujenga picha kuwa mpinzani wao mkuu, Lowassa, hafai ndio maana jina lake lilikatwa katika mchakato wa chama hicho kupata mgombea wake.
Kujenga picha kuwa Lowassa, pamoja na viongozi wachache wa CCM walimfuata huko upinzani ni wenye uchu wa madaraka, wanaotumia malalamiko ya wananchi dhidi ya CCM kwa manufaa yao kisiasa.
Tuhuma za ufisadi dhidi ya Lowassa ambazo kimsingi zilitangazwa zaidi na vyama vya upinzani hususan Chadema. Katika hoja hiyo, CCM pia imejaribu kuionyesha Chadema na Ukawa kwa ujumla kama wanasiasa wasio na msimamo na walioikimbia ajenda yao ya kupinga ufisadi ili ‘kumsitiri’ Lowassa.
Kutofanikiwa kwa Lowassa na Ukawa kuelezea kwa undani kuhusu ajenda yao ya mabadiliko. CCM na mgombea wake Magufuli wamekuwa wakitumia muda mwingi kubainisha sera zao na jinsi watakavyotekeleza.
Takriban asilimia 85 ya Watanzania wanaishi maeneo ya vijijini ambayo kiasili ni ngome kubwa ya CCM kwenye chaguzi. Kwa upande mwingine, Ukawa hawajafanikiwa kujipenyeza vya kutosha katika maeneo hayo, ambapo pia kuna uelewa mdogo kuhusu muundo wa umoja huo.
Kwa mujibu wa takwimu za Tume ya Taifa ya Uchaguzi, idadi ya wanawake –kundi ambalo kiasili ni ngome muhimu ya CCM – ni kubwa zaidi ya wanaume, na hii inatarajiwa kukinufaisha chama hicho tawala na mgombea wake Magufuli.
Magufuli, amekuwa waziri kwenye awamu mbili za urais Tanzania, Awamu ya Tatu ya Rais Benjamin Mkapa, na hii ya Nne ya Rais Jakaya Kikwete, na anasifika kwa uchapakazi. Kwa upande mwingine, ugombea wa Lowassa umeendelea kugubikwa na kashfa ya Richmond iliyosababisha ajiuzulu Uwaziri Mkuu mwaka 2008.
Kadhalika, licha ya kuwa na mtandao mkubwa nchi nzima, kuanzia ngazi ya mtaa hadi taifa, CCM inanufaika na hoja inayojiri kwenye kila uchaguzi mkuu, kuwa kuwapa ushindi Wapinzani ni sawa na kuwapa fursa ya kufanya majaribio ya uongozi ilhali CCM ina uzoefu wa kutosha.
Mapema wiki hii ziliibuka tena taarifa kuwa mmoja wa viongozi wakuu wa Chadema alihamisha mabilioni ya shilingi kwenda nje ya nchi, fedha zinazodaiwa zilipatikana baada ya kiongozi huyo ‘kukiuza chama hicho’ kwa Lowassa.
Hata hivyo, changamoto kubwa kwa CCM ni kinachotafsiriwa kama hasira za Watanzania wengi kutokana na matatizo mbalimbali yanayoikabili nchi hiyo, ambayo CCM inabebeshwa lawama, kubwa zaidi likiwa ufisadi unaotajwa kama chanzo kikuu cha umasikini.
Wachambuzi mbalimbali wa siasa za Tanzania wanatafsiri kuwa ufuasi mkubwa kwa Lowassa na Ukawa unachangiwa zaidi na manung’uniko ya wananchi wengi dhidi ya CCM, kiasi cha kuwa radhi kumwamini mwanasiasa ambaye kwa muda mrefu ameandamwa na tuhuma za ufisadi. Kauli kama ‘bora kulipigia kura jiwe kuliko CCM’ sio tu imekuwa ikisikika mra kwa mara miongoni mwa wafuasi wa upinzani bali pia inaashiria manung’uniko hayo.
Kadhalika, kwa vyama vinne vya upinzani kuweza kushirikiana na kumsimamisha mgombea mmoja wa urais, na kuongezewa nguvu na ujio wa Lowassa pamoja na makada kadhaa waliohama CCM, kwa mara ya kwanza Wapinzani wanaona kuna uwezekano wa kukishinda chama hicho tawala. Mikutano yao ya kampeni imeshuhudia umati mkubwa japokuwa lawama kwa Lowassa imekuwa ni kuhutubia kwa muda mfupi mno.
Wakati Magufuli na CCM wanaonekana kujiamini na kuwa na uhakika wa ushindi, kwa upande wa Lowassa na Ukawa, licha ya kuwa na matumaini makubwa ya kushinda, wanaonekana kuwa na hofu ya kuhujumiwa na chama hicho tawala.
Kwenye nafasi za ubunge na udiwani, CCM inatarajiwa kusinda viti vingi zaidi kwa sababu licha ya kuwa na mtandao mzuri majimboni, Ukawa inaonekana kuwekeza nguvu zaidi katika kumnadi Lowassa kuliko katika kampeni zake majimboni. Kadhalika, takwimu zinaonyesha kuwa mgombea wa CCM, Magufuli, ametembelea maeneo mengi zaidi ya mgombea wa Ukawa, Lowassa.
Kwa upande wa vyama vingine vinavyoshiriki uchaguzi huo, inatarajiwa kuwa ACT-Wazalendo kitashika nafasi ya tatu nyuma ya CCM na Ukawa, na kinatarajiwa kuimarika zaidi baada ya uchaguzi huo hasa kwa vile inahisiwa kwamba iwapo Ukawa itashindwa, wafuasi wake wengi wanaweza kuiona ACT-Wazalendo kama mpinzani wa kweli dhidi ya CCM.
Kwa hitimisho, changamoto kubwa kwa chaguzi nyingi barani Afrika huwa kwa chama cha kikuu cha upinzani kukubali matokeo pindi kikishindwa. Kwa mara ya kwanza, Tanzania inafanya uchaguzi wake mkuu huku kambi ya upinzani ikiwa na imani kubwa kuwa itaibuka na ushindi.
Kadhalika, kadri uchaguzi unavyozidi kukaribia ndivyo Wapinzani (hasa Ukawa) wanavyozidi kuonyesha kutokuwa na imani na mfumo mzima wa uchaguzi. Bila kujali upande gani utakaoibuka na ushindi, mustakabali wa Tanzania unategemea busara za viongozi na wafuasi wa kila chama kuhamasisha amani badala ya vurugu. Ushindi mkubwa katika uchaguzi huo ni kwa Watanzania kuendelea kubaki na umoja na amani.
Pia, mshindi katika uchaguzi huo atakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazoikabili Tanzania, kubwa zaidi ikiwa kuleta uwiano kati ya utajiri wa raslimali lukuki katika nchi hiyo na hali ya maisha ya wananchi, kupunguza pengo kati ya matajiri na masikini, na kuwaunganisha Watanzania kuwa kitu kimoja baada ya uchaguzi huu ambao kwa kiasi kikubwa umejenga mpasuko kijamii na kisiasa.
Mwisho, kwa vile hii ni makala yangu ya mwisho kabla ya uchaguzi huo hapo Jumapili, na kwa vile safu hii imekuwa ikifuatilia maendeleo ya uchaguzi huo tangu mwanzo, basi si vibaya kufanya ubashiri wa matokeo katika nafasi ya urais. Na ubashiri kuwa Magufuli atashinda urais, na CCM itashinda viti vya jumla katika nafasi za ubunge na udiwani, huku Ukawa, hususan Chadema, ikipata viti pungufu zaidi ya ilivyokuwa katika uchaguzi mkuu uliopita.
Hata hivyo, mshindi halisi katika uchaguzi huo ni Tanzania na Watanzania wenyewe. Kuna maisha baada ya uchaguzi, kwa hiyo ni muhimu kwa upande utakaoshindwa kutanguliza mbele maslahi ya taifa, badala kufanya vurugu.
MUNGU UBARIKI UCHAGUZI MKUU. MUNGU IBARIKI TANZANIA.



Sababu Tisa kwanini CCM itashinda katika Uchaguzi Mkuu Jumapili hii, Oktoba 25

Na January Makamba

Tarehe 25 mwezi huu Oktoba, Watanzania watapiga kura kumchagua rais wao wa tano, wabunge na madiwani. Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu umekuwa na msisimko mkubwa zaidi tangu kuanzishwa kwa mfumo wa siasa za vyama vingi mwaka 1995. Mengi yamendikwa kuhusu uchaguzi huu, hususan kutokana na hisia kwamba safari hii Upinzani una nafasi ya kukiondoa madarakani moja ya vyama vikubwa na vyenye muundo bora barani Afrika, chama tawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM). Matukio mbalimbali kuelekea uchaguzi huo yameleta shauku inayoweza kutengeneza hadithi ya kusisimua.

Nikiwa sehemu ya Timu ya Kampeni ya CCM,na kwa manufaa ya wote ambao wangependa kuwa na mtizamo tofauti, ninatoa sababu 9 kwanini tunaamini kuwa CCM itaibuka mshindi na kwanini Dkt John Pombe Magufuli atakuwa Rais ajaye wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

1.    Ugombea ‘fyongo’ (flawed) wa Edward Lowassa

Ilishabainika kuwa uchaguzi huu ungekuwa mgumu kwa CCM bila kujali nani angekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Upinzani. Lakini matokeo ya uchaguzi huu yalielemea upande wa CCM pale Upinzani ulipomchagua Lowassa kuwa mgombea wao. Ni rahisi kwa CCM kuchuana na Lowassa kuliko laiti mgombea wa Upinzani angekuwa Dkt Wilbrod Slaa, ambaye ndiye aliandaliwa kuwa mgombea kabla ya ‘ukusukumwa kando’ na nafasi hiyo kupewa Lowassa. Slaa alikuwa na uadilifu katika maeneo mengi, na aliaminika. Kwa Lowassa, ni vigumu na inanyima raha kuchuana na mfumo aliyoshiriki kujenga na ambao ulikuwa sehemu ya maisha yake hadi Agosti mwaka huu alipohamia Upinzani. CCM ilikuwa na nafasi ya kumpitisha Lowassa kuwa mgombea wake wa nafasi ya urais. Hatukufanya hivyo kwa sababu rahisi tu kwamba ingekuwa vigumu mno kumkabidhi kwa wananchi mgombea wa matarajio ya baadaye ambaye ni kiashirio cha yale yasiyowaridhisha wananchi kuhusu CCM. Kuna wanaoamini kuwa uchaguzi huu ni mgumu kwa vile Lowassa ndiye mgombea wa Upinzani. Sisi twaamini kwamba uchaguzi huu ungekuwa mgumu mara kumi zaidi laiti Lowassa angekuwa ndiye mgombea wetu.

2.    Upinzani umesalimisha ajenda yake ya kupinga ufisadi

Kipindi cha miaka 10 iliyopita kimetawaliwa na matukio mbalimbali ya kuwabainisha mafisadi na kuwachukulia hatua. Vyombo vya habari, taasisi za kiraia na Bunge vimefanya kazi nzuri kushughulikia suala hilo. Rais Jakaya Kikwete ameweka historia kwa kuamuru ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kupatikana kwa wananchi na kujadiliwa kwa uwazi Bungeni. Waziri Mkuu aliyekuwa madarakani, si mwingine bali Lowassa, alijiuzulu kwa sababu ya kashfa ya rushwa. Mawaziri kadhaa walitimuliwa kazi na manaibu waziri wawili wanatumikia vifungo jela. Huu ni uwajibikaji wa hali ya juu japokuwa kuna wanaoweza kudhani ni hatua ndogo. Umma umeamka.

Upinzani ulijenga hadhi yake kwa kuongelewa sana kuhusu ufisadi. Kilele cha Upinzani kilijiri mwaka 2007 katika mikutano mkubwa wa hadhara ambapo walitangaza majina 10 ya watu waliowaita mafisadi wakubwa zaidi, katika kilichokuja kufahamika kama Orodha ya Aibu (List of Shame). Lowassa alikuwa kinara kwenye orodha hiyo.

Ilitarajiwa kuwa Uchaguzi Mkuu huu uwe ‘hukumu’ kwa CCM kuhusu ufisadi. Upinzani ulitarajiwa kuitumia ajenda ya ufisadi ambayo inawagusa watu wengi. Lakini ghafla, kwa kumteua mwanasiasa, ambaye kwa jitihada zao wenyewe Wapinzani,  amefahamika zaidi kwa ufisadi, iliwalazimu kuzika ajenda hiyo. Kilichofuata baada ya hapo ni kituko na kichekesho. Wale mashujaa wa mapambano dhidin ya ufisadi walijikuta wakilazimika ‘kulamba matapishi yao.’ Wengi wao waliokuwa mahiri katika mitandao ya kijamii walilazimika kufuta historia ya baadhi ya waliyoyaandika mtandaoni walipokuwa wakikemea ufisadi, lakini si kabla ya maandiko yao kunaswa kwa ‘screenshots.’ Ulikuwa ni ukweli wa kushangaza. Ni Dkt Slaa na Professa Ibrahmi Lipumba, viongozi muhimu wa Upinzani tangu miaka ya Tisini, walioamua kujiuzulu nyadhifa zao kwa kukerwa na uamuzi wa Upinzani kumpokea Lowassa.Matokeo yake, Upinzani walijikuta wakichana kadi yao turufu- ajenda dhidi ya ufisadi. Ni nadra kwao kuongelewa suala hilo, na wanapojaribu kufanya hivyo, ni kwa kujitetea tu.

Jioni moja mwezi Agosti, nilimwona Mbunge wa Upinzani, Peter Msigwa, katika mdahalo kwenye runinga. Aliongelea kitu ambacho kilijumuisha mtizamo wa Upinzani kwa muda huo, na kiliniacha hoi. Alisema, kabla hawajampokea Lowassa, walifanya utafiti wao, na “ufisadi sio ajenda muhimu kwa taifa letu.” Alidai kwamba wenye ushahidi kuhusu ufisadi wa Lowassa wajitokeze hadharani.Alionekana kusahau kuwa walipomtaja Lowassa katika List of Shame, walitangaza hadharani kuwa wana ushahidi. Muda si mrefu uliopita, CCM ilikuwa ikiwaomba Wapinzani kuleta ushahidi kila yalipojitokeza madai ya ufisadi dhidi ya viongozi wa chama na serikali allegations were leveled against the party and its leaders. Haikupendeza kuingiza hoja za kisheria katika masuala ya kimaadili. Upinzani sasa umeamua kwa hiari yao kuchukua ‘chembemoyo’ wakati ambapo viongozi wa CCM wanaongelea ufisadi kwa ujasiri na msisitizo.

Uchaguzi huu Mkuu ni muhimu sana kwa Upinzani. Kimsingi, unaweza kuwa na madhara makubwa. Endapo watashindwa hapo Jumapili, ‘watapotea’ kwa muongo mzima ujao. Ndio maana inashangaza kuona wamechukua uamuzi wa kukimbia ajenda yao kuu ya kupambana na ufisadi  ambayo iliwatambulisha na kuwaimarisha. Na kuwapa nguvu kukubalika kwa wapigakura. Kuona wanatarajia kushinda ni miujiza mkubwa.

3.    Mabadiliko ambayo kamwe huwezi kuyaamini

Ukizinguka jijini Dar es Salaam utakutana na mabango ya Upinzani yanayodaia “Ni Muda wa Mabadiliko.” Lakini ukisikiliza mikutano yao ya kampeni, ni porojo na hasira tu. Wasemaji wakuu katika mikutano hiyo ni Waziri Mkuu wa zamani na kada wa muda mrefu wa CCM, Frederick Sumaye na Lowassa mwenyewe. Kwa pamoja, wamekuwa wana-CCM na katika nyadhifa  za juu serikalini kwa zaidi ya miaka 50. Kwa hiyo inasikitisha kusikiliza kauli zao – zinazokosa imani na kupalizwa na aibu – wakipambana na mfumo walioshiriki kujenga, uliojenga tabia zao za kisiasa, na ambao walikuwa wakiusifu miezi mwili tu iliyopita.
Kutokuwa wakweli na kuweka mbele maslahi binafsi kwawatuma kudai kuwa CCM haijafanya chochote katika miaka miaka 50 iliyopita. Inapotokea viongozi wawili waandamizi wa chama na serikali  kwa zaidi ya miaka 30, wote wakiwa walioshika Uwaziri Mkuu, kudai kuwa hakuna chochote kilichofanyika katika miaka 50 iliyopita, wajihukumu wenyewe. Si kwa muundo, mwonekano au ukweli, wanasiasa hao wanasimamia mabadiliko. Yayumkinika kuhitimisha kuwa mabadiliko wanayoongelea ni kuhusu kubadili chombo kilichowaingiza madarakani, mabadiliko ya sare tu za chama. Hawana habari na mabadiliko ya maisha ya wananchi wa kawaida. Wapigakura wameanza kushtukia ukweli huo.

4.    Migogoro na mkanganyiko ndani ya UKAWA

Huko nyuma, kila ulipojiri uchaguzi, Upinzani ulijaribu kuunganisha nguvu ili kuing’oa CCM madarakani.Na kila mara jitihada za ushirikiano zilishindikana. Mwaka 2014, mjadala kuhusu Katiba Mpya kuataka serikali tatu uliwapatia ajenda ya kuwaunganisha pamoja. Kisha wakaamua kutafsiri ushirikiano huo kuwa wa kisiasa, wakaafikiana kusimamisha mgombea mmoja katika nafasi ya urais na kugawana majimbo.

Baada ya hapo kukajitokeza unafiki wa wazi. Kuonyesha kuwa matamanio yaliwekwa mbele ya kanuni zilizopatikana kwa jitihada ngumu, chama ambacho jina lake linajumuisha maneno ‘demokrasia’ na ‘maendeleo’ kilitemea mate mchakato wake chenyewe wa kidemokrasia na mshikamano kupata mgombea wake wa urais, na kukurupuka kumpitisha kada wa muda mrefu wa CCM ambaye jitihada zake kuwania urais kwa tiketi ya chama hicho tawala ziligonhga mwamba.

Waliamini kwamba uamuzi wa Lowassa kuhama CCM ungekiathiri chama hicho tawala, wakitarajia vigogo kadhaa wangemfuata huo Upinzani. Badala yake, ujio wake huko ukapelekea kuondoka kwa wanasiasa wawili waliokuwa nguzo muhimu kwa Upinzani, Dkt Slaa na Prof Lipumba.Kadhalika, wanachama wengine muhimu waliohama na kujiunga na chama cha ACT- Wazalendo, ambacho hakikujiunga na UKAWA.
Kana kwamba hiyo haitoshi, makubaliano ya UKAWA kusimamisha mgombea mmoja  kila jimbo yalikumbwa na mushkeli katika majimbo kadhaa na kupelekea malalamiko yaliyosababisha ugumu katika kampeni za Lowassa.

Huko Masasi, mgombea mwenza wa Lowassa, Juma Duni, alilazimika kuokolewa jukwaani baada ya waliohudhuria mikutano wake wa kampeni kupiga kelele kuwa wataipigia kura CCM. Katika jimbo la Nzega, Lowassa alilazimika kuendesha ‘kura ya sauti’ kuwauliza waliohudhuria mikutano wake wa kampeni wanamhitaji mgombea gani kati ya wawili wa UKAWA waliokuwa wanachuana. Mpango mzima wa ushirikiano miongoni mwa vyama vinavyounda UKAWA umekwenda mrama.CCM sasa ipo katika nafasi nzuri ya kujinyakulia majimbo ambayo vinginevyo yangekwenda kwa wagombea wa Upinzani.

Lakini kilele cha unafiki wa UKAWA ni hiki. Umoja huo uliundwa ili kutetea Katiba Pendekezwa iliyoshauri muundo wa Muungano wa serikali tatu. Kanuni hiyo ya msingi iliwekwa kando pale UKAWA walipomchagua mgombea wao wa tiketi ya urais, Lowassa, ambaye alikuwa mtetezi mkubwa wa muundo wa Muungano wa serikali mbili. Kwa wengi wasioendeshwa na propaganda, uamuzi wa kutelekeza suala la msingi lililopelekea umoja wa vyama hivyo, kwa ajili tu ya imani ya kufikirika ya kushinda urais, yaashiria uchu wa madaraka na sio mabadiliko yanayohubiriwa kwa wananchi.


5.    Lowassa kushindwa kufanya kampeni nchi nzima

Lowassa anaonekana kutokuwa na uwezo wa kusafiri kwa urefu na upana wa Tanzania kufanya kampeni. Mara nyingi amekuwa akitumia usafiri wa anga kwenda mikoani ambako hufanya mikutano mikubwa kwenye makao makuu ya mikoa, kutembelea majimbo mawili au matatu ya jirani kwa helikopta, na kurejea jijini Dar es Salaam. Huko Tanga, kwa mfano, alifanya kampeni katika majimbo matatu tu kati ya tisa mkoani humo. Mkoani Ruvuma, alifanya kampeni katika majimbo matatu kati ya tisa, Kigoma majimbo mawili kati ya manane, na Kagera majimbo matatu tu.

Kinyume chake, mgombea wa CCM, Magufuli amekuwa barabarani tangu Agosti 23, huku akipumzika kwa siku tatu. Anatumia usafiri wa gari, akitembelea kijiji baada ya kijiji, na kufanya mikutano kati ya minane hadi 12 kwa siku. Aina hii ya kufanya kampeni ‘kwa rejareja’ inabaki kuwa nguzo pekee ya kujihakikishia ushindi kwenye uchaguzi mkuu nchini Tanzania, hususan katika maeneo ya vijijini ambayo usikivu na kuonekana kwa vyombo vya habari ni mdogo. Wakati Lowassa anavutia wahudhuriaji wengi katika mikutano yake katika miji mikubwa, Magufuli anajipatia wahudhuriaji wengi katika kila kona ya Tanzania. Kama idadi ya wahudhuriaji katika mikutano hiyo ya kampeni inamaanisha wingi wa kura, basi kwa hakika CCM itashinda. Lakini tofauti na Upinzani, CCM haidanganyiki na wingi huo wa wahudhuriaji katika mikutano ya kampeni. Rekodi ya mahudhurio makubwa ilikuwa ikishikiliwa na Agustino Lyatonga Mrema, mgombea maarufu wa kiti cha urais kwa tiketi ya Upinzani mwaka 1995 (ambaye pia alijiunga na Upinzani akitokea CCM). Hata hivyo alishindwa kwenye uchaguzi huo. Sie twategemea kitu kingine.

6.    Mfumo imara wa CCM katika uhamasishaji kuanzia ngazi ya chini kabisa.

Katika Tanzania, vyama vichache mno vinavyoweza kuchuana na uwezo wa CCM kuhamasisha wananchi. Wakati Wapinzani huhadaiwa na ‘mahaba’ wakati wa kampeni za uchaguzi, mahudhurio makubwa kwenye mikutano yao ya kampeni na vichwa vya habari magazetini, CCM hutumika nguvu yake ya kimuundo na kuwasha ‘mashine zake za kisiasa,’ kuanzia ngazi ya mtaa (ujumbe wa nyumba kumi) kwa nchi nzima. Kimuundo, jumiya ya wanawake wa CCM (UWT) pekee ni kubwa kuliko Chadema, chama kikuu cha upinzani. CCM Haihitaji kusafiri ili kufanya kampeni. CCM ipo kila mahala, ikifanya kampeni katika makundi madogo, vijijini na mitaani, kila siku na mbali ya upeo wa vyombo vya habari. Kwa wanaofahamu muundo wa chama hicho, ushindi kwake si jambo la kushangaza.

Kwenye miaka ya 1950s, wakati wa harakati za kusaka uhuru kutoka kwa mkoloni, uwezo wa TANU kuhamasisha ulikuwa nguzo muhimu kwa Tanganyika kupata uhuru wake.CCM imerithi vinasaba vya TANU. Mwalimu Nyerere aliijenga CCM kuwa imara kwa nyakati kama hizi. Mwaka jana, huku umaarufu wake ukiwa umepungua, CCM ilimudu kushinda uchaguzi wa serikali za mitaa kwa asilimia 80 dhidi ya umoja Huohuo wa Upinzani inaokabilina nao katika uchaguzi huu Mkuu.Tofauti haipo kwenye nini kinachoonekana kwenye vyombo vya habari au mitandao ya kijamii bali jinsi gani makada wa chama hicho tawala walivyofanya uhamasishaji katika kila mtaa na kijiji. Uchaguzi huo wa serikali za mitaa, ambao hufanyika mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu, hutoa dalili nzuri kuhusu matokeo ya uchaguzi mkuu.

7.    Umahiri wa Dkt Magufuli

Mwaka jana, baadhi ya waandishi wa habari walikiri kwamba ni vigumu mno kumshambulia na kumshinda Dkt Magufuli. Ana rekodi imara ya usafi, uchapakazi na anayetaka kuona matokeo sahihi. Hajawahi kuvutiwa na harakati za kisiasa, na ilikuwa mshangao alipotangaza kuwania urais. Na alipotangaza, hakufanya mbwembwe wala kijitangaza kwenye vyombo vya habari. Alizingatia kanuni za chama kwa ukamilifu. Dkt Magufuli analeta kumbukumbu za mgombea mwingine aliyekuwa hajulikani mwaka 1995 -  Benjamin Mkapa. Wakati umaarufu wa CCM ukiwa chini, huku ikikabiliwa na upinzani kutoka kwa Naibu Waziri Mkuu aliyehama kutoka chama hicho tawala, CCM ilimchagua turufu yake ambayo ilikuwa ngumu kuikabili.Miaka 20 baadaye, ikikabiliwa na upinzani wa Waziri Mkuu maarufu wa zamani aliyehama chama hicho na kujiunga na Upinzani, CCM imefanya tena ‘vitu vyake.’ Siku zote, CCM hujua ‘kufanya pigo la haja.’

8.    Ufanisi wa CCM katika maeneo ya vijijini

Mimi ni Mbunge wa jimbo lisilo mjini, lenye idadi ya wastani ya wapigakura. Mwaka 2010, katika uchaguzi ulionekana kuwa mgumu, CCM ilishinda jimbo langu kwa asilimia 80., na kitaifa kwa asilimia 61. Hivi sasa, tunatarajia ushindi wa CCM kuwa wa asilimia 90 hivi. Tanzania ina  majimbo kadhaa yaliyo kama jimbo langu. Upinzani hupenda kuwapuuza wananchi katika majimbo yasiyo ya mijini, kama jimbo langu, kwa kudai kuwa wanaichagua CCM kutokana na ujinga wao. Wasingeweza kukosea zaidi ya hivyo.

Popote walipo, watu hupiga kura kulingana na mahitaji yao. Mwaka 2000, vijiji vinne tu katika jimbo langu ndivyo vilikuwa na umeme. Leo, vijiji 44 vina umeme. Japo hatujaweza kutoa huduma zote kwa kiwango cha kumfurahisha kila mtu, lakini hali halisi yaonyesha wingi wa wanafunzi mashuleni, walimu zaidi, madaktari na manesi zaidi, zahanati nyingi zaidi zimejengwa, huduma za mawasiliano ya simu zinapatikana kwa wingi, barabara nyingi za lami, nk. Porojo kuwa hakuna kilichofanyika Kwahiyo wapigakura wasiichague CCM haieleweki katika maoneo hayo ambay kimsingi ndiyo yenye wapigakura wengi. Na wagombea wa CCM wanaposema watafanya zaidi ya waliyokwishafanya, kwa kuzingatia mafanikio yaliyokwishapatikana, wananchi wanawaamini. Hotuba za kampeni ni mwonekano na mantiki.

Chaguzi sio kuhusu ahadi tu bali jinsi gani ahadi hizo zitaandaliwa na kutekelezwa. Jukwaa ambalo kila chama kitanadi ajenda zake za uchaguzi hujengwa wakati wa uzinduzi wa kampeni za chama husika. Yahitaji mtu kuangalia tu uzinduzi wa kampeni za za Lowassa na Magufuli. Lowassa aliongea kwa dakika 9 tu  - akiahidi, pamoja na mambo mengine, kuwaachia huru wabakaji (sio kama ninazusha hili) wanaotumikia vifungo vyao na watuhumiwa ugaidi wanaosubiri kesi zao. Bila kujali alikuwa na malengo gani wakati anatoa ahadi hizo, makosa hayo hayastahili msamaha wa rais.  Kwa upande wake, Magufuli aliongea kwa dakika 58, akielezea kwa undani ajenda za maendeleo katika nyanja za elimu, ajira, afya, ufisadi, huduma za maji, na miundombinu. Kuanzia hapo, kwa muda wote wa kampeni, mwenendo umekuwa hivyo, kwa uzito wa ujumbe kwenye hotuba zake na muda wa kuhutubia

Wanaohudhuria mikutano ya Dkt Magufuli huondoka katika mikutano hiyo wakiwa na matumaini na wenye nguvu. Kwa upande mwingine, wahudhuriaji katika mikutano ya Lowassa huondoka wakiwa wamekanganywa. Siku ya kupiga kura, wapigakura wanamkumbuka jinsi mgombea alivyoonekana na alivyoongea, na jinsi walivyojisikia walipomwona jukwaani. Kwa kigezo hiki, ni bora ningekuwa upande wa Magufuli.  

9.    Uongo, uongo na takwimu

Tanzania haina utamaduni wa kura za maoni kupima nafasi za wagombea katika uchaguzi. Tuna utaratibu wa muda mrefu wa kupata maoni ya wananchi katika maamuzi makubwa ya kisera – kuingia mfumo wa vyama vingi vya siasa, marekebisho ya Katiba, na kadhalika. Mwaka 2005, kulifanyika kura ya maoni, iliyobashiri ushindi mkubwa kwa CCM. Na kwa hakika, CCM ilishinda kwa asilimia 80. Mwaka 2010, kura ya maoni iliyoendeshwa na kampuni ya Ipsos-Synovate iliashiria kuwa idadi ya kura za CCM ingepungua hadi kufikia asilimia 61. CCM ilipinga matokeo ya kura hiyo ya maoni ikidani kuwa yalikuwa kiasi kidogo sana. Matokeo ya uchaguzi huo yalikuwa kama yalivyotabiriwa katika kura hiyo ya maoni. CCM ilipata asilimia 61 ya kura zote.

Hivi karibuni, kura mbili za maoni zilichapishwa. Zote zilifanywa na taasisi huru zinazoheshimika. – Twaweza and Synovate-Ipsos tena- zote zikijihusisha na utafiti wa kusaka maoni. Taasisi mbili tofauti, zilizotumia mbinu tofauti za kufanya utafiti, katika nyakati tofauti, matokeo yaleyale. CCM itashinda kwa asilimia 62 ya kura zote.

Inaruhusiwa, na kwa yumkini ni jambo zuri, kupingana na sababu hizi tisa za kwanini CCM itashinda. Lakini namba zina tabia ya ukandamizaji. Ndio mwelekeo wa kura huwezi kubadilika. Lakini kwa kuzingatia yote yaliyokwishaongelewa kuhusu kinachodaiwa kuwa ufuasi mkubwa kwa Upinzani, basi muda huu ingetarajiwa tuwa tunajadiliana kuhusu ufuasi wa wengi kutoka Upinzani kuelekea CCM– na sio kutarajiwa ufuasi wa wengi kutoka CCM kuelekea Upinzani. Na ndiyo, kura za maoni zaweza kukosea, na tusiwekee mkazo sana.Lakini hoja hii sasa ndiyo hupendelewa zaidi na upande unaelekea kushindwa kwenye uchaguzi.


January Makamba ni Mbunge wa Bumbuli (CCM), Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, na msomaji wa Kampeni za CCM 

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.