1 Apr 2016

Baada ya kada wa muda mrefu wa CCM, Balozi Juma Mwapachu kutangaza kurudi CCM baada ya kukihama chama hicho tawala wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita, aliyekuwa mpigadebe maarufu wa mgombea urais kwa tiketi ya UKAWA, Waziri Mkuu wa zamani Frederick Sumaye, ametangaza kujiunga tena na chama hicho tawala.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa kuna uwezekano wa wana-UKAWA wengine, mgombea wa kiti cha urais, Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa na aliyekuwa kada mkongwe Kingunge Ngombale Mwiru, kufuata mkumbo wa Balozi Mwapachu na Sumaye, ambapo tetesi zinadai kuwa wanaweza kutangaza kurejea CCM muda wowote kuanzia sasa.

Kwa habari kamili na picha, BONYEZA HAPA

25 Mar 2016

HATIMAYE baada ya vuta nikuvute ya muda mrefu, Zanzibar ilifanya marudio ya uchaguzi wake Jumapili iliyopita na Dk. Ally Mohamed Shein kushinda kiti cha urais kwa asilimia takriban 91.

Bila ‘kuuma maneno,’ uchaguzi huo ni mzaha wa kidemokrasia. Ni mzaha kwa sababu ingewezekana kabisa kutofanya marudio ya uchaguzi huo na matokeo ya sasa – yaani CCM kushinda – yakabaki kuwa yale yale.


Yayumkinika kuhitimisha kuwa upande unaoshikilia madaraka visiwani humo umedhamiria kwa dhati kuwa upande pinzani kamwe hautoruhusiwa kutawala, kwa amani au kwa shari.

Kwa lugha nyepesi, ‘piga ua’ chama cha CUF hakitoruhusiwa kutawala Zanzibar hata kama kitashinda uchaguzi kwa asilimia 99. Na tunapozungumzia asilimia ya ushindi, ni vigumu mno kwa sasa kwa chama chochote visiwani humo kupata ushindi mkubwa wa kukipa uhalali wa kutosha kutawala, sababu kuu ikiwa ni mgawanyiko sugu kati ya Waunguja na Wapemba.


Wengi wetu tunachukizwa na kinachoendelea Zanzibar lakini yaelekea hakuna mwenye uwezo wa kushauri nini kifanyike. Nami ninaangukia katika kundi hilo. Sababu za kihistoria zimeendelea kuitesa Zanzibar miaka nenda miaka rudi. Tangu kuruhusiwa kwa mfumo wa siasa za vyama vingi, visiwa hivyo vimeendelea kugawanyika kiitikadi kwa misingi ya Upemba (CUF) na Uunguja (CCM).

Japo inaweza kutopendeza kutumia mfano huu, lakini yayumkinika kulinganisha siasa za Zanzibar na mgogoro kati ya Wapalestina na Wayahudi. Kikubwa kinachowaogopesha Waisraeli kukubali amani ya kudumu na Wapalestina ni hofu ya kisasi.

Kwa bahati mbaya, siasa za chuki na ubaguzi visiwani Zanzibar nazo zinajenga mazingira hayo ya hofu, kwamba laiti ‘Wapemba wa CUF’ wakiingia madarakani watalipiza kisasi.

Na hoja hiyo inazidi kuchochewa na ukweli kwamba kuna ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu visiwani humo na unaofumbiwa macho na vyombo vya dola, huku kila upande ukitupa lawama kwa wapinzani wake.

Inapotokea waathirika wa siasa za chuki kukamatwa na kudhalilishwa wakiwa rumande, ni wazi watoto na wajukuu zao watabaki na chuki ya muda mrefu, chuki ambayo huko mbele sio tu itazidisha uhasama bali pia yaweza kuzua balaa kubwa.

Tukirejea kwenye uchaguzi huo wa Jumapili iliyopita, nimeeleza hapo awali kuwa ‘mshindi anajulikana’ kabla haya ya kupigwa kura kwa sababu zilizo wazi. Kwanza, CUF kilishatangza msimamo wake kususia uchaguzi huo. Kwa maana hiyo, asilimia kubwa ya waliopiga kura ni wana-CCM, ambao ni dhahiri wamekipigia kura chama chao.


Kwa kuzingatia kanuni ya demokrasia ya wengi wape, ushindi wa CCM utakuwa halali kwa vile wapigakura wengi wamekipigia chama hicho. Lakini wengi hapo haimaanishi Wazanzibari wote kwa ujumla bali wengi kwa maana ya wana-CCM.


Pili, hata kama CUF wasingewakataza wafuasi wao kushiriki uchaguzi huo, ni wazi kuwa CCM ingefanya kila iwezalo – na ina uwezo mkubwa tu – kuhakikisha kuwa CUF haiibuki na ushindi. Hicho, kimsingi, ndicho kilichosababisha kurudiwa kwa uchaguzi huo.

Hali hiyo haipendezi lakini ndio hali halisi. Ni ukweli mchungu, lakini ukweli una sifa kuu moja: uwe mchungu au mbaya unabaki kuwa ukweli. Ingependeza kuona Wapemba na Waunguja wakiungana kwa maslahi ya Zanzibar lakini hilo si rahisi kwa sasa.


Ugumu wa kuzungumzia siasa za Zanzibar unachangiwa na ukweli kwamba sio rahisi japo kushauri nini kifanyike angalau kupunguza migogoro isiyokwisha ya kisiasa visiwani humo.

CCM wakishindwa, CUF watasusia matokeo. Hali hiyo itaendelea kwa muda mrefu mpaka zifanyike jitihada mpya za kuunda serikali ya umoja wa kitaifa. Kibaya zaidi, mtu pekee anayewezesha uwepo wa serikali ya umoja wa kitaifa ni mgombea wa kudumu wa urais kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif Shariff Hamad. Hata jitihada zilizofeli za kutatua mgogoro uliosababisha kurudiwa uchaguzi huo zilitegemea zaidi jitihada za Seif.

Je, hali itakuwaje iwapo Seif akiondoka kwenye ulingo wa siasa? Lakini hata kama ataendelea kuwepo, je, wafuasi wa CUF wataendelea kumvumilia milele kila atakapojaribu kutafuta mwafaka kwa kukubali serikali ya umoja wa kitaifa? Hatari inayomkabili Seif kwa kuwa msuluhishi wa kudumu ni uwezekano wa yeye kuonekana msaliti miongoni mwa wafuasi wa chama chake.

Lakini ukweli kwamba Seif ni miongoni mwa viongozi wa zamani wa kitaifa, na hivyo kuwa mnufaika wa stahili mbalimbali kutoka serikalini unaweza kumkwaza kuelemea zaidi maslahi upande wa chama chake. Tumeshuhudia majuzi jinsi serikali ilivyogharimia matibabu yake. Sasa busara kidogo tu zapaswa kutukumbusha kuwa ni vigumu kwa mtu kukata mkono unaomlisha.

Baadhi yetu tunadhani hakukuwa na haja ya kupoteza fedha sio tu kurudia uchaguzi huo bali hata kufanya uchaguzi mwezi Oktoba mwaka jana kwa sababu imekwishakuwa kama kanuni ya siasa za Zanzibar kuwa lazima mshindi wa urais atoke CCM.


Sasa kuna haja gani ya kupoteza fedha kwa ajili ya mchakato ambao hautabadili chochote? Sawa, demokrasia ina gharama zake lakini gharama nyingine zinaepukika.

Nihitimishe makala hii kwa kubashiri kwamba jitihada zikifanyika, Zanzibar itapata tena serikali ya umoja wa kitaifa. Hata hivyo, mwaka 2020 visiwa hivyo vitajikuta kwenye hali tata kama iliyojiri katika kila chaguzi katika mfumo wa vyama vingi.


Ningetamani sana kuhitimisha makala hii na ushauri wa nini cha kufanya lakini ninatambua bayana kuwa njia pekee (na isiyofaa) ni CUF kuendelea kuvumilia ubabe wa CCM katika kila uchaguzi, na kukubali kushiriki katika serikali ya umoja wa kitaifa (ikiundwa). Lakini njia hiyo (ukitoa serikali ya umoja wa kitaifa) ndio sababu kuu ya mgogoro huo wa kudumu wa kisiasa huko Zanzibar. Na kama tunavyofahamu sote, tatizo haliwezi kutatuliwa na tatizo jingine.


18 Mar 2016

NIANZE makala hii kwa kuomba radhi kutokana na safu hii kutochapishwa wiki iliyopita. Hali hiyo ilitokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wangu.

Miongoni mwa mada zinazotawala katika mijadala mbalimbali ya Watanzania hususan katika mitandao ya kijamii ni pamoja na suala linalofahamika kama ‘Kiingereza cha Rais John Magufuli.’ Mjadala huo umepamba moto zaidi kwenye mitandao ya kijamii ya Jamii Forums na Facebook. Mjadala huo ulianza rasmi baada ya kikao cha wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambapo hotuba ya Rais Magufuli ilizua hoja kuwa ‘Kiingereza chake kina kasoro.’ 

Kama Mtanzania mwenye makazi hapa Uingereza, nchi ambayo ndio ‘wenyeji wa Kiingereza,’ na ambaye kwa sasa ninafundisha kundi la watafiti (profesa mmoja, wahadhiri saba na wanafunzi wa shahada ya uzamivu wanane) wanaotarajia kuja huko nyumbani kwa ajili ya utafiti, nimeguswa sana na mjadala huo. 

Kwanza tuweke rekodi sawa. Kimsingi, Kiingereza alichoongea Rais Magufuli kinakubalika. Sawa, kinaweza kuwa sio timilifu lakini moja ya ‘siri’ za kuongea lugha ya kigeni, ikiwa ni pamoja na Kiingereza kwetu, ni uwezo wa kueleweka.

Pili, bila kuonekana ninamtetea Rais Magufuli, ni muhimu tukumbuke kuwa asili yake kitaaluma ni mwanasayansi. Na japo si kila mwanasayansi anasumbuliwa na Kiingereza, sio jambo la kushangaza kukutana na Wanasayansi ambao hawamudu Kiingereza vizuri. Hii inatokana na ukweli kuwa masomo yao sio ya lugha, na Kiingereza wanachotumia ni cha kitaalamu zaidi kuliko cha maongezi ya kawaida. 

Lakini tatu, na hili ni la muhimu zaidi, Kiingereza sio lugha yetu ya asili. Katika hili nitoe mfano ufuatao. Nilipoombwa kufundisha kundi hilo la watafiti wanaotarajia kuja huko nyumbani, awali nilidhani ni kundi la wanafunzi wa shahada ya uzamifu pekee. Kwa hiyo, licha ya ukweli kwamba sijafundisha darasani kitambo, nilijipa matumaini kuwa jukumu lililo mbele yangu sio gumu sana kwa vile nitakuwa nafundisha wanafunzi pekee.

Hata hivyo, kabla ya kuanza kufundisha kozi hiyo, nilipatiwa orodha ya ‘wanafunzi’ wangu, ambapo kwa mshangao, ilijumuisha profesa na wahadhiri kadhaa (wahitimu wa shahada ya uzamivu ambao miongoni mwao wapo wanaofanya kitu kinachojulikana kama ‘post-doctorate.’) Kwa hiyo, kule kujiamini kwangu kwa awali kuliyeyuka ghafla kwani kumfundisha mwanafunzi ni suala moja, lakini kumfundisha mhadhiri, hususan huyo profesa, ni shughuli pevu. 

Lakini mkuu wa idara inayohusika na ufundishaji wa kozi za lugha za kigeni alinipa maneno haya ya kutia moyo; “…bila kujali kuna profesa na wahadhiri, wewe ndiye mwalimu wao. Uprofesa na uhadhiri ni kwenye fani zao, lakini katika Kiswahili hao wote ni wanafunzi wako.” Hiyo ilinipa moyo, na kozi hiyo imekuwa ikiendelea kwa ufanisi mkubwa.

Lengo la mfano huo ni kuonyesha kuwa linapokuja suala la lugha ya kigeni, Haijalishi fulani ni kiongozi wa nchi au profesa, kwa sababu ni watu wachache tu wanaomudu vilivyo lugha zisizo zao. Hao ‘wanafunzi’ wangu ni wasomi waliobobea katika fani zao, lakini hawajui Kiswahili japo cha kuombea maji. Na huwezi kuwalaumu kwa sababu lugha hiyo ni ngeni kwao.

Kuna kasumba moja inayokera sana kuhusu baadhi ya ‘wasomi’ wetu wa Kitanzania, ambapo kuongea Kiingereza kunawafanya wajione wapo daraja la juu zaidi ya wasiomudu vema lugha hiyo au wasioiongea kabisa. Kwa sisi wengine ambao tunaamka, tunashinda, na tunakwenda kulala huku tunasikia Kiingereza, tunakerwa na mazingira ambapo unakutana na Mswahili mwenzako, badala ya kukupatia fursa mwanana ya kuongea naye lugha yetu ya asili, anatumia Kiingereza.

Ni kasumba iliyoshamiri mno kwenye mitandao ya kijamii ambapo baadhi ya wenzetu hawataki kabisa kuzungumza Kiswahili. Mara kadhaa nimekuwa nikiwakumbusha Watanzania wenzangu kuwa sijawahi kuwaona Waingereza wakifanya maongezi kwa lugha ya kigeni labda iwe ni kwa minajili ya kujifunza tu. Tena kimsingi, Waingereza wanashutumiwa vikali na wenzao wa nchi mbalimbali za Ulaya kwa kupuuza lugha nyingine na kuiendekeza lugha yao.

Tofauti na sisi, wenzetu Wakenya wapo mahiri sana katika kukienzi na kukiendeleza Kiswahili. Kwa hapa Uingereza, Wakenya wengi wanajihusisha na shughuli za utafsiri wa Kiswahili kwenda Kiingereza au kinyume chake, kwa sababu wanamudu vema lugha zote mbili. Lakini kubwa zaidi ni mapenzi yao kwa Kiswahili, licha ya ukweli kuwa Kiswahili chetu Watanzania ni bora zaidi cha majirani zetu hao.

Ni nadra kwa hapa kukutana na Mkenya akazungumza nawe kwa Kiingereza. Atajikakamua hivyo hivyo na Kiswahili ‘chao’ lakini la muhimu mtaweza kuelewana. Sasa sisi Kiingereza chenyewe ni mgogoro mkubwa, lakini watu wapo radhi kujikakamua, na wengine kutokwa macho kama mjusi aliyebanwa na mlango, ili tu waongee ‘kimombo.’ Kwani wakizungumza Kiswahili wanapungukiwa na nini hasa?

Nimeambiwa kuwa katika hotuba yake kwenye dhifa ya kumkaribisha Rais wa Vietnam, Troung Tang Sang, Rais Magufuli alihutubia kwa Kiswahili. Nadhani huo ni mwanzo mzuri, na ninamsihi aendelee kuenzi lugha yetu ya taifa kwa sababu tusipoienzi sisi ‘wamiliki,’ ni dhahiri itapuuzwa na wengineo.

Inakadiriwa kuwa Kiswahili kinazungumzwa na takriban watu milioni 50 duniani. Ni lugha ya kimataifa. Wenye jukumu kubwa la kukienzi, kukiendeleza na kukitangaza ni Watanzania ambao kimsingi ndio tunaozungumza Kiswahili fasaha zaidi ya wenzetu wengine katika nchi kama Kenya, Uganda au Burundi.

Nimalizie makala hii kwa kuhitimisha kuwa pengine ‘lawama’ hizo zinazoelekezwa kwa Rais Magufuli kwa ‘Kiingereza chake’ zinaweza kuleta kitu Waingereza wanaita ‘blessing in disguise,’ yaani pale kitu kisichopendeza kinapoleta matokeo chanya. Kwa mfano, iwapo ‘lawama’ hizo zitasababisha Rais wetu sio tu kutumia zaidi Kiswahili katika matukio ya kimataifa bali pia kuhamasisha matumizi ya lugha yetu hiyo ya taifa.

Tukumbuke, mkataa asili yake ni mtumwa.

17 Mar 2016


Nilianza kumsikia Balozi Mwapachu tangu nikiwa mtoto mdogo. Huyu ni miongoni mwa yale majina ambayo miaka nenda miaka rudi utayasikia, kama sio kwenye uwaziri basi ni kwenye ukurgenzi wa taasisi flani, au uongozi wa tume flani kama sio ubunge. Wenzetu hawa ni kama watu waliozaliwa ili kuwa viongozi. Lakini hio sio dhambi wala kosa, maana yawezekana kuzeekea kwao katika uongozi ni matokeo ya uongozi wao wa kupigiwa mstari.

Hold on, nimesema 'uongozi wa kupigiwa mstari'? May be, maana dunia hii tunayoishi sasa hata sifa za uognzi hazijulikani ni zipi. Na sababu ya wazi ya sifa za uongozi kupoteza maana yake ni ubabaishaji, usanii,ufisadi, ujambazi, na kila baya unaloweza kulihusisha na tasnia ya uongozi.

Sie wengine tulikulia zama za chama kimoja. Tulishuhudia uongozi uliotukuka wa Mwalimu Nyerere. Ndio, kulikuwa na kasoro zake, kama vile viongozi kuonekana kama miungu-watu, lakini hawakuonekana miungu-watu kwa sababu ya utajiri wao bali angalau waliutumikia umma kwa namna moja au nyingine.

Tuliwaona viognozi mashambani, tuliwaona wakishiriki katika shughuli za ujenzi wa taifa, matengenezo ya barabara, ushiriki katika ujenzi wa miradi ya maendeleo, na vitu kama hivyo. Kumbuka, enzi hizo tulikuwa nchi ya ujamaa na kujitegemea, na miongoni mwa features za kujitegemea ilikuwa kutumia raslimali zetu, sio siku hizi zama za kutembeza bakuli kwa wafadhili, kisha kinachopatikana 'kinapigwa panga,' watu wanaporomosha mahekalu, wanaongeza idadi za magari yao ya kifahari, na sensa ya nyumba ndogo zao inazidi kukua.

Kwanini nimeandika 'kwa hasira' hivi? Jana nimesikia kituko kilichonichefua. Mmoja wa Watanzania wenye majina makubwa katika medani za uongozi, Balozi Juma Mwapachu, jana alitangaza kurejea CCM baada ya kukihama chama hicho tawala wakati tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu.

Kama nilivyosema awali, nimekuwa nikimsikia Juma Mwapachu tangu nikiwa mdogo. Lakini, mwaka jana nilipata fursa ya kuwasiliana nae. Sio uso kwa uso bali kupitia kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter. Sijui tulikuwa tunajadili nini lakini moja ya ajenda iliyojitokeza ni sapoti yake kwa Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa, ambaye baadaye aliteuliwa kuwa mgombea Urais kwa tiketi ya UKAWA. 

Balizo Mwapachu alijitokeza kuwa miongoni mwa watetezi wakuu wa Lowassa, huku nyakati kadhaa akitukumbusha 'yeye ni nani.' Wapo walioungana nae mkono lakini baadhi yetu tulimpinga waziwazi na kueleza bayana kuwa ni 'wazee' kama yeye walioifikisha Tanzania yetu mahali hapa pasipoeleweka. Baadaye akapotea mtandaoni, pengine kwa sababu 'wazee' kama yeye hawajazowea sana 'mbinde' za social media.

Alipotangaza kuachana na CCM na kumfuata Lowassa, halikuwa jambo la kushangaza kwa sie tuliowahi kushuhudia akimtetea huko Twitter. Baada ya kuhama CCM akajitahidi kutumia uweledi wake kueleza, kwanza kwanini CCM ni 'kimeo,' na pia kwanini Lowassa ndio ufumbuzi wa matatizo yanayoikabili Tanzania. Baadhi ya aliyoyasema yalikuwa na ukweli, lakini baadhi yetu hatukumuelewa kwa sababu moja tu: "alikuwa wapi siku zote hizo?" Yaleyale ya akina Lowassa, Kingunge, Sumaye na wengineo waliogeuka wakosoaji wakubwa wa mfumo walioshiriki kuuasisi huko CCM, mfumo wa wateule wachache huku mamilioni ya walalahoi wakiishia kuahidiwa hili kama sio lile.

Sasa jana akaamua kubadili gea angani, akatangaza kurudi CCM. Good, kuhama sio dhambi. Tatizo la msingi ni baadhi ya sababu alizoeleza kuwa zilimpelekea kuhama CCM na sasa kuamua kurejea.

Anadai 'alilewa' na ahadi ya Lowassa kuwa angepewa Uwaziri wa Mambo ya Nje. Hivi inaingilia akilini kweli kwa mtu kama huyo ambaye alikuwa miongoni mwa 'vijana wa Nyerere' kuhama chama alichokiasisi baba wa taifa kwa sababu tu alitarajia kupewa uwaziri wa mambo ya nje? Pengine sio kosa kwa sababu ni watu wangapi wasiotaka madaraka?

Lakini ili umuelewe vema ni muhimu kurejea posts zake mbalimbali huko Facebook na kwingineko alivyokuwa akiwahadaa vijana kuhusu ajenda ya mabadiliko. Kwanini nasema alihadaa? Kwa sababu mwenyewe amekiri jana kuwa kilichomvutia kwa Lowassa ni ahadi ya uwaziri wa mambo ya nje. Kule anahubiri kuhusu mabadiliko, huku anawazia uwaziri wa mambo ya nje. Baada ya Lowassa kushindwa kupata urais, na ndoto ya Mwapachu kuwa waziri wa mambi ya nje kuota mbawa, kaamua kurejea CCM. 

Tabia kama hizi zinaweza kuigharimu CCM huko mbeleni. Watu walioikimbia wakati wa shida (kwa maana ya mapambano ya kumwingiza mgombea wake Ikulu) wanaruhusiwa kurejea kiulaini tu na kigeugeu chao kurushwa na vyombo vya habari kana kwamba ni matukio yenye umuhimu mkubwa kihistoria.

Laiti ningekuwa na mamlaka huko CCM, ningemweka benchi Mwapachu kwa sababu kama alivyoondoka akiwa hana umuhimu wowote kwa chama hicho, ndivyo alivyorudi akiwa na umuhimu mdogo zaidi ya ule ambao hakuwa nao wakati anahama.

Nimalizie makala hii ya dharura kwa kutamka bayana kuwa Tanzania yetu imefikishwa hapa na vipongozi kama hawa, walafi wa madaraka licha ya kuwepo madarakani miaka nenda miaka rudi, viongozi wasio na msimamo, wanaoweza kuhadaa umma kuhusu mabadiliko ilhali mabadiliko pekee wanayopigania ni ya maslahi yao binafsi.

Nigusie jambo moja dogo baada ya majuzi kutangazwa viongozi wapya na wa zamani kuongoza mikoa yetu kama ma-RC. Sina tatizo na wengi walioteuliwa lakini kilichonisikitisha ni kuona baadhi ya sura zilezile za miaka nenda miaka rudi zikirudishwa kwenye uongozi. Kama mtu alikataliwa na wapigakura jimboni kwake kwanini apelekwe kuongoza watu wa mkoa mwingine? 

Na lini vijana wapya watapewa fursa ya kuongoza Watanzania wenzao iwapo tunaendelea ku-recycle sura zilezile? Mimi ni sapota mkubwa wa Rais Magufuli, tangu wakati wa kampeni hadi sasa. Ninaridhishwa mno na uongozi wake. Hata hivyo, hiyo haimaanishi akikosea sintomkosoa. Na kama nina moja la kumkosoa ni kutujazia sura za watu waliokaa kwenye uongozi miaka nenda miaka rudi [na usidhani ninalaumu kuhusu hilo kwa vile nilikuwa/nina matarajio ya uongozi. Licha ya kuridhiska na kidogo ninachopata hapa, pia ninaamini kuwa ili kuitumikia Tanzania yetu sio lazima mtu awe kiongozi. Just be a good mwananchi]

Yayumkinika kuhisi kuwa watu wa aina hiyo hawana cha kupoteza wakiboronga na kutimuliwa, kwa sababu baadhi yao tayari wanakula pensheni za ubunge au ukurugenzi wa kitu gani sijui. Wakitimuliwa, watanufaika kwa nyongeza ya fedha tu.

Na sintoshangaa pengine Mwapachu karudi CCM kubahatisha kupewa 'pande' la ubalozi. Na huwezi kumlaumu sana kwa sababu medani ya uongozi wetu imekuwa ni suala la ku-recycle watu walewale, wengi wakiwa ndio walioifikisha Tanzania yetu hapa tusipostahili kuwa.





15 Mar 2016

Rais Dkt John Magufuli amekutaa kukutana na ujumbe wa maseneta sita wa Marekani, tukuio lililojiri tarehe 18 ya mwezi uliopita. Ombi la maseneta hao kukutana na Rais liliwasilishwa na Waziri wa zamani wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, ambaye alikuwa mwenyeji wa maseneta hao walioongozwa na Seneta James Inhofe wa chama cha Republican kutoka jimbo a Oklahoma. Hata hivyo, Rais Magufuli alikataa ombi la kukutana na maseneta hao akidumisha taswira yake ya kujiweka mbali na wafanyabiashara na lobbyists.

Mwaka juzi, Seneta huyo mhafidhina alishutumiwa vikali na kundi moja la utetezi wa haki za wanyama baada ya kuhudhuria hafla moja ambapo njiwa walirushwa hewani na kutunguliwa kwa risasi.



Mtandao wa kiuchunguzi wa African Intelligence unaripoti kwamba waziri huyo ya zamani katika serikali ya Rais Mstaafu Jakaya Kikwete anajulikana kwa kuwa karibu na Wamarekani matajiri wanaohusiana na Mfuko wa Kuhifadhi Mazingira wa Friedkin. Mfuko huo unamiliki makampuni ya Tanzania Game Trackers Safaris, Wengert Windrose Safaris na Mwiba Holdings Limited. Kampuni hiyo ya mwisho imekuwa ikihusishwa mara kadhaa na kesi za ujangili


4 Mar 2016

MWISHONI mwa wiki iliyopita, mitandao kadhaa ya kijamii ilitawaliwa na shutuma dhidi ya tabia inayotoa mizizi kwa majirani zetu wa Kenya kutumia vivutio vya Tanzania kujitangaza kana kwamba vipo katika nchi hiyo.

Katika tukio la majuzi, video moja ilisambaa mtandaoni ikimwonyesha binti mmoja wa Kenya akihutubia mkutano mmoja wa kimataifa, huku akieleza bila aibu kuwa miongoni mwa vivutio vilivyopo nchini Kenya ni Bonde la Olduvai (Olduvai Gorge).


Tukio hilo ni moja tu katika mlolongo mrefu wa majirani zetu hao ‘kutupora’ umaarufu wetu, huku ‘uongo’ maarufu zaidi ukiwa kuutangaza Mlima Kilimanjaro kuwa upo Kenya. Hata Jumapili wiki hii nilipotembelea mtandao wa kijamii wa Twitter, nilikutana na ‘tweet’ moja inayodai kuwa Mlima huo unaonekana vizuri zaidi nchini Kenya (kuliko Tanzania).


Pamoja na lawama kadhaa zilizoelekezwa kwa majirani zetu hao, baadhi ya Watanzania walikwenda mbali zaidi na kuhoji kwa nini nchi jirani inapata ujasiri wa kujinadi kwa kutumia vivutio vyetu. Ukweli mchungu ni kwamba sisi wenyewe tumekuwa wazembe kwa kiasi kikubwa.


Uzembe huo unaonekana katika sura nyingi lakini pengine ya wazi zaidi ni katika ukweli mchungu kuwa licha ya madini ya Tanzanite kupatikana Tanzania pekee, nchi zinazoongoza kwa mauzo ya madini hayo ni India ikifuatiwa na Kenya. Hiki ni kichekesho kinachokera mno.


Binafsi, ninaona udhaifu katika kunadi vivutio vyetu na nchi yetu kwa ujumla unachangiwa na sababu kuu tatu. Ya kwanza, ni uhaba wa uzalendo. Mara kadhaa nimekuwa nikiandika kuhusu suala hili. Moja ya vitu muhimu alivyotuachia Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ni kuthamini Utanzania wetu. Na thamani hiyo ya asili yetu haikuwa kwa sababu tu ni nchi yetu bali pia katika mambo kadhaa ya kujivunia kama vile mchango wa taifa letu katika mapambano ya ukombozi kusini mwa bara la Afrika.


Leo hii baadhi yetu tukikutana na Waafrika Kusini au Wazimbabwe, kwa mfano, wanaikumbuka Tanzania kama nchi iliyoshirikiana nao katika mapambano ya kudai haki yao ya kujitawala. Hata hivyo, baadhi hutuhoji kwa nini Tanzania imepoteza umaarufu mkubwa wa enzi za Mwalimu Nyerere.


Sababu ya pili, inayoshabihiana na hiyo ya kwanza ni ubinafsi. Watanzania wengi wamekuwa wakiweka mbele zaidi maslahi yao binafsi kuliko maslahi ya taifa letu. Umaarufu binafsi umekuwa ukipewa kipaumbele zaidi kuliko umaarufu wa nchi yetu. Kibaya zaidi, wachache tunaojitahidi kuitangaza nchi yetu kwa namna moja au nyingine huishia kuzodolewa kuwa tunafanya hivyo kwa minajili ya kujikomba au kusaka ukuu wa wilaya.


Katika hilo la ubinafsi, kunapojitokeza mawazo ya kuitangaza nchi yetu kimataifa, badala ya kuangalia taasisi au watu wenye uwezo wa kutekeleza jukumu hilo kwa ufanisi, fursa huelekezwa kwa ndugu, jamaa na marafiki wasio na uwezo. Kipaumbele huwa kwenye fedha zilizotengwa kwa shughuli hiyo na wala sio matokeo chanya.


Sababu ya tatu ni kutowatumia vema Watanzania walio nje ya nchi. Kimsingi, kuwa Mtanzania nje ya nchi ni kama laana ya aina fulani. Kwa kiasi kikubwa tu, baadhi ya Watanzania wenzetu wanatuona sisi tulio nje ya nchi kama Watanzania vipande, yaani tusio kamili, na hatupaswi kujihusisha na masuala yanayohusu nchi yetu.


Baadhi yetu tunapojaribu kushiriki ujenzi wa taifa letu kwa njia kama hizi za maandiko huishia kukatishwa tamaa na kauli kama acha kutukebehi. Shida tunazopata hapa wazijua? Kana kwamba mtu akiwa nje ya Tanzania ndio amepoteza kila mawasiliano (connection) aliyonayo na nchi yetu, kuanzia ndugu, jamaa na marafiki hadi uraia.


Kama kuna nchi mbili barani Afrika ambazo zimenufaika sana kuwatumia raia wake wanaoishi nje ya nchi, nchi hizo ni Rwanda na Nigeria. Kwa Rwanda, takriban kila mwaka nchi hiyo hufanya makongamano katika nchi mbalimbali duniani, hususan hapa Uingereza na Marekani. Wiki iliyopita, Rais Paul Kagame yupo nchini Marekani, ambapo pamoja na mambo mengine anahamasisha Wanyarwanda walio nje ya nchi kushiriki katika ujenzi wa taifa lao.


Katika makongamano yaliyopita ya Rwanda hapa Uingereza, Rais Kagame alifanikiwa kuwashawishi Wanyarwanda kadhaa waliokuwa wanaishi hapa kurejea nyumbani na kuwapatia fursa mbalimbali zilizoendana na sifa, ujuzi na uzoefu wao walioupata walipokuwa hapa.
Kwa Nigeria, kabla ya kuunda serikali yake, na wakati huu ambapo nchi hiyo inapitia mageuzi makubwa ya kiuchumi, Rais Muhammad Buhari amekuwa akifanya jitihada kubwa kuwashawishi raia wa nchi yake waliotapakaa sehemu mbalimbali duniani kurejea katika taifa hilo ili kushiriki katika kulijenga na kuliboresha.


Sambamba na hatua hizo, badala ya kutumia fedha nyingi katika tenda za kuzipromoti nchi hizo nje ya nchi, kipaumbele kimekuwa katika kuwatumia raia wake kadhaa waliopo nje ya nchi hizo.


Licha ya kuvunjwa moyo, baadhi yetu tumeendelea na jitihada hizo za kuitangaza Tanzania yetu kwa kutumia njia mbalimbali. Kwa mfano, kwa muda sasa, binafsi nimekuwa nikijaribu kuitangaza Tanzania yetu kwenye mtandao wa kijamii wa twitter kwa mabandiko (tweets) yanayoambatana na hashtag #VisitTanzania (kwa kila habari au picha inayohusu vivutio vyetu) na #InvestInTanzania (kwa habari au picha zinazohusiana na fursa za uwekezaji huko nyumbani. Hata hivyo, mapokeo yamekuwa sio ya kuridhisha japo hainivunji moyo.


Kwa upande mwingine, licha ya uandishi wa vitabu kwa lugha ya Kiswahili kuchangia jitihada za kuitangaza Tanzania yetu kupitia lugha yetu ya taifa, ninaitumia pia fursa niliyoipata hivi majuzi ya kufundisha Kiswahili kwa kundi la wanafunzi wa shahada ya uzamifu katika Chuo Kikuu cha Glasgow, (wanaotarajia kuja huko nyumbani kwa ajili ya tafiti zao) kuitangaza nchi yetu kwa namna moja au nyingine.


Nihitimishe makala hii kwa kuwakumbusha Watanzania wenzangu kuhusu busara hii: “…usipoeleza mazuri yako wewe mwenyewe, wenzako wataeleza mabaya yako au kuyapora mazuri yako hayo.” Hicho ndio kinachofanywa na majirani zetu wanaojinadi kwa kutumia vivutio vyetu. Sisi wenye vivutio hivyo tumejisahau/tunazembea, wenzetu wanaojua umuhimu wa kujinadi wanatumia vyema kujisahau kwetu/uzembe wetu kwa manufaa yao.
Kadhalika, ninatoa wito kwa Serikali ya Rais Dk. John Magufuli kutumia vyema Watanzania wenye uwezo na fursa za kuinadi nchi yetu, ndani na nje ya Tanzania.


Mungu Ibariki Tanzania

26 Feb 2016

WIKI mbili zilizopita nilishiriki katika mjadala maalumu ulioendeshwa na Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Ujerumani kuhusu siku 100 za utawala wa Rais John Magufuli.
Lengo la makala hii sio kuzungumzia mjadala huo bali mada ya hiyo muhimu kwa Dk. Magufuli na serikali yake ya Awamu ya Tano, pamoja na Watanzania kwa ujumla.
Katika baadhi ya makala za hivi karibuni nilieleza kuhusu kitabu nilichochapisha kuhusu Dk. Magufuli na safari yake ya kuelekea Ikulu, sambamba na mafanikio na changamoto kwa urais wake. Lakini nilikosolewa na watu kadhaa waliodai ni mapema mno kuzungumzia mafaniko ya kiongozi huyo katika muda mfupi aliokaa madarakani.
Hata hivyo, wakosoaji hao walikerwa na mafaniko tu na si changamoto kwake, ikiashiria bayana kuwa wangependa zaidi kuona Dk. Magufuli akikosolewa kuliko kupongezwa.
Mshiriki mmoja katika mjadala huo naye aligusia hoja hiyo na alitumia muda mwingi kukumbusha kuwa hata watangulizi wake (Dk. Magufuli) walianza urais wao kwa kasi kama hii tunayoshuhudia hivi sasa.
Sina tatizo sana na wanaodhani ni mapema mno kusherehekea ufanisi mkubwa unaoendelea kuonekana katika uchapakazi wa Magufuli na serikali yake. Kimsingi, hofu waliyonayo wanaodhani ni mapema mno ina mantiki, hasa kwa vile yalishatukumba huko nyuma.
Kwa mfano, katika awamu yake ya kwanza, Rais Benjamin Mkapa alifanikiwa kurejesha nidhamu ya matumizi na takwimu za uchumi wetu zilipaa. Hata hivyo, awamu ya pili ya uongozi wake ilikuwa na mengi yaliyoathiri mazuri mengi aliyofanya katika awamu yake ya kwanza.
Kadhalika, katika utawala wa Rais Jakaya Kikwete, mwanzoni ilonekana kuwa Tanzania imempata kiongozi ambaye sio tu anayajua matatizo yanayoikabili nchi bali pia mwenye nia ya dhati ya kuyatatua. Kaulimbiu ya Maisha Bora kwa Kila Mtanzania ilileta matumaini kwa kila Mtanzania. Vile vile, maelezo yake kwamba sio tu anawafahamu wala rushwa bali pia anawafahamu kwa majina ilileta hisia kuwa arobaini ya wala rushwa imewadia. Sote tunafahamu kilichojiri katika miaka 10 ya utawala wake.
Kwa mantiki hiyo, wenye kumbukumbu hizo zisizopendeza wana haki ya kuwa na hofu ya mwenendo wa kuridhisha wa utawala wa Dk. Magufuli na serikali yake inayoendeshwa kwa kuzingatia kaulimbiu ya Hapa Kazi Tu.
Hata hivyo, nilitumia mfano huu katika mjadala huo wa Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Ujerumani, timu mbovu ya soka, ambayo miaka nenda rudi imekuwa ikiboronga, itakapokuwa na mechi muhimu, ikafunga goli la kwanza tu, basi mashabiki hawawezi kuacha kushangilia kisa huko nyuma ilikuwa kichwa cha mwendawazimu.
Mashabiki wataishangilia na kuihamasisha, ambapo hamasa hiyo ikichanganywa na goli moja walilokwishafunga, vyaweza kuipa nguvu timu hiyo ya kichovu kupata bao jingine na pengine mengi zaidi.
Kwa mashabiki wa soka wa ligi kuu ya hapa Uingereza, ni nani alidhani timu ya kawaida tu ya Leicester City ingekuwa miongoni mwa timu zenye nafasi kubwa ya kuchukua ubingwa kuliko wakongwe kama Manchester United?
Mfano huo unamaanisha kwamba kwa vile mwenendo wa Tanzania yetu katika awamu zilizopita ulianza kwa matumaini na kisha matumaini hayo kuyeyuka haimaanishi kuwa lazima iwe hivyo milele. Tukumbuke kuwa penye nia pana njia, pasipo na nia pana visingizio.
Pengine kabla ya kumhukumu Magufuli kama Rais ni vema kuangalia utendaji wake huko nyuma katika nyadhifa mbalimbali alizoshika. Kimsingi, moja ya ugumu mkubwa niliokumbana nao wakati naandika kitabu kinachomhusu ni uhaba wa maelezo kutoka kwake mwenyewe. Yaani machache yaliyo kwenye vyombo vya habari yanaelezea zaidi kuhusu aliyokuwa akitenda kuliko aliyoongea.
Wakati pekee ambapo kauli za Magufuli zilisikika zaidi ni wakati wa kampeni za kuwania urais. Na kauli hizo ndizo zilizotupatia ushawishi sisi wengine kuamini kuwa huyo ndiye kiongozi ambaye Tanzania inamhitaji. Sio tu alionyesha kujua kwa undani matatizo yanayoikabili nchi yetu bali pia alikuwa na mwelekeo kuhusu jinsi ya kuzikabili na kuzitatua.
Na kama ilivyokuwa kwenye zama za uwaziri, Magufuli tangu aingie Ikulu amekuwa mwingi wa vitendo kuliko maneno. Anapozungumza, unatamani aendelee maana hazungumzia kama kiongozi tu bali pia kama Mtanzania ambaye amechoshwa na mwenendo wa taifa letu na amedhamiria kubadilisha mwelekeo kwa uzuri.
Changamoto si lazima ziwe kikwazo kwa kiongozi. Kimsingi, changamoto ni kipimo kizuri kwa kiongozi kwa sababu kadri anavyozishughulikia zinaonyesha uwezo wake wa kiuongozi. Na itakuwa sio kumtendea haki kama akili yetu itaelekezwa kwenye changamoto tu (na ambazo baadhi amekuwa akizishughulikia vema) na kupuuzia mafaniko ya kihistoria aliyokwishapata.
Vile vile ni muhimu kutambua hali ya nchi yetu ilivyokuwa wakati Magufuli anaingia madarakani. Takriban kila eneo lilikuwa shaghalabaghala. Angeweza kabisa kujipa kisingizio kwa hotuba mfululizo kutueleza mlolongo wa matatizo na changamoto zilizopo huku akihitaji muda wa kuanza kuzishughulikia.
Lakini kama tunavyoshuhudia, na kwa vile sote tunamfahamu kama mtu wa vitendo zaidi kuliko maneno, anashughulikia matatizo na changamoto hizo zaidi ya kuongea tu.
Kuna tatizo kuhusu Zanzibar, ambalo kwa hakika linatia doa kuhusu Awamu ya Tano. Hata hivyo, kumlaumu Magufuli kwa vile ni Rais wa Tanzania nzima ni kupuuza mkanganyiko wa kikatiba kati ya ile ya Muungano na hiyo ya Zanzibar. Tunapoambiwa kuwa Magufuli hawezi kutatua mgogoro huo ni ukweli, na kama tunavyofahamu, ukweli una sifa moja kuu: hata ukiwa mchungu, hauwi uongo bali unabaki ukweli. Tungependa afanye kitu fulani kuhusu mgogoro huo lakini Katiba inambana.
Kuhusu ushauri wa nini kifanyike baada ya siku hizo 100 za urais, nafasi katika makala hii haitoshi kuelezea kwa kirefu lakini machache ni haya: mosi, asiingie mtego wa kutanguliza maslahi ya kisiasa badala ya maslahi ya nchi (na historia yaonyesha kuwa amekuwa akiongozwa na utaifa kuliko itikadi za kisiasa.
Pili, sambamba na mapambano endelevu kuhusu ufisadi, rushwa na uhalifu mwingine, aweke mkazo katika kuhamasisha uzalendo ambao umepotea kwa kiasi kikubwa. Hii itasaidia pia kupata uungwaji mkono kwenye mapambano yake dhidi ya ufisadi na uhalifu mwingine.
Tatu, kuhamasisha kilimo kwa vitendo badala ya sera mfululizo zilizoishia kuwa sera tu pasi mafanikio. Vile vile, aweke kipaumbele kuhakikisha kuwa licha ya kuwa mkombozi wa kiuchumi kwa wakulima, kilimo kinakuwa chanzo cha ajira.

Nne, haja ya kuyaangalia maendeleo ya sayansi na teknolojia kama mahitaji muhimu (basic needs) na sio anasa (luxury), kwa sababu katika miaka michache ijayo, tunapopuuza maendeleo ya sayansi na teknolojia tutabaki kuwa kama kisiwa.
Tano, kuendeleza mabadiliko ya Katiba ambayo yatazingatia maslahi ya nchi badala ya chama, na hili linaweza kutoa ufumbuzi wa migogoro isiyoisha kila kunapofanyika uchaguzi mkuu huko Zanzibar.
Sita, tumbua majipu ihamie kwenye chama tawala, hasa kwa vile huko ndiko kunakoweza kumkwaza zaidi kuliko vyama vya upinzani. Inakera mno kuona mwanasiasa mwenye lundo la tuhuma za ufisadi akichaguliwa kushika nafasi muhimu kwenye taasisi kama Bunge, kwa vile tu amepigiwa debe na wana-CCM wenzake.
Saba, hatujawa na mfumo wa kuthamini mchango wa Watanzania wenzetu, walio ndani au nje ya nchi yetu, wanaojitoa mhanga kupigania maslahi ya nchi yetu. Ifike mahala michango yao itambuliwe, si kwa kupewa vyeo bali hata kutambua rasmi (acknowledge) jitihada zao kwa pongezi tu.
Nane, kubwa zaidi ni mageuzi kwenye Idara ya Usalama wa Taifa (nimeyaeleza kwa kirefu katika kitabu nilichochapisha majuzi kuhusu taaluma hiyo nyeti).
Mwisho, kama alivyoeleza katika hotuba yake kwa wazee wa Jiji la Dar es Salaam, wakati tunajadili siku zake 100 tangu aingie aingie madarakani, je, sisi wenyewe kama wananchi tumefanya nini kwa nchi yetu katika siku hizo 100?
Tusijadili tu Magufuli ameifanyia nini Tanzania, tujiulize pia nasi tumeifanyia nini nchi yetu. Tusitarajie tu Magufuli atafanya nini, tutafakari nasi tunafanya au tutafanya nini kwa nchi yetu.
Hongera Magufuli kwa kutimiza siku 100 za urais wako kwa ufanisi wa kupigiwa mstari. Mungu akuongoze uendelee kuwa mtumishi bora wa umma, na atuongoze nasi wananchi kukuunga mkono na kutimiza wajibu wetu wa kiraia.
Mungu mbariki Rais Magufuli
Mungu Ibariki Tanzania yetu.
Mungu tubariki Watanzania

ANGALIZO: Makala hii ilipaswa kuchapishwa Jumatano mbili zilizopita lakini haikuchapishwa kwa sababu zilizokuwa nje ya uwezo wangu. Iliandikwa maalum kwa ajili ya tathmini ya siku 100 tangu Rais Dokta Magufuli aingie madarakani.



29 Jan 2016

KATIKA tasnia ya ushushushu kuna kitu kinachoitwa Moscow Rules (yaani Kanuni za Moscow). Hizi ni kanuni za zama za Vita Baridi ambazo majasusi waliopangiwa kazi nchini Urusi walipaswa kuzizingatia, kwa sababu nchi hiyo ilikuwa nguli wa kukabiliana na majasusi. Moja ya kanuni hizo inasema; “Once is an accident. Twice is a coincidence. Three times is an enemy action.” Kwa tafsiri isiyo rasmi; kitu kinachojiri mara moja ni ajali; kikijiri mara ya pili ulinganifu wa bahati mbaya, sio makusudi; kikijiri mara ya tatu ni kitendo cha adui.”

Nimeanza makala hii na angalizo hilo kwani ndio wazo lililoniingia kichwani mara baada ya kusoma kauli za aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, katika Serikali ya Awamu ya Nne, Bernard Membe.

Wiki iliyopita, Membe alinukuliwa na vyombo vya habari akimkosoa Rais Dk. John Magufuli, angalau katika maeneo matatu. Kwanza, Membe alidai kuwa kiuhalisi, Dk. Magufuli hajapunguza idadi ya wizara kama alivyoahidi bali amepunguza idadi ya mifuko, na kutanabaisha kuwa Rais hajabana matumizi yoyote kwa kupunguza ukubwa wa baraza la mawaziri, bali alichofanya ni kupunguza idadi ya mawaziri na sio wizara.

Alichofanya ni sawa na kuwa na mayai kumi halafu ukaamua kuyaweka kwenye mifuko kumi, maana yake ni kwamba utakuwa na mifuko kumi yenye mayai,” alisema waziri huyo wa zamani ambaye pia alikuwa miongoni mwa makada wa CCM waliowania kuteuliwa kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho tawala.

Lakini unaweza kuwa na idadi hiyo hiyo ya mayai na ukaamua kuyagawanya; mayai matatu unayaweka kwenye mfuko mmoja, mawili kwenye mfuko mwingine na yaliyobaki kwenye mfuko mmoja. Maana yake ni kwamba utaendelea kuwa na mayai kumi lakini idadi ya mifuko imepungua. Hapa sasa utakuwa hujapunguza gharama za kuyatunza hayo mayai,”aliongeza Membe.

Membe alidai kwamba Magufuli ameendeleza wizara zile zile lakini kaamua kuzikusanya pamoja, na kuona kuwa mfumo huo mpya wa wizara unaweza kuathiri uwasilishaji wa bajeti bungeni kwa vile mawaziri sasa watahitaji muda mwingi zaidi kuliko ilivyokuwa awali.

Hilo tutaliona kwenye Bajeti ya Serikali ya mwaka huu. Tuone kama bajeti itaongezeka au itapungua? Kwa sababu kama wizara zimepungua kama tunavyoamini, lazima bajeti ipungue, sasa bajeti ikiongezeka au ikibaki vile vile maana yake hakuna kilichofanyika,”alitahadharisha.

Eneo la pili ambalo Membe alimkosoa Magufuli ni udhibiti wa safari za nje, akidai kuwa Tanzania si kisiwa. Membe, aliyekuwa mtetezi mkuu wa safari mfululizo za Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete nje ya nchi, alisema kuwa safari za nje zina manufaa kwa taifa, na kusisitiza kuwa lazima Rais Magufuli asafiri kwenda nje ya nchi.

Tanzania si kisiwa, hata ukiwa tajiri namna gani lazima utoke nje ya nchi yako,” alisema Membe, na kutahadharisha kuwa nchi yetu inaweza kuwa kama Zimbabwe kwani ukijitenga, utatengwa.
Alisema nchi ina mabalozi 36 tu duniani kote kati ya nchi 194 zinazohitaji uwakilishi huo na kibaya zaidi, mabalozi hawaruhusiwi kuingia kwenye baadhi ya vikao, na hata wakiingia wakifika kwenye hatua ya uamuzi watazuiwa kushiriki.

Eneo la tatu ambalo japo hakumtaja Magufuli wala kukosoa moja kwa moja lakini linaloweza kutafsiriwa kama kuikosoa serikali kuhusu wafanyabiashara, ambapo alitahadharisha serikali kutowachezea.

Waziri huyo ambaye pia ni mbunge wa zamani wa Mtama (CCM) alipongeza kasi ya Magufuli katika vita dhidi ya ufisadi na kudhibiti mianya ya kukwepa kodi lakini akatahadharisha kuhusu haja ya kuwa mwangalifu katika kuwashughulikia wafanyabiashara. Alidai kuwa wafanyabiashara wana masikitiko makubwa dhidi ya serikali, na anaona suala hilo litaibuka kwa kishindo bungeni.

Licha ya maeneo hayo matatu, Membe alizungumzia kauli ya aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa, aliyedai wafanyabiashara waliomuunga mkono wananyanyaswa. Alieleza kuwa si dhambi kwa wafanyabiashara kufadhili vyama vya siasa wakati wa uchaguzi, na kwamba serikali ya chama kilichoshinda uchaguzi inapaswa kuwakusanya wafanyabiashara wote na kufanya nao kazi na sio kuwaburuza.

Kadhalika, mwanasiasa huyo alizungumzia kuhusu “timua timua” ya watumishi wa umma wanaohusishwa na tuhuma za ufisadi.

Ni rahisi kumshughulikia mtu usiyemfahamu lakini siyo rahisi kumshughulikia mtu unayemfahamu,” alidai Membe, na kuongeza kuwa haitokuwa shida kwa Magufuli kuwashughulikia watendaji aliowakuta serikalini ambao kimsingi hakuwateua, na hawafahamu. Alihoji iwapo Rais ataweza kuwatimua aliowateua mwenyewe.

Kauli hizo za Membe zimezua mjadala mkubwa, hususan kwenye mitandao ya kijamii. Japo kabla yake, aliyekuwa Naibu wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Makongoro Mahanga, alimkosoa Magufuli kuhusu ukubwa wa kabineti yake, ukweli kwamba Membe bado ni kiongozi wa juu wa CCM ilhali Mahanga alihamia upinzani, unaashiria mengi.

Lakini binafsi sikushangazwa na kauli hizo za Membe, hasa kwa vile awali, katika kitabu nilichokichapisha hivi karibuni kuhusu safari ya urais wa Magufuli, mafanikio na changamoto katika urais wake, nilibainisha kuwa moja ya changamoto zinazoweza kumkabili Rais huyo wa Awamu ya Tano ni maadui wa ndani ya chama chake.

Kimsingi, hoja zote za Membe hazina mashiko. Kuhusu anachoita ukubwa wa baraza la mawaziri, la muhimu kwa Watanzania si ukubwa au udogo bali uchapakazi. Ni bora kuwa na mawaziri, manaibu na makatibu wakuu hata 1,000 wachapakazi, kuliko kuwa na serikali ndogo inayokumbatia mafisadi.
Pia Membe alipaswa kufahamu kuwa utendaji kazi wa viongozi wa serikali unategemea sana utendaji kazi na msimamo wa bosi wao, yaani Rais aliyewateua. Ni dhahiri kuwa Membe anatambua kuwa Magufuli si mtu wa porojo, mtoa ahadi anazoshindwa kuzitekeleza mwenyewe (rejea kauli ya “ninawajua wala rushwa kwa majina” ya Kikwete), na kimsingi Watanzania na dunia nzima wanafahamu kuwa kaulimbiu ya Hapa Kazi Tu ya Magufuli ni tofauti na zama za nchi kujiendesha yenyewe (on autopilot).

Kuhusu safari za nje, Membe amepotoka mno, pengine kwa sababu kwa wadhifa wake wakati huo, alikuwa mmoja wa wasafiri nje ya nchi mara kwa mara. Kwanza, Rais Magufuli hajawahi kutamka kuwa hatosafiri. Kwa hiyo, kauli ya Membe kuwa lazima atasafiri ni fyongo.

Pili, zuio la safari za nje sio ‘blanket ban’ bali ni kwa safari zisizo na tija. Lakini kwa nini tushangazwe na kauli hiyo ya Membe ilhali tunafahamu misafara ya serikali iliyopita ilivyosheheni wajumbe kwa kutumia fedha za umma? Ni mtu mwenye matatizo tu anayeweza kutetea safari zenye manufaa zinazoligharimu taifa matrilioni ya shilingi huku faida tarajiwa zikiwa pungufu ya gharama husika.

Mwanadiplomasia msomi kama Membe alipaswa kuangalia hapo jirani tu kwa Rais Paul Kagame, kulinganisha idadi ya safari zake nje na zile za Kikwete kisha kuangalia hali ya uchumi kati ya nchi hizo mbili.

Vilevile ni rahisi kwa Membe kuzungumzia mafanikio ya safari hizo kwa vile ni Watanzania wachache wanaofahamu vituko vilivyoambatana na safari hizo. Ni mara ngapi safari hizo za ‘manufaa’ zilijumuisha shopping, kuhudhuria birthday parties, na matukio mengine yasiyo na tija kwa serikali?

Kuhusu wafanyabiashara, ni upuuzi wa hali ya juu kuhisi tu kuwa kuna uonevu dhidi ya mfanyabiashara yeyote. Kama kuwabana wafanyabiashara wakwepa kodi ni uonevu basi Magufuli aongeze dozi, maana hizi sio zama za Tanzania kuwa shamba la bibi.

Membe anadai wafanyabiashara wana masikitiko na suala hilo linaweza kuibuka bungeni. Anamaanisha Bunge limejaa wafanyabiashara au? Na kama masikitiko yao ni kutokana na Serikali ya Awamu ya Tano kuwabana ili wasikwepe kodi na kwamba masikitiko hayo yanaweza kusababisha kupoteza wawekezaji, basi na waondoke hata kesho. Hatuhitaji wakwepa kodi nchini. Kimsingi, wanaolalamika wala hawastahili kuitwa wafanyabiashara bali wahujumu wa uchumi wetu.

Na hoja yake kuhusu ‘timua timua’ haishangazi kwani moja ya udhaifu wa serikali ambayo Membe alikuwa waziri ilikuwa ni kuwaonea aibu wanaoboronga, na matokeo yake hali hiyo ilivutia waborongaji wapya kwani walishabaini kuwa hakuna wa kuwachukulia hatua. Hivi Membe anaweza kutuambia lolote kuhusu ahadi ya Riais Kikwete aliyoitoa Februari 2006 kwamba anawafahamu wala rushwa kwa majina na anawapa muda wajirekebishe? Sawa, Magufuli alipoingia Ikulu alikuta orodha hiyo ya wala rushwa aliowajua Kikwete na kuamua kuifanyia kazi?

Nimeeleza awali kuwa nimelizungumzia suala hilo kwa kirefu kitabuni. Sitaki kabisa kuamini kuwa kauli za Membe ni zake peke yake. Hisia zinanituma kuamini kuwa huu ni moshi tu unaoashiria moto unaowaka ndani kwa ndani ya CCM kati ya makundi makuu mawili: la Hapa Kazi Tu la Magufuli linalotaka kuiondoa Tanzania katika lindi la ufisadi unaoifanya nchi yetu kuzidi kuwa masikini, na kundi la wanufaika wa ufisadi linalomwona Magufuli kama mtu anayewaziba pumzi. Naam, ufisadi ni ‘lifeline’ ya watu walioigeuza nchi yetu Shamba la Bibi, wakivuna wasichopanda.

Nimalizie makala hii kwa kutoa wito kwa makada wa CCM, ambao wengi wao wanaimba Hapa Kazi Tu, lakini wakisikia madhambi yaliyofanywa na mwana-CCM fulani wanakimbilia kuwanyooshea vidole wapinzani. Wapinzani wakuu wa Magufuli hawapo Chadema au nje ya nchi bali wapo ndani ya chama hicho tawala. Na njia pekee ya kupambana nao ni kuweka mbele maslahi ya taifa badala ya kutanguliza umoja na mshikamano wa chama. Kuna usemi mchawi akimaliza kuroga mtaa hugeukia familia yake. Majipu yaliyomo ndani ya CCM yasipotumbuliwa mapema yatamkwaza Magufuli na nchi yetu kwa ujumla.


Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.