16 May 2016

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akihutubia Watanzania wanaoishi hapa Uingereza



Sehemu ya hotuba ya Waziri Mkuu Majaliwa


Baadhi ya Watanzania wanaoishi hapa Uingereza wakiwa katika mkutano huo na Waziri Mkuu Majaliwa



Sehemu ya hotuba ya Waziri wa Mambo ya Nje Balozi Mahiga

Waziri Mkuu Majaliwa na Balozi Mahiga 

Baadhi ya Watanzania wanaoishi hapa Uingereza wakiwa katika mkutano huo




Waziri Mkuu Majaliwa akiwa na Kaimu Balozi Mr Marwa (wa kwanza kushoto), Balozi Mahiga na Jaji Mkuu Chande (kulia)

Waziri Mkuu Majaliwa akihutubua


Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Valentino Mlowola akiongea kwenye mkutano huo


Jaji Mkuu Chande akiongea


Jaji Mkuu Chande akiongea. Kushoto kabisa ni Balozi Mahiga na kulia ni Kamanda Mlowola

Waziri Mkuu Majaliwa akihutubia


Meza kuu


Sehemu ya Watanzania waliohudhuria Mkutano huo uliofanyika kwenye ubalozi wa Tanzania jijini London hapo jumamosi Mei 14, 2016

14 May 2016


Jana nilibandika makala kuhusu manung'uniko ya Watanzania wengi wanaoishi hapa Uingereza ambao walikuwa hatarini kukosa fursa ya kuhudhuria mkutano na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye yupo nchini hapa kikazi.

'Kelele' hizo zimezaa matunda, na leo Waziri Mkuu Majaliwa atakutana na Watanzania wote wanaoishi nchini humu wanaoweza kumudu kufika ubalozini London saa kumi alasiri. Awali, maofisa husika katika ubalozi huo walialika kundi dogo tu la Watanzania kuhudhuria mkutano huo, hatua iliyotafsiriwa na wengi kama ubaguzi na pengine jitihada za kuficha majipu yanayoukabili ubalozi huo.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu imeandikwa kidiplomasia, ambapo kwa upande mmoja imejitoa lawama ya kuhusika na maandalizi ya mkutano huo (na hakuna aliyemlaumu Waziri Mkuu au Ofisi yake bali lawama zilielekezwa kwa ubalozi) .



Kwa upande mwingine ni kama imekanusha 'madai ya watu' kuwa kuna watu maalum waliochaguliwa kuhudhuria mkutano huo (badala ya kuwa mkutano wa wazi kwa kila Mtanzania anayeishi hapa). Nimesema ni "lugha ya kidiplomasia" kwa sababu uthibitisho kwamba awali mpango wa ubalozi ulikuwa ni kama ulivyolalamikiwa jana , yaani kundi la watu kadhaa tu ndio wakutane na Waziri Mkuu, na uthibitisho huo unasikika katika audio hii ya mmoja wa maofisa wa ubalozi wetu anayetukebehi kwa kudai haki ya kukutana na Waziri Mkuu. Msikilize kwa kubonyeza play


Ni wazi kuwa laiti afisa ubalozi huyo ndio angekuwa na mamlaka ya mwisho basi ni wazi angebaki na hao watu wachache ambao awali ndio waliteuliwa kuhudhuria mkutano huo kana kwamba ni wa siri.

Badala ya kukiri kwamba ubalozi ulifanya makosa kuteua watu wachache tu, afisa huyo anaelekea kutuona kituko kwa kudai haki ya msingi ya kukutana na viongozi wetu wa kitaifa. Na badala ya kutumia fursa hiyo kuwaeleza Watanzania ratiba ya mkutano huo (tetesi zinasema utafanyika ubalozni mida ya saa 10 jioni) yeye ameamua kutunanga. Madaraka huwafanya baadhi ya wenzetu kujisahau sana.

Tukiweka kando lugha ya kidiplomasia ya Ofisa ya Waziri Mkuu na kebehi za afisa ubalozi, la muhimu ni kwamba sasa Watanzania wote wanaoishi hapa Uingereza wamepewa fursa ya kuhudhuria mkutano huo muhimu na Waziri Mkuu. Binafsi nimefarijika sana kwa sababu nilijitahidi kulipigia kelele suala hilo kwenye kundi la Whatsapp la jumuiya ya Watanzania ambayo ipo katika hatua za awali za kuundwa, japo mapokeo hayakuwa ya kuridhisha (watu wanahimiza umoja lakini walikalia kimya 'ubaguzi' uliotaka kufanywa na baadhi ya maafisa ubalozi wetu hapo London). 

"Kelele" zangu hazikutokana na mie kutopewa mwaliko, kwa sababu hata kama ningekuwa miongoni mwa watu hao takriban 40 walioalikwa bado nisingehudhuria (na leo sintohudhuria...kwa sababu zangu binafsi). Nilipiga kelele kwa maslahi ya walio wengi ambao pengine kwa namna moja au nyingine walishindwa kupiga kelele hizo wao wenyewe. Sie wengine tuna kumbi kama hii ya blogu au makala magazetini ambazo ni rahisi kupiga kelele na watawala kutusikia. Lakini si kila mtu ni blogs au mwandishi wa makala. Ni matumaini yangu kuwa 'kelele' hizi zitawahamasisha wengi kutambua kuwa 'kelele dhidi ya jambo lisilofaa' sio uchizi, kusaka umaarufu au ukorofi. Marehemu Kighoma Ali Malima aliwahi kutuusia kwamba "HAKI HAIPASWI KUOMBWA KAMA ZAWADI. HAKI HUDAIWA...KWA NGUVU IKIBIDI."

13 May 2016

Ubalozi wa Tanzania hapa Uingereza umeingia lawamani kufuatia uamuzi wake wa 'kuwabagua' baadhi ya Watanzania wanaoishi nchi hapa na kuwanyima fursa ya kuhudhuria mkutano unaotarajiwa kufanyika kesho kati ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Watanzania wanaoishi hapa.

Kwa kawaida, viongozi wa kitaifa wanapokuja hapa kutoka huko nyumbani huongea na Watanzania wanaoishi hapa, na utaratibu uliozoeleka ni kutangaza tarehe, mahala na muda wa mkutano, kinyume na hali iliyojitokeza sasa ambapo inaelezwa kuwa kuna kikundi kidogo tu cha watu walioteuliwa kukutana na Waziri Mkuu Majaliwa.

Blogu hii ilifanya jitihada za kuwasiliana na Watanzania kadhaa wa hapa, na ukiweka kando wachache waliosema kuwa wasingeenda katika mkutano huo hata kama wangealikwa, wengi wao walilaumu kitendo hicho cha ubalozi kuteua kundi la watu wachache, ambapo wala haifahamiki wachache hao waliteuliwa kwa vigezo gani.

Baadhi ya waliohojiwa na blogu hii walieleza kuwa huenda "ubalozi huo ni jipu, na umeamua kuteua kundi la watu wachache ili kuepusha uwezekano wa mtu 'asiyejulikana' kukurupuka na kumfahamisha Waziri Mkuu kuhusu malalamiko yanayouhusu ubalozi huo (kama kweli yapo)."

Kadhalika, ilielezwa kuwa kitendo cha ubalozi huo kufanya 'ubaguzi' huo kinaweza kuijiengea serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Magufuli taswira mbaya, kwamba "Waziri Mkuu amekwepa kuongea na Watanzania kwa wingi au uwazi na badala yake anakutana na kikundi kidogo cha wateule wachache."

Vilevile, kitendo hicho kinaweza kumtengenezea mazingira magumu Balozi mpya wa Tanzania nchi hapa, Dkt Asha-Rose Migiro, iwapo 'walionyimwa fursa ya kuhudhuria mkutano huo' watabaki na mtizamo kuwa "mnatutenga wakati wa ziara za viongozi wa kitaifa basi nasi twawatenga katika maisha yetu ya kila siku."

" Au ndio yale ya Bunge Dodoma kwamba halirushwi live, basi sasa hata viongozi wetu wakuu wakija hapa, badala ya kukutana nasi kwa uwazi na wingi, fursa hiyo inatolewa kwa wateule wachache tu...kwa maslahi binafsi."

Wakati ubalozi hauwezi kukwepa lawama kwa vile kimsingi wenyewe ndio wenye mamlaka ya kufanya maandalizi ya mkutano huo, haieleweki kwanini 'jumuiya kuu mbili za Watanzania hapa Uingereza,' Kikosi Kazi na Kamati ya Mpito hazijafanya jitihada zozote kupigia kelele kuhusu kasoro hiyo. Badala yake, kila upande umekuwa ukiutuhumu upande mwingine 'kutumiwa na Ubalozi kwa maslahi binafsi.'

Awali, jana kulipatikana kipande cha sauti kilichorekodi sehemu ya kipindi cha Jahazi cha Clouds FM ya huko nyumbani, ambapo waendesha kipindi walijadili kwa ufupi kuhusu kasoro hiyo ya Waziri Mkuu kuandaliwa mkutano wa kuongea na idadi ndogo tu ya Watanzania, katika utaratibu usio wazi. Bonyeza hapa chini kusikiliza
Hadi wakati blogu hii inakwenda mitamboni, hakuna taarifa yoyote rasmi kutoka kwa ubalozi au makundi makuu mawili yanayowakilisha Watanzania hapa, kuhusu kwa mfano mkutano huo utafanyika lini, wapi na muda gani.

Hata hivyo, baadhi ya waliohojiwa walionyesha matumaini kuwa inawezekana Waziri Mkuu haelewi kuhusu 'usanii unaofanywa na ubalozi,' na akipata taarifa atauagiza ubalozi huo kufanya maandalizi ya kuwezesha Watanzania wengi zaidi kuhudhuria mkutano huo.

6 May 2016

Bila shaka matokeo ya utafiti huu yatawashangaza watu wa nchi nyingine, lakini sio sie Watanzania, ambao tumebainika kuwa watu wanafiki zaidi kuliko wote duniani. Sio jambo la kushangaza kwa sababu unafiki umekuwa sehemu ya utamaduni wetu.

Na mfano mwepesi wa unafiki wetu ni kuhusu uamuzi wa serikali kuipiga marufuku video ya msanii Snura iitwayo 'Chura' ambayo ilivuka mipaka ya ustaarabu. Awali, watu wengi waliishutumu Serikali kwa kuruhusu video hiyo 'chafu' kuonyeshwa ilhali vikao vya bunge vikizuiwa kuonyeshwa 'live.' Well, japo bunge laendelea 'kufichwa,' lakini serikali imejitutumua na kipiga kufuli video ya 'Chura.'

Lakini hatua hiyo imewakera baadhi ya wenzetu. Wengine wanadai serikali ina vitu muhimu zaidi vya kufanya badala ya kufungia video. Wengine wanadai mbona kuna video chafu zaidi za 'akina Rihanna' kuliko hiyo ya Chura. Wengine wanakwenda mbali na kudai kuwa alichofanya Snura na hao mabinti wa kwenye video ni UBUNIFU. Really?????

Twende kwenye maisha yetu ya kila siku. Tuchukulie mfano vifo. Utakuta watu wanasubiri mpaka mtu afe ndio waanze kumwagia sifa, "Oh marehemu alikuwa mtu mzuri sana, oh marehemu alikuwa mwema sana...RIP...RIP..." Hii tabia ya kuwapenda watu wakifa lakini kuwachukia walipokuwa hai ni nini kama sio UNAFIKI? Angalia Marehemu Kanumba alivyoandamwa wakati wa uhai wake. Msanii aliyefanya kazi kubwa kabisa kuiinua medani ya filamu za Kitanzania aliandamwa mfululizo na hili na lile, huku watu wasio na vipaji ya kitu chochote kile wakigeuka mahakimu na majaji dhidi ya kipaji cha msanii huyo. 

Tuangalie huko mitaani tunakoishi na 'makazi yetu mapya' mitandaoni. Huko mitaani, wenzetu wenye umuhimu mkubwa kwa jamii - madaktari, manesi, walimu, nk -  hawapewi heshima kubwa kulinganisha na wanayopewa wahalifu kama wauza madawa ya kulevya au wabadhirifu serikalini. Twaita wauza unga WAZUNGU WA UNGA, na wabadhirifu twawaita MAPEDEJEE, VIBOSILE, VIGOGO, na majina mengine ya kuwatukuza, ilhali jina lao stahili ni WAHALIFU. 

Nenda mtandaoni, kwa mfano Instagram. Ukiacha wasanii wetu na watu wengine muhimu, watu maarufu zaidi katika mtandao huo kwa Tanzania ni wale wenye kuongoza makundi ya matusi, picha za utupu, majungu, na madudu kama hayo. Sio kwamba hawa 'wameroga' ili kuwa maarufu. Hapana. Umaarufu wao unatokana na Watanzani wengin kupenda vitu hivyo: picha za utupu, majungu, nk.

Angalia wakati wa uchaguzi. Wanasiasa wetu hujiweka karibu kabisa na wananchi. Si ajabu kuona mwanasiasa akiwasalimia wananchi kwa kupiga magoti 'kwa heshima' wakati anaomba kura.Subiri ashinde uchaguzi. Humsikii japo akicheka au kuzomea bungeni. Unaweza kuhisi kuwa asilimia kuwab ya wabunge wetu wanatoka majimbo ya nchi kama Uingereza au Marekani, ambazo zina matatizo machache kwa wapigakura, kwani haiingii akilini kwa mbunge ambaye jimbo lake lina matatizo lukuki awe haonekani bungeni unless kwenye kukusanya posho tu, na akitokea bungeni, si ajabu kuona amepigwa picha huku kachapa usingizi (labda alishindwa kulala kutokana na kuzongwa na mawazo kuhusu jimbo lake?)

Anyway, turudi kwenye utafiti unathibitisha tulivyobobea kwa unafiki. Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Nottingham cha hapa Uingereza waliendesha utafiti wa kupima kushamiri kwa ukiukwaji wa kanuni katika nchi 159 duniani, wakitumia takwimu za kutoka mwaka 2003 kuhusu ubadhirifu katika siasa, ukwepaji kodi na rushwa.

Twende tena mtaani. Kuna suala la ushoga ambalo taarifa zinaeleza kuwa unakua kwa kasi huko nyumbani. Juzi kuna shoga mmoja kafiwa Dar, na inaelezwa kuwa takriban kila mtu maarufu jijini hapo hakukosekana msibani. Lakini sio katika msiba huo tu, nenda Instagram halafu angalia akaunti za mashoga na idadi ya 'followers' wao. Hivi yawezekanaje kama 'ushoga sio tu ni laana bali pia ni kinyume cha sheria za Tanzania,' then shoga awe na 'followers' zaidi ya laki moja? Kwanini kila shughuli ya mastaa wetu haiwi kamili bila uwepo wa mashoga wa 'kukata viuno' kwenye shughuli hiyo?


Habari kamili kuhusu utafiti huo ipo HAPA na kuna MAKALA HII katika gazeti la kila wiki la RAIA MWEMA Toleo la wiki hii imeandika kwa kirefu kuhusu suala hilo

28 Apr 2016

MIONGONI mwa wahadhiri walionifundisha nilipokuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ni Mmarekani mmoja aliyependa sana kufundisha kwa kutumia mifano halisi. Moja ya mada ambazo zilizonigusa sana ni kuhusu ‘undugunaizesheni.’ Alieleza kuwa hata Marekani kuna tabia hiyo, ambapo mara nyingi watu wenye nyadhifa muhimu hupenda kufanya kazi na watu wanaowafahamu au hata ndugu zao. 

Na kwa vile mfumo wa serikali nchini humo sio kama wetu wa ‘ili mtu ateuliwe kuwa waziri sharti awe mbunge – awe wa kupigiwa kura na wananchi jimboni, wa viti maalumu au wa kuteuliwa na rais. Kwa wenzetu huko, rais anaweza kumteua mtu yeyote kuwa kwenye “kabineti” yake japo baadhi ya nyadhifa zinahusisha mteuliwa kuidhinishwa na mabunge ya nchi hiyo. 

Mhadhiri huyo Mmarekani alitanabaisha kuwa baadhi ya viongozi ‘huwavuta’ ndugu zao wa karibu, jamaa au marafiki sio tu kwa vile ni watu wao wa karibu bali pia kulingana na sifa walizonazo. Lakini la muhimu zaidi ni matarajio kuwa ndugu, jamaa au rafiki anaweza kuwa mtiifu sana kwa aliyemteua, hasa ikizingatiwa kuwa ‘akimwangusha, anajiangusha naye pia.’

Kwa hiyo, si kwamba suala la undugunaizesheni – kufanya upendeleo kwenye maeneo kama vile teuzi za nafasi za uongozi, halipo Afrika, au huko nyumbani pekee bali hata huku kwa hawa wenzetu wanaojigamba kwa kuzingatia taratibu na kanuni. 

Kimsingi, kumteua mtu unayemjua, alimradi ana sifa stahili, sio kuvunja taratibu na kanuni, hususan kama mchanganuo wa kumteua mtu huyo haukuwanyima watu wengine fursa ya kuteuliwa. 

Suala la ‘undugunaizesheni’ limekuwa likinijia akilini kila ninapokutana na habari kuhusu sakata la Lugumi. Lakini pengine kabla ya kuingia kwa undani kujadili sakata hilo ni vema nikaweka bayana msimamo wangu maana ‘wenye nchi’ wamekuwa wakali kweli, ukikosoa kidogo tu unaonekana kuwa wewe ni jipu au mtetezi wa majipu.

Ni kwamba namuunga mkono Rais Dk. John Magufuli, katika jitihada zake kubwa za kutumbua majipu. Hata hivyo, mara kadhaa amekuwa akitusihi Watanzania tumsaidie katika jitihada zake hizo. Na miongoni mwa njia za kumsaidia mtu ni kumshauri au hata kumkosoa pale inapobidi. Binafsi, ninaamini kuwa mtu pekee anayeweza kumaliza sakata la Lugumi ni Rais Magufuli tu, hakuna cha Bunge wala Takukuru. Ni hivi, si mfanyabiashara yeyote tu anayeweza kupewa zabuni nyeti ya kuweka mashine za kuchukua alama za vidole katika mamia ya vituo vya polisi nchini. Mtu anayepewa dhamana kubwa namna hiyo lazima awe ‘mtu fulani.’ 

Mengi yanayozungumzwa kuhusu mmiliki wa kampuni hiyo ya Lugumi yamebaki kuwa tetesi tu, lakini moja linalisikika zaidi ni madai kuwa alikuwa ‘karibu na watawala’ katika Serikali ya Awamu ya Nne. Na kwa jinsi tunavyoelewa nchi yetu ilivyokuwa inajiendesha yenyewe (on autopilot) katika awamu hiyo, hakuna miujiza hapa wala hakuna la ajabu ambalo lisingewezekana. Tuwe wakweli, nchi ilikuwa inaendeshwa kimzaha. 

Tetesi pia zinadai kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga, ambaye sio tu ndiye mwenye dhamana ya kufuatilia kuhusu sakata hilo kwa vile linaihusu wizara yake, lakini pia ni mmoja wa wanaotajwa kuhusika na ufisadi huo kupitia umiliki wa kampuni yake ya Infosys. 

‘Mazingaombwe’ yanayolizunguka sakata hili yanazidi kuendelea. Awali, ilielezwa kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi aliikwepa Kamati husika ya Bunge alipotakiwa kutoa maelezo kuhusu sakata hilo. Baadaye, tukasikia Bunge likitoa taarifa za kujikanganya, ikiwa na pamoja na kituko cha kudai kuwa kamati husika haikuomba mkataba husika bali maelezo tu (kana kwamba kuomba mkataba huo ni kuvunja sheria za nchi). 

Siku chache baadaye, ikaibuka video inayomwonyesha mtendaji mmoja wa kampuni ya Infosys akieleza kuwa Waziri Kitwanga sio mmiliki wa kampuni hiyo, na kwamba aliachana nayo kabla haijaingia mkataba huo wenye utata. 

Baadaye tena, Waziri Kitwanga mwenyewe akajitokeza kuzungumzia suala hilo akidai kuwa wakati suala hilo linatokea, yeye hakuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, na ndio maana hapendi wala hataki kuzungumzia suala hilo. 

Kauli hii inatoka kwa waziri ambaye Jeshi la Polisi lipo chini ya wizara yake. Sawa, hakuwa waziri wakati suala hilo linatokea, lakini sasa ni waziri. Kwa nini basi asipende wala kutaka kuongelea suala ambalo sio tu linaitia doa wizara yake na jeshi la polisi bali pia linaweza kuathiri usalama wa taifa letu? 

Kwa nini kama Waziri Kitwanga anajua vema majukumu yake hakushughulikia suala hilo kabla ya kuibuliwa na Kamati ya Bunge? Na hapo tunaweza kujiuliza, kwa nini Rais Magufuli hakuchukua hatua stahili dhidi ya mtendaji wake huyo, kwa staili ya kutumbua majipu? 

Sarakasi za sakata la Lugumi zimeendelea kwa Bunge kuunda timu maalumu ya kuchunguza suala hilo. Nilidhani kuwa Takukuru wangeweza kufanya kazi hiyo kwa ufanisi zaidi kwa vile sidhani kama wabunge walioteuliwa ni wataalamu wa uchunguzi wa masuala yenye dalili za ufisadi. Labda tuwape muda, huenda wanajua wanachofanya. 

Kichekesho zaidi kimeibuka muda mfupi kabla sijaandaa makala hii, ambapo Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu ameibuka na kudai kuwa kampuni ya Lugumi ilitekeleza mkataba husika, na kukanusha madai ya Kamati husika ya Bunge, na taarifa zilizosambaa mtandaoni na kwenye vyombo vya habari kuwa kampuni hiyo ilishindwa kufunga mashine za kuchukulia alama za vidole kwenye vituo 108 kama ilivyotamkwa kwenye mkataba. 

IGP Mangu alidai kushangazwa na habari hizo na kueleza kuwa kampuni ya Lugumi ilitekeleza mkataba husika kama ilivyokubaliana na serikali. 

“Siyo kweli, watu wana ugomvi wao, lakini nakueleza wazi kwamba, tembelea vituo vyote tulivyokubaliana, utakuta mashine zipo. Inawezekana zingine hazifanyi kazi kwa sababu ya kukosekana kwa intaneti,” alisema mkuu huyo wa jeshi la polisi. 

Ni akina nani hao “wenye ugomvi wao” ambao jeshi la polisi linashindwa sio tu kuwachukulia hatua bali hata kuwataja majina hasa ikizingatiwa kuwa kashfa hiyo inachafua taswira ya taasisi hiyo ya dola? 

Na kama huo ndio ukweli, kwa nini basi IGP Mangu hakujitokeza kwenye kikao cha Kamati ya Bunge iliyokutana kufuatilia suala hilo? Si angeenda tu na kuwaeleza kama anavyosema sasa kuwa suala hilo linatokana na “ugomvi” wa watu fulani? 

Lakini utetezi wake ungekuwa na maana tu kama angeweza kubainisha ni vituo vingapi na vipi ambavyo mashine hizo zilifungwa, na vingapi na vipi ambavyo mashine zinafanya kazi au hazifanyi kazi. 

Na kuhusu uwezekano wa kuwepo mashine zisizofanya kazi kutokana na kutokuwepo kwa Intaneti, basi ni uzembe wa wazi wa IGP na Waziri wake Kitwanga kwa sababu hilo ni jipu lililopaswa kutambuliwa mapema kabla ya kuibuliwa na kamati ya Bunge. Je, huduma ya Intaneti ilikatwa kwa kutolipiwa kwa vile Jeshi la Polisi lilinyimwa fungu husika au ni habari zile zile wa ‘watumishi hewa’? 

Nilianza makala hii kwa kuzungumzia suala la undugunaizesheni. Kuna hisia kuwa uteuzi wa Waziri Kitwanga ulitokana na ukaribu alionao na Rais Magufuli. Hilo sio kosa. Lakini ni jukumu la mteuliwa kuhakikisha hamwangushi aliyemteua. Na katika sakata hili la Lugumi, yayumkinika kuhisi kuwa Waziri Kitwanga anamwangusha Rais Magufuli. 

Wengi tuna imani na Dk. Magufuli, lakini ni ukweli usiofichika kuwa moja ya mitihani mikubwa inayomkabili ni pamoja na uwezekano wa kuangushwa na ‘maswahiba zake,’ watu anaowaamini lakini wasioitendea haki imani hiyo, shinikizo ndani ya chama chake CCM, na kubwa zaidi, ‘madudu’ yaliyofanyika katika awamu iliyopita hususan yale ambayo akiyagusa tu, nchi itatikisika (rejea kauli ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliyowahi kuitoa bungeni kuhusu sakata moja la ufisadi ambapo aliwaambia bayana wabunge wamsulubu tu lakini asingeweza kuongelea suala husika). 

Nimalizie makala hii kwa kumsihi Rais Magufuli kuwa uungwaji mkono anaohitaji zaidi ni kutoka kwa Watanzania wa kawaida, waliompigia kura na hata waliomnyima kura. Hawa hawatomwangusha kwa sababu wanamhitaji, na hadi sasa amewathibitishia hivyo. Baadhi ya watendaji wake wapo kwa maslahi yao binafsi, na hawa watamwangusha asipokuwa makini. Ni muhimu kwa Rais wetu kukumbuka kuwa utumbuaji majipu halisi unamtengenezea maadui lukuki, ambao wanaweza kuunganisha nguvu na kumyooshea kidole pale yanapojitokeza mambo kama haya ya kina Lugumi. 


Mpendwa Rais Magufuli, chukua hatua moja tu na sakata hili la Lugumi litamalizika (kwa maslahi ya Watanzania) 

21 Apr 2016


MAJUZI nilibandika habari mbili kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook zilizohusu ufisadi na umasikini. Habari moja ilihusu taarifa za vyombo vya habari kwamba wabunge wameshtushwa na ripoti inayoonyesha Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetumia shilingi bilioni 18 kwa ajili ya mafunzo, semina na warsha.

Niliambatanisha habari hiyo na nyingine iliyoonyesha ‘shule ya kipekee’ ambayo madarasa matatu yanalazimika kutumia jengo moja, kitu ambacho kinaweza kuiingiza shule hiyo katika rekodi ya miujiza ya Guinness.

Lengo lilikuwa kuonyesha kuwa wakati TCRA ikitumia mabilioni hayo kwa ajili ya mafunzo, semina na warsha, kuna wanafunzi wanaosoma katika mazingira magumu kwa kulazimika ‘kuchangia’ jengo la darasa.

Watumiaji wengi wa mtandao huo wa kijamii waliguswa na habari hiyo, lakini kilijitokeza kikundi kidogo kilichoitetea TCRA kwa nguvu zote. Hoja yao kuu ni kuwa majukumu ya taasisi hayo ni muhimu na teknolojia inabadilika kwa kasi, kwa hiyo ni sahihi kutumia fedha nyingi kuiwezesha taasisi hiyo kwenda na wakati.

Kilichonisikitisha zaidi ni pale wanahabari wawili wakongwe (mmoja wa gazeti hili) ‘walipomvuta’ kiongozi mmoja wa TCRA, sio kwa minajili ya kumbana kuhusu taarifa hiyo bali kuvilaumu vyombo vya habari vilivyoripoti habari hiyo, sambamba na kutetea matumizi hayo ya mabilioni kwa mafunzo, semina na warsha.

Nilikerwa mno na utetezi wa wanahabari hao kwa sababu laiti wangerejea ripoti za nyuma kuhusu matumizi ya taasisi hiyo wangetambua tukio hilo sio la mara ya kwanza. Mwaka 2011, Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) ilikagua hesabu za TCRA na kugundua madudu ya kutisha, ikiwa ni pamoja na mamlaka hiyo kusomesha nje wafanyakazi wake watatu kwa gharama ya shilingi bilioni 2.2

Na hata kama TCRA ingekuwa haijawahi kuingia matatizoni kutokana na matumizi hayo makubwa ya fedha za umma, bado isingehalalisha taasisi hiyo kutumia shilingi bilioni 18 kwa ajili ya mafunzo, semina na warsha. Sio kwa Tanzania yetu hii ambayo ni moja ya nchi masikini kabisa duniani.

Lakini kingine kilichonikera kuhusu matumizi hayo ya ‘anasa’ ya TCRA ni ukweli kwamba mamlaka hiyo kwa kiwango kikubwa imekuwa butu hususan katika eneo la udhibiti dhidi ya makosa ya mtandaoni. Taasisi hiyo ilikuwa mstari wa mbele kutetea muswada wa sheria ya makosa ya mtandao (Cybercrime Bill 2015) hadi ilipopitishwa kuwa sheria kamili.

Binafsi niliunga mkono muswada huo na hatimaye sheria husika kwa sababu, kwa upande mmoja, nilikwishawahi kuwa mhanga wa unyanyasaji mtandaoni, na kwa upande mwingine, nilikuwa nikikerwa mno na matumizi mabaya ya uhuru mtandaoni yaliyojumuisha matusi, picha za utupu na vitendo vingine visivyofaa, hususan katika mtandao wa kijamii wa Instagram.

Sasa, tangu sheria hiyo dhidi ya uhalifu wa mtandaoni ipitishwe imeishia kuungana na lundo la sheria nyingine kali lakini zisizo na ufanisi wowote. Ni kweli kwamba hoja za waliokuwa wakiipinga sheria hiyo zilikuwa na mantiki, hususan hofu kuwa itatumika vibaya, hususan uwezekano wa kutumika kisiasa zaidi kuliko kisheria.

Inatusikitisha baadhi yetu tuliotumia nguvu kubwa kuunadi muswada wa sheria hiyo ambao ulipata upinzani mkali kutoka kila kona ya Tanzania, lakini hatimaye ulifanikiwa na kuwa sheria kamili.

Majuzi, sheria hiyo imeonekana kufanya kazi ‘ghafla.’ Kijana mmoja amekamatwa na kufikishwa mahakamani chini ya ulinzi mkali kabisa, kwa kosa la kumtukana Rais John Magufuli.

Hakuna Mtanzania mwenye akili timamu anayeweza kuunga mkono kuwatusi viongozi wetu, awe Rais au mwenyekiti wa kijiji. Tatizo ni kwamba sheria hiyo dhidi ya uhalifu mtandaoni inaonekana kuwa na meno pale tu ‘wakubwa’ wanapoguswa.

Kwa yeyote anayetaka kuthibitisha jinsi gani sheria hiyo ‘ina upendeleo’ atembelee mtandao wa kijamii unaohusu picha, yaani Instagram, ambapo huko kuna kila aina ya laana: kuna ushoga wa waziwazi, kuna lundo la akaunti zinazobandika picha za utupu, kuna ‘ligi kuu’ ya matusi ambapo kadri watu wanavyoonyesha umahiri wa matusi ndivyo kadri wanavyopata wafuasi wengi.

Hali huko Instagram ni mbaya mno kiasi kwamba ni rahisi kudhani kuwa wanaofanya ‘madudu’ huko wapo katika nchi isiyo na sheria (lawless country). Kwa vile ‘wakongwe’ wa matusi wameendelea kupata umaarufu kwa kutukana pasipo kuchukuliwa hatua zozote, mtandao huo umewavutia hata watu ‘wasio na matusi’ kujaribu fursa ya kujipatia umaarufu wa bure.

Na umaarufu huo una ‘faida’ kwani akaunti zinazosheheni matusi pia hufanya matangazo ya biashara mbalimbali, kuanzia ‘video za ngono’ hadi tiba za ajabu ajabu.

Wakati fulani niliwajulisha watu wa TCRA kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter, lakini ‘bosi’ wa mamlaka hiyo aliishia kutoa ‘darasa’ refu lisilo na maana akidai kuwa ni muhimu Watanzania watambue sheria zilizoianzisha Mamlaka hiyo na shughuli zake kwa ujumla. Alidai kuwa jukumu la udhibiti wa matusi na uchafu mwingine huko Instagram ni la polisi. Kichekesho ni kwamba kesi ya huyo jamaa aliyemtukana Rais inaendeshwa kwa ushirikiano kati ya polisi na TCRA.

Kwa hiyo si kwamba TCRA haina mamlaka ya kupambana na ‘laana’ inayoendelea huko Instagram, lakini kinachoonekana ni kwamba haina muda na adha zinazowakumba wananchi wa kawaida. Uvunjifu huo wa sheria ukimgusa kiongozi, basi mamlaka hiyo na sheria dhidi ya uhalifu wa mtandaoni vinafufuka ghafla. Hii sio sawa hata kidogo.

Nimalizie makala hii kwa kuisihi serikali ifanye jitihada za makusudi kukomesha hali mbaya inayoendelea katika mtandao huo wa kijamii. Haihitajiki kukamata kila mhusika lakini vinara wachache tu wakitiwa nguvuni itasaidia kufikisha ujumbe kwa wenzao.

Suala hili linaweza kuihusu wizara yenye dhamana na masuala ya afya pia, kwa sababu mtandao huo umegeuka kuwa duka lisilo rasmi la dawa za aina mbalimbali, suala ambalo linaziweka afya za Watanzania shakani.

Penye nia pana njia, pasipo na nia pana kisingizio. 

8 Apr 2016

MOJA ya masuala yanayotawala anga za habari na mijadala mbalimbali mtandaoni ni uamuzi wa Bodi ya Taasisi ya Changamoto ya Milenia (Millennium Challenge Corporation - MCC) ya Marekani kusitisha misaada kwa Tanzania.
Sababu kuu mbili zilizotolewa na bodi hiyo kuhusu uamuzi huo ni marudio ya uchaguzi huko Zanzibar Machi 20, mwaka huu, ambao licha ya kususiwa na chama kikuu cha upinzani cha CUF, ulilalamikiwa kwa kiasi kikubwa na baadhi ya nchi wahisani, ikiwa ni pamoja na Marekani.

Sababu ya pili, kwa mujibu wa bodi hiyo, ni uamuzi wa Serikali ya Tanzania kupitisha Sheria Uhalifu wa Mtandaoni (Cybercrime Act) ya mwaka 2015 licha ya upinzani mkali dhidi ya muswada wa sheria hiyo, iliyotafsiriwa kuwa imelenga kukandamiza uhuru wa habari na haki za binadamu.

Kabla ya kuingia katika uchambuzi huu kiundani, nieleze mtazamo wangu kuhusu sababu hizo mbili zilizotolewa na Bodi ya MCC. Kwanza, kwa mtazamo wangu, suala la marudio ya uchaguzi wa Zanzibar ni mzaha wa kidemokrasia. Haihitaji uelewa mkubwa wa siasa za Zanzibar kufahamu kuwa kuna ‘sheria isiyo rasmi’ kuwa ‘kamwe CUF hawapaswi kutawala Zanzibar.’

Bila kuuma maneno, hiyo ndiyo sababu pekee ya kufutwa kwa uchaguzi wa awali (ambao inadaiwa mgombea wa CUF, Seif Shariff Hamad, alishinda) na kuamriwa uchaguzi huo urudiwe huku CCM ikiwekeza nguvu zake zote kuhakikisha inashinda. Hata kama CUF wasingesusia uchaguzi huo, bado CCM wangeshinda kwa sababu ‘ni lazima iwe hivyo,’ kwa ‘kanuni’ zao.

Je, MCC ipo sahihi kutumia kigezo cha Zanzibar kusitisha misaada yao? Kwa upande mmoja, wapo sahihi. Kwa sababu, hata katika uhusiano wetu wa kawaida tu kibinadamu, anayekupa msaada anapata ruhusa pia ya ‘kukutawala’ kwa kukupa masharti ambayo ukiyakiuka, yanaweza kuathiri uhusiano kati ya mtoa msaada na mpokea msaada. Miongoni mwa masharti ya MCC ni pamoja na masuala ya demokrasia, na haihitaji kukuna kichwa sana kubaini kuwa marejeo ya uchaguzi wa Zanzibar, ambayo binafsi ninayaona kuwa ni mzaha wa kidemokrasia, yamewapa MCC ‘kisingizio chepesi’ hata kama hawangekuwa na sababu nyingine.

Mgogoro wa muda mrefu wa kisiasa huko Zanzibar ni zaidi ya jipu. Ni kansa ambayo imeshachafua sura ya Tanzania huko nyuma ambapo kwa mara ya kwanza tulizalisha wakimbizi baada ya vurugu za Uchaguzi mkuu mwaka wa 2000.

Ni kansa ambayo sasa imewapa MCC kisingizio cha kutunyima misaada yao. Kwa bahati mbaya au makusudi, hakuna utashi wa kisiasa wa kusaka ufumbuzi wa kudumu wa mgogoro huo. Kila kiongozi wa CCM, kwa upande wa Bara, anaogopa suala hilo kwa kuhofia kuvunjikiwa na Muungano mikononi mwake.

Baadhi ya wanasiasa wa Zanzibar sio tu wanaufahamu udhaifu huo bali pia wanautumia vema. Wanaendesha siasa za chuki na uhasama watakavyo wakifahamu kuwa hakuna mwana-CCM wa Bara mwenye jeuri ya kuwaingilia.

Sina hakika Zanzibar itaathirika vipi kwa uamuzi wa MCC kukata misaada, lakini kinachowapa kiburi viongozi wa huko ni kwamba ‘Tanganyika’ haina jeuri ya kuisusa Zanzibar au kuinyooshea kidole katika mwendelezo wa siasa za chuki na ubaguzi.

Lakini kwa upande wa pili, hao MCC ni wanafiki tu. Huhitaji kuwa na uelewa mkubwa wa siasa za kimataifa kutambua unafiki wa Marekani linapokuja suala la demokrasia. Nchi hiyo ni mshirika mkubwa wa tawala za kidikteta kama vile huko Misri, Saudi Arabia na kwingineko. Sawa, labda Zanzibar wamefanya mzaha wa kidemokrasia lakini vipi kuhusu demokrasia isiyopo kabisa huko Saudi? Jibu rahisi ni kwamba Zanzibar na Tanzania sio muhimu sana kwa Marekani ilhali taifa hilo linazitegemea mno tawala za kibabe za nchi kama Misri au Saudi, hususan katika masuala ya ushushushu au mapambano dhidi ya ugaidi wa kimataifa.

Kuhusu suala la Sheria ya Uhalifu wa Mtandao, hapa kumesheheni unafiki, na upo wa aina mbili. Kwanza, Wamarekani na pili ni Watanzania wenyewe. Binafsi ni mfuatiliaji wa karibu wa masuala ya usalama mtandaoni, ambao kwa namna moja au nyingine unahusiana na hiyo masuala ya Cybercrime Act.
Kwa kifupi tu, Marekani ina sheria kandamizi mno dhidi ya uhuru wa raia mtandaoni. Naamini umekwishasikia kuhusu jamaa anayeitwa Edward Snowden. Huyu bwana alikuwa mtumishi katika Shirika la Kijasusi la Marekani linalohusika na kunasa mawasiliano mbalimbali (NSA – National Security Agency) na baadaye nafsi yake ilimsuta, akaamua ‘kuingia mitini’ na kumwaga siri lukuki kuhusu jinsi NSA inavyohujumu haki za raia kimawasiliano. Hawa jamaa wamekuwa wakinasa mawasiliano ya takriban kila mtu, wakishirikiana kwa karibu na mashushushu wenzao wa hapa Uingereza, GCHQ, taasisi ya kishushushu inayohusika na kunasa mawasiliano.
Lakini hata tukiweka kando suala la NSA kunasa mawasiliano mbalimbali (waliwahi kuzua kasheshe kubwa baada ya mashushushu wa Ujerumani kubaini kuwa NSA walikuwa wakinasa kwa siri mawasiliano ya Kansela Angela Markel hadi waliposhtukiwa), mashambulizi ya kigaidi nchini humo mwaka 2001 yalisababisha kuundwa kwa sheria kali kabisa dhidi ya uhuru wa habari na haki za kibinadamu kwa kisingizio cha usalama wa taifa. Kwa hiyo, kwa kifupi, ni uhuni tu wa Marekani kudai Sheria ya Makosa ya Mtandaoni inakiuka uhuru wa Watanzania. Sheria zao za wazi na za kificho ni mbaya mara milioni zaidi yetu.

Hata hivyo, katika suala hili la Cybercrime Act, tuna wanafiki kadhaa huko nyumbani. Kwa kumbukumbu tu, nilikuwa mtetezi mkubwa wa muswada uliozaa sheria hiyo, yaani Cybercrime Bill, na niliunga mkono kwa nguvu zote jitihada za aliyekuwa Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, kuhusu muswada huo.

Hata hivyo, baadhi ya watu ambao sasa wanailaumu Marekani na wafadhili wengine kuhusu suala la Tanzania kukatiwa misaada, walikuwa mstari wa mbele wakati huo kuziomba nchi wahisani ziingilie kati kuibana serikali ili muswada huo usipitishwe kuwa sheria. Sasa kama uamuzi huo wa Marekani umechangiwa na ‘kelele’ zao hizo, kwa nini leo wanalalamika?

Ninakerwa kuona kundi la wanafiki hawa likiilaumu MCC au Marekani au nchi nyingine wahisani kuhusu suala la kutukatia misaada, kwa sababu wao walikuwa mstari wa mbele kuhamasisha nchi wahisani zichukue hatua, na ‘hatua maarufu’ ya wahisani huwa ni kukata misaada. Badala ya kulalamika, wanafiki hawa wanapaswa kufanya sherehe maana dua zao zimetimia.

Sasa niangalie upande wa athari za uamuzi huo wa MCC kukata misaada. Tuwe wakweli, kwa watu masikini kama sisi, hatua yoyote ile ya kutupunguzia msaada wa aina yoyote ile itatuathiri. Hilo halihitaji uelewa wa jinsi gani misaada inavyofanya kazi au jinsi gani nchi yetu ilivyo “mtegemezi mzoefu wa misaada”.

Tatizo kubwa hapa kuhusu kukatiwa misaada kutatuathiri au hakutatuathiri ni tofauti zetu za kiitikadi. Kwa kiasi kikubwa, suala hilo linaangaliwa katika lensi ya u-CCM na u-Ukawa /Upinzani. Kwa wana-CCM, ni mwendo wa ‘kiburi’ kwenda mbele, kwamba “waende tu na misaada yao,” au “hela yenyewe ilikuwa ya mradi wa kifisadi wa Symbion,” mara “ah misaada gani hiyo yenye masharti kibao.” Wanamhadaa nani? Kama misaada hiyo haikuwa na umuhimu, kwa nini basi tuliiomba?

Kwa upande wa wana-Ukawa /Wapinzani, bila kujali kuwa wao kama Watanzania ni waathirika watarajiwa wa uamuzi huo wa nchi yetu kukatiwa misaada, wanakenua meno yote 32 kwa furaha, huku wakiwazodoa wenzao wa CCM kwa vijembe kama “...ndio matunda ya ubabe wenu huko Zanzibar, tuone sasa…” au “mtaisoma namba” au “mtakula jeuri yenu…”
Ulemavu huu wa kifikra unaosababishwa na kuliangalia suala la kiuchumi kwa mtizamo fyongo wa itikadi za kisiasa. Naam, suala la Zanzibar ni la kisiasa, lakini athari za uamuzi wa Marekani (MCC) wahisani ni la kiuchumi.


Mimi si mchumi lakini naelewa fika kuwa uchumi wetu umekuwa tegemezi tangu tupate uhuru. Kabla ya kuipa kisogo siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, tulikuwa tukipata misaada kutoka kwa marafiki zetu wa mrengo wa Ukomunisti. Baada ya kuzika Ujamaa, tumekuwa kama puto linaloyumbishwa na upepo, tupo radhi kumpigia magoti yeyote anayeweza kutusaidia. Kimsingi, tuna ombwe la kiitikadi: majukwaani, CCM wanasema sisi ni Wajamaa, vitendo vyetu havipo kwenye Ujamaa wala Ubepari, tupo tupo tu. Huo ndio ukweli mchungu kuhusu ubabaishaji wetu.

Kwa hiyo, tuache kudanganyana kuwa kukatiwa misaada hakutotuathiri. Huko ni kujipa jeuri tu. Tunachoweza kukubaliana ni kwamba suala hilo limekwishakutokea, tumekwishakatiwa misaada, na si ajabu wahisani wengine wakaamua kufuata mkumbo na kufanya hivyo pia.

Jukumu letu kubwa kwa sasa sio kuendelea kunyoosheana vidole bali tuwe kitu kimoja kama taifa bila kujali nani hasa aliyetusababishia tatizo hili. Ni tatizo la Watanzania wote bila kujali itikadi zao. Uamuzi wa wahisani kukata misaada utawaathiri wana-CCM wanaodai hautowaathiri kama ambavyo utawaathiri wana-CUF au Chadema wanaokenua meno yote 32 kufurahia hatua hiyo. Na utatuathiri (angalau kisaikolojia) hata sisi ambao itikadi yetu pekee ni Tanzania yetu. Huo ni ukweli usiopingika (we are all in this together).

Kuna mambo mawili ya kupigiwa mstari. Kwanza, kwa miaka mingi tumekuwa tukiishi kifahari mno kuliko uwezo wetu. Na kimsingi, uwezo wetu duni haukupaswa kuwepo kwani sisi si masikini hata kidogo. Tuna kila aina ya utajiri lakini kuna majambazi walioigeuza Tanzania yetu kuwa kitu cha kufisadiwa kila kukicha. Kila mwenye uelewa anafahamu kilichojiri katika takriban miaka 30 iliyopita. Tanzania yetu ilikuwa shamba la bibi, watu wanafisadi wapendavyo kiasi kwamba kuwa na uchungu na nchi ilionekana kama uwendawazimu.

Kwa bahati nzuri, Mwenyezi Mungu amesikia kilio cha baadhi yetu na sasa tumempata Rais, Dk John Magufuli, ambaye anaonekana amedhamiria kurekebisha mwenendo wa mambo. Kikwazo chetu kikubwa kilikuwa ufisadi, lakini sasa Magufuli ameamua kuvalia njuga kupambana na ufisadi kwa nguvu zote. Mwanzo ni mgumu lakini angalau dalili za mafanikio zimeanza kujionyesha. Tumuunge mkono, tuchukie ufisadi, tuongeze uzalendo, tuikwamue Tanzania yetu, tujikwamue nasi wenyewe, tuache kutafuta njia za mkato za mafanikio, tufanye kazi, tuache majungu na kusaka sifa za kijinga mitandaoni, tuwajibike.
Tunahitaji kujifunga mikanda. Haiwezekani wafadhili wetu waishi kimasikini ilhali sisi wafadhiliwa tunaishi kama matajiri. Viongozi wetu waache kuchuana na wauza unga kushindana jinsi ya kuishi kitajiri, wawabane wauza unga hao, majangili na maharamia wengine ili tuiokoe Tanzania yetu.

Je, tunaweza kujitegemea? Naam, lakini tusidanganyane kuwa tunaweza kufanya hivyo ghafla. Tukumbuke, mtoto hazaliwi na kisha akatembea. Tumekuwa wategemezi mno wa misaada kiasi kwamba tumesahau kuwa tunapaswa kujitegemea. Tunahitaji kuchukua na kukubali uamuzi mgumu wa kutuwezesha kujitegemea.

Jambo jingine, kwa hisia zangu, japo suala la Zanzibar na Cybercrime Act zinatajwa kama sababu za uamuzi wa kutunyima misaada, ninashawishika kuamini kuwa baadhi ya nchi wahisani hawapendezwi na kasi ya Rais Magufuli kuziba mianya ambayo kimsingi licha ya kuwanufaisha mafisadi wa ndani, ilikuwa pia inanufaisha taasisi za kifisadi za kimataifa

Wengi wa majambazi waliokuwa wakitupora fedha zetu walikuwa hawahifadhi fedha zao katika benki zetu bali zilizopo katika nchi za wahisani hao. Wanaweza kudhani huu ni utani mbaya, lakini jiulize, je kama unamfadhili mtu pesa za kumsaidia yeye na familia yake, lakini anatumia fedha hizo kufanya matumizi ya anasa, kwa nini usichukue hatua?
Mfano huo unamaanisha hivi: kwa nini wahisani wetu walionekana kutokerwa na jinsi pesa walizokuwa wanatupatia zikifisadiwa kila kukicha lakini wakaendelea kutumwagia misaada? Na kwa nini sasa, tumempata Magufuli ambaye amepania kwa dhati kupambana na ufisadi, wahisani wanaanza kuvaa sura ya ubabaishaji.

Kuna tunaodhani kuwa hao wahisani wanataka tuendelee kuwa wategemezi wao milele. Kwa upande mmoja utegemezi wetu unawapa uhuru wa kukwapua kila rasilimali tuliyonayo, na kwa upande mwingine, wananeemesha taasisi zao za fedha kwa vile mafisadi wetu wa ndani wanahifadhi fedha zao kwenye taasisi hizo.


Mwisho, tuache porojo, tuache unafiki, tuwe kitu kimoja, athari za kukatiwa misaada zipo, tukishikamana tutaweza kukabiliana nazo japo mwanzoni itakuwa ngumu. Yawezekana uamuzi huo wa Wamarekani ukawa ‘blessing in disguise’ kwa maana ya kutupa ‘wake-up call’ tuanze kujitegemea kwa lazima badala ya kutembeza bakuli letu huko na kule, kisha kile kidogo kinachopatikana kikaishia kwenye ujenzi wa mahekalu ya mafisadi, ongezeko la magari yao ya kifahari, na kutanua ukubwa wa nyumba ndogo zao.

Mungu ibariki Tanzania

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.