24 Jul 2016


Jana Julai 23, 2016 Rais Dokta John Magufuli alichaguliwa kwa asilimia 100 kuwa Mwenyekiti mpya wa Taifa wa chama tawala CCM, na mtangulizi wake, Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete, kung'atuka rasmi. Ufuatao ni uchambuzi wa kina kuhusu mabadiliko hayo ya uongozi wa juu kabisa wa chama hicho kikongwe, hasa fursa na changamoto kwa Mwenyekiti mpya Magufuli. Karibuni
Check this out on Chirbit


Naomba kuwasilisha ujumbe husika kama nilivyotumiwa. Ukishasoma, usikose kutahadharisha na mwenzako. Kwa kufanya hivyo sio tu itaepusha watu kuingia kwenye mtego wa tapeli huyo lakini pia itasaidia kuwezesha atiwe nguvuni


23 Jul 2016

Munich-locator-600px
Ujerumani imekumbwa na janga jingine baada ya lile la siku nne ambapo kijana mmoja, mhamiaji kutoka Afghanistan, aliwashambulia abiria kwenye treni kwa kutumia shoka na kujeruhi watu wanne. 

Kijana huyo, Riaz Khan Ahmadzai (au Muhammad Riyad, kwa jina jingine), aliyekuwa na umri wa miaka 17, na aliyewasili Ujerumani mwaka jana kama mtoto anayesaka ukimbizi, aliuawa kwa kupigwa risasi na polisi.
Katika tukio lililotokea jana, watu 10 wameuawa hadi wakati ninaandika makala hii na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya shambulio la risasi katika mgawaha wa McDonald kwenye kitongoji cha biashara katika jiji la Munich.
Awali, ilikuwa haifahamiki idadi kamili ya waliofanya shambulio hilo japo taarifa za awali zilitaja wahusika kuwa watatu. Licha ya shambulio hilo kwenye mgahawa huo ulio kwenye duka kubwa (mall), ilidaiwa kuwa milio ya risasi ilisikika pia maeneo mengine ya Munich.
Kulikuwa kuna theories tatu - mbili zenye uzito na moja yenye uzito mdogo kiasi - kuhusu nani hasa alihusika na tukio hilo. Theories hizo ni kama ifuatavyo.

Theory ya kwanza: shambulio hilo ni kazi ya magaidi, sanasana ISIS

Imekuwa ni kawaida sasa kwa nchi za Magharibi kwamba kunapotokea tukio lolote la kigaidi, hisia za kwanza ni usual suspects, yaani kama sio ISIS basi ni Al-Qaeda. Haya ndio makundi mawili ya kigaidi yanayoziandama mno nchi za Magharibi. Na kwa sasa, ISIS ndio inaongoza kwa mfululizo wa mashambulizi ilhali Al-Qaeda 'imekuwa kimya' kitambo sasa.

Hisia kwamba wahusika katika shambulio hilo walikuwa ISIS (au Al-Qaeda) ni, kwanza, tukio la majuzi la huyo kijana aliyefanya shambuli kwa kutumia shoka ambalo nimelieleza mwanzoni mwa makala hii. 

Pili, ni ukweli kwamba ISIS imekuwa ikifanya jitihada kubwa kuishambulia Ujerumani na nchi nyingine za Magharibi. Kama ilivyo kwa Uingereza, wataalamu wa usalama wa kimataifa wanaeleza kuwa shambulio la ISIS kwa Ujerumani sio suala la "iwapo litatokea" bali "lini litatokea." 

Tatu, ISIS walishangilia tukio hilo la Munich, katika akaunti yao ya Telegram, kama inavyoonyesha pichani chini
ISIS rejoice in Munich attack

Hata hivyo, theory hii kuwa wahusika ni ISIS ilikabiliwa na 'pungufu' hili: ilielezwa kuwa moja ya maiti hizo 9 ni ya mmoja wa wahusika wa tukio hilo. Hiyo ilikuwa na maana gani? Ni kwamba, magaidi wa ISIS na wenzao wenye mrengo kama wao, hupania kuuawa na sio kujiuwa. Wanaamini kuwa kwa kuuawa - badala ya kujiuwa - wanakuwa wamejitoa mhanga kwa ajili ya imani yao. Kama sio kuuawa kwa kupigwa risasi basi kifo kitokane na kujilipua kwa bomu la kujitoa mhanga.

Lakini kifo cha mtu huyo anayedhaniwa kuwa mmoja wa wahusika wa shambulio hilo hakikutokana na kupigwa risasi na polisi au yeye kujilipua. Sababu pekee ya kifo inaweza kuwa alijipiga risasi mwenyewe, mbinu ambayo sio chaguo la magaidi wa ISIS na wenzao.

Theory ya pili: Wahusika walikuwa kikundi cha wabaguzi wa rangi wenye msimamo mkali dhidi ya Waislam, wakimbizi na raia wa kigeni

Jana ilikuwa ni kumbukumbu ya miaka mitano ya shambulio kubwa la kigaidi lililofanyika huko Utoya, nchini Norway, Julai 22 mwaka 2011 ambapo mbaguzi wa rangi mwenye msimamo mkali, Anders Behring Breivik, aliwapiga risasi na kuwauwa watu 77.
Wachunguzi wa masuala ya usalama walieleza kuwa kulikuwa na uwezekano kwamba shambulio hilo la Munich lilifanywa na kikundi cha kibaguzi chenye mrengo mkali kama maadhimisho ya tukio hilo la Norway, na pengine kama kumwenzi Breivik ambaye ni 'shujaa' kwa vikundi vya wabaguzi wa rangi.
Kingine kilichoipa uzito theory hii ni ukweli kwamba mmoja wa wahusika wa shambulio hilo alisikika akisema kuwa yeye ni Mjerumani asilia, na akawatukana wahamiaji nchini humo. Wataalamu wa lafidhi walieleza kuwa sio rahisi kwa mtu asiye mzaliwa wa Ujerumani kuwa na lafidhi iliyotumiwa na mtu huyo.

Theory ya tatu, wahusika sio watatu bali mtu mmoja tu aliyekuwa anayesumbuliwa na matatizo ya akili

Katika kile kinachotafsiriwa kama unafiki, 'mzungu' akiuwa watu kadhaa, maelezo yatakuwa "mtu mwenye matatizo ya akili." Uthibitisho wa hivi karibuni ni maelezo kuhusu mtu aliyemuuwa mbunge Jo Cox wa hapa Uingereza hivi karibuni. Ilielezwa kuwa muuaji huyo "alikuwa na historia ya matatizo ya akili."
Laiti angekuwa Muislam au Mwarabu basi maelezo hapo yangeelemea zaidi kuhusu Uislam wake, na wabaguzi wasingekawia kudakia hoja kuwa dini hiyo ni tishio kwa ustawi wa mataifa ya Magharibi.

Ilielezwa kuwa mtu huyo niliyemwelezea katika theory ya pili, licha ya kudai yeye ni Mjerumani na kuwatukana wahamiaji, pia alieleza kuwa ni mgonjwa wa akili na yupo kwenye matibabu.

Taarifa rasmi ya polisi kuhusu mhusika

Baadaye, polisi wa Munich waliitisha mkutano na waandishi wa habari na kueleza kuwa uchunguzi wao umethibitisha kwamba aliyefanya shambulio hilo ni kijana mwenye umri wa miaka 18, Mjerumani mwenye asili ya Aljeria, na alihamia nchini humo miaka miwili iliyopita.

Kama taarifa hiyo ya polisi haina mapungufu, ukweli kwamba siku 4 zilizopita mhamiaji kutoka Afghanistan alifanya shambulio la kigaidi kwa kutumia shoka na kujeruhi watu wanne kabla ya kuuawa, na jana mhamiaji mwingine kutoka Iran, mwenye umri wa mwaka mmoja tu zaidi ya huyo wa majuzi, naye amefanyanya shambulizi na kuuwa watu 10 (hadi wakati naandika makala hii), chuki dhidi ya wageni inaweza kuongezeka maradufu.

Ikumbukwe kuwa Ujerumani imekuwa ikipokea idadi kubwa ya wakambizi miongoni mwa nchi za Magharibi. Licha ya upinzani mkali, hususan kutoka kwa makundi ya kibaguzi yenye mrengo mkali, Kansela Angela Markel amekuwa mstari wa mbele sio tu kuhamasisha nchi za Magharibi zipokee wakimbizi, bali pia ameruhusu idadi kubwa kabisa ya wakimbizi kuingia na kuishi katika nchi hiyo.

Kama kuna 'nafuu' kidogo, basi ni hiyo asili yake ya Iran, nchi ambayo ni nadra kuzalisha magaidi. Pia ukweli kuwa alijiuawa mwenyewe inaweza kuendana na hiyo theory ya pili hapo juu kuwa magaidi wa ISIS na wenzao huwa hawajiuwi kwa kujipiga risasi, huuawa kwa kupigwa risasi au kujilipua wenyewe, na kwa kufanya hivyo huwa wamejitoa mhanga kwa ajili ya imani yao.

Hata hivyo, huo u-Iran wake unaweza kuwapa nguvu wabaguzi wa rangi kuendeleza upinzani wao dhidi ya serikali ya Kansela Markel kuruhusu ujio wa wakimbizi nchini humo, ambao wanatizamwa kama 'magaidi watarajiwa.'

Endelea kutembelea blogu hii kwa uchambuzi wa kina wa mada mbalimbali kama hii inayohusu masuala ya intelijensia, na nyinginezo.







21 Jul 2016


Julai 15 mwaka huu, serikali ya Uturuki ilinusurika kupinduliwa katika jaribio la mapinduzi liliyodumu kwa chini ya masaa 12. Tayari watu zaidi ya 60,000 aidha wamekamatwa, wamesimamishwa au wamefukuzwa kazi kwa tuhuma za kuhusiana na jaribio hilo lililofeli.

Jaribio la mapinduzi lilitokeje?

Awali daraja kuu katika mkondo wa Bosphorous liliwekewa vizuizi na kundi la wanajeshi wakitumia vifaru, na wakati huohuo ndege za kivita zilikuwa zikiruka katika anga la mji mkuu wa nchi hiyo, Ankara, huku milio ya bunduki ikisikika sehemu mbalimbali.

Baadaye, Waziri Mkuu Binali Yildrim, alitangaza kwamba kulikuwa na jaribio linaloendelea la kuipindua serikali.

Muda mfupi baadaye, kikundi cha wanajeshi kilitangaza kupitia radio ya taifa kuwa jeshi limechukua madaraka kutoka kwa Rais Recep Tayyip Erdogan ili kulinda demokrasia.

Kisha likafuatia tangazo la hali ya hatari (curfew), sheria za kijeshi (marshall law) na maandalizi ya katiba mpya.

Rais Erdogan ambaye alikuwa likizoni alifanikiwa kuwasihi wananchi waingie mtaani kupinga mapinduzi hayo. Alitoa wito huo kwa kutumia app ya Facetime ya iPhone na kuonyeshwa live kama inavyoonekana pichani chini.




Katika usiku huo, vituo vya televisheni vilivamiwa na wanajeshi, milipuko kadhaa ilisikika sehemu mbalimbali za Ankara na Istanbul, abaadhi ya waandamaji walishambuliwa na wanajeshi na kuuawa au kujeruhiwa, jengo la bunge na ikulu zilishambuliwa, helikopta ya jeshi ilitunguliwa, na mnadhimu wa jeshi kuchukuliwa mateka.


Jaribio la mapinduzi liliishaje?

Ili jaribio hilo la mapinduzi lifanikiwe, wahusika walihitaji sapoti ya sehemu kubwa zaidi ya jeshi badala ya kikundi kidogo tu, na sapoti ya wananchi mtaani. Yote mawili hayakutokea. Kana kwamba hiyo haikutosha, vyama vya upinzani navyo vilijitokeza kulaani jaribio hilo.

Kufikia Jumamosi asubuhi -  chini ya masaa 12 baada ya tangazo la mapinduzi - baadhi ya wanajeshi walioshiriki katika jaribio hilo walianza kujisalimisha.

Soldiers involved in the coup surrender on the bridge over the Bosphorus in Istanbul (16 July)



Kadhalika, polisi walifanikiwa kurejesha sehemu mbalimbali muhimu mikononi mwa dola kutoka kwa waasi. Kufikia Jumamosi mchana, mitaa ilikuwa imesheheni wananchi wakilaani jaribio hilo la mapinduzi na kuunga mkono serikali ya Erdogan.


Kwanini jaribio hili la mapinduzi lilifeli?

Kwanza, jaribio hilo halikuwa na sapoti ya kutosha ndani ya jeshi la nchi hiyo. Kilichoonekana ni kikundi kidogo tu cha wanajeshi kilichojumisha wanajeshi wapya, pasipo uwepo wa viongozi waandamizi wa jeshi la nchi hiyo.

Pili, jaribio hilo halikuwa na spaoti ya wananchi. Mara baada ya Rais Erdogan kuwataka wananchi waingie mtaani kupambana na jaribio hilo, ikageuka kuwa mapambano kati ya wanajeshi na wananchi, kitu ambacho kwa vyovyote kingeathiri 'uhalali' wa mapinduzi hayo.

Tatu, wahusika wa jaribio hilo la mapinduzi kushindwa kudhibiti njia zote za mawasiliano kati ya viongozi wakuu wa serikali na wananchi, kwa mfano vituo vya televisheni na redio. Mwelekeo wa jaribio hilo la mapinduzi ulibadilika kwa kiasi kikubwa baada ya Rais Erdogan kuonekana kwenye kituo kimoja cha televisheni akiwataka wananchi waingie mtaani.

Nne, Uturuki ni taifa lenye asilimia kubwa ya watu wenye kipato cha kati na cha juu. Ni vigumu sana kwa taifa lenye wananchi wa aina hii kuunga mkono mapinduzi. Ni rahisi kwa mapinduzi kuungwa mkono katika nchi masikini ambapo mara nyingi 'chuki' dhidi ya serikali huwa kubwa.

Jaribio hilo la mapinduzi lilionekana kufeli bayana baada ya Rais Erdogan kurejea Instanbul na kuhutubia katika uwanja wa ndege wa Ataturk.

Arriving at Ataturk airport in Istanbul, President Erdogan was greeted by hundreds of supporters


Hali ikoje sasa?

Idadi halisi ya waliokamatwa, kusimamishwa kazi au kutimuliwa kazi na hatua nyingine zilizochukuliwa ni kama ifuatavyo

  • Watumishi 300 wa Wizara ya madini wametimuliwa.
  • Watumishi 184 wa Wizara ya Forodha wametimuliwa.
  • Waandamizi wanane wa Bunge wameondolewa.
  • Waturuki wote wanapaswa kuwa na nyaraka za ziada wanapofanya safari nje ya nchi.
  • Watumishi 86 wa taasisi ya udhibiti na usimamizi wa mabenki wametimuliwa.
  • Watumishi 51 wa Soko la Hisa wametimuliwa.
  • Majaji 140 wa Mahakama Kuu wametumiwa hati za kukamatwa.
  • Watumishi 15,200 wa Wizara ya Elimu wametimuliwa.
  • Vyombo vya habari 24 vimefutiwa hati za usajili.
  • Watu 429 wa taasisi ya umma ya masuala ya dini (Diyanet) wameondolewa.
  • Walimu binafsi 21,000 wamefutiwa leseni zao.
  • Watumishi 393 w Wizara ya Familia na Sera za Jamii wametimuliwa.
  • Watumishi 257 katika ofisi ya Waziri Mkuu wametimuliwa.
  • Wakuu (deans) 1577 wa vyuo vikuu wametakiwa kujiuzulu.
  • Magavana 33 wametimuliwa.
  •  Watumishi 9,000 wa Wizara ya Mambo ya Ndani wametimuliwa.
  • Maafisa Usalama wa Taifa 180 wamesimamishwa kazi
  • Majaji 2,745wametimuliwa.
  • Watumishi wa umma milioni tatu wamezuwia kwenda likizo.
  • Mjadala kuhusu kurejeshwa kwa hukumu ya kifo umeanza, na Rais Erdogan ametanabaisha kuwa pindi bunge likiridhia kurejeshwa kwa hukumu hiyo basi wote waliohusika na jaribio hilo la mapinduzi watahukumiwa kifo.
  • Maafisa 1,500 wa Wizara ya Fedha wametimuliwa.
  • Majenerali na maadmirali 85 ni miongoni mwa maelfu ya wanajeshi waliokwishakamatwa. Pia zaidi ya polisi 8,000 wamekamatwa, wametimuliwa au wamesismamishwa kazi.
Mashushushu wa Uturuki walikuwa wapi wakati mapinduzi hayo ynaandaliwa na hadi yakakaribia kufanikiwa?

Makala hii inahusu hasa swali hilo hapo juu, kwa moja ya kazi kuu za Idara ya Usalama ya taifa lolote lile ni kutambua, kuzuwia na kudhibiti matishio ya usalama wa taifa, ikiwa ni pamoja na mapinduzi. Sasa wakati serikali ya Uturuki ikionekana kuchukua hatua kali dhidi ya watumishi mbalimbali wa umma ikiwa ni pamoja na kuwakamata, kuwasimamisha kazi na kuwatimua, ni idadi ndogo tu ya maafisa usalama wa taifa waliochukuliwa hatua (angalia juu nilipoandika kwa maandishi mekundu).

Lakini swali kubwa zaidi ni kwamba je Idara ya Usalama wa Taifa ya nchi hiyo, MIT, haikufahamu kuhusu mipango ya kufanyika kwa mapinduzi hayo, na kwanini?

Turudi nyuma kidogo. Oktoba mwaka jana, mhadhiri wa chuo kikuu cha Haifa , Israel, Norman Bailey, alieleza kwa uhakika kuwa jeshi la Uturuki linaweza kuchukua madaraka ya nchi hiyo iwapo litaona nchi inaelekea kusikofaa.

Kadhalika, Machi mwaka huu, wachunguzi wa masuala ya usalama wa Russia walionya kuwa jeshi la Uturuki lilikuwa likijiimarisha kisiasa, na hivyo kujenga msingi wa mapinduzi.

Baadaye mwezi huohuo, Michael Rubin wa taasisi ya American Enterprise, aliuliza "je Uturuki itakumbwa na mapinduzi?" na akajibu kwamba "isiwe jambo la kushangaza iwapo jeshi la Uturuki litajaribu kumng'oa (Rais) Erdogan na kuwatupa jela watu wake wa karibu."

Machi 30, jarida linaloheshimika la Foreign Affairs lilichapisha makala ya Gonul Tol, Mkurugenzi mwanzilishi wa Taasisi ya Mashariki ya Kati, kituo cha stadi za Uturuki, alieleza kuwa nchi hiyo ilikuwa ikikabiliwa na mapinduzi.

Kadhalika, mwanzoni mwa mwezi huu, Joseph Fitsanakis wa tovuti ya IntelNews alizungumzia kuhusu hali tete iliyokuwa ikiikabili Uturuki na kutanabaisha kuwa hakuna nchi katika eneo hilo ambayo ilikuwa 'haijatulia' kama Uturuki.

Pia, wachambuzi wa taarifa za kiusalama wa Marekani walikuwa wakihofia kitambo kuhusu hali ya usalama nchini Uturuki. Swali lilibaki kuwa lini kungetoa jaribio la mapinduzi na lingeongozwa na nani.

Sasa, kama wataalamu hao mbalimbali wa masuala ya usalama waliokuwa wakitegemea 'vyanzo vya wazi vya taarifa za kishushushu' (open sources) waliweza kutoa tahadhari kuhusu uwezekano wa jaribio hilo la mapinduzi, inatarajiwa kuwa mashushushu wa Uturuki pia walikuwa na tahadhari hiyo.

Kwa kuangalia 'sintofahamu' iliyoikumba serikali ya Rais Erdogan wakati wa jaribio hilo la mapinduzi, yayumkinika kuhisi kuwa idara ya ushushushu ya nchi hiyo nayo ilikuwa katika 'sintofahamu' pia. 

Na kuthibitisha kuwa taasisi hiyo haikuwa imejipanga vizuri, asuhuhi ya Julai 16 makao makuu yake yalishambuliwa na helikopta za jeshi pasipo upinzani wowote. 

Wakati serikali ikikabiliwa na jaribio la mapinduzi, mkuu wa idara ya ushushushu ya nchi hiyo, Hakan Fidan, alikuwa mafichoni.




Kuna sababu kuu tatu zinazoweza kueleza kwanini idara ya ushushushu ya nchi hiy, MIT, ilionekana kutokuwa na taarifa kuhusu jaribio hilo la mapinduzi na kushindwa kwake kulizuwia.

Kwanza, uwezo wa utendaji kazi wa taasisi hiyo ni duni, na kwa kiasi kikubwa umekuwa ukikuzwa na vyombo habari kuliko hali halisi. Taasisi hiyo inaelezwa kuwa yenyeurasimu mkubwa, yenye kutumia mbinu za kale, in uhaba mkubwa katika mtandao wake wa upatikanaji taarifa za kiusalama, sambamba na mapungufu katika uwezo wake kwenye uchambuzi wa taarifa za kiusalama.


Pili, kuchanganya siasa na taaluma ya ushushushu. Awali, taasisi hiyo ilikuwa ikijitegemea na kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia taaluma na utaalam wa ushushushu. Hata hivyo, tangu Erdogan aingie madarakani mwaka 2003, taasisi hiyo imekuwa kama chobo cha kisiasa cha AKP, chama tawala chenye mrengo wa kulia kidogo kidini kinachoongozwa na Erdogan.

Tatu, kwa takriban muongo mzima sasa, MIT imekuwa 'bize' zaidi na changamoto za matishio ya usalama kwa Uturuki kutoka nje, yaani tishio la kikundi cha kigaidi cha ISIS, harakati za uhuru za Wakurdi na wapiganaji wao wa PKK, kuibuka kwa taifa lisilo rasmi la Rajava huko Syria, na  hali tete ya usalama huko Iraki na Syria kwa ujumla. Changamoto hizo zimepeleka taasisi hiyo kuwekeza nguvu nyingi katika kukabiliana na matishio kutoka nje badala ya matishio ya kiusalama ya ndani ya nchi.


Kwa upande mwingine, kumekuwa na hisia kwamba huenda Erdogan alishirikiana na MIT kuruhusu wapinzani wa chama tawala na serikali ndani ya jeshi la nchi hiyo kufanya jaribio hilo la mapinduzi , lengo likiwa ni kuwa mapinduzi hayo yakishindikana (na lengo ni yashindikane) basi Erdogan awe na kila sababu na haki ya kuendesha taifa hilo kwa mkono wa chuma. Ikumbukwe kuwa kwa muda mrefu Erdogan amekuwa akifanya jitihada za kutaka taasisi ya urais wa nchi hiyo iwe ya kiutendaji kuliko sasa ambapo kinadharia mkuu wa serikali ni Waziri Mkuu.

Nimalizie makala hii kwa kuahidi kufanya uchambuzi mwingine kadri taarifa mbalimbali zitakavyopatikana. Kwa habari zaidi kuhusu masuala ya ushushushu, bonyeza hapo juu palioandikwa 'INTELIJENSIA,' sambamba na kusoma habari nyingine katika blogu hii.


15 Jul 2016

Anaitwa Karrima Carter, mwanadada mwenye asili ya Tanzania mwenye makazi yake hapa Uingereza. Kwa miaka kadhaa amekuwa akijitolea kukusanya misaada mbalimbali kwa ajili ya kuyasaidia makundi yenye uhitaji huko Tanzania. Tayari ametoa misaada kwa shule mbalimbali za msingi na sekondari katika maeneo mbalimbali ya Tanzania, anaendesha vituo vya kulea watoto yatima na kusaidia wazee. 

Tukio hili pichani ni mfululizo wa matukio anayofanya kabla ya kuelekea Tanzania wiki ijayo kukabidhi misaada kadhaa kwa makundi mbalimbali yenye uhitaji, ikiwa ni pamoja na kuambatana na wahisani kutoka hapa Uingereza kwenye hafla kwenye kituo cha yatima huko Bagamoyo, sambamba na uzinduzi wa vyoo kadhaa katika shule ya msingi Ilala.

Blogu hii inafuatilia kwa karibu jtihada za mwanadada huyu hasa ikizingatiwa kuwa kuna makundi mengi yenye uhitaji huko nyumbani ilhali suala la kujitolea bado halijapata mwamko miongoni mwa Watanzania wengi. 

Chini ni baadhi ya picha za kikundi cha watoto wa Kiingereza walioshiriki katika shughuli hiyo kwa 'kujipaka rangi usoni' (face painting) na kuigiza tamthilia maarufu ya Simba the Lion kwa lugha mbalimbali ikiwa pamoja na Kiswahili. Licha ya kushiriki kukusanya michango, watoto hao pia wanachangia kuwasaidia watoto wenzao huko Tanzania, kwa uratibu wa Karrima.

Waweza kuangalia video mbalimbali kwenye ukurasa wake wa Facebook HAPA au kwenye akaunti yake ya Instagram HAPA.















Uchambuzi wangu wa kiintelijesnia kuhusu shambulio la kigaidi lililotokea jana usiku katika jiji la Nice, nchini Ufaransa ambapo hadi sasa watu 84 wameuawa na wengine zaidi ya 100 kujeruhiwa baada ya gaidi mmoja kuliingiza lori kwenye kundi la watu waliokuwa wakisherehekea siku ya kitaifa nchini humo. Bonyeza hapo chini kusikiliza uchambuzi huo

Check this out on Chirbit

10 Jul 2016


Check this out on Chirbit

8 Jul 2016

Ilikuwa masaa, siku, wiki, miezi na sasa mwaka. Ni vigumu sana kuamini kuwa baba umeondoka moja kwa moja. Kila siku nakumbuka, lakini kuna kitu kingine kinachonikumbusha kila wiki: makala zangu katika gazeti la Raia Mwema. Ulikuwa 'shabiki nambari wani' wa safu yangu katika gazeti hilo, na ulihakikisha unasoma kila toleo la gazeti hilo.

Pamoja na mengi uliyotuachia wanao, moja ninalofanya kila siku ni kusoma na kuandika, vitu viwili ulivyonisisitiza mno tangu nikiwa mtoto mdogo. Na kwa hakika kama ulivyopenda sana kusoma na kuandika, ndivyo ambavyo kwangu vitu hivyo vimekuwa sehemu muhimu ya maisha yangu ya kila siku.

Pia wewe na marehemu mama mlinisisitza mno kuhusu umuhimu wa elimu.Nawashukuru sana mlivyojinyima ili kuhakikisha ninatimiza ndoto zangu za kielimu. Ninasikitika kwamba wakati wewe na mama mlikuwa na kiu sana ya kuniona nahitimu shahada ya uzamifu (PhD), kwa bahati mbaya nyote mmeondoka kabla sijahitimu. Hata hivyo, nime-dedicate thesis yangu kwenye.

Nakushukuru pia wewe na marehemu mama kwa kutuhimiza mno watoto wenu kuhusu upendo, kuthamini utu na kubwa zaidi, kumtanguliza Mungu katika kila tufanyalo. Upendo wako baba ulikufilisi mapema mara baada ya kustaafu mwaka 1981, ambapo mipango yako ya kuwekeza katika kilimo ilizidiwa nguvu na moyo wako wa kuwasaidia ndugu na jamaa pale Ifakara. 

Miaka kadhaa baadae, marupurupu yako ya utumishi wako katika Jumuiya ya Afrika Mashariki nayo yaliishia kwenye kuwasaidia ndugu, jamaa na marafiki. Siku zote ulikuwa unasisitiza kuwa utu ni muhimu ziadi kuliko vitu (including pesa). 

Iliniuma mno kushindwa kuja kukuaga katika safari yako ya mwisho. Lakni nakumbuka sana maeneo yako kuwa "lolote likinitokea, hakikisha kwanza usalama wako..." Wewe baba na marehemu mama siku zote mlikuwa mnahofia kuhusu kazi niliyokuwa naifanya lakini kwa vile mlinipenda mno, mlikuwa mkiniombea kila siku ya Mungu.

Kama kuna kitu kinaniumiza mno ni mapacha Kulwa (Peter) na Doto (Paul). Kwa vile wao walizaliwa wakati umri umeshawapita mkono nyie wazazi wetu, mapacha hawa walikuwa kama wajukuu zenu. Lakini kubwa zaidi, walikuwa ndio marafiki zenu wakubwa. Kila ninapoongea nao najiskia uchungu sana kwa sababu sio tu wamepoteza wazazi lakini pia wapoteza their best friends. Ninaendelea kuwasapoti ili wasielemewe na huu uyatima tulionao.

Kama kuna kitu kimoja nilikuangusha mno ni kutofuata matakwa yako nijiunge na seminari ya Kasita baada ya kuwa mmoja wa wavulana wanne tu waliochaguliwa kujiunga na seminari hiyo. Ulitamani sana niwe padri. Hata hivyo, japo nilikuangusha, angalau mdogo wangu, Sista Maria Solana aliweza kujiunga na utawa, na yeye sasa ndio guide wetu mkuu katika sala.

Pamoja na uchungu nilionao kutokana na kifo chako baba, faraja pekee ni kuwa ninaamini muda huu upo na mkeo mpendwa, mama yetu mpendwa, marehemu Adelina Mapango a.k.a Mama Chahali. Tangu mama afariki, baba ulikuwa ukisononeka mno, kwa vile mama hakuwa mkeo tu bali pia rafiki yako mkuu. Siku zote baada ya kifo cha mama ulijisikia kuwa wewe ndo ulistahili kutangulia kabla yake kwa vile ulikuwa umemzidi umri.

Kipimo cha upendo wako baba ni kipindi kile mama alipopoteza fahamu kuanzia mwishoni mwa Januari 2008 hadi alipofariki Mei 29, 2008. Baba ulikuwa unafunga mfululizo kumwombea mama apate nafuu.Nakumbuka nilipokuja kumuuguza mama tulikushauri upunguze kufunga mfululizo hasa pale sauti yako ilipoanza kukauka na nguvu kupotea kutokana na mwili kukosa lisha na maji. Ulimpenda mno mkeo, na kwa hakika mmetachia fundisho kubwa sana.

Mwaka 2005 niliwarekodi wewe na mama, katika maadhimisho ya miaka 50 ya ndoa yenu. Bado ninayo video ile lakini nashindwa kuiangalia kwa sababu inanitia uchungu sana. Hata hivyo, kila siku ninazingatia yote mliyoniusia katika video hiyo, na ndio mwongozo wa maisha yangu.

Basi baba, nakuombea uendelee kupumzuka kwa amani na marehemu mama na mwanga wa milele uangaziwe na Bwana. Mie ninawakumbuka kwa sala kila siku kabla ya kulala. Sie tulikupenda wewe baba na mama, lakini Baba yenu wa Mbunguni aliwapenda zaidi, akawachukua. Jina lake lihimidiwe milele. AMINA



5 Jul 2016


Check this out on Chirbit

4 Jul 2016



Zaidi kuhusu kundi hilo la kigaidi, BONYEZA HAPA

CHANZO: Amor Shabbi (@amorshabbi), mwandishi  wa habari anayeripoti kuhusu eneo la Sahel na Mashariki ya Kati na Afrika ya Kaskazini (MENA). Waweza kuwasiliana nae [email protected] simu +213660376006 Constantine, Aljeria




Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.