12 Mar 2017

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinafanya Mkutano wake Mkuu Maalum huko Dodoma, ambapo pamoja na mambo mengine ni ajenda kuu ya "kujadili na kupitisha marekebisho ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 Toleo la 2012, pamoja na kanuni za chama hicho na jumuiya zake."

Nimeyawekea msisitizo maneno "kujadili na kupitisha" kwa sababu inaonekana kuwa wazi kuwa majadiliano yatakayofanyika hayapaswi kutoyapitisha marekebisho hayo. 

Ni rahisi kutafsiri hatua hiyo kama ya kunyima demokrasia (kwa maana kwamba kujadili pekee hakutoshi bali pia kuwepo uhuru wa kuyakubali au kuyakataa mapendekezo husika) lakini pengine ni rahisi pia kutambua kwanini CCM "imejihami" mapema.

Sijui ni watu wangapi wanaofahamu kwa hakika mabadiliko yanayotarajiwa kufanyika kwenye katiba hiyo ni yapi, lakini nitakurahisishia msomaji kwa kuyaorodhesha baadhi:
  • Kupunguza idadi ya wajumbe wa vikao vya ngazi za juu vya chama hicho
  • Kupunguza 'kofia mbili' kwa viongozi wenye vyeo ndani ya chama, serikalini au bungeni.
Kwa mujibu wa mabadiliko hayo, mwanachama anatakiwa kushika nafasi moja tuya uongozi, katika ngazi za Mwenyekiti wa Tawi, Kijiji, Mtaa, Kata, Wadi, Jimbo, Wilaya na Mkoa. Wengine ni Makatibu wa Halmashauri Kuu wa ngazi zote, Diwani na Mbunge/Mwakilishi.

Kwahiyo ni wazi kuwa mabadiliko hayo yatawaathiri 'vigogo' kadhaa wa chama hicho, na pengine ndio maana ikaamuliwa kuwe na "mjadala na kupitisha mabadiliko hayo" badala ya "mjadala na kupitisha au kutopitisha mabadiliko husika."

Kadhalika, mabadiliko hayo yatapelekea kupungua kwa idadi ya wajumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, kutoka 34 hadi 24.

Vilevile, idadi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho itapungua zaidi ya nusu, kutoka 388 hadi 158.

Miongoni mwa 'vigogo' watakaoathiriwa na mabadiliko hayo kutokana na kushika nyadhifa zaidi ya moja ni pamoja na William Lukuvi, Makame Mbarawa, Dkt Hussein Mwinyi, na Shamsi Vuai Nahodha.

'Kigogo' mwingine ni Mama Salma Kikwete, ambaye licha ya kuwa mjumbe wa NEC wa Mkoa wa Lindi, majuzi ameteuliwa na Rais Dkt John Magufuli kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri.

Wengine ni wenyeviti wa CCM mikoa ambao pia ni wabunge, kama vile Joseph Musukuma, Martha Mlata na Deo Simba, ilhali Godfrey Zambi ni mbunge na mkuu wa mkoa, Adam Kimbisa ni Mjumbe wa Kamati Kuu na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma.

Kuna usemi mmoja, kwamba sio kila kitu sahihi ni kizuri, na sio kila kitu kizuri ni sahihi. Uamuzi wa CCM kuwapunguzia wanachama wake kofia zaidi ya moja kwenye uongozi ni sahihi lakini sio mzuri kwa watakaoathiriwa nao. Jicho la uchambuzi litaelekezwa kwa 'wahanga' hao kadri chama hicho kinavyoingia kwenye mchakato wake wa uchaguzi mkuu baadaye  mwaka huu, na kwenye kinyang'anyiro cha urais kupitia CCM katika uchaguzi mkuu ujao, mwaka 2020.

Kuna tetesi zisizothibitishwa kuwa miongoni mwa mabadiliko yatayofanyika katika Mkutano huo Mkuu Maalum ni pamoja na kumwezesha Rais aliyepo madarakani kuwa mgombea pekee kwenye mchakato wa chama hicho kumpata mgombea wake. Siwezi kujadili kitu ambacho sina uhakika nacho. Hata hivyo, tutalijadili suala hilo iwapo litajitokeza kwenye Mkutano huo.

Kufuatia vikao vya awali vilivyofanyika jana, chama hicho tawala kilitangaza adhabu kwa viongozi wake kadhaa, kubwa zaidi ikiwa kuvuliwa uanachama kwa Sophia Simba, kada mkongwe wa chama hicho na ambaye hadi jna alikuwa Mwenyekiti wa Taifa wa  jumuiya ya wanawake wa CCM (UWT), mjumbe wa Kamati Kuu na Mbunge.

Orodha kamili ya viongozi walioadhibiwa ni hiyo pichani chini

 




Hatua hizo kali zilizochukuliwa na CCM chini ya uenyekiti wa Rais Magufuli, sambamba na mabadiliko niliyoyaongelea awali, yana tafsiri kuu mbili. Kwanza, hatua kali za kinidhamu zinapeleka ujumbe kwa wana-CCM wa kada mbalimbali kuwa Rais Magufuli amepania kwa dhati kukisafisha chama hicho tawala. Ifahamike tu kuwa kilichojiri jana kinaingia moja kwa moja kwenye vitabu vya historia ya chama hicho na siasa za Tanzania kwa ujumla.

Pili, mabadiliko kusudiwa - na yakipita salama - sambamba na hatu kali zilizochukuliwa dhidi ya viongozi kadhaa wa chama hicho ni mtihani mkubwa, kwa Mwenyekiti Magufuli na CCM kwa ujumla.

Kwa Mwenyekiti Magufuli, hatua hizo zimemwongezea idadi ya maadui zaidi ya wale ambao tayari ni waathirika wa msimamo wake dhidi ya ufisadi na rushwa, ambapo watendaji kadhaa wa serikali wametumbuliwa huku wakwepakodi wakidhibitiwa, na majangili na 'wauza unga' wakibanwa. Japo ni mapema mno kufanya tathmini timilifu kwa hatua hizo, ile kuzichukua tu sio tu kwaonyesha dhamira lakini pia ni wazi zimetengeneza maadui wa kutosha dhidi ya Dkt Magufuli.

Katika hili, ni muhimu kutambua kuwa ni bora kuwa na kiongozi atakayechukiwa na kwa kutenda vitu sahihi kuliko atakayependwa kwa kufanya madudu.

Jana pia zilipatikana taarifa za kukamatwa kwa makada watatu wa Chama hicho, Msukuma, Hussein Bashe na Adam Malima. Sintoshangaa iwapo miongoni mwao akatimuliwa mtu uanachama. Kilichonisikitisha ni maelezo kuwa "walikamatwa na kuhojiwa na polisi kwa tuhuma za kupanga njama za kuvuruga Mkutano Mkuu Maalum wa CCM."

Katika mazingira ya kawaida, sio rahisi kwa makada hao watatu kupanga kuvuruga mkutano mkubwa kama huo ila yayumkinika kuhisi kuwa kilichofanyika ni kuzuwia kile nilichogusia awali, yaani "sio kujadili na kupitisha tu mabadiliko husika" bali pia "kujadili na kupitisha au kutopitisha mabadiliko hayo."

Hili la kuminya fursa ya upinzani kwa mabadiliko hayo linaweza kuwa na athari kwa chama hicho huko mbeleni. Sauti za manung'uniko ni kitu cha kawaida lakini sauti hizo zikiakisi mtazamo wa watu wengi, zinaweza kuathiri mshikamano wa chama hicho.

Hata hivyo, kwa wanaotegemea kuwa "CCM itakufa kutokana na mabadiliko haya" wanapaswa wazielewe vema siasa za Tanzania yetu. Si kwamba CCM itatawala milele, lakini kwa mazingira tuliyonayo, hakuna chama mbadala. Huo ni ukweli mchungu.

CCM wanaweza kukandamiza upinzani dhidi ya mabadiliko ya Katiba yao lakini angalau wamefanya mkutano mkuu, na wameadhibu waliokiuka taratibu za chama hicho. Je katika vyama vya upinzani kuna ujasiri wa aina hiyo? 

Ukiangalia wapinzani wakuu wa CCM, yaani Chadema, sio tu "wamegoma kabisa" kufanya tathmini ya kilichowaangusha katika uchaguzi mkuu uliopita bali pia wametelekeza turufu yao kubwa na iliyowajengea imani kubwa kwa Watanzania, yaani mapambano ya dhati dhidi ya ufisadi, yaliyoibua 'List of Shame,' skandali nzito kama Richmond, EPA, Kiwira,nk. 

Cha kusikitisha ni kwamba vyama vyetu vya upinzani sasa vimekuwa kama vinachezeshwa ngoma na CCM. Wafuasi wa vyama hivyo "wapo bize" kujadili matukio yanayoihusu CCM badala ya kuwekeza nguvu kwenye mustakabali wa vyama hivyo. Jiulize, hivi ajenda kuu ya Chadema, au CUF au ACT- Wazalendo ni ipi muda huu?

Ni katika mazingira hayo, baadhi ya viongozi wa CCM watavumilia mabadiliko yanayoendelea ndani ya chama chao kwa sababu hakuna mbadala wa chama hicho tawala kwa sasa. Tumebaki na miaka mitatu na miezi saba kabla ya uchaguzi mkuu ujao lakini wapinzani wetu wapo bize kuijadili CCM na serikali yake badala ya kujipanga vyema kwa uchaguzi ujao.

Unajua moja kati ya vitu vilivyoiangusha UKAWA katika uchaguzi mkuu uliopita ni "kusubiri makapi ya CCM" badala ya kutangaza mgombea wao mapema na kisha kumnadi kwa nguvu zote, kipindi ambacho CCM ilikuwa na shika-nikushike ya makada wake 40+ waliojitokeza kuwania kuteuliwa kuwa wagombea wa nafasi ya urais kupitia chama hicho tawala.

Nihitimishe makala hii kwa kupigia mstari uwezekano wa aina mbili: 

kwanza, CCM kuibuka imara zaidi baada ya Mkutano huo Mkuu Maalum pamoja na hatua za kinidhamu zilizochukuliwa dhidi ya makada kadhaa, kwa sababu nidhamu katika taasisi yoyote ile ni nguzo ya mafanikio, na pia, ili maendeleo yafikiwe shurti kuwepo na mabadiliko, na mabadiliko hukumbana na vikwazo ambavyo vyaweza kurukwa iwapo kuna nidhamu bora. 

Pili, mabadiliko hayo na hatua dhidi ya makada hao zinaweza kuzua mgogoro ndani ya chama hicho. Ni wazi kuwa waathirika wa kuvuliwa kofia zaidi ya moja za uongozi na hao waliochukuliwa hatua za kinidhamu hawatoridhishwa na hatua hizo. Hata hivyo, je wana pa kukimbilia? Na hapo ndipo utapobaini kuwa siasa za nchi yetu "zingechangamka sana" laiti tungekuwa na upinzani imara.

Na upinzani imara sio lazima upewe ruhusa na serikali kufanya mikutano/maandamano bali kama ule ulioibua 'List of Shame,' Richmond, EPA,nk...hawakuwa na ruhusa ya kufanya hivyo, na pia wanasiasa kama Dkt Willbrord Slaa na Zitto Kabwe walinusurika kwenda jela kwa ajili ya kuwapigani Watanzania. 

Kwa uchambuzi kamili kuhusu Mkutano Mkuu Maalum wa CCM na hatua za nidhamu zilizochukuliwa na chama hicho dhidi ya baadhi ya makada wake, ungana nami kwenye toleo la wiki hii la gazeti bora kabisa Tanzania la Raia Mwema hapo Jumatano panapo majaliwa.


9 Mar 2017


KATIKA hitimisho la makala yangu katika safu hii wiki iliyopita niliahidi kuwaletea uchambuzi kuhusu mivutano ya kugombea madaraka (power struggles) ndani ya chama tawala CCM.Kwa bahati nzuri, kati ya makala hiyo na hii, kumejitokeza tukio ambalo linaweza kuhusishwa na mada hiyo ninayoiongelea katika makala hii.
Wiki iliyopita, Rais Dk. John Magufuli alimteua Salma Kikwete, mke wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete, kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri.Uteuzi huo umepokelewa kwa hisia tofauti, na kuzua mjadala unaoendelea hadi wakati ninaandika makala hii.
Kwa upande mmoja, inaonekana kama kuna mwafaka wa kutosha kwamba Rais ametumia madaraka yake kikatiba kufanya uteuzi huo.
Kwa upande mwingine, pengine kutokana na ukweli kuwa hii ni mara ya kwanza katika historia ya Tanzania kwa Rais kumteua mke wa mtangulizi wake kuwa mbunge, kuna hisia za hapa na pale kwamba uteuzi huo hauleti picha nzuri.
Kwamba, labda kwa vile Salma alikwishakaa Ikulu kwa miaka 10 kama mke wa Rais basi pengine nafasi hiyo ya ubunge wa kuteuliwa ingeenda kwa mtu mwingine.
Hata hivyo, licha ya kuwa Rais ameshaeleza kwa nini alifanya uteuzi huo, ukweli unabaki kuwa Katiba inamruhusu kufanya hivyo, na Salma Kikwete kama Mtanzania mwingine ana haki ya kuteuliwa kushika wadhifa wowote ule bila kujali historia yake kama mke wa rais mstaafu.
Lakini licha ya kuruhusiwa na Katiba kufanya uteuzi, kwa sisi tunaofuatilia kwa karibu siasa za Tanzania, tunauona uteuzi huo kama wa kimkakati, kwa maana ya Dk. Magufuli kujipanga vyema kwa ajili ya mitihani miwili ya kisiasa inayomkabili:  uchaguzi mkuu wa CCM baadaye mwaka huu, na kubwa zaidi, kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Ni hivi, katika nchi zetu zinazoendeshwa kwa mazoea, ni dhahiri kuwa kiongozi wa aina ya Magufuli hawezi kuwa maarufu miongoni mwa waliozoea kuona mambo yakiendeshwa sio yanavyopaswa kuwa, au kwa njia sahihi, bali kwa mazoea, hata kama mazoea hayo yana matokeo hasi.
Viongozi wa aina ya Magufuli wanaominya mianya ya ulaji, wanaozuia safari za ‘matanuzi’ ughaibuni, na wanaojaribu kuwa upande wa wananchi wanyonge badala ya kuendelea kutetea masilahi ya tabaka tawala, hawawezi kuwa na marafiki wengi.
Na ukweli kuhusu Dk. Magufuli ni kwamba kwa muda mfupi aliokaa madarakani ametengeneza maadui wengi tu serikalini na ndani ya chama chake. Kwa serikalini, maadui hao sio tishio kwake kwa sababu mfumo wa utawala sio tu unamwezesha kuwadhibiti kirahisi maadui hao bali pia hata kufahamu dhamira zao ovu mapema.
Changamoto kubwa zaidi kwake ipo ndani ya chama chake. Sio siri kwamba CCM aliyoirithi Magufuli imekuwa, kwa muda mrefu, kichaka cha mafisadi, sehemu ambayo watu waliohitaji kinga dhidi ya mkono mrefu wa sheria walikimbilia huko. Hii haimaanishi kuwa CCM nzima imesheheni watu wa aina hiyo.
Kwa vile licha ya kuwa Mwenyekiti wa taifa wa chama hicho tawala, Magufuli ni kama mgeni kwenye medani za uongozi wa juu wa chama hicho, maadui zake ndani ya chama wanaweza kutumia fursa walizonazo – kama vile ushawishi wao au kukubalika kwao – kumhujumu kiongozi huyo.
Lakini kama ilivyo serikalini, Magufuli ametengeneza maadui ndani ya chama chake kwa sababu ile ile ya kuanzisha zama mpya za kuachana na siasa za/uongozi wa mazoea.
Katika ngazi mbalimbali za uongozi wa chama hicho, kuna viongozi waliozoea kujiona kama wanaendesha kampuni binafsi, huku wakitumia fursa zao kufanya ufisadi. Hali hiyo ilisababisha baadhi ya watu kuiona alama ya jembe na nyundo kwenye bendera ya CCM ikigeuka kuwa umma na bunduki kuashiria ulaji.
Uadui mkubwa ni kinyang’anyiro cha urais kupitia CCM katika uchaguzi mkuu ujao mwaka 2020. Kwa mujibu wa wajuzi wa mambo, kuna jitihada za chinichini ndani ya chama hicho tawala kuangalia uwezekano wa kumfanya Magufuli awe rais wa awamu moja.
Angalau hadi muda huu hakuna dalili kuwa uchaguzi mkuu wa CCM unaweza kuwa na athari zozote katika uenyekiti wa Magufuli japo ni wazi maadui zake watatumia kujipanga kwa ajili ya kinyang’anyiro cha mwaka 2020.
Kwa kumteua Salma Kikwete, Magufuli amemleta karibu mtu muhimu katika siasa za CCM, na pengine kujenga ngome imara ya kumwezesha sio tu kushinda uchaguzi mkuu ujao kwa tiketi ya CCM bali pia kumrahisishia kazi ngumu ya kuleta mabadiliko ndani ya chama hicho tawala.
Nimalizie kwa kuahidi kuendelea na uchambuzi huu katika makala zijazo
Barua-pepe: [email protected] Blogu: www.chahali.com Twitter: @chahali  

2 Mar 2017


MWAKA 1990 nikiwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Tabora, kuliibuka mgomo mkubwa uliodumu kwa siku kadhaa. Kwangu, mgomo huo ulikuwa ni mtihani mkubwa, kwani sikuwa ‘mwanafunzi’ wa kawaida, bali nilikuwa kamanda wa wanafunzi au chifu.
Shule hiyo, pamoja na Sekondari ya Wasichana Tabora, zilikuwa shule pekee nchini zilizokuwa na mchepuo wa kijeshi. Hata sare zetu zilikuwa ‘magwanda,’ na baadhi ya walimu wetu wakiwa askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ).
Huo wadhifa wa kuwa chifu ulikuwa ni ukiranja mkuu. Kwa hiyo mgomo huo ulitokea wakati nikiwa kiranja mkuu katika shule hiyo yenye historia ya kipekee. Chanzo kikuu cha mgomo huo kilikuwa madai ya wanafunzi kuwa chakula kilikuwa duni.
Nimesema kuwa mgomo huo ulikuwa mtihani kwangu kwa sababu kwa upande mmoja nilikuwa mwanafunzi kama wenzangu waliogoma, na upande mwingine, nilikuwa sehemu ya uongozi wa shule hiyo. Na kwa hakika, nilikuwa kiungo kati ya utawala na wanafunzi.
Hatimaye mgomo huo ulimalizika na kwa vile sikuwa nimeelemea upande wowote wakati wa mgomo huo, kumalizika kwake kuliniacha nikiwa ‘sijauudhi’ upande wowote – wa utawala wa shule na wa wanafunzi wenzangu. Na nyenzo yangu muhimu ilikuwa kusimamia kwenye kanuni na sheria, sambamba na kushawishi matumizi ya busara ili kufikia mwafaka. Mara nyingi huwa vigumu kuziridhisha pande zote za mgogoro husika.
Nimelikumbuka tukio hilo muhimu baada ya kutupia jicho baadhi ya mambo yanayoendelea kwenye Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais Dk. John Magufuli. Ni kwamba, kwa kiasi kikubwa, baadhi ya mawaziri wameonyesha bayana kuwa aidha hawaendani na kasi ya Dk. Magufuli au wanamhujumu kwa makusudi.
Baadhi yetu tunaofuatilia siasa za Tanzania tulikwishahisi mapema kuwa uamuzi wa Dk. Magufuli kuzileta baadhi ya sura zile zile ambazo zilikuwa mzigo kwa taifa huko nyuma, ungeweza kusababisha matatizo mbele ya safari.
Kwa kurejea tukio la mgomo nililolielezea hapo juu, Rais anajikuta kwenye ‘mtihani’ kwa sababu kwa upande mmoja anapaswa kuwa upande wa watendaji wake aliowateua kwa umakini mkubwa (ndio maana ilichukua wiki kadhaa kabla Rais hajatangaza Baraza lake la Mawaziri) na kwa upande mwingine yeye sio rais wa mawaziri wake pekee bali Watanzania wote.
Sakata la vita dhidi ya dawa za kulevya lililoibuliwa upya na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, limechangia kwa kiasi kikubwa kuonyesha kukosekana ‘visheni’ ya pamoja miongoni mwa mawaziri katika Baraza la Mawaziri la Rais Magufuli.
Kwa mtazamo wangu, pengine ingekuwa vema kama Rais alipounda Baraza lake la Mawaziri angeepuka kuwaingiza makada wengi wa chama chake kwenye baraza hilo. Hiyo ni kutokana na ukweli kwamba chama hicho tawala kimeshika hatamu za uongozi wa taifa na ukada unawapa jeuri baadhi ya watendaji wa serikali. Na si kosa lao kwa sababu ukada umekuwa nyenzo muhimu katika uongozi wa Tanzania huku baadhi ya wakosaji wakiepuka adhabu kwa vile tu ni makada muhimu.
Wakati wa sakata la dawa za kulevya lililoibuliwa na RC Makonda, angalau waziri mmoja alijitokeza waziwazi kupingana na uamuzi wa kutangaza majina ya watuhumiwa, akidai hatua hiyo ingeathiri chapa (brands) za wasanii waliotajwa katika orodha ya watumiaji au wauzaji wa dawa za kulevya.
Kanuni muhimu ya uongozi ni uwajibikaji wa pamoja, na pindi mtendaji mmoja akikosea, basi kuna fursa ya kuongea tofauti za kimtazamo faragha badala ya kuitisha mikutano na waandishi wa habari kuonyesha mpasuko.
Naomba ieleweke kuwa sio ninakemea uhuru wa kujieleza miongoni mwa watendaji wa serikali, ikiwa pamoja na mawaziri, lakini uhuru huo sharti uzingatie kanuni.
Hata tukiweka kando hali tata iliyotokana na sakata hilo la dawa za kulevya, haihitaji uelewa mkubwa wa siasa za nchi yetu kutambua kuwa baadhi ya watendaji wa Rais Magufuli ni mzigo kwake. Ni mzigo kwa vile aidha hawaendani na kasi yake au wanafanya makusudi kwa minajili ya kumkwamisha.
Ndio maana, picha inayopatikana mtaani ni kwamba mara kadhaa ni mpaka rais aingilie kati ndio hiki au kile kifanyike. Swali linalojitokeza ni je, rais haoni hali hiyo? Je, washauri wake (kwa mfano ndugu zetu wa Idara ya Usalama wa Taifa) nao hawaoni hali hiyo?
Nimalizie makala hii kwa kumshauri Rais Dk. Magufuli kuwa pengine imefika wakati mwafaka kufanya utumbuaji kwa watu baadhi ya aliowakabidhi dhamana ya uwaziri kwenye kabineti yake. Asipochukua hatua mapema, inaweza kugharimu urais wake.
Nitaendelea na makala hii wakati mwingine kujadili kile Waingereza wanaita ‘power struggles’ zinazoendelea ndani ya CCM na ambazo kwa kiasi fulani zinachangia utendaji duni wa baadhi ya watendaji wa Rais Magufuli (kwa maana ya utendaji duni kama mkakati wa makusudi).

Baruapepe: [email protected] Tovuti: www.chahali.com Twitter: @chahali

26 Feb 2017








DK 1. Mpira umeanza

DK 3: Yanga wanapata penati baada ya Chirwa kuangushwa na mlinzi wa Simba eneo la Penati.

DK 4: Mathew Akrama anamlamba kadi ya njano Lufunga kwa kumuangusha Chirwa

DK 5 - GOOOAAL: Simon Msuva anawaandikia Yanga bao la kwanza kwa mkwaju wa penati.



DK 10: Simba wanaonesha kumiliki mpira, Yanga wanakuwa makini.

DK 13: Mavugo anapokea pasi nzuri lakini anakuwa butu na kupoteza mpira ule muhimu langoni mwa Yanga, Dida anaudaka.

DK 15: Mchezo sasa upo balanced huku mipango ya Simba ikiwa haijakaa vizuri, wanashindwa kujiamini.

DK 16: Juma Luizio anaotea.

DK 17: Simba wanafanya mashambulizi lakini Dida anawahi na kudaka, Yondani yupo chini baada ya kugongwa katika purukushani hiyo.

DK 19: Kamusoko anapiga krosi murua kutokea kulia, Chirwa anaunganisha kwa kichwa na Agyei anadaka.

DK 20: Yanga wanafanya shambulizi lakini Niyonzima anapiga shuti la kitoto Agyei anaudaka.

DK 22: Kotei anafanya kazi ya ziada kuokoa mpira miguuni kwa Msuva

DK 23: Krosi safi ya Juma Abdul, Zimbwe anaokoa na kuwa kona ya kwanza

DK 23: Niyonzima anachonga kona nzuri hapa lakini Agyei anaruka na kupangua

DK 25: Kamusoko anapokea pasi murua kutoka kwa Chirwa, anapiga shuti lakini mpira haujai vizuri mguu hivyo kuwa dhaifu, Agyei anaudaka.

DK 26 - Sub: Simba wanafanya mabadiliko ya mapema, Anaingia Ndemla na kutoka Luizio.

DK 28: Zuru anapoteza pasi muhimu sana ambayo ingewapa Yanga goli la pili muhimu

DK 29: Nafasi nzuri zaidi kwa Simba, Mavugo akiwa amebaki yeye peke yake na kipa Dida, anapiga mpira wa kichwa dhaifu na unatoka nje.

DK 32: Mavugo anawachambua kama karanga mabeki wa Yanga, Yondani anazuia shuti la Mavugo na Munishi anaudaka.

DK 34: Munishi analeta mbwembwe baada ya kudaka mpira baada ya kukaa na mpira mkononi kwa zaidi ya muda unaoruhusiwa. Simba wanapiga mpira wa adhabu ndogo ndani ya eneo la 18.

DK 35: Said Mdemla anapiga shuti linapaa aka mnazi.

DK 37: Yanga wanafanya shambulizi lakini Agyei anauwahi mpira. Ndemla anapiga shuti maridadi lakini linatoka nje ya lango la goli.

DK 40: Mo Ibrahim anaachia shuti kali sana lakini Munishi anaupoza mpira kwanza na kuudaka.

DK 41: Simba wanaonekana kuzinduka wakati huu wa kuelekea mapumziko. Wanapiga moja mbili lakini Dida anaudaka mpira.

DK 42: Kamusoko anapiga shuti tena lakini mpira haujai mguu, mpira unatoka nje na kuwa goal kick

DK 42: Kamusoko yuko chini baada ya kugongana na Muzamiru

DK 44: Mo Ibrahim analazwa chini karibu na eneo la boksi, anajirusha hadi kwenye 18, wachezaji wa Simba wanadai penati ila refa anasema ni kwenye ukingo wa boksi.

DK 45: Hajibu anapiga mpira wa adhabu, inakuwa goli kick.

DK 45+1: Kamusoko anaonekana hali yake haijatengamaa, analala chini na refa anaita huduma ya kwanza na kumtoa nje ya uwanja

DK 45+3 - Sub: Kamusoko anatoka, anaingia Said Juma Makapu

DK 45+4: Mpira ni mapumzikooooooooo

DK 46: Mpambano wa mahasimu unarejea tena kipindi cha Pili huku Yanga wakiwa kifua mbele kwa bao moja la Msuva.

DK 46: Simba wanafanya mashambulizi ya mfululizo mara mbili lakini umakini wa Munishi anaweza kuokoa hatari zote.

DK 48: Simba wanafanya mashambulizi karibu kabisa na lango la Yanga, Mavugo anamfanyia madhambi mchezaji wa Yanga.

DK 50 -SUB: Anatoka Lufunga anaingia Shiza Kichuya.

DK 52: Mavugo anachezewa madhambi, refa anampa kadi ya njano Vincent wa Yanga

Dk 53: Banda analazimika kufanya kazi ya ziada na kuwa kona
KADI Dk 52, Vicent analambwa kadi ya njano kwa kumfanyia madhambi Mavugo

Dk 53: Msuva anageuka vizuri kwenye boksi la Simba na kuachia mkwaju mkali kabisa, GOAL KICK

DK 55- RED CARD: Boukungu anamuangusha Chirwa akiwa amebaki peke yake nje ya eneo la hatari, anatolewa nje kwa kadi nyekundu

DK 56: Anapiga faulu nzuri lakini Agyei anauona mpira na kuudaka.

DK 57: Simba wanafanya shambuli na kupata kona, Kichuya anaenda kuchonga kona.

DK 57- SUB: Simba wanamtoa Mo Ibrahim na nafasi yake inachukuliwa na Jonas Mkude

DK 63: Yanga wanafanya shambulizi lakini Agyei anatokea na kuondosha hatari

DK 64: Hajibu anapiga shuti kimo cha sungura na Munishi anaudaka kwa umaridadi

DK 66- GOOOOAAL: Mavugo anaisawazishia Simba kwa goal la kichwa kwa pasi Murua ya Shiza Kichuya.

DK 68: Simba pamoja na kuwa pungufu wanaonesha kurudi mchezoni na sasa mchezo ni vuta nikuvute.

DK 70- SUB: Anaingia Deus Kaseke kuchukua nafasi ya Hamis Tambwe, Tambwe leo katiwa kibindoni hafurukuti.

DK 72: Yanga wanakwenda vizuri na krosi ya MSuva inazuliwa na Kichuya na kuwa kona

Simba wanaonesha kupambana huku Yanga wakiwa hawajui walifanyalo, Yanga wanapoteza mipira muhimu ambayo ingeweza kuleta madhara.

DK 77: Haruna Niyonzima anaoneshwa kadi ya njano kwa kucheza ndivyo sivyo

DK 78- SUB: Yanga wanafanya mabadiliko, anaingia Mahadhi na kutoka Zuru

DK 81- GOOOOOAL: Shiza Kichuya akitokea upande wa kulia anaingia vizuri na katikati na kumtungua Munishi goal la kiwango, Munishi hakuwa na ujanja wowote wa kuufikia mpira ule.

DK 83: Defence ya Yanga inaonesha kuchoka kabisa, haina tena maelewano.

DK 85: Mavugo anawachambua kama karanga mabeki wa Yanga wasiopungua watatu, anapiga shuti kali sana na linagonga nguzo ya goli.

DK 90: Zinaongezwa dakika 4 za lala salama, Yanga wanaonesha kuchanganyikiwa. Wachezaji wa Simba Kichuya na Mavugo wanajiangusha ili kupoteza muda.

DK 90+1: Hatari langoni mwa Simba lakini inakuwa goal kick, Agyei anachelewesha mpira Msuva anaukimbilia na kumtengea kipa.

DK 90+4: Mpiraaa umekwishaaaaaa, Simba wanaondoka kidedea na point tatu.

23 Feb 2017


MOJA ya sababu zilizosababisha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kifikie hatua ya kuwa chama kikuu cha upinzani ni msimamo mkali ambao chama hicho ulikuwa nao dhidi ya ufisadi.
Kadhalika, Chadema sio tu kilionyesha dalili za kuweza kuwa mbadala wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) bali pia kiliweza kujijengea hadhi kubwa ya ‘sauti ya wasio na sauti’ (voice of the voiceless) na chenye kupigania haki za wanyonge.
Chadema hawakuuchukia ufisadi kwa maneno matupu bali kwa vitendo, ambavyo mara nyingi vilisababisha viongozi wakuu wa chama hicho kuchukuliwa hatua na Bunge au serikali/vyombo vya dola. Katika harakati za kuwapigania wanyonge, baadhi ya wafuasi wa chama hicho walipoteza maisha na wengine kuachwa na ulemavu wa kudumu.
Japo kwa kiasi kikubwa, mafanikio ya Chadema kisiasa yalichangiwa na ‘madudu’ ya chama tawala CCM takriban katika kila eneo, hiyo sio kusema kuwa chama hicho cha upinzani ‘kilidondoshewa’ mafanikio hayo.
Kupitia viongozi wake makini, chama hicho kiliwekeza vya kutosha katika upatikanaji wa taarifa sahihi, ambazo japo kila zilipotolewa zilikutana na vitisho vya “nitawaburuza mahakamani,” hakuna mmoja wa waliotoa vitisho hivyo aliyethubutu kwenda mahakamani.
Orodha ya ufisadi ulioibuliwa na Chadema ni ndefu, lakini matukio muhimu kabisa, na yatakayobaki katika historia ya taifa letu ni pamoja na skandali nzito kama ile ya Richmond, EPA, Buzwagi, Meremeta, Tangold, ‘Minara Pacha’ ya Benki Kuu na Deep Green Finance.
‘Dream team’ ya Dk. Willbrord Slaa, Zitto Kabwe na Freeman Mbowe ilikuwa ‘moto wa kuotea mbali’ kiasi kwamba ingekuwa ni ushirikiano wa ushambuliaji katika soka basi ni sawa na ‘MSN’ ya Messi, Suarez na Neymar huko Barcelona.
Ilifika mahala ambapo mstari ulichorwa bayana kwamba Chadema kilikuwa chama cha kutetea maslahi ya wanyonge wa Tanzania, hususan kwa kupambana na kila aina ya ufisadi, ilhali chama tawala CCM kikionekana kama kichaka cha kuhifadhi mafisadi, huku kikiandamwa na skandali moja baada ya nyingine.
Kwa hakika, tukiangalia jinsi Tanzania yetu ilivyotafunwa katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita, ni maajabu makubwa kushuhudia Mahakama Maalumu ya Ufisadi ikiwa haina kesi huku waziri husika, Dk. Harrison Mwakyembe akituhadaa kuwa kukosekana kwa kesi ni ishara ya mafanikio ya mahakama hiyo. Nchi yetu haiishiwi vituko.
Laiti dhamira nzuri ya Rais Dk. John Magufuli kuanzisha mahakama hiyo ya ufisadi ingeambatana na utashi wa kisiasa ili kuifanya iwe na ufanisi, basi kazi kubwa iliyofanywa na Chadema huko nyuma ingekuwa imeirahisishia kazi mahakama hiyo.
Sogeza mbele (fast-forward) hadi mwaka 2015 na kuendelea (hadi muda huu ninapoandika makala hii), Chadema ile iliyowanyima usingizi mafisadi na kuwapa matumaini walalahoi imegeuka kuwa kama taasisi inayoendeshwa na matukio. Kimsingi, sidhani kama hata uongozi wa juu – achilia mbali wananchama na wafuasi wa kawaida wa chama hicho – wanaofahamu chama hicho kinasimamia nini kwa sasa.
Kwa tunaofahamu ‘yanayoendelea nyuma ya pazia’ ya siasa za Tanzania, Chadema ilihujumiwa vya kutosha, huku miongoni mwa waliokihujumu chama hicho wakiwa watu muhimu walioshiri kukifikisha chama hicho katika umaarufu wa kisiasa. Tamaa ya madaraka kwa baadhi ya viongozi muhimu wa chama hicho ilitoa fursa mwafaka kwa hujuma hizo kufanikiwa.
Lakini kosa kubwa kabisa walilofanya Chadema, na ambalo linaweza kuwa na madhara makubwa zaidi yenye utata unaoendelea hivi sasa ni kumpokea aliyekuwa kada maarufu wa CCM, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, sio tu kujiunga na chama hicho bali pia kuwa mgombea wa kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Uamuzi wa Chadema kumpokea Lowassa na kumfanya mgombea wa urais ulikuwa ni kioja cha kihistoria, hasa ikizingatiwa kwamba Chadema hiyo hiyo ilitumia takriban miaka tisa mfululizo kumtambulisha Lowassa kama kinara wa ufisadi nchini Tanzania. Sasa kwa busara japo ‘kiduchu’ tu, huwezi kumchafua mtu kwa miaka tisa mfululizo kisha ukajaribu kumsafisha kwa miezi mitatu kabla ya uchaguzi mkuu.
Ninakumbuka wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka juzi, kada mmoja wa ngazi za juu wa CCM alinieleza kuwa “kwa kumpokea Lowassa, Chadema wameturahisishia safari yetu ya Ikulu,” akibainisha kuwa ajenda ya ufisadi ingeweza kuiangusha CCM katika uchaguzi huo. Hata hivyo, kwa Chadema kumkumbatia ‘mwanasiasa waliyemwita fisadi miaka nenda miaka rudi,’ chama hicho kilijinyima uhalali wa kushikilia hoja ya ufisadi dhidi ya CCM.
Kibaya zaidi, Chadema haijaona umuhimu wa kufanya sio tu tathmini ya kina ya ‘athari za ujio wa Lowassa,’ bali pia jitihada za kuwarejesha wafuasi wa chama hicho ‘walioondoka na Dk. Slaa (yaani waliokerwa na ujio wa Lowassa na kuamua kujiweka kando)
Nimalizie makala hii kwa kuikumbusha Chadema kuwa kuna umuhimu mkubwa kwa chama hicho kujitathmini upya, na kifanye jitihada za kurudi zama zile za ‘List of Shame,’ EPA, Richmond, nk – yaani kuwa sauti ya wasio na sauti na wapigania haki za wanyonge. Ukimya wa Lowassa katika kipindi muhimu kama hiki cha vita dhidi ya biashara ya dawa za kulevya huku Mwenyekiti Freeman Mbowe akitajwa kuwa mtuhumiwa wa biashara hiyo ni ishara mbaya kwa chama hicho kilichowahi kuwa mbadala wa CCM.

Barua-pepe: [email protected] Blogu: www.chahali.com Twitter: @chahali  

16 Feb 2017


KATIKA nchi nyingi za huku Magharibi, kila mwanzoni mwa mwaka Idara zao za Usalama wa Taifa huchapisha ripoti inayoelezea kwa kina maeneo yanayoonekana kuwa yanaweza kuwa tishio kwa usalama wa mataifa husika.
Kwa ‘akina siye’ kwa maana ya nchi nyingi za Afrika na Dunia ya Tatu kwa ujumla, kila chapisho la Idara ya Usalama wa Taifa ni siri kuu isiyopaswa kuonekana kwa mwananchi wa kawaida.
Na ni katika mazingira haya ya kufanya ‘kila taarifa ni siri’ hata zile ambazo zingepaswa zifahamike kwa wananchi, ndio tunashuhudia uhusiano kati ya Idara zetu za Usalama wa Taifa na wananchi wa kawaida sio mzuri, uliojaa shaka na kutoaminiana, kwa kiasi kikubwa wananchi kuziona taasisi hizo kama zipo dhidi yao.
Na hiyo ndio moja ya sababu kuu zilizonifanya, mwaka jana, kuchukua uamuzi wa kuandika kitabu kuhusu taaluma ya uafisa usalama wa taifa, si kwa Tanzania pekee, bali duniani kwa ujumla. Na kama nilivyotarajia, wasomaji wengi wamenipa mrejesho kuwa kitabu hicho kimewasaidia mno kutambua kuwa Idara za Usalama wa Taifa ni ‘rafiki mwema’ kwao na ni taasisi muhimu mno kama moyo au ubongo kwa nchi husika.
Kadhalika, wasomaji wengi wamekiri kuwa kabla ya kusoma kitabu hicho walidhani kuwa kazi kuu za watumishi wa Idara ya Usalama wa Taifa ni kutesa watu, u-mumiani (kunyonya damu) na vitu vingine vya kuogofya, na kwamba hakuna lolote jema kwa masilahi ya wananchi.
Sitaki kujipongeza lakini ninaamini kuwa kitabu hicho kimesaidia sana, pamoja na mambo mengine, kujenga taswira nzuri kwa Idara yetu ya Usalama wa Taifa, hasa ikizingatiwa kuwa kutokana na wananchi wengi kutofahamu umuhimu wa taasisi za aina hiyo, imekuwa ikibebeshwa lawama nyingi isizostahili.
Lakini lengo la makala hii sio kuongelea kitabu hicho au shughuli za Idara za Usalama wa Taifa, bali kuzungumzia maeneo ambayo kwa utafiti, uchambuzi na mtazamo wangu yanaweza kuwa tishio kwa usalama wa taifa letu.
Eneo la hatari zaidi ni kuminywa kwa kile kinachoitwa kwa kimombo ‘political space,’ yaani mazingira ambayo shughuli za kisiasa hufanyika pasi kuingiliwa na dola. Bila hata haja ya kuingia kiundani kwenye hili, ukweli ni kwamba kuminya ‘political space’ sio tu kunajenga chuki ya wananchi kwa dola bali pia kunazuia fursa ya wananchi kujadiliana kuhusu manung’uniko yao, ambayo sote tunafahamu kuwa ‘yakijaa sana bila kuwepo upenyo wa kuyapunguza, yatapasuka pasipotarajiwa.’
Suala jingine ni hisia za ukabila/ukanda. Kuna kanuni moja inasema ‘ni silika ya mashushushu kuongea na kila mtu.’ Naam, kwa kuongea na kila mtu, inakuwa rahisi kusikia ‘mazuri’ na ‘mabaya,’ na pia mitazamo ya watu mbalimbali hata ile tusioafikiana nayo.
Na katika kuongea na watu mbalimbali, nimebaini manung’uniko ya chini chini kuhusu ukabila na ukanda, huku baadhi ya watu wakienda mbali na kutamka bayana kuwa wanaona kama eneo fulani analotoka kiongozi fulani linapendelewa zaidi.
Sambamba na ukabila ni udini. Hili ni tatizo kubwa pengine zaidi ya kuminywa ‘political space’ na hilo la ukanda/ukabila, kwa sababu tatizo hili limekuwepo kwa muda mrefu huku kila awamu ya serikali iliyopita ikipiga danadana kwenye kusaka ufumbuzi wa muda au wa kudumu.
Wakati angalau kuna jitihada za makusudi za kupunguza pengo kati ya walio nacho na wasio nacho, umasikini bado ni tatizo kubwa, ni muhimu kwa serikali kuwa ‘honest’ kwa wananchi kwa kuepuka kutilia mkwazo takwimu za kupendeza (na lugha ya kitaalamu) zinazokinzana na hali halisi mtaani. Rais Dk. John Magufuli awaagize watendaji wake wawe wakweli kwa wananchi, wawafahamishe taifa linapitia hatua gani muda huu, na matarajio ni yapi, na waongee lugha inayoeleweka kirahisi.
Sambamba na umasikini ni janga la ukosefu wa ajira. Japo kilimo kinaweza kutoa fursa kwa vijana wengi wasio na ajira, bado hakuna dhamira ya dhati ya kisiasa ya kukifanya kilimo kiwe kweli uti wa mgongo wa taifa letu.
Wakati jitihada za serikali kupambana na ufisadi na uhalifu zinaleta matumaini, kasi ya kushughulikia watuhumiwa ni ndogo huku mahakama ya mafisadi ikiwa kama kichekesho fulani kwa kukosa kesi, japo waziri husika anajaribu kutueleza kwamba kukosekana kesi ni mafanikio kwa mahakama hiyo. Ikumbukwe kuwa wahusika wa ufisadi, biashara ya dawa za kulevya, ujangili na uhalifu kama huo ni watu wenye uwezo mkubwa, na wanaoweza kuunganisha nguvu za ndani na nje ya nchi ili kuliyumbisha taifa. Kibaya zaidi ni kwamba baadhi ya majina maarufu ya wahalifu, kwa mfano ‘wauza unga,’ yanahusisha familia maarufu kisiasa, na hiyo inakuwa kama kinga kwao. Sheria haipaswi kubagua kati ya ‘huyu mtoto wa fulani’ na yule ni mtu wa kawaida.
Kimataifa, kama kuna kitu kinanipa wasiwasi sana ni kinachoonekana kama uhusiano wetu mzuri na nchi moja jirani, uhusiano ambao ulichora picha ya kudorora katika miaka ya hivi karibuni. Kiintelijensia, hao sio marafiki zetu hasa kwa kuzingatia historia na siasa za ndani za nchi hiyo. Naamini wahusika wanatambua changamoto kutoka kwa majirani zetu hao. Mbali na nchi hiyo jirani, hali ya shaka huko Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni tishio kwa usalama wa nchi yetu pia. La muhimu zaidi ni kuimarisha usalama wa mipaka yetu ili kudhibiti uhamiaji haramu kutoka nchi hizo.
Binafsi, ninauona ushirikiano wa Afrika Mashariki kama urafiki wa shaka. Tatizo kubwa linaloukabili ushirikiano huo ni kuendekeza zaidi siasa na kupuuzia kabisa ukweli kuwa nchi zinazounda ushirikiano huo zinajumuisha watu wa kawaida, na sio wanasiasa pekee. Ili ushirikiano huo uwe na manufaa ni lazima uwe na umuhimu kwa watu wa kawaida katika nchi husika.
Mwisho ni tishio la ugaidi wa kimataifa. Japokuwa hakuna dalili za kutokea matatizo hivi karibuni, masuala kadhaa niliyokwishayagusia yanaweza kutoa fursa kwa tishio hilo. Kwanza, kuminya ‘political space,’ udini, umasikini na ukosefu wa ajira. Utatuzi wa matatizo haya utasaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa tishio la ugaidi wa kimataifa.
Angalizo: Huu sio utabiri, kuwa hiki na kile kitatokea. Hii ni tathmini ya jumla ya maeneo yanayoweza kuhatarisha usalama wa taifa letu. Tathmini hii imetokana na ufuatiliaji wangu wa masuala mbalimbali, hasa ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiusalama kuhusu Tanzania yetu.

Barua-pepe: [email protected] Blogu: www.chahali.com Twitter: @chahali  

10 Feb 2017


Kwamba Idara yetu ya Usalama wa Taifa imekuwa ikibebeshwa lawama mbalimbali kwa takriban 'kila baya' linaloihusu Tanzania yetu, sio siri. Ni kitu cha wazi ambacho ninaamini hata wana-Usalama wetu pia wanakifahamu.

Hata hivyo, kwa kiasi kikubwa lawama hizo huchangiwa na uelewa mdogo au usiopo kabisa kuhusu dhamana muhimu ya taasisi za usalama wa taifa kwa nchi husika, na jinsi taasisi hizo zinavyofanya kazi muda wote kuhakikisha usalama wa nchi husika.

Lakini pengine kabla ya kuingia kiundani kuhusu mada yangu, nigusie maongezi yangu na jamaa yangu mmoja, shushushu mstaafu kutoka nchi moja ya Afrika Magharibi. Jana aliamua 'kunifungukia,' kwanini mtu mwenye umri wa kati kama yeye ni 'shushushu mstaafu' (tumezowea kuona wastaafu wakiwa watu wenye miaka 50 na kuendelea, lakini huyo bwana ni wa umri wa miaka thelathini na kitu tu).

Alinidokeza kwa kifupi kuwa alilazimika 'kutoroka' nchini kwake baada ya kufeli kwa jaribio la mapinduzi katika taifa analotoka ambalo huko nyuma lilikuwa kama linapendelea zaidi mapinduzi kuliko chaguzi.  Alidai kuwa "mapinduzi hayo yalikuwa ni kwa minajili ya kuikwamua nchi hiyo kutoka katika nira ya utawala wa kidikteta wa kijeshi."

Hadi kufikia hatua hiyo ya maongezi hayo, ilitokana na huyo jamaa kuwa alitembelea kwenye ukurasa wangu wa Facebook, na kuona matangazo ya kitabu changu kuhusu taaluma ya Uafisa Usalama wa Taifa (USHUSHUSHU). Awali hakuelewa kitabu kinahusu nini kwa sababu maelezo yote kuhusu kitabu hicho yapo kwa Kiswahili, na yeye haielewi lugha hiyo. Alichofanya ni "kuomba msaada wa Google Translate," na akaweza kufahamu kitabu hicho kinahusu nini.

Akanambia kuwa amevutiwa sana na kitabu hicho kwa sababu kwa Bara la Afrika lina uhaba mkubwa mno wa katika fasihi simulizi kuhusu taaluma ya Uafisa Usalama wa Taifa. Na akanishauri nianze haraka iwezekanavyo kukitafsiri kitabu hicho kwa lugha ya Kiingereza ili kiweze kuwafikia wana-Usalama wengi zaidi katika nchi mbalimbali zenye uhaba mkubwa wa maandiko ya wazi kuhusu taaluma yao.

Japo sijawahi kuliongelea hili hadharani, moja ya mafanikio mkaubwa mno ya kitabu hiki yamekuwa katika wananchi wa kawaida kuielewa Idara ya Usalama wa Taifa kwa mtazamo chanya zaidi, hasa kutokana na maelezo ya kina ya kazi za taasisi hiyo muhimu kabisa kwa ustawi na uhai wa taifa lolote lile.

Angalia pongezi za msomaji mmoja wa kitabu hicho


Na kwa hakika, licha ya kuandika kitabu hicho kwa ajili ya jamii kwa ujumla, walengwa wakuu pia ni maafisa usalama wa taifa popote pale walipo. Kwa umahiri mkubwa, kitabu kimeepuka 'kuandika yasiyopaswa kuandikwa,' na kuwekea mkazo katika maoeneo ambayo licha ya kujenga ufahamu, yanasaidia kuwaelimisha raia kuwa Idara za Usalama wa Taifa ni kama roho na pumzi za taifa lolote lile. 


Naomba kutumia fursa hii kuwakaribisha ndugu zangu wa Idara ya Usalama wa Taifa kukinunua kitabu hiki kwa minajili ya kujielimisha, sambamba na kupata mtazamo wa 'akina sie' ambao ni wadau wa sekta ya Usalama wa Taifa. 

Kadhalika, kitabu hiki ni dedicated kwa Maafisa wa Usalama wa Taifa popote pale walipo, hasa kwa kutambua safari ndefu na ngumu waliyopitia hadi kufika walipo sasa, na "kuwa kwao macho masaa 24 ya siku 365 za mwaka" kwa minajili ya usalama wa mataifa yao. 


Kwa walio nje ya Tanzania, kitabu kinapatikana www.chahalibooks.com na AMAZON 

Kwa Tanzania, kitabu kinapatikana katika maduka ya vitabu yafuatayo


DAR ES SALAAM:

TPH BOOKSHOP, 24 Samora Street jirani na Sapna (Simu 0687-238-126/ 0759-390-082);
GENERAL BOOKSELLERS, Mtaa wa Mkwepu (Simu MAMA MEENA 0784-887-871)
DAR ES SALAAM BOOSHOP, Mtaa wa Makunganya (Simu MR MPONDA 0657-827-172)
MLIMANI BOOKSHOP, Kariakoo (Simu 0754-269-042)
ZAI BOOKSHOP, Kariakoo (Simu0754-292-532)
ELITE BOOKSTORE, Mbezi Beach Tangi Bovu karibu na Goba Road (Simu 0754-767-336)

MOSHI: APE BOOK, Rindi Lane, Opoosite I&M Bank (Simu 0754767336)

ARUSHA: KASE BOOKSTORE, ELCT Building, Joel Maeda Street

TANGA: HAFAT BOOKSHOP, Barabara ya Saba (Simu HASSAN SHEDAFA 0767-216-403)

MWANZA:
GUNDA BOOKSHOP Karibu na NHC Regional Office Bantu Street/Kemondo (Simu 0753-969-421)
VICTORIA BOOKSHOP, along Bantu Street, Kemondo (Simu 0755-375-034)

MUSOMA: NYAMBUSI BOOKSHOP, Opposite NMB Bank Main Branch (0767-578-565)

IRINGA: LUTENGANO INVESTMENT (Bakwata House), Miomboni St mkabala na Akiba House (Simu 0763-751-978)

KIGOMA: NDAMEZYE ENTERPRISES, Mkabala na NBC Bank (0713534116)

MBEYA VOLILE BOOKSHOP, Mount Loleza, mkabala na TRA (Simu SANGA 0754412075)

MOROGORO: Wasiliana na Marcelino kwa simu 0767612566 ; 0621081500; 0655612566. 






9 Feb 2017

MWEZI Machi mwaka jana, watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Nottingham cha hapa Uingereza walichapisha matokeo ya utafiti wao kuhusu kushamiri kwa tabia ya uvunjaji wa sheria. Katika matokeo hayo ya utafiti uliochunguza nchi 159, Watanzania tuliibuka vinara kwa kuwa watu wanafiki kupita kiasi, tukifuatiwa na watu wa Morocco.
Na mifano ya unafiki wetu ipo mingi tu, sisi ni miongoni mwa wapinzani wakubwa wa suala la ushoga. Lakini ukitaka kufahamu unafiki wetu katika suala hilo, nenda kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram, shuhudia lundo la mashoga wa Kitanzania waliojitundika huko, wakifanya vitu vichafu kabisa, huku wakiwa na “followers” hadi laki kadhaa, hao si tu ni Watanzania wenzetu bali ni miongoni mwa sisi ‘wapinga ushoga.’ Unafiki wa daraja la kwanza.
Na sababu kuu tunayoitumia kupinga ushoga ni imani zetu za kidini. Na kwa hakika tumeshika dini kweli, hasa kwa kuangalia jinsi nyumba za ibada zinavyojaa. Lakini kuthibitisha unafiki wetu, ucha-Mungu huo sio tu umeshindwa kudhibiti kushamiri kwa ushoga (na usagaji) bali pia kutuzuia tusishiriki kwenye maovu katika jamii.
Kwa taarifa tu, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa miaka michache iliyopita na taasisi ya Pew ya Marekani, Watanzania tunaongoza duniani kwa kuamini ushirikina. Na kwa mujibu wa taarifa ninazozipokea kutoka huko nyumbani, ushirikina umeshamiri mno kiasi kwamba sasa ni kama sehemu ya kawaida ya maisha ya Watanzania.
Wacha-Mungu lakini tumebobea kwenye ufisadi, rushwa, ujangili na biashara ya dawa za kulevya. Na asilimia kubwa ya kipato haramu kinachotokana na uhalifu huo kinachangia kushamiri kwa “michepuko” na “nyumba ndogo.”
Mfano wa karibuni kabisa kuhusu unafiki wetu ni katika mshikemshike unaoendelea hivi sasa huko nyumbani (Tanzania) ambao watu kadhaa maarufu aidha wametakiwa kuripoti polisi au ‘kuhifadhiwa’ na polisi wakichunguzwa kuhusiana na biashara ya dawa za kulevya. Hali hiyo inatokana na tangazo rasmi la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ‘kujitoa mhanga’ kukabiliana na biashara hiyo haramu.
Lakini licha ya kuwepo kwa lundo la lawama mfululizo kwa serikali kuwa imekuwa ‘ikiwalea’ watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya, tangazo la Makonda limesababisha kuibuka kwa lawama lukuki dhidi yake, huku wengine wakidai anatafuta ‘kiki (sifa) za kisiasa’ na wengine kudai amekurupuka kwa kutaja majina ya watu maarufu, na wengine wakimlaumu kwa kukamata ‘vidagaa’ na kuacha ‘mapapa.’
Kwa watu hao, na wapo wengi kweli, Makonda atashindwa kama alivyoshindwa kwenye amri zake nyingine. Sawa, rekodi ya Mkuu wa Mkoa huyo katika ufanisi wa maagizo yake sio ya kupendeza. Hata hivyo, kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, kiongozi sio tu ametangaza vita dhidi ya biashara ya dawa za kulevya bali pia ametaja baadhi ya majina ya wahusika, na kuwafikisha polisi. Hili ni tukio la kihistoria.
Lakini ‘wapinzani’ wa RC Makonda sio wananchi wa kawaida tu. Kuna ‘wapinzani wa asili,’ mbunge wa Chadema, Tundu Lissu, ambaye aliandika ujumbe mtandaoni, “kuwataja vidagaa na kuwaacha nyangumi/papa si ajabu ni moja kati ya mambo ya ovyo ya awamu ya tano.” Huyu ni mnafiki wa mchana kweupe. Sasa kama anawajua hao nyangumi/papa si awataje?
Kilichonisikitisha zaidi ya vyote ni kauli za Waziri Nape Nnauye alipozungumza na waandishi wa habari huko Dodoma. Pamoja na mambo mengine, Waziri Nape alidai kuwa, “ …watumiaji ni wengi lakini wanaoonekana zaidi ni wale wenye majina makubwa,” (sijui kwa mujibu wa utafiti gani); “Kama wizara tunaunga mkono juhudi za kupambana na dawa za kulevya, tatizo ni namna ya kushughulika na wahusika ikiwemo busara” (sijui alitaka tatizo lishughulikiwe kwa namna gani – na kwa nini hakuongoza kwa mfano kwa kutumia namna hiyo – na sijui busara ipi iliyokosekana katika utekelezaji wa agizo la Makonda); “Tunaunga jitihada za mapambano lakini ni vizuri lifanywe katika namna ya kulinda haki ya mtuhumiwa ili heshima yake isipotee” (haelezi hiyo ‘namna ya kulinda haki ya mtuhumiwa ili heshima yake isipotee’ ni kitu cha aina gani)
Nilimshutumu vikali Waziri Nape kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter (nilim-tweet yeye mwenyewe), na kumweleza bayana kuwa alihitaji kutumia busara badala ya kukurupuka kutetea wasanii wanaotuhumiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya. Kadhalika, kama mtendaji wa serikali, alikuwa na nafasi nzuri kuzungumza na watendaji wenzake wa serikali faragha badala ya kuongea suala hilo hadharani. Kadhalika, kuonekana anahofu zaidi kuhusu “brand” (thamani/hadhi ya msanii, kwa tafsiri isiyo rasmi) badala ya athari kubwa zinazosababishwa na biashara ya dawa za kulevya sio busara hata kidogo.
Nihitimishe makala hii kwa kutoa wito kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba naye ajitokeze hadharani kuongelea suala hili maana amekuwa kimya mno. Awali, naibu wake alipohojiwa na wanahabari alikuwa mkali na alitoa kauli zisizopendeza. Ili vita hii ifanikiwe ni lazima serikali iwe kitu kimoja na viongozi na wananchi kwa ujumla waache unafiki, na wampe ushirikiano RC Makonda na Jeshi la Polisi.
Tanzania bila dawa za kulevya inawezekana

Barua-pepe: [email protected] Blogu: www.chahali.com Twitter: @chahali

7 Feb 2017

Related image

Mara "Makonda hili, Wema lile," mara "Mapapa, mara vidagaa." Habari kama hizo zinaumiza vichwa. Hata hivyo, kuna habari tamu, na zisizoumiza kichwa,  kwa wapenzi wa mifululizo (series) ya tamthiliya za kishushushu. Hapa twaongelea HOMELAND na 24. Zimerejea hewani kwa kasi mpya, ari mpya na nguvu mpya. Haha!

Season 6 ya Homeland imeshafika episode ya tatu sasa, na kila episode ni nzuri mno. Yaani hizo dakika 55 za kila episode ni kama zinayeyuka tu. 
Sekou
Katika episode ya kwanza, Sekou Bah, kijana Mmarekani Mweusi Muislam, ana-post video mtandaoni baada ya kurekodi katika maeneo ambayo siku za nyuma kulitokea matukio ya kigaidi. Baadaye anakamatwa na shushushu wa FBI Ray Collins na kufunguliwa mashtaka ya ugaidi.

Carrie, sasa ni mfanyakazi katika shirika lisilo la kutengeneza faida (not-for-profit organisation) linaloshughulikia kuwatetea Wamarekani Weusi walio Waislam. Anakutana na Sekou ili kuwa wakili wake.

Pia Carrie anamtembelea Quinn ambaye ni kama amewehuka kutokana na kuwekwa chumba chenye gesi ya sumu, katika hitimisho la season 5. 
Saul na Dar Adal ni mabosi wa ushushushu, na wanampa taarifa Rais mteule, mwanamama Elizabeth Kaine. Baada ya briefing hiyo, Dar anaelezwa hofu yake kuhuthu uimara wa Rais Mteule, na baadaye anakutana na jasusi wa Mossad, Tovah Rivlin.

Katika Episode ya Pili, Carrie na Reda, profesa wa sheria anayefanya kazi na Carrie, wanamuuliza Sekou kuhusu dola 5,000 zilizokutwa na FBI chini ya kitanda chake. FBI wanadai fedha hizo ni kwa ajili ya Sekou kuzipeleka Nigeria kuwasaidia Boko Haram.
Reda na Carrie
Carrie anakuja kubaini kuwa fedha hizo zilitolewa na FBI kwa rafiki wa Sekou aitwaye Saad, ambaye ni mtoa habari wa FBI, ili kumpeleleza zaidi Sekou. Carrie anamvaa Saad, ambaye baadaye anaripoti kwa FBI kuwa ametishiwa na Carrie, na hiyo inatishia uwezekano wa Sekou kupew adhabu nafuu.

Dar Adal akutana na Rais Mteule Keane kumhabarisha kuhusu programu ya nyukilia ya Iran kwa kushirikiana na Korea ya Kaskazini. Saul amtembelea Carrie na kumtuhumu kuwa ni mshauri wa siri wa Rais Mteule Keane. Dar apata picha za siri zinazomwonyesha Carrie akiingia Ikulu kwa siri.

Katika episode ya tatu, Carrie anamjulisha Sekou kuwa (yeye Carrie) 'amelikoroga' kwa kuongea na Saad, na sasa FBI wanataka kudai kifungo cha miaka 15 kwa Sekou badala ya miaka 7. Sekou anaghadhibika, anamtimua Carrie, ambaye anajisikia vibaya. Hata hivyo, anafanikiwa kupata rekodi ya siri ya maongezi kati ya Conlin wa FBI na Saad, na anaitumia kama turufu yake.
Saul
Saul anafika Abu Dhabi ili kumhoji Farhad Nafisi, 'mtu wa mafedha' wa Iran. Nafisi anajiingiza mkenge hadi kukamatwa baada ya kumtembelea kahaba ambaye kumbe ni afisa wa Mossad. Mahojiano hayazai matunda, japo Nafisi anapewa kibano kikali. Baadaye Saul anaripoti kwa Dar kuwa hakupata lolote, lakini Dar anatoa taarifa tofauti kwa Rais Mteule, kitu ambacho baadaye Carrie anamfahamisha Rais Mteule

Hiyo ndo HOMELAND SEASON 6 ilipofikia hadi sasa. Episode 4 itarushwa wiki hii. Nitakueleza hapo chini jinsi unavyoweza kuona tamthiliya hii na nyinginezo bure. 

Sintoongelea 24 kwa leo kwa sababu ndo kwanza natarajia kuangalia episode ya kwanza kati ya mbili zilizokwishaoonyeshwa. Hata hivyo, nimesoma 'reviews' zake, zote zinaisifia kwa kiwango cha juu. Ila tu ni kwamba Jack Bauer hayupo, na badala yake ni staa mweusi Corey Hawkins, aliye-act kama Dr Dre kwenye filamu ya Straight Outta Compton.



Sasa, ukitaka kuangalia Homeland, 24 na series yoyote ile, au filamu, au mechi za soka kimataifa, unahitaji kitu kinaitwa KODI. Hiki kinageuza runinga ya kawaida kuwa 'smart TV.' Kama hujawahi kufahamu kuhusu 'smart tv,' basi kwa kifupi ni zenye uwezo wa kufanya kazi kama kompyuta, ikiwa ni pamoja na kutumia internet kwenye TV hizo.

Maelezo ya jinsi ya kutumia KODI yapo HAPA. Nitaelezea kwa kirefu kuhusu kifaa hicho, kwenye mada zangu kila wikiendi kupitia #ElimikaWikiendi

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.