18 Mar 2019


 
Leo Machi 18, 2019 ni siku ambayo lazima iingie kwenye vitabu vya kumbukumbu kwa sababu kuu tatu, ambazo zote zinamhusu mwanasiasa mkongwe Seif Sharif Hamad na Chama cha Wananchi (CUF)

Sababu ya kwanza, leo ni siku ambayo mwanasiasa huyo, maarufu kwa jina la Maalim Seif, "ametimuliwa" rasmi kutoka chama alichoshiriki kukiasisi (CUF).
Kibaya zaidi, "kutimuliwa" huko kumekuwa na baraka kisheria, baada ya Mahakama Kuu kumtambua Profesa Ibrahim Lipumba kuwa mwenyekiti halali wa chama hicho.

Ikumbukwe tu Lipumba alitangaza kujiuzulu uenyekiti kwa sababu anazozijua yeye kabla ya kuamua kurejea kwenye wadhifa huo "kwa mabavu." Kwa bahati mbaya – au pengine makusudi – sheria na kanuni za CUF zilikuwa zinatoa mwanya kwa Lipumba (au mwanasiasa mwingine yeyote yule) kufanya "uhuni" kama huo.

Sababu ya pili, ni kwamba leo CUF imekabidhiwa rasmi kwa Lipumba. Kisheria. Mahakama imetenda haki kwake kwa sababu japo alichofanya ni uhuni, kisheria uhuni huo ulihalalishwa na CUF yenyewe.

Hili la Lipumba kukabidhiwa chama si jambo dogo. Kuna mawili hapa. Moja, hii inaweza kuwa fursa nzuri kwa Lipumba kukijenga chama hicho na hatimaye kukirejesha kwenye nafasi ya kuaminika kama "mbadala wa CCM."

Lakini la pili, na hili ndilo ninahisi litatokea, ni mwanzo wa mwisho wa CUF. Sio siri kuwa Lipumba amesaidiwa sana na CCM kuipora CUF kutoka mikononi mwa Maalim Seif. CCM hawajafanya hayo kwa vile wanampenda Lipumba.Hapana. Wanamtumia tu kumdhibiti Maalim Seif ambaye licha ya kila hujuma zilizokuwa zikifanywa na CCM na taasisi zake, ameendelea kuwa mwanasiasa maarufu zaidi kuliko wote katika siasa za Zanzibar.

Sasa, baada ya Lipumba kutumika "kummaliza Seif ndani ya CUF," kuna uwezekano wa aina mbili tu. Wa kwanza ni kwa mwanasiasa huyo msomi kukubali kuendelea kutumika kama kibaraka wa CCM huku CUF ikigeuka kuwa CCM-B, na wa pili, ni kujaribu kusimama kama chama halisi cha upinzani na hapohapo "kumwagiwa radhi na CCM" na hatimaye kupelekea kifo cha chama hicho.

Uwezekano mkubwa zaidi ni huo wa kwanza - ukibaraka. Kwamba CUF haitokufa. CUF itaendelea kushiriki chaguzi mbalimbali. CUF itajenga taswira ya chama kamili cha upinzani. Lakini uwepo huo wa CUF hautokuwa kwa manufaa ya chama hicho au siasa za upinzani bali kwa manufaa ya CCM.

Kuna kila dalili kuwa CCM itaisaidia CUF kujitanua nchi nzima kwa sababu moja kuu: uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 utakuwa mbovu kuliko chaguzi zote zilizowahi kutokea Tanzania. Kuna uwezekano mkubwa tu kwa baadhi ya vyama vikuu vya upinzani kutishia kususia uchaguzi huo. Na hapo ndipo CUF ya Lipumba itakapotumika kuhalalisha "ushindi wa Magufuli/CCM."

CCM itaisaidia CUF kuweza kusimamisha wagombea takriban kila jimbo kwa upande wa Tanzania Bara. Lakini pia CCM itaisaidia CUF kuendelea kuwa chama imara cha upinzani huko Zanzibar, ambako uimara wake utasaidia kugawa kura dhidi ya CCM na wagombea wake.

Hata hivyo, "laana ya kutumika" itaikumba CUF baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 na kama isipoishia kusambaratika basi itabaki "chama jina" kama TLP ya Mrema.

Kuhusu uamuzi wa Maalim Seif kuhamia ACT- Wazalendo, japo hatua hiyo inaweza kuwashangaza baadhi ya watu, ukweli mchungu baada ya Mahakama Kuu kuhalalisha "uhuni" wa Lipumba, sambamba na "uhuni" wake mwingine majuzi ambapo "alijitangaza" kuwa Mwenyekiti kupitia "uchaguzi mkuu hewa" ambao pia "ulimtimua Maalim Seif" kwa kuteua mtu mwingine kushika wadhifa wa Katibu Mkuu.

Kwa kuzingatia muda mfupi uliosalia kabbla ya uchaguzi mkuu wa mwakani, Maalim Seif kuendelea kutafuta haki yake mahakamani kungeweza kumkuta akiwa bado kwenye korido za mahakama wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu ujao. Ni vigumu mno kwa chama cha siasa kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi mkuu huku kikiwa kinakabiliwa na mpasuko katika uongozi wake wa juu.

Kwahiyo, kimkakati, uamuzi huo wa Maalim Seif unaeleweka, na unaweza kuwa ni mbinu muhimu kwake kuendelea kuwa relevant kisiasa.

Hata hivyo, kuna uwezekano wa aina mbili kuhusu mustakabali wa Maalim Seif na wa chama chake kipya cha ACT- Wazalendo.

Uwezekano wa kwanza ni kwa chama hicho kuibuka kuwa tishio katika siasa za Tanzania. ACT – Wazalendo ni chama kizuri lakini ambacho hakikui. Kimeendelea kuwa "chama cha mtu mmoja" chini ya uongozi wa Zitto Kabwe. Kwa muda mwingine, chama hicho kimekuwa cha kiharakati zaidi kuliko cha kisiasa.

Mapungufu hayo yanaweza kubadilika kwa njia kuu tatu. Kwanza, Maalim Seif hajawahi kupata fursa nzuri ya kunadi mvuto wake kwenye majukwaa ya siasa za Tanzania Bara. ACT-Wazalendo wanaweza kuwa Jukwaa muhimu katika hilo.

Pili, Zitto  hajawahi kupata jukwaa mwafaka kunadi mvuto wake wa kisiasa huko Zanzibar. Kwa kuungana na Maalim Seif, hii inaweza kuwa ndio fursa mwafaka kwake.

Tatu, ACT-Wazalendo kama chama inaweza kupata fursa mwafaja kabisa ya kuwa chama cha kitaifa badala ya kuwa "chama cha Kigoma."

Haya yote yatawezekana tu endapo kutakuwa na "kujitoa mhanga" kati ya mwenyeji Zitto na mgeni Maalim Seif. Kwa mara ya kwanza, Zitto atajikuta akiongoza chama ambacho ndani yake kuna mwanasiasa maarufu zaidi yake. Naam, Maalim Seif ni mkongwe zaidi kisiasa kuliko Zitto. Endapo Zitto "atajitoa mhanga" (make a sacrifice) na kukubali "kumezwa" na umaarufu wa Maalim Seif, basi chama hicho kitakuwa na fursa kubwa ya kupanuka zaidi na hata kuja kuwa chama kikuu cha upinzani katika pande zote za Muungano.

Lakini endapo kutakuwa na mgongano wa ego kati ya wanasiasa hao, basi mustakabali wa chama hicho utakuwa mashakani. Lakini pengine uwezekano wa hili kutokea ni mdogo kutokana na ukweli kwamba suala la Maalim Seif kujiunga na ACT-Wazalendo sio limetokea tu ghafla. Ni dhahiri kuwa kulikuwa na majadiliano ya muda mrefu na yayumkinika kuhisi kwamba tofauti kati ya wanasiasa hao wawili (Maalim Seif na Zitto) zilifanyiwa kazi wakati wa majadiliano hayo.

Suala jingine ambalo linaweza kuijenga ACT-Wazalendo "mpya" (ya Zitto na Maalim Seif) au kuibomoa ni mtihani ulioikumba Chadema mwaka 2015.

Kwa mwelekeo ulivyo ndani ya CCM ambapo Magufuli hafanyi siri kuwa anataka chama hicho kiwe chini ya uongozi wa watu wake (wengi wao wakiwa wana-Kanda ya Ziwa wenzake), kuna uwezekano mkubwa wa kuibuka wimbi kubwa tu la wanasiasa wenye majina watakaotaka kuhamia Upinzani. Na endapo Zitto na Maalim Seif watakuwa "dream team" ya kuaminika, basi ACT-Wazalendo inaweza kuwa na mvuto zaidi kwa "wakimbizi kutoka CCM" kuliko Chadema.

Si ajabu kwa wanasiasa kama Nape Nnauye, Mwigulu Nchemba, Bernard Membe kujiunga na ACT-Wazalendo endapo chama hicho kitaonekana kuwa kinaweza kutoa ushindani wa dhati dhidi ya CCM hapo mwakani.

Sasa, wakati kupokea "majina makubwa" kutoka CCM husaidia kuongeaza umaarufu wa chama, uzoefu umeonyesha kuwa wengi wao wenye majina hayo makubwa ni wanafiki wanaokwenda upinzani kwa sababu zao binafsi na sio kwa maslahi ya vyama husika vya upinzani.
Kibaya zaidi, kila ujio wa "wahamiaji" hao ni fursa mwafaka kwa CCM kupandikiza "mamluki" wake kama ilivyotokea kwa Chadema ilipompokea Lowassa mwaka 2015.

Je ACT-Wazalendo "mpya" inaweza kutoa upinzani wa dhati dhidi ya CCM hapo mwakani? Jibu fupi ni "muda ndio utaongea" (time will tell). Jibu pana zaidi ni kwamba japo uwezekano huo upo lakini sidhani kama muda unatosha kukitanua chama hicho nchi nzima hususan katika kipindi hiki ambacho chama pekee cha siasa kinachoruhusiwa kufanya shughuli za siasa ni CCM tu.

Hata hivyo, endapo mkazo wa ACT-Wazalendo utakuwa katika sio tu kuongeza idadi ya wanachama bali kujenga kuaminika kwa "Watanzania wasio na vyama," basi huenda chama hicho kikafanya vizuri kwenye uchaguzi mkuu huo.

Ni hivi, kundi muhimu kabisa la wapigakura katika uchaguzi mkuu wowote ule nchini Tanzania ni "Watanzania wasio na vyama." Kwamba, hakuna chama cha upinzani kinachohitaji kupoteza muda wake kuwashawishi wafuasi wa CCM wakipigia kura, kama ambavyo CCM haina muda na wafuasi wa upinzani kuwashawishi waipigie kura. Vilevile, si CCM wala vyama vya upinzani vinavyohitaji kuwashawishi wanachama/wafuasi wao wapigie kura vyama vyao. Watu wanaohitaji kushawishiwa ni hao wasio na vyama. Na habari njema ni kwamba kundi hilo ndilo lwenye idadi kubwa zaidi ya wapiga kura.

Kwa mujibu wa takwimu zisizo rasmi, CCM ina takriban wanachama milioni 8 ilhali wapinzani wana wanachama takriban milioni 5. Kwa makadirio, takriban Watanzania milioni 25 walijiandikisha kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Kwahiyo, milioni 8 wa CCM jumlisha milioni 5 wa upinzani jumla inakuwa milioni 13. Ukichukua milioni 25 kutoa miloni 13 unabakiwa na milioni 12. Kwa makadirio, hawa ni "wapigakura wasio na vyama." Na kimahesabu, hata nusu tu ya kundi hili likielemea upande mmoja, upande huo unaweza kabisa kushinda uchaguzi husika. Of course, hapo tunaweka kando hujuma za kawaida za kuibeba CCM kwenye takriban kila uchaguzi mkuu.

Nimalizie kwa kukumbusha kuwa uchambuzi huu sio exact science. Umeelemea kwenye uelewa wa kutosha wa mchambuzi kuhusu siasa za Tanzania.

Kadhalika, uchambuzi huu ni endelevu. Utafanyiwa marejeo mara kwa mra kila kutakapokuwa na umuhimu wa kufanya hivyo


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.