19 Mar 2020

Ili uielewe vema makala hii ni vema ufanye kulinganisha kinachojiri Tanzania muda huu baada ya kutangazwa kuingia kwa Coronavirus na kinachojiri katika nchi jirani ambazo pia zimekumbwa na janga hilo la kimataifa.

Tuanze na Kenya. Mara baada ya kuthibitika kuwa taifa hilo lina mgonjwa mmoja aliyeambukizwa maradhi hayo, Rais Uhuru Kenyatta aliongea na Wakenya ambapo pamoja na mambo mengine aliwahakikishia kuwa serikali yake ipo nao bega kwa bega katika kipindi hiki kigumu.
Twende Afrika Kusini. Mara baada ya kufahamika kuwa nchi hiyo imekumbwa na Coronavirus, Rais Cecil Ramaphosa aliwapatia Waafrika Kusini taarifa hiyo huku akitanabaisha kuwa hakuna sababu yakuona aibu wala kuficha taarifa hiyo kwa sababu ugonjwa huo umezikumba nchi nyingine pia.
Kwa majirani zetu wa Rwanda, Rais Paul Kagame alikwenda hatua kadhaa mbele kwa kujipanga vilivyo dhidi ya Coronavirus kabla haijaingia nchini humu ambapo licha ya kuweka sehemu za kuosha mikono katika maeneo mbalimbali,
Rais Kagame alimtimua Waziri wake wa Elimu kwa kutoa taarifa za uongo kuhusu vifaa kwa ajili ya Coronavirus.
Na baada ya nchi hiyo kukumbwa na janga hilo, Rais huyo aliongea na Wanyarwanda na kuwataka wachukue hatua za tahadhari badala ya kuwa na hofu tu.
Na kwa majirani zetu wa DRC, Rais Felix Tshisekedi alihutubia taifa na kueleza mikakati mbalimbali ya serikaliyake katika kupambana na janga hilo la Coronavirus.
Nchini Ethiopia, Waziri Mkuu Ahmed Abiy amekwenda mbali zaidi ya kuwajali Waethiopia wenzie na amefanikiwa kupata sapoti ya mmoja wa matajiri wakubwa duniani Jack Ma, kutoa sapoti kwa mataifa mengine ya Afrika kupambana na janga la Coronavirus.

Na huko Uganda, licha ya nchi hiyo kutokuwa na maambukizi yoyote ya Coronavirus, Rais Yoweri Museveni amehutubia taifa na kutangaza hatua kadhaaza kujikinga dhidi ya janga hilo
Sasa turudi Tanzania kwetu. Mara ya mwisho kwa Rais Magufuli kusikika na kuonekana hadharani ni majuzi ambapo sio tu alidai kuwa Coronavirus haijaingia nchini Tanzania (japo masaa machache baadaye Waziri wake, Ummy Mwalimu alitangaza kuwa in fact tayari Tanzania ina mgonjwa mmoja mwenye maradhi hayo) bali pia hakutangaza hatua zozote za msingi kukabiliana na ujio wa janga hilo. Na kama mzaha vile, alikiri kuwa alikosea kusababisha mkusanyiko wa watu kusikiliza hotuba yake.

Lakini siku hiyohiyo, Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt Abbasi aliongea upuuzi mkubwa dhidi ya Watanzania walioonyesha hofu kuhusu janga la Coronavirus.
Masaa machache baadaye, Waziri wa Afya Ummy Mwalimu akatangaza kuwa Tanzania ina mgonjwa mmoja wa Coronavirus.
Na Waziri Ummy amegeuka simulizi baadaya kupatikana video hii ambapo anatanabaisha kuwa Tanzania haiwezi kukabiliana na Coronavirus.
Tangu tutangaziwe uwepo wa ugonjwa huo hatujamsikia tena Magufuli. Sijui amejificha wapi. Na kama ilivyozoeleka katika nyakati za majanga, "ghafla" Waziri Mkuu Kassim Majaliwa "amekuwa Waziri Mkuu tena"
 ambapo ndio amekuwa "sauti ya serikali" kuhusu hatua mbalimbali dhidi ya janga hilo, ikiwa ni pamoja na hatua ya kufunga shule za awali, msingi na sekondari na vyuo.

Lakini uzeofu unaonyesha kuwa kila inapotokea Tanzania kukumbwa na janga fulani, Magufuli hukwepa dhamana aliyonayo kama "comforter-in-chief," yaani "mfariji mkuu wa taifa." Uthibiisho kuhusu hilo upo kwenye matukio mengi lakini pengine tukio lililoacha kumbukumbu ya muda mrefu kwa Watanzania ni dharau alizowafanyia wahanga wa tetemeko la ardhi huko Kanda ya Ziwa.

Licha ya yeye kuwa mzaliwa wa eneo hilo, alikaa muda mrefu bila kwenda kuwapa pole wahanga wa tetemeko hilo, na alipokwenda "akawasemea ovyo."

Huu si wakati wa kulaumiana lakini pia huu si wakati wa kuzembea. Ni kwa minajili hiyo nimekuwa nikitoa wito kwa viongozi wakuu wa Upinzani, Mheshimiwa  Zitto Kabwe, Mheshimiwa Freeman Mbowe na Mheshimiwa Maalim Seif kutoa ninachokiita "uongozi mbadala wakati huu ambapo Tanzania inakabiliwa na janga kubwa la Coronavirus.
Na endapo Magufuli hatobadilika, kwa maana ya "kuendelea kujificha," basi Watanzania watakuwa na kila sababu ya kutomhitaji tena kwenye uchaguzi mkuu ujao hapo Oktoba mwaka huu

Nimalizie makala hii kwa kukumbushia umuhimu wa kuchukua hatua binafsi dhidi ya maambukizi ya ugonjwa huu hatari wa Coronavirus. Nimekutengenezea video hii fupi

 Mungu atulinde sote. Amen.

17 Mar 2020


Imeniwia vigumu sana kuandika makala hii fupi lakini nalazimika kuiandika hivyo hivyo maana kukaa kimya is not an option. Kuna busara moja maarufu inayosema kinachohitajika kwa uovu kushamiri ni kwa watu wema kukaa kimya.


Hebu tutupie jicho mlolongo wa matukio jana kuhusu ishu ya Coronavirus.



Mnamo majira ya saa 4 asubuhi, "msema chochote" wa serikali anabwabwaja kuwazodoa wananchi wenye haki ya kuwa na hofu kuhusu Coronavirus.


Majira ya saa 7 mchana, Magufuli akawahadaa Watanzania kuwa Coronavirus haijaingia Tanzania

Na akaendelea kutawala anga za habari kwa "maigizo" yake yaliyomhusisha pia rafiki yake Kamwele.

baadaye kidogo Waziri Ummy akatangaza kuwa Corona virus imeingia rasmi Tanzania

Lakini ili uelewe vema sarakasi hizi ni muhimu utambue kuwa jana pia ilikuwa siku ambapo Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe alikuwa anaongea na Watanzania kupitia mkutano wake na waandishi wa habari.

Na huhitaji kuwa jasusi mstaafu kama mie kubaini kuwa sarakasi hizo za jana zililenga "kuharibu"  mkutano huo wa Mbowe.


Endapo walifanikiwa azma yao hiyo au la, wanajua wao.



Lakini si lengo la makala hii kuongelea "hujuma hiyo dhidi ya Mbowe," bali kutanabaisha kuwa Magufuli na serikali yake hawasemi ukweli kuhusu Coronavirus. 



Hata hivyo badala ya mie "raia wa kawaida" kuthibitisha kuwa kuna urongo unafanyika kuhusu suala hilo, nawapa changamoto viongozi wakuu wa upinzani, Mheshimiwa Mbowe na Mheshimiwa Zitto Kabwe kuchunguza suala hili na kisha kuwaambia Watanzania ukweli.



Rekodi ya Magufuli katika kudili na majanga ni mbovu mno. Kila mmoja wetu anakumbuka matusi yake kwa wahanga wa tetemeko la rdhi huko Kanda ya Ziwa (nyumbani kwake huko) kuwa si yeye aliyeleta tetemeko hilo.


Na akawadhihaki zaidi
Lakini kingine cha muhimu ni kwamba kama nilivyotahadharisha katika makala hii, Magufuli ni mtu anayetaka habari nzuri tu hata kama ni za hadaa. Na hili la Coronavirus sio tu ni habari mbaya lakini pia linaweza kuonyesha mapungufu makubwa ya utawala wake ambao umekuwa ukificha mapungufu hayo kwa kutumia ubabe dhidi ya uhuru wa kujieleza, kuvibana vyama vya upinzani na kuvifunga mdomo vyombo vya habari.

Nimalizie makala hii kwa kuwakumbusha Waheshimiwa Mbowe na Zitto kufuatilia hadaa waliyofanyiwa Watanzania kuhusu Coronavirus na ikiwezekana wao ndio wachukue uongozi wa umma katika kukabiliana na janga hili hatari. 



11 Mar 2020


Kusema hukumu nzito dhidi ya viongozi kadhaa wa Chadema iliyotolewa jana kuwa ni ishara mbaya kwa demokrasia nchini Tanzania ni kutoitendea haki hali ya demokrasia katika nchi yetu. Kilichotokea jana hakipaswi kuangaliwa kama tukio pekee bali mwendelezo wa matukio lukuki yaliyojiri tangu Rais Magufuli aingie madarakani takriban miaka mitano iliyopita.


Sidhani kama kuna haja ya kueleza kwanini hukumu hiyo ni ya uonevu uliopindukia kwani takriban kila mtu aliyekuwa anafuatilia mwenendo wa kesi hiyo anaelewa kuhusu hilo. Lakini pia, takriban kila anayefuatilia mwenendo wa Magufuli na demokrasia Tanzania anaelewa hali ikoje kwa sasa.



Kwahiyo, badala ya kutumia muda mwingi kulalamika ni vema kujaribu kutafuta suluhisho japo la muda mfupi kuhusu hali hiyo. Kwa bahati mbaya, uzoefu wangu binafsi kuhusu kuwashauri ndugu zangu wa Chadema haujawahi kuwa mzuri. Kila inapotokea aidha kuwashauri au kuwakosoa, huwa wakali kama pilipili huku wengine wakitumia lugha isiyofaa.



Yayumkinika kuhitimisha kuwa tofauti pekee kati ya Chadema na CCM when it comes to kuwakosoa, ni kwamba CCM ipo madarakani na Chadema wapo upinzani, lakini tabia zao wanapokosolewa ni sawa: hawataki kusikia ushauri wowote tofauti na mtazamo wao hata kama ni fyongo.



Ni muhimu kutambua kuwa unyanyaswaji unaofanywa na Magufuli kwa Chadema hakuanza jana. Tangu kiongozi huyo aingie madarakani hajawahi kuficha chuki yake dhidi ya Chadema. Na anayedhani kuwa kuna siku hali itabadilika, kwamba ghafla chuki hiyo itageuka upendo, basi kichwani hayupo vema.



Ndio maana baadhi yetu tulimshutumu vikali mwenyekiti wa taifa wa Chadema, Freeman Mbowe, alipomwomba Magufuli kuwe na MARIDHIANO. Lakini kama ilivyo kawaida ya wafuasi wa chama hicho, sio tu walimtetea Mbowe bali pia waliturukia kama mwewe sie tulioona mkakati huo ni fyongo.



It is this simple, huwezi kutaka maridhiano na mtesi wako. It simply doesn't work. Unawezaje kutaka maridhiano na mtu ambaye utawala wake umetawaliwa na matukio mabaya kabisa kuhusiana na wanasiasa na wanachama kadhaa wa Chadema?



Unasakaje maridhiano na Magufuli ilhali siku chache tu baada ya kuingia madarakani Kamanda Mawazo aliuawa kinyama?

Unatakaje maridhiano na Magufuli ambaye muda mfupi tu baada ya kuingia madarakani aliharamisha shughuli halali kikatiba za vyama vya upinzani ikiwa ni pamoja na Chadema?


Unatakaje maridhiano na Magufuli ambaye alimfunga mbunge Joseph Mbilinyi aka Sugu kwa "kosa feki"?

Image result for sugu afungwa

Unatakaje maridhiano na Magufuli ambaye utawala wake unapaswa kuwaeleza Watanzania alipo kada maarufu na mkosoaji mkubwa wa Magufuli, Ben Saanane?

Image result for bring back ben saanane
Unatakaje maridhiano na Magufuli ambaye utawala wake una damu za Diwani Luena na Katibu Kata Daniel?




Orodha ni ndefu lakini so far response ya Chadema imekuwa ya kusuasua




Na kibaya zaidi, baadhi ya tuonaguswa na madhila yanayowasibu tukijitolea kuwashauri twaishia kutukanwa.



Ni hivi, ili Magufuli alazimike kubadilika, ni lazima kuwa na "incentive" ya kumfanya abadilike. Naamini mmeona jinsi "shinikizo la mabeberu" lilivyomlazimisha amwachie huru mwandishi Eric Kabendera, aitishe mkutano wa kizushi na Maalim Seif, Mbatia na Lipumba, na amemtuma "Profesa aliyeokotwa jalalani" Kabudi aende kuomba suluhu huko Marekani. 



Pia sote ni mashuhuda wa jitihada binafsi za kiongozi mkuu wa chama cha ACT-Wazalendo kuishinikiza benki ya dunia isitoe mkopo kwa Tanzania zilivyozaa matunda. Chadema kama chama kikuu cha upinzani ilishindwa kuwa mstari wa mbele katika hili.



Na hadi wakati huu hakujawa na mwamko wa kitaifa kwa chama hicho kushinikiza mabadiliko katika mwenendo wa siasa za Tanzania. Na kichekesho ni kwamba ajenda kuu ya chama hicho kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ilikuwa MABADILIKO. Je ajenda hiyo ilikufa baada ya Lowassa kushindwa uchaguzi huo na hatimaye kukikimbia chama hicho?



Pengine hadi kufikia hapa, msomaji ambaye ni kada wa Chadema utakuwa umefura kwa hasira ukilaumu kuwa sionyeshi huruma kwa yanayokisibu chama hicho na viongozi wake. Nawaonea huruma sana lakini ni nadra kwa hisia pekee kuleta mabadiliko. Huruma kwa akina Mbowe na wanasiasa wengine wanaoteswa na Magufuli haiwezi kumfanya dikteta huyo abadilike.



Ieleweke kuwa chuki ya Magufuli kwa Chadema inatokana na ukweli kwamba chama hicho ndicho cha pili kwa ukubwa baada ya CCM na kina mtandao mpana wa nchi nzima, na licha ya kuwa chama kikuu cha upinzani, pia ni potential mbadala wa CCM. Kwahiyo, kwa Magufuli ambaye anajua fika kuwa akirogwa tu kutoka madarakani ataishia jela, ni lazima kwake kuibana Chadema kwa nguvu zake zote. Huyu si mtu wa kutaka maridhiano nae hata chembe.



Kwa vile lawama pekee hazijengi, nihitimishe makala hii kwa kuikumbusha tena Chadema kuwa dhamira kuu ya Magufuli ni kuhakikisha chama hicho kinakufa. Najua kuna wanaosema "hawezi kukiua chama hiki" lakini ukweli ni kwamba kifo cha chama cha siasa sio lazima kiwe kama kifo cha binadamu. Endapo dhamira ya Magufuli kuwa katika uchaguzi mkuu ujao Chadema isiambulie jimbo na kata hata moja itatimia, huo ni mwanzo wa kifo cha chama hicho. 



Simaanishi kuwa kitakufa kwa maana ya kutokuwa na mwanachama hata mmoja bali kitabaki "chama kama chama" kama ilivyo CUF ya Lipumba au TLP ya Mrema au NCCR ya Mbatia. Uwepo au kutokuwepo kwa vyama hivyo hakuna maana kwa Watanzania.



Lakini ukiwakumbusha Chadema kwa mifano hai kuwa Magufuli amedhamiria kwa dhati kukiangamiza chama chao, sana sana utaishia kuambulia matusi. 



Nini kifanyike? Kwa bahati mbaya imebaki mezi saba tu kabla ya uchaguzi mkuu ujao hapo Oktoba. Kwa maana hiyo, hakuna muda wa kutosha kwa chama hicho kuanzisha programu kabambe ya kupambana na udikteta wa Magufuli.



However, uchaguzi huo unaweza kutoa fursa ya "kuua ndege wawili kwa jiwe moja," - kutekeleza programu kabambe ya kukomesha udikteta wa Magufuli kama mkakati kabambe wa chama hicho kuingia Ikulu. Kwamba, kama ajenda fyongo ya MABADILIKO (ya Lowassa) ya mwaka 2015, safari hii ajenda iwe kukomesha udikteta wa Magufuli na hatimaye kumng'oa hapo Oktoba.



Lakini ili hilo liwezekane ni muhimu kwa chama hicho kuachana kabisa na mtazamo fyongo miongoni mwa viongozi wengi wa ngazi za juu wa chama hicho na makada mbalimbali kuwa "adui yao mwingine zaidi ya  Magufuli na CCM ni Zitto na ACT-Wazalendo." Kuna wahuni kwenye chama hicho kama "jasusi Yeriko" ambao wamekuwa wakijibidiisha kujenga chuki dhidi ya Zitto na ACT-Wazalendo kwa ujumla pasipo viongozi wa Chadema kukemea upuuzi huo. 



Japo muda ni mchache kabla ya uchaguzi mkuu ujao, lakini ushirikiano wa dhati kati ya Chadema na ACT-Wazalendo - na pengine makundi mengine ya kijamii (rejea wazo la Zitto kuhusu "united front") - pamoja na shinikizo kwa mabeberu ambao fedha zao ndio zinampa jeuri Magufuli, unaweza kabisa kumwondoa madarakani huyo dikteta kwa njia za amani. Uzuri ni kwamba mabeberu wanafuatilia kwa karibu kila kinachojiri Tanzania


Mwisho, japo ninawapa pole viongozi wa Chadema kwa madhila wanayopitia, wanachohitaji zaidi sio huruma yetu bali ujasiri wa kupambana na huyo dikteta kwa kila njia inayowezekana. Na japo sidhauri matumizi ya nguvu katika kudai haki, busara hii ya marehemu Profesa Kighoma Ali Malima bado ina relevance kubwa kwa wanasiasa wa upinzani ikiwa ni pamoja na Chadema.


9 Mar 2020


#Thread: Naamini kwamba takriban kila mmoja wetu - hata wale wenye uadui na news - wanafahamu kuhusu balaa jipya la virusi vya #Corona.

Na ni balaa kubwa kweli kweli, maana licha ya wataalam wa afya kutofahamu kwa undani hukusu virusi hivyo, kuna mambo kadhaa yanayoweza kulifanya janga hilo kuwa kubwa zaidi. Hadi wakati naandaa #thread hii, idadi ya maambukizi imevuka watu 100,000 na zaidi ya nchi 90 duniani zimeripoti kufikwa na janga hilo. Japo takriban nusu ya waliokumbwa na virusi hivyo wamepona, idadi ya maambukizi mapya inazua tafaruki kubwa. 

Lakini hofu kubwa zaidi ni pindi janga hilo litakaposambaa barani Afrika, bara ambalo linakabiliwa na changamoto lukuki. Tayari takriban nchi 8 za Afrika zimeripoti maambukizi ya virusi hivyo. Nchi hizo ni Misri, Aljeria, Naijeria, Senegal, Kameruni, Togo, Moroko, na karibu nasi (Afrika Mashariki) ni Afrika Kusini ambakoidadi ya maambukizi hadi jana ni watu wawili. 

Siku chache zilizopita nilihudhuria mkutano flani hapa Uskochi, na japo haukuhusu masuala ya afya, suala la virusi vya #corona liliibuka kwenye maongezi. Kilichonisikitisha ni kwamba watu wengi walionekana kudhani kuwa (a) hofu kuhusu virusi hivyo inakuzwa kuliko hali halisi (b) virusi hivyo ni sawa tu na vya mafua (flu)

Tunaishi katika zama ngumu kwa kweli. Ofkoz, tuna janga jingine (japo si hatari kama virusi vya #corona) na #fakenews. Na kwa hakika watu wana sababu za msingi kutoamini baadhi ya vyombo vya habari hasa kutokana na kasumba ya "kuongeza chumvi" au kuongopa waziwazi. 

Hata hivyo, licha ya kasoro hizo, tegemeo kubwa zaidila kupata jabari ni kwa kupitia vyombo vya habari hivyo hivyo ambavyo baadhi ya watu hawana imani navyo. Na yayumkinika kuamini kuwa endapo vyombo vya habari vikipuuzia kuhusu virusi vya #corona vitaishia kulaumiwa. 

Kuna "janga" jingine huko Marekani. Janga hili ni Donald Trump na wapambe wake. Kwa upande mmoja Trump na wapambe wake wanaamini kuwa "janga hilo la virusi vya #corona linakuzwa makusudi ili yeye aonekane hafai, na hivyo asichaguliwe tena kwenye uchaguzi mkuu ujao hapo Novemba."


Kwa upande mwingine, Trump na chama chake ni "maadui wa kudumu dhidi ya sayansi." Kwahiyo si jamba la kushangaza kusikia wengi wao wakidai "virusi vya #corona havina tofauti na vile vya mafua (flu)," na kwamba taarifa za wanasayansi na vyombo vya habari ni #fake news. 

Virusi vya #corona ni janga pia kwa sababu kutokana na "upya" wake, inawawia vigumu wataalam wa afya kufahamu vya kutosha kuhusu janga hilo, na hivyo kuwa ngumu kwao kupambana nalo. Ni vigumu kukabiliana na adui usiyemjua vizuri. 

Lakini kama "upya" huo wa virusi hivyo hautoshi kuwa janga kubwa, kuna tatizo jingine la jinsi maambukizi yanavyosambaa kwa kasi. Kwahiyo kwa upande mmoja kuna "race against time" kutafuta chanjo na/au tiba, na kwa upande mwingine ni kukabiliana na maambukizi mapya. 

Ni kwamba, hata mtu akiona dalili zakuwa na virusi vya #corona, anapokwenda hospitali anaweza asipatiwe tiba "ya maana" zaidi ya "tiba ya mafua" kwa sababu hadi muda huu hakuna tiba dhidi ya virusi hivyo. Nimetanabaisha awali kuwa janga hili likisambaa barani Afrika itakuwa balaa kubwa hasa kwa sababu bara hilo linakabiliwa na chngamoto nyingi.

Changamoto hizo ni pamoja na umasikini. Licha ya umasikini ambao umedumu miaka nenda miaka rudi huku baadhi ya wanasiasa wakishindana kutumia #fakenews kuwaaminisha wananchi kuwa umasikini unapungua, kuna umasikini unaochangiwa na vipaumbele fyongo vya serikali zilizo madarakani. 

Pengine ni vema kutumia mifano hai. Kwa mfano wa Tanzania yetu, wakati ununuzi wa bombadia ni muhimu, uwekezaji kwenye sekta ya afya ni muhimu zaidi. Na hauhitaji kuwa mwelewa sana wa Tanzania yetu kubaini kuwa mabilioni yaliyotumika kununua bombadia yalihitajika zaidi mahospitalini.

Kwahiyo moja ya sababu zinazochangia umasikini wa nchi nyingi za Afrika ni vipaumbele fyongo vya watawala. Na japo twaombea Mola aepushe janga hilo lisifike huko nyumbani, vipaumbele vya watawala wetu ni moja ya vikwazo hata wakati huu. 

Kama ambavyo Trump yupo bize kuonyesha kila kitu kipo vizuri huku maambukizi yakisambaa, watawala wetu nao wapo bize kujigamba kuwa "tupo vizuri" ilhali twaelewa vema kuwa wababaishaji hawa hawana A wala B wajualo katika kujiandaa kukabiliana na janga hilo. 

Na majuzi tu tumeshuhudia lundo wa watalii kutoka China wakiwasili huko KIA. Yaani wakati nchi zilizopiga hatua kubwa kimaendeleo zikidhiditi wasafiri kutoka China, sie hohehae twafanya ubishi katika suala hatari kama hili. Niliandika kirefu kuhusu hilo katika makala hii "Hatuna Uhaba Wa Vingozi Wapumbavu Lakini Hili La Kupuuza #Coronavirus Ni Zaidi Ya Upumbavu (bit.ly/2wHI8oA)

Wakati tunapaswa kuendelea kumuomba Mola ili janga hilo lisitie mguu huko nyumbani, ni muhimu pia kujiandaa kisaikolojia endapo (God forbid) hatimaye litafika huko.atuna Uhaba wa Viongozi Wapumbavu Lakini Hili La Kupuuza #Coronavirus Ni Zaidi Ya Upumbavu

Kuna watakaolaumu kuwa "unatisha watu bure) lakini naamini kuwa ni vema kuchukua tahadhari kabla ya hatari. Majuzi, Rais Cecil Ramaphosa wa Afrika Kusini alipotangaza kuwa tayari nchi hiyo ina mgonjwa mmoja (wapo wawili hadi wakati naandika makala hii), alitanabaisha kuwa haoni haja ya kuficha ukweli kuwa nchi hiyo nayo imekumbwa na janga hilo. 

Nimegusia hilo kwa sababu utawala wa wa Rais @Magufuli umekuwa maarufu mno kwenye "kanusha,kanusha, na kanusha zaidi." Ni utawala unaotaka kuongelea "habari njema" tu. Je kwa bahati mbaya, virusi hivyo vikiingia Tanzania (Mola aepushie mbali hili), hawatokanusha pia? 

Enewei, lengo la #thread hii sio kuzungumzia vitu vya kufikirika - kwa mfano hali itakuwaje pindi virusi vya #corona vikiingia Tanzania - japo ni muhimu kuchukua tahadhari kabla ya hatari. Badala yake, lengo ni kutoa elimu kuhusu virusi hivyo, kwa lugha rahisi kueleweka. Na kwa vile mie sio tabibu, nitaeleza kwa lugha isiyo ya kitalaamu/kitaaluma, kwa kimombo wanasema "in layman's language."

Kwanza, wakati janga hilo linafahamika zaidi kwa jina la virusi husika, yaani #coronavirus, maradhi yanayotokana na maambukizi ya virusi hivyo yanafahamika kama COVID-19, kifupi cha "Corona Virus Disease 2019."

Japo kama nilivyoeleza awali kuwa mengi hayafahamiki kuhusu virusi na maradhi husika, watu walio kwenye hatari zaidi ya maambukizi ni ambao tayari wana magonjwa mengine na watu ambao kinga za mwili ni pungufu. Kundi hili linajumuisha watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi. 

Lakini kana kwamba habari hiyo sio mbaya, kwa Afrika kuna tatizo la ziada kuhusu "uhusiano kati ya virusi vya #corona na watu ambao tayari wana maradhi mengine." Kutokana na sababu mbalimbali, kuna idadi kubwa ya watu barani Afrika ambao wana "maradhi mengine" lakini hawafahamu. Aidha hawafahamu kwa vile hawajafanya jitihada ya kufahamu kuhusu afya zao au hawajafahamu kwa sababu wana vipaumbele vingine muhimu zaidi ya kufahamu kuhusu afya zao.

 Kuna watu wanakwepa kupima ukimwi kwa vile "wana mambo mengi mno kichwani, na wasingependa kuongeza mengine (kama kubaini wana ukimwi baada ya kupima).Na huwezi kumlaumu mtu "anayekwepa habari mbaya kwa vile hata akijua hatojua cha kufanya kuhusu habari hiyo mbaya.

Kingine cha kuogofya kuhusu virusi hivyo ni ukweli kwamba ni vigumu mno kukwepa "mikusanyiko" katika maisha yetu ya kila siku barani Afrika. Hebu pata picha ya sehemu kama "Shimoni Kariakoo" au kwenye jinsi daladala zinavyopenda "nyomi" (hivi msamiati huu bado hai?)

Kama nilivyotanabaisha awali, kuna wanaodai "COVID-19 ni sawa na mafua tu." Japo mie si mwanasayansi, lakini kwa mujibu wa takwimu zilizopo, wakati "kiwango cha vifo" (mortality rate) kwa mafua ni 0.1%, kwa upande wa COVID-19 tayari ni 2.5% na huenda kiwango hicho kikaongezeka. 

Hata hivyo, kiwango hicho ni kidogo kulinganisha na "majanga" mengine kama Ebola, ambayo "mortality rate" yake ni kati ya 25% na 90%. Again, hali inaweza kuwa mbaya zaidi kwa upande wa COVID-19 kutokana na kusambaa kwake kwa kasi. 

Wengi wa wanaopatwa na maambukizi ya virusi vya #corona huwa na dalili kama za homa kidogo, kikohozi na kupumua kwa shida kidogo. Takriban 20% ya wagonjwa afya zao huwa mbaya na kupatwa na "numonia" (pneumonia) na matatizo makubwa ya kupumua yanayoweza kupelekea mtu apumue kwa mashine.

Lakini si kila anayeambukizwa virusi vya #corona huugua sana au kwa wastani. Makundi yaliyo kwenye hatari zaidi ni watu ambao tayari wana maradhi mengine kabla ya kuambukizwa virusi hivyo: 5.6% kwa wenye kansa; 6% kwa wenye "BP," 6.3%; 7.3% kwa wenye kisukari na 10.5% kwa wenye ugonjwa wa moyo. 

Kundi lililo kwenye hatari kubwa zaidi ni wazee wenye miaka 80 na kuendelea, wakiwa na takriban 15 ya maambukizi ya virusi hivyo hatari. Hata hivyo, habari njema ni kwamba watoto hasa wenye chini ya umri wa miaka 9 wanaonekana kutoathiriwa na janga hilo. 

Kadhalika, takwimu zilizopo zinaashiria kuwa wanaume wapo hatarini zaidi kuliko wanawake, lakini takwimu hizo zinaweza kuathiriwa na ukweli kwamba kwa mahali zilipokusanywa, yaani China, wanaume wengi huvuta sigara kuliko wanawake. Hadi muda huu wataalamu hawajui inachukua muda gani kwa virusi hivyo. 

Hata hivyo kwa wanaopatwa na maambukizi ya virusi vya #corona na hatimaye kuugua ugonjwa wa COVID-19, dalili huwa homa, kikohozi na "kuishiwa pumzi," lakini ni za muda mfupi tu. Kadhalika, mtu akifikia hatua ya kuugua COVID-19, seli za njia ya hewa kwenye mapafu huathirika, lakini kuathirika huko "hushtua" kinga ya mwili ambayo hatimaye hukabiliana na virusi vilivyosababisha maradhi hayo, yaani vya #corona. Ndio maana watu wenye mapungufu kwenye kinga ya mwili wanakuwa kwenye hatari pindi wakiambukizwa virusi hivyo.

Njia zinazoshauriwa "kupunguza uwezekano wa maambukizi ya virusi vya virusi hivyo" ni pamoja na kutowajongelea watu wenye maambukizi; kuepuka kufikicha macho na kuepuka kugusa mdomo na pua; kutotoka nyumbani pindi endapo unaumwa; kuziba mdomo kwa tishu pindi unapopiga chafya au kukohoa, na kutupa tishu baada ya kuitumia;


Ushauri wa muhimu zaidi ni kunawa mikono mara kwa mara, na kwa wastani wa sekunde 20, hususan baada ya kwenda msalani, kabla ya kula, baada ya kupiga chafya au kukohoa. Sijui kama unafahamu hili, ila "kanuni isiyo rasmi" ya kunawa mikono ni "kunawa mikono huku unaimba wimbo wa hepi besidei mpaka uishe." Kwa wastani, wimbo huo una sekunde 20

Nimalizie #thread hii kwa kurudia kukumbusha kuwa mie si mwanasayansi wala mtaalam wa afya. Nimeandika #thread hii kwa msaada wa machapisho mbalimbali kuhusiana na virusi vya #corona na ugonjwa wa COVID-19. Nakaribisha kukosolewa na wataalam.

7 Mar 2020


#Thread: katika vitu ambavyo namshukuru sana Mungu ni kunijalia uwezo wa kutumia vema akili yangu. Sote tuna akili lakini kinachotutofautisha ni uwezo wa akili husika na jinsi tunavyotumia uwezo huo pindi mtu anapokuwa nao. 

Katika #thread hii nitakueleza baadhi ya "mbinu zangu"

Binafsi nina "bahati tatu" hivi zinazonisaidia. Kwanza, udogoni nililazimishwa na mmoja wa watu wawili muhimu kabisa katika maisha yangu, marehemu baba yangu Mzee Chahali (mwingine ni mama yangu marehemu Mama Chahali), kuhusu matumizi chanya ya "akili"

Sambamba na hilo, marehemu baba alinishurutisha kwa kutumia mbinu mbalimbali, kujenga uwezo kiakili na kuhakikisha kuwa sio tu uwezo huo unatumia vema bali "naumwagilia maji" au/na "kuua mlo" ili uzidi kunawiri na kuwa na ufanisi zaidi. 

Moja ya silaha muhimu aliyonipatia ni MANENO. Alinifundisha "kijeshi" sio tu jinsi ya KUSOMA bali pia "kusoma kwa ufanisi." Yaani kwa kifupi, husomi ili kusoma tu au kusoma ili kuelewa tu bali unasoma ili ulichosoma kiwe na impact flani kupitia wewe msomaji

Nakumbuka kitabu cha kwanza kusomewa na marehemu baba ni cha mmoja cha watunzi bora kabisa wa riwaya kimataifa, James Hadley Chase. Kitabu husika kinaitwa "Come Easy Go Easy."
Baada ya kunisimulia kitabu hicho, marehemu baba alinishurutisha nami nikisome kisha niwasimulie kaka na dada zangu. Hiki ndio kitabu cha kwanza kabisa cha Kiingereza kwa mie kukisoma. Na tangu hapo, kusoma kumekuwa kama basic need kwangu. 

Kitu cha pili kuhusu MANENO ambacho marehemu baba alinisistiza mno ni KUANDIKA. Na cha tatu ni KUSIKILIZA. Na cha nne ni KUONGEA. Kwahiyo kama upo nami hadi hapa, nyenzo kuu NNE za MANENO nilizopatiwa na "Chahali Sr," ni
1. KUSOMA
2. KUANDIKA
3. KUSIKILIZA
4. KUONGEA

Fastforward miaka kadhaa mbele nikabahatika kuingia Kitengo (siku nafsi ikinituma nitaelea jinsi nilivyoingia huko japo it is now irrelevant). Pamoja na mambo mengi niliyopata huku, kubwa na la muhimu zaidi linahusu taaluma yenyewe: INTELIJENSIA

Kwa kimombo ni INTELLIGENCE, yaani AKILI. Naam, sio tu taaluma hiyo yahitaji watu wenye uwezo wa hali ya juu kiakili bali pia nayo huwajengea watu hao uwezo zaidi wa kuwa na akili, na jinsi ya kuitumia vema akili hiyo. Unfortunately, #MATAGA hawakupata fursa hii. Kwa kifupi, mwana-intelijensia bora anapaswa
KUSOMA sana
KUSIKILIZA sana
KUANDIKA sana (taarifa za kiusalama)
KUONGEA sana (si kuropoka bali kuongea na watu muhimu). Kuna msemo wa kishushushu kuwa "ni silika kwa majasusi kuongea na kila mtu."

Kama wanavyosema kuwa "once a teacher always a teacher," kwenye intelijensia nako ni hivyo hivyo, once a spy always a spy." Kwahiyo, hayo mahitaji ya "kusoma sana, kusikiliza sana, kuandika sana na kuongea sana" sasa ni sehemu ya maisha yangu ya kila siku

Enewei lengo la #thread hii sio kukusimulia historia yangu balikukutaji baadhi ya nyenzo nazotumia kutunza na kuboresha uwezo wa kiakili. Siwezi kusema "nina uwezo mkubwa wa akili," maana wa kunihukumu ni watu kama wewe unayesoma #thread hii

Nikijihukumu nitajipendelea/ntajionea
Nyenzo ya kwanza, ofkoz ni KUSOMA. Nasoma mno. Lakini kama nilivyofundishwa na marehemu Mzee Chahali, nasoma si kwa ajili ya kuelewa tu bali piakwa ajili ya kuelimisha, kuhabarisha na pengine kuburudisha (inapobidi)

Nyenzo nyingine ni KUSIKILIZA watu. Na moja ya sababu yamie kufolo watu wachache sana kwenye akaunti zangu za mitandao ya kijamii ni kujijengea mazingira mazuri ya KUSIKILIZA vizuri watu/vitu mbalimbali. Again, kusikiliza huku si kwa ajili yangu tu bali ajili ya jamii pia

Nyenzo nyingine ni KUONGEA. Naongea na watu wengi sana. Takriban kila wiki ninawasiliana na watu 5,000 hivi kupitia vijarida vyangu mbalimbali. Na pindi nikichapisha makala kwenye blogu zangu mbili, naweza kujikuta "naongea" na watu hadi 10,000 kwa wiki. 

Lakini mengi ya maongezi yangu ni kwa kutumia maandishi zaidi kuliko "maneno kutoka mdomoni." Japo naandika sana, mwenyewe hujitambulisha zaidi kama "mwanamaongezi," kwa kimombo "conversationalist."

Na nyenzo nyingine ni huko KUANDIKA. Kama nilivyotanabaisha hapo juu, maandiko yangu hulenga zaidi KUFUNDISHA na/au KUHABARISHA japo from time to timehuwa nachomekea kuburidisha pia. 

Lakini sipendi kuitwa MWANDISHI bali najiona MWANAMAONGEZI (conversationalist)

Ukifanya ku-search "@chahali #Tools" utakutana na lundo la nyenzo mbalimbali kwa ajili ya kada mbalimbali. Nyingi ni nyenzo za mitandao ya kijamii (social media tools) lakini pia kuna nyenzo za ushushushu, usalama wa mtandaoni, journalism, nk
Moja ya mbinu ninazotumia kufahamu nyenzo hizo ni kwa kutumia "mbinu mbalimbali za kutafuta vitu" (hususan mtandaoni). 

Kwa mfano, jinsi ya kutumia alama ya reli kutafuta kitu kwenye mitandao ya kijamii. Mfano, kuandika #Tools kwenye Twitter search. Kingine kinachonisaida sana ni KUALAMISHA. 

Sijui "uelewa wako wa Kiswahili ni mkubwa kiasi gani," ila kama hufahamu maana ya "kualamaisha,," jibu ni "ku-bookmark." Na Twitter ina kitufe maalum kwa ajili ya kualamisha
Kanuni yangu ni hii: kila ninapokutana na kitu chochote kile ninachodhani kina umuhimu, lazima nikialamishe. Iwe ni tweet, video, picha, habari, nukuu, just almost certainly anything and everything. Nina lundo la apps za kualamisha. 

Ukiniuliza niapps zipi zilizo bora zaidi kualamisha (kwa simu za Android) nitakutajia hizi
Evenote
Google Keep
Pocket
Microsoft OneNote
Insapaper
Zoho Notebook
Nyenzo ninazotumia sana kwenye mitandao ya kijamii hususan hapa Twitter ni za kufanya AUTOMATION. Hii inamaanisha, kwa lugha nyepesi, kuifanya app itekeleze majukumu bila wewe kuwepo kwenye app hiyo. 

Kwa mfano, muda mwingi mie sipo Twitter, na nyingi ya tweets zangu huji-post zenyewe.Nachofanya ni kuandika tweets usiku kisha nazipangia muda wakuji-post. 

Mfano halisi ni hizo "motivational quotes" za kila siku. Huwa nazipangia kuji-post 6am, 8am,12pm,2pm na 4pm UK Time. Apps zinazoniwezesha kufanya hivyo ni
Hootsuite
Buffer
Post It Later
Everypost
Crowdfire
Recurpost,

Pia web apps nazotumia ni Tweetsmap na Twittimer
Sambamba na apps hizo kwa ajili ya ku-automate posts, pia ninatumia nyenzo moja bora kabisa iitwayo IFTTT. Kirefu chake ni "If This Then That," yaani "kama hivi basi vile."
Natumia IFTTT kufanya mambo mengi. Kwa mfano nikiposti kitu bloguni kwangu nimeielekeza IFTTT ifanye kupost chapisho hilo hapa Twitter. 

Kadhalika, nimeielekeza IFTTT kuwa niki-like post basi ialamishe post hiyo kwenye app ya Evernote. Nimeielekeza pia kuwa nikipost #NenoLaLeoKiroho huko Pinterest basi ifanye kupost hapa insta pia. 

Pia naitumia IFTTT "kufuatilia watu ninaohitaji kuwafuatilia kwa sababu zangu binafsi." Kwa mfano, mlengwa akinitaja kwenye twiti, IFTTT inahifadhi twiti hiyo kwenye app flani 😊

Kuhusu hizi #thread, nikiwa na muda naandika thread husika kwa kuunganisha twiti kama mnyororo. Lakini muda ukiwa tight, natumia web app iitwayo Chir App ambayo ni ya bure au Hypefury ambayo ni ya kulipia.
Nimalizie #thread kwa kukutajia nyenzo ambayo kwenye taaluma ya masoko inaitwa NICHE. Ni hivi, kama ambavyo huwezi kwenda chuoni na kusoma kila kozi au somo, ndivyo maisha ya mtandaoni yanavyostahili kuwa. 

Usipokuwa na "mkazo" kwenye mada/sekta (niche) flani unaweza kuyumba
Kwangu, nina "niche" kadhaa ambazo ndio "zinaniweka kwenye mitandao ya kijamii."

Niche hizo ni siasa kwa ujumla (zaidi za Tanzania), teknolojia hususan usalama wa mtandaoni na ufanisi katika matumizi ya mitandao ya kijamii. Vilevile "personal development yaani "jinsi ya kuwa mtu bora." Niche nyingine ni lugha ya Kiswahili na uandishi wa vitabu. 

Je wewe "niche" yako ni ipi?

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.