4 Oct 2009


Polisi waua raia 33 bila ya hatia kati ya 2007-2009

Na Waandishi wetu

MAUAJI ya mkazi wa Segera yaliyotokea katikati ya wiki hii yamefanya idadi ya raia waliouawa na askari wa Jeshi la Polisi bila ya hatia kufikia 33 katika kipindi cha miaka miwili (2007 hadi 2009), kwa mujibu wa takwimu za Mwananchi Jumapili.

Mwananchi huyo, Idd Mtimbasi ambaye ni fundi redio wa Segera, aliuawa wakati wananchi walipofunga barabara itokaye Chalinze kwenda mikoa ya kaskazini wakipinga kuporwa ardhi. Polisi aliyekuwa kwenye gari la fedha la benki ya CRDB alifyatua risasi iliyomuua raia huyo katika harakati za kutawanya wananchi kutoka barabarani.

Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali zilizoripotiwa kwenye vyombo vya habari nchini, matukio hayo ni pamoja na lile lililotokea mkoani Kilimanjaro ambako watu 14, miongoni mwao wakiwa ni raia wa Kenya, waliuawa na jeshi hilo kwa kwa kupigwa risasi kwa tuhuma za ujambazi.

Watu hao wote waliuawa katika tukio ambalo Jeshi la Polisi lilidai kuwa lilitokana na kurushiana risasi, lakini wananchi waliibuka baadaye na kukanusha taarifa hizo huku wakidai waliouawa hawakuwa majambazi.

Waliouawa katika tukio hilo ni Hannah Kingara, mkazi wa Kiambu, ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya ulinzi ya Annkan, aliyekutwa na kitambulisho cha kazi namba 6256476, huku wengine wakikutwa na hati za kusafiria za nchi hiyo.

Wengine ni Simon Maina Ndabuki, Moses Kuria Kamau, David Njuguna Mbugua, Peter Maina Waweru, William Muiruri Kamau na Phillipo Irungu Wanjiru, wakazi wa maeneo mbalimbali jijini Nairobi. Wengine ambao pia ni wakazi wa Nairobi ni Rudovick Giceru Kariuki, John Gikonyo Buku, Zacharia Mwangi Kamathiro na Jeremiah Macharia.

Mkoani Dodoma watu nane waliuawa katika matukio mawili tofauti, sita kati yao wakiuawa katika kijiji cha Mloda baada ya kufuatiliwa na polisi. Habari zinasema kuwa polisi waliwafuatilia kwa madai kuwa walikuwa wamepora fedha na vitu mbalimbali kutoka kwa abiria kwenye Barabara ya Dodoma-Mtera.

Polisi iliripoti kuwa watu hao, ambao walikutwa katika kijiji cha Mloda, waliuawa na wananchi wa kijiji hicho, lakini wanakijiji walikanusha kuhusika na tukio hilo, jambo lililozua maswali mengi miongoni mwa wananchi.

Tukio lingine lilitokea wilayani Mpwapwa mkoni Dodoma Aprili mwaka huu wakati watu wawili waliodaiwa kuwa ni majambazi, waliuawa kwa kupigwa risasi na polisi.

Katika matukio mengine yaliyotokea jijini Dar es Salaam, polisi walituhumiwa kuwaua Zakayo Mwapi ambaye ni mkazi wa Kimara, Rashid Tuga (Gongo la Mboto) na Thomas Mwingira ambaye ni mkazi wa Yombo Bwawani.

Katika tukio la Mei 24 mwaka huu lililotokea eneo la Kimara Stop Over, Zakayo Mwapi, 24, aliyekuwa dereva teksi aliuawa kwa kupigwa risasi na ofisa wa polisi wa kikosi cha askari wa dharura. Kijana huyo alitii amri ya polisi waliovalia kiraia ya kumtaka asimamishe gari, lakini akakataa kushusha vioo, jambo lililomfanya askari huyo amfyatulie risasi na kumuua.

Tukio hilo lilitokea wakati polisi hao wakifuatilia majambazi waliohusika katika matukio mawili ya kupora kwa kutumia silaha katika eneo hilo.

Watu walioshuhudia tukio hilo walisema baada ya mahojiano ya muda mrefu na dereva huyo, walisikia mlio mkubwa ambao ulitumika kuvunja kioo cha gari na baadaye mlio wa bunduki kabla ya polisi hao kuita gari na kuupakia mwili wa kijana huyo.

Jijini Arusha watu watatu waliuawa katika matukio matatu tofauti likiwemo la mfanyabiashara Ramadhani Mussa ambaye aliuawa baada ya kupata mateso makali kutoka kwa polisi hao. Watu wengine ni Shadrack Motika, 22, na Ewald Mtui, 36, ambao waliuawa kwa kupigwa risasi wakidaiwa kuwa ni majambazi.

Tume iliyoundwa na mkuu wa mkoa kuchunguza tukio hilo ilibaini kuwa watu hao waliuawa kimakosa na hawakuwa majambazi.

Matukio mengine ni yale yaliyotokea mkoani Mara ambapo watu watatu waliuawa kwa kupigwa risasi na polisi Februari 18 na Mei 7. Iranda Matoka, 26, na Abbas Adek, 23, waliuawa kwa kupigwa risasi Mei 7, wakati Jacob Waibina aliuawa kwa risasi Februari 18.

Katika tukio la Mei 7 mwaka huu watu hao waliuawa wakati polisi walipokabiliana na wakazi wa kijiji cha Moharango walioandamana kwenda kituo cha polisi Utegi, wakitaka kuachiwa huru kwa wazee wanne wa mila. 



Wazee hao waliojulikana kwa majina ya Kahanga Mwando, Odila Runyola, Saba Kahanga na Wasaga Mganga, walikamatwa kwa madai ya kutishia kumroga na kumuua mkazi wa kijiji hicho, Joseph Ngondi. 


Kwenye mji wa Tunduma mkoani Mbeya, kulitokea machafuko Juni 28 wakati wananchi walipovamia kituo cha polisi kwa kuwa askari walimuua mfanyabiashara Frank Mwachembe kwa tuhuma za ujambazi.

Baada ya tukio hilo jeshi la polisi liliunda tume ya kuchunguza tukio hilo kabla ya kuukabidhi mwili wa marehemu kwa ndugu zake ambao waliuzika kijijini kwao Imezu mkoani Mbeya.

Tukio lingine ni lile lililotokea Julai 14 ambapo polisi walidaiwa kumkamata na kumpiga Lucas Mwaipopo na kusababisha kifo chake.

Kutokana na tukio hilo wananchi zaidi ya 300 wilayani Kyela walivamia kituo cha polisi kwa lengo la kuwateka askari waliohusika na tukio hilo. Askari watatu na wananchi 15 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kutokana na kuhusika kwenye vurugu hizo zilizosababisha watu watatu kulazwa hospitali kwa kujeruhiwa na risasi.


Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba hakutaka kuzungumzia wimbi hilo la mauaji ya raia wasio na hatia na badala yake akamtaka mwandishi aongee na msemaji wa Jeshi la Polisi, Abdallah Msika ambaye aliomba aandikiwe maswali ili aandae majibu.

“Kwa sasa nipo safarini Mbeya ambako tumekuja kwa ajili ya maadhimisho ya Wiki ya Usalama. Wewe niandikie maswali halafu uniletea ofisini Jumanne na nitayajibu,” alisema Msika.

Katibu mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa amemtaka rais kuingilia kati suala hilo akidai litapoteza imani kati ya chombo hicho na wananchi.

Alisema ili kuhakikisha suala hilo linakomeshwa, rais anatakiwa aingilie kati na kuhakikisha tume zilizoundwa kuchunguza matukio ya polisi kuua raia wasio na hatia zinawekwa hadharani na wahusika wanachukuliwa hatua.

Alisema vitendo hivyo ambavyo vimeshamiri hapa nchini ni hatari kwa usalama wa taifa kwa kuwa kama vitaachwa viendelee vitawakatisha tamaa wananchi na kuwafanya kufuatilia haki zao wao wenyewe.

Habari hii imeandaliwa na Geofrey Nyang’oro Hussein Kauli na Mussa Mkama.

CHANZO: Mwananchi

2 comments:

  1. Sijui ni nini tunahitaji nchini mwetu. Yaani hii tabia ya kuwa-treat watu kama takwimu inaniuma saaana
    Juzu nimeangalia kipindi cha ABC Tv kuhusu mauaji ya albino na Waziri Mkuu anaulizwa kuwa kwa miaka 2 ya mauaji hayo, na watu 200 kuwekwa mbaroni, mbona hakuna kesi inayoendelea anasema "tunalifania kazi. Vitendea kazi havitoshi".
    Sasa watu wanaouawa waifikiriaje serikali? Na sasa ona idadi hii
    Mie sijui la kuifanyia serikali kwa kweli

    ReplyDelete
  2. Biashara ya viungo vya ma-albino inafanywa na mafisadi maana hata hiyo bei ya viungo ni ghali sana kwa mamilioni ya shilingi hivyo ni moja kwa moja ni mafisadi. Ambao ushahidi unaonesha kuwa kuna mafisadi na nje ya serikali hii ya sasa, Na kamwe hawawezi kufanya lolote. Ushahidi mmoja wapo hivi karibuni fisadi mmoja alitangazwa na taasisi kuu ya kupambana na rushwa kama inavyojiita na kujibatiza jina. Bila aibu wala haya mkuu wao aliposema huyo bwana kesi yake ya ufisadi imefutwa na taasisi ya kweli ya kiengereza ya kupambana na rushwa na michezo michafu.....Kesho yake balozi wa Uingereza Tanzania alikanusha na hakuna chochote kilichofanyika kumwajibisha huyo kiongozi aliyasema hayo...Hivyo husishangae kauli ya waziri mkuu kuhsu watuhumiwa wa biashara ya viungo vya ma-albino...

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.