1 Jan 2020


Kwa zaidi ya miaka 10 sasa nimekuwa na utaratibu wa kufanya ubashiri kuhusu yanayotarajiwa kutokea katika mwaka mpya, zoezi ninalolifanya siku ya kwanza ya mwaka mpya husika.

Mwaka huu 2020 unatarajiwa kuwa mgumu sana kwa Tanzania. Na bila kuumauma maneno, ugumu wa mwaka huo utachangiwa na "utawala wa mkono wa chuma" - unaozidi kuota mizizi -wa Rais John Magufuli. 

Moja ya matukio yatakayotawala vichwa vya habari mwaka huu ni pamoja na watu kadhaa maarufu kutoka kada mbalimbali "kupotea." Wahanga wakubwa wanatarajiwa kuwa wanaharakati wanaodiriki kukemea maovu mbalimbaliyanayofanywa na utawala wa Rais Magufuli.

"Kupotea" huko kutaendelea kufanya tishio la "Watu Wasiojulikana" liendelee kuwasumbua Watanzania kama ilivyokuwa mwaka jana 2019.

Kinachotarajiwa kufanya hali kutokuwa nzuri ni pamoja na hofu isiyo na msingi aliyonayo Rais Magufuli kuhusu uwezekano wa yeye kuchaguliwa kuwa mgombea urais kwa tiketi ya CCM na uwezekano wa yeye kushinda nafasi hiyo. 

Hofu hiyo inachangiwa na kile Waingereza wanasema "the guilty are always afraid." Sio siri kwamba Rais Magufuli amejitahidi sana kuwavunja moyo watu wengi tu ambao sio tu walikuwa na matarajio makubwa kwake bali baadhi yao  - ikiwa ni pamoja na mie -walishiriki kumnadi kwa nguvu zote katika kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Kubwa zaidi lililowavunja moyo watu hao ni "valid excuse" ya Rais Magufuli kuwa Watanzania waelekeze nguvu zao kwenye kuchapa kazi ilivyogeuka kuwa excuse ya kuwanyima raia haki zao za msingi. Kukandamiza haki ya kikatiba ya vyama vya upinzani kufanya shughuli zao za kisiasa, kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari, kuwabambikiziawatumbalimbali kesi zisizo na kichwa wala miguu, kuendeleza siasa za chuki, ubaguzi na ukanda wa mchana kweupe, matusi ya hadharani dhidi ya watendaji mbalimbali wa serikali, na mlolongo wa vitu visivyopendeza. 

Kwa vile Rais Magufuli anafahamu kuwa "amewageuka" wengi wa waliomnadi na kumuunga mkono, anajikuta akiwa kwenye kundi la "the guilty are always afraid." Gulity for what? Well, hadi muda huu serikali yake inabaki suspect number one katika "kupotea" kwakda maarufu wa Chadema Ben Saanane ambaye alikuwa critic mkubwa wa Rais Magufuli; suspect number one katika jaribio la kumuua Tundu Lissu; suspect number one katika "kupotea" kwa mwanahabari Azory Gwanda; suspect number one katika yanayodaiwa kuwa "mauaji ya mamia" huko Mkuranga, Kibiti na Rufiji (MKIRU), suspect number one katika kifo cha afisa wa hazina kitengo cha EU, Marehemu Leopold Lwajabe ambaye kabla ya kuuawa alitekwa, akateswa na kubakwa. Unyama usiomithilika.

Serikali ya Rais Magufuli ni suspect number one katika kinachodaiwa kuwa ufisadi wa kihistoria wa fedha za umma, jambo lililopelekea kuondolewa kwa CAG Prof Assad ili ufisadi huo uendelee kufichwa.

In short tema, Rais Magufuli anaishi na hofu ya kitakachomtokea pindi akiwa sio rais, iwe kwa kushindwa uchaguzi, kung'olewa madarakani au kumaliza muhula wake. Kilicho wazi ni kwamba kwa aliyokwishatenda katika miaka hii minne kuelekea mitano, sio rahisi kwake japo kufikiria kuhusu kuwa nje ya nafasi ya urais. 

Na kwa vile mbinu yake kuu ya utawala - UBABE - inaelekea kuwa na ufanisi, kwa maana ya kwamba hakuna jitihada zozote zilizofanyika kupambana na mengi yasiyopendeza yanayofanywa na utawala wake, mwaka huu unatarajiwa kushuhudia ubabe maradufu. Kwa upande mmoja ubabe huo utakuwa mwendelezo tu wa yanayojiri muda huu lakini kwa upande mwingine utakuwa ni mkakati wa kuhakikisha anarudi Ikulu baada ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba.

Talking of uchaguzi mkuu, inatarajiwa kuwa uchaguzi huo mkuu utatawaliwa na hila na vituko na hujuma na mbinu chafu maradufu ya ilivyokuwa kwenye mzaha wa kisiasa uliopewa jina la "uchaguzi wa serikali za mitaa," ambapo pasi haya, chama tawala CCM kilijitangaza mshindi kwa asilimia 99.

Wakati endapo kila kitu kitabaki "constant" (yaani endapo hakutokuwa na mabadiliko), Rais Magufuli na CCM yake watajitangaza washindi wa kishindo kwenye uchaguzi huo mkuu ambapo kura zake na za CCM zitakuwa zaidi ya asilimia 90.

Kadhalika, endapo kila kitu ktabaki "constant," vyama vya upinzani vitaambulia kati ya viti 10 hadi 20 tu (yawezekana vikawa hata pungufu ya 10) vya ubunge kwenye uchaguzi huo mkuu.

Kadhalika, kadri uchaguzi huo mkuu utakavyozidi kujongea ndivyo Rais Magufuli na CCM yake watakavyozidi kuongeza jitihada za kuwanunua wabunge na madiwani wa vyama vya upinzani ili wajiondoe kwenye vyama vyao na kutangaza kujiunga na CCM. Mkakati huo ni sehemu ya jithada za kukomboa majimbo yaliyo chini ya wabunge wa upinzani.

Sambamba na hilo ni kukua kwa "uhasama" kati ya Chadema na ACT-Wazalendo, kitu kitakachochochewa na jitihada endelevu za CCM kuhujumu vyama vyaupinzani sambamba na jitihada za mapandikizi waliomo kwenye vyama hivyo vya upinzani wakiwana jukumu moja tu- kuvikwamisha.

Ukandamizwaji dhidi ya wanasiasa utawakumba pia baadhi ya wana-CCM hususan wanaohisiwa kuwa karibu na Bernard Membe, mwanasiasa anayemnyima usingizi Rais Magufuli kwa kudhani kuwa anataka kuchuana nae kwenye kinyang'anyiro cha kuwania urais kwa tiketi ya CCM.

Kuna uwezekano mkubwa kwa wana-CCM kadhaa wenye majina makubwa kufukuzwa uanachama. Licha ya hatua hiyo, wana-CCM hao watafunguliwa kesi za uhujumu uchumi.

Kwa upande mwingine, mwaka huu utashuhudia angalau mabadiliko mawili ya baraza la mawaziri. Sambamba na hilo, endapo Rais Magufuli atafanikiwa kuwa mgombea pekee wa CCM, inatarajiwa atashinikiza kuteuliwa kwa mgombea mwenza mwingine badala ya Mama Samia. 

Kuna uwezekano wa kujitokeza matishio ya mashambulizi ya kigaidi yatakayohusiana na hali tete iliyopo kwenye mpaka wa Tanzania na Msumbiji. 

Kuhusu Idara ya Usalama wa Taifa, nabashiri kutokea kwa mabadiliko makubwa yanayoweza kupelekea Mkurugenzi Mkuu wa sasa, Diwani Rajabu kuondolewa kwenye wadhifa ho na nafasi yake kuchukuliwa na aliyewahi kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Idara hiyo, Robert Makungu ambaye awali alitumbuliwa na kuwa RAS huko Tabora. 

Kiuchumi, vyuma vitaendelea kukaza. Na hali inatarajiwa kuwa ngumu zaidi mwaka huu kwa sababu CCM itaongeza jitihada za kukusanya fedha kwa ajili ya uchaguzi mkuu. Neno "jitihada" hapa linamaanisha mbinu chafu na za kifisadi kama ilivyokuwa kwenye skandali ya EPA/Kagoda.

Uchumi pia unatarajiwa kuwa mgumu kwa sababu kuna uwezekano wa baadhi ya nchi wahisani kusitisha misaada yao kufuatia ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu nchini Tanzania. 

Jambo jingine linalotarajiwa kuathiri uchumi na matumizi holela yanayofanywa na serikali ya Rais Magufuli bila kuzingatia idhini yabunge au/na kanuni za bajeti. 

Moja ya matukio ya nje ya Tanzania yanayoweza kuigusa Tanzania ni uhasama endelevu kati ya Rais Museveni na Kagame. Unfortunately, Tanzania ni eneo muhimu kimkakati kwa nchi zote mbili hasa kwa vile ndipo kunapotokea "vita ya kijasusi" kati ya Uganda na Rwanda. Kwamba nchi hizo mbili zinaweza kuingia vitani sio jambo lisilowezekana japo sio rahisi sana.

Kabla ya kuhitimisha makala hii, naomba kusisitiza kuwa ubashiri huu sio exact science bali ni matokeo ya mie mtumishi wako kumudu kusoma mwenendo wa mambo (trends) huko Tanzania. Japo ni rahisi kuhisi kwamba MATAGA na Praise Teram watatafsiri ubashiri huu kuwa ni "kazi ya kibaraka wa mabeberu kuiombea mabaya Tanzania," ukweli ni kwamba ubashiri huu umefanyika objectively.

Mwisho, haitokuwa jambo la kushangaza endapo mgombea urais wa CCM katika uchaguzi mkuu ujao hatokuwa Rais Magufuli. Si kwamba jina lake litakatwa lakini "laweza kutokea la kutokea."

Nimalizie kwa kuwatakia nyote heri ya mwaka mpya 2020.14 Apr 2019

[Uchambuzi wa ACT Wazalendo Kuhusu Maeneo Kumi (10) Muhimu Kwenye Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa Mwaka wa Fedha wa 2017/18].

- Ikulu Yatumika Kuficha Ukaguzi wa Manunuzi ya Ndege

- Bilioni 800 Hazikutolewa kwa Ukaguzi
- Trilioni 4.8 Zimetumika Bila Kupita Mfuko Mkuu wa Hazina
- Mikopo ya Ndani Yashindwa Kulipa Madeni Kikamilifu
- 40% ya Bajeti yategemea Mikopo na Misaada Kutoka NjeNdugu WanahabariA: Utangulizi Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Juma Assad ametoa taarifa yake ya Ukaguzi wa Mapato na Matumizi ya Fedha za Umma kwa mwaka wa fedha wa 2017/18. Licha ya changamoto mbalimbali zilizotokea kabla ya CAG kukamilisha wajibu wake huu wa kikatiba, taarifa hiyo sasa iko wazi kwa umma, baada ya kuwa imekabidhiwa rasmi bungeni. Sisi ACT Wazalendo, tumeisoma, kuipitia na kuichambua taarifa husika, kwa lengo la kuitumia ili itusaidie kutimiza wajibu wetu wa kuisimamia Serikali kama chama mbadala nchini na kama Chama cha Upinzani Bungeni. Tunafurahi kupata fursa ya kuwa nanyi hapa ili kuzungumza na umma, kupitia nyinyi, juu ya maeneo Kumi (10) muhimu kwenye ripoti ya CAG kwa mwaka wa fedha wa 2017/18.B: Maeneo Kumi (10) Muhimu Katika Ripoti ya CAG1. Bajeti ya Serikali Sio Halisia, Mapato Yasiyokusanywa ni Tarakimu MbiliKwenye bajeti ya mwaka wa fedha wa 2016/17, ambayo ni bajeti ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Tano, mipango ya Serikali ilikuwa ni kukusanya shilingi 29.5 trilioni, kwa mujibu wa ripoti ya CAG ya 2016/17, kati ya fedha hizo, Serikali ilikusanya shilingi 25.3 trilioni. Na hivyo, kutokufikia lengo la makusanyo kwa 14.33%. Kwenye uchambuzi wetu wa mwaka jana tulieleza kuwa bajeti za Serikali si halisia.Kwenye ripoti hii ya mwaka 2017/18, kwa mara nyengine, CAG amelithibitishia Taifa kuwa Serikali ya awamu ya tano inatunga Bajeti ambayo sio halisia. Katika Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha wa 2017/18 jumla ya shilingi 31.7 trilioni zilitarajiwa kukusanywa na zilipitishwa kutumika na Bunge. Hata hivyo, kwa mujibu wa ripoti hii ya CAG, Serikali iliweza kukusanya kutoka vyanzo vyake vyote shilingi 27.7 trilioni tu, na kutumia shilingi 26.9 trilioni. Hivyo ikikosa makusanyo kwa 12.66% na ikikosa matumizi kwa 15.2%.Kwa miaka mitatu ya mwisho ya Serikali ya awamu ya nne, wastani wa lengo lisilofikiwa na Serikali katika ukusanyaji wa mapato ya Bajeti ni tarakimu moja, 6.3% tu, ambapo kwa mwaka 2013/14 lengo halikufikiwa kwa 9%, kwa mwaka 2014/15 nako lengo halikufikiwa kwa 4%, na kwa mwaka wa fedha wa 2015/16 lengo halikufikiwa kwa 6% tu.Hii inadhihirisha Kwa mara nyengine tena kuwa Serikali ya Awamu ya Tano hutangaza viwango vikubwa vya Bajeti ili kufurahisha umma ilhali uhalisia ni kuwa Bajeti ni ndogo zaidi. Kwa miaka 2 mfululizo CAG ametuonyesha kuwa Serikali inashindwa kufikia makadirio ya Bajeti Kwa zaidi ya shilingi Trilioni 4 kutoka Bajeti inayopitishwa na Bunge.2. 40% ya Bajeti Inategemea Misaada na MikopoRipoti ya CAG imetuonyesha kuwa ndani ya miaka miwili ya Serikali ya awamu ya tano uwezo wetu wa kujitegemea kibajeti umezidi kuzorota. Kwa mwaka wa fedha wa 2016/17 nchi yetu ilijitegemea Kibajeti kwa 65% kwa mapato ya ndani ya nchi, na 35% iliyobaki ndiyo iliyotokana na mikopo pamoja na misaada ya Wahisani. Hali Hiyo ni tofauti kwa mwaka wa Fedha wa 2017/18, tumedidimia zaidi.CAG ameonyesha katika uchambuzi wake kuwa, nanukuu “Uchambuzi unaonyesha kwamba bila Mikopo na misaada kutoka kwa wahisani wa maendeleo, makusanyo ya ndani ya nchi yetu yangeweza kugharamia matumizi yote ya Serikali kwa asilimia 60 tu” (Chanzo: Ripoti ya Ukaguzi-Serikali Kuu-2017/18: Ukurasa wa 89).Hii inaonyesha kuwa Bajeti yetu ya Tanzania ni tegemezi kwa 40% tofauti na tunavyoelezwa na Serikali kila wakati kuwa nchi yetu inaondoa utegemezi kwenye bajeti. Kwa mwaka 2016/17 utegemezi wetu uliongezeka kwa 27%, na kwa mwaka 2017/18 utegemezi wetu umeongozeka kwa 22%.CAG ameonyesha kuwa Serikali ilikusanya shilingi 27.7 trilioni tu (makusanyo yote, ikiwemo misaada na mikopo kutoka ndani na nje) kwa mwaka wa fedha wa 2017/18. Makusanyo ya ndani yakiwa ni shilingi 16.7 trilioni, sawa na 60% ya makusanyo yote, na kwamba matumizi ya kawaida yaliyofanyika mwaka huo ni shilingi 15.3 trilioni, ambayo ni sawa na asilimia 55% ya makusanyo yote lakini ni 93% ya mapato ya ndani. Utegemezi huu utaathiri sana nchi yetu kwani gharama za kulipia mikopo (riba) zitakuwa kubwa kuliko hata uwezo wetu wa kuongeza mapato ya ndani.3. Shilingi 800 Bilioni Hazikutolewa kwa UkaguziKatika Uchambuzi wetu wa mwaka jana tulionyesha kuwa 6% ya fedha zilizokuwa zimekusanywa na Serikali hazijulikani zilipokwenda. Hizi zilikuwa ni shilingi 1.5 trilioni ambazo mjadala wake ulichukua mwaka mzima. Hoja yetu hiyo ilipelekea kufanyika kwa uhakiki maalumu na CAG, na ambapo bado Serikali ilishindwa kuonyesha zilipokwenda fedha hizo, zaidi ya kudai kuwa ilihamishia Ikulu matumizi ya shilingi 976 bilioni kati ya hizo 1.5 trilioni bila kumpa CAG uthibitisho wa uhamishaji huo wala kuonyesha fedha hizo zimefumikaje huko Ikulu.Katika ukaguzi wa CAG wa Bajeti ya mwaka 2017/18, ambayo ni Bajeti ya Pili ya Serikali ya awamu ya 5, ameonyesha kuwa katika Bajeti ya shilingi 31.7 trilioni iliyoidhinishwa na Bunge, Serikali iliweza kukusanya shilingi 27.7 trilioni tu kutoka kwenye vyanzo vyote vya kodi, vyanzo visivyo vya kodi, mikopo ya ndani na nje, na misaada ya wahisani na washirika wa maendeleo. Serikali ilishindwa kukusanya kiasi cha shilingi 4 trilioni kama ilivyokuwa mwaka uliopita ingawa sasa ni sawa na 13% ya Bajeti yote ya mwaka 2016/17. Hata hivyo CAG anaonyesha kuwa shilingi 26.9 trilioni tu ndio zilitolewa kutoka Mfuko Mkuu wa Serikali na kwenda kutumika, hivyo shilingi 800 bilioni kati ya shilingi 27.7 trilioni zilizokusanywa kutokujulikana ziliko na hazikutolewa kwa ukaguzi.4. Shilingi 4.8 Trilioni Zimetumika Bila Kupita Kwenye Mfuko MkuuKatika Ukurasa wa 91 wa ripoti yake yam waka wa fedha wa 2017/18, CAG anasema, nanukuu “Ikilinganishwa taarifa ya kutoa fedha (exchequer issue report) na taarifa ya Fedha zilizopokelewa na kuripotiwa katika taarifa za fedha za Mafungu husika pamoja na barua za kukiri mapokezi ya fedha kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, imebaini utofauti wa taarifa zilizoripotiwa…”. CAG ameeleza kuwa tofauti hiyo imesababishwa na kutokuwepo kwa mifumo thabiti ya usuluhishi kati ya fedha zilizotolewa na hazina na fedha zilizotolewa na wahisani wa maendeleo moja kwa moja kwenye miradi ya maendeleo katika Wizara. Ni muhimu sana kusisitiza hapa kuwa kwa mujibu wa CAG kuna fedha shilingi trilioni 4.8 ambazo makusanyo yake hayakuingizwa mfuko mkuu wa Serikali (tazama uk 91 wa Taarifa, tanbihi namba 15).Suala la udhaifu wa Mifumo Katika Hazina pia limeelezwa kwa kina Katika Taarifa ya CAG ya Uhakiki wa Tofauti ya shilingi 1.5 Trilioni Katika mwaka wa Fedha 2016/17. Bado udhaifu huu unaendelea na madhara yake Katika usimamizi wa Fedha za Umma ni makubwa sana.5. Bilioni 678 za Mamlaka Nyengine Ziliporwa na Mlipaji Mkuu wa SerikaliKwenye ripoti ya CAG ya 2017/18 imeonyeshwa kuwa bado Serikali inatumia fedha ambazo sio zake (ring fenced) kama ilivyoonyeshwa kwenye ripoti ya mwaka 2016/17. Kwa mwaka 2017/18 CAG amebaini jumla ya shilingi 678 bilioni zilizokusanywa na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kwa niaba ya taasisi nyengine hazikuhamishwa kwenda kwenye taasisi husika, na badala yake zilihamishiwa kwa Katibu Mkuu Hazina ambapo huko hazikuonekana kwenye ukaguzi kama sheria inavyotaka. Fedha zilizoporwa na Hazina ni pamoja na shilingi 169 bilioni za Shirika la Reli, shilingi 168 bilioni za Wadau wa Korosho nchini na shilingi bilioni 16 za Wakala wa Umeme Vijijini (REA). CAG kwa mara nyengine tena amependekeza sheria iheshimiwa kuhusu matumizi ya fedha hizi za Taasisi mbalimbali. Kwenye ripoti ya CAG ya mwaka 2016/17 kiasi cha shilingi 2.2 trilioni za mamlaka mbalimbali nchini hazikurejeshwa kwenye mamlaka husika mara baada ya fedha hizo kukusanywa na TRA. Tabia hii ya kupora Fedha za Mamlaka nyengine licha ya Kwamba Fedha hizo zimewekwa kisheria na kikatiba inaua misingi ya matumizi bora ya Fedha za Umma.Kwa Upande wa TRA Bado kuna changamoto kubwa ambazo zinahitaji kutatuliwa. Makusanyo yetu ya kodi Bado ni kidogo sana (tax yield) tukiwa wa mwisho Katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, uwiano wa makusanyo ukiwa ni 12% tu ya Pato la Taifa. Hii inatokana tax base kuwa ndogo na mifumo sio rafiki kwa walipa kodi. Inawezekana TRA huchukua Fedha za Taasisi kupeleka Hazina ili kuonyesha makusanyo zaidi ilhali hali sio hiyo. Serikali inapaswa kukaa na sekta Binafsi kujadili kwa unyoofu (honestly) njia bora ya kupanua wigo wa Kodi ili nchi iweze kujitegemea. Katika uchambuzi wetu tumeacha mambo Mengi ikiwemo upotevu mkubwa wa mizigo ya transit ambao CAG ameuonyesha.6. Kushuka kwa Thamani ya Shilingi Kunakuza Zaidi Deni la TaifaRipoti ya CAG ya 2017/18 imetuonyesha kuwa Deni la Taifa (Deni la Serikali) limefikia shilingi 50 trilioni mpaka Juni 30, 2018 likiwa na ongezeka la shiingi 4.85 trilioni, sawa na 10% kutoka shilingi 46 trilioni za Juni 30, 2017, deni hili likikua kwa shilingi 9.8 trilioni kwa muda wa miaka miwili tu kutoka Juni 30, 2016 mpaka Juni 30, 2018. CAG ameeleza kwamba kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya fedha za kigeni kumechangia kuongezeka kwa Deni kwa 20% kwa mwaka wa fedha wa 2017/18 (ongezeko kubwa zaidi ukilinganisha na 9% za mwaka wa fedha wa 2016/17). Hii inatokana na Deni letu la Nje kuwa kwenye Fedha za Kigeni na hivyo kuathirika sana kutokana na thamani ya shilingi kutetereka. Baada ya makosa ya kimaamuzi kwenye suala la Zao la Korosho, ni dhahiri kuwa Deni letu la Nje litaongezeka zaidi baada ya shilingi ya Tanzania kutetereka zaidi kwa kukosa Mapato ya Fedha za Kigeni. MAARIFA makubwa yanahitajika kuhami nchi kutokana na janga la Deni la Taifa.7. Mikopo ya Ndani Yashindwa Kulipa Madeni Kikamilifu Lakini pia CAG ameeleza kuwa sababu Kuu zaidi ya kukua kwa deni la Taifa ni kwa kuwa tunaendelea kukopa zaidi. Kwa miaka mitatu iliyopita kukopa zaidi kulichangia ukuaji wa deni letu kwa 70%, ambapo kwa mwaka 2016/17 ilikuwa juu zaidi na kufikia 88%.Zaidi CAG ameonyesha pia kuwa tulikopa mikopo ya ndani ya shilingi 5.7 trilioni kwa mwaka 2017/18 ambayo pamoja na kuwa na athari mbaya kwenye mikopo ya sekta binafsi nchini (maana inapunguza fursa ya wafanyabiashara wetu kukopeshwa na taasisi za ndani za fedha), lakini pia mikopo hiyo imeshindwa kulipa riba za mwaka za shilingi 6.1 trilioni. Na hivyo ilibidi Serikali kutafuta shilingi 448 bilioni kutoka kwenye vyanzo vingine ili kuweza kulipa riba hizo. Ripoti ya CAG imeeleza, nanukuu “Deni la Ndani halikuchangia kwenye miradi ya Maendeleo”. Hivyo tulikopa ndani ya nchi si kwaajili ya kufanya shughuli za maendeleo, bali kulipa deni la nyuma, na bado hata hiyo mikopo haikutosheleza ulipaji wa hayo madeni ya nyuma. Hali hii si afya kwa taifa letu.Mfano kwa mwaka 2017/18 Kiwango cha kuhudumia Deni la nchi ni 108% ya fedha zilizopatikana kutoka kwenye mikopo ya ndani, na CAG ameonya kuwa jambo hilo lina athari kubwa. Ukurasa wa 141 wa Ripoti ya Ukaguzi wa Serikali Kuu CAG ameeleza, nanukuu “kuna uwezekano wa kuwa na madhara kwa uchumi (hali ya kuhudumia deni kwa 108%) isipotafutiwa ufumbuzi”. CAG pia ameonyesha kuwa kasi ya kukua kwa mikopo ya nje ni 38%, hali ambayo inaongeza gharama za kuhudumia madeni. Na jambo baya zaidi ni kuwa tunakopa zaidi mikopo ya kibiashara. CAG ameshauri watunga sera kuwa na busara wakati wa kuchagua miradi ya kupewa fedha za mikopo ya kibiashara, akishauri maamuzi yazingatie uzalishaji wa miradi husika. Vinginevyo Bajeti ya Taifa itakwenda kuhudumia deni tu.Kwenye eneo hilo la Deni la Taifa pia ripoti ya CAG imeonyesha kuwa kuna upotoshwaji mkubwa wa mapokezi ya mikopo kutokana na mapungufu ya udhibiti wa ndani. Pia CAG ameonyesha kuwa mifumo wa kutunza madeni ni kianalojia (ya kizamani), jambo ambalo linaathiri kumbukumbu za madeni. 8. Serikali Imeanza Kushindwa Kulipa Madeni (Defaulting)Ripoti ya CAG imeonyesha kuwa Serikali imeshaanza kushindwa kulipa baadhi ya madeni yake (Defaulting). Tayari kuna fedha kiasi cha shilingi 212.7 bilioni Serikali imeshindwa kuzilipa kwa Benki Kuu nchini (BOT), zikiwa shilingi 199.79 bilioni ni riba ya nakisi ya Serikali, na shilingi 12.9 bilioni ni sehemu ya Serikali ya gharama za kudhibiti ukwasi kuanzia mwaka 2015/16 hadi 2017/18.Serikali ilisaini Mkataba wa Makubaliano (MoU) na BOT, ambao unaitaka kulipa kila robo mwaka sehemu yake ya gharama ya kudhibiti ukwasi pindi hati ya madai inapotolewa. Ucheleweshwaji huu wa malipo utaongeza uwepo wa mali za BOT zisizo na tija, na ni dalili ya Serikali kushindwa majukumu yake kifedha.9. Ikulu Yatumika Kuficha Ukaguzi wa Manunuzi ya NdegeHatujafanikiwa kuona Ukaguzi wa Manunuzi ya Ndege ikiwemo Ununuzi wa Ndege za Shirika la Ndege Nchini, ATCL ambao kwa sehemu umefanyika mwaka wa fedha 2016/17 na 2017/18.Katika uchambuzi wetu wa ripoti ya CAG ya mwaka jana (ripoti ya mwaka wa fedha wa 2016/17) tuliwaeleza kuwa katika ripoti ile licha ya kuwa ni taarifa bora sana kwa maudhui na uchambuzi, kuna mambo muhimu kadhaa ambayo CAG aliyaacha. Na tukamtaka kwenye ripoti yake ya mwaka 2017/18 ayafanyie kazi, mojawapo ni ukaguzi wa Ununuzi wa Ndege Sita (6) zinazoendeshwa na Kampuni ya Ndege nchini, ATCL.Mpaka sasa Serikali imeshatumia jumla ya Shilingi Trilioni1 kununua ndege sita (6) na katika makadirio ya Bajeti ya mwaka 2019/20 yanayoendelea sasa bungeni Serikali imeomba Bunge liidhinishe shilingi Bilioni 500 kwa ajili ya kulipia ndege mpya nyengine. Ufuatiliaji wetu umegundua kuwa Serikali imekuwa ikichukua Fedha za Umma kupitia Fungu 62 (Wizara ya Uchukuzi) na kufanya manunuzi ya ndege. Ndege hizo wanakabidhiwa Wakala wa Ndege za Serikali kama wamiliki na shirika la ATCL inakodishiwa ndege hizo kwa Mkataba maalumu (ambao haujawekwa wazi popote, hata kwa Bunge).Tulitarajia kuwa ripoti hii ya CAG ya mwaka 2017/18 kwenye ukaguzi wa fungu Namba 62 tungeweza kuona ukaguzi wa manunuzi ya ndege hizi. Lakini Serikali kwa lengo la kuficha taarifa imeamua kuhamishia kwenye Ofisi ya Rais (fungu 20) Wakala wa Ndege za Serikali kupitia tangazo la Serikali namba 252 la Juni 2018.Tumetafuta taarifa ya ukaguzi wa fedha hizo za umma zilizofanya manunuzi ya ndege bila mafanikio. Tunamwomba CAG;
- Afanye Ukaguzi Maalumu wa Fedha za Umma Shilingi Trilioni 1 zilizotumika kununua ndege.
- Afanye Ukaguzi wa usimamizi wa mkataba wa ukodishwaji wa ndege hizo kati ya Wakala wa ndege za Serikali na Shirika la Ndege la ATCL ili Watanzania wajue matumizi sahihi ya Fedha zao za Kodi.Jambo hili ni muhimu sana, kwa sababu uzoefu unaonyesha kuwa kila jambo lenye harufu ya wizi au matumizi yenye mashaka basi Serikali huliamishia jambo hilo ikulu (Kwa kuwa inajua ukaguzi wake hautawekwa wazi). Hata kwenye fedha shilingi 1.5 trilioni ambazo tulizianisha kuwa hazijulikani ziliko kutokana na uchambuzi wetu wa ripoti ya CAG ya mwaka 2016/17, baada ya kuibana Serikali na kumtaka CAG afanye uchunguzi maalum, mwishowe Serikali ilihamishia Ikulu matumizi ya Shilingi 976 bilioni kati ya hizo shilingi 1.5 trilioni ili isihojiwe.Mafungu mawili, Fungu 20 (Ofisi ya Rais Ikulu) na Fungu 30 (Sekretariati ya Baraza la Mawaziri) yanapaswa kumulikwa sana katika matumizi ya Fedha za Umma. Tumeona mwaka huu Serikali inaomba Bunge litenge shilingi Bilioni 302 kwa Fungu 30 kwa kile kinachoitwa ‘matumizi mbalimbali ya kitaifa’. Mwaka ujao, Mungu akituweka hai, tutafuatilia kwa kina kaguzi za mafungu Haya kwani inaonyesha ndimo inakuwa kichaka Cha kuficha Taarifa za namna Fedha za Umma zinatumika.10. Hoja za Ukaguzi za Shilingi Bilioni 225 hazina majibu kabisa
Kwa ujumla, na kwa Serikali Kuu peke yake, Hoja zote za Ukaguzi zilizoibuliwa na CAG kwenye Hesabu za Mwaka 2017/18 ukiachana na hoja kubwa nilizoeleza hapo juu, zina thamani ya shilingi 225 bilioni kati ya Fedha zote zilizokusanywa kwenye mwaka wa Fedha husika. Hii inaonyesha kuwa bado Serikali haijaweza kufanyia kazi Hoja za CAG kwa wakati na kwamba mifumo ya Serikali bado inavujisha Fedha za Umma.C: Mapendekezo ya ACT Wazalendo Baada ya kusoma taarifa hiyo ya CAG na kuyaanisha maeneo Kumi (10) muhimu, sisi ACT Wazalendo tuna mapendekezo yafuatayo:1. ACT Wazalendo tunawasihi Wabunge wote bila kujali vyama vyao kutekeleza wajibu wao wa kuisimamia Serikali. Wabunge wasipotekeleza wajibu wao huo basi nchi yetu itaangushwa na matumizi mabovu na ya kinyume na Sheria kama tulivyoaina kwenye Uchambuzi wetu.2. Serikali iwe inatunga Bajeti Halisia ambayo inatekelezeka, tofauti na inavyofanya kwa miaka minne mfululilo sasa, ambapo inataja namba kubwa ambayo Bajeti husika huwa haipatikani kwa ukamilifu wake na hivyo kuathiri sana miradi ya Maendeleo ambayo inakuwa imepangiwa mafungu ya Fedha. Ni bora kuwa na Bajeti ndogo ambayo inatekelezwa badala ya kuwa na Bajeti kubwa ambayo haitekelezwi ipasavyo.3. Serikali itazame upya utekelezaji wa Sera zake za kiuchumi kwani dalili zinadhihirisha kuwa Uchumi wetu unaanguka. Ikibidi Kuwe na Mjadala wa Kitaifa juu ya hali ya uchumi wa nchi yetu, mjadala huo usaidie kupata uhalisia wa hali mbaya ya uchumi wetu, mbinu za kuunasua, na mawazo ya kuinasua nchi kutoka kwenye utegemezi wa misaaada pamoja na mikopo inayoongeza ukuaji wa deni la Taifa.4. Serikali ionyeshe ilipo shilingi 800 bilioni isiyoonekana matumizi yake katika ripoti ya CAG yam waka wa fedha 2017/18.5. Serikali ileze ni kwa nini Fedha Jumla ya shilingi Trilioni 4.8 hazikupita kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina ili utolewaji wake uweze kufuata masharti ya Katiba na Sheria za nchi. Fedha hizi za Wafadhili zinaonekana Katika Vitabu vya Bajeti Lakini CAG hazioni kuingia mfuko Mkuu na hivyo kutoka kwake kunaweza kuwa ni kinyume Cha Sheria. Menejimenti ya Wizara ya Fedha na Mipango ihakikishe inafanya usuluhishi sahihi wa taarifa za fedha zilizotolewa kwa Wizara mbalimbali na fedha zilizopokelewa moja kwa moja na wahisani wa maendeleo katika miradi. Hazina ifanyiwe usafi maalumu ili kuhakikisha ‘credibility’ ya Taarifa zake.6. Serikali izingatie Sheria na Katiba Kuhusu Fedha za Taasisi ambazo zimetengwa kisheria Lakini Hazina inazitumia bila kujali Sheria. Hazina ihakikishe inazirejesha kwa wenyewe Ada, Tozo na mapato hayo ambayo TRA ilikusanya kwa niaba ya Idara, Wakala na Taasisi nyengine.7. Wabunge, kama sehemu ya wenye wajibu wa kutunga sera tunayo nafasi ya kuisimamia Serikali kwenye suala la kushuka kwa thamani ya shilingi, kwanza kwa kuwawajibisha wote waliosababisha sintofahamu ya zao la korosho ambalo kama tungeuza basi kungepatikana unafuu kwenye deni la Taifa.8. Ili kudhibiti kasi ya ukuaji wa Deni la Taifa, haswa Deni la Nje, kutokana na kushuka kwa thamani ya shilingi yetu, tunapendekeza kuwa Serikali ifanye hedging ya Deni la Nje ili kuwa na uhakika wa thamani ya fedha itakayotumika muda wote kuhudumia Deni hilo. Serikali ya Awamu ya Tano imeonyesha kutegemea sana mikopo ya kibiashara kutoka Mabenki ya Nje na hivyo kuweka nchi kwenye hatari kubwa ya Mtego wa Madeni (Debt Trap). Hedging inaweza kusaidia kudhibiti kasi ya ukuaji wa Deni la Nje.9. Tunamsihi ndugu Rais atambue kuwa njia ya bora ya kupambana na rushwa na ufisadi ni kuwezesha mifumo kufanya kazi. Mtu mmoja hawezi kamwe kuwa dawa ya ufisadi ulioota mizizi nchini kwetu. Ripoti za CAG na madudu yaliyoibuliwa kila kona inaonyesha dhahiri kuwa silaha ya uhakika ni kujenga Taasisi imara za Uwajibikaji ili kudhibiti Fedha za Umma. Miaka 4 aliyepo madarakani imethibitisha kuwa nguvu ya Mtu mmoja haitoshi kukomesha ubadhirifu bali Mifumo Imara.Ni matarijio yetu kuwa Watanzania wataendelea kuisoma na kuichambua Taarifa ya CAG na kuwaomba Wabunge watimize wajibu wao wa kuisimamia Serikali ili kujibu hoja zote za Ukaguzi. Bila Bunge kutimiza wajibu wake ipasavyo mzunguko wa uwajibikaji unakuwa haufungi. Tumeona Katika Taarifa ya CAG kuwa Hoja hazijibiwi na hivyo hazifungwi na madhara yake ni kuwa kila mwaka hoja zinaongezeka tu.


Ahsanteni Sana.

Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Mbunge, Kigoma Mjini
Kiongozi wa Chama, ACT W
azalendo
Aprili 14, 2019
Dodoma

18 Mar 2019


 
Leo Machi 18, 2019 ni siku ambayo lazima iingie kwenye vitabu vya kumbukumbu kwa sababu kuu tatu, ambazo zote zinamhusu mwanasiasa mkongwe Seif Sharif Hamad na Chama cha Wananchi (CUF)

Sababu ya kwanza, leo ni siku ambayo mwanasiasa huyo, maarufu kwa jina la Maalim Seif, "ametimuliwa" rasmi kutoka chama alichoshiriki kukiasisi (CUF).
Kibaya zaidi, "kutimuliwa" huko kumekuwa na baraka kisheria, baada ya Mahakama Kuu kumtambua Profesa Ibrahim Lipumba kuwa mwenyekiti halali wa chama hicho.

Ikumbukwe tu Lipumba alitangaza kujiuzulu uenyekiti kwa sababu anazozijua yeye kabla ya kuamua kurejea kwenye wadhifa huo "kwa mabavu." Kwa bahati mbaya – au pengine makusudi – sheria na kanuni za CUF zilikuwa zinatoa mwanya kwa Lipumba (au mwanasiasa mwingine yeyote yule) kufanya "uhuni" kama huo.

Sababu ya pili, ni kwamba leo CUF imekabidhiwa rasmi kwa Lipumba. Kisheria. Mahakama imetenda haki kwake kwa sababu japo alichofanya ni uhuni, kisheria uhuni huo ulihalalishwa na CUF yenyewe.

Hili la Lipumba kukabidhiwa chama si jambo dogo. Kuna mawili hapa. Moja, hii inaweza kuwa fursa nzuri kwa Lipumba kukijenga chama hicho na hatimaye kukirejesha kwenye nafasi ya kuaminika kama "mbadala wa CCM."

Lakini la pili, na hili ndilo ninahisi litatokea, ni mwanzo wa mwisho wa CUF. Sio siri kuwa Lipumba amesaidiwa sana na CCM kuipora CUF kutoka mikononi mwa Maalim Seif. CCM hawajafanya hayo kwa vile wanampenda Lipumba.Hapana. Wanamtumia tu kumdhibiti Maalim Seif ambaye licha ya kila hujuma zilizokuwa zikifanywa na CCM na taasisi zake, ameendelea kuwa mwanasiasa maarufu zaidi kuliko wote katika siasa za Zanzibar.

Sasa, baada ya Lipumba kutumika "kummaliza Seif ndani ya CUF," kuna uwezekano wa aina mbili tu. Wa kwanza ni kwa mwanasiasa huyo msomi kukubali kuendelea kutumika kama kibaraka wa CCM huku CUF ikigeuka kuwa CCM-B, na wa pili, ni kujaribu kusimama kama chama halisi cha upinzani na hapohapo "kumwagiwa radhi na CCM" na hatimaye kupelekea kifo cha chama hicho.

Uwezekano mkubwa zaidi ni huo wa kwanza - ukibaraka. Kwamba CUF haitokufa. CUF itaendelea kushiriki chaguzi mbalimbali. CUF itajenga taswira ya chama kamili cha upinzani. Lakini uwepo huo wa CUF hautokuwa kwa manufaa ya chama hicho au siasa za upinzani bali kwa manufaa ya CCM.

Kuna kila dalili kuwa CCM itaisaidia CUF kujitanua nchi nzima kwa sababu moja kuu: uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 utakuwa mbovu kuliko chaguzi zote zilizowahi kutokea Tanzania. Kuna uwezekano mkubwa tu kwa baadhi ya vyama vikuu vya upinzani kutishia kususia uchaguzi huo. Na hapo ndipo CUF ya Lipumba itakapotumika kuhalalisha "ushindi wa Magufuli/CCM."

CCM itaisaidia CUF kuweza kusimamisha wagombea takriban kila jimbo kwa upande wa Tanzania Bara. Lakini pia CCM itaisaidia CUF kuendelea kuwa chama imara cha upinzani huko Zanzibar, ambako uimara wake utasaidia kugawa kura dhidi ya CCM na wagombea wake.

Hata hivyo, "laana ya kutumika" itaikumba CUF baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 na kama isipoishia kusambaratika basi itabaki "chama jina" kama TLP ya Mrema.

Kuhusu uamuzi wa Maalim Seif kuhamia ACT- Wazalendo, japo hatua hiyo inaweza kuwashangaza baadhi ya watu, ukweli mchungu baada ya Mahakama Kuu kuhalalisha "uhuni" wa Lipumba, sambamba na "uhuni" wake mwingine majuzi ambapo "alijitangaza" kuwa Mwenyekiti kupitia "uchaguzi mkuu hewa" ambao pia "ulimtimua Maalim Seif" kwa kuteua mtu mwingine kushika wadhifa wa Katibu Mkuu.

Kwa kuzingatia muda mfupi uliosalia kabbla ya uchaguzi mkuu wa mwakani, Maalim Seif kuendelea kutafuta haki yake mahakamani kungeweza kumkuta akiwa bado kwenye korido za mahakama wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu ujao. Ni vigumu mno kwa chama cha siasa kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi mkuu huku kikiwa kinakabiliwa na mpasuko katika uongozi wake wa juu.

Kwahiyo, kimkakati, uamuzi huo wa Maalim Seif unaeleweka, na unaweza kuwa ni mbinu muhimu kwake kuendelea kuwa relevant kisiasa.

Hata hivyo, kuna uwezekano wa aina mbili kuhusu mustakabali wa Maalim Seif na wa chama chake kipya cha ACT- Wazalendo.

Uwezekano wa kwanza ni kwa chama hicho kuibuka kuwa tishio katika siasa za Tanzania. ACT – Wazalendo ni chama kizuri lakini ambacho hakikui. Kimeendelea kuwa "chama cha mtu mmoja" chini ya uongozi wa Zitto Kabwe. Kwa muda mwingine, chama hicho kimekuwa cha kiharakati zaidi kuliko cha kisiasa.

Mapungufu hayo yanaweza kubadilika kwa njia kuu tatu. Kwanza, Maalim Seif hajawahi kupata fursa nzuri ya kunadi mvuto wake kwenye majukwaa ya siasa za Tanzania Bara. ACT-Wazalendo wanaweza kuwa Jukwaa muhimu katika hilo.

Pili, Zitto  hajawahi kupata jukwaa mwafaka kunadi mvuto wake wa kisiasa huko Zanzibar. Kwa kuungana na Maalim Seif, hii inaweza kuwa ndio fursa mwafaka kwake.

Tatu, ACT-Wazalendo kama chama inaweza kupata fursa mwafaja kabisa ya kuwa chama cha kitaifa badala ya kuwa "chama cha Kigoma."

Haya yote yatawezekana tu endapo kutakuwa na "kujitoa mhanga" kati ya mwenyeji Zitto na mgeni Maalim Seif. Kwa mara ya kwanza, Zitto atajikuta akiongoza chama ambacho ndani yake kuna mwanasiasa maarufu zaidi yake. Naam, Maalim Seif ni mkongwe zaidi kisiasa kuliko Zitto. Endapo Zitto "atajitoa mhanga" (make a sacrifice) na kukubali "kumezwa" na umaarufu wa Maalim Seif, basi chama hicho kitakuwa na fursa kubwa ya kupanuka zaidi na hata kuja kuwa chama kikuu cha upinzani katika pande zote za Muungano.

Lakini endapo kutakuwa na mgongano wa ego kati ya wanasiasa hao, basi mustakabali wa chama hicho utakuwa mashakani. Lakini pengine uwezekano wa hili kutokea ni mdogo kutokana na ukweli kwamba suala la Maalim Seif kujiunga na ACT-Wazalendo sio limetokea tu ghafla. Ni dhahiri kuwa kulikuwa na majadiliano ya muda mrefu na yayumkinika kuhisi kwamba tofauti kati ya wanasiasa hao wawili (Maalim Seif na Zitto) zilifanyiwa kazi wakati wa majadiliano hayo.

Suala jingine ambalo linaweza kuijenga ACT-Wazalendo "mpya" (ya Zitto na Maalim Seif) au kuibomoa ni mtihani ulioikumba Chadema mwaka 2015.

Kwa mwelekeo ulivyo ndani ya CCM ambapo Magufuli hafanyi siri kuwa anataka chama hicho kiwe chini ya uongozi wa watu wake (wengi wao wakiwa wana-Kanda ya Ziwa wenzake), kuna uwezekano mkubwa wa kuibuka wimbi kubwa tu la wanasiasa wenye majina watakaotaka kuhamia Upinzani. Na endapo Zitto na Maalim Seif watakuwa "dream team" ya kuaminika, basi ACT-Wazalendo inaweza kuwa na mvuto zaidi kwa "wakimbizi kutoka CCM" kuliko Chadema.

Si ajabu kwa wanasiasa kama Nape Nnauye, Mwigulu Nchemba, Bernard Membe kujiunga na ACT-Wazalendo endapo chama hicho kitaonekana kuwa kinaweza kutoa ushindani wa dhati dhidi ya CCM hapo mwakani.

Sasa, wakati kupokea "majina makubwa" kutoka CCM husaidia kuongeaza umaarufu wa chama, uzoefu umeonyesha kuwa wengi wao wenye majina hayo makubwa ni wanafiki wanaokwenda upinzani kwa sababu zao binafsi na sio kwa maslahi ya vyama husika vya upinzani.
Kibaya zaidi, kila ujio wa "wahamiaji" hao ni fursa mwafaka kwa CCM kupandikiza "mamluki" wake kama ilivyotokea kwa Chadema ilipompokea Lowassa mwaka 2015.

Je ACT-Wazalendo "mpya" inaweza kutoa upinzani wa dhati dhidi ya CCM hapo mwakani? Jibu fupi ni "muda ndio utaongea" (time will tell). Jibu pana zaidi ni kwamba japo uwezekano huo upo lakini sidhani kama muda unatosha kukitanua chama hicho nchi nzima hususan katika kipindi hiki ambacho chama pekee cha siasa kinachoruhusiwa kufanya shughuli za siasa ni CCM tu.

Hata hivyo, endapo mkazo wa ACT-Wazalendo utakuwa katika sio tu kuongeza idadi ya wanachama bali kujenga kuaminika kwa "Watanzania wasio na vyama," basi huenda chama hicho kikafanya vizuri kwenye uchaguzi mkuu huo.

Ni hivi, kundi muhimu kabisa la wapigakura katika uchaguzi mkuu wowote ule nchini Tanzania ni "Watanzania wasio na vyama." Kwamba, hakuna chama cha upinzani kinachohitaji kupoteza muda wake kuwashawishi wafuasi wa CCM wakipigia kura, kama ambavyo CCM haina muda na wafuasi wa upinzani kuwashawishi waipigie kura. Vilevile, si CCM wala vyama vya upinzani vinavyohitaji kuwashawishi wanachama/wafuasi wao wapigie kura vyama vyao. Watu wanaohitaji kushawishiwa ni hao wasio na vyama. Na habari njema ni kwamba kundi hilo ndilo lwenye idadi kubwa zaidi ya wapiga kura.

Kwa mujibu wa takwimu zisizo rasmi, CCM ina takriban wanachama milioni 8 ilhali wapinzani wana wanachama takriban milioni 5. Kwa makadirio, takriban Watanzania milioni 25 walijiandikisha kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Kwahiyo, milioni 8 wa CCM jumlisha milioni 5 wa upinzani jumla inakuwa milioni 13. Ukichukua milioni 25 kutoa miloni 13 unabakiwa na milioni 12. Kwa makadirio, hawa ni "wapigakura wasio na vyama." Na kimahesabu, hata nusu tu ya kundi hili likielemea upande mmoja, upande huo unaweza kabisa kushinda uchaguzi husika. Of course, hapo tunaweka kando hujuma za kawaida za kuibeba CCM kwenye takriban kila uchaguzi mkuu.

Nimalizie kwa kukumbusha kuwa uchambuzi huu sio exact science. Umeelemea kwenye uelewa wa kutosha wa mchambuzi kuhusu siasa za Tanzania.

Kadhalika, uchambuzi huu ni endelevu. Utafanyiwa marejeo mara kwa mra kila kutakapokuwa na umuhimu wa kufanya hivyo


1 Jan 2019

Image result for happy new year 2019

Heri ya mwaka mpya 2019.

Kila mwaka mpya, blogu hii huwaletea ubashiri kuhusu masuala mbalimbal yanayotarajiwa kutokea nchini Tanzania katika mwaka husika. 

Hata hivyo, ni muhimu kutanabaisha mapema kuwa ubashiri huu sio exact science. Unatokana tu na ufahamu mkubwa wa mwandishi kuhusu siasa za Tanzania sambamba na mwenendo wa mabo ulivyokuwa mwaka jana 2018.

Moja ya matukio yanayotarajia kutikisha Tanzania ni jaribio la kumpindua Rais Magufuli. Jaribio hilo ni mwendelezo wa lile lililoshindikana mwezi Novemba mwaka jana na mwandishi alikuwa mtu pekee aliyeliweka hadharani.

Iwapo jaribio hilo litafanikiwa au la ni nje ya uwezo wa blogu hii kubaini hilo, lakini wahusika ni kundi lilelile lililojaribu kumdhuru Magufuli Novemba mwaka jana, kundi linalohusisha baadhi ya viongozi wa juu wa Idara ya Usalama wa Taifa.

Haitokuwa jambo la kushangaza endapo baadhi ya wahusika "wakadhibitiwa mapema" japo blogu hii haiwezi kueleza kwa hakika "kudhibitiwa" huku kutahusisha hatua gani. 

Sambamba na hilo ni ubashiri wa mabadiliko makubwa ya uongozi wa juu wa Idara ya Usalama wa Taifa.

Tukiweka hilo kando, inabashiriwa kuwa uhusiano kati ya Tanzania na nchi wahisani/jumuiya za kimataifa utakuwa mbaya zaidi ya ilivyokuwa mwaka jana, japo hatimaye Magufuli atafyata mkia na kuwaangukia wahisani hao kufuatia hali mbaya ya fedha serikalini.

Kadhalika, sokomoko la korosho sio tu litaendelea kupelekea watendaji kadhaa wa serikali kupoteza madaraka - sio kutokana na kufeli kwao bali kufanywa mbuzi wa kafara - lakini pia litajitokeza kwenye mazao mengine/sekta nyingine pia. 

Hata hivyo kama ambavyo tayari serikali imeanza "kubadili gia angani" katika suala la korosho, huko kwenye mazao mengine/sekta nyingine nako hatimaye serikali itaufyata lakini sio kabla ya kusababisha mkanganyiko mkubwa.

Inabashiriwa kuwa "hama hama" ya wabunge na madiwani wa upinzani kwenda CCM itarejea kwa kasi kubwa, hatua itakayolenga zaidi kudhoofisha jitihada za wapinzani kushikamana na kupambana na Magufuli.

Inabashiriwa pia kuwa baadhi ya miradi mikubwa inayopigiwa chapuo na serikali ya Magufuli itakwama kutokana na hali mbaya ya kifedha. 

Kadhalika kuna uwezekano wa ATC kuanzisha safari za kimataifa lakini itakuwa kwa muda mfupi tu baada ya ndege kuzuiwa nje ya nchi kutokana na madeni ya serikali nje ya nchi.

Vilevile, inabashiriwa kuibuka upya na kushamiri kwa "kelele" za kutaka muhula wa urais uongezwe kutoka miaka mitano ya sasa hadi miaka saba au zaidi. 

Inabashiriwa pia kuwa muswada wa mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa utapita licha ya upinzani mkali kutoka kwa vyama vya upinzani. 

Sambamba na tukio hilo ni uwezekano kwa Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe na mbunge wake Esther Matiko kuhukumiwa kifungo katika kipindi cha vuguvugu la kupitishwa sheria hiyo kandamizi.

Kadhalika, inabashiriwa kuwa kunaweza kufanyika jaribio la kumdhuru Mbunge wa Chadema Tundu Lissu kabla hajarejea nyumbani baada ya kuwa nje ya nchi kitambo kwa matibabu kufuatia jaribio la kutaka kumuua. Inabashiriwa kuwa kutakuwa na jitihada za makusudi za kumzuwia mbunge huyo machachari kurudi nyumbani.

Inabashiriwa pia kuwa baadhi ya wanachama maarufu wa CCM watavuliwa uanachama katika jitihada za Magufuli kutunisha misuli yake katika uongozi wa chama hicho. Walengwa ni wana-CCM ambao majina yao yanatajwa kama potential candidates katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Maamuzi ya kiuendawazimu ya Wakuu wa Mikoa/Wilaya yataendelea kutawala mwaka huu, wahusika wakuu wakiwa walewale waliovuma kwa maamuzi ya hovyo mwaka jana.

Habari njema kwa Watanzania wengi ni anguko la Daudi Albert Bashite na mpambe wake Musiba. 

Habari nyingine njema ni jinsi utawala wa Magufuli sio tu utawaleta viongozi mbalimbali wa upinzani karibu zaidi lakini pia kuna uwezekano wa viongozi hao kupata ujasiri na kushawishi wafuasi wao kuingia mtaani kudai haki kwa nguvu.

Kwa upande mwingine, hali ya uchumi itazidi kuwa ngumu kutokana na sababu za ndani na nje ya nchi.Ndani ya nchi ni pamoja na ukweli kwamba serikali ya Magufuli imeingia mwaka huu 2019 ikiwa na hali mbaya kifedha japo kumekuwa na jitihada kubwa za kutoa takwimu feki kuashiria kuwa uchumi uko vizuri. Kwa nje ni uwezekano wa mtikisiko wa kiuchumi kama ule wa mwaka 2008 ambao utatikisa sekta ya fedha/uchumi kimataifa.

Mwisho, kuna uwezekano wa kutokea shambulio la kigaidi - halisi au la kutengenzwa. Halisi ni kutokana na tishio linaloendelea huko Msumbiji ambako sio tu kuna "magaidi" kutoka Tanzania wanaosumbua huko bali pia kuna vikosi vya JWTZ vinavyosaidiana na jeshi la nchi hiyo kukabiliana na mashambulizi ya kigaidi nchi humo.

Uwezekano wa kutengenezwa tishio la ugaidi ni mbinu inayoweza kutumiwa katika kipindi ambapo serikali ya Magufuli itakuwa inaandamwa na suala linaloipelekesha.

Nimalizie makala hii kwa kutakia heria ya mwaka mpya 2019 na kusisitiza tena kuwa ubashiri huu sio exact science. 

Categories

Blog Archive

© Evarist Philemon Chahali 2006-2018

Powered by Blogger.

Download "Chahali Blog ANDROID App"