1 Oct 2009


PINDA ASHAURIWA AANZE KUMSHAURI JK KUHUSU SUTI ZA GHARAMA
Na Waandishi wetu
MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Lipumba, amemtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuwahamasisha viongozi ndani ya serikali akianzia na bosi wake Rais Jakaya Kikwete, aache kuvaa suti za gharama kubwa kutoka Ulaya na Marekani, badala yake wavae nguo za viwanda vya ndani, iwapo ana nia ya dhati ya kuikomboa jamii kiuchumi.

Juzi Waziri Mkuu ,Pinda alitoa kauli kuwataka Watanzania kuepuka kuvaa mavazi ya gharama kubwa ikiwemo suti, akieleza kuwa halizifai kwa nchi maskini kama Tanzania. Aidha alirejea kauli yake ya kupinga matumizi ya magari ya kifahari kwa mawaziri na viongozi wengine wa serikali.

“Mtu ambaye anaongoza kwa kuwakoga watanzania kwa kuvaa suti za bei mbaya, ni Rais Jakaya Kikwete ambaye anavaa suti za hariri kutoka nchi za Ulaya na Marekani,” alisema Profesa Lipumba na kuongeza:

“Kiongozi ni kioo cha jamii, sasa kama Pinda ana nia ya dhati ya kuwakomboa watanzania, kwanza aanze na bosi wake Rais Kikwete ili aonyeshe mfano kwa kuvaa nguo zinazotengenezwa na viwanda vyetu vya Urafiki na KTM”.

Mbali na Lipumba, Naye Mbunge wa Karatu, Dk Wilbrod Slaa (Chadema), aliungana na kiongozi huyo wa CUF kupinga kauli hiyo akisema inashangaza na kuonyesha wazi udhaifu wa serikali ya awamu ya nne katika kufanya maamuzi.

Dk. Slaa aliyasema hayo jana akiwa mjni Arusha anakohudhuria mkutano wa Chama cha Mabunge ya Jumuiya ya Madola (CPA).

Alihoji ,' Kama Pinda ambaye ni kiongozi mkuu serikalini analalamika kuhusu hali hiyo, Mtanzanzania wa kawaida atafanya nini?

“Kama yeye Waziri Mkuu ambaye ni mtendaji analalamika, mimi Dk Slaa nifanye nini,” alihoji mbunge huyo machachari wa kambi ya upinzani ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chadema.

Alimtaka Waziri Mkuu kuwa mkali katika kusimamia maadili mema kwa walio chini yake badala ya kulalamika kwenye majukwaa.

Mbunge wa Ilala Mussa Azan Zungu, alisema tamko la Waziri Mkuu ni zuri na linaonyesha wazi mkakati wa serikali ya awamu ya nne katika kupunguza gharama ambazo zinaweza kusaidia mambo mbalimbali ya kijamii.

“Jambo la msingi hapa ni kwa watendaji wote kila mmoja kwa nafasi yake kutimiza wajibu na kuyaingiza katika utekelezaji matamko ya Waziri Mkuu bila kusukumwa,” alisema Zungu.

Mbunge wa viti maalumu, Anna Abdallah licha ya kuunga mkono kauli ya Pinda, alishauri uwepo utaratibu maalumu wa mavazi ili kuepusha mkanganyiko kwa wananchi na hata watendaji serikalini.

Kwa upande wake, Balozi mstaafu ,Job Lusinde naye aliunga mkono kauli ya Pinda na kusema kuwa kiongozi huyo yuko sahihi.

Pinda alitolea mfano wa nchi ya Indonesia ambako wameamua kubana matumizi kulingana na uchumi wa nchi hiyo na kwamba hivi sasa hata rais wao ameamua kutumia vazi la kitambaa aina ya batiki kinachotengenezwa nchini humo.

Akizungumzia kauli hiyo ya Pinda jana, Lusinde alisema kuwa hata yeye amekuwa akiwashangaa viongozi wengi wanapofanya ziara zao kwenda mashambani wakiwa wamevalia vazi hilo la nchi za Magharibi, jambo alilolielezea kuwa ni kichekesho.

Alisema hata yeye wakati akiwa kiiongozi, hakupenda kuvaa suti mara zote na alikuwa haoni umuhimu wa kuvaa suti wakati kiongozi wake Hayati Baba wa Taifa akiwa na mavazi ya kawaida.

Lusinde alisema "katika kipindi cha utawala wa Nyerere hata wakati nakwenda kujitambulisha katika nchi nilizowahi kuwa balozi, nilikuwa katika vazi la ’Chu Eng-Lai’ ambalo kwa wakati huo lilikuwa kama vazi rasmi lililotoholewa kutoka China na hata picha zangu zote ukiziona utakuta niko katika vazi hilo kwa kulinda na kuenzi utamaduni wa Mtanzania”

Imeandikwa na Salim Said, Leon Bahati, Arusha na Habel Chidawali, Dodoma

CHANZO: Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.