2 Mar 2010

Japokuwa kutolewa kwa Yanga katika michuano ya kimataifa kunaweza kupokelewa kama habari njema kwa watani wao wa jadi Simba, lakini ukweli unabaki kuwa hiyo ni habari mbaya kwa medani ya soka la kimataifa kwa nchi yetu. Lakini kipigo hicho kinaweza pia kuwa fundisho zuri kwa vilabu vyetu vya soka,hususan Simba na Yanga,vilivyokumbwa na “ugonjwa” wa makocha wa kigeni.

Nimesoma utetezi wa kocha wa Yanga, Kosta Papic, kwenye gazeti la Mwananchi kwamba sababu kuu za kutolewa kwa timu hiyo ni uwanja mbovu, hali ya hewa na matokeo mabaya katika pambano la awali. Kwa ujumla sababu zote hizo si za kitaalamu kwani hata shabiki ambaye hajawahi kucheza chandimu anaweza kukurupuka na sababu kama hizo. Papic anatoa visingizio hivyo huku akielewa fika kuwa havitoi majibu ya kwanini timu yake ilipata matokeo kama hayo (kufungwa) katika mchezo wa kwanza uliofanyika Dar es Salaam.

Je hali ya hewa ya Dar nayo ilichangia Yanga kupoteza mchezo wa awali? Vipi kuhusu uwanja wetu mpya na wa kisasa? Ni dhahiri kuwa alichofanya kocha huyo ni kuamua “kusema chochote” badala ya kukaa kimya. Kufungwa, na hatimaye kutolewa kwa Yanga hakuwezi kutohusishwa na mapungufu ya kocha huyo wa kigeni, na Papic analijua hilo ndio maana akakimbilia kuja na visingizio visivyo na uzito.

Lakini kwa namna flani, kuwalaumu makocha wa kigeni kwa asilimia 100 ni kama kutowatendea haki kwa vile hawakujiajiri wenyewe.Vilabu vyetu, licha ya kuwa ombaomba na kutegemea hisani za wafadhili, ziko tayari kujikakamua na umasikini wao wa kujitakia ili ziwe na “ujiko” wa kocha wa kigeni. La muhimu sio kocha anatoka wapi bali umuhimu wake kwa maendeleo ya timu husika.

Na kwa upande flani angalau makocha wazawa, au wa kutoka nchi jirani, wanaweza kuvumilia “mbinde” zinazotawala kila kukicha katika vilabu vyetu vya soka. Sasa kwa makocha wanaotoka sehemu zenye “tamaduni tofauti” kama Papic,kwa hakika kumudu soka letu inakuwa shughuli pevu.Sote twajua,kwa mfano,jinsi vilabu vyetu vinavyoendekeza “kamati za ufundi” kuliko ushauri wa wataalam wa soka. Sasa kwa kocha “mzungu” mwenye “roho nyepesi”, mambo kama hayo yanaweza kumkimbiza mapema tu.

Ni muhimu sasa kwa Yanga na timu zetu nyingine za soka kutafakari upya “ugonjwa” huu wa makocha wa kigeni. Ikumbukwe kuwa wakati kocha ni sehemu muhimu ya mafanikio ya klabu, wachezaji na mazingira ya soka katika mahala husika ni muhimu pia katika kupata mafanikio. Kwa mfumo wa kibabaishaji unaotawala medani ya soka letu, hata akija kocha mahiri kama Sir Alex Ferguson au Jose Maurinho bado hadithi inaweza kuendelea kuwa kama hiyo ya Yanga huko DRC.

Vilabu vyetu vinapaswa kutengeneza mazingira mazuri hususan kwenye ngazi ya uongozi na kujijengea uwezo wa kujiendesha pasipo kutegemea ridhaa za wafadhili.Ni katika mazingira hayo ndipo vitamudu kufanya usajili wa kutengeneza vikosi vya ushindi visivyo hitaji kusajili na kuacha wachezaji mara kwa mara.Kadhalika,ili kuunda timu ya ushindi ni muhimu kwa vilabu hivyo sio tu kuwa na vikosi visivyobadilika kila msimu bali pia kuwa na walimu (makocha) wanaookaa na wachezaji kwa muda mrefu ili kujenga mshikamano na kuelewana.Vingenevyo,tutaendelea kuwa wasindikizaji tu katika michuano ya kimataifa.


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.