31 Dec 2010



Muda huu natoka Kanisani.Dada yangu mmoja wa Kizulu alinialika kanisani kwao.Ibada ilikuwa ya kumshukuru Mungu kwa kumaliza mwaka huu 2010 salama,na kuomba baraka kwa ajili ya mwaka 2011 ambao tunatarajia kuuona takriban masaa 13 kutoka sasa (kwa mujibu wa masaa ya hapa-tuko nyuma masaa matatu kulinganisha na huko nyumbani Tanzania,na masaa sita mbele ya Houston kwa Mrs Chahali mtarajiwa.Lol!).

Cutting the story short,Mchungaji wa Kibrazili aliyeendesha ibada ya leo alitushtua aliposema,"Samahani,ningependa sana kuwatakia heri ya mwaka mpya lakini...".Kisha akafafanua kwanini amemalizia na LAKINI.Alitoa mfano huu ulionigusa mno.Alisema kwamba kuingia mwaka mpya ni mithili ya kwenda sehemu ambayo hujawahi kufika kamwe.Tuchukulie mfano wa mahala nilipozaliwa,Ifakara.Je haingekuwa jambo la busara kuwapata wadogo zangu Peter na Paul (Kulwa na Doto,respectively) wakakuelekeza ulipo Mto Lumemo au Mto Kilombero?Au wakakuelekeza shule ya msingi niliyosoma ya Mapinduzi au sekondari nilyosoma ya Kilombero Day?Au pengine ungetaka kwenda Hospitali ya Mtakatifu Fransis au kufika eneo la Viwanja Sitini.Au labda ungetaka kwenda mahala zilipo ofisi mbalimbali za serikali huko Kibaoni,na mapacha hao wakakupatia guidance.

Katika ufafanuzi wake,Mchungaji huyo alieleza kwamba kama ilivyo tunapoingia mwaka mpya ambao hatujui kinachotusubiri,ndivyo ilivyo tunapoingia sehemu ambayo hatujui lolote kuihusu.Hatujui maeneo yenye vibaka ambapo kuonyesha simu au saa ni sawa na kutangazwa mwaliko wa kupigwa roba ya mbao.Hatujui mitaa ambayo mtu wa heshima ukionekana unaweza kudhaniwa unasaka huduma ya dada poa.Na kwa uswahilini,huwezi kujua mitaa inayoaminika kuwa makazi ya majini,mashetani,vibwengo,wanga,na viumbe kama hao.Kumpata mwenyeji kutakuepusha na sintofahamu hiyo.

Basi,Mchungaji alieleza kuwa safari ya kwenda mji ambao hatujawahi kufika-yaani mwaka 2011- ina mwenyeji wake.Kuna akina Kulwa na Doto wa Ifakara katika safari hiyo.Na mwenyeji huyo si mwingine bali ni Muumba wetu,Mungu mweza wa yote.Yeye anajua kila litakalotokea kuanzia saa 6 na kamili na sekunde moja hadi saa tano usiku na sekunde hamsini na tisa ya tarehe 31.12.2011.Mungu ni mzaliwa na mwenyeji wa mji huo tusioujua wa MWAKA 2011.

Sasa kwanini tuhangaike kuuliza huku na kule,hapa na pale kuhusu mji huo wakati tuna mwenyeji ambaye sio tu anaufahamu vilivyo mji huo wa mwaka 2011,lakini pia yuko tayari kutupatia makazi na mlo wa bure buleshi?Sharti lake jepesi ni moja tu: KUMWAMINI YEYE KUWA NDIYE MWEZA WA YOTE.Kumkabidhi kila tulichonacho kwa maana na mwili na roho na kuamini kuwa atatupatia ulinzi na mwongozo.

Hebu rewind tarehe hii miezi 12 iliyopita.Ni watu wangapi walikutakia HAPPY NEW YEAR?Bila shaka ni wengi.Lakini hebu tutafakari.Je hizo best wishes zimetisaidia vipi kukwepa madeni,magonjwa,chuki,migongano ya kifamilia, na matatizo mengine tuliyokutana nayo mwaka huu tunaoumaliza leo?Ndio,napaswa kuwatakia heri ya mwaka mpya wasomaji wangu wapendwa wa blogu hii.Lakini je salamu hizo za heri pekee zitatosha kuifanya 2011 kuwa mwaka wa maana kwako na kwangu?

Basi,nami naomba nifuate mfano wa Mchungaji Mbrazil kwa kusema HERI YA MWAKA MPYA,LAKINI....(TUJIKABIDHI KWA MWENYEJI WA MJI HUU TUSIOJUA AMBAO TUTAUINGIA MUDA MFUPI UJAO-YAANI MWAKA 2011.NA KWA VILE MWENYEJI WETU HUYO NI MWENYE UPENDO,ATATUPATIA TOUR GUIDE YA BURE,MAKAZI NA MLO BURE).

6 comments:

  1. Asante kwa ujumbe Mkuu na Heri ya Mwaka Mpya!

    ReplyDelete
  2. Mkuu,tunakutakia kila heri na wewe pia.

    ReplyDelete
  3. KHERI YA MWAKA MPYA NA WEWE KAKA EVARIST!!

    ReplyDelete
  4. HAPPY NEW YEAR TO YOU TO MY DEAR BROTHER EVARIST. MUNGU AZIDI KUKUBARIKI.

    ReplyDelete
  5. Kila la heri. Mapya na mazuri zaidi kwa mwaka huu. Pamoja daima!!!

    ReplyDelete
  6. Heri ya mwaka mpya wa mapambano ya kupata uhuru wa kweli na kamili, yaani katiba mpya iliyo yetu na kwa ajili yetu.

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.