11 Feb 2012


Uongo una tabia moja kuu: usipokanushwa huweza kujenga hadhi ya kuonekana ukweli.Ni kwa sababu hiyo,mara nyingi siruhusu kitu kisicho na ukweli kiachwe kuishi na hatimaye kionekane ni cha kweli.

Nilipoingia kwenye ukurasa wangu wa Twitter hapo jana nilikumbana na tweets za waungwana wawili, Bwana @semkae na Ndugu @chiume, ambapo pasipo kuingia kiundani kunukuu kila walicho-tweet,waliniona kiojakwa mambo mawili: kwanza, "kuingizwa mkenge" kunukuu tweets za Rais Jakaya Kikwete kwenye makala yangu katika toleo lililopita la jarida la Raia Mwema,na pili,kuandika "nilifanya maongezi yasiyo rasmi na Rais Kikwete."

Nianze na hilo la pili.Tofauti na ilivyokuwa nyakati za Zama za Mawe ambapo njia pekee ya mawasiliano ilikuwa kukutana uso kwa uso,maendeleo ya teknolojia sasa yanawezesha mawasiliano kwa njia mbalimbali kama vile barua-pepe,SMS,mitandao ya jamii,nk.Kwa watu wenye mawazo ya kale,ukisema NIMEONGEA NA FLANI basi kwao lazima iwe aidha maongezi hayo ni ya barua kupitia posta,uso kwa uso au (kidogo) SMS au e-mail.Kwa mtizamo wa watu hao,ukijadiliana na mtu huko Facebook au Twitter basi huna haki ya kusema MMEONGEA.Kwao maongezi ni lazima ufumbue mdomo na maneno yatoke mdomoni kama si maandishi kwenye barua,nk.

Chanzo cha nukuu husika ni swali nililomuuliza Rais kuhusiana na mkanganyiko uliojitokeza kuhusiana na suala la posho za wabunge.Nilijibiwa na mheshimiwa,na kwa vile makala yangu katika toleo lililopita la Raia Mwema ilikuwa inazungumzia suala hilo basi sikuona ubaya wa kunukuu majibu hayo ya Rais Kikwete (pasipo kupunguza au kuongeza neno).Na kwa kuondoa utata,nikaandika "nilifanya MAZUNGUMZO YASIYO RASMI na Rais kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter kwa kumuuliza...."

Sikuandika hivyo kwa minajili ya kutaka sifa kuwa "eeh nimeongea na Rais..." bali kama muumini wa kuthibitisha hoja kwa mifano hai ilikuwa muhimu kuambatanisha nukuu hizo.

Lakini pengine kuwafumbua macho waungwana hawa kuelewa kuwa katika zama tunazoishi hata tweet ya kiongozi inaweza kuchukuliwa kama tamko lake rasmi,angalia taarifa ifuatayo ya Shirika la Utangazaji la Kenya ambalo (kama nilivyofanya mie) walinukuu tweet ya Rais Kikwete

Kama KBC walinukuu tweet ya Kikwete na haikuwa tatizo kwa @semkae na @chiume kwanini basi matumizi yangu ya nukuu ya aina hiyohiyo iwe tatizo?

Twende kwenye hoja ya kwanza kwamba handle ya @jmkikwete sio ya Rais Jakaya Kikwete.Awali ilidaiwa kuwa inatumiwa na timu yake ya mitandao ya kijamii lakini kadri mjadala ulivyoendelea ikadaiwa kuwa hiyo handle ya @jmkikwete ni feki,huku wengine wakiita ni mzimu.

Hoja baada ya hoja.Hivi kweli pamoja na madudu mbalimbali yanayoendelea huko nyumbani,inawezekana kweli mtu mmoja akakurupuka na kujiita Jakaya Kikwete,Rais wa Nne wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania,na asichukuliwe hatua?


Lakini hata tukikutana na hoja kama "ah kama wameshindwa kuwakamata majambazi wa Kagoda wataweza kumkamata huyu anayejifanya Rais Kikwete huko Twitter?" bado kuna hoja nyingine kadhaa zinazoweka nguvu kwenye ukweli kuwa @jmkikwete ni Rais mwenyewe.

Hebu bonyeza LINK HII na utapelekwa kwenye ukurasa wa Social Good Summit iliyofanyika jijini New York Marekani kuanzia tarehe 19 hadi 22 Septemba mwaka jana.Kwenye ukurasa huo,ukishuka hadi profile ya mtoa mada (speaker) wa 31 utakutana na picha na wasifu mfupi wa Rais Kikwete.Chini ya maelezo hayo kuna link ya akaunti yake ya Twitter.Guess what?Ni hiyohiyo @jmkikwete ambayo @semkae na @chiume wanadai ni feki.

Kila mtoa mada ameweka link ya social media profile zake.Sasa kwanini Rais Kikwete atumie profile ya mtu hewa?Halafu habari husika imewekwa kwenye tovuti ya Mashable ambayo kwa anayefuatilia teknolojia na social media atakuwa anaelewa fika hadhi yake mtandaoni.Au nao waliingizwa "choo cha kike" (kunukuu kebehi ya @chiume)?


Ukienda kwenye ukurasa husika  na hatimaye kwenda kwenye wasifu wa Kikwete,ukibonyeza 'kindege cha Twitter' utapelekwa @jmkikwete.Hiyo ina maana gani?Tuwaachie @semkae na @chiume watueleze

Lakini hata kama hiyo si hoja ya msingi,ukienda kwenye ukurasa wa profile @jmkikwete ambayo hadi sasa ina followers 11336 (yani watu wote hawa nao wameingizwa "choo cha kike"?) utakuta watu na taasisi zenye heshima waki/zikimufata @jmkikwete.Kuanzia CCM hadi Chadema,Mbowe hadi  Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu Salva Rweyemamu na Ubalozi wa Uingereza huko nyumbani.Lakini kubwa zaidi ni familia ya Kikwete mwenyewe,yaani mkewe Mama Salma na wanae Ridhiwani na Miraji.Yaani hata familia ya Kikwette nayo inamfuata @jmkikwete 'feki'!!!!?????

Na MAKALA HII kutoka Rwanda inatanabaisha kuwa Rais Kikwete ni miongoni mwa viongozi wachache wa Afrika-pamoja na marais Paul Kagame na Jacob Zuma-ambao wapo Twitter.Je @semkae na @chiume wanaweza kutwambia kama @jmkikwete sio Rais Kikwete then anatumia handle gani?

Talking of Zuma,waungwana hao walidai kuwa kinachowafanya waamini kuwa @jmkikwete si Rais Kikwete ni kwa vile akaunti hiyo haijawa verified.Wanasema hayo ilhali wao wenyewe akaunti zao haziko verified lakini tunaamini tunao-interact nao ni wao halisi.Na kama suala ni verification,mbona hata Rais Zuma naye akaunti yake ya Twitter (@therealjz) sio verified?Au naye ni mzimu?Hoja mfu hazina uhai mrefu kabla ya kurejea tena kaburini.
La mwisho,na ambalo nisngependa kuingia kwa undani ni vyanzo vyangu binafsi.Kila mmoja wetu ana past yake.Kwa sababu za kimaadili,huwa sipendi kuzungumzia past yangu.Ninachoweza kuandika hapa ni kwamba kupitia past hiyo nimeweza kuthibitisha mambo mbalimbali kabla siyaandika kwenye makala zangu.Na licha ya past hiyo,hakuna kitu ninachoepuka kwa nguvu zote kama kupotosha wasomaji wa jarida lenye heshima kubwa huko nyumbani la Raia Mwema.Mara nyingi ninalazimika kuwapigia simu angalau watu wawili hadi watatu kabla sijaandika makala ili kuhakikisha kuwa ninachoandika ni sahihi.Na watu hao ninaowauliza ni vyanzo vya uhakika kabisa.Lakini kwa mtu mbishi anaweza kudai huo pia ni uzushi...au kwa kunukuu nkauli ya Bwana @semkae, ni MISREPRESENTATION tu.

Nakuachia msomaji ufikie hitimisho mwenyewe.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.