13 Sept 2013

NIANZE makala hii kwa kuungana na Watanzania wenzangu katika ‘maombolezo’ ya kifo cha heshima na hadhi ya Bunge letu tukufu. Kilichotokea bungeni wiki iliyopita, ambapo kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu, mbunge aliyechaguliwa na wananchi alibebwa mzobemzobe kana kwamba ni mhalifu fulani, ‘kimeua’ kabisa hata ile hadhi na heshima kidogo kwa taasisi hiyo muhimu ya kutunga sheria.
Pengine kutokana na majonzi ya ‘kifo hicho cha heshima na hadhi ya Bunge’ ndio maana Watanzania wengi tayari wamesahau kuhusu tukio hilo la aibu na kufedhehesha (wanasema wakati mwingine moja ya njia za kukabiliana na majonzi yanayoambatana na msiba ni kujaribu kusahau kuhusu msiba huo ili maisha yaweze kuendelea kama kawaida).
Lakini pengine kuanza kusahaulika kwa tukio hilo ni mwendelezo tu wa kasumba ya Watanzania wengi, ambapo hata kukitokea tukio gani linalopaswa angalau kukemewa tu, baada ya siku mbili tatu huwa limesahaulika. Ninachelea kuiita kasumba hiyo kuwa ni uzembe, kwa hiyo labda neno mwafaka ni upole.
Nadhani, anayepaswa kubebeshwa lawama kuhusu tukio hilo ni Naibu Spika Job Ndugai, ambaye takriban kila kikao cha Bunge amekuwa akifanya kila awezalo kuwaonyesha ubabe wabunge wa vyama vya upinzani. Hivi kilichomshinda Ndugai kumruhusu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe, azungumze alichotaka ni kipi hasa?
Ni vema Naibu Spika huyo akatambua kuwa hatokuwa na wadhifa huo au ubunge milele. Ukosefu wa busara katika uamuzi wake huko bungeni unaweza kumgharimu sana huko mbele, hasa baada ya kustaafu au kung’olewa katika wadhifa huo.
Pamoja na ubaya wa tukio hilo, angalau kumejitokeza sauti za hekima, tena kutoka ndani ya chama tawala CCM. Mwanasiasa wa kwanza kutoka chama hicho kupingana na ‘hekima’ za Ndugai ni Mbunge wa Msalala, Ezekiel Maige, ambaye ameeleza bayana kuwa vurugu zilizotokea bungeni zingeweza kuepukika laiti busara ingetumika na kumruhusu Mbowe azungumze alichotaka.
Mbunge mwingine ni Lazaro Nyalandu. Kauli yake ina umuhimu zaidi kwa vile yeye pia ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii. Nyalandu, ambaye binafsi ninamwona kama mfano wa kuigwa na viongozi wenzie wa CCM kutokana na kutanguliza maslahi ya taifa badala ya itikadi za siasa pekee, alieleza kupitia mtandao wa Twitter kuwa naye anaamini vurugu zilizojiri bungeni zingeweza kuepukwa laiti Mbowe angeruhusiwa kuzungumza.
Japo kauli hizi mbili zinaweza kuonekana za nadra kutoka kwa viongozi wa CCM, na si ajabu zikawatengenezea upinzani ndani ya chama hicho kilichozoeleka kwa mtizamo finyu wa kuwachukia wapinzani kana kwamba ni maharamia fulani, zinabainisha jambo moja la msingi, pamoja na mengi yanayokera kuhusu CCM, bado chama hicho kina hazina japo ndogo ya wanasiasa wenye upeo na uelewa wa umuhimu wa siasa za maridhiano na upendo kwa maslahi ya nchi.
Lengo la makala hii si kujadili ‘kifo cha hadhi na heshima ya Bunge’ kilichojiri wiki iliyopita huko Dodoma. Ninachodhamiria kukiongelea leo ni ‘reactions’ zilizotokana na makala yangu katika toleo lililopita la gazeti hili ambayo ilizungmzia suala la uraia pacha.
Tangu nianze kuandika makala katika gazeti hili maridhawa sijawahi kupata maoni mengi kama ilivyokuwa wiki iliyopita. Kwa bahati mbaya au nzuri, wengi wa waliotoa maoni walionyesha kutoafikiana na makala hiyo, huku wengine wakienda mbali zaidi na kunitupia shutuma mbalimbali.
Kuna walionituhumu kuwa ‘ninajikomba’ kwa Waziri Membe (ambaye nilimpongeza katika makala hiyo kwa jitihada zake katika suala hilo la uraia pacha), na wengine wakaenda mbali zaidi na kudai ‘kujikomba’ huko kunahusiana na tetesi kuwa Waziri Membe ni mmoja wa wanaoweza kuwania urais, mwaka 2015 kupitia CCM.
Wengine wakadai kuwa ninatumiwa na Waziri Membe, huku wakihusisha ‘kutumiwa’ huko na kile walichokiita ‘harakati zake za kujijengea jina kwa ajili ya kuwania urais katika uchaguzi mkuu ujao.’
‘Kosa’ langu (na pengine la Waziri Membe) ni kuwa na mtizamo unaotofautiana na baadhi ya Watanzania wenzetu ambao hawataki kabisa kusikia kuhusu suala la uraia pacha.
Bahati nzuri, mwenye mtizamo chanya kuhusu suala hilo si Waziri Membe pekee. Kwa tunaofuatilia suala hili kwa karibu tunatambua kuwa hata Rais Jakaya Kikwete anaafiki umuhimu wa uraia pacha. Kadhalika, takriban wanasiasa watatu niliowasiliana nao kupitia mtandao wa twitter wamebainisha kuunga mkono wazo hilo. Wanasiasa hao ni pamoja na Nyalandu, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Januari Makamba na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Abdallah Mwinyi (ambaye ni mtoto wa Rais wa Awamu ya Pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi).
Hadi sasa, hoja kubwa ya wanaopinga suala la uraia pacha ni uzalendo. Wanadai kuwa Mtanzania aliyeamua kuchukua uraia wa nchi nyingine na kuukana wa Tanzania hana uzalendo. Waungwana hawa hawataki kabisa kuelewa kuwa uamuzi wa kuukana uraia wa Tanzania unatokana na sheria iliyopo ambayo inamlazimisha Mtanzania anayechukia uraia mwingine kuukana uraia wake wa asili wa nchi yetu.
Kadhalika, wapinzani wa uraia pacha hawataki kabisa kuangalia ukweli kwamba matatizo mawili makubwa yanayoikabili nchi yetu kwa sasa- ufisadi na dawa za kulevya- yanafanywa zaidi na Watanzania wenzetu wasio na uraia wa nchi nyingine. Kwa lugha nyingine, kuwa Mtanzania ‘kamili’ (kwa maana ya kutochukua uraia wa nchi nyingine) hakumzuii mtu kuwa fisadi kwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
Na licha ya kupuuza kuwa uraia pacha ni haki ya kibinadamu kwa Mtanzania yoyote yule, wapinzani wa hoja hiyo hawataki kupanua mtizamo wao katika hoja yao ya uzalendo. Hivi kwa mtizamo mwepesi tu, nani mzalendo zaidi kati ya Watanzania kama sisi tulio nje lakini tunapigia kelele maovu na kupigania haki za walalahoi katika Tanzania yetu (hadi kufikia hatua ya kuhatarisha maisha yetu) na baadhi ya Watanzania wenzetu wanaolipwa mishahara minono ya zaidi ya shilingi milioni 10 kwa mwezi ili kuwawakilisha Watanzania wenzao huko bungeni lakini wameishia kuligeuza Bunge kuwa uwanja wa mipasho, matusi na sasa kupigana bungeni na kutoana mzobemzobe nje ya ukumbi wa Bunge?
Simaanishi kila Mtanzania aliye nje au mwenye uraia wa nchi nyingine anashiriki katika harakati tunazohangaika nazo, lakini ukweli unabaki kuwa hoja ya uzalendo kwa minajili ya kuwa ndani au nje ya nchi haina mashiko. Kupinga uraia pacha kwa hoja ya kufikirika kuwa mwanamke mmoja hawezi kuwa na mabwana wawili” (na huu ni mfano wa ubaguzi kwa sababu kwa nini iwe dhambi kwa mwanamke mmoja kuwa na mabwana zaidi ya mmoja lakini ni ‘sifa’ kwa mwanaume kufanya hivyo- tukiweka kando sheria za ndoa za kiislamu zinazoruhusu mwanaume kuoa hadi wanawake wanne)?
Nimalizie makala hii kwa kusisitiza tena kuwa suala la uraia pacha linahusu haki za kibinadamu za Watanzania wenzetu waliolazimika kuchukua uraia wa nchi nyingine. Hawa ni Watanzania kama Mtanzania mwingine yoyote yule, lakini kinachowatenganisha na Watanzania wenzao ‘halisi’ ni sheria ya kibaguzi inayoharamisha Utanzania wao.
Wito wangu kwa wapinzani wa hoja ya uraia pacha ni kujaribu kuweka kando hisia (kama hiyo ya kuwaona Watanzania waliochukua uraia wa nchi nyingine wana uhaba wa uzalendo) na kukazania kwenye uhalisi (kwa mfano kwa baadhi ya wabunge wetu ambao licha ya kuwapatia marupurupu manono ili wawakilishe wananchi vizuri wamegeuka ‘wana-maigizo’, mabingwa wa matusi na ubabe). Lakini kingine cha msingi zaidi ni kujaribu kujiuliza mzalendo halisi ni Mtanzania wa aina gani?

- See more at: http://raiamwema.co.tz/mzalendo-halisi-ni-mtanzania-wa-aina-gani#sthash.PIKUdrXR.dpuf

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.