14 Nov 2013


Kapuya matatani
•  ADHIBITIWA NA KITOTO KINACHODAI ALIKIBAKA, AKAKIAMBUKIZA VIRUSI


MBUNGE wa Urambo Magharibi, Profesa Juma Kapuya (CCM), ameingia katika matata. Katika kujaribu kudhibiti mtoto wa shule ambaye anadai alibakwa naye na kuambukiwa virusi vya ukimwi, mbunge huyo ametoa vitisho vya kuua mtoto huyo na kujiua kama njia ya kuepuka dhahama inayoelekea kumkabili.

Siku moja baada ya gazeti hili kuripoti habari za mbunge mmoja (bila kumtaja jina), jana asubuhi Profesa Kapuya ameibuka na kumtisha mwanafunzi huyo mwenye miaka 16 anayesoma Shule ya Sekondari Turiani iliyoko Magomeni jijini Dar es Salaam.

Baada ya kujua kuwa mtoto huyo ndiye alitoa habari za masahibu hayo, ambayo mbunge hakutaka yajulikane, alimpigia simu mtoto huyo, na baadaye kutuma meseji kadhaa za vitisho.

Jana Tanzania Daima ilishuhudia baadhi ya meseji za simu zilizotumwa na Profesa Kapuya kwenda kwa mtoto huyo.

Alfajiri saa 11:21 kupitia simu yake ya mkononi yenye namba 0784993930, Profesa Kapuya alituma ujumbe ufuatao kwa mtoto huyo: “chagueni kunisubiri tuje tuongee au mnataka kufa?”

Baadaye saa 1:07 asubuhi, alituma ujumbe mwingine kutoka simu hiyo hiyo kwenda kwa mtoto huyo, ukisema: “Mkiuawa, itakuwa nzuri, itawapunguzia gharama za kuishi. Usitake kugombana na serikali, mtoto mdogo kama wewe. Sisi ndo wenye nchi yetu.

“Mwambieni Mbowe mwenye hilo gazeti awape nyumba ya kuishi. Si mmemuingizia hela leo? Mnatumika bure watu wanaingiza hela nyingi, mmenitibua lazima niwauwe wiki hiii haitaisha, nitapanga kambi popote.

“Jana si wamekuficha? Tuone kama utalindwa milele. Kazi ya kulindwa imeisha, maana wameshatengeneza hela. Lazima mvae sanda. Hilo sio ombi, ni wajibu wenu. Mnajitia mafia watoto sio? Watoto wetu wanauza unga, nani anawakamata? Nani atapigana nasi?”

Hata hivyo, baada ya kuhisi kuwa watoto hao wamedhamiria kumchukulia hatua, na wamewasiliana na taasisi mbalimbali za kiraia na serikali zenye uwezo wa kumtia adabu, mbunge huyo alimtumia mtoto huyo ujumbe wa kuonyesha alikuwa anafikiria kunywa sumu..
Ujumbe huo uliotumwa kwa mtoto huyo saa 11:2 3 ulisema: “nimwakosea sana, acha nife mie nakunywa sumu nijiue, na nyie mje mnizike.”

Hasira za Profesa Kapuya dhidi ya mtoto hao zilitokana na hatua ya mtoto huyo na dada yake kufichua unyama wanaodai kutendewa na mbunge huyo, ambaye amewahi kushika nyadhifa kadhaa za uwaziri katika Serikali ya Awamu ya Nne.

Tangu alipogundua kuwa mtoto huyo alizungumza na gazeti hili juzi, saa 5:17 usiku wa kuamkia jana alituma ujumbe usemao: “Si mpo Bilz? Sasa tupo pamoja na nyie mpaka usiku.”

Baadaye saa 5:31 alituma ujumbe  huu: “Hivi hamkubali kushindwa? Leo ulifuata nini ofisi ya CCM?”

Ujumbe huo ulitokana na ukweli kwamba dada wa mtoto anayedaiwa kubakwa alifika Makao Makuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) juzi asubuhi kuonana na Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana, ili kuomba chama kimsaidie kumbana Profesa Kapuya, ambaye alikuwa ameanza kuwatisha yeye na mdogo wake.

Hata hivyo, kwa mujibu wa mtoto huyo, Kinana alisema suala hilo si la chama bali la Profesa Kapuya binafsi.

Mtoto huyo alikataa ushauri wa kupeleka shauri hilo mbele ya vyombo vya sheria, akidai kuwa jitihada zake zimekuwa zinazimwa na mbunge huyo anayedai serikali haiwezi kumfanya lolote.

Alisisitiza kuwa hana imani na serikali, lakini akasema yupo tayari kuchukua hatua kali dhidi ya Profesa Kapuya iwapo atasimamiwa na watetezi wa haki za binadamu.

Baadhi ya mashirika yanayotetea makundi kadhaa yakiwamo Kituo cha Sheria na Haki za BInadamu (LHRC) na Mtandao wa Kijinsia Tanzania (TGNP) yalijitokeza kumsaidia watoto hao, ambao ni yatima.

Mtoto huyo na dada yake, wakizungumza na gazeti hili kwa hofu mafichoni, walisema kwa sasa hawana imani tena kama kuna serikali nchini Tanzania kwa kuwa wamedhalilishwa, wametembezwa hadi Bungeni na wabunge bila hatua kuchukuliwa, licha ya kutoa taarifa katika kituo cha polisi Oysterbay tangu mwaka jana.

Hata hivyo, kabla ya tukio la watoto hao kuripoti, ofisi za gazeti hili juzi usiku kulikuwa na watu waliokuja wakiwatafuta watoto hao, huku wakiwatisha kwa simu na kuwatolea maneno ya kejeli, wakidai watawamwagia tindikali.

Mmoja wa watoto hao, alidai kuwa miongoni mwa vijana waliokuwa wanawatisha juzi walikuwa katika gari T170 BGY, Benz, Cream Metalic, ambayo inamilikiwa na mbaya wao.

Jana gazeti  hili lilichapisha habari kuwa  mwanafunzi huyo aliyesema kuwa waziri huyo  alimbaka kwenye hoteli moja ya kitalii iliyoko jijini Dar es Salaam mwaka 2011, na kurudia tena kitendo hicho katika Jengo la Biashara Complex lililoko Mwananyamala Juni 3, 2012 alipoitwa kwenda kuchua ada kwa mara ya pili. 

Akizungumza kwa uchungu, alisema mbunge huyo alifanya kitendo hicho kwenye Hoteli ya Giraffe, Jijini Dar es Salaam mwaka 2011.

Alisema kuwa yeye alikuwa na urafiki na mwanafunzi mwenzake Zuhura Mwaking’inda. Mwaking’inda amewahi kuwa Diwani wa Kata ya Sinza Jimbo la Ubungo, Jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa mwanafunzi huyo, rafiki yake (mtoto wa Mwaking’ida) alikuwa amepooza hivyo alikuwa analazimika kumhudumia hali iliyowaunganisha hadi huyo mtoto alipochukua jukumu la kumtambulisha kwa baba yake ambaye naye alimtambulisha kwa Kapuya ili aweze kumsaidia fedha kwa jili ada.

Mwanafunzi huyo alisema baada ya kutambulishwa aliitwa katika hoteli moja jijini Dar ambapo baada ya kufika mapokezi wafanyakazi wa  hoteli hiyo walimkataza kuingia chumbani katika maana kwamba umri wake alikuwa mdogo (mwaka 2011 alikuwa na miaka 14), lakini Kapuya aliamrisha aje chumbani pamoja na dereva na kumwingiza kwa nguvu.

Akiwa chumbani alimlazimisha kulala naye kisha kumpa sh laki saba, badala ya sh elfu sitini na saba kiasi ambacho kilikuwa ndio mahitaji halisi ya ada.

Mwanafunzi huyo amesema baada ya muhula mmoja aliitwa tena na mbunge huyo katika Jengo la Biashara Complex lililoko Mwananyamala tarehe 3 June 2012, ambapo pia alimlazimisha kulala naye kwenye zulia la ofisi yake, kisha kumpa sh 350,000/.

Alisimulia kwamba wakati anatoka kwa huzuni ofisini kwa mbunge huyo, mmoja wa wahudumu wa hapo alimuuliza kwanini anatoka kwa huzuni, alimweleza kisa hicho, na huyo mama aliangua kilio kwa kumwambia “mwanangu umekufa pole tu, huyu baba ni muathirika wa ukimwi”.

Aliongeza kuwa baada ya kuambiwa vile alilia na kufanya fujo hapo mapokezi hadi alipokamatwa na walinzi wa kisha kupelekwa kituo cha polisi kufunguliwa mashtaka, lakini akiwa polisi alipoeleza mkasa wote, Polisi walilazimika kumwita Kapuya na wakawasuluhisha kwa makubaliano kwamba Kapuya atakuwa anamlipia ada, na kumpa pesa za matumizi sh. laki tatu kila mwezi, jambo ambalo amekuwa akilitekeleza kupitia simu yake ya mkononi 0755993930.

Kwa mujibu wa mwanafunzi huyo, 24 Januari 2013, alifika mtu nyumbani kwao mtu mmoja (jina tunalihifadhi) na kujitambulisha kuwa yeye ni jambazi na kuwa alitumwa kwenda kuwaua kwa malipo ya sh. milioni 50, lakini alipokuta ni watoto wadogo aliwasamehe, na kusema yeye ni jambazi sugu hawezi kupoteza nguvu zake kuua vitoto.

Alienda akiwa na bastola, maji kwenye chupa yanayodhaniwa kuwa ni tindikali na bomba la sindano. Kwa mujibu wa mtoto huyo, jambazi huyo anasema kuwa tayari alilipwa milioni 15 za awali.

Mtoto huyo alisema jambazi huyo aliwambia kuwa yeye ni rafiki wa mtoto wa Kapuya na wanamfahamu vizuri, lakini hataweza kuaua baada ya kubaini kuwa wao ni yatima tu.

Hata hivyo kufikia mwezi Februari mwaka huu, mtu asiyefahamika alienda nyumbani na kutelekeza gari aina ya T.199 BGY Mercedes Benzi ya Blue wakati wanafunzi hao wakiwa shuleni, kisha kuacha ufunguo kwa jirani yao kwa maelekezo kuwa wakifika awapatie.

Na Kapuya aliwapigia simu kuwaarifu kuwa amempa zawadi ya gari kwa ajili ya matumizi ila yeye na dada yake wanaruhusiwa kuuza ili wapate pesa kwa ajili ya mahitaji yake siku zilizosalia, kwani muda sio mrefu baada ya uchaguzi mkuu 2015, Kapuya atakuwa Waziri Mkuu, hivyo itakuwa ngumu yeye kumtumia huyo binti pesa kama alivyoelekezwa na jeshi la polisi kituo cha Oysterbay.

Baada ya mwanafunzi huyo na dada yake ambaye ana umri wa miaka 20, kupewa gari walishindwa kulitumia hivyo kutoa taarifa polisi kwani kwa kupokea gari hilo  ilikuwa ni kuwatelekeza kwani yeye hana hata hela ya kuweka mafuta ya gari, hivyo walienda polisi ili kesi ipelekwe mahakamani kumshtaki kapuya.

Polisi wa Oysterbay walikubali kulipeleka tatizo hilo kwa Katibu wa Bunge, ambaye alimwita mwanafunzi huyo na mdogo wake waende Dodoma kukutana na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ingawa walipofika Dodoma walikaa na kamati ya hiyo kwa maelezo kuwa Kapuya hakuwepo hadi Bunge lilipoisha walirejeshwa Dar es Salaam.

Mtoto huyo na dada yake alitoka ofisi za CCM lakini akiwa anaelekea kituo cha basi alithadharishwa na mwanafunzi mwingine kwa haraka kuwa akimbie kwa kuwa atamwagiwa tindikali na watu waliokuwa wanamfuata nyuma, alikimbilia katika mtaa wa Hoteli ya Star light kisha aliomba msaada baada ya kupotea njia na hivyo alisaidiwa na mama mmoja kufikishwa chumba cha habari cha Channel Ten.

Ni katika chumba hicho ndio mwandishi wa habari hizi alienda na kuwakuta watu wawili hao waliokuwa wanamhitaji binti huyo lakini walikatazwa kumchukua.





0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.