22 Aug 2014

Ijumaa ya leo imekuwa siku ngumu sana kwangu. Rafiki yangu mmoja wa karibu, mhamiaji kutoka Ireland ya Kaskazini aliyehamia hapa Uskochi, anajiandaa kwa ajili ya upasuaji wa moyo hapo Jumatatu. Leo tumeonana 'kwa mara ya mwisho' kwa vile atatumia wikiendi hii kujaindaa na upasuaji huo, na wiki Ijayo ndo shughuli yenyewe.

Nimepata wakati mgumu sana kuagana nae jioni hii wakati anaelekea nyumbani kwake nami narudi kwangu. Japo aliniaga kwa kujiamini kuwa tutaonana Jummatano ijayo, lakini hali ya uoga iligubika ujasiri wake, na kwa hakika almanusra niangushe chozi. 

Huyu bwana alipatwa na mshtuko wa moyo miezi kadhaa iliyopita. Naikumbuka vema siku hiyo. Tulipokutana asubuhi baada ya kuwasili kazini alionekana anatoka jasho japo siku hiyo ilikuwa ya baridi kali. Muda mfupi baadae alionekana anapumua kama mtu aliyekimbia umbali mrefu, na muda mfupi baadaye akaanguka na kupoteza fahamu. Tuliita gari ya kuhumia wagonjwa, na akakimbizwa hospitalini haraka. Kwa mujibu wa maelezo yake mwenyewe, alikuwa kama amekufa kwa masaa kadhaa. Lakini kubwa lililosaidia kuokoa uhai wake ni huduma ya kwanza tuliyompatia wakati tunasubiri gari la wagonjwa, vinginevyo moyo wake ungezimika moja kwa moja.

Alikaa hospitalini kwa wiki kadhaa na huko walimwekea mashine inayousaidia moyo wake kufanya kazi zake kwa ufanisi. 

Sasa upasuaji atakaofanyiwa Jumatatu ijayo ni kwa ajili ya uchunguzi mkubwa wa jinsi mashine hiyo inavyofanya kazi.Ikumbukwe kuwa mashine hiyo inafanya kazi kuusaidia moyo, na kwahiyo moyo wake bado unafanya kazi japo ni kwa msaada wa mashine hiyo iliyowekwa juu kidogo ya moyo wake, kifuani.

Kitakachofanyika Jumatatu ni kilekile walichomfanyia wakati wanaweka mashine hiyo, yaani watatumia kompyuta kufanya kazi ya moyo, na kisha kuusimamisha moyo, na kwa wakati huo uhai wake utakuwa unategemea kompyuta hiyo. Wataitoa mashine waliomwekea mwilini na kuisafisha, sambamba na kuichunguza. Kadhalika, moyo wake nao utafanyiwa uchunguzi wa kina. Yote hayo yatatokea wakati uhai wake unategemea kompyuta inayofanya kazi ya moyo.

Japo upasuaji huo haumaanishi kifo lakini kuna uwezekano-japo si mkubwa- wa moyo kurejeshwa mwilini na ukagoma kufanya kazi kama awali. Kadhalika, ile mashine inayousaidia moyo nayo inaweza kugoma 'kuwajibika ipasavyo.' Lakini cha kutisha ni ukweli kwamba wakati upasuaji huo unafanyika, rafiki yangu huyo atakuwa kama amekufa- kwa maana ya kazi zinazofanywa na moyo wa asili kutegemea msaada wa kitu cha nje- in this case ni hiyo kompyuta. Yaani kwa lugha nyingine ni kama mtu anayepumulia mashine, ikizimwa, yaweza kuwa ndio mwisho wa uhai wake.

Wakati tunaondoka eneo la kazi, rafiki yangu huyo alisema waziwazi kuwa muda huo ndo unaweza kuwa wa mwisho kwa yeye kuwepo hapo. Japo aliongea kwa utani lakini uwezekano huo upo japo si mkubwa. Teknolojia ya matibabu ya moyo imepiga hatua kubwa sana lakini si ya uhakika wa asilimia 100.

Kwangu, nabaki kumfanyia sala, upasuaji huo ufanyie salama, na tukutane tena Jumatano kama alivyoahidi mwenyewe. Nina imani na teknolojia ya matibabu ya hawa wenzetu lakini ukweli kwamba kiungo muhimu kama moyo kitasimamishwa na kazi yake kufanywa na kompyuta inanipa msisimko wa uoga. Na hilo limeonekana hata kwa 'mgonjwa' mweyewe.'

I thought si vibaya ku-share stori hii ya kuogofya ambayo inanigusa kwa kiasi kikubwa. Kwa nman flani yanikumbusha jinsi nilivyompoteza mama yangu mpendwa, ambaye nae kama ilivyo huyo rafiki yangu alipatwa na mshtuko wa moyo, akapoteza fahamu, na fahamu hazikumrejea tena hadi anafariki Mei 29, 2008.

Natumaini msomaji mpendwa utaungana nami kumwombea rafiki yangu huyo upasuaji atakaofanyiwa uwe wa mafanikio na aendelee kuishi salama. Nitawafahamisha kilichojiri Jumatano ijayo.

Asanteni

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.