12 Sept 2014

Nimekutana na makala hii katika gazeti la Mwananchi toleo la Jumanne Septemba 9, 2014 na nimeona ni-share nanyi
Betty Ndejembi ni msichana mrembo na mwanamitindo ambaye anatumia sana huduma za mitandao ya kijamii kwa ajili ya shughuli zake mbalimbali za kujiingizia kipato na kujitangaza zaidi. 

Siku moja alibakwa mpaka akapoteza fahamu, akaokotwa na watu akapelekwa hospitali. Alipofika hospitali aliendelea kutumia mitandao ya kijamii, kwa ajili ya kufahamisha wenzake anavyoendelea kwa nia nzuri kabisa. 

Jinsi alivyokuwa anafahamisha umma kuhusu maendeleo yake, baadhi yao walitumia fursa hiyo kumtukana, kumnyanyapaa, kutumiana picha zake na dhihaka nyingine nyingi kwa njia ya mitandao hiyo hiyo. 

Betty alifariki dunia baadaye wakati anaendelea na matibabu, lakini matusi aliyovurumishiwa, maneno aliyoambiwa na unyanyasaji mwingine, umeleta historia mpya katika matumizi salama ya mitandao ya mawasiliano. 

Jijini Arusha kijana mmoja alikutwa na mke wa mtu, akadhalilishwa huku akipigwa picha. Zile picha zikawekwa kwenye mitandao kadhaa ya kijamii, baada ya siku chache yule kijana alionekana amejinyonga chini ya daraja. 

Huko Marekani dada mmoja anayeitwa Rebecca Ann Sedwick aliamua kujitoa uhai baada ya kudhalilishwa kupitia mtandao wa kijamii. 

Kitendo alichofanyiwa Betty, kijana wa Arusha na huyo mwanadada wa Kiingereza, kinaitwa kitaalamu kwa jina la cyberbulling, yaani mtu kutumia njia za mawasiliano kwa nia ya kuumiza, kudanganya au kumdhalilisha mwingine. 

Vitendo hivi ni kama kutumia picha ambayo mwenyewe hajaruhusu, kuandika habari za uongo hasa za udaku, kuandika au kutoa maoni ambayo si ya kweli kwa nia ya kudhalilisha au kuumiza, kudanganya kuhusu bidhaa au huduma fulani kwa nia hiyo hiyo.
Mimi binafsi niliwahi kukumbana na sakata kama hili, lakini lilimkuta rafiki wa rafiki yangu mmoja. Yeye alikuwa na mpenzi wake, kumbe wakiwa kwenye starehe yule mwanaume alikuwa na tabia za kumpiga picha. 

Siku ikafika hawakuelewana ikabidi kila mtu aendelee na maisha yake, yule kijana akaingia katika mtandao wa kijamii wa facebook akatengeneza jina bandia akaweka picha za yule binti na kuwarushia watu wa karibu wa binti halafu akafuta lile jina. 

Binti alienda kituo cha polisi kutoa taarifa, polisi wakaomba ushahidi wa picha, lakini ndiyo hivyo jamaa alikuwa ameshafuta mpaka jina, kwa hiyo wakaomba msaada, nikawapeleka polisi makao makuu kitengo cha uhalifu wa mtandao. 
Polisi waliweza kupata taarifa zote zinazohusu yule kijana kwenye mitandao ya kijamii na wakaenda kumkamata alipokuwa anaishi wakakagua simu zake, kompyuta na nyaraka nyingine wakapata picha zote kama ushahidi na sasa hivi huyu kijana yuko jela. 

Huko mitaani kuna kina Betty wengi wamezushiwa, wamedhalilishwa, wamepakaziwa na kutengenezewa habari nyingi mbaya na za kuumizwa na watu wanaowajua au kutowajua, lakini wanakaa kimya. Madhara yake ni makubwa. 
Ieleweke kuwa kukaa kwao kimya hakumaanishi kitendo hiki kinakubalika. La hasha hili ni kosa kubwa la jinai ambalo hapa nchini linaanza kuota mizizi. Watu wanatumia mitandao ndivyo sivyo. 
Unachotakiwa kujua ni kwamba mawasiliano yote kuanzia simu na mitandao ya kijamii, hata kama mtu alifuta, kampuni inayotoa huduma husika huwa ina sehemu yake ya kuhifadhi mawasiliano yote. 
Tushirikiane pamoja ili kuweza kumaliza au kupunguza tatizo hili la unyanyasaji, kwa kutumia vyombo vya mawasiliano ili tuweze kuwa na jamii iliyostaarabika.
CHANZO: Mwananchi 


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.