29 Apr 2007

KULIKONI UGHAIBUNI-59

Asalam aleykum,

Majuzi nimesoma habari flani kwenye gazeti la Daily Mail la hapa Uingereza kuhusu harakati za mwanamuziki wa kimataifa Madonna ambaye tayari amesha “adopt” mtoto mmoja huko Malawi.Inaweza kuwa habari njema kwa mtoto huyo kupata bahati ya kuingizwa kwenye familia ya mwanamuziki huyo maarufu na tajiri kabisa duniani.Nadhani hakuna mmoja wetu sie tulio hohehahe ambaye asingependa kuzaliwa kwenye familia ya vibopa,au kubahatika kurithiwa na familia tajiri.Kwa mtoto huyo wa Kimalawi hiyo ni sawa na bahati ya mtende kuota Jangwani.

Hata hivyo,kuna taarifa ambazo sio za kufurahisha kuhusiana na suala zima la Madonna kurithi watoto huko Malawi.Mwanamuziki huyo ni mfuasi wa dhehebu jipya la Kabbalah.Na kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana,amekuwa akitumia “upendo” wake kwa watoto wa Malawi kueneneza dini hiyo ambayo kwa kiasi flani imegubikwa na utata.Mwanamuziki huyo anamiliki vituo kadhaa vya kulelea yatima nchini humo,na inaelezwa kuwa vinaendeshwa kwa pamoja na wafuasi wengine wa madhehebu hayo ya Kabballah.Wapo wanaoona kuwa dhamira nzuri ya Madonna kuwasaidia watoto hao inapotezwa na hiyo ajenda yake ya siri ya “umisionari” wa Kabbalah.Kwa wengine,hiyo ni sawa na kumbukumbu za ukoloni ambapo wamisionari walitumia misaada yao kubadili imani za asili za watu.Ni sawa na kutoa msaada wenye masharti magumu,hasa ikizingatiwa kuwa Madonna na wana-Kabbalah wenzie wanatumia umaskini na uyatima wa watoto wa Malawi kuwaingiza kwenye madhehebu ambayo pengine wangekuwa na uwezo wasingetaka kujiunga nayo.

Tukiachana na Madonna,tuangalie mambo yalivyo huko nyumbani.Moja ya mambo ambayo yamenigusa sana wiki hii ni taarifa nilizosoma kwenye gazeti moja la kila siku la huko Bongo kuwa hivi majuzi kuwa Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu imewaachia mtuhumiwa mmoja aliyekuwa akikabiliwa na kesi ya mauaji na mwingine aliyekuwa akikabiliwa na mashtaka ya madawa ya kulevya yenye thamani ya shilingi milioni 250.Uamuzi huo wa mahakama umetokana na maelezo ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ambaye aliamua kuachana na kesi hiyo kwa kutumia kipengele cha kisheria kiitwacho “nolle prosequi” (yaani mtuhumiwa hana kesi ya kujibu) lakini bila DPP kutoa sababu zozote.

Habari hii imenishtua kwa vile kwa mtizamo wangu nadhani DDP anawajibika kwa umma wa Watanzania.Yaani kwa lugha nyepesi,yeye ndiye mwakilishi wa Jamhuri kwenye mashtaka ambayo kwa namna moja au nyingine yanawaweka wananchi wa kawaida upande mmoja na watuhumiwa upande mwingine.Sasa anapoamua kutumia nguvu zake kisheria kufuta kesi bila kutoa maelezo anataka kutueleza nini?Hapa UK kuna mamlaka iitwayo Crown Prosecution Service (CPS) ambayo kwa namna flani ni kama ofisi ya DPP huko nyumbani.Ni kweli kuwa mamlaka hiyo imekuwa ikifuta baadhi ya kesi,lakini nyingi ya kesi hizo ni zile ambazo huhitaji hata kozi fupi ya sheria kutambua kuwa mtuhumiwa hana hatia ,na umma huwa unajulishwa kwanini CPS imeamua kufuta kesi husika.

Pengine tofauti ninayoiona kati ya CPS ya hapa na DPP wa huko Bongo ni kwamba hapa CPS inatoa maamuzi ya kitaasisi zaidi wakati kwa huko nyumbani maamuzi ya DPP yanaonekana kama ya mtu binafsi anayewakilisha taasisi.Kuna tofauti kubwa hapo.Lakini bila kujali tofauti hizo,nashawishika kuhofu kuwa DPP anaweza kuamua kumwachia mtuhumiwa kwa utashi wake binafsi,hasa ikizingatiwa kuwa hawajibiki kuelezea kwanini ameamua hivyo.Ikumbukwe kuwa kwenye kesi ya Dito,kauli za DPP (kama mtu binafsi) zilileta hisia kuwa Mheshimiwa huyo anatumia u-Mungu mtu wake kisheria kuendesha mambo anavyjiskia yeye.Hiyo ni hatari kwenye nchi inayoendeshwa kwa kufuata utawala wa sheria.

Pasipo kutaka kuingilia utendaji kazi wa DPP,nadhani kuna umuhimu wa kuwepo mamlaka ambayo inaweza kumbana DPP katika maamuzi yake hasa hayo ya kuwaachia watuhumiwa bila kutoa sababu.Kwa nchi ambayo “wenye nazo” wanaweza kupindisha sheria,yayumkinika kuamini kuwa baadhi ya kesi ambazo DPP anazitupilia mbali zinapata “bahati” hiyo baada ya “kuwepo namna flani.”Kuwa na nguvu kubwa kisheria ni suala zuri lakini iwapo nguvu hizo zikitumika vibaya basi hapo inakuwa balaa.Nadhani ni vema kukawekwa utaratibu utakaouhakikishia umma kuwa pindi DPP akiamua kufuta kesi kwa madai kuwa “mtuhumiwa hana kesi ya kujibu” basi ALAZIMIKE kuujulisha umma sababu zilizomfanya afikie uamuzi huo.

Jingine ambalo nilishalizungumzia huko nyuma ni ubabaishaji wa viongozi wa klabu ya Simba.Na kama nilivyotabiri,hatimaye Mbrazili waliyemleta kwa mbwembwe kibao ameamua kuwaacha kwenye mataa.Nakubaliana na kauli ya Katibu Mkuu wa TFF kuwa viongozi wa timu hiyo wanapaswa kuwa makini wanapokimbilia kuchukua makocha kutoka nje ya nchi bila kuzingatia suala la mikataba.Laiti viongozi hao wangekuwa wamewekeana mkataba wa kueleweka na kocha huyo ni dhahiri kuwa asingeamua kuondoka bila kuwaaga kwa vile anafahamu kuwa sheria ingekuwa dhidi yake.Niliposikia viongozi hao wakijigamba kuwa licha ya kelele walizokuwa wakipigiwa wameweza kumleta kocha kutoka Brazil,nilipata hisia kuwa wamekurupuka kufanya hivyo ili kuua tuhuma kadhaa zilizokuwa zikiwakabili.Na kweli “triki” hiyo ilifanya kazi kwani mizuka ya wapenzi wa klabu hiyo ilitulia na wakaungana na viongozi hao wababaishaji kumpatia kocha huyo mapokezi makubwa na ya kihistoria.

Muda mfupi kabla sijamaliza kuandaa makala hii nimesoma kwenye gazeti moja mtandaoni kuwa viongozi hao wa Simba wanataka kuleta kocha kutoka Ureno.Hivi kwanini wana-Simba wanafanywa wajinga kiasi hicho?Kabla uongozi haujaweka bayana kilichomkimbiza kocha Mbrazil,wanakimbilia kuleta habari za kocha mwingine kutoka ng’ambo!Huo ni ubabaishaji wa daraja la kwanza.Nilishasema kuwa ni vigumu sana kwa vilabu vyetu kudumu na makocha wenye upeo hasa wa kutoka nje ya nchi kwani mfumo wa soka katika ngazi ya vilabu umetawaliwa sana na ubabaishaji.Viongozi wa Simba wanaweza kuwabeza “Friends of Simba” lakini wanasahau kuwa “wamekalia makuti makavu” kwa vile hawana mbinu za kuiingizia mapato klabu hiyo kongwe bila kutegemea hisani za wafadhili.Vyanzo vya mapato vipo waziwazi lakini kwa vile viongozi hao wametawaliwa na fikra finyu ambazo kwa kiasi kikubwa zinaelemea kwenye maslahi yao binafsi badala ya maendeleo ya klabu,wanajikuta wakiitisha “press conferences” moja baada ya nyingine kutoa “mipango hewa” ya maendeleo kama zile ndoto za alinacha za kujenga uwanja wa kisasa.Wito wangu kwa wana-Msimbazi ni kuachana na wababaishaji hao mapema kadri iwezekanavyo,la sivyo mambo yatakuwa mabaya zaidi ya yalivyo sasa.

Mwisho ni uchungu wangu mkubwa baada ya kuona wenzetu Wakenya wakitesa kwenye London Marathon huku sie wabongo tukiwa hatuna mwakilishi.Hivi kizazi za akina Ikangaa,Bayi,Shahanga,Nyambui na wengineo kimepotelea wapi.Hivi kweli tunahitaji wawekezaji hata kwenye “kufukuza upepo”?Jiografia ya mkoa kama Kilimanjaro inatoa upendeleo mkubwa kwa Watanzania kuzalisha wanariadha wa kiwango cha kimataifa.Riadha iliwahi kutupa jina kubwa huko nyuma lakini sijui tatizo liko wapi.Wakongwe wa riadha walioingia kwenye uongozi wa vyama vya riadha na kamati ya Olimpiki wanaelekea wameridhika na mafanikio waliyoyapata wao miaka ya nyuma na hawajali kama kutawekwa historia nyingine.Ni wivu wa kutaka rekodi zao zisifikiwe na wanariadha wa sasa,uzembe na kutojua kazi yao, au ndio yaleyale ya kuthamini zaidi matumbo yao kuliko maslahi ya Taifa?

Alamsiki

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.