22 Oct 2008


Viongozi wa dini waonya nchi inaelekaa pabaya
*Washauri Rais apunguze safari za nje

Na Waandishi Wetu

VIONGOZI wa dini wamesema kukithiri kwa migomo, maandamano, vitendo vya kikatili, na migogoro kati ya serikali na watumishi wa umma ni ishara tosha kwamba, mambo hayako sawa nchini.

Wakizungumza na Mwananchi nyakati tofauti jana, viongozi hao walisema hali hiyo inaipeleka nchi pabaya na kuitaka serikali kutafuta suluhisho la matatizo hayo haraka iwezekanavyo.

Walisema kuwa kinachotokea sasa ni matokeo ya ahadi zisizotekelezeka na kwamba njia pekee ni kuyashughulikia madai hayo ya wananchi.

Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Kanisa la Katoliki jijini Dar es Salaam, Mhashamu Methodius Kilaini alisema, iwapo hali hiyo haitashughulikiwa mapema itasababisha hali kuwa mbaya zaidi nchini.

Kauli hiyo imeungwa mkono na Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ramadhan Sanze aliyesema kuwa, ili kuondoa mitafaruku iliyopo nchini serikali lazima iwe tayari kuwajibika kwa jamii kisheria, kisiasa.

Aliishauri serikali kuyashirikisha makundi mbalimbali ya kijamii na kisiasa katika kupanga na kubuni sera mbalimbali kiutawala na maendeleo ya nchi kwa ujumla.

Sanze alimwomba Rais Jakaya Kikwete kupunguza safari za nje na hasa Marekani, akidai kuwa nchi hiyo si marafiki wazuri kwa ustawi wa taifa la Tanzania.

“Sidhani kama rais safari hizi za Marekani anapanga mwenyewe au anapangiwa, kama anapangiwa basi itifaki hii sio nzuri, hivyo tunamwomba apunguze safari za huko,” alisema Sheikh Sanze.

Alifafanua kuwa, ni vema kwa sasa rais akabakia nchini kuwatumikia Watanzania na kutuliza mitafaruku iliyopo badala ya kusafiri safiri tu huku nchi ikiwa inateketea kwa kuzongwa na migogoro ya kijamii.

Sheikh Sanze alionya kuwa, ikiwa hali itaendelea kama ilivyo sasa bila hatua madhubuti kuchukuliwa, basi kwa mara ya kwanza historia inaweza kubadilika kwa kuwa na rais wa kipindi kimoja.

Awali, Askofu Kilaini alisema ingawa tatizo la migomo linaonekana kuwa ni la miaka mingi, lakini ishara ya sasa inatia mashaka kwani serikali imekuwa ikitoa ahadi nyingi kwa wananchi na mambo machache tu ndiyo yanatekelezwa

“Hatuwezi tukasema kuwa mambo haya yanayoendelea kujiri ni ishara ya kukua kwa demokrasia, bali inatubidi tufahamu kuwa, serikali isipotekeleza ahadi zake kwa wananchi tutaendelea kushuhudia vitendo hivi kila mara.

Alisema uchumi wa dunia unapotikiswa, nchi zinazoendela ndizo zinazoathirika zaidi, hivyo ni vema serikali kupitia wizara zake ikatafuta mbinu zaidi za kuhakikisha kuwa suala la mfumuko wa bei unadhibitiwa ili mwananchi wa kawaida aweze kumudu maisha.

Alisema watu wanapochoka, na kukata tamaa na serikali yao, hutafuta njia nyingine kujinasua na matatizo yanayowakabili.

“ Ukizingatia kuwa suala la maandamano au migomo ni haki za msingi za wafanyakazi, hivyo kama serikali inataka kupunguza masuala haya ni vema ikabeba gharama na siyo kukwepa,” alisema Askofu Kilaini na kuongeza:

“Ninawaomba wananchi wenzangu watafute madai yao kwa kufanya mazungumzo na si kushiriki kwenye vurugu na migomo na pia serikali inapaswa kuwajibika kwa ahadi zake na si kuwayumbisha Watanzania.”

Hata hivyo, Askofu Kilaini alipoulizwa kwamba alishawahi kutamka kuwa Rais Jakaya Kikwete ni chaguo la Mungu na hivi sasa ana maoni gani, alisema kuwa kiongozi yeyote anayechaguliwa kwa ridhaa ya wananchi ni chaguo la Mungu.

“Ni vema nikaeleweka kuwa maandiko ya Mungu yanasema uongozi na mamlaka yote hutoka kwa Mungu, hivyo basi rais aliyechaguliwa kwa ridhaa ya wananchi wenyewe ndilo chaguo la Mungu na sisi tutaendelea kuwa na msimamo huo,” alisema Askofu Kilaini.

Alisema pamoja na kwamba Rais Kikwete ni chaguo la Mungu, anahitaji kusaidiwa katika kutekeleza sera na kutimiza ahadi zote zilizoahidiwa katika serikali yake, kwa sababu viongozi wengine wakimwachia na kushughulikia zaidi maisha yao binafsi, hakuna jambo litakalotekelezeka.

Aliwataka mawaziri na watendaji wengine serikalini wakawa mstari wa mbele kumshauri Rais mambo mema na si kumpotosha ili aweze kutekeleza.

Naye Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Salum Fereji na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT), Padri Charles Kitima walisema jana kwenye semina ya waandishi wa habari toka mikoa mbalimbali nchini inaendelea katika Hoteli ya Isamo mkoani hapa kuwa sera na sheria na madini vimetungwa kwa masilahi ya watu wachache walafi ambao wanajali masilahi yao na hivyo lazima vibadilishwe sambamba na mikataba yote ambayo makampuni ya wawekezaji yameingia katika uchimbaji wa madini hapa nchini.

Sheikh Ferej alisema ni lazima serikali kuamka kwa kuwa sasa nchi inaelekea pabaya kutokana na rasilimali muhimu kama madini kuachiwa watu toka nje ya nchi kuwaacha Watanzania kuendelea kuisha katika umaskini uliotopea.

"Ndugu zangu, sisi kama viongozi wa dini tulitembelea maeneo ya migodi yote, kule hali ni mbaya Watanzania wanaishi maisha ya dhiki, wamefukuzwa katika maeneo yao na watu toka nje ya nchi ndio wananufaika na madini haya kwa kupeleka kwao," alisema Sheikh Fereji.

Alisema wao kama viongozi wa dini wamebaini serikali imefanya makosa katika kuingia mikataba na wawekezaji toka nje ya nchi kwa sababu Watanzania hawanufaiki na madini hayo ambayo miaka michache ijayo yatakuwa yamekwisha na kuacha mashimo.

Naye Padri Kitima alisema bila serikali kufanyika marekebisho sheria na sera za madini Tanzania itaendelea kuwa maskini na siku zijazo yanaweza kukatokea mapigano kama ilivyo katika nchi nyingine barani Afrika ambapo kulikuwa na madini.

Alisema mikataba mingi ya wawekezaji ni mibaya na inatakiwa irekebishwe, lakini inavyoonekana hakuna wa kubadilisha hadi vyombo vya habari na wananchi washikamane na kudai mikataba hiyo ivunjwe au kurekebishwa.

Padri Kitima alisema katika mazingira ya sasa angependa yafanyike mabadiliko makubwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake kabla ya mwaka 2010 na kuwa na kundi la wafuasi wa Nyerere ambao watatetea rasilimali za nchi hii.

"Mimi binafsi kwa hali ilivyo ningependa CCM igawanyike najua kuna watu wazuri ndani ya CCM, lakini wanashindwa kuifanya nchi hii kuwa mikononi mwa Watanzania badala yake kundi la watu wabinafsi ndilo lina nguvu na hata katika kambi ya upinzani kuna matatizo makubwa ya ubinafsi na kuwepo viongozi wasio na sifa," alisema Padri Kitima.

Alisema nchi imepoteza agenda muhimu alizoziacha hayati Mwalimu Julius Nyerere alipounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sasa ubinafsi umetawala hadi kutishia kuvunja Muungano.

CHANZO: Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.