22 Oct 2008

Daniel Mjema na Ally Sonda
Siku saba zikiwa zimebaki kabla ya kile kinachoelezwa kuwa ni kiama cha mafisadi kutimia, mwananchi mmoja mkazi wa Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, jana alichomoza na kumuhoji Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuhusu ukimya wa serikali katika kuwashughulikia watuhumiwa wa ufisadi.

Hali hiyo ilijitokeza jana nje ya jengo la ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Rombo wakati waziri mkuu aliposimama kwa muda kuwasalimia wananchi waliokuwa wamefurika nje ya ofisi hizo kwa lengo la kumuona.

Wakati waziri mkuu aliporuhusu maswali machache ndipo mwananchi mmoja alipomhoji Waziri Pinda akimuuliza kwa nini wanawaacha bila kuwashughulikia mafisadi hadi Bunge lilipoamua kuchukua jukumu hilo.

Mwananchi huyo, ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja, alitaka serikali itunge sheria kali ya kuwashughulikia mafisadi.

Mbali na kumhoji Waziri Mkuu kuhusu ukimya huo wa serikali katika kuwashughulikia mafisadi, pia alitaka uteuzi wa Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) na makanda wa mikoa, uthibitishwe na Bunge.

Alisema kuwa hiyo itakuwa rahisi kwa chombo hicho cha wawakilishi wa wananchi kuweza kuwawajibisha viongozi watakaothibitika kujihusisha na vitendo vya ufisadi.

Akijibu swali hilo na mengine, Waziri Pinda alisema suala la ufisadi linapaswa kupigwa vita kuanzia ngazi ya familia kwa sababu viongozi wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu wanatoka katika familia.

Waziri Mkuu alisema hali sasa imebadilika na kwamba suala la kuwachukulia hatua mafisadi lazima lifuate taratibu na sheria za nchi, ikiwamo kuheshimu haki za binadamu na utawala wa sheria.

Suala la kutochukuliwa hatua kwa mafisadi limekuwa mdomoni mwa watu wengi baada ya Rais Jakaya Kikwete kulieleza Bunge la Muungano kuwa watu waliochota Sh133 bilioni kutoka kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) warejeshe fedha hizo ifikapo Oktoba 31, la sivyo wafikishwe mahakamani Novemba mosi.

Kauli hiyo ilionekana kama kuwapa ahueni mafisadi hao kuwa iwapo watarejesha fedha hizo ambazo zilichotwa kati ya mwaka 2005/06, hawatachukuliwa hatua zozote.

Kauli hiyo ilifanya watu kuwa na maoni tofauti, wengi wakihoji sababu za serikali kuwapa ahueni watu waliochota mamilioni ya fedha na wengine wakitaka wezi hao watajwe majina yao, lakini serikali imekuwa ikisema kuwa imeshachukua hatua, ikiwa ni pamoja na kuzuia akaunti zao na kushikilia mali zao.

Hadi sasa serikali inadai kuwa mafisadi hao wamesharejesha kiasi cha Sh61 bilioni, lakini haijataja waliokwisha rejesha fedha hizo wala wale ambao hawajarejesha, ikisema kuwa kufanya hivyo kutaharibu mikakati yao.

Akianza ziara yake mkoani Mbeya, Rais Jakaya Kikwete alikumbana na umati wa watu waliozuia msafara wake maeneo ya Mwanjelwa na wengi wakipiga kelele kutaja neno mafisadi, huku wakihoji maisha bora na ajira.

Mapema wiki hii, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kilisema kuwa kitaifungulia serikali mashtaka ya kuwalinda mafisadi iwapo haitawafikisha mahakamani wale wote wanaohusika na tuhuma za uchotaji wa mabilioni hayo ya fedha.

Kashfa ya wizi wa fedha hizo ilibainika wakati kampuni ya Ernst and Young ilipopewa kazi ya kukagua mahesabu ya Benki Kuu (BoT) ya kipindi cha mwaka 2005/06. Kampuni hiyo iligundua kuwepo na malipo ya kasi ya mamilioni ya fedha kwa wafanyabiashara wa ndani katika kipindi hicho na hivyo kutoa ripoti iliyofichua wizi huo.

Fedha hizo, zilizohamishiwa kwenye akaunti hiyo maalum BoT kutoka NBC, ni zile zilizokuwa zikilipwa na wafanyabiashara wa ndani ambao walinunua bidhaa kutoka makampuni ya nje kwa dhamana ya serikali, ambayo ilikuwa inakabiliwa na uhaba mkubwa wa fedha za kigeni.

Akijibu swali la upungufu wa mbolea ya ruzuku, Waziri Pinda alikiri kwamba mbolea hiyo haitoshelezi mahitaji, hivyo akawashauri wakulima wajiunge na vyama vya akiba na mikopo ili waweze kupata mikopo.

Baadaye waziri mkuu alizindua awamu ya tatu ya mradi wa maji unaosimamiwa na kampuni ya Kiliwater ambao baada ya kukamilika utagharimu zaidi ya Sh10 bilioni.

Aliwataka wananchi kuutunza mradi huo dhidi ya hujuma zozote huku akiiagiza Bodi ya Wakurugenzi kuhakikisha wanaifanyia matengenezo ya mara kwa mara miundo mbinu yake ili iwe endelevu.

Katika ziara hiyo ya siku tano mkoani Kilimanjaro, waziri mkuu anafuatana na viongozi mbalimbali wa serikali, akiwemo Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, Dk. Cyrill Chami.

Wengine ni mkewe, Tunu Pinda, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mohamed Babu na Mwenyekiti wa CCM mkoani Kilimanjaro, Vicky Nsilo Swai na watendaji wengine wa serikali na mashirika ya umma.

Wakati huohuo, ziara ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambayo leo inaingia Siku ya tatu mkoani Kilimanjaro, imegeuka msumari wa moto kwa vijana wa mji wa Moshi ambao wengi wao wanashikiliwa na polisi baada ya msako mkali uliofanywa jana.

Taarifa zilizoifikia Mwananchi jana, zimedai kuwa vijana wengi waliokamatwa ni wafanyabiashara ndogondogo (machinga) kwenye maeneo ya sokoni, Mtaa wa Kiusa ambako Waziri Pinda amepangiwa kuhutubia wananchi leo jioni.

Haikufahamika haraka kiini cha polisi kuendesha operesheni hiyo kali ambayo imesababisha vijana wengi kushindwa kumuona Waziri Pinda jana, lakini taarifa zisizo rasmi zimedai kuwa huenda vyombo vya ulinzi na usalama vina hofu na yale yaliyomkumba Rais Jakaya Kikwete mkoani Mbeya.

"Hivi sasa watu waliokata tamaa ni wengi…….hii kamatakamata inayofanywa na polisi leo (jana) ni kuweka mambo sawa ujio wa Waziri Mkuu, Pinda, bila hivyo yapo majitu yanaweza kumzomea," alisema kiongozi mmoja wa dini.

Mwananchi ilipotembelea mitaa ambayo polisi wanasemekana kufanya msako huo ilielezwa kuwa, baadhi ya vijana waliokamatwa walikuwa wakifanya biashara zao za kujiajiri zikiwemo za kuuza vocha za simu.

''Hatukatai Polisi kufanya kazi zao, lakini misako hii isiwaonee vijana kwa kuwa siyo kila kijana ni mwizi au mkorofi……..mimi nadhani Polisi wanatumika kujenga chuki kati ya serikali na wananchi na kitendo hiki ni hatari kwa amani ya nchi,'' alisema mfanyabiashara wa Soko Kuu la mjini Moshi.

Alipohojiwa kuhusu kamatakamata hiyo, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Ramadhani Baruti alisema operesheni hiyo haikufanywa kwa ajili ya ujio wa Waziri Pinda, bali ni ya kawaida na kwamba baada ya uchunguzi wapo watakaofikishwa mahakamani.

CHANZO: Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.