4 Feb 2009


Wafanyakazi wote wa Shirika la Bima la Taifa (NIC) wameachishwa kazi na kulipwa mafao yao kuanzia jana ili kupisha mpango wa kuliboresha shirika hilo litoe huduma kwa ufanisi.

Taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya NIC, Dk. Hamis Kibola jana, ilisema kuwa shirika hilo litaajiri wafanyakazi wapya kulingana na mahitaji ya shirika. Dk. Kibola alisema leo na kesho shirika hilo halitatoa huduma ili kupisha kazi ya kuajiri upya na huduma itarejea tena Jumatatu ijayo wakati mchakato wa kuajiri utakapokuwa umekamilika.

Inakadiriwa wafanyakazi 500 wataachishwa kazi na shirika hilo litaajiri wafanyakazi wachache wenye ufanisi na wanaoweza kuleta changamoto mpya ya kulifanya shirika hilo liwe na tija na kuhimili ushindani wa biashara ya bima.

Dk. Kibola alisema mpango huo wa kuwaachisha kazi ni kwa mujibu wa makubaliano kati ya wafanyakazi kupitia chama chao TUICO –NIC, Serikali na Shirika la Kusimamia Mali za Serikali (CHC).

Alisema hadi jana taratibu za kuajiri upya zilikuwa zimekamilika, lakini hakusema ni kiasi gani kilichotumika kuwalipa wafanyakazi, lakini taarifa za NIC kwa Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi mwaka jana zilionyesha shirika hilo limetenga Sh bilioni 5.2 kwa ajili ya malipo ya wafanyakazi. Mwaka jana, Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo alisema serikali itauza hisa nyingi za NIC kwa wananchi pindi shirika hilo litakapoweza kusimama lenyewe miaka michache ijayo.

Akizungumza baada ya mkutano wa 12 wa Siku ya Bima, Novemba mwaka jana, Mkulo alisema serikali itapeleka bungeni mabadiliko ya sheria mbalimbali ili kuibadilisha NIC kutoka kwenye shirika kuwa kampuni na serikali iongeze fedha zaidi kuliokoa ili baadaye hisa zake ziuzwe kwa wananchi na lijiendeshe kwa faida. “Tayari mchakato wote umeshakamilika wa kuliboresha shirika hili ambapo lengo la serikali si kuliuza, bali kuliendeleza,” alisema Mkulo.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.