5 Feb 2009

Picha kwa hisani ya rasodo.wordpress.com
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi mjini hapa, imewahukumu vijana watano wa kiume wakazi wa kijiji cha Uhamaka manispaa ya Singida faini ya Sh250,000 baada ya kuwatia hatiani kwa kosa la kukaidi kushiriki mafunzo ya mgambo. Vijana hao ni Khalid Hassan,Yahaya Jumanne, Issa Jumanne, Mohamed Omari na Mohamed Omari Salumu.

Awali, mwendesha mashitaka inspekta wa polisi Joseph Bukombe alidai mbele ya hakimu wa mahakama hiyo, Ruth Massamu kuwa mnamo Juni 22 mwaka 2006 washitakiwa wote kwa pamoja walikaidi kwa makusudi kuhudhuria mazoezi ya mafunzo ya mgambo. Bukombe alisema washitakiwa walikaidi maagizo yaliyotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Singida katika barua yake ya Mei 28 mwaka 2006 iliyowataka vijana wote wenye sifa ya kuhudhuria mafunzo ya mgambo, wakahudhurie bila kukosa.

Kabla ya kutolewa adhabu hiyo,kila mshitakiwa kwa wakati wake, aliiomba mahakama hiyo kumpa adhabu nafuu kwa vile, hilo ni kosa la kwanza na kwamba hawatarudia tena kutenda kosa hilo. Akitoa hukumu hiyo, hakimu Massamu, alisema upande wa mashitaka umethibitisha bila kuacha shaka kuwa washitakiwa wanayo hatia kama walivyoshitakiwa.

"Kwa hiyo, mahakama hii inawahukumu kila moja kulipa faini ya Sh50,000 na atakayeshindwa kulipa faini hiyo, atakwenda jela mwaka moja",alisema Massamu. Washitakiwa wote walilipa faini na kuachiwa huru.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.

Podcast

Chaneli Ya YouTube