22 Apr 2009


Na Waandishi Wetu

VURUGU kubwa zimeibuka katika Makao Makuu ya taasisi ya Development of Entrepreneurship for Community Initiative (Deci), wanachama wake walipokuwa wakigombea kuingia ndani ya ofisi hizo kuorodhoresha majina yao kwa ajili ya kung’oa mbegu walizopanda.

Kati msongamano wa wanachama waliokuwa wakigombea kuingia ndani ya ofisi za taasisi hiyo jana; baadhi ya watu walianguka chini, kumi kati yao walipoteza fahamu na saba walinusurika kufa baada ya kutumbukia kwenye kisima cha maji kilichopo katika eneo hilo.

Mashuhuda wa tukio hilo waliliambia gazeti hili kuwa watu hao walianza kusukumana kwenye lango la kuingilia ndani ya ofisi hizo, muda mfupi baada ya kufunguliwa na kukaidi amri ya kufuata foleni iliyotolewa na muhudumu wa Deci.

Walisema baada ya wanachama hao kukaidi amri hiyo, walijazana kwenye mlango wa kuingilia ndani ya ofisi hizo na ndipo walinzi wa kampuni binafsi wanaolinda ofisi hizo walitumia nguvu kuwarudisha nyuma wanachama hao bila mafanikio.

“Baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya walifunga mlango wa kuingilia na shughuli za taasisi hiyo kusimamishwa kwa muda,” alisema mmoja wa mashuhuda.

Alisema ofisi zilisitishwa kuanzia saa 3:00 hadi saa 4:05 zilipofunguliwa baada ya kuwasili kwa askari polisi kutoka Kituo cha Magomeni.

Polisi hao wakiwa na silaha waliwasili kwenye ofisi hizo na kuingia ndani kupitia katika mlango uliokuwa umezingirwa na umati wa watu, ili waweze kuwalazimisha kufuata foleni.

Hata hivyo, zoezi hilo lilizidi kuwa gumu bada ya watu hao kuendelea kusukumana mlangoni hapo licha ya polisi kuingia ndani ya ofisi hizo na wahudumu wa Deci kutangaza kuwa wanachama waliopanda mbegu zao Machi mosi hadi 10, mwaka huu kuwa ndio wanatakiwa kuingia kupata huduma.

Kutokana na vurugu kuongezeka, ofisi hizo zilifungwa tena saa 7:45 mchana na kuwataka wanachama waondoke hadi kesho saa 2:00 asubuhi.

Hata hivyo muhudumu aliyekuwa anatoa taarifa kwa wanachama hao aliwataka kutofuata ratiba iliyoandaliwa na taasisi hiyo awali ya kuwahudumia waliopanda mbegu zao Februari. Badala yake aliwataka waliopanda mbegu zao kuanzia Machi mosi hadi 5, mwaka huu ndio watatakiwa kwenda kujiorodhesha leo.

Mmoja wa wanachama waliotumbikia kwenye kisima, Getruda Moto aliliambia Mwananchi kuwa akiwa na wenzake, alishituka baada ya mbao alizokuwa amesimamia juu yake zikizama.

“Mimi nilikuwa nimesimama pembeni, lakini kuna watu walikuja na kukanyaga mbao iliyogusa kwenye mgomba, ndipo ikatengua mbao zilizoegeshwa kwenye kisima hiki na mimi pamoja na wenzangu kutumbukia,” alisema Moto.

Hata hivyo alisema mara baada ya kuokolewa alifarijiwa na wanachama wenzake, wakimtaka asiilaumu Deci, bali serikali ambayo ndiyo chanzo cha yote hayo.

“Usiilaumu Deci hii haikudhamiria kufanya haya bali ni serikali iliyoifunga na kusababisha yote haya” alisema mama mmoja ambaye jina lake halikupatikana.


Mchungaji wa Kanisa la Sharoom Gospel la Yombo Buza, Kamiliusi Macha ambaye ni mmoja wa wanachama wa Deci aliilalamikia serikali kwa kutoweka ulinzi wa kutosha katika eneo hilo linalokusanya umati mkubwa wa watu.

“Hapa walitakiwa kuwepo askari wa Kikosi cha Kuzuia Ghasia (FFU), ndiyo wangeweza kuwalazimisha wanachi kupanga foleni na hali hii ya wanachama ya kujazana mlangoni isingekuwapo,” alisema Macha.

Akizungumzia kampuni hiyo alisema kwa sasa inakatisha tamaa kwani taarifa zake ni za kutatanisha. Ofisi hizo pia ziligubikwa na kila aina ya vituko baada ya vibaka kuibuka na kuwaibia watu simu za mkononi pamoja na risiti zao za Deci.

Mwanachama mmoja aliporwa risiti zote za Deci zenye thamani ya Sh 200,000 akiwa nje ya makao makuu ya ofisi hizo. Mwanachama huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini alisema aliporwa karatasi hizo alizokuwa amezishika mkononi na kuachiwa karatasi ya ratiba.

Alisema mara baada ya kuporwa stakabadhi hizo alikwenda kituo cha polisi cha Urafiki kutoa taarifa, lakini alipofika huko aliambiwa arudi katika ofisi za Deci ambako angepewa barua ya utambulisho.

Hata hivyo juhudi za kupata barua hiyo zilishindikana baada ya watendaji wa Deci kukataa kufungua mlango wa ofisi hizo kwa madai kuwa muda wa kufanya kazi ulikuwa umemalizika.

“Nifungulieni mimi nimeibiwa naomba mnisaidie, nimeshaenda polisi nimeambiwa nije huku mniandikie barua,” alilalamika bila mafanikio baada ya sauti kutoka ndani ya ofisi hizo ikidai muda wa kazi umeisha.

Mwenyekiti wa kamati ya dharura ya wanachama wa Deci, Mchungaji Isaack Kalenge alifika katika ofisi hizo na kuwatangazia wanachama juu ya mkutano wao utakofanyika Jumamosi wiki hii kuanzia saa 7:00 katika viwanja vya Jangwani na kuwataka wanachama wote kufika bila kukosa.

Kabla ya kufika katika ofisi hizo mkutano aliokuwa ameuitisha na waandishi wa habari Ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo, ulivunjwa na maofisa wa maelezo kwa kushirikiana na maafisa usalama, baada ya mchungaji huyo kutoa kauli iliyodaiwa kumdhihaki Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Mkutano huo ulivunjwa baada ya mchungaji huyo kusema kuwa kauli ya Waziri Mkuu kuwa Deci ina Sh1.8 bilioni katika akaunti yake badala ya 54bilioni zilizotajwa na viongozi wa taasisi hiyo, ni ya kuropoka na kupotosha umma.

Kauli hiyo iliwaudhi maofisa wa maelezo hivyo kumtaka aache kuongea habari za viongozi wa taasisi hiyo, hata wa serikali badala yake kusoma maandishi aliyoyaandika katika karatasi yake.

“Wewe siyo kiongozi wa Deci hivyo unatakiwa kuzungumzia masuala yako binafsi kwa kuwa ni mwanachama wa taasisi hiyo, si kumdhihaki na kumtukana Waziri Mkuu,” alisikika kiongozi mmoja wa maelezo na kuamsha kelele kutoka kwa waandishi waliokuwepo katika mkutano huo.

Hata hivyo mchungaji huyo aliitaka serikali kupitia Wizara ya Fedha kuwajengea wananchi mazingira ya kupata fedha zao.

Hata hivyo Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alimtaka mchungaji huyo kufuata utaratibu uliowekwa na jeshi hilo kabla ya kufanya mkutano wake Jumamosi ijayo kwa kuwa kufanya hivyo bila kibali ni kukiuka Sheria namba 322 ya Jeshi la Polisi iliyofanyiwa mabadiliko mwaka 2002.

Katika tawi la Deci lililopo maeneo ya Gongo la Mboto, jijini Dar es Salaam umati mkubwa wa wanachama ulikusanyika huku ukiulalamikia utaratibu wa kujiandikisha majina na kuacha risiti mpaka siku ya kurudishiwa fedha zao.

Mwananchi lilishuhudia washiriki hao wakizozana na baadhi ya viongozi wa tawi hilo na kuwalazimu kubadili uamuzi huo kwa kubandika tangazo ambalo lilikuwa linaonyesha utaratibu wa malipo kwa waliopanda mbegu kuanzia Oktoba mwaka jana mpaka Aprili, mwaka huu.

“Hatutaki kabisa kuacha risiti hapa kwani ikifika siku ya malipo mtaturuka. Tunasema hatutaki, nyie tuambieni siku ya kuja kuchukua fedha zetu, tutakuja na risiti zetu,” walisema washiriki hao.

Wakati hayo yakiendelea Deci katika taasisi nyingine ya Malingumu Investment iliyopo maeneo ya Ukonga karibia na lilipo tawi la Deci wanachama wake walionekana wakiendelea kupanda kama kawaida.

Mwananchi lilifika eneo hilo saa tisa alasiri ilikuta wanachama wa taasisi hiyo wakigombania kuingia ndani, huku wakiwa wanazuiwa na walinzi wa kampuni binafsi waliokuwa wakilinda eneo hilo.

CHANZO: Mwananchi
Baadhi ya washiriki hao walikuwa na nia ya kung’oa mbegu zao kwa kuhofia taasisi hiyo kufungiwa kama ilivyofungiwa Deci.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.