24 Apr 2009

Boniface Meena na Mkinga Mkinga

MFANYABIASHARA maarufu nchini, Reginald Mengi jana aliamua kujitoa muhanga alipotangaza majina ya wafanyabiashara watano wenye asili ya Kiasia ambao anadai kuwa ni mafisadi papa wanaoiba mabilioni ya fedha za wananchi na kutaka wachukuliwe hatua kwa madai kuwa wataiyumbisha na kuitingisha nchi.

Kati ya wafanyabiashara waliotajwa na Mengi, wawili wamefunguliwa mashtaka ya tuhuma za wizi wa fedha kwenye Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), wengine wakiwa wameshatajwa kwenye kashfa mbalimbali, zikiwemo za zabuni ya utoaji umeme wa dharura ya Richmond Development na uuzwaji wa jengo la Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Mengi, ambaye anamiliki kampuni ya IPP yenye kampuni mbalimbali zikiwemo za habari na vinywaji, alitaja wafanyabiashara hao watano akisema kuwa ndio papa kwa ufisadi lakini akasema idadi ya mafisadi wanaofilisi nchi hawazidi 10.

"Wanaotuhumiwa kuwa mafisadi papa wanahusishwa na karibu kila kashfa kubwa hapa nchini zikiwepo kashfa za Richmond, EPA, Dowans, helikopta na magari ya jeshi, ndege ya rais, rada, NSSF, Bahati Nasibu ya Taifa, mradi wa makaa ya mawe wa Mchuchuma na kadhalika," alidai Mengi katika mkutano wake na waandishi wa habari alioufanya kwenye ofisi yake jijini Dar es salaam.
>
Kati ya wafanyabiashara hao watano ambao Mengi alidai ni mapapa wa ufisadi, wamo Rostam Aziz, Yusuf Manji na Jayantkumar Chandubhai Patel (Jeetu Patel), ambao Mwananchi ilipata nafasi ya kuzungumza nao kuhusu tuhuma hizo za Mengi.

Hata hivyo, Mengi hakuwa tayari kutoa vielelezo kuthibitisha madai yake, lakini akasema iwapo watamshtaki mahakamani na wafanye hivyo kwa kuwa huko ndiko haki inakopatikana.

Mengi alirusha tuhuma nyingi kwa watu hao ambao alidai kuwa wamecharuka baada ya Rais Jakaya Kikwete kuamua kupambana nao na hivyo wameamua kupambana na yeyote anayemsaidia mkuu huyo wa nchi katika vita hiyo.

"Jitihada kubwa za Mhe. Rais za kuleta maendeleo na maisha bora kwa kila Mtanzania zinazoofishwa na wizi mkubwa wa rasilimali za taifa. Bado Watanzania wengi wanaandamwa na umaskini mkubwa; hawajui hata mlo mmoja kwa siku utatoka wapi," alidai Mengi ambaye pia alitoa taarifa ya maandishi aliyoisaini.

"Cha kusikitisha ni kuwa pale Mtanzania mwema mwenye uwezo anaposaidia jamii kuondokana na umasikini, mafisadi wanapiga kelele kuwa misaada ya aina hiyo ina agenda. Wanapinga kwa kuwa wanataka Watanzania wafe na njaa na matatizo mengine."

Mengi alikwenda mbali zaidi na kudai mafisadi anaowatuhumu wanaweza wakaunga mkono matatizo yanayotokana na Deci, taasisi inayoendesha mchezo wa kuchangisha fedha na kulipa maradufu na Watanzania kubakia "wakifukuzana na wachungaji bila ya kujiuliza ni kina nani hasa wanachochea vurugu".

Wakiongea na Mwananchi, watu hao wanaotuhumiwa kwa ufisadi hawakutaka kujibu kwa kirefu na badala yake walimtuhumu mwenyekiti huyo mtendaji wa IPP kuwa ana wivu, fitina chuki na ambaye ameshindwa kuendesha nyumba na biashara zake, huku mwingine akieleza kuwa anatumia haki yake ya kidemokrasia ya kutoa maoni yake.

"Mengi... (si mstaarabu)," alisema Manji ambaye anamiliki kampuni ya Quality Group. " Biashara zake zimemshinda ndio maana anazungumza ovyo." Rostam Aziz, ambaye ni mbunge wa Igunga anayejishughulisha na biashara mbalimbali za miradi mikubwa ya ujenzi, uchimbaji na habari, alimuelezea Mengi kama mtu ambaye analingana kwa umri na baba yake mzazi na hivyo hawezi kubishana naye.

Lakini akasema: "Mengi amejaa chuki, wivu na fitina. Sina cha kumsaidia isipokuwa kumuombea Mungu ili amsaidie kwa kumpuuzia hayo maana ni adhabu kwa nafsi yake mwenyewe. Kwa malezi niliyopata, siwezi kubishana na mzee."

Jeetu Patel naye alisema haoni busara kujibizana na Mengi na kwamba alichofanya mwenyekiti huyo wa Chama cha Wafanyabiashara Wenye Viwanda (CTI) ni kutumia haki yake ya kidemokrasia ya uhuru wa kuongea.

“Hayo ni matatizo yake," alisema Patel, ambaye anakabiliwa na kesi ya tuhuma za wizi wa fedha za EPA. "Amewaita waandishi kuzungumza nao... sikumsikia lakini ninachoweza kusema ni kwamba anatumia uhuru wake wa kujieleza.>
"Binafsi sijui chochote kuhusu hizo tuhuma za Mengi dhidi yangu, ila anayo haki ya kusema chochote. Nina mambo mengi ya kufanya hivyo sioni kama itanisaidia kwenye biashara zangu za kila siku kuanza majibizano na Mengi."

Katika mkutano wake na waandishi wa habari, Mengi alidai kuwa watu hao aliowataja si tu kwamba wanaiba rasilimali za Tanzania, bali pia wanaiba muda wa Watanzania.

"Badala ya kutumia muda katika shughuli za maendeleo, tunajikuta tukitumia muda mwingi kupambana nao na hawatingishiki," alidai Mengi. "Badala yake wanatumia fedha walizotuibia kuanzisha magazeti ya kujenga kiburi cha kutudharau, kututukana na kutunyanyasa. Inakuwa kesi ya mwizi kumkimbiza na kumpiga aliyeibiwa.

"Hata sasa hivi, mafisadi papa wanaendelea kutumia uwezo wao wa kiuchumi uliotokana na wizi wa rasilimali za nchi yetu kushawishi na kupata miradi mikubwa mikubwa kwa kutumia majina tofauti tofauti huku wakipuuza kabisa kelele za wananchi kuhusu ufisadi wao.

Alisema ni muhimu wananchi wakajiuliza hawa mafisadi wanapata wapi ujasiri wa majigambo, dharau na nguvu za kutukana na kunyanyasa watu.

Alisema mafisadi papa ni lazima wajue kwamba iwapo wapambanaji wa ufisadi watapata madhara kwa njia yoyote hapa nchini au nje ya nchi, wananchi wa Tanzania watawawajibisha.

"Ni lazima Watanzania wote tuone kwamba sasa tumefika mahali pa kusema imetosha," alidai Mengi.

CHANZO:Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.