13 Sept 2009



Na Mwandishi Wetu
KUNA kila dalili kwamba Rais Jakaya Kikwete ameamua kuwakana marafiki zake wa karibu baada ya kuueleza umma kuwa, hana urafiki wala udugu katika vita vya kupambana na ufisadi nchini.

Akizungumza na taifa kwa staili mpya ya kuwasiliana moja kwa moja na wananchi Alhamisi wiki hii, Kikwete alionya kuwa katika masuala ya rushwa, hasa ya Richmond na Kagoda, hana udugu wala urafiki.

“Mimi niseme kwamba, katika mapambano ya rushwa hakuna udugu wala urafiki, na suala la kuamua nani ashtakiwe au nani asishtakiwe halipo katika mamlaka yangu, hilo ni la Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP),” alifafanua Rais Kikwete.

“DPP akiridhika kwamba, mtu fulani ana la kujibu mahakamani wanastahiki kumfikisha mahakamani bila ya ushauri kutoka , kwa sababu katika vita hii hakuna rafiki wala ndugu."

Rais Kikwete alikuwa akijibu swali la msikilizaji aliyejitambulisha kwa jina la Joseph Machumu, aliyetaka kujua kwamba kashfa za Richmond na Kagoda zinachelewa kushughulikiwa kutokana na Rais Kikwete kuwa na urafiki na watu wanaotuhumiwa kuhusika.

Kauli hiyo ya Rais Kikwete iliibua maswali miongoni mwa wachunguzi wa mambo ya kisiasa, wakihoji kama ni kweli ameamua kwa dhati kuwatosa marafiki zake wa karibu waliohusishwa na Richmond au ililenga tu kufurahisha wananchi.

Kamati ya Bunge iliyokuwa ikichunguza kashfa ya Richmond ilimhusisha katika kashfa hiyo aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa na Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz na watumishi wengine wa serikali.

Wengine waliotajwa kuhusika katika kashfa hiyo ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, aliyekuwa Waziri wa Afrika Mashariki, Ibrahim Msabaha na watendaji wengine wa serikali, wakiwamo wanaoteuliwa na rais.

Baadhi ya watendaji hao ni Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Edward Hosea, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Athur Mwakapugi na wengineo.

Lowassa, Karamagi na Msabaha walijiuzulu mara tu baada ya kamati hiyo iliyoongozwa na Mbunge wa Kyela, Dk Harrison Mwakyembe kuwasilisha bungeni ripoti yake, Februari mwaka jana.

Miongoni mwa waathirika hao wa kashfa ya Richmond, ni Lowassa na Rostam pakee ambao Rais Kikwete aliwahi kukiri kuwa ni rafiki zake wakati akichukua fomu za kuwania uteuzi wa CCM kugombea urais mwaka 2005 mjini Dodoma.

Kikwete aliwataja maswahiba wake hao baada ya kuulizwa swali kwamba, alikuwa anajiamini nini hadi akateua baraza la mawaziri kabla ya kuteuliwa kugombea, jambo alilolipinga akifafanua kuwa akina Lowassa na Rostam walikuwa wanatajwa kwa kuwa ni marafiki zake na yeye kama mgombea hakuwa anazuiliwa kuwa na marafiki.

Baada ya uteuzi huo kumpitisha yeye na baadaye kunyakua urais, alimteua Lowassa kuwa Waziri Mkuu na Rostam akawa Mweka Hazina wa CCM na wawili hao walishiriki kwa kiwango kikubwa katika kampeni zilizomweka Rais Kikwete madarakani.

Lakini mara kwa mara Rais Kikwete amekuwa akieleza bayana kuwa hana ubia kwenye urais wake, isipokuwa Makamu wake, Dk Ali Mohamed Shein aliyekuwa mgombea wake mwenza.

Vilevile kitendo cha Rais Kikwete kukubali kupokea barua ya kujiuzulu kwa Lowassa kutoka kwenye nafasi hiyo ya juu, na kuondolewa kwa Rostam katika uweka hazina wa CCM kunawafanya baadhi ya watu waamini kuwa kweli Rais Kikwete hakuwa na ubia naye na kukubali maneno yake kuwa, kwenye suala la Richmond na kashfa nyingine za ufisadi hana urafiki wala udugu.

Pamoja na ufafanuzi huo wa Rais Kikwete suala la Richmond limekuwa ni tete tangu kuibuka kwake, huku likiwa limewagawa wabunge katika mapande mawili, moja likiwatetea washirika wa kampuni hiyo na jingine lenye nguvu likitaka watoswe kabisa.

Pia mgongano huo umehamia kwenye vikao vya CCM ambapo pande hizo zimeendelea kukamiana huku lile la watetezi wa Richmond likiwa na nguvu kuliko jingine linalotaka watoswe kwenye chama

Kutokana na mpambano uliopo kwenye suala hilo limekuwa likiibuka kila kukicha na ndio maana wasikilizaji waliamua kutumia nafasi hiyo adimu kumuuliza rais wao.

Akifafanua zaidi kuhusu suala hilo, Rais Kikwete alisema kampuni hiyo iliteuliwa na Tanesco katika mchakato wao. "Mimi nilipoambiwa nilisema kwamba, ni jambo zuri kumpata mwekezaji huyo."

Lakini Rais alikiri kwamba, ripoti za uchunguzi wa Richmond zinaonyesha kulikuwa na uzembe katika mchakato wa kuipata kampuni hiyo ya kufua umeme kwa sababu mchakato ulifanyika bila ya kamati kuthibitisha uwezo wa kampuni.

“Ingefanya utafiti wa kutosha, ikiwa ni pamoja na kutembelea ofisi za kampuni hiyo ili kujua uwezo wao na kurudisha ripoti kwa waziri na baadaye kwa waziri mkuu, lakini hilo halikufanyika. Yangefanyika haya matatizo yote yangeepukika,” alisema.

Alisema ukiachia mawaziri waliowajibika kwa kujiuzulu, maofisa wa chini waliofanya mchakato huo kushughulikiwa kwake hakujaridhisha.

“Tunapenda kuona kwamba, maofisa hawa washughulikiwe na mambo haya bado yanaendelea, katika vikao vijavyo tutapata taarifa nzuri kwa sababu hawa ndio tuliotegemea watuepushe na hasara hii, hivyo walistahili wachukuliwe hatua zinazostahili,” alisisitiza.

CHANZO: Mwananchi

TATIZO LA WENGI WA WAANDISHI WETU WA HABARI NI UVIVU WA KUCHAMBUA HABARI,SAMBAMBA NA KUJIKOMBA/KUJIPENDEKEZA KWA WATAWALA.UCHAMBUZI WENYE MANUFAA UNAPASWA KWENDA BEYOND RHETORICS NA KUNUKUU.UZEMBE WA KUSOMA "KATI YA MISTARI" UNASABABISHA UCHAMBUZI MWINGI KUWA RIPOTI YA KILICHOSEMWA NA FLANI.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.