13 Sept 2009


Lowassa Tishio Ndani ya CCM

Nguvu ya kundi lake yatawala ndani ya NEC

KUNA kila dalili kwa aliyekuwa Waziri Mkuu na Mbunge wa Jimbo la Monduli, Edward Lowassa, kupitishwa na vikao vya juu vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa mgombea urais wa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu ujao, mwaka 2010.

Taarifa za kuaminika kutoka kwa vigogo kadhaa ndani ya CCM na kwa baadhi ya wabunge wa chama hicho kikongwe nchini, zimethibitisha nia ya Lowassa kuwania kiti hicho, huku kukiwa na uwezekano mkubwa wa kupitishwa na vikao vya juu kuwa mgombea pekee badala ya Rais Jakaya Kikwete, anayetarajiwa kuomba tena nafasi hiyo ili kumalizia kipindi kingine cha miaka mitano cha kuliongoza taifa.

Taarifa hizo zimefafanua kuwa nafasi ya Kikwete kupitishwa na CCM kuwa mgombea urais haitabiriki iwapo Lowassa ataamua kuwania nafasi hiyo ambayo pia humpa nafasi kiongozi kuwa mwenyekiti wa chama.

Ikiwa imesalia miezi 13 kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo, tayari Lowassa anaonekana kuwa na nguvu kubwa ndani ya chama, huku akiungwa mkono na wajumbe wengi wa vikao vya juu, hususan wale wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho (NEC).

Siku moja tu baada ya Rais Kikwete, kuzungumza na wananchi kwa staili mpya ya kujibu maswali ya papo kwa papo, Tanzania Daima Jumapili, ilizungumza na mbunge mmoja maarufu wa CCM, juu ya mustakabali wa chama hicho kuelekea Uchaguzi Mkuu 2010, kwa sharti la kutotajwa jina lake.

“Kwa NEC hii niliyoiona kwenye kikao kilichopita, Lowassa anaweza kabisa kupitishwa kuwa mgombea urais wa CCM 2010 badala ya Bwana Mkubwa (Kikwete). Maana kwanza urais anautaka na jinsi nilivyoiona hii NEC, wajumbe wengi tayari wamesha declare interests kwa Lowassa …wengi wanamuunga mkono na ndiyo maana tumekuwa na vita kali ya makundi ndani ya chama.

“Kwa kweli Bwana Mkubwa sijui hali itakuwaje, nafasi ya kupitishwa kwake eti kwa sababu ni rais anayemaliza muda wake itakuwa ngumu sana, niseme tu kwamba haitabiriki,” alisema mbunge huyo aliyejizolea umaarufu kwa kupambana na ufisadi.

Nguvu ya Lowassa ndani ya NEC ndiyo inayodaiwa nusura imwangushe Spika wa Bunge, Samuel Sitta, baada ya wajumbe wengi kudai kwamba anaihujumu serikali bungeni, hivyo kupendekeza avuliwe uanachama, hali inayotafsiriwa kuwa walikusudia kulipiza kisasi dhidi ya hatua ya spika huyo kuunda Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza sakata la Richmond na ripoti yake kusababisha Lowassa kujiuzulu.

Kwa upande mwingine, baadhi ya vigogo kadhaa wa CCM wamekanusha kauli ya Rais Kikwete aliyoitoa wiki hii kwamba kuna uadui miongoni mwa wabunge na baina ya wabunge na mawaziri, na kufafanua kuwa uadui uliopo ni baina ya baadhi ya wabunge na chama chao.

“Alichosema rais kwamba wabunge wana uadui hata wanafikia hatua ya kuogopana, kwamba wanaweza kuwekeana sumu, kwa kweli si sahihi, uadui uliopo si kati ya wabunge na wabunge, bali ni kati ya baadhi ya wabunge na chama chenyewe. Kwani waliotaka kumsulubu Sitta kwenye NEC ni wabunge wenzake? Si wabunge wenzake, walikuwa ni wajumbe tu wa kikao kile cha chama, ambao wengi wako upande wa Lowassa. Wao bado wana kisasi na lile suala la Richmond na wako wengi kweli,” alisema kigogo huyo wa CCM.

Lowassa ambaye inaaminika kuwa ni rafiki wa siku nyingi wa Rais Kikwete, alijiuzulu uwaziri mkuu Februari 2007, kutokana na kuhusishwa na kashfa ya kutoa zabuni ya kufua umeme wa dharura kwa kampuni ‘hewa’ ya Richmod Development Company LLC.

Baadhi ya watu walio karibu na watu hao wanadai tangu kujiuzulu kwake, amekuwa katika kundi tofauti na Kikwete, huku akiwa na nguvu kubwa ya kichama inayodaiwa kuzidisha uhasama wa kimakundi ndani ya chama hicho.

Mbali ya nguvu hiyo ya kichama, wadadisi wa mambo waliozungumza na gazeti hili, walisema uwezekano wa Lowassa kuwania nafasi hiyo ya juu kabisa serikalini unatokana na ukweli kuwa mwenendo wa hivi karibuni wa utekelezaji wa maazimio ya Bunge kuhusu sakata la Richmond umeonekana kumsafisha mwanasiasa huyo kuwa hakuhusika kabisa katika sakata hilo, kwani tayari serikali yenyewe imeshatangaza kutowachukulia hatua baadhi ya watendaji waliokuwa chini yake kwa sababu ya kile kilichoelezewa kuwa hawakuhusika katika sakata hilo.

Katika mkutano wa 16 wa Bunge, serikali ilitangaza kuwa haijawachukulia hatua baadhi ya watumishi wake kadhaa ilioagizwa na Bunge, kwa sababu ya kutobainika kuhusika na mazingira ya rushwa na kuwafanya waipe ushindi wa zabuni ya kuzalisha umeme Kampuni ya Richmond.

Miongoni mwa watumishi ambao kamati teule ya Bunge iliyokuwa chini ya Mbunge wa Kyela, Dk. Harrison Mwakyembe, ilipendekeza wachukuliwe hatua za kinidhamu na kisheria lakini hawakuchukuliwa hatua kama ilivyopendekezwa na Bunge ni Mwanasheria Mkuu, Johnson Mwanyika, huku Mkurugenzi wa Tume ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Edward Hosea, akichukuliwa hatua ndogo ya kuonywa.

“Lowassa anaweza kabisa kugombea urais, kwa sababu tayari jina lake limeshatakata, maana serikali yenyewe imeshasema kwamba kina Mwanyika hawakuwa na makosa yoyote katika suala la Richmond. Sasa kama Mwanyika hakuwa na kosa basi ni dhahiri kuwa kwa mtazamo wa watu Lowassa alionewa tu, kwa hiyo anaweza kabisa kufufuka kisiasa na kugombea urais,” alisema.

Wakati hali ikiendelea hivyo, hatima ya vita hiyo ya makundi sasa inaonekana kumtegemea Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, ambaye ndiye Mwenyekiti wa kamati maalumu iliyoundwa na Kikwete ili kufanya kile kinachoelezewa na baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa kama utafiti wa kutafuta suluhu ya kuinusuru CCM kutoka kwenye vita hiyo.

Wakati kamati hiyo ina wajumbe wengine kama Abdulhaman Kinana na Pius Msekwa, ni Mwinyi pekee anayeonekana kuungwa mkono na wana CCM wa makundi yote, hivyo kuwa tegemeo pekee katika kutafuta suluhu, kwani wajumbe wenzake bado wanaonekana kuwa ni sehemu ya watu wanaochochea vita hiyo ya makundi.


1 comment:

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.