8 Sept 2009


RAIS Jakaya Kikwete leo ataanza staili mpya ya kuwasiliana moja kwa moja na wananchi kwa njia ya simu na barua pepe, akisikiliza hoja, kujibu maswali na kupata maoni yao juu ya mustakabali wa nchi , Ikulu imesema jana.

Kikwete, ambaye alizungumza na taifa kwa mara ya mwisho Juni 11 alipozungumza na wazee wa mkoani Dodoma, atafanya mazungumzo hayo ya dakika 90 kwa njia ya televisheni kuanzia saa 2:30 usiku wakati atakapopokea simu na kusikiliza maswali, ushauri, maoni na kujibu moja kwa moja.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais inaeleza kuwa katika staili hiyo ya aina yake, Rais Kikwete pia atapokea ushauri kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu (sms) kutoka kwa watazamaji na ujumbe wa barua pepe, ikiwa ni mpango wa kusikiliza matarajio ya wananchi katika jitihada zao za kuboresha maisha yao kwa kujiletea maendeleo.

"Rais atatumia aina mpya ya kuwasiliana na wananchi kwa kusikiliza hoja zao, kwa kujibu maswali yao, kusikiliza ushauri wao na kupata maoni juu ya mambo yanayohusu mustakabali wa nchi yetu, serikali yetu na maendeleo yetu," inaeleza taarifa hiyo.

"Mazungumzo hayo yatakachukua muda wa dakika 90 kuanzia saa mbili unusu usiku (saa 2:30 usiku) hadi saa nne kamili usiku."

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, chini ya mpango huo rais atazungumza moja kwa moja kupitia vituo vya redio na televisheni vya Shirika la Utangazaji (TBC) na vyombo vingine vya utangazaji nchini.

Kurugenzi hiyo ya Mawasiliano Ikulu, ilifafanua kwamba "mbali na TBC, televisheni nyingine za ITV, TVZ, Mlimani TV, Tumaini TV na Channel Ten zinatarajiwa kuonyesha mazungumzo hayo".

Taarifa ya kurugenzi hiyo imevitaja vituo vitakavyotangaza moja kwa moja mazungumzo hayo kuwa ni TBC-Taifa, Sauti ya Tanzania Zanzibar (STZ), Radio Mlimani, Radio Clouds, Radio Tumaini, na Radio Uhuru.

Ikulu pia imetaja namba zitakazotumika kwa ajili ya maswali, maoni, hoja, ushauri utakaotolewa moja kwa moja kupitia TBC. Namba hizo ni +255-22-2772448, +255-22-2772452 na +255-22-2772454.

Pia kwa watakaotaka kutuma ujumbe mfupi wa simu watatakiwa kutuma kwenda namba 0788-500019, 0714-591589 na 0764-807683, huku wale watakaotaka kutumia barua pepe watatuma kwenda anuani ya [email protected].

Hii ni mara ya kwanza kwa Rais Kikwete kutumia aina hiyo ya mazungumzo na wananchi baada ya viongozi wengine waliomtangulia kutumia hotuba za mwisho wa mwezi kwa kupitia redio na televisheni na pia mikutano na wazee au na waandishi wa habari.

Kikwete anaanza utaratibu huo akionekana kufuata nyayo za aliyekuwa Rais wa Philippines, hayati Gloria Macapagal Arroyo, ambaye amekuwa alikuwa na utaratibu wa kuruhusu wananchi kupiga simu na kuuliza maswali.

Lakini Rais wa Uganda, Yoweri Museveni ana utaratibu tofauti. Kiongozi huyo wa muda mrefu wa Uganda ana kawaida ya kuingilia mijadala inayoendeshwa moja kwa moja na vituo vya redio na kujibu tuhuma dhidi ya serikali yake au kutoa ufafanuzi.

Rais wa Marekani, Barack Obama husikiliza maoni, ushauri na kujibu maswali ya wananchi kupitia barua pepe.

Utaratibu huo mpya utamfanya rais apokee maswali ya aina tofauti na kumuwezesha kujua kero hasa za wananchi tofauti na vilio vya wanasiasa, hali ambayo itafanya muda wa dakika 90 kuwa mfupi kuweza kukidhi utashi.

Katika hotuba yake ya Juni 11, Rais Kikwete alizungumzia athari za mtikisiko wa uchumi na kutangaza mpango mkubwa wa kutenga Sh1.7 trilioni kwa ajili ya kunusuru uchumi.


CHANZO: Mwananchi

HIVI MPAKA LEO KIONGOZI WETU HAJUI MUSTAKABALI WA TAIFA LETU HADI AOMBE MAONI KUTOKA KWA WANANCHI?HIZO DAKIKA TISINI ZINATOSHA KWELI KUMFAHAMISHA KUWA NCHI INAELEKEA PABAYA?
JE INA MAANA ZIARA ZA KILA KUKICHA ZA VIONGOZI WETU HAZIJAFANIKIWA KUWAFAHAMISHA KERO ZA WANANCHI NI ZIPI?
NAULIZA HAYO KWA VILE HUU NI MWAKA WA 4 TANGU AWAMU YA NNE IINGIE MADARAKANI.SASA KAMA HADI LEO HAWAFAHAMU KINACHOIANGAMIZA TANZANIA....
LAKINI KUBWA ZAIDI YA KWAMBA LICHA YA UFINYU WA MUDA ULIOTOLEWA KWA WAULIZA MASWALI/ATOA USHAURI,NA LICHA YA UKWELI KWAMBA UTARATIBU HUO UNAWAPENDELEA WACHACHE WENYE ACCESS NA SIMU AU KOMPYUTA (KUTUMA BARUA-PEPE),KUNA UHAKIKA GANI KUWA KERO ZITAKAZOTOLEWA ZITAFANYIWA KAZI?KAMA USHAURI WA KITAALAM WA KAMATI YA AIKNA MWAKYEMBE KUWA WASHIRIKI WA UTAPELI WACHUKULIWE HATUA NA HADI LEO "BADO WANAPETA" KERO NA VILIO VYA WALALAHOIKWENYE SIMU/SMS/E-MAIL ZITABADILISHA KITU GANI?
KADRI 2010 INAVYOJONGEA NDIVYO KADRI VITUKO VINAVYOONGEZEKA.NA TUTASHUHUDIA MENGINE MENGI.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.