25 Feb 2013
26 Jun 2010
16 Feb 2010
13 Oct 2009
- 13.10.09
- Evarist Chahali
- CCM, UFISADI, USANII WA KISIASA
- No comments
Hivi mwenzangu unapoiangalia CCM kwa mtazamo wa kawaida tu (yaani usiohisha uchambuzi wa kitaaluma) unaielezeaje?Pengine huafikiani na mtizamo wangu wa “kawaida” na kitaaluma kwamba pamoja na hadi lukuki za kuwakomboa Watanzania kutoka kwenye lindi la umasikini,chama hicho hakijaonyesha dhamira ya dhati kutimiza ahadi hizo.
Tukiendeleza mazowea tutazidi kuumia.Kuna wanaodhani kwamba Tanzania haiwezi kuwa kisiwa cha amani pasipo utawala wa CCM.Wanachosahau kuwa hata hao CCM ni Watanzania wenzetu japo wanawathamini zaidi wageni (wawekezaji) kuliko sie wenye nchi.Wanasahau pia kuwa wingi wa wabunge wa CCM unakwaza jitihada wa wapambanaji kama akina Dokta Slaa kuwakalia kooni wababaishaji waliojazana chini ya utawala wa CCM.
Kusanya hasira zako lakini usipigane bali pugie kura ya kujiletea maisha yako bora wewe mwenyewe kwa kuwaondoa wanaokwaza uwezekano huo.Ifike wakati tusema tumechoshwa na ahadi na maneno matamu (na mengine si matamu bali ya dharau kama hayo ya kudai wameweka historia ya kupambana na rushwa wakati wanajua waziwazi kuwa wamekuza rushwa kupindukia).
It can be done if you play your part.
Inawezekana ukiamua kutimiza wajibu wako.
8 Oct 2009
• Homa ya Kilimo Kwanza
na Mwandishi Wetu
WAFANYABIASHARA wawili maarufu hapa nchini wenye asili ya Kiasia, Yusuf Manji na Jayantkumar Chandubhai Patel, maarufu kwa jina la Jeetu Patel, wanadaiwa kuingia katika mzozo mkubwa wa kibiashara wakati wakigombea kupata zabuni ya mradi wa kuingiza nchini na kusambaza matrekta, wenye thamani ya zaidi ya sh bilioni 50.
Habari ambazo Tanzania Daima Jumatano limezipata kutoka vyanzo vyake vya habari vya kuaminika zimeeleza kuwa, Manji na Patel ambao wanadaiwa kuhusika kwa namna moja au nyingine katika kuomba zabuni hiyo, sasa wanawindana huku wakitishana kumalizana kibiashara.
Baadhi ya watu wa karibu na wafanyabiashara hao mabilionea waliozungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti katika siku za karibuni walieleza kuwa, kumekuwa na jitihada za chini kwa chini zinazofanywa na wapambe wao kuvujisha katika vyombo vya habari mbinu zao wanazotumia kupata zabuni kubwa za serikali.
Mfanyabiashara mmoja maarufu ambaye yuko karibu na wafanyabiashara hao, alilieleza gazeti hili kuwa, mabilionea hao sasa wamekuwa mahasimu baada ya kuzidiana ujanja katika zabuni hiyo ambapo kila mmoja anatishia kutoa siri za kibiashara za mwenzake.
“Sasa wanatishana, kila mmoja anatishia kutoa siri za mwenzake kibiashara. Wote wanapata tenda kubwa kutoka serikalini, wanavyozipata wanajua wao. Kinachotushangaza kila mmoja anasema atamuanika mwenzake,” alisema mfanyabiashara huyo aliyeomba jina lake lisitajwe.
Taarifa za ndani kutoka kwa watu walio karibu na Manji, zinadai kuwa mfanyabiashara huyo hakufurahishwa na jinsi mchakato wa upatikanaji zabuni hiyo ulivyoendeshwa, na sasa anakusudia kuvujisha katika vyombo vya habari taratibu zilizokiukwa katika mchakato wa utoaji wa zabuni hiyo.
Zinadai kuwa, Manji anajiandaa kuweka wazi jinsi sheria ya manunuzi ya umma ya mwaka 2004 ilivyokiukwa wakati wa mchakato wa utoaji zabuni hiyo.
Katika mradi huo, Jeetu ambaye anatajwa kuwa mwakilishi wa Kampuni ya Escort hapa nchini, yenye makao makuu yake nchini India, ambayo imeshinda zabuni hiyo, anadaiwa kuwashawishi maofisa wa juu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambalo limekabidhiwa jukumu la kuutekeleza mradi huo na serikali, kuipatia kampuni hiyo.
Habari hizo zimedai kuwa, Jeetu alifanikisha mpango huo baada ya kuwaunganisha maofisa kadhaa wa ngazi za juu wa JKT na watendaji wakuu wa Escort walioko India, ambao baada ya kuhakikishiwa kupewa zabuni hiyo, waliwaalika maofisa kadhaa wa JKT kwenda nchini humo kwa ajili ya kusaini mkataba wa utekelezaji wa kazi ya kusambaza matrekta hapa nchini.
Taarifa zaidi zilidai kuwa, tayari baadhi ya viongozi wa juu wa JKT wamekwisha safiri hadi India kusaini mkataba huo.
Hata hivyo, inadaiwa kuwa, Manji anapinga hatua ya viongozi wa JKT kwenda kusaini mkataba huo nchini India, ikizingatiwa kuwa baadhi ya watendaji wa serikali wamekwishalalamikiwa kwa kusaini mikataba inayohusu miradi ya kitaifa nje ya nchi.
Aidha, inadaiwa kuwa, baadhi ya habari zinazotarajiwa kusambazwa zitakuwa zinahoji ukiukwaji wa taratibu kwa kutoa zabuni hiyo pasipo kuitangaza kama sheria ya manunuzi ya umma inavyoelekeza, licha ya Baraza la Mawaziri kuujadili mradi huo na kutoa baraka kwa JKT kuutekeleza.
Kwa upande wa Jeetu, taarifa zinadai kuwa, anajiandaa kujibu tuhuma za aina yoyote zitakazotolewa katika vyombo vya habari, zikiwa na lengo la kuichafua Kampuni ya Escort au zinazohusu upatikanaji wa zabuni hiyo.
Baadhi ya maofisa wa serikali waliozungumza na Tanzania Daima Jumatano kuhusu suala hilo walieleza kuwa, serikali ina taarifa kuhusu jambo hilo na inalifuatilia kwa karibu ili kuhahakisha hakuna taratibu zinazokiukwa katika utekelezaji wa mradi huo.
Mmoja wa maofisa wa ngazi za juu serikalini aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina lake alieleza kuwa, anafahamu kuwa Serikali ya India ilitoa mkopo usiokuwa na riba, wa zaidi ya sh bilioni 50 kwa Serikali ya Tanzania kwa ajili ya kununulia matrekta, wakati Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein, alipofanya ziara nchini humo mapema mwaka huu, kwa sharti la kulipwa katika kipindi cha miaka 10.
Alisema sharti jingine lililotolewa katika kutoa mkopo huo, linaitaka Serikali ya Tanzania kuhakikisha inanunua matrekta hayo kutoka kampuni za India na si vinginevyo.
Ofisa huyo alisema, serikali iliamua kuikabidhi JKT jukumu la kusimamia utekelezaji wa mradi huo ili kuondoa mazingira yoyote ya kutokea udanganyifu katika kuutekeleza.
Hata hivyo, alieleza wasiwasi wake iwapo kuna taarifa za baadhi ya maofisa wa JKT waliokabidhiwa jukumu la kusimamia utekelezaji huo, kuzungumza na mwakilishi wa Kampuni ya Escort hapa nchini (Jeetu), kisha wakaipa kampuni anayoiwakilisha zabuni hiyo bila kufuata taratibu.
“Hili jambo linaweza kuharibu kabisa sifa ya JKT kama litakuwa kweli, kwa sababu itakuwa ni kashfa kubwa kwa jeshi kukiuka taratibu za manunuzi ya umma. Ingawa kuna imani kuwa si rahisi mambo ya kijeshi kuchunguzwa, lakini hili liko wazi mno kwa sababu ni zabuni iliyo wazi iliyokuwa ikifuatiliwa na wafanyabiashara wengi, hivyo hao hao wanaweza kuwa wametoa siri za taratibu kukiukwa,” alisema ofisa huyo.
Waziri mmoja aliyezungumza na gazeti hili hivi karibuni, alisema suala hilo lilizungumzwa katika Baraza la Mawaziri na kupatiwa baraka zote za kulitekeleza. Aliongeza kuwa, anaamini hakuna taratibu zilizokiukwa.
Hata hivyo, alionya kuwa Baraza la Mawaziri linazo taarifa za mfanyabiashara mmoja maarufu kufanya mpango wa kutoa taarifa za uongo kuhusu mchakato wa upatikanaji zabuni hiyo kwa sababu ya kisasi cha kukosa zabuni hiyo.
Tanzania Daima Jumatano lilipowasiliana na Ofisa Habari wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Nadhifa Omary, ili kupata ufafanuzi wa suala hilo, alisema jambo hilo linaweza kuzungumziwa na waziri tu kwa sababu ya unyeti wake.
Alieleza zaidi kuwa, hawezi kulizungumzia kwa sababu yuko nje ya ofisi kwa mapumziko, hivyo hana maelezo ya kina ya kulitolea ufafanuzi.
Alipoulizwa, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga, Dk. Hussein Mwinyi, alisema analifahamu vizuri suala hilo na alilihakikishia gazeti hili kuwa, hakuna utata wowote katika utekelezaji wa mradi huo, isipokuwa linaweza kufanywa ajenda ya kuchafuana na watu ambao wana malengo binafsi na mradi huo.
“Ninalijua vizuri jambo hilo, tenda zilitangazwa na zikafunguliwa, nakuhakikishia. Mimi mwenyewe niliona kampuni kama 11 hivi zilizoomba zabuni hiyo, sasa kama kuna mtu anasema kulikuwa na kasoro, ni mambo ya wafanyabiashara kutaka kuchafuana tu kwa malengo binafsi waliyonayo katika mradi huo,” alisema.
Naye Manji alipotafutwa kupitia simu yake ya kiganjani ili kuzungumzia suala hilo, kwa mara kadhaa ilikuwa ikipokelewa na wasaidizi wake na kueleza ameweka utaratibu wa kutoongea na waandishi wa habari mpaka inapobidi.
CHANZO: Tanzania Daima
NILIWAHI KUANDIKA HUKO NYUMA KWANZA HUU WIMBO WA "KILIMO KWANZA" HAUNA TOFAUTI NA USANII WA "MAISHA BORA KWA KILA MTANZANIA."NGONJERA ZA KISIASA ZINAZOHANIKIZWA NA KAULI-MBIU MWANANA HAZIWEZI KUMKOMBOA MTANZANIA KATIKA LINDI LA UMASIKINI UNAOMKABILI.BADALA YAKE,JITIHADA KUBWA ZINAHITAJIKA KATIKA KUPAMBANA NA UFISADI NA MAFISADI,VIKWAZO VIWILI VIKUU VYA MAENDELEO YETU.HILO HALIWEZEKANI CHINI YA UTAWALA WA CCM KWA VILE CHAMA HICHO NI KITALU MWAFAKA KWA MAZALISHO NA HIFADHI YA UFISADI NA UFISADI.
6 Oct 2009
17 Sept 2009
HEBU SOMA HII,KISHA TAFAKARI:
Makamba amfuata Spika Sitta Urambo, ampigia magoti
*ASEMA HANA UGOMVI NAYE, ASEMA ALIKUWA MLEZI WA NDOA ZA WANAYE
Na John Dotto, Tabora
KATIKA kile kilichoelezwa kwamba, ni kujisafisha mbele ya Spika wa Bunge, Samuel Sitta, CCM imesema ipo pamoja naye katika kutekeleza majukumu yake kama Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Katibu Mkuu wa CCM, Yusufu Makamba; ikiwa ni siku chache baada ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete kuondoa utata uliotokana na maazimio ya Halmashauri Kuu ya chama hicho ulioonyesha kuwa wabunge wanaopiga kelele dhidi ya ufisadi, wanakichafua chama na serikali yake.
Akizungumza na viongozi wa CCM wilaya ya Urambo kwenye mkutano wa ndani uliohudhuriwa na Spika Sitta, Makamba, alitumia muda mwingi kumsifia Sitta kwamba ni mtu muelewa, asiyetetereka na wala kuyumbishwa na mtu yeyote na kwamba anachokifanya ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya chama hicho.
Makamba aliwaambia wanaCCM hao kwamba, hana chuki na Sitta, kwani hata alipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alimkaribisha katika ndoa za wanawe na akapewa nafasi ya kuzungumza kama baba mlezi, heshima ambayo alisema hataisahau katika maisha yake.
Alisema wana CCM wanatakiwa kupuuza maneno ya watu wanaodai chama kina mgogoro na Spika, kwasababu hakuna kitu kama hicho na yote anayoyatekeleza kwenye Bunge ni kwa niaba ya chama chake.
Hata hivyo, baada ya kikao cha NEC, Makamba alikuwa mstari wa mbele kudai kuwa kikao kile kina uwezo wa kumuhoji mbunge yoyote hata Sitta kama anakwenda tofauti na chama.
Makamba alinukuliwa akisema NEC ni mama na akina Spika ni watoto hivyo ina mamlaka ya kuhoji mienendo yao.
Mara baada ya kikao cha NEC, Sitta alifanya ziara mkoani Tabora na kulalamika kwamba, CCM makao makuu wamewakataza viongozi wa chama hicho mkoani kumpokea.
Hatua ya Makamba kwenda Urambo kuhutubia na Sitta, inatafsiriwa kama njia ya kuweka mambo sawa na kufuta makovu ya huko nyuma baina yake na Spika.
Kwa upande wake, Sitta alimshukuru Makamba kwa kutembelea jimboni kwake na mkoa wa Tabora kwa ujumla.
Katika mkutano wa hadhara uliofanyika baada ya kikao cha ndani kumalizika, Makamba aliwahakikishia wananchi wa Urambo kwamba CCM kipo pamoja na mbunge wao Sitta, ndiyo maana wanatekeleza ahadi zote ikiwemo ujenzi wa barabara ya Urambo Kaliua mpaka Tabora Mjini.
Akizungumzia suala la ufisadi, Makamba alisema kuwa wanaCCM wote kuanzia ngazi ya matawi wanapaswa kuungana na wabunge wanaopiga vita ufisadi, kwani vita dhidi ya rushwa ni ya wanaCCM wote.
Alisema anakerwa na watu wanaosema CCM ni chama cha mafisadi kwani ufisadi wa mtu mmoja si wa CCM na akatoa mfano kuwa dhambi ya Mkatoliki mmoja si dhambi ya Askofu Kilaini wala kanisa lote.
Makamba alimaliza ziara yake jana mkoani Tabora na juzi alipokuwa akizungumza na viongozi wa CCM wakiwemo makatibu wote wa wilaya za Tabora kwenye ukumbi wa mikutano wa CCM mkoa, aliwalaumu viongozi hao kukaa kimya wakati wapinzani wanakishambulia chama hicho kwa kukipakazia maneno machafu.
Aliwataka waamke na kukipigania chama na kuacha kukaa kimya na kusubiri makao makuu ama Makamba kujibu mashambulizi.
Baada ya kikao cha Nec kilichofanyika Dodoma mwezi uliopita, Makamba na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, John Chilligati kwa nyakati tofauti walisema CCM imeunda kamati ya watu watatu, inayoongozwa na Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi kuwachunguza wabunge wenye tabia ya kuishambulia serikali nje ya vikao vya chama.
Habari za ndani ya kikao hicho ambazo baadaye zilivuja kwa vyombo vya habari, zilieleza kuwa Nec ilimweka kitimoto Spika Sitta kwa madai kuwa anaruhusu mijadala inayokichafua chama na serikali, huku baadhi ya wajumbe wakishinikiza anyang'anywe kadi ya CCM kwa madai kuwa anawapa uhuru bungeni watu wanaoishambulia serikali kwa ufisadi.
Hata hivyo, mwanzoni mwa wiki hii baada ya hotuba ya Rais, Chilligati alisema chama hicho hakina ugomvi wala uadui na wabunge wake wanaoongoza vita dhidi ya mafisadi nchini.
Kabla ya hapo, Mwenyekiti wa Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita ambaye alisemekana kumwandama Spika Sitta katika kikao cha NEC na akamwita faru aliyejeruhiwa anayetakiwa kumalizwa kabla hajasababisha madhara zaidi, naye alibadili msimamo na kuwaunga mkono wapiganaji wa ufisadi pamoja na Spika Sitta kwamba, wanatekeleza ilani ya CCM, hivyo wanastahili kuungwa mkono.
Mabadiliko haya ya siasa ndani ya chama hiki tawala na mfululizo wa matukio ya aina hiyo likiwemo la Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, John Mwakipesile ambaye amekaririwa katika vyombo vya habari akisema hana ugomvi na Mbunge wa Kyela, Dk Harrison Mwakyembe, anayesemekana kuwa ni hasimu wake kisiasa.
CHANZO: Mwananchi
8 Sept 2009
Kikwete, ambaye alizungumza na taifa kwa mara ya mwisho Juni 11 alipozungumza na wazee wa mkoani Dodoma, atafanya mazungumzo hayo ya dakika 90 kwa njia ya televisheni kuanzia saa 2:30 usiku wakati atakapopokea simu na kusikiliza maswali, ushauri, maoni na kujibu moja kwa moja.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais inaeleza kuwa katika staili hiyo ya aina yake, Rais Kikwete pia atapokea ushauri kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu (sms) kutoka kwa watazamaji na ujumbe wa barua pepe, ikiwa ni mpango wa kusikiliza matarajio ya wananchi katika jitihada zao za kuboresha maisha yao kwa kujiletea maendeleo.
"Rais atatumia aina mpya ya kuwasiliana na wananchi kwa kusikiliza hoja zao, kwa kujibu maswali yao, kusikiliza ushauri wao na kupata maoni juu ya mambo yanayohusu mustakabali wa nchi yetu, serikali yetu na maendeleo yetu," inaeleza taarifa hiyo.
"Mazungumzo hayo yatakachukua muda wa dakika 90 kuanzia saa mbili unusu usiku (saa 2:30 usiku) hadi saa nne kamili usiku."
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, chini ya mpango huo rais atazungumza moja kwa moja kupitia vituo vya redio na televisheni vya Shirika la Utangazaji (TBC) na vyombo vingine vya utangazaji nchini.
Kurugenzi hiyo ya Mawasiliano Ikulu, ilifafanua kwamba "mbali na TBC, televisheni nyingine za ITV, TVZ, Mlimani TV, Tumaini TV na Channel Ten zinatarajiwa kuonyesha mazungumzo hayo".
Taarifa ya kurugenzi hiyo imevitaja vituo vitakavyotangaza moja kwa moja mazungumzo hayo kuwa ni TBC-Taifa, Sauti ya Tanzania Zanzibar (STZ), Radio Mlimani, Radio Clouds, Radio Tumaini, na Radio Uhuru.
Ikulu pia imetaja namba zitakazotumika kwa ajili ya maswali, maoni, hoja, ushauri utakaotolewa moja kwa moja kupitia TBC. Namba hizo ni +255-22-2772448, +255-22-2772452 na +255-22-2772454.
Pia kwa watakaotaka kutuma ujumbe mfupi wa simu watatakiwa kutuma kwenda namba 0788-500019, 0714-591589 na 0764-807683, huku wale watakaotaka kutumia barua pepe watatuma kwenda anuani ya [email protected].
Hii ni mara ya kwanza kwa Rais Kikwete kutumia aina hiyo ya mazungumzo na wananchi baada ya viongozi wengine waliomtangulia kutumia hotuba za mwisho wa mwezi kwa kupitia redio na televisheni na pia mikutano na wazee au na waandishi wa habari.
Kikwete anaanza utaratibu huo akionekana kufuata nyayo za aliyekuwa Rais wa Philippines, hayati Gloria Macapagal Arroyo, ambaye amekuwa alikuwa na utaratibu wa kuruhusu wananchi kupiga simu na kuuliza maswali.
Lakini Rais wa Uganda, Yoweri Museveni ana utaratibu tofauti. Kiongozi huyo wa muda mrefu wa Uganda ana kawaida ya kuingilia mijadala inayoendeshwa moja kwa moja na vituo vya redio na kujibu tuhuma dhidi ya serikali yake au kutoa ufafanuzi.
Rais wa Marekani, Barack Obama husikiliza maoni, ushauri na kujibu maswali ya wananchi kupitia barua pepe.
Utaratibu huo mpya utamfanya rais apokee maswali ya aina tofauti na kumuwezesha kujua kero hasa za wananchi tofauti na vilio vya wanasiasa, hali ambayo itafanya muda wa dakika 90 kuwa mfupi kuweza kukidhi utashi.
Katika hotuba yake ya Juni 11, Rais Kikwete alizungumzia athari za mtikisiko wa uchumi na kutangaza mpango mkubwa wa kutenga Sh1.7 trilioni kwa ajili ya kunusuru uchumi.
26 Jun 2009
21 Feb 2009
Na Boniface Meena
TAASISI ya Kupambana na Kuzuia Rushwa nchini(Takukuru) imetangaza kutoa donge nono kwa mtu yeyote atakayefanikisha kukamatwa kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi (DPA) wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba ambaye hadi hivi sasa hajulikani halipo.
Wakati Takukuru ikifikia hatua hiyo, tayari kuna wananchi ambao wametoa taarifa kwenye baadhi ya vyombo vya habari kuwa wanaweza kutoa taarifa za alipo Liyumba. Akizungumza na Mwananchi Jumapili jana Afisa Uhusiano wa Takukuru, Doreen Kapwani alisema wameamua kutangaza doge nono ambalo hakulitaja ni kiasi gani cha fedha ili wananchi wasaidie kupatikana kwa Liyumba. Alisema Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru Dk Edward Hoseah ,anakaribisha watu ambao wanaweza kutoa taarifa au kusaidia alipo Liyumba ili aweze kukamatwa.
"Kuna wananchi tumesikia wako tayari kuisaidia Takukuru, tunawakaribisha na Dk Hoseah anawakaribisha ili waweze kutusaidia na donge nono litatolewa kwa atakayesaidia kukamatwa kwa Liyumba," alisema Kapwani.
Wakati Takukuru ikifikia maamuzi hayo Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imesema kama Takukuru itahitaji msaada wa Wizara hiyo kumtafuta Liyumba iko tayari kutoa msaada huo.
Akizungumza na Mwananchi Jumapili Waziri wa Wizara hiyo, Lawrance Masha alisema wakipewa maombi ya kumtafuta Liyumba, watasaidia kumtafuta kwa kuwa wote ni Serikali. "Juzi nilitoa tamko kuwa hatujaletewa maombi ya kumtafuta, lakini Takukuru wakituletea tutafanya hivyo, kwa kuwa sisi ni Serikali," alisema Masha.
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilifuta dhamana ya Liyumba Februari 19 na kutoa amri ya kuwakamata wadhamini wake ambao walikamatwa siku hiyohiyo na baadaye kuachiwa. Wadhamini hao ni wafanyakazi wa BoT Benjamin Nduguru (mhasibu wa benki hiyo) na Agaterus Oto (Afisa Usalama wa ndani wa benki hiyo).
Hata hivyo, licha ya mahakama kufuta dhamana kuwakamata wadhamini hao, ilitoa amri ya kumtafuta na kumkamatwa Liyumba.Liyumba pamoja na aliyekuwa Meneja Miradi wa BoT, Deogratius Kweka wameshitakiwa mahakamani kwa tuhuma za kutumia vibaya madaraka yao katika mradi wa ujenzi wa majengo pacha ya benki hiyo na kuisababishia hasara serikali jumla ya Sh221 bilioni.
Liyumba alipewa dhamana na Hakimu Mkaazi wa Kisutu, Hadija Msongo kwa kutumia hati ya nyumba yake iliyoko Mbezi Juu, jijini Dar es Salaam yenye thamani ya Sh800 milioni, ambayo hata hivyo ililalamikiwa na upande wa mashitaka kwamba imetolewa katika mazingira tata kwa kuwa haijafikisha kiwango cha Sh50 bilioni walizotakiwa kutoa
Juzi Wakili wa serikali, Prosper Mwangumila aliileza mahakama kwamba, Liyumba bado hajapatikana. Hakimu alisema amri ya kumkamata Liyumba bado inaendelea na ya kuwakamata wadhamini imesitishwa hadi kesi itakapotajwa Februari 24, mwaka huu.
Katika hatua nyingine Mawakili wanaomtetea mtuhumiwa huyo waliulalamikia upande wa mashitaka kwa kitendo chake cha kuwanyanyasa ndugu wa mtuhumiwa huyo ambapo walidai kuwa uliwanyang’anya baadhi ya mali zao.
Mmoja wa mawakili hao wa utetezi, Majura Magafu aliiomba mahakama kutoa amri ya kuutaka upande wa mashitaka kuacha kuinyanyasa familia ya Liyumba na kwamba warudishe gari ya mmoja wa wadhamini ambayo waliikamata. Akijibu hoja hiyo, Hakimu Msongo aliutaka upande wa utetezi kama una maombi yoyote kuyapeleka kwa utaratibu wa mahakama kwa kuwa juzi haikuwa tarehe ya kesi.
Wakati akitoa dhamana hiyo Februari 17, mwaka huu, Hakimu Msongo alisema mshitakiwa huyo, atakuwa nje kwa dhamana ya Sh882 milioni wakati mahakama inajiridhisha na hati nyingine zilizopingwa na upande wa mashitaka. Alisema mshitakiwa atatakiwa kutimiza masharti ya dhamana ya kiasi kilichobaki cha Sh54,417,344,800.23 endapo mahakama itabaini kuwa hati hizo zina kasoro.
Hata hivyo baada ya kutolewa maamuzi hayo Wakili wa serikali Justus Mulokozi alisema hawajaridhika na maamuzi yaliyotolewa na kwamba watakaa kuyajadili na kuyatolea maamuzi. Upande wa mashitaka ulipinga kupokelewa kwa hati 10 kati ya 11 zilizowasilishwa mahakamani hapo na upande wa utetezi kwa madai kuwa zina kasoro, zikiwemo za kuwa na mali zisizokuwa za kudumu kama mbuzi, ng’ombe na kuku.
Siku mbili baada ya mtuhumiwa huyo kuachiwa huru na mahakama kutokana na kutimiza masharti, mahakama ilitoa amri ya kukamatwa tena jambo lilosababisha wadhamani wake kushikiliwa kwa muda na kisha kuachiwa.
Liyumba na Kweka walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza , Januari 27, mwaka huu kwa tuhuma za kutumia madaraka yao vibaya na kuisababishia hasara serikali kiasi cha Sh 221 bilioni. Kweka bado hajapata dhamana.CHANZO: Mwananchi Jumapili