6 Mar 2010


CCM kinara wa rushwa

Yahya Charahani

WAKATI vita dhidi ya ufisadi ikionekana kupoteza mwelekeo, Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndicho kinachoongoza kwa rushwa nchini, kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Matokeo ya utafiti huo, unaojulikana kama 'Mapambano ya Rushwa kwenye Serikali za Mitaa' ambazo unalenga ngazi za vitongoji, vijiji, mitaa na kata', yalitangazwa jana jijini Dar es Salaam na mtafiti kiongozi wa jopo la utafiti, Profesa Suleyman Ngware wa Taasisi ya Taaluma na Maendeleo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (IDS).

Watafiti wengine waliokuwapo katika jopo hilo ni pamoja na Peter Tumaini-Mungu, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (IDS), Anthony Kiberiti wa Takukuru na Stephen Ndaki wa Takukuru.Kwa mujibu wa utafiti huo, CCM inaongoza katika kujihusisha na vitendo vya rushwa kwenye uchaguzi kwa kuzoa asilimia 49.5, ikifuatiwa na Chadema 7.0, CUF 2.7, NCCR 0.5 na TLP iliyoambulia asilimia 0.5.

Hata hivyo, utafiti huo umeonyesha kuwa CCM, ambayo ilitingishwa na vita dhidi ya ufisadi iliyoendeshwa kijasiri na kikundi cha wabunge kabla ya jitihada hizo kupunguzwa kasi, imetambulika kama chama kilichoamka zaidi katika mapambano na rushwa baada ya kujinyakulia asilimia 45.1, ikifuatiwa na Chadema kilicho na asilimia 16.0 na CUF yenye asilimia 6.8.

Ngware aliwaambia wadau mbalimbali kutoka Tamisemi, baadhi ya wakurugenzi wa miji, manispaa na jiji, mameya, wenyeviti wa halmashauri, Tume ya Uchaguzi ya Taifa, wanaharakati, wanasiasa na wanahabari jana kuwa utafiti huo uliofanyika kwa miezi sita, kati ya Mei na Novemba 2009, ulihusisha katika 41 zilizo kwenye wilaya 11 zilizo ndani ya mikoa saba.

Alisema kuwa jumla ya watu 380 walihojiwa (233 wakiwa wanaume na 167 wanawake) kutoka kada mbalimbali za jamii, wakiwamo wakuu wa mikoa, makatibu tawala wa mikoa, maafisa wa Tamisemi, makamanda wa Takukuru, mameya na wenyeviti wa halmashauri za wilaya.

Wengine ni wakurugenzi wa halmashauri, viongozi wa dini, wanasheria, madiwani, viongozi wa vyama, wabunge, wanaharakati, wakuu wa shule na wananchi wa kawaida.

Alitaja mikoa hiyo kuwa ni Arusha, Dar es Salaam, Kilimanjaro, Manyara, Morogoro, Dodoma, na Tanga.

"Utafiti huu tumeufanya katika ngazi ya chini kabisa, ambayo ni pamoja na kata, vijiji na wilaya. Umewajumuisha watu wa rika zote ambao tulikuwa tukiwauliza maswali mbalimbali kuhusu rushwa," alisema Profesa Ngware.

"Lengo la utafiti huu ni kuweka msingi wa majadiliano baina ya wananchi na serikali kwa sababu njia hii pekee ndio inaweza kuleta majadiliano na siku zote majadiliano ni mwanzo wa kutatua matatizo."

Kwa mujibu wa Profesa Ngware, wananchi wanatambua uwapo wa Takukuru na mapambano yake dhidi ya rushwa kwa asilimia 79.5, ikifuatiwa na polisi asilimia 31.1, Tume ya Uchaguzi asilimia 18.6, Mamlaka za mikoa na manispaa asilimia 12.4 na waangalizi wa uchaguzi asilimia 7.5, lakini hawaridhiki na ufanisi wao katika mapambano na rushwa.

Alifafanua kuwa lengo kuu la utafiti huo lilikuwa kujifunza hali ya rushwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa 2009. Kiwango cha tatizo hilo, mbinu zitumiwazo kutenda kosa hilo, wahusika wakuu, mitazamo ya wananchi kuhusu suala la uongozi na rushwa na mbinu na mikakati inayofaa kutekelezwa kupambana na janga hilo.

Kuhusu swali lililouliza kama uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2004 ulikuwa huru na wa haki, asilimia ya jumla ilionyesha 63 kuwa ulikuwa huru na wa haki huku asilimia nyingine 24.7 zilizosalia zikionyesha kuwa haukuwa huru wala wa hali na asilimia nyingine 11.8 hazikujibiwa.

Hata hivyo kwa mkoa mmoja mmoja, Tanga imeongoza kwa asilimia za kukubali kuwa ulikuwa huru na wa haki kwa asilimia 79.2, Manyara (74.3), Morogoro (73.1), Kilimanjaro (72.4), Dodoma (56.0), Arusha (51.4) na Dar es Salaam ikishika nafasi ya mwisho kwa kupata sifuri.

Kwenye utekelezaji wa ahadi zilizotolewa na viongozi wa serikali za mitaa katika uchaguzi wa mwaka 2004 maoni ya wananchi kutoka ngazi mbalimbali yalionyesha kuwa asilimia 67.5 hazikutekelezwa na asilimia 32.5 ndiyo waliokubali kuwa ahadi hizo zilitekelezeka.

"Utafiti huu unaonyesha wazi kuwa rushwa bado ipo na imeanzia katika ngazi za chini kabisa. Kutokana na ukweli huo moja ya mapendekezo yetu ni kuitaka serikali kuanzisha kitengo maalumu cha kupambana na rushwa wakati wa uchaguzi," alisema.

Pia alipendekeza kuongezwa nguvu zaidi kwa mapambano ya rushwa na si kutegemea Takukuru peke yao kwani utafiti umeonyesha kuwa uwapo wa sheria pekee siyo suluhisho la mapambano dhidi ya rushwa.

Pia alitaka kuwapo kwa kamati maalumu za vijiji kwa ajili ya kupambana na rushwa na kwamba watu wengi walioulizwa walisema kuwa chanzo cha rushwa ni kutotekelezwa kwa sheria zilizopo.

Alisema kuwa asilimia kubwa ya watu waliokuwa wakiulizwa chanzo cha rushwa katika maeneo yao walieleza kuwa inachangiwa zaidi na ubinafsi na ulafi.

Alisisitiza kuwa moja ya umuhimu wa utafiti huo ni kuwafanya wadau mbalimbali nchini na nje ya nchi kujua nini kinafanyika mara baada ya kutoa misaada kwa ajili ya maendeleo ya sekta mbalimbali.

Alieleza kuwa asilimia 37.6 ya watu waliohojiwa walionyesha kujua maana ya rushwa wakiihusisha na fedha, ngono au chochote kinachowanywa kwa malengo binafsi huku asilimia 24.8 wakiitambua kama utoaji wa vitu vyovyote visivyokuwa halali.

Akizungumza wakati akifungua warsha ya utangazaji wa matokeo ya uchaguzi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hosea alisema wamefanya utafiti huo ili kubaini nini vyanzo vya rushwa na mbinu zitumiwazo kutenda kosa hilo ili iweze kuwasaidia wadau mbalimbali wakiwamo serikali, vyama vya siasa na hata Takukuru kukabiliana nayo.

Pia alisema utafiti huo umefanyika kwa lengo la kuondokana na kufanya kazi kwa hisia na kuondokana na utamaduni wa kulaumu bila ya kuwapo taarifa sahihi ambazo mara nyingi hutokana na utafiti.

CHANZO: Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.