SERIKALI ya Awamu ya Nne imeendelea kukumbwa na jinamizi la matumizi mabaya ya fedha za umma (ufisadi), baada ya kubainika kuwa imetumia sh trilioni 1.7 kwa kipindi cha mwaka 2008/2009 bila maelezo ya kina.
Uchambuzi huo ni ule uliotolewa na Shirika lisilo la kiserikali la ‘Agenda Participation 2000’ juu ya ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) iliyotolewa hivi karibuni, umethibitisha kuwepo kwa ufisadi mkubwa wa fedha za walipa kodi.
Uchambuzi wa ripoti hiyo ya CAG kwa mwaka 2008/2009, umeonyesha ufisadi wa kutisha serikalini kwa kiasi cha sh trilioni 1.7 uliofanyika ndani ya mwaka huo.
“Jumla ya fedha za serikali ambazo ama zilitumiwa vibaya au wahusika wameshindwa kutoa maelezo ya kuridhisha jinsi fedha hizo zilivyotumiwa inafikia shilingi trilioni 1.7. Kwa kweli fedha hizi ni nyingi sana…”, ilisema sehemu ya taarifa hiyo ya shirika hilo.
Kiasi hicho kilichofujwa ni sawa na fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya bajeti ya Wizara ya Elimu na mafunzo ya Ufundi na ile ya Miundombinu katika mwaka huo wa fedha.
Kiasi hicho pia ni sawa na mara mbili ya fedha zilizokuwa zimetengwa mwaka huo kwa ajili ya Wizara ya Afya ambayo ilipata sh bilioni 589 na mara nne ya kiasi kilichokuwa kimetengwa kwa ajili ya Wizara za Kilimo na Maji, ambazo zilitengewa shilingi bilioni 379 na shilingi bilioni 309 katika mwaka wa bajeti wa 2008/2009.
Kwa ujumla, ufisadi huo unahusisha makadirio ya fedha zilizotumiwa vibaya katika eneo la manunuzi yasiyo ya kawaida ya sh bilioni 12.8, masuala ambayo hayakushughulikiwa tangu kaguzi zilizopita sh bilioni 95.7 na misamaha ya kodi ya sh bilioni 752. 3.
Maeneo mengine ni udhaifu katika ulipaji wa mishahara uliofuja sh bilioni 3. 078, masuala yahusuyo malipo ya marupurupu sh milioni 395.8, ukiukwaji katika ununuzi wa magari wa sh bilioni 4. 018, pamoja na kiasi cha sh bilioni 203.2 zilizotumiwa vibaya au kupotea katika serikali za mitaa.
Katika ufisadi huo, Wizara ya Maliasili na Utalii ndiyo imetajwa kama mfano wa kusikitisha wa wizara zilizotumia vibaya fedha za umma.
Sehemu ya ufisadi uliofanyika ndani ya wizara hiyo inahusisha ubadhirifu wa sh milioni 12 zilizolipwa kama mishahara zaidi ya viwango halali vya mishahara ya wafanyakazi na sh milioni 53 zilizolipwa bila kutolewa viambatanisho vya kuhalalisha malipo hayo.
Sh milioni 445 pia zilitumika kulipa wastaafu, marehemu na wafanyakazi walioachishwa kazi, fedha ambazo walengwa hawakujitokeza kulipwa lakini hazikurudishwa hazina.
“Jambo jingine la kusikitisha ni kwamba Wizara ya Maliasili na Utalii ilishindwa kueleza yalipo mapato ya jumla ya shilingi bilioni 19.6,” ilisema sehemu ya uchambuzi huo wa Agenda Participation ikirejea ripoti ya CAG.
Mbali na wizara hiyo ya Maliasili na Utalii, wizara, idara au taasisi nyingine za umma zilizopata taarifa mbaya za fedha kutoka kwa CAG ni Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Jeshi la Polisi na Ofisi ya Makamu wa Rais.
Nayo Serikali ya Norway imeendelea kudai kurudishiwa sh bilioni 2.6 zilizotumiwa vibaya na Wizara ya Maliasili na Utalii.
Hata hivyo, katika taarifa ya bajeti ya wizara hiyo ya mwaka huu wa fedha, wizara hiyo ilisema kuwa ingeilipa Serikali ya Norway fedha hizo.
“Taarifa ya CAG pia inaonyesha utendaji usioridhisha katika nyanja ya mikopo iliyokuwa ikisimamiwa na taasisi za serikali kwa ajili ya wajasiriamali wadogo wadogo miongoni mwa wanawake na vijana nchini.
“Kwa mfano jumla ya sh milioni 355 zinazodaiwa kutolewa kwa wajasiriamali wanawake na vijana hazikuonyeshwa jinsi zilivyotumika. Taarifa za fedha kutoka halmashauri 41 hazikupatikana,” ilieleza taarifa hiyo.
Mashirika ya umma na mamlaka kama vile Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Shirika la Bima la Taifa (NIC), Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Shirika la Taifa la Umeme (TANESCO), Mamlaka ya Bandari (TPA) na Mfuko wa Hifadhi wa Serikali za Mitaa (LAPF) ni maeneo mengine ya upotevu mkubwa wa fedha.
Kwa mfano, ilithibitishwa kuwa jumla ya sh bilioni 58 zilizokuwa zimetolewa kama mkopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu mwaka 2006, mpaka sasa hakuna uhakika wa kulipwa kwa fedha hizo ambazo zilitolewa dhamana na serikali.
“Kinachowasikitisha wengi ni kwanini serikali bado inashindwa kuziba mianya ya baadhi ya maofisa wake kuendelea kutafuna fedha za umma,” umehitimisha muhtasari wa wachambuzi wa wanaharakati hao.