14 Jul 2010

Nimekumbana na swali hili tangu udogoni:Alianza kuku,au lilianza yai?Kama alianza kuku,alitoka wapi ilhali sote twajua kuku anatoka kwenye yai?Na kama lilianza yai,lilitoka wapi wakati tunafahamu kuwa yai hutagwa na kuku?Baada ya kukosa jibu lenye mantiki niliamua kuachana na swali hali maana kujihangaisha kutafuta jibu ilikuwa kazi bure.Nahisi hata nawe msomaji umeshakumbana na swali hilo mara kadha wa kadha.

Lakini hatimaye kitendawili hicho kimepata ufumbuzi.Kwa mujibu wa gazeti la bure la Metro,watafiti wa Kiingereza wanasema kuwa kuku ndiye aliyeanza kabla ya yai kwa vile yai linaweza kupatikana tu kwa chembechembe za protini zinazopatikana katika mifuko ya uzazi ya kuku.

"Imekuwa ikidhaniwa kwa muda mrefu kuwa yai ndilo lililoanza kabla ya kuku lakini sasa tuna ushahidi wa kisayansi kuwa kwa hakika alianza kuku kabla ya yai",alisema Dakta Colin Freeman kutoka Chuo Kikuu cha Sheffield,aliyeshirikiana na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Warwick.

"Protini hiyo ilitambuliwa kabla na ilihusishwa na uzalishaji wa yai lakini kwa kuchunguza kwa undani tumegundua namna gani protini hiyo inavyowezesha hatua hiyo (ya kutengeneza yai).

Protini hiyo-inayofahamika kitaalam kama ovocledidin-17 (OC-17) inafanya kazi kama kichocheo (catalyst) kuharakisha maendeleo ya yai.

Wanasayansi hao walitumia kompyuta yenye uwezo wa hali ya juu (supercomputer) ifahamikayo kama HECToR,ambayo ipo jijini Edinburgh,Scotland, kukuza (zoom) hatua zinazoonyesha jinsi yai linavyozalioshwa.

Ilibainika kuwa OC-17 ni muhimu katika kuanzisha kukomaa (crystallization)-hatua ya awali katika uundwaji wa gamba la yai.Protini hiyo hugeuza calcium carbonate kuwa chembechembe za calcium (calcite crystals) ambazo ndizo zinazounda gamba la yai,huku zikitengeneza gramu 6 za gamba katika kila masaa 24.

Profesa John Harding,pia kutoka Chuo Kikuu cha Sheffield,alisema kuwa ugunduzi huo unaweza kuwa na matumizi mengine pia."Kufahamu namna gani kuku wanatengeneza mayai ni jambo la kupendeza lakini pia linaweza pia kutupatia vidokezo katika namna ya kutengeneza vitu vipya".

Imetafsiriwa kutoka gazeti la Metro toleo la leo.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.