5 Aug 2010

Natoa wito kwa wanachama walioomba nafasi lakini wakakosa, jamani msiwe chanzo cha mifarakano ndani ya chama, KAZI ZIPO NYINGI,TUNAWEZA KUTEUANA, fanyeni kazi ya ushindi kwa chama chetu,” .Hayo si maneno yangu bali ya Rais Jakaya Kikwete aliyoyatoa siku alipochukua fomu za kuogombea tena urais kwa tiketi ya CCM.Ni kweli kazi zipo nyingi ikiwa ni pamoja na kilimo au biashara lakini haiingii akilini kwa watu waliokataliwa na wananchi kupewa nafasi kwa mlango wa "kuteuana".

Hili ni tatizo sugu katika siasa za Tanzania.Utakuta mtu ameboronga sehemu moja kisha anahamishiwa sehemu nyingine.Yayumkinika kusema kuwa kuteua "rejects" hao sio tu matumizi mabaya ya ruhusu inayotolewa na katika kufanya teuzi mbalimbali bali pia ni dharau ya moja kwa moja kwa wananchi.

Haiwezekani kwamba nchi yenye watu zaidi ya milioni 40 iwe na kikundi kidogo tu cha watu wenye uwezo wa kuwa viongozi.Na kibaya zaidi kikundi hicho kikijumuisha watu waliokataliwa na wananchi katika chaguzi au maombi yao ya kutaka wachaguliwe kuongoza.

Na ukiingia kiundani zaidi kuangalia tabia hii isiyopendeza,unaweza kuyumkinisha kuwa hata uteuzi wa Dkt Gharib Bilal unaangukia kwenye eneo hilohilo.Bilal alitaka ridhaa ya vikao vya CCM kuwa mgombea wa Zanzibar lakini "kura hazikutosha".Hata hivyo,katika kile kinachoelezwa kama kujenga mshikamano miongoni mwa wana-CCM,Bilal aliteuliwa na JK kuwa mgombea mwenza wake.Kwa maana nyingine,mtu aliyekataliwa na kikundi kidogo (kikao cha CCM kilichpiga kura kumpata mgombea urais wa Zanzibar) anaweza kuwa Makamu wa Rais wa Watanzania milioni 40 na ushee pindi JK akishinda katika uchaguzi ujao.

Tumekuwa tukishuhudia teuzi za mabalozi wetu nje ya nchi,wenyeviti wa bodi za wakurugenzi wa taasisi mbalimbali,wakuu wa mikoa na wilaya na nafasi mbalimbali zinazojazwa kwa teuzi zinazofanywa na rais zikijazwa na "rejects"-watu walionyimwa ridhaa ya kuongoza na wananchi lakini wanaishia kuwa viongozi kwa mlango wa nyuma.Yaleyale ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa UWT,Hasna Mwilima.Kikundi kidogo katika jumuiya hiyo ya akinamama wa CCM kilimkataa,huku sababu kuu ikitajwa kuwa ni uongozi mbovu.Lakini siku chache baadaye,Rais akamteua mwanamama huyo kuwa Mkuu wa Wilaya.Busara kidogo tu zinaweza kubainisha kuwa kuwa mtu alokataliwa kuongoza UWT hawezi kuwa "rais wa wilaya" (DC) lakini kwa vile Katiba inamruhusu Rais kuteua yeyote amtakaye,analotaka liwe litakuwa.

Ni katika mazingira haya ndio maana tetesi kuwa Lowassa,Waziri Mkuu aliyelazimishwa kujiuzulu kutokana na ufisadi wa Richmond,atarejea madarakani pindi JK akishinda hapo Oktoba zinazidi kupata nguvu kwa vile Rais akiamua iwe na itakuwa.Na kwa vile Watanzania wanasifika kwa upole wao,hakutokuwa na "kelele" za kupinga uteuzi huo.

Nguvu anazopewa Rais kwenye Katiba hazimaanishi ajifanyie mambo anavyotaka bali ni kwa minajili ya kuwatumikia Watanzania kwa ufanisi.Lakini kwa upande mwingine,lawama zinaweza kuelekezwa kwa taasisi zinazomshauri Rais kuhusu teuzi mbalimbali (ikiwa ni pamoja na kuchunguza 'usafi' na uwezo wa wateuliwa watarajiwa) kwa sababu inaelekea kwa wao,kila jina linaloletwa na Rais ni 'safi'.Professionalism na ethics zinawekwa kando kwa minajili ya kumfurahisha mkuu wa nchi.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.