Kitu kimoja cha wazi ni kwamba kama kuna mtu anayetegemea Kikwete na CCM yake wataleta ufumbuzi wa matatizo ya Tanzania,basi anaweza pia kutarajia kugema damu kwenye jiwe.Kulalamika peke yake hakuwezi kuleta ufumbuzi wa matatizo.Mkoloni,Makaburu,Nduli Idi Amini hawakuondoka kwa vile tuliwatukana au kuwalalamikia,bali tulijiunga kwa umoja wetu na kupambana nao (hata kwa nguvu ilipobidi).
Anyway,soma habari hii hapa chini inayodhihirisha kuwa wababaishaji hawa (Kikwete na chama chake cha Magamba) wapo too busy katika vita vyao vya kimaslahi to care about matatizo ya Watanzania
Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Benno Malisa
WENYEVITI MIKOA WALIPINGA, BARAZA KUU UVCCM LAUNGA MKONO ZIARA ZA KINA NAPE
Waandishi Wetu
MPANGO mkakati wa kujivua gamba kwa lengo la kurejesha uhai ndani ya CCM unaelekea kuwa bomu la maangamizo kwa chama hicho, baada ya baadhi ya wenyeviti wa mikoa kuupinga huku wakiagiza wafuasi wao kuwashusha majukwaani makada wanaoupigia debe.
Wakati wenyeviti hao wakiupinga, Baraza Kuu la Umoja wa Vijana CCM (UVCCM), jana limetoa tamko rasmi la kuunga mkono ziara hizo zinazofanywa na Katibu wa Itikadi na Uenezi Taifa wa chama hicho, Nape Nnauye za kutekeleza mkakati huo.
Mpango huo wa kujivua gamba ulitangazwa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete katika maadhimisho ya miaka 34 ya kuzaliwa chama hicho kikongwe barani Afrika, lakini jana baadhi ya wenyeviti wake wa mikoa akiwamo, John Guninita wa Dar es Salaam na Hamis Mgeja wa Shinyanga, waliupinga wakisema unamwaga sumu kali dhidi ya chama.
Msimamo wa UVCCM
Baraza Kuu la UVCCM limetoa msimamo wake kuunga mkono ziara za mikoani zinazoongozwa na Nnauye za kujivua gamba huku likiweka bayana kuwa huo ni msimamo wa Halmashauri Kuu (Nec) ya chama na si wa Katibu huyo wa Itikadi na Uenezi.
Mbali na Nape, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe na Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka wamekuwa wakifanya ziara mikoani hasa katika mwisho wa wiki ambazo pamoja na mambo mengine, wamekuwa wakifanya mikutano ya kukipa uhai chama huku wakitangaza uvuaji gamba.
Kaimu Mwenyekiti wa UVCCM, Benno Malisa alisema UVCCM ilipongeza uamuzi wote wa NEC: "Kila kinachofanyika ni sahihi na sisi tunaunga mkono kabisa."
Guninita awatangazia vita
Wakati vijana wakiuunga mkono ziara hizo, juzi Guninita aliwaambia wanaCCM wa Tawi la Sinza kwamba watakapomuona kiongozi yeyote mkubwa wa chama hicho anakikiponda katika wasisite kumshusha jukwaani.
Guninita alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na wanachama hao kuhusu matatizo mbalimbali ya chama hicho na kusisitiza kwamba Waziri Sitta asipojibiwa kauli zake atajiona kuwa ni mkubwa zaidi.
Wiki iliyopita Mwenyekiti huyo alimtupia kijembe Sitta akidai kwamba waziri huyo ana mpango wa kuhakikisha kuwa Serikali ya chama hicho inaondolewa madarakani kwa kuwa bado ana hasira za kupoteza wadhifa wa Spika wa Bunge.
“Chama chetu kinazidi kupoteza sifa, hii ndiyo sababu ya mimi kufanya ziara katika majimbo ambayo yalishindwa katika ngazi zote kukipatia chama ushindi wakati wa uchaguzi. Kumekuwa na viongozi wakubwa wa chama hicho wanaozunguka nchi nzima na kuchochea ili Serikali iondolewe madarakani, nawaambieni mkiwaona viongozi hao wanakiponda chama washusheni majukwaani, wanataka kujiona wao ndiyo wakubwa zaidi ya wengine.”
Alisema chama hicho kinajipanga kikamilifu ili kuhakikisha uchaguziwa mwaka 2015, kinashinda kwa kishindo ikiwa ni pamoja na kupambana na tatizo la rushwa lililokitawala.
Guninita ambaye amekuwa akipingana hadharani na wapambanaji hao wa ufisadi ndani ya CCM, alisema katika uchaguzi huo hawatahitaji ushahidi kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (Takukuru) na kuwa mtu atakapobainika anajihusisha na rushwa atachukuliwa hatua hapohapo.
“Tatizo la rushwa katika chama lipo hasa wakati wa uchaguzi. Ninachotaka kuwahakikishia ni kwamba tunajipanga na katika uchaguzi ujao hatutahitaji ushahidi wa PCCB (Takukuru), tutakapombaini mtu tutampeleka mahakamani wenyewe. Hatutaki aibu ya mwaka huu itukumbe tena.”
Alisema tayari chama kimewabainisha viongozi wote walioingia madarakani kwa rushwa na kuwa wanaendelea kujadiliana hatua za kinidhamu dhidi yao.
Guninita alisema katika uchaguzi wa mwaka 2015, chama hicho hakitapeleka majina ya watu watakaobainika kutoa rushwa kwa ngazi za juu ili wakubalike katika kura za maoni.
Mgeja atoa tahadhari
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja alisema juzi kwamba licha ya kuwakaribisha wapambanaji hao na mkakatio wao wa kujivua gamba katika mkoa wake, waende na majibu ya kero za wananchi.
Alisema viongozi wa chama chake wanatakiwa kwenda na majibu ya kero zilizopo katika mkoa huo za wakulima kuuziwa dawa feki za pembejeo, rushwa, umasikini na rasilimali kama madini kushindwa kuwanufaisha, badala ya kutumia ziara hiyo kuwapaka matope wenzao.
“Ziara za kusafisha chama siyo mbaya, kama zitatumika vyema, lakini hali ambayo imeanza kujitokeza ni wazi haijengi chama, bali inaendelea kumwaga sumu,” alisema.
Millya, Porokwa waponda ziara hizo
Mbali ya Guninita na Mgeja, Mwenyekiti wa UVCCM, mkoani Arusha, James Ole Millya naye ameziponda ziara hizo za kujivua gamba akisema hazina tija kwa chama na Serikali kwa kuwa Sitta, ni waziri ndani ya Serikali hiyohiyo anayoituhumu na kueleza kwamba anaona kuna uchafu ndani yake ni vyema akatoka.
Millya aliwatuhumu Sitta, Nape, Ole Sendeka na Dk Mwakyembe kuwa wamekuwa wakitumia mwanya wa ziara hizo kuichafua Serikali na chama tawala huku akisisitiza: "Kama wanaona Serikali hiyo haifai ni bora wangeondoka. Sitta ni waziri, Mwakyembe ni waziri na wengine wako ndani ya Serikali na chama hawa wote ni viongozi, sasa kitendo cha wao kuzunguka na kuisema vibaya Serikali na chama tawala hakifai.”
Alisema viongozi hao wameamua kuanza mashambulizi dhidi ya Serikali kwa kuwa ni wabinafsi, huku akikitahadharisha chama hicho kuwa makini na ziara hizo kwa kuwa huenda zikakiingiza katika hatua mbaya.
Naibu Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, Daniel Porokwa naye aliziponda ziara za viongozi hao akisema zimejaa unafiki kwa kuwa Sitta na Nape walikuwa waanzilishi wa Chama cha Jamii (CCJ) na kuwaita wasaliti ndani ya CCM.
Alisema pamoja na kutoa tuhuma mbalimbali dhidi ya viongozi hao kuwa ni waasisi wa CCJ, anashangaa hadi leo uongozi wa chama chake haujawahi kumwita au kumwomba udhibitisho juu ya madai aliyoyasema.
Katibu wa Itikadi na Uenezi Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Nape akutana na mabango Moshi
Ziara ya Nape, juzi mkoani Kilimanjaro ilikumbana na upinzani mara baada ya kiongozi huyo kupokewa kwa mabango mbalimbali wakati akishuka kwenye gari lake katika Kituo cha Mabasi Moshi Mjini tayari kwa kuhutubia mkutano wa hadhara katika eneo hilo.
Hata hivyo, tofauti na mikutano mingine kama ule wa mkoani Mbeya, huo ulihudhuriwa na watu wachache huku wengine walionekana wakishuka kutoka kwenye mabasi uwanjani hapo.
Nape aliyefika kituoni hapo mnamo a saa 9:00 mchana akitokea Mwika katika ufunguzi wa Tawi la CCM Chuo Kikuu cha Tumaini (Smmuco), alikutana na mabango yaliyokuwa yameshikiliwa na vijana wa CCM wilayani Moshi ambayo yalikuwa yamebeba ujumbe mbalimbali.
Baadhi ya mbango hayo yalikuwa yakisomeka: ”CCJ nao wajivue gamba,” “Hatutaki makundi ndani ya CCM,” ”Vijana tumechoka na wana CCJ, wana CCJ ondokeni mtuachie CCM yetu.”.
Wakati vijana hao wakibeba mabango hayo mbalimbali yaliyolenga kufikisha ujumbe kwa Nape, vijana wa ulinzi wa CCM maarufu kama “Green Guard,” iliwabidi kutumia nguvu za ziada kuzima juhudi za vijana hao waliobeba mabango hayo na waliyakamata na kisha kuyachana baadhi yao huku mengine yakiwasilishwa katika Ofisi ya Katibu wa CCM wilayani Moshi.
Akimkaribisha Nape jukwaani, Katibu wa CCM Wilaya ya Moshi Mjini, Amos Shimba aliyaponda vikali mabango hayo huku akisema vijana walioyabeba siyo wakazi wa Mji wa Moshi, bali wanatoka mkoani Arusha huku akiwaonya, kamwe wasithubutu kuleta mambo hayo mkoani Kilimanjaro.
“Kuna vijana wanaotaka kutuletea vurugu na tunajua wanatoka tu Arusha, tunawaambia tafadhali sana msituletee mambo yenu ya vurugu za Arusha hapa mkoani kwetu,” alionya Shimba.
Akihutubia mkutano huo, Nape alisema lengo la ziara yake mkoani Kilimanjaro ni kuleta matumaini kwa wanachama wa CCM sanjari na kufafanua falsafa ya kujivua gamba ambayo alidai inapotoshwa na watu wachache hapa nchini.
Alikishambulia Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) hususan viongozi wake kwamba wanapenda vurugu na maandamano huku akionya kwa kutumia mifano na nahau mbalimbali ya kuwa kamwe Serikali ya CCM haitakubali amani ya nchi ichezewe.
Aliendelea kumshambulia vikali Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa akidai kuwa ameamua kukishinikiza chama chake kumlipa kiasi cha Sh7 milioni ihali alikuwa kinara wa kupinga mishahara minono na marupurupu ya wabunge.
“Namtaka Dk Slaa aishi kama anavyoongea, alinituhumu nahusika na EPA mkiniangalia mimi sura yangu inafanania na EPA? Mbona yeye amekishinikiza chama chake kimlipe Sh7milioni wakati alikuwa akipinga mishahara na marupurupu ya wabunge? Huyu ni mnafiki,” alisema Nape.
Alisema falsafa ya kujivua gamba ndani ya CCM imekuwa ikipotoshwa na baadhi ya watu hususan wapinzani na kuuita kuwa ni dhana ya kishetani kwa kuwa imetumia mfano wa nyoka na kuwabeza watu hao kwa kuwataka wasome biblia na msaafu na kuwaeleza kuwa nyoka ametajwa ndani ya vitabu hivyo.
Akizungumzia kauli za wanaCCM wanaoipinga dhana hityo, alisema asingependa kujibizana na watu wanaouzungumza barabarani kwani chama kina vikao ambavyo vitawahukumu.
Alichokisema Sitta
Akizungumza Dar es Salaam juzi, Sitta alisema Serikali makini lazima ikiri mapungufu kutokana na makosa yake: "Nilichokisema Mbeya ni kuwaambia Watanzania ukweli na nitaendelea kuwaambia ukweli."
Alisema serikali makini haiwezi kuwadanganya wananchi wake na kusisitiza, "Watanzania wa leo ni watu wenye akili huwezi kuwambia habari nzuri za umeme wakati umeme ni tatizo."
"Kule Mbeya nilieleza ule umati ukweli kuhusu upungufu wetu serikalini na wananchi walituelewa. Kuna upungufu tumeukiri na tunajipanga kuupatia ufumbuzi. Umeme ni tatizo kubwa huwezi kueleza uongo kwa Watanzania wakakuelewa, waambie wananchi ukweli watakuelewa. Sasa huu ndiyo upungufu wetu, lakini wanatokea baadhi ya watu wenye upeo mdogo ndani ya CCM wanaoendekeza siasa za ufuasi, wanakaa na kuzungumza mambo ya hovyo."
Imeandaliwa na Ramadha Semtawa, Minael Msuya, Dar, Habiel Chidawali, Dodoma, , Moses Mashalla, Moshi