20 Jun 2011


Sio siri kwamba Rais Jakaya Kikwete anapenda sana kusafiri.Kuna vijimikutano vya kimataifa mbavyo kwa hakika visihitaji Tanzania iwakilishwe na Rais na badala yake akaenda Waziri Mkuu au kwa stahili kabisa Waziri wa wizara husika.Lakini asipokwenda yeye,watajuaje kama Kikwete ndiye Rais wa Tanzania?

Tuweke hilo kando.Tatizo jingine la Kikwete ni kutoa kauli ambazo yayumkinika kuamini kuwa hazijafanyiwa tafakuri ya kutosha.Huku nyuma,alishawahi kusema haelewi kwanini Tanzania ni masikini,na Waziri Mkuu wake,Mizengo Pinda, akaakisi kauli hiyohiyo.Sasa kama Rais hajui chanzo cha umasikini wa nchi anayoongoza,anafanya nini hapo Ikulu?

Safari hii kaibuka na madai kwamba kinachokwaza maendeleo yetu ni ukosefu wa fedha.Fedha zipi hizo?Mbona yeye kiguu na njia huku safari zake zikilibebesha taifa mzigo mkubwa wa gharama?Na fedha zipi anazozungumzia ilhali wabunge wetu wanalipwa mamilioni ya posho kwa "ku-rubber stamp" kila kinachowasilishwa kwao na serikali huku jitihada kubwa zaidi wanayofanya ni kubamiza meza (pongezi) kama sio kuwazomea wabunge wa upinzani?

Hebu soma porojo zake hapa chini

JK: Ukosefu wa fedha unakwamisha maendeleo
Sunday, 19 June 2011 20:57
Mwandishi Wetu
RAIS Jakaya Kikwete amesema ukuaji wa kasi wa uchumi na maendeleo katika Bara la Afrika unakwamishwa na ukosefu wa fedha za kutosha za kugharimia miradi ya maendeleo. 
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu jana, Rais Kikwete alikuwa akizungumza kwenye siku ya kwanza ya mkutano wa Kimataifa wa mwaka huu wa Taasisi ya Smart Partnership Dialogue ambao pia unajulikana Langkawi International Dialogue 2011, ulioanzishwa rasmi mwaka 1995. 
Rais Kikwete alisema kwamba njia za jadi za kupata fedha za kutosha ili kuharakisha ukuaji kasi wa uchumi, hazina uwezo wa kutoa fedha za kutosha kwa ajili ya maendeleo. 
Rais Kikwete alisema kutokana hali hiyo ni lazima nchi za Afrika zitafute namna nyingine mpya ya kugharimia maendeleo ya bara hilo na watu wake. 
“Tatizo ni ukosefu wa fedha za kutosha kugharimia miradi inaweza kuzitoa nchi za Afrika na watu wake katika umasikini kwa haraka zaidi,” Rais Kikwete, mjini Kuala Lumpur, Malaysia. 
Shabaha kuu ya Smart Partnership ama Langkawi International Dialogue ni kufanya majadiliano ya kimataifa ya jinsi ya kuharakisha maendeleo ya kiuchumi duniani. Mada kuu katika mkutano wa mwaka huu ni ‘Enhancing Smart Partnership for Socio-Economic Transformation’. 
Akishiriki katika mjadala huo, Rais Kikwete aliwaambia mamia ya washiriki tatizo kubwa linalokwamisha ukuaji kasi wa uchumi na maendeleo katika Afrika ni ukosefu wa fedha za maendeleo kwenye sekta binafsi, sekta ya umma na kwa Serikali. 
Rais alisema chanzo kikuu cha fedha za maendeleo kwa nchi masikini za Afrika ni misaada ya maendeleo (ODA), lakini sasa fedha za ODA zimekuwa zikipungua na wakati mwingine hazipatikani.
“Hata ukitofautiana na kampuni yenye asili ya nchi inayotoa misaada, basi utanyimwa misaada hata kama kampuni yenyewe ndiyo yenye makosa,” alisema Rais Kikwete. 
Rais alisema wakati mwingine inakuwa vigumu kuvutia fedha za maendeleo kutoka nje. 
“Hakuna fedha za kutosha kwenye masoko ya fedha ya ndani na msingi mzima wa kifedha ni dhaifu sana. Msingi wa fedha wa ndani ni dhaifu na hata msingi wa fedha za kigeni wa nchi zetu ni masikini,”alisema Rais Kikwete. 
Rais alisema hali hiyo imezifanya nchi za Afrika kujikuta katika wakati mgumu wa kutimiza wajibu na majukumu yake katika kuwaletea wananchi maendeleo. 
“Hivyo, sisi katika Afrika tunahitaji kutafuta na kuangalia njia nyingine za ubunifu zaidi za jinsi ya kupata fedha za maendeleo,” alisema Rais Kikwete. 
Mapema mkutano huo ulifunguliwa na Waziri Mkuu wa Malaysia, Dato’ Sri Mohammed Najib Tun Abdul Razak ambaye hotuba yake ilizungumza masuala mengi na matatizo mengi yanayoikabili dunia kwa sasa pamoja na umuhimu wa ushirikiano baina ya nchi zinazoendelea.

CHANZO: Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.