10 Jun 2011

Zitto ajitoa kupokea posho za Bunge Send to a friend
Thursday, 09 June 2011 23:25
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe
Exuper Kachenje
MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, ameiandikia barua Ofisi ya Bunge kuiomba isimamishe kumlipa posho zake zinazotokana na vikao vya Bunge kuanzia juzi.Zitto ametoa ombi hilo kwa barua rasmi aliyoiwakilisha kwa Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah Juni 7 mwaka huu.
Katika barua hiyo, ambayo gazeti hili limefanikiwa kuiona, Zitto alisema anaamini kuwa watumishi wa Serikali na wabunge, hawastahili kulipwa posho wanapohudhuria vikao rasmi vya uwajibikaji wao wa kawaida.
Zitto alisema kuwa posho hiyo haistahili kulipwa kwake, wabunge wengine wala watumishi wa umma kwa kuwa kuhudhuria vikao ni sehemu ya kazi zao.
"Kwa mujibu wa Sheria ya Utawala wa Bunge (National Assembly Act of 2008) na kwa mujibu wa Masharti ya Kazi za Mbunge niliyokabidhiwa, ninastahili kupata posho za vikao, (sitting allowances) kila ninapohudhuria vikao vya Bunge na Kamati zake,"alisema Zitto na kuongeza:
"Ni imani yangu kuwa posho ya kikao haistahili kulipwa kwa mbunge na mtumishi mwingine yeyote wa Serikali kwani kuhudhuria kikao ni sehemu ya kazi yangu,".
Kupitia barua hiyo, Zitto ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Fedha, alieleza kwamba amekuwa akipendekeza posho za vikao hivyo ifutwe, jambo ambalo pia limo katika mapendekezo ya chama chake (Chadema) katika Bajeti ya 2011/2012.
"Nimekuwa nikipendekeza kuwa posho hii ifutwe. Chama changu cha Chadema pia kimependekeza jambo hili katika mapendekezo yake ya Bajeti 2011/2012," alisema Zitto na kuendelea:
"Mpaka hapo mfumo wa kulipana posho za vikao utakapofutwa, ninaelekeza kwamba stahili zangu zote za posho zielekezwe katika Taasisi ya Kigoma Development Initiative (KDI).., utaratibu huu uanze kuanzia tarehe 8/6/2011."

Katibu wa Bunge agoma kuizungumzia
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alipoulizwa jana kama amepokea barua hiyo ya Zitto, alisema kuwa, yeye kama mtendaji wa mhimili huo wa Dola, anapokea barua nyingi, hivyo si rahisi kukumbuka kama barua hiyo imefika ofisini kwake.
Lakini akasema, hata kama barua hiyo itakuwa imemfikia ofisini, kanuni na taratibu haziruhusu Bunge kutangaza habari za mtu binafsi.Alisema ofisi yake hairuhusiwi kuandika masuala binafsi ya wabunge yanayofikishwa ofisini na kwamba hilo linawezekana ikiwa mhusika (Zitto), ameruhusu lifanyike kwa maandishi.
"...Haturuhusiwi kuandika habari  za mtu. Nikiwa Katibu wa Bunge, napokea barua nyingi 'personal' (binafsi), lakini kama yeye mwenyewe amewaambieni kuwa kaleta barua hiyo, basi mwambieni pia atuandikie barua kuturuhusu na sisi ili tulitangaze hilo," alisema Dk Kashililah.
Bajeti ya posho kulipa walimu laki moja
Uamuzi huo wa Zitto ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, umekuja huku taarifa za utafiti wa taasisi ya Policy Forum inayojihusisha na tafiti mbalimbali za sera zikionyesha kuwa, katika mwaka 2008/2009, Serikali katika bajeti yake ilitenga Sh506 bilioni kwa ajili ya malipo ya posho.
Kwa mujibu wa utafiti huo, ambao taarifa yake ilitolewa mwaka uliopita, fedha hizo ni sawa na mishahara ya mwaka mzima kwa walimu 109,000 ambao ni robo tatu ya walimu wote nchini.
Kwa mujibu wa utafiti huo mwaka 2009/10 kiasi cha fedha zilizotengwa kwa ajili ya posho za watumishi wa umma kilikuwa sawa na asilimia 59 ya malipo ya wafanyakazi wa ngazi ya chini .  
CHANZO: Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.