[Uchambuzi wa ACT Wazalendo Kuhusu Maeneo Kumi (10) Muhimu Kwenye Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa Mwaka wa Fedha wa 2017/18].
- Ikulu Yatumika Kuficha Ukaguzi wa Manunuzi ya Ndege
- Bilioni 800 Hazikutolewa kwa Ukaguzi
- Trilioni 4.8 Zimetumika Bila Kupita Mfuko Mkuu wa Hazina
- Mikopo ya Ndani Yashindwa Kulipa Madeni Kikamilifu
- 40% ya Bajeti yategemea Mikopo na Misaada Kutoka Nje
Ndugu Wanahabari
A: Utangulizi
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Prof. Mussa Juma Assad ametoa taarifa yake ya Ukaguzi wa Mapato na Matumizi ya Fedha za Umma kwa mwaka wa fedha wa 2017/18. Licha ya changamoto mbalimbali zilizotokea kabla ya CAG kukamilisha wajibu wake huu wa kikatiba, taarifa hiyo sasa iko wazi kwa umma, baada ya kuwa imekabidhiwa rasmi bungeni.
Sisi ACT Wazalendo, tumeisoma, kuipitia na kuichambua taarifa husika, kwa lengo la kuitumia ili itusaidie kutimiza wajibu wetu wa kuisimamia Serikali kama chama mbadala nchini na kama Chama cha Upinzani Bungeni. Tunafurahi kupata fursa ya kuwa nanyi hapa ili kuzungumza na umma, kupitia nyinyi, juu ya maeneo Kumi (10) muhimu kwenye ripoti ya CAG kwa mwaka wa fedha wa 2017/18.
B: Maeneo Kumi (10) Muhimu Katika Ripoti ya CAG
1. Bajeti ya Serikali Sio Halisia, Mapato Yasiyokusanywa ni Tarakimu Mbili
Kwenye bajeti ya mwaka wa fedha wa 2016/17, ambayo ni bajeti ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Tano, mipango ya Serikali ilikuwa ni kukusanya shilingi 29.5 trilioni, kwa mujibu wa ripoti ya CAG ya 2016/17, kati ya fedha hizo, Serikali ilikusanya shilingi 25.3 trilioni. Na hivyo, kutokufikia lengo la makusanyo kwa 14.33%. Kwenye uchambuzi wetu wa mwaka jana tulieleza kuwa bajeti za Serikali si halisia.
Kwenye ripoti hii ya mwaka 2017/18, kwa mara nyengine, CAG amelithibitishia Taifa kuwa Serikali ya awamu ya tano inatunga Bajeti ambayo sio halisia. Katika Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha wa 2017/18 jumla ya shilingi 31.7 trilioni zilitarajiwa kukusanywa na zilipitishwa kutumika na Bunge. Hata hivyo, kwa mujibu wa ripoti hii ya CAG, Serikali iliweza kukusanya kutoka vyanzo vyake vyote shilingi 27.7 trilioni tu, na kutumia shilingi 26.9 trilioni. Hivyo ikikosa makusanyo kwa 12.66% na ikikosa matumizi kwa 15.2%.
Kwa miaka mitatu ya mwisho ya Serikali ya awamu ya nne, wastani wa lengo lisilofikiwa na Serikali katika ukusanyaji wa mapato ya Bajeti ni tarakimu moja, 6.3% tu, ambapo kwa mwaka 2013/14 lengo halikufikiwa kwa 9%, kwa mwaka 2014/15 nako lengo halikufikiwa kwa 4%, na kwa mwaka wa fedha wa 2015/16 lengo halikufikiwa kwa 6% tu.
Hii inadhihirisha Kwa mara nyengine tena kuwa Serikali ya Awamu ya Tano hutangaza viwango vikubwa vya Bajeti ili kufurahisha umma ilhali uhalisia ni kuwa Bajeti ni ndogo zaidi. Kwa miaka 2 mfululizo CAG ametuonyesha kuwa Serikali inashindwa kufikia makadirio ya Bajeti Kwa zaidi ya shilingi Trilioni 4 kutoka Bajeti inayopitishwa na Bunge.
2. 40% ya Bajeti Inategemea Misaada na Mikopo
Ripoti ya CAG imetuonyesha kuwa ndani ya miaka miwili ya Serikali ya awamu ya tano uwezo wetu wa kujitegemea kibajeti umezidi kuzorota. Kwa mwaka wa fedha wa 2016/17 nchi yetu ilijitegemea Kibajeti kwa 65% kwa mapato ya ndani ya nchi, na 35% iliyobaki ndiyo iliyotokana na mikopo pamoja na misaada ya Wahisani. Hali Hiyo ni tofauti kwa mwaka wa Fedha wa 2017/18, tumedidimia zaidi.
CAG ameonyesha katika uchambuzi wake kuwa, nanukuu “Uchambuzi unaonyesha kwamba bila Mikopo na misaada kutoka kwa wahisani wa maendeleo, makusanyo ya ndani ya nchi yetu yangeweza kugharamia matumizi yote ya Serikali kwa asilimia 60 tu” (Chanzo: Ripoti ya Ukaguzi-Serikali Kuu-2017/18: Ukurasa wa 89).
Hii inaonyesha kuwa Bajeti yetu ya Tanzania ni tegemezi kwa 40% tofauti na tunavyoelezwa na Serikali kila wakati kuwa nchi yetu inaondoa utegemezi kwenye bajeti. Kwa mwaka 2016/17 utegemezi wetu uliongezeka kwa 27%, na kwa mwaka 2017/18 utegemezi wetu umeongozeka kwa 22%.
CAG ameonyesha kuwa Serikali ilikusanya shilingi 27.7 trilioni tu (makusanyo yote, ikiwemo misaada na mikopo kutoka ndani na nje) kwa mwaka wa fedha wa 2017/18. Makusanyo ya ndani yakiwa ni shilingi 16.7 trilioni, sawa na 60% ya makusanyo yote, na kwamba matumizi ya kawaida yaliyofanyika mwaka huo ni shilingi 15.3 trilioni, ambayo ni sawa na asilimia 55% ya makusanyo yote lakini ni 93% ya mapato ya ndani. Utegemezi huu utaathiri sana nchi yetu kwani gharama za kulipia mikopo (riba) zitakuwa kubwa kuliko hata uwezo wetu wa kuongeza mapato ya ndani.
3. Shilingi 800 Bilioni Hazikutolewa kwa Ukaguzi
Katika Uchambuzi wetu wa mwaka jana tulionyesha kuwa 6% ya fedha zilizokuwa zimekusanywa na Serikali hazijulikani zilipokwenda. Hizi zilikuwa ni shilingi 1.5 trilioni ambazo mjadala wake ulichukua mwaka mzima. Hoja yetu hiyo ilipelekea kufanyika kwa uhakiki maalumu na CAG, na ambapo bado Serikali ilishindwa kuonyesha zilipokwenda fedha hizo, zaidi ya kudai kuwa ilihamishia Ikulu matumizi ya shilingi 976 bilioni kati ya hizo 1.5 trilioni bila kumpa CAG uthibitisho wa uhamishaji huo wala kuonyesha fedha hizo zimefumikaje huko Ikulu.
Katika ukaguzi wa CAG wa Bajeti ya mwaka 2017/18, ambayo ni Bajeti ya Pili ya Serikali ya awamu ya 5, ameonyesha kuwa katika Bajeti ya shilingi 31.7 trilioni iliyoidhinishwa na Bunge, Serikali iliweza kukusanya shilingi 27.7 trilioni tu kutoka kwenye vyanzo vyote vya kodi, vyanzo visivyo vya kodi, mikopo ya ndani na nje, na misaada ya wahisani na washirika wa maendeleo.
Serikali ilishindwa kukusanya kiasi cha shilingi 4 trilioni kama ilivyokuwa mwaka uliopita ingawa sasa ni sawa na 13% ya Bajeti yote ya mwaka 2016/17. Hata hivyo CAG anaonyesha kuwa shilingi 26.9 trilioni tu ndio zilitolewa kutoka Mfuko Mkuu wa Serikali na kwenda kutumika, hivyo shilingi 800 bilioni kati ya shilingi 27.7 trilioni zilizokusanywa kutokujulikana ziliko na hazikutolewa kwa ukaguzi.
4. Shilingi 4.8 Trilioni Zimetumika Bila Kupita Kwenye Mfuko Mkuu
Katika Ukurasa wa 91 wa ripoti yake yam waka wa fedha wa 2017/18, CAG anasema, nanukuu “Ikilinganishwa taarifa ya kutoa fedha (exchequer issue report) na taarifa ya Fedha zilizopokelewa na kuripotiwa katika taarifa za fedha za Mafungu husika pamoja na barua za kukiri mapokezi ya fedha kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, imebaini utofauti wa taarifa zilizoripotiwa…”.
CAG ameeleza kuwa tofauti hiyo imesababishwa na kutokuwepo kwa mifumo thabiti ya usuluhishi kati ya fedha zilizotolewa na hazina na fedha zilizotolewa na wahisani wa maendeleo moja kwa moja kwenye miradi ya maendeleo katika Wizara. Ni muhimu sana kusisitiza hapa kuwa kwa mujibu wa CAG kuna fedha shilingi trilioni 4.8 ambazo makusanyo yake hayakuingizwa mfuko mkuu wa Serikali (tazama uk 91 wa Taarifa, tanbihi namba 15).
Suala la udhaifu wa Mifumo Katika Hazina pia limeelezwa kwa kina Katika Taarifa ya CAG ya Uhakiki wa Tofauti ya shilingi 1.5 Trilioni Katika mwaka wa Fedha 2016/17. Bado udhaifu huu unaendelea na madhara yake Katika usimamizi wa Fedha za Umma ni makubwa sana.
5. Bilioni 678 za Mamlaka Nyengine Ziliporwa na Mlipaji Mkuu wa Serikali
Kwenye ripoti ya CAG ya 2017/18 imeonyeshwa kuwa bado Serikali inatumia fedha ambazo sio zake (ring fenced) kama ilivyoonyeshwa kwenye ripoti ya mwaka 2016/17. Kwa mwaka 2017/18 CAG amebaini jumla ya shilingi 678 bilioni zilizokusanywa na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kwa niaba ya taasisi nyengine hazikuhamishwa kwenda kwenye taasisi husika, na badala yake zilihamishiwa kwa Katibu Mkuu Hazina ambapo huko hazikuonekana kwenye ukaguzi kama sheria inavyotaka.
Fedha zilizoporwa na Hazina ni pamoja na shilingi 169 bilioni za Shirika la Reli, shilingi 168 bilioni za Wadau wa Korosho nchini na shilingi bilioni 16 za Wakala wa Umeme Vijijini (REA). CAG kwa mara nyengine tena amependekeza sheria iheshimiwa kuhusu matumizi ya fedha hizi za Taasisi mbalimbali. Kwenye ripoti ya CAG ya mwaka 2016/17 kiasi cha shilingi 2.2 trilioni za mamlaka mbalimbali nchini hazikurejeshwa kwenye mamlaka husika mara baada ya fedha hizo kukusanywa na TRA. Tabia hii ya kupora Fedha za Mamlaka nyengine licha ya Kwamba Fedha hizo zimewekwa kisheria na kikatiba inaua misingi ya matumizi bora ya Fedha za Umma.
Kwa Upande wa TRA Bado kuna changamoto kubwa ambazo zinahitaji kutatuliwa. Makusanyo yetu ya kodi Bado ni kidogo sana (tax yield) tukiwa wa mwisho Katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, uwiano wa makusanyo ukiwa ni 12% tu ya Pato la Taifa. Hii inatokana tax base kuwa ndogo na mifumo sio rafiki kwa walipa kodi. Inawezekana TRA huchukua Fedha za Taasisi kupeleka Hazina ili kuonyesha makusanyo zaidi ilhali hali sio hiyo. Serikali inapaswa kukaa na sekta Binafsi kujadili kwa unyoofu (honestly) njia bora ya kupanua wigo wa Kodi ili nchi iweze kujitegemea. Katika uchambuzi wetu tumeacha mambo Mengi ikiwemo upotevu mkubwa wa mizigo ya transit ambao CAG ameuonyesha.
6. Kushuka kwa Thamani ya Shilingi Kunakuza Zaidi Deni la Taifa
Ripoti ya CAG ya 2017/18 imetuonyesha kuwa Deni la Taifa (Deni la Serikali) limefikia shilingi 50 trilioni mpaka Juni 30, 2018 likiwa na ongezeka la shiingi 4.85 trilioni, sawa na 10% kutoka shilingi 46 trilioni za Juni 30, 2017, deni hili likikua kwa shilingi 9.8 trilioni kwa muda wa miaka miwili tu kutoka Juni 30, 2016 mpaka Juni 30, 2018. CAG ameeleza kwamba kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya fedha za kigeni kumechangia kuongezeka kwa Deni kwa 20% kwa mwaka wa fedha wa 2017/18 (ongezeko kubwa zaidi ukilinganisha na 9% za mwaka wa fedha wa 2016/17).
Hii inatokana na Deni letu la Nje kuwa kwenye Fedha za Kigeni na hivyo kuathirika sana kutokana na thamani ya shilingi kutetereka. Baada ya makosa ya kimaamuzi kwenye suala la Zao la Korosho, ni dhahiri kuwa Deni letu la Nje litaongezeka zaidi baada ya shilingi ya Tanzania kutetereka zaidi kwa kukosa Mapato ya Fedha za Kigeni. MAARIFA makubwa yanahitajika kuhami nchi kutokana na janga la Deni la Taifa.
7. Mikopo ya Ndani Yashindwa Kulipa Madeni Kikamilifu
Lakini pia CAG ameeleza kuwa sababu Kuu zaidi ya kukua kwa deni la Taifa ni kwa kuwa tunaendelea kukopa zaidi. Kwa miaka mitatu iliyopita kukopa zaidi kulichangia ukuaji wa deni letu kwa 70%, ambapo kwa mwaka 2016/17 ilikuwa juu zaidi na kufikia 88%.
Zaidi CAG ameonyesha pia kuwa tulikopa mikopo ya ndani ya shilingi 5.7 trilioni kwa mwaka 2017/18 ambayo pamoja na kuwa na athari mbaya kwenye mikopo ya sekta binafsi nchini (maana inapunguza fursa ya wafanyabiashara wetu kukopeshwa na taasisi za ndani za fedha), lakini pia mikopo hiyo imeshindwa kulipa riba za mwaka za shilingi 6.1 trilioni. Na hivyo ilibidi Serikali kutafuta shilingi 448 bilioni kutoka kwenye vyanzo vingine ili kuweza kulipa riba hizo.
Ripoti ya CAG imeeleza, nanukuu “Deni la Ndani halikuchangia kwenye miradi ya Maendeleo”. Hivyo tulikopa ndani ya nchi si kwaajili ya kufanya shughuli za maendeleo, bali kulipa deni la nyuma, na bado hata hiyo mikopo haikutosheleza ulipaji wa hayo madeni ya nyuma. Hali hii si afya kwa taifa letu.
Mfano kwa mwaka 2017/18 Kiwango cha kuhudumia Deni la nchi ni 108% ya fedha zilizopatikana kutoka kwenye mikopo ya ndani, na CAG ameonya kuwa jambo hilo lina athari kubwa. Ukurasa wa 141 wa Ripoti ya Ukaguzi wa Serikali Kuu CAG ameeleza, nanukuu “kuna uwezekano wa kuwa na madhara kwa uchumi (hali ya kuhudumia deni kwa 108%) isipotafutiwa ufumbuzi”.
CAG pia ameonyesha kuwa kasi ya kukua kwa mikopo ya nje ni 38%, hali ambayo inaongeza gharama za kuhudumia madeni. Na jambo baya zaidi ni kuwa tunakopa zaidi mikopo ya kibiashara. CAG ameshauri watunga sera kuwa na busara wakati wa kuchagua miradi ya kupewa fedha za mikopo ya kibiashara, akishauri maamuzi yazingatie uzalishaji wa miradi husika. Vinginevyo Bajeti ya Taifa itakwenda kuhudumia deni tu.
Kwenye eneo hilo la Deni la Taifa pia ripoti ya CAG imeonyesha kuwa kuna upotoshwaji mkubwa wa mapokezi ya mikopo kutokana na mapungufu ya udhibiti wa ndani. Pia CAG ameonyesha kuwa mifumo wa kutunza madeni ni kianalojia (ya kizamani), jambo ambalo linaathiri kumbukumbu za madeni.
8. Serikali Imeanza Kushindwa Kulipa Madeni (Defaulting)
Ripoti ya CAG imeonyesha kuwa Serikali imeshaanza kushindwa kulipa baadhi ya madeni yake (Defaulting). Tayari kuna fedha kiasi cha shilingi 212.7 bilioni Serikali imeshindwa kuzilipa kwa Benki Kuu nchini (BOT), zikiwa shilingi 199.79 bilioni ni riba ya nakisi ya Serikali, na shilingi 12.9 bilioni ni sehemu ya Serikali ya gharama za kudhibiti ukwasi kuanzia mwaka 2015/16 hadi 2017/18.
Serikali ilisaini Mkataba wa Makubaliano (MoU) na BOT, ambao unaitaka kulipa kila robo mwaka sehemu yake ya gharama ya kudhibiti ukwasi pindi hati ya madai inapotolewa. Ucheleweshwaji huu wa malipo utaongeza uwepo wa mali za BOT zisizo na tija, na ni dalili ya Serikali kushindwa majukumu yake kifedha.
9. Ikulu Yatumika Kuficha Ukaguzi wa Manunuzi ya Ndege
Hatujafanikiwa kuona Ukaguzi wa Manunuzi ya Ndege ikiwemo Ununuzi wa Ndege za Shirika la Ndege Nchini, ATCL ambao kwa sehemu umefanyika mwaka wa fedha 2016/17 na 2017/18.
Katika uchambuzi wetu wa ripoti ya CAG ya mwaka jana (ripoti ya mwaka wa fedha wa 2016/17) tuliwaeleza kuwa katika ripoti ile licha ya kuwa ni taarifa bora sana kwa maudhui na uchambuzi, kuna mambo muhimu kadhaa ambayo CAG aliyaacha. Na tukamtaka kwenye ripoti yake ya mwaka 2017/18 ayafanyie kazi, mojawapo ni ukaguzi wa Ununuzi wa Ndege Sita (6) zinazoendeshwa na Kampuni ya Ndege nchini, ATCL.
Mpaka sasa Serikali imeshatumia jumla ya Shilingi Trilioni1 kununua ndege sita (6) na katika makadirio ya Bajeti ya mwaka 2019/20 yanayoendelea sasa bungeni Serikali imeomba Bunge liidhinishe shilingi Bilioni 500 kwa ajili ya kulipia ndege mpya nyengine. Ufuatiliaji wetu umegundua kuwa Serikali imekuwa ikichukua Fedha za Umma kupitia Fungu 62 (Wizara ya Uchukuzi) na kufanya manunuzi ya ndege. Ndege hizo wanakabidhiwa Wakala wa Ndege za Serikali kama wamiliki na shirika la ATCL inakodishiwa ndege hizo kwa Mkataba maalumu (ambao haujawekwa wazi popote, hata kwa Bunge).
Tulitarajia kuwa ripoti hii ya CAG ya mwaka 2017/18 kwenye ukaguzi wa fungu Namba 62 tungeweza kuona ukaguzi wa manunuzi ya ndege hizi. Lakini Serikali kwa lengo la kuficha taarifa imeamua kuhamishia kwenye Ofisi ya Rais (fungu 20) Wakala wa Ndege za Serikali kupitia tangazo la Serikali namba 252 la Juni 2018.
Tumetafuta taarifa ya ukaguzi wa fedha hizo za umma zilizofanya manunuzi ya ndege bila mafanikio. Tunamwomba CAG;
- Afanye Ukaguzi Maalumu wa Fedha za Umma Shilingi Trilioni 1 zilizotumika kununua ndege.
- Afanye Ukaguzi wa usimamizi wa mkataba wa ukodishwaji wa ndege hizo kati ya Wakala wa ndege za Serikali na Shirika la Ndege la ATCL ili Watanzania wajue matumizi sahihi ya Fedha zao za Kodi.
Jambo hili ni muhimu sana, kwa sababu uzoefu unaonyesha kuwa kila jambo lenye harufu ya wizi au matumizi yenye mashaka basi Serikali huliamishia jambo hilo ikulu (Kwa kuwa inajua ukaguzi wake hautawekwa wazi). Hata kwenye fedha shilingi 1.5 trilioni ambazo tulizianisha kuwa hazijulikani ziliko kutokana na uchambuzi wetu wa ripoti ya CAG ya mwaka 2016/17, baada ya kuibana Serikali na kumtaka CAG afanye uchunguzi maalum, mwishowe Serikali ilihamishia Ikulu matumizi ya Shilingi 976 bilioni kati ya hizo shilingi 1.5 trilioni ili isihojiwe.
Mafungu mawili, Fungu 20 (Ofisi ya Rais Ikulu) na Fungu 30 (Sekretariati ya Baraza la Mawaziri) yanapaswa kumulikwa sana katika matumizi ya Fedha za Umma. Tumeona mwaka huu Serikali inaomba Bunge litenge shilingi Bilioni 302 kwa Fungu 30 kwa kile kinachoitwa ‘matumizi mbalimbali ya kitaifa’. Mwaka ujao, Mungu akituweka hai, tutafuatilia kwa kina kaguzi za mafungu Haya kwani inaonyesha ndimo inakuwa kichaka Cha kuficha Taarifa za namna Fedha za Umma zinatumika.
10. Hoja za Ukaguzi za Shilingi Bilioni 225 hazina majibu kabisa
Kwa ujumla, na kwa Serikali Kuu peke yake, Hoja zote za Ukaguzi zilizoibuliwa na CAG kwenye Hesabu za Mwaka 2017/18 ukiachana na hoja kubwa nilizoeleza hapo juu, zina thamani ya shilingi 225 bilioni kati ya Fedha zote zilizokusanywa kwenye mwaka wa Fedha husika. Hii inaonyesha kuwa bado Serikali haijaweza kufanyia kazi Hoja za CAG kwa wakati na kwamba mifumo ya Serikali bado inavujisha Fedha za Umma.
C: Mapendekezo ya ACT Wazalendo
Baada ya kusoma taarifa hiyo ya CAG na kuyaanisha maeneo Kumi (10) muhimu, sisi ACT Wazalendo tuna mapendekezo yafuatayo:
1. ACT Wazalendo tunawasihi Wabunge wote bila kujali vyama vyao kutekeleza wajibu wao wa kuisimamia Serikali. Wabunge wasipotekeleza wajibu wao huo basi nchi yetu itaangushwa na matumizi mabovu na ya kinyume na Sheria kama tulivyoaina kwenye Uchambuzi wetu.
2. Serikali iwe inatunga Bajeti Halisia ambayo inatekelezeka, tofauti na inavyofanya kwa miaka minne mfululilo sasa, ambapo inataja namba kubwa ambayo Bajeti husika huwa haipatikani kwa ukamilifu wake na hivyo kuathiri sana miradi ya Maendeleo ambayo inakuwa imepangiwa mafungu ya Fedha. Ni bora kuwa na Bajeti ndogo ambayo inatekelezwa badala ya kuwa na Bajeti kubwa ambayo haitekelezwi ipasavyo.
3. Serikali itazame upya utekelezaji wa Sera zake za kiuchumi kwani dalili zinadhihirisha kuwa Uchumi wetu unaanguka. Ikibidi Kuwe na Mjadala wa Kitaifa juu ya hali ya uchumi wa nchi yetu, mjadala huo usaidie kupata uhalisia wa hali mbaya ya uchumi wetu, mbinu za kuunasua, na mawazo ya kuinasua nchi kutoka kwenye utegemezi wa misaaada pamoja na mikopo inayoongeza ukuaji wa deni la Taifa.
4. Serikali ionyeshe ilipo shilingi 800 bilioni isiyoonekana matumizi yake katika ripoti ya CAG yam waka wa fedha 2017/18.
5. Serikali ileze ni kwa nini Fedha Jumla ya shilingi Trilioni 4.8 hazikupita kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina ili utolewaji wake uweze kufuata masharti ya Katiba na Sheria za nchi. Fedha hizi za Wafadhili zinaonekana Katika Vitabu vya Bajeti Lakini CAG hazioni kuingia mfuko Mkuu na hivyo kutoka kwake kunaweza kuwa ni kinyume Cha Sheria. Menejimenti ya Wizara ya Fedha na Mipango ihakikishe inafanya usuluhishi sahihi wa taarifa za fedha zilizotolewa kwa Wizara mbalimbali na fedha zilizopokelewa moja kwa moja na wahisani wa maendeleo katika miradi. Hazina ifanyiwe usafi maalumu ili kuhakikisha ‘credibility’ ya Taarifa zake.
6. Serikali izingatie Sheria na Katiba Kuhusu Fedha za Taasisi ambazo zimetengwa kisheria Lakini Hazina inazitumia bila kujali Sheria. Hazina ihakikishe inazirejesha kwa wenyewe Ada, Tozo na mapato hayo ambayo TRA ilikusanya kwa niaba ya Idara, Wakala na Taasisi nyengine.
7. Wabunge, kama sehemu ya wenye wajibu wa kutunga sera tunayo nafasi ya kuisimamia Serikali kwenye suala la kushuka kwa thamani ya shilingi, kwanza kwa kuwawajibisha wote waliosababisha sintofahamu ya zao la korosho ambalo kama tungeuza basi kungepatikana unafuu kwenye deni la Taifa.
8. Ili kudhibiti kasi ya ukuaji wa Deni la Taifa, haswa Deni la Nje, kutokana na kushuka kwa thamani ya shilingi yetu, tunapendekeza kuwa Serikali ifanye hedging ya Deni la Nje ili kuwa na uhakika wa thamani ya fedha itakayotumika muda wote kuhudumia Deni hilo. Serikali ya Awamu ya Tano imeonyesha kutegemea sana mikopo ya kibiashara kutoka Mabenki ya Nje na hivyo kuweka nchi kwenye hatari kubwa ya Mtego wa Madeni (Debt Trap). Hedging inaweza kusaidia kudhibiti kasi ya ukuaji wa Deni la Nje.
9. Tunamsihi ndugu Rais atambue kuwa njia ya bora ya kupambana na rushwa na ufisadi ni kuwezesha mifumo kufanya kazi. Mtu mmoja hawezi kamwe kuwa dawa ya ufisadi ulioota mizizi nchini kwetu. Ripoti za CAG na madudu yaliyoibuliwa kila kona inaonyesha dhahiri kuwa silaha ya uhakika ni kujenga Taasisi imara za Uwajibikaji ili kudhibiti Fedha za Umma. Miaka 4 aliyepo madarakani imethibitisha kuwa nguvu ya Mtu mmoja haitoshi kukomesha ubadhirifu bali Mifumo Imara.
Ni matarijio yetu kuwa Watanzania wataendelea kuisoma na kuichambua Taarifa ya CAG na kuwaomba Wabunge watimize wajibu wao wa kuisimamia Serikali ili kujibu hoja zote za Ukaguzi. Bila Bunge kutimiza wajibu wake ipasavyo mzunguko wa uwajibikaji unakuwa haufungi. Tumeona Katika Taarifa ya CAG kuwa Hoja hazijibiwi na hivyo hazifungwi na madhara yake ni kuwa kila mwaka hoja zinaongezeka tu.
Ahsanteni Sana.
Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Mbunge, Kigoma Mjini
Kiongozi wa Chama, ACT W
azalendo
Aprili 14, 2019
Dodoma