15 Sept 2011



Raia Mwema Ughaibuni
Rais Kikwete na ‘usanii’ wa Mahakama ya Kadhi!
Evarist Chahali
Uskochi
14 Sep 2011
Toleo na 203
NIANZE makala hii kwa kutoa salamu zangu za rambirambi kwa wafiwa waliopoteza ndugu na/au jamaa zao katika ajali ya boti ilivyotokea usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita kwenye Bahari ya Hindi kati ya Nungwi na Pemba.
Kwa mara nyingine tena Watanzania tunashuhudia wenzetu wakipoteza maisha katika ajali ambayo, kwa namna moja au nyingine, ingeweza kuepukika.
Japo hadi wakati naandaa makala hii hakujatolewa taarifa rasmi ya chanzo cha ajali hiyo, lakini kwa mujibu wa abiria walionusurika katika ajali hiyo inadaiwa kuwa chanzo inaweza kuwa boti husika kuelemewa na wingi wa abiria na mizigo.
Kwa nini ninasema ajali hiyo ingeweza kuepukika? Ni wazi kuwa laiti mamlaka zinazohusika zingeweka mbele uhai wa abiria na kuzingatia sheria zinazotawala usafiri wa majini, ni wazi kuwa chombo hicho cha usafiri kisingezidisha shehena zaidi ya uwezo wake.
Lakini kwa kuwa kipindi hiki ni cha maombolezo, naomba nisiingie kiundani zaidi kuhusu namna taifa linavyoweza kuepusha matukio ya kusikitisha kama hili kutokea tena. Kwa sasa tuelekeze nguvu zetu katika kuwasaidia majeruhi na kuwafariji wafiwa.
Nielekee kwenye dhima ya makala hii. Katika maadhimisho ya hivi karibuni ya sherehe za Idd, Rais Jakaya Kikwete alitoa hotuba iliyoelekea kuwagusa wengi ambapo, pamoja na mengine, alizungumzia suala la kurejesha (na si kuanzisha) Mahakama ya Kadhi.
Nasema kurejesha kwa vile mahakama hiyo ilikuwepo huko nyuma kabla ya kufutwa.Kwahiyo,iwapo itafanikiwa kuwepo tena itakuwa si kwa mara ya kwanza; bali mwendelezo tu wa ile iliyokuwepo awali.
Bila kuuma maneno, napenda kumwaga shutuma kwa Rais Kikwete mwenyewe kama sehemu ya tatizo la uanzishwaji wa mahakama hiyo. Ikumbukwe kuwa Chama cha Mapinduzi katika Ilani yake ya Uchaguzi ya mwaka 2005 kiliahidi kushughulikia uanzishwaji wa mahakama hiyo.
Kimsingi, hakukuwa na shinikizo lolote kwa chama hicho kuja na ahadi hiyo hewa, lakini baadaye kukatokea kurushiana mpira kati ya watendaji wa serikali na wale wa CCM.
Kama ambavyo Watanzania wengine ‘walivyoingizwa mkenge’ na ahadi hewa za kuletewa maisha bora (na badala yake kuishia kushuhudia maisha bora kwa mfisadi pekee),CCM ilitumia ahadi hiyo ya kurejesha Mahakama ya Kadhi kwa minajili tu ya kupata kura za Waislam.
Kwa bahati mbaya,Waislam hawakuibana CCM wakati huo kuhoji kwa undani namna ahadi hiyo ingetekelezwa. Kwa mfano, hawakujihangaisha kukibana chama hicho kiwape ratiba kamili ya utekelezaji wa ahadi hiyo.
Lakini haikuwachukua muda mrefu kubaini kuwa ahadi hiyo ilikuwa ni ‘changa la macho’ na ya kisiasa zaidi kuliko yenye nia ya kusikiliza kilio chao cha muda mrefu.
Binafsi, licha ya kuwa Mkristo, sina tatizo na uanzishwaji wa mahakama hiyo alimradi sheria na taratibu zikizingatiwa. Msimamo wangu huo unatokana na ukweli kwamba kihistoria huko nyuma hakukuwa na tatizo lolote lililotokana na uwepo wa mahakama hiyo.
Ni muhimu kwetu kutambua kuwa, kwa muda mrefu tofauti zetu za kidini zimefunikwa na Utanzania wetu; japokuwa baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakifanya kila wawezalo kupanda mbegu za udini kwa maslahi yao binafsi.
Siamini kabisa kuwa iwapo Mahakama ya Kadhi ikirejeshwa itawaathiri wasio Waislam kwa vile lengo kuu la chombo hicho ni kuwahudumiwa Waislam pekee.
Na jingine zuri ni kwamba mahakama hiyo inaweza kusaidia kupambana na maovu katika jamii; hususan suala la ufisadi.
Kwa nini ninamlaumu Kikwete kuhusu sakata hilo la Mahakama ya Kadhi? Licha ya utetezi wake wakati fulani kuwa si yeye aliyeandika Ilani ya Uchaguzi ya chama chake mwaka 2005, ukweli ni kwamba aliitumia ilani hiyo kugombea kura takriban nchi nzima.
Ni wazi kuwa aliona mahala fulani kwenye ilani hiyo ikieleza kwamba chama anachokitumikia na kukitumia kugombea urais kimeahidi jambo ambalo, kimsingi, yeye mwenyewe linamgusa (kwa maana naye ni Muislam).
Lakini katika ubabaishaji uliozoeleka wa wanasiasa wetu, ‘maji yalipozidi unga’, Kikwete alifikia hatua ya kudai aliyeanzisha wazo la kurejeshwa Mahakama ya Kadhi ni Augustine Mrema, na sio yeye (Kikwete).
Huku ni kukwepa wajibu; kwani hata kama wazo hilo lingekuwa kweli limeanzishwa na Mrema, lakini lina umuhimu kwa sehemu fulani ya jamii, basi, la msingi sio aliyenazisha wazo; bali kulitekeleza katika namna inayostahili.
Katika hotuba hiyo,Kikwete alizungumzia pia suala la udini na kuonya viongozi wa dini kutotumia nafasi zao kuchochea chokochoko za kidini.
Ninaamini wakati Kikwete anazungumza hayo, alikuwa anafahamu fika kuwa siasa sio jambo haramu kuingizwa kwenye dini; hasa ikizingatiwa michango ya dini katika harakati za uhuru wa nchi yetu.
Kauli za kuhamasisha kutenganisha dini na siasa hazina mashiko makubwa kwa vile hazina tofauti na kauli zilizokuwa zikitolewa na mkoloni kwa minajili ya kukwaza jitihada zetu za kupata uhuru.
Kwa wanaofahamu historia za mapambano ya ukombozi wetu kutoka himaya ya mkoloni, watakumbuka fika namna misikiti ilivyokuwa sehemu muhimu ya harakati hizo.
Mkoloni alijaribu kuharamisha dini kwenye siasa kwa vile alifahamu kuwa dini inagusa imani na inawaunganisha wanajamii/waumini kirahisi zaidi kufikia lengo wanalokusudia.
Wanasiasa wa zama za Kikwete wanarejea kauli kama hizo za mkoloni si kwa minajili ya hofu ya vurugu; bali kwa vile wanafahamu kuwa pindi wananchi watakapounganishwa na imani zao kupambana na siasa za kibabaishaji, basi, watawala watakuwa katika nafasi ileile iliyomkuta mkoloni enzi za kupigani uhuru.
Katika hotuba hiyo, Kikwete aliwataka viongozi wa dini kuhubiri amani ili kuepusha waumini wao kujihusisha na mambo yasiyokubalika. Kwa maana nyingine, alikuwa anawahamasisha kuhubiri dhidi ya maovu kama ufisadi na mengine yanayoshabihiana nayo.
Sasa, watumishi wa Mungu watawezaje kuepuka kuzungumzia siasa iwapo baadhi (kama si wengi) ya mafisadi, ni wanasiasa?
Naomba unielewe hapo.Utawezaje kuzungumzia mwanasoka, kwa mfano, pasipo kuzungumzia soka?
Kimsingi, Kikwete na wanasiasa wengi wa Tanzania wanapaswa kuwashukuru sana viongozi wa dini; kwani viongozi hao wamechangia sana kuwawezesha wanasiasa wasiofaa kuchaguliwa au kuendelea kuwepo madarakani.
Ni wazi Rais anakumbuka kuwa wakati anagombea urais kwa mara ya kwanza, baadhi ya viongozi wa dini walimtakasa na kudai yeye ni ‘chaguo la Mungu.’
Kwa nini basi hakuwakemea wakati huo kuwa wanachanganya dini na siasa? Lakini kibaya zaidi ni namna baadhi ya watu wa karibu wa timu ya kampeni ya Kikwete kwenye uchaguzi mkuu uliopita walivyofanya kila waliloweza kupandikiza mbegu za udini.
Kila aliyefuatilia kampeni hizo kwa makini atakumbuka namna mgombea wa tiketi ya urais kupitia CHADEMA, Dkt Willibrod Slaa ‘alivyochorwa’ taswira ya ‘mgombea wa Kanisa Katoliki’ huku baadhi ya vyombo vya habari vinavyomilikiwa na serikali vikidiriki kumwita padre licha ya ukweli kuwa Dk. Slaa hakuwa padre wakati huo.
Pamoja na lawama hizo kwa Kikwete, naungana naye mkono katika maelezo yake kwa Waislam kuwa adui wao katika azma yao ya kurejeshewa Mahakama ya Kadhi si kanisa au maaskofu.
Ni kweli kwamba kanisa na maaskofu wameonyesha hofu yao (si upinzani) pengine kwa kuwa kumekuwa na jitihada duni kwa Waislam wenyewe kukazani kwenye elimu ya uraia (kwa Waislam na wasio Waislam) kuhusu namna mahakama hiyo zitakavyofanya kazi.
Kama alivyosema Kikwete, Mahakama ya Kadhi haitashughulikia kesi za jinai, na hivyo wanaohofia adhabu za kukatwa mikono au kuuawa kwa mawe hawapaswi kuwa na hofu hiyo. Kinachohitajika hapo ni elimu ya kutosha kwa umma.
Nimalizie kwa kurejesha lawama tena kwa Kikwete; kwani japo aliwahakikishia Waislam kuwa kikwazo cha urejeshwaji wa Mahakama ya kadhi si Kanisa au maaskofu, hakuwaeleza ukweli kwamba kikwazo kikubwa ni walaghai wa CCM ambao mwaka 2005 walitoa ahadi hiyo kwa minajili ya kupata kura za Waislam pasipo dhamira ya dhati ya kushughulikia suala hilo.
Kabla ya kuahidi kuwa suala hilo linashughulikiwa, Kikwete alipaswa kuwaomba radhi Waislam kwa ‘usanii uliofanywa na CCM kuingiza hoja hiyo kwenye ilani yake ya uchaguzi mwaka 2005’ lakini hadi sasa imeendelea kuwa ahadi tu - kama zilivyo ahadi nyingine lukuki zinazoendelea kutolewa kila kukicha.

Wasomaji

200
Wasiliana


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.