5 Jan 2012


2012, mwaka wa chuki za kisiasa, kiuchumi

CCM, Upinzani ishara si njema
Nchi tajiri kuiyumbisha Tanzania
NIANZE makala hii ya kwanza kwa mwaka huu kwa kupigia mstari pointi mbili za msingi. Kwanza, kama nilivyokwishawahi kubainisha huko nyuma, katika kujiingiza kwenye fani ya uandishi magazetini, niliwahi kuwa na safu ya “unajimu wa kisanii” katika baadhi ya “magazeti pendwa” (jina la kistaarabu la magazeti ya udaku).
Ninauita unajimu wa kisanii kwa vile haukubeba ukweli wowote bali lengo lilikuwa kuburudisha tu. Kwa mfano, katika moja ya safu zangu nilibashiri yafuatayo:
Wiki hii itatawaliwa na mkosi utakaokuletea neema. Mwanao atagongwa na gari la ubalozi wa nchi moja tajiri. Usipaniki kwa vile mwanao atapona. Na hapo ndipo neema itakapokuangukia. Licha ya kugharamia matibabu ya mwanao, ubalozi huo utampatia viza ya kwenda kuishi katika nchi hiyo ya ahadi. Angalizo: usimkataze mwanao kucheza barabarani.”
Ni “upuuzi” wa aina hii ndio uliowasukuma rafiki zangu waliokuwa kwenye medani ya uandishi wa habari kunishauri kujikuta kwenye uandishi wa makala za “mambo ya msingi”, hoja yao kubwa ikiwa kama ninamudu kuandika “nyota za kisanii” na kuburudisha jamii, basi inawezekana nikaandika makala za masuala muhimu za kuelimisha, kukosoa na kuhabarisha.
Ushauri huo ndiyo kiini cha “kifo cha safu za unajimu za Ustaadh Bonge (jina nililojipachika kuendana na suala zima la ‘unajimu’ huo).”
Nimegusia suala la utabiri kwa vile makala hii inalenga kubashiri masuala na matukio mbalimbali katika mwaka huu mpya. Tofauti na unajimu wa Ustaadh  Bonge kwenye “magazeti pendwa” ya SanifuKasheshe na Komesha, utabiri huu ni makini na unazingatia mwenendo wa mambo katika mwaka uliopita, sambamba na ufahamu wangu wa kitaaluma na binafsi.
Pointi ya pili inawahusu watu wawili maarufu kwenye medani ya siasa za Marekani. Wa kwanza ni Profesa Larry Sabato, mwanasayansi ya siasa (political scientist), mchambuzi wa siasa na Mkurugenzi wa Kituo cha Siasa katika Chuo Kikuu cha Virginia.
Sabato ni maarufu kwa utabiri wake katika chaguzi kuu nchini Marekani. Tovuti yake ya Sabato’s Crystal Ball huchambua duru za siasa za nchi hiyo na kutabiri matokeo ya uchaguzi wa wawakilishi, maseneta na urais. Kinachosababisha msomi huyo na tovuti yake kuwa muhimu ni usahihi mkubwa wa utabiri husika.
Mtu mwingine ni Paul Begala, gwiji la mikakati ya siasa (political strategist) na mshauri wa zamani wa aliyekuwa Rais wa Marekani, Bill Clinton. Pamoja na mshiriki wake wa karibu James Carville, Begala ambaye pia ni Profesa wa utafiti (research professor) katika sera za umma (public policy) katika Chuo Kikuu cha Georgetown, waliwezesha ushindi wa Rais Clinton katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1992, sambamba na kumwezeshea ushindi wa maseneta kadhaa.
Nimewataja Sabato na Begala kwa sababu, kwanza, hao ni role models (mifano ya kuigwa) kwa upande wangu, na pili, wote ni mahiri katika utabiri wa siasa za Marekani, hususan kwenye chaguzi.
Sasa tuangalie utabiri wangu wa mwaka 2012, hususan kwenye medani ya siasa (za kimataifa na huko nyumbani-Tanzania) na maeneo mengine muhimu.
Nitagusia maeneo machache yenye umuhimu zaidi kwa vile ni vigumu kuzungumzia kila eneo la maisha katika makala moja.
Siasa za kimataifa
Tukianza na siasa za kimataifa, mwaka huu unatarajiwa kutawaliwa zaidi na kinyang’anyiro cha Uchaguzi Mkuu nchini Marekani, Rais Barack Obama atakuwa anajaribu kupata ridhaa ya kuongoza taifa hilo kubwa duniani kwa muhula wa pili.
Obama, Mmarekani mweusi wa kwanza kuwa rais wa nchi hiyo anatarajiwa kukumbana na upinzani mkali kutoka kwa mgombea wa chama cha Republican (ambaye hajafahamika hadi sasa).
Kwa kuzingatia uchambuzi wa watu mbalimbali na kwa kadiri ninavyofuatilia siasa za Marekani, dau (bet) langu ni ushindi “kiduchu” kwa Obama dhidi ya Mitt Romney, mgombea ninayetabiri atapitishwa na Republican (iwapo upepo wa kisiasa hautabadilika).
Turufu kubwa kwa Obama ni kupendwa (likeability) kwake dhidi ya mgombea mwingine yeyote. Hata hivyo, busara za siasa zinatanabaisha kwamba, mwanasiasa anayependwa lakini hamudu kazi yake vyema anaweza kung’olewa madarakani.
Lakini ili Obama ashinde inategemea sana mwenendo wa uchumi wa nchi hiyo ambao kwa sasa ni mbaya (japo si kosa la moja kwa moja kwa Rais huyo).
Obama aliingia madarakani huku Marekani ikiwa kwenye hali mbaya ya kiuchumi, na kwa namna fulani kuna mtizamo kuwa ingehitajika miujiza kwa yeye kuboresha uchumi huo katika kipindi cha miaka minne aliyokuwa madarakani.
Turufu nyingine kwa Obama ni kile kinachoweza kuiangamiza CCM mwaka 2015, yaani kukosekana kwa mwafaka wa jumla katika kumuunga mkono mgombea urais kwa tiketi ya Republican.
Hadi sasa, hakuna mwanasiasa miongoni mwa waliokwishajitokeza kuwania nafasi hiyo anayeonekana kuungwa mkono vya kutosha ndani na nje ya chama.
Na kwa vile urais si suala la majaribio, Obama anaweza kuwa salama zaidi kwa kigezo cha “jini likujualo” nikimaanisha angalau Wamarekani wanafahamu ubora na udhaifu wake kuliko kubahatisha kwa mgombea wasiyemjua kwa namna hiyo.
Naomba kusisitiza kuwa lolote linawezekana katika siasa. Iwapo hali ya uchumi wa Marekani itazidi kudhoofika, basi nafasi ya Obama kurejea Ikulu ya nchi hiyo itazidi kuwa finyu.
Ikumbukwe kuwa tofauti na huko nyumbani, wenzetu huku Magharibi hawapendi mambo ya ‘bora liende’ ni kwamba kama mtu ameshindwa kazi basi awajibishwe.
Kwa ufupi, utabiri mwingine kwenye duru za kimataifa ni uwezekano wa Marekani kuishambulia kijeshi Iran (hasa ikizingatiwa kuwa kufanya hivyo kutampa Obama nafasi nzuri ya kushinda uchaguzi utakaofanyika Novemba, mwaka huu).
Shambulizi hilo linaweza pia kuijumuisha Israel ambayo inaitazama Iran kama tishio kwa ustawi wake.
Jingine ni uwezekano wa kuanguka kwa utawala wa Rais Bashir al-Asad wa Syria, sambamba na uwezekano wa machafuko makubwa zaidi ya kidini Nigeria.
Hali ya uchumi wa dunia itaendelea kuwa fyongo huku nchi masikini kama Tanzania zikiguswa na domino effect (zahama) ya kinachojiri katika nchi wafadhili.
Ndani ya CCM
Kwa huko nyumbani (Tanzanaia), ninatabiri kuwa siasa zetu zitatawaliwa zaidi na kinyang’anyiro cha Uchaguzi Mkuu wa chama tawala, CCM.
Japo kila mmoja wetu angetamani kuona uozo, ubabaishaji na ufisadi uliotawala mwaka 2011 unapungua kama si kufutika kabisa, kwa bahati mbaya (au kwa makusudi) dalili zinaashiria kuwa wanasiasa wetu wakiwamo wa CCM, wapo madarakani kwa ajili ya maslahi yao, na hakuna njia mwafaka ya kudumisha nafasi zao zaidi ya kuwa na nyadhifa ndani ya chama.
Kwa hiyo, tutarajie kuona wanasiasa wa CCM wakipigana vikumbo kuhakikisha wao au wagombea wanaowaunga mkono wanashinda katika uchaguzi huo.
Ikumbukwe kuwa uchaguzi huo una umuhimu wa kipekee kwa wanasiasa wanaotamani urais kupitia CCM katika Uchaguzi Mkuu, 2015 kwa vile hiyo ni nafasi mwafaka kwao kutengeneza “timu ya ushindi.”
Wakati Uchaguzi Mkuu wa CCM usingepaswa kuwaathiri wananchi wengine wasioshabikia chama hicho, mfumo mbaya wa kiuongozi ambao, Serikali kuanzia ngazi ya taifa hadi wilaya inaendeshwa zaidi kisiasa (wakuu wa mikoa na wilaya kuteuliwa kutokana na ukada wa CCM, sambamba na wao kutumia muda mwingi kwenye shughuli za chama, bila kusahau malengo yao binafsi ya kisiasa), harakati za kusaka uongozi ndani ya chama tawala zinatarajiwa kuwaathiri Watanzania wote.
Viongozi wengi wa Serikali katika ngazi zote wanatarajiwa kutumia muda mwingi kujihusisha na uchaguzi huo kuliko kutekeleza majukumu yao kwa umma.
Kambi ya Upinzani
Kwa upande wa siasa za upinzani, kuna uwezekano mkubwa wa “vita ya wenyewe kwa wenyewe” na dalili ni dhahiri ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) na NCCR-Mageuzi, hasa baada ya vyama hivyo kumaliza mwaka 2011 kwa kutishiana na kufukuzana.
Wakati vita vya panzi vinapaswa kuwa sherehe kwa kunguru (kwa maana ya migogoro ndani ya CUF na NCCR kuwanufaisha CCM na CHADEMA), kuna uwezekano, CCM kunufaika zaidi kuliko CHADEMA.
Kimsingi, mwanasiasa wa upinzani akihamia CCM hawezi kukiyumbisha chama hicho katika namna ya akina John Shibuda alivyogeuka “maumivu” kwa CHADEMA.
Ili wasikumbwe na vurugu kama zinazoendelea kwa wenzao, CHADEMA wajiepushe kudaka kila “korokoro la kisiasa” linalowajia baada ya kufukuzwa au kunyimwa nafasi katika chama kingine.
Hali ya uchumi
Nimalizie kwa kutabiri hali ya uchumi na maisha kwa ujumla. Kwa kusikiliza hotuba ya mwisho wa mwaka ya Rais Jakaya Kikwete, ni dhahiri mwaka huu utaendelea kuwa mchungu kwa walalahoi.
Katika hotuba hiyo ya kisiasa, Kikwete hakujihangaisha kuwapa matumaini Watanzania kuwa anaelewa hali yao ngumu ya maisha (na akatoa takwimu za kukua kwa uchumi), akikwepa kuzungumzia wimbi la ufisadi.
Japokuwa aligusia tatizo la uhalifu ambalo anadai limepungua, lakini inaelekea kwake ufisadi si uhalifu na ndiyo maana aliwahi kutetea haki za binadamu za mafisadi.
Haihitaji upeo wa akina Sabato au Begala kubashiri kuwa tutaendelea kushuhudia mafisadi wakigeuza nchi yetu kuendelea kuwa shamba la bibi, huku Rais akiendeleza huruma kwa watuhumiwa wa ufisadi (na alihitimisha mwaka 2011 kwa picha yenye tabasamu akiwa na Katibu Mkuu (mstaafu) Philemon Luhanjo, ambaye dalili zinaashiria ameruhusiwa kustaafu kwa heshima - kama ilivyokuwa kwa aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika, licha ya kudaiwa kuhusika kwenye tuhuma za ufisadi). Kila la heri kwa mwaka huu mpya 2012.


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.