31 Aug 2012


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimemshukia Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, kikisema kiongozi huyo si mwadilifu, si mwaminifu na mnafiki, akiwa ni mwakilishi na kielelezo cha mfumo uliooza katika serikali ya CCM uliolifikisha taifa hapa lilipo.
Kimesema kuwa tabia za Sitta hasa katika kuua mijadala ya kifisadi ndani ya bunge, kwa ajili ya kulinda maslahi yake binafsi ya kusaka vyeo, inamfanya asiwe tofauti na watuhumiwa wengine wa ufisadi ndani ya chama chake na serikalini, kikishutumu kuwa mlinda ufisadi na mafisadi ama ni naye ni fisadi kama wenzake au ni fisadi mkubwa kuliko mafisadi wenyewe.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Iringa jana Ijumaa, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Willibroad Slaa alisema kuwa Sitta hana uwezo wowote wa kukisema chama hicho wala viongozi wake, akimtaka amalize kwanza matatizo waliyonayo yeye na wenzake ndani ya CCM, likiwemo la kujivua gamba, ambalo linaonekana kuwashinda.

Katika mkutano huo chama hicho kilisema pia kuwa hatua ya polisi kuzuia mikutano ya Operesheni Sangara-M4C kwa siku tano, kupisha shughuli ya sensa, kumekisaidia chama hicho kugundua mbinu na mikakati mizuri ya kuwafikia wananchi kwa mikutano ya ndani, ikiwa ni maandalizi ya mikutano ya hadhara, hivyo kupata mafanikio zaidi mkoani Iringa kuliko ilivyokuwa mkoani Morogoro.

Sitta ni kielelezo

Katibu Mkuu huyo wa CHADEMA ambaye aliwaambia waandishi wa habari kuwa amelazimika kumzungumzia mtu lakini kwa nia ya kuonesha alivyo kielelezo cha ubovu wa mfumo na uongozi wa serikali na CCM, alidai kuwa kwa sababu ya tabia ya unafiki aliyonayo Sitta, kiongozi huyo ni sawa na viongozi wengi wa serikali ya CCM akiwafafanisha na mbwa mwitu waliovaa ngozi ya kondoo.

“Nchi hii imefika hapa ilipo kwa sababu ya viongozi aina ya Sitta ambao hawasiti kusema uongo hadharani, wanafiki, hawana uadilifu, waongo, walio tayari kusaliti maslahi ya umma kulinda maslahi ya tumbo, Sitta yeye ana uzoefu gani, huu wa kulinda mafisadi bungeni kwa kupindisha hoja za ufisadi ili apate ubunge na uspika.

“Hivi Sitta atuambie anaposema CHADEMA haina watu wenye uwezo lini tuliwahi kusema tukiingia serikalini tutakuja na watu wetu wote au ndiyo yale mawazo ya kijinga kwamba CHADEMA wakishika nchi watapata wapi ikulu…atuambie kuna chuo kikuu chochote kinafundisha uwaziri au kuna chuo kikuu kinafundisha ukatibu mkuu wa wizara, asitupangie sisi namna ya kupata viongozi wetu.

“Hivi hajui kuwa Mwalimu alipopata nchi aliandaa watendaji. Hoja za kipuuzi, mtu akitoa hoja za kipuuzi, naye atakuwa mpuuzi tu wa kupuuzwa, tumefika hapa, nchi imegubikwa na uozo wa ufisadi kwa sababu ya mawaziri wa aina ya Sitta ambaye haogopi kuropoka hadharani, tena akiwatukana wapiga kura, ambao pia wengi wao ni vijana.

Hoja ya kuchezesha disko

“Anaposema Mbowe ni mchezesha disko anataka kupeleka ujumbe gani, anataka kusema nini…kwamba ni kosa, kwa hiyo anamaanisha wacheza disko ni criminals (watenda jinai), kwa hiyo wacheza disko ambao pia ni wapiga kura na wengi ni vijana ni criminals, je hajui kuwa kuna mawaziri wenzake wanaokesha pale Billicanas Club,” alisema Dkt. Slaa.

Aliongeza kusema kuwa hoja hiyo ya kumshambulia Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe kwa sababu ya kumiliki ukumbi wa mziki, kuwa nayo ni hoja mbele ya watu makini, Dkt. Slaa alisema waziri huyo amedhihirisha alivyo mbumbumbu wa sheria na hajui lolote, tofauti na ambavyo siku zote ametaka kuonekana mbele ya jamii.

“Ni dhahiri hana uzoefu wowote na hajui, ndiyo maana ameishia kwenda kuwatukana wapiga kura yeye akifikiri anaimaliza CHADEMA, maana wacheza disko ndiyo wapiga kura hao hao, lakini yeye kama msomi kweli, tena anasema ni mwanasheria, alipaswa aelewe kuwa duniani kuna nyumba za disko za staha, zimesajiliwa na zinafanya kazi kwa mujibu wa sheria na zimepewa leseni na serikali.

“Huyu Sitta kila siku anajiita yeye mwanasheria kumbe mbumbumbu kupindukia tu hana tofauti na wana CCM wenzake ambao jamii inawashangaa kwa matendo na kauli zao, ku-run club ni sawa na ku-run biashara nyingine yoyote, almuradi iendeshwe kisheria na kihalali, sasa kama anaona ni kosa aiambie serikali yake ifute leseni ya biashara hizo.

“Tulitegemea mtu ambaye anataka kuonekana ni mstaarabu, anahoji uzoefu wa wenzake nay eye anasema ana uzoefu angekuja na mawazo ya kupeleka nchi mbele kumbe yuko sawasawa tu na wenzake ndani ya CCM,” alisema Dkt. Slaa.

Ameingia kichwakichwa, kwenye tope

“Leo nalazimika kumzungumzia mtu, Watanzania wanajua mara chache sana CHADEMA huwa tunalazimika kuzungumzia watu badala ya masuala…lakini nitazungumza kwa namna ambayo huyo mtu atakuwa anawakilisha mfumo huu wa serikali ya CCM na chama chao jinsi ulivyooza na kutufikisha Watanzania hapa tulipo.

“Samuel Sitta ameingia kichwa kichwa kwenye matope ambayo hawezi kutoka wala kujinasua, muda mrefu tumemhifadhi lakini leo tutampiga ngumi za uso lakini kwa namna ambayo atakuwa anawakilisha mfumo huu uliooza…

“Ghafla tu ameamua kuibuka na kuzingumzia CHADEMA, badala ya kujenga chama chake, bila kujua amedhihirisha kuwa CHADEMA sasa ni tishio kwao, maana huwezi kuzungumzia kitu ambacho hakikuathiri, amedhihirisha namna ambavyo yeye wenzake sasa wanatapatapa kweli kwa sababu ya CHADEMA.”

Makombora zaidi; mlinda ufisadi na mafisadi

Dkt. Slaa alisema kuwa wakati chama hicho kilipoanza kuasisi hoja ya ufisadi nchini kikiwa mstari wa mbele kupiga vita kila aina ya ufisadi, Sitta wakati huo akiwa Spika wa Bunge, ndiye alikuwa mtu wa kwanza kuweka vikwanzo na vizingiti akilinda maslahi yake nay ale ya chama chake, badala ya maslahi ya wananchi.


“Yeye ndiye aliyepindisha hoja ya Zitto katika kashfa ya Buzwagi ambapo waziri alikuwa amesaini mkataba uliokuwa kinyume kabisa na maslahi ya nchi, tena akasaini nje ya nchi hotelini. Zitto aliposimama bungeni, Sitta badala ya kuangalia hoja hiyo kwa maslahi ya nchi, yeye na wenzake akaipindua kuwa Zitto amesema uongo bungeni.

“Huyu bwana hastahili hata kuwa waziri, anajidai yeye mpiganaji na mpambanaji, wapi? Katika hoja ile nani alikuwa mpiganaji Zitto au Sitta, akapindisha makusudi hoja ya ufisadi mkubwa wa Buzwagi kulinda maslahi anayoyajua mwenyewe. Wakamfukuza Zitto bungeni kwa miezi minne, baadae kelele zilivyozidi huku nje, wakaamua kumrejesha bungeni kimya kimya baada ya mwezi mmoja tu hivi.

“Lakini pia ni Sitta huyu huyu alizima hoja ya ufisadi wa BoT, mambo yote yale ya EPA, Kagoda, Deep Green sijui nini kila kitu kilichokuwa kikihusu BoT. Mtakumbuka aliwatangazia Watanzania kuwa nyaraka za Dokta Slaa ni fake za kuokoteza kwenye internet na nitampeleka polisi, mpaka leo hakunipeleka. Lakini Sitta alikuwa anajua tangu mwanzo, kadri nilivyokuwa nikikusanya documents alikuwa anajua na nampatia copy, mpaka ikafikia ile document kubwa ya mwisho.

“Lakini kwa unafiki wake ameahirisha bunge Ijumaa, Jumamosi akachukua ile document na kwenda nazo TBC akisema ni fake na atanipeleka polisi, lakini leo yako wapi…sasa mtu wa namna hii hafai hata kuwa naibu waziri, mtu yeyote anayelinda mafisadi na ufisadi ni fisadi kuliko mafisadi wenyewe, nawaambia haya kwa sababu tumefika hapa kwa sababu ya kuwa na viongozi, wakiwemo mawaziri wanafiki na waongo kama hawa.

“Lakini ili mjue Sitta ni mtu wa aina gani na kwamba hastahili kuaminika na Watanzania, haikuishia hapo, ufisadi wa Richmond mnajua alivyomaliza mjadala ule kihuni bungeni. Hadi leo hoja ile haina majibu, wakati tunahoji bungeni akafunga hoja ile kidikteta, sasa tunauliza huo ndiyo uzoefu alionao yeye au walionao wenzake, uzoefu wa kulinda mafisadi na ufisadi wa CCM na serikali yao, lakini sisi tunajua kwa nini alipindisha hoja ya Richmond, wakati huo alikuwa anabembeleza ili ateuliwe kuwania ubunge na baadae uspika, mnaona huyu ni mtu wa kuaminika kweli?”

“Hivi kwa matendo ya aina hii Sitta anaweza kutoka nje na kusema yeye ni jasiri na mzalendo, katika majasiri na wazalendo wa kweli Sitta hana sifa hizo, ndiyo maana wameshindwa hata kuyavua magamba kama walivyosema, sasa aende kwanza kwenye chama chake na serikalini, asaidie kuyaondoa magamba kabla hajaanza kutafuta aibu ya kuanikwa zaidi,” alisema Dkt. Slaa.

Siri zaidi; Sitta haaminiki

Dkt. Slaa aliongeza kusema kwa kutoboa siri zaidi namna ambavyo, yeye na Mwenyekiti wa CHADEMA Mbowe, walikuwa wakiendesha mazungumzo na Sitta wakati mwingine kwenye Ofisi ya Spika juu ya Sitta kuhamia CHADEMA na kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, akisema kuwa ulikuwa ni wakati ambapo waziri huyo pamoja na wenzake walipokuwa wameunda Chama Cha Jamii (CCJ) wakiwa bado wako CCM.

Alisema kuwa hata wakati huo bado Sitta alikuwa akionekana kutojiamini na maamuzi yake, ambapo wakati wa majadiliano ya kugombea urais, Sitta alisema kuwa kuna kundi la wabunge takriban 55 watiifu kwake ambao walikuwa tayari kuhama naye kumfuata CHADEMA. 

“Leo natoa siri ambayo sijawahi kuitoa, Sitta ni mhanini. Tumekutana naye mara 100 na zaidi, tumeandikiana vimemo bungeni vya kukutana, wakati mwingine tumekutana hata Speaker’s lounge, tumekutana na Sitta na Mwenyekiti Mbowe, ambaye leo anamwita ni mchezesha disko mara nyingi tu. Lakini hata wakati huo pia hakuonekana kuwa jasiri, maana alikuwa ana wasiwasi nani wanamfuatilia au nani wanamuona, si mtu jasiri hivyo. 

“Zikiwa zimebaki kama siku tano kabla ya kumaliza bunge la mwezi wa saba, kila nikimwandikia kimemo, hataki hata kunitazama, Sitta akayeyuka bila hata kutuaga, baadae CHADEMA tukaamua kutumia utaratibu mwingine na tukaweza kusonga mbele mpaka kufika pale tulipofika. Lakini baada ya uchaguzi akaja mwenyewe kunifuata akinishukuru sana na kunipongeza kuwa nilikuja na hoja tofauti kwenye uchaguzi akisema hata yeye asingeweza kufika tulipofika.

“Lakini hapo sasa tulishamshtukia na kugundua kuwa anataka kugombea uspika kupitia CHADEMA, nataka kuonesha namna huyu mtu alivyo mnafiki, mpotoshaji, nampatia challenge kama kweli yeye ni muumini mzuri akanushe haya, maana ametulazimisha kusema, kwa hoja zake za kupotosha watu na akumbuke, maana huwa anakwenda makanisani na anachanga mapesa, akumbuke maandiko yanasema, yeyote atakayepotosha wadogo hawa, anastahili kutoswa baharini, Makamu Mwenyekiti hapa ametumia Quran kufafanua vizuri,” alisema Dkt. Slaa.

“Maana kwa hakika anataka kupotosha watu ili waone kuwa kuchezesha disko ni suala lisilokuwa sahihi, huo ni upotoshaji, kama anataka kuonesha si sahihi mbona serikali yake hiyo hiyo inaendelea kukusanya kodi. Sasa ilipofikia kwenye suala la kugombea uspika, siku ile jina lake limekatwa kwa sababu walitaka mgombea mwanamke, alinipigia simu usiku wa saa tisa, bahati mbaya nilikuwa nimeweka simu silence, hakunipata.

“Saa 12 nikapokea simu ya mke wake, Margreth Sitta, anasema baba anakutafuta tangu usiku, anataka kuzungumza nawe, nikasema sawa, akaniambia Dokta Slaa wamenifanyia kitu kibaya sana, mimi nimeamua sasa nitagombea uspika kwa tiketi ya CHADEMA, najua umeshateua tayari mtu wa kugombea tayari, lakini naomba nikuhakikishie nafanya press conference saa 4 asubuhi leo, natangaza rasmi kugombea uspika kupitia CHADEMA. Nikamjibu CHADEMA maamuzi hayafanywi na mtu mmoja, nikamwambia asubiri niwasiliane na Mwenyekiti wangu wa chama.

“Baadae tukakubaliana tukutane nyumbani kwake, lakini akawa anasema tusubiri kwanza anamalizia kupanga mikakati na wabunge 55 wa CCM, lakini akisisitiza kuwa uamuzi wake uko pale pale, nikamuuliza vipi kuhusu press conference mbona muda unakaribia, akasema hakuna shida yeye atatuma tu watu wake wataitisha haraka, akasema lakini wanataka kumpatia unaibu waziri, hivyo bado anasumbuana nao, kengele ikalia kichwani sasa huyu mtu akipewa uwaziri itakuwaje.

“Baadae ananiambia, Dokta Slaa nimepigiwa simu na bwana mkubwa naenda kuonana naye, tangu wakati huo Sitta akapotea mpaka saa 8 ndiyo anapatikana, akaanza kuniambia ni lazima aende kwanza Urambo kuwaaga wazee, maana hawezi kuhama bila baraka zao, nikamuuliza vipi kuhusu press conference akasema tutaifanya Jumatatu ijayo Dar es Salaam, akaniambia; tena saa 9 uje uone statement ambayo nimeshaiandika ili na wewe uongeze inputs, Sitta huyu akaniambia kuwa Anne Makinda hatakaa zaidi ya miezi sita kwenye kiti cha uspika.”

Dkt. Slaa alisisitiza akisema kuwa nchi imefika hapa ilipo ikiwa imegubikwa na uozo wa ufisadi kila kona, ukiongeza idadi ya maadui wa taifa, kutoka watatu hadi wanne (umaskini, ujinga, maradhi na ufisadi/CCM) kuanzia ngazi ya chini hadi juu, kwa sababu ya ukosefu wa uadilifu, uaminifu kama Waziri Sitta.

Atalipuliwa zaidi


Dkt. Slaa alisema kuwa ameamua kuzungumza hayo machache kwa sasa, lakini ataongeza ‘kumlipua’ zaidi Sitta endapo atajitokeza kujibu haya ya sasa.

“Yeye ana uzoefu gani Sitta, hana uadilifu, si mwaminifu, nchi hii imeoza kwa sababu ya viongozi ya aina ya Sitta, nataka ajibu kwanza hayo kisha nitamlipua zaidi. Ana uadilifu gani katika nchi hii, ametumia mabilioni ya hela ya walipa kodi wa Tanzania kujijengea Ofisi ya Spika Urambo, tunauliza kuna spika wa Urambo au alijua yeye atakuwa spika wa milele au basi Makinda awe anakwenda Urambo wakati wa mapumziko ya bunge.
“Tulichoamua bungeni ni kwamba kila mbunge ajengewe ofisi yenye thamani isiyozidi milioni 40, lakini yeye akaenda kujijengea ofisi ya milioni 350 tena kwa kasma tofauti na inavyotakiwa lakini kibaya zaidi tendering process ya vifaa vya ofisi haikufutwa na vililetwa na kampuni ambayo majuzi imehusishwa na Blandina Nyoni, hakuna mahali tendering imefanyika, amefanyia ufisadi mali ya taifa,” alisema Dkt. Slaa.


More still to come about the press conference...


CHANZO: Afisa Habari wa Chadema TUMAINI MAKENE

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.