Showing posts with label POLITICAL CONMANSHIP. Show all posts
Showing posts with label POLITICAL CONMANSHIP. Show all posts

31 Aug 2012


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimemshukia Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, kikisema kiongozi huyo si mwadilifu, si mwaminifu na mnafiki, akiwa ni mwakilishi na kielelezo cha mfumo uliooza katika serikali ya CCM uliolifikisha taifa hapa lilipo.
Kimesema kuwa tabia za Sitta hasa katika kuua mijadala ya kifisadi ndani ya bunge, kwa ajili ya kulinda maslahi yake binafsi ya kusaka vyeo, inamfanya asiwe tofauti na watuhumiwa wengine wa ufisadi ndani ya chama chake na serikalini, kikishutumu kuwa mlinda ufisadi na mafisadi ama ni naye ni fisadi kama wenzake au ni fisadi mkubwa kuliko mafisadi wenyewe.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Iringa jana Ijumaa, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Willibroad Slaa alisema kuwa Sitta hana uwezo wowote wa kukisema chama hicho wala viongozi wake, akimtaka amalize kwanza matatizo waliyonayo yeye na wenzake ndani ya CCM, likiwemo la kujivua gamba, ambalo linaonekana kuwashinda.

Katika mkutano huo chama hicho kilisema pia kuwa hatua ya polisi kuzuia mikutano ya Operesheni Sangara-M4C kwa siku tano, kupisha shughuli ya sensa, kumekisaidia chama hicho kugundua mbinu na mikakati mizuri ya kuwafikia wananchi kwa mikutano ya ndani, ikiwa ni maandalizi ya mikutano ya hadhara, hivyo kupata mafanikio zaidi mkoani Iringa kuliko ilivyokuwa mkoani Morogoro.

Sitta ni kielelezo

Katibu Mkuu huyo wa CHADEMA ambaye aliwaambia waandishi wa habari kuwa amelazimika kumzungumzia mtu lakini kwa nia ya kuonesha alivyo kielelezo cha ubovu wa mfumo na uongozi wa serikali na CCM, alidai kuwa kwa sababu ya tabia ya unafiki aliyonayo Sitta, kiongozi huyo ni sawa na viongozi wengi wa serikali ya CCM akiwafafanisha na mbwa mwitu waliovaa ngozi ya kondoo.

“Nchi hii imefika hapa ilipo kwa sababu ya viongozi aina ya Sitta ambao hawasiti kusema uongo hadharani, wanafiki, hawana uadilifu, waongo, walio tayari kusaliti maslahi ya umma kulinda maslahi ya tumbo, Sitta yeye ana uzoefu gani, huu wa kulinda mafisadi bungeni kwa kupindisha hoja za ufisadi ili apate ubunge na uspika.

“Hivi Sitta atuambie anaposema CHADEMA haina watu wenye uwezo lini tuliwahi kusema tukiingia serikalini tutakuja na watu wetu wote au ndiyo yale mawazo ya kijinga kwamba CHADEMA wakishika nchi watapata wapi ikulu…atuambie kuna chuo kikuu chochote kinafundisha uwaziri au kuna chuo kikuu kinafundisha ukatibu mkuu wa wizara, asitupangie sisi namna ya kupata viongozi wetu.

“Hivi hajui kuwa Mwalimu alipopata nchi aliandaa watendaji. Hoja za kipuuzi, mtu akitoa hoja za kipuuzi, naye atakuwa mpuuzi tu wa kupuuzwa, tumefika hapa, nchi imegubikwa na uozo wa ufisadi kwa sababu ya mawaziri wa aina ya Sitta ambaye haogopi kuropoka hadharani, tena akiwatukana wapiga kura, ambao pia wengi wao ni vijana.

Hoja ya kuchezesha disko

“Anaposema Mbowe ni mchezesha disko anataka kupeleka ujumbe gani, anataka kusema nini…kwamba ni kosa, kwa hiyo anamaanisha wacheza disko ni criminals (watenda jinai), kwa hiyo wacheza disko ambao pia ni wapiga kura na wengi ni vijana ni criminals, je hajui kuwa kuna mawaziri wenzake wanaokesha pale Billicanas Club,” alisema Dkt. Slaa.

Aliongeza kusema kuwa hoja hiyo ya kumshambulia Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe kwa sababu ya kumiliki ukumbi wa mziki, kuwa nayo ni hoja mbele ya watu makini, Dkt. Slaa alisema waziri huyo amedhihirisha alivyo mbumbumbu wa sheria na hajui lolote, tofauti na ambavyo siku zote ametaka kuonekana mbele ya jamii.

“Ni dhahiri hana uzoefu wowote na hajui, ndiyo maana ameishia kwenda kuwatukana wapiga kura yeye akifikiri anaimaliza CHADEMA, maana wacheza disko ndiyo wapiga kura hao hao, lakini yeye kama msomi kweli, tena anasema ni mwanasheria, alipaswa aelewe kuwa duniani kuna nyumba za disko za staha, zimesajiliwa na zinafanya kazi kwa mujibu wa sheria na zimepewa leseni na serikali.

“Huyu Sitta kila siku anajiita yeye mwanasheria kumbe mbumbumbu kupindukia tu hana tofauti na wana CCM wenzake ambao jamii inawashangaa kwa matendo na kauli zao, ku-run club ni sawa na ku-run biashara nyingine yoyote, almuradi iendeshwe kisheria na kihalali, sasa kama anaona ni kosa aiambie serikali yake ifute leseni ya biashara hizo.

“Tulitegemea mtu ambaye anataka kuonekana ni mstaarabu, anahoji uzoefu wa wenzake nay eye anasema ana uzoefu angekuja na mawazo ya kupeleka nchi mbele kumbe yuko sawasawa tu na wenzake ndani ya CCM,” alisema Dkt. Slaa.

Ameingia kichwakichwa, kwenye tope

“Leo nalazimika kumzungumzia mtu, Watanzania wanajua mara chache sana CHADEMA huwa tunalazimika kuzungumzia watu badala ya masuala…lakini nitazungumza kwa namna ambayo huyo mtu atakuwa anawakilisha mfumo huu wa serikali ya CCM na chama chao jinsi ulivyooza na kutufikisha Watanzania hapa tulipo.

“Samuel Sitta ameingia kichwa kichwa kwenye matope ambayo hawezi kutoka wala kujinasua, muda mrefu tumemhifadhi lakini leo tutampiga ngumi za uso lakini kwa namna ambayo atakuwa anawakilisha mfumo huu uliooza…

“Ghafla tu ameamua kuibuka na kuzingumzia CHADEMA, badala ya kujenga chama chake, bila kujua amedhihirisha kuwa CHADEMA sasa ni tishio kwao, maana huwezi kuzungumzia kitu ambacho hakikuathiri, amedhihirisha namna ambavyo yeye wenzake sasa wanatapatapa kweli kwa sababu ya CHADEMA.”

Makombora zaidi; mlinda ufisadi na mafisadi

Dkt. Slaa alisema kuwa wakati chama hicho kilipoanza kuasisi hoja ya ufisadi nchini kikiwa mstari wa mbele kupiga vita kila aina ya ufisadi, Sitta wakati huo akiwa Spika wa Bunge, ndiye alikuwa mtu wa kwanza kuweka vikwanzo na vizingiti akilinda maslahi yake nay ale ya chama chake, badala ya maslahi ya wananchi.


“Yeye ndiye aliyepindisha hoja ya Zitto katika kashfa ya Buzwagi ambapo waziri alikuwa amesaini mkataba uliokuwa kinyume kabisa na maslahi ya nchi, tena akasaini nje ya nchi hotelini. Zitto aliposimama bungeni, Sitta badala ya kuangalia hoja hiyo kwa maslahi ya nchi, yeye na wenzake akaipindua kuwa Zitto amesema uongo bungeni.

“Huyu bwana hastahili hata kuwa waziri, anajidai yeye mpiganaji na mpambanaji, wapi? Katika hoja ile nani alikuwa mpiganaji Zitto au Sitta, akapindisha makusudi hoja ya ufisadi mkubwa wa Buzwagi kulinda maslahi anayoyajua mwenyewe. Wakamfukuza Zitto bungeni kwa miezi minne, baadae kelele zilivyozidi huku nje, wakaamua kumrejesha bungeni kimya kimya baada ya mwezi mmoja tu hivi.

“Lakini pia ni Sitta huyu huyu alizima hoja ya ufisadi wa BoT, mambo yote yale ya EPA, Kagoda, Deep Green sijui nini kila kitu kilichokuwa kikihusu BoT. Mtakumbuka aliwatangazia Watanzania kuwa nyaraka za Dokta Slaa ni fake za kuokoteza kwenye internet na nitampeleka polisi, mpaka leo hakunipeleka. Lakini Sitta alikuwa anajua tangu mwanzo, kadri nilivyokuwa nikikusanya documents alikuwa anajua na nampatia copy, mpaka ikafikia ile document kubwa ya mwisho.

“Lakini kwa unafiki wake ameahirisha bunge Ijumaa, Jumamosi akachukua ile document na kwenda nazo TBC akisema ni fake na atanipeleka polisi, lakini leo yako wapi…sasa mtu wa namna hii hafai hata kuwa naibu waziri, mtu yeyote anayelinda mafisadi na ufisadi ni fisadi kuliko mafisadi wenyewe, nawaambia haya kwa sababu tumefika hapa kwa sababu ya kuwa na viongozi, wakiwemo mawaziri wanafiki na waongo kama hawa.

“Lakini ili mjue Sitta ni mtu wa aina gani na kwamba hastahili kuaminika na Watanzania, haikuishia hapo, ufisadi wa Richmond mnajua alivyomaliza mjadala ule kihuni bungeni. Hadi leo hoja ile haina majibu, wakati tunahoji bungeni akafunga hoja ile kidikteta, sasa tunauliza huo ndiyo uzoefu alionao yeye au walionao wenzake, uzoefu wa kulinda mafisadi na ufisadi wa CCM na serikali yao, lakini sisi tunajua kwa nini alipindisha hoja ya Richmond, wakati huo alikuwa anabembeleza ili ateuliwe kuwania ubunge na baadae uspika, mnaona huyu ni mtu wa kuaminika kweli?”

“Hivi kwa matendo ya aina hii Sitta anaweza kutoka nje na kusema yeye ni jasiri na mzalendo, katika majasiri na wazalendo wa kweli Sitta hana sifa hizo, ndiyo maana wameshindwa hata kuyavua magamba kama walivyosema, sasa aende kwanza kwenye chama chake na serikalini, asaidie kuyaondoa magamba kabla hajaanza kutafuta aibu ya kuanikwa zaidi,” alisema Dkt. Slaa.

Siri zaidi; Sitta haaminiki

Dkt. Slaa aliongeza kusema kwa kutoboa siri zaidi namna ambavyo, yeye na Mwenyekiti wa CHADEMA Mbowe, walikuwa wakiendesha mazungumzo na Sitta wakati mwingine kwenye Ofisi ya Spika juu ya Sitta kuhamia CHADEMA na kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, akisema kuwa ulikuwa ni wakati ambapo waziri huyo pamoja na wenzake walipokuwa wameunda Chama Cha Jamii (CCJ) wakiwa bado wako CCM.

Alisema kuwa hata wakati huo bado Sitta alikuwa akionekana kutojiamini na maamuzi yake, ambapo wakati wa majadiliano ya kugombea urais, Sitta alisema kuwa kuna kundi la wabunge takriban 55 watiifu kwake ambao walikuwa tayari kuhama naye kumfuata CHADEMA. 

“Leo natoa siri ambayo sijawahi kuitoa, Sitta ni mhanini. Tumekutana naye mara 100 na zaidi, tumeandikiana vimemo bungeni vya kukutana, wakati mwingine tumekutana hata Speaker’s lounge, tumekutana na Sitta na Mwenyekiti Mbowe, ambaye leo anamwita ni mchezesha disko mara nyingi tu. Lakini hata wakati huo pia hakuonekana kuwa jasiri, maana alikuwa ana wasiwasi nani wanamfuatilia au nani wanamuona, si mtu jasiri hivyo. 

“Zikiwa zimebaki kama siku tano kabla ya kumaliza bunge la mwezi wa saba, kila nikimwandikia kimemo, hataki hata kunitazama, Sitta akayeyuka bila hata kutuaga, baadae CHADEMA tukaamua kutumia utaratibu mwingine na tukaweza kusonga mbele mpaka kufika pale tulipofika. Lakini baada ya uchaguzi akaja mwenyewe kunifuata akinishukuru sana na kunipongeza kuwa nilikuja na hoja tofauti kwenye uchaguzi akisema hata yeye asingeweza kufika tulipofika.

“Lakini hapo sasa tulishamshtukia na kugundua kuwa anataka kugombea uspika kupitia CHADEMA, nataka kuonesha namna huyu mtu alivyo mnafiki, mpotoshaji, nampatia challenge kama kweli yeye ni muumini mzuri akanushe haya, maana ametulazimisha kusema, kwa hoja zake za kupotosha watu na akumbuke, maana huwa anakwenda makanisani na anachanga mapesa, akumbuke maandiko yanasema, yeyote atakayepotosha wadogo hawa, anastahili kutoswa baharini, Makamu Mwenyekiti hapa ametumia Quran kufafanua vizuri,” alisema Dkt. Slaa.

“Maana kwa hakika anataka kupotosha watu ili waone kuwa kuchezesha disko ni suala lisilokuwa sahihi, huo ni upotoshaji, kama anataka kuonesha si sahihi mbona serikali yake hiyo hiyo inaendelea kukusanya kodi. Sasa ilipofikia kwenye suala la kugombea uspika, siku ile jina lake limekatwa kwa sababu walitaka mgombea mwanamke, alinipigia simu usiku wa saa tisa, bahati mbaya nilikuwa nimeweka simu silence, hakunipata.

“Saa 12 nikapokea simu ya mke wake, Margreth Sitta, anasema baba anakutafuta tangu usiku, anataka kuzungumza nawe, nikasema sawa, akaniambia Dokta Slaa wamenifanyia kitu kibaya sana, mimi nimeamua sasa nitagombea uspika kwa tiketi ya CHADEMA, najua umeshateua tayari mtu wa kugombea tayari, lakini naomba nikuhakikishie nafanya press conference saa 4 asubuhi leo, natangaza rasmi kugombea uspika kupitia CHADEMA. Nikamjibu CHADEMA maamuzi hayafanywi na mtu mmoja, nikamwambia asubiri niwasiliane na Mwenyekiti wangu wa chama.

“Baadae tukakubaliana tukutane nyumbani kwake, lakini akawa anasema tusubiri kwanza anamalizia kupanga mikakati na wabunge 55 wa CCM, lakini akisisitiza kuwa uamuzi wake uko pale pale, nikamuuliza vipi kuhusu press conference mbona muda unakaribia, akasema hakuna shida yeye atatuma tu watu wake wataitisha haraka, akasema lakini wanataka kumpatia unaibu waziri, hivyo bado anasumbuana nao, kengele ikalia kichwani sasa huyu mtu akipewa uwaziri itakuwaje.

“Baadae ananiambia, Dokta Slaa nimepigiwa simu na bwana mkubwa naenda kuonana naye, tangu wakati huo Sitta akapotea mpaka saa 8 ndiyo anapatikana, akaanza kuniambia ni lazima aende kwanza Urambo kuwaaga wazee, maana hawezi kuhama bila baraka zao, nikamuuliza vipi kuhusu press conference akasema tutaifanya Jumatatu ijayo Dar es Salaam, akaniambia; tena saa 9 uje uone statement ambayo nimeshaiandika ili na wewe uongeze inputs, Sitta huyu akaniambia kuwa Anne Makinda hatakaa zaidi ya miezi sita kwenye kiti cha uspika.”

Dkt. Slaa alisisitiza akisema kuwa nchi imefika hapa ilipo ikiwa imegubikwa na uozo wa ufisadi kila kona, ukiongeza idadi ya maadui wa taifa, kutoka watatu hadi wanne (umaskini, ujinga, maradhi na ufisadi/CCM) kuanzia ngazi ya chini hadi juu, kwa sababu ya ukosefu wa uadilifu, uaminifu kama Waziri Sitta.

Atalipuliwa zaidi


Dkt. Slaa alisema kuwa ameamua kuzungumza hayo machache kwa sasa, lakini ataongeza ‘kumlipua’ zaidi Sitta endapo atajitokeza kujibu haya ya sasa.

“Yeye ana uzoefu gani Sitta, hana uadilifu, si mwaminifu, nchi hii imeoza kwa sababu ya viongozi ya aina ya Sitta, nataka ajibu kwanza hayo kisha nitamlipua zaidi. Ana uadilifu gani katika nchi hii, ametumia mabilioni ya hela ya walipa kodi wa Tanzania kujijengea Ofisi ya Spika Urambo, tunauliza kuna spika wa Urambo au alijua yeye atakuwa spika wa milele au basi Makinda awe anakwenda Urambo wakati wa mapumziko ya bunge.
“Tulichoamua bungeni ni kwamba kila mbunge ajengewe ofisi yenye thamani isiyozidi milioni 40, lakini yeye akaenda kujijengea ofisi ya milioni 350 tena kwa kasma tofauti na inavyotakiwa lakini kibaya zaidi tendering process ya vifaa vya ofisi haikufutwa na vililetwa na kampuni ambayo majuzi imehusishwa na Blandina Nyoni, hakuna mahali tendering imefanyika, amefanyia ufisadi mali ya taifa,” alisema Dkt. Slaa.


More still to come about the press conference...


CHANZO: Afisa Habari wa Chadema TUMAINI MAKENE

7 Jul 2010


Demokrasia katika jamii isiyojali utawala bora ni sawa na kufukia makaratasi ardhini kwa matarajio ya kuota mmea wenye matunda ya noti.Ni mithili ya kualika timu ya Taifa ya Brazil kwa mabilioni ya shilingi kisha mechi husika ituache na bili kubwa pasipo manufaa yoyote.Hebu tafakari.Mwezi Oktoba Watanzania kwa mamilioni yao watapiga kura kumchagua Rais na Wabunge.Japo shughuli hiyo ni ya siku moja tu,maandalizi yake yanagharimu mabilioni ya shilingi.Wenyewe wanasema ndio gharama ya demokrasia.Lakini baada ya uchaguzi,wengi-kama sio wote-wa tutakaowachagua watasahau kabisa kwanini tumewachagua,huku wakiwa bize kutafuta namna ya kufidia gharama walizotumia kuingia madarakani.

Zamani hizo tuliambiwa kuwa demokrasia ni pamoja na uwepo wa vyama vingi vya siasa.Takriban miongo miwili baadaye Watanzania wameshuhudia namna uwepo wa vyamahivyo vingi vya siasa ulivyoshindwa kulikwamua taifa letu kutoka kwenye lindi la umasikini.Sanasana umasikini umekuwa ukizidi kuongezeka huku wanasiasa wetu wakibadili kauli mbiu kila baada ya muhula (kwa mfano kutoka Ari Mpya,Kasi Mpya na Nguvu Mpya kuwa Ari Zaidi,Kasi Zaidi na Nguvu Zaidi).Tumeshuhudia pia mlolongo wa sera,mikakati,mpingo na vitu kama hivyo,from MKUKUTA to MKURABITA to KILIMO KWANZA.Na kwa mawazo mapya hatujambo,shughuli ipo kwenye utekelezaji.

Siku chache zilizopita nilitundika makala kuhusu utata wa kauli za Waziri wa Sheria na Katiba Mathias Chikawe na zile za Makamu Mwenyekiti wa CCM Pius Msekwa kuhusu suala la uanzishwaji Mahakama ya Kadhi.Wakati Waziri Chikawe aliahidi kuwa mahakama hizo zingeanza kazi mwakani,Msekwa alitamka bayana kuwa suala hilo haliwezekani.Hadi leo hakuna ufafanuzi uliotolewa kuhusu suala hilo ila kilicho bayana ni kuwa CCM imeamua kuachana nalo baada ya kuliingiza kwenye manifesto yake ya Uchaguzi mwaka 2005.Kwa vile sie ni mahiri zaidi wa kuhangaika na mambo kwa mtindo wa zimamoto tunasubiri liwake la kuwaka ndipo tuanze kuhangaika namna ya kudhibiti.Taasisi zenye majukumu ya kuwa proactive (yaani kuazuia majanga kabla hayajatokea) ziko busy zaidi na kuhakikisha CCM inarejea madarakani kwa ushindi wa kishindo badala ya kujishughulisha na jukumu lao la msingi la kulinda na kutetea ustawi wa taifa letu.Kwao,siasa (yaani CCM) ndio nchi na ndio kila kitu.

Majuzi umejitokeza utata mwingine wa kauli kati ya mawaziri wawili waandamizi kuhusu suala la uraia wa nchi mbili (dual citizenship).Na kichekesho ni kwamba tofauti na ule mgongano wa kauli kati ya Chikawe na Msekwa,safari hii mgongano wa kauli za mawaziri hao umejiri ndani ya jengo la Bunge katika kikao kinachoendela cha bajeti ya mwaka 2010/11.Awali,Waziri wa Mambo ya Ndani Lawrence Masha alilieleza Bunge Tukufu kuwa serikali imeamua kuwa huu sio wakati mwafaka kwa suala la uraia wa nchi mbili,na kwamba serikali anaangalia uwezekano wa kuanzisha ukaazi wa kudumu (permanent residency).Waziri Masha alieleza kuwa serikali inaandaa hoja kuhusu suala hilo la permanent recidency kwa minajili ya kuileta bungeni ijadiliwe. "Huu sio wakati mwafaka kuruhusu uraia wa nchi mbili,serikali inaangalia uwezekano wa kuanzisha ukaazi wa kudumu badala ya uraia wa nchi mbili", alisema Masha.

Wakati Masha akisema hivyo,Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bernard Membe alilieleza Bunge hilohilo kuwa serikali imeridhia suala la uraia wa nchi mbili na kwamba Wizara yake iko kwenye mchakato wa kuwasilisha suala hilo kwenye kikao cha Barza la Mawaziri.Pia Membe alieleza kuwa anafanya mawasiliano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ili kupata baraka zao kutokana na suala hilo kuwa la Muungano.Akihitimisha hoja ya bajeti ya wizara hiyo, kwa mwaka wa fedha 2010/2011, Waziri Membe alisema siyo dhambi, Watanzania kutafuta riziki nje ya nchi na ni haki yao kubaki na uraia wa Tanzania.Alisema wakati umefika kwa Watanzania, kupatiwa haki yao ya msingi kwani licha ya kuwa ni manufaa kwao pia ni manufaa kwa nchi kutokana na fursa ya kuongeza pato la taifa.

Kadhalika,inadaiwa kuwa Waziri Membe aliwaeleza Watanzania waliohudhuria mkutano wa Diaspora jijini London hivi karibuni kwamba suala hilo limeshajadiliwa na baraza la mawaziri na linasubiri kuwasilishwa bungeni ili upitishwe au kupingwa na wabunge.Mimi sikuhudhuria Mkutano huo wa Diaspora kwa vile niliamini ungenipotezea muda wangu tu kwa sababu viongozi wetu ni mahiri sana katika kuahidi mambo mazuri kwenye hadhara,na hujifanya wasikivu sana lakini utekelezaji ni zero,sifuri,zilch!

Ni dhahiri kwamba mmoja kati ya mawaziri hawa anadanganya.Wakati sina la kusema kuhusu kauli ya Waziri Masha,kauli za Waziri Membe huko Bungeni na London zinaleta utata unaoweza kuyumkinisha kuwa kuna urongo wa namna flani.Je kauli ipi ni sahihi kati ya hiyo alotoa London kuwa suala hilo limeshajadiliwa na Baraza la Mawaziri na hiyo ya bungeni kuwa suala hilo bado liko wizarani huku likifanyiwa mchakato wa kulipeleka kwenye Baraza la Mawaziri?

Unajua kwanini mmoja wao anadanganya?Sababu ni kadhaa,lakini kwa ufupi,moja,ni kwa vile mdanganyifu huyo anafahamu bayana kuwa wabunge wanaoelezwa suala hilo wapo bize zaidi kufikiri namna watakavyorudi bungeni baada ya uchaguzi (sambamba na kuwazia posho zao nono za vikao vya bunge) kuliko kumkalia kooni waziri aeleze kinagaubaga.Ndio maana mwanzoni mwa makala hii nilibainisha uselessness ya demokrasia yetu.Tunapoteza mabilioni ya shilingi (sambamba na muda wetu kusikiliza porojo za "mkituchagua tufafanya hiki na kile") kuwachagua watu wa kutuwakilisha bungeni lakini wakishafika huko wanakuwa bize zaidi na maslahi yao binafsi.

Pili,anayedanganya kati ya mawaziri hao anafahamu kuwa aliyemteua hatamwajibisha.Kama kuna mtu alimudu kumzuga Rais kwa kuchomekea ishu kadhaa kwenye muswada wa sheria za gharama za uchaguzi na kisha akasalimika,kwanini basi mdanganyifu huyo katika suala hili la uraia mbili awe na hofu?

Tatu,waziri anayedanganya kati ya hao wawili anafahamu udhaifu wa Watanzania katika kudai haki zao za msingi.Kiongozi anaweza kudanganya waziwazi kwenye umati wa watu lakini bado akaishia kupigiwa makofi na vigeregere.Ule wimbo wa "Ndio Mzee" wa Profesa Jay unawakilisha hali halisi ya namna Watanzania wengi wanavyoridhia kuzugwa na wanasiasa wababaishaji.Hebu angalia namna harakati za kuirejesha tena madarakani CCM zinavyopamba moto huko nyumbani.Kwa mgeni,anaweza kudhani labda chama hicho ni kipya na hakihusiki kabisa na kashfa za ufisadi,kubebana,kubomoa uchumi wetu na madudu mengine chungu mbovu yanayoifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi masikini kabisa duniani licha ya raslimali lukuki iliyojaaliwa kuwa nazo.Binafsi naamini kuwa unyonge huo wa Watanzania umechangiwa sana na siasa za chama kimoja ambapo kiongozi alikuwa mithili ya Mungu-mtu,hakosei,lazima ashangiliwe hata akiongea utumbo,sambamba na suala la kujikomba kwa viongozi kwa matarajio ya kujikwamua kwa namna moja au nyingine.

Na kwa vile vyama vya upinzani vimetuthibitishia kuwa uwezo wao katika kuing'oa CCM madrakani ni kama haupo,basi mazingaombwe kama hayo ya Chikawe na Msekwa,na haya ya sasa kati ya Masha na Membe yataendelea kuwepo kwa muda mrefu sana.Unaweza kuhisi kama nimekata tamaa vile kwa namna ninavyoandika.Hapana,ila safari yetu ni ndefu sana,na tatizo sio urefu tu bali ni kiza kilichotanda kwenye njia yetu ambayo imejaa mashimo kadhaa.Ni sawa na kipofu kumsaka paka mweusi kwenye chumba chenye giza ilhali paka huyo hayumo chumbani humo.

31 Jul 2009


Ushaskia kuhusu political conmanship?Hebu soma kwanza habari ifuatayo kisha tujadili




Spika Sitta aomba ulinzi zaidi, adai nguvu ya mafisadi inahatarisha maisha yake

Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muuangano wa Tanzania sasa anahofia maisha yake kutokana na vitisho vya mafisadi

Spika Sitta aomba ulinzi zaidi, adai nguvu ya mafisadi inahatarisha maisha yake

Kizitto Noya, Dodoma na Boniface Meena

SPIKA wa Bunge Samuel Sitta ameiomba Serikali kumwongezea ulinzi kwa kuwa mafisadi wameongeza nguvu ya vita dhidi yake.

Spika Sitta alisema hayo alipokuwa akizungumzia tuhuma dhidi yake, zilizoripotiwa jana na baadhi ya vyombo vya habari (sio Mwananchi) kuwa anafanya njama kuchoma nyaraka za Bunge.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, Spika anadaiwa kula njama ili kuchoma ofisi ya mhasibu wa Bunge ili kuharibu nyaraka muhimu zinazomhusisha na ubadhirifu wa fedha za Bunge.

Lakini Spika Sitta alijibu tuhuma hizo bungeni akisema taarifa hizo zina mkono wa wabaya wake, wenye lengo la kumchafua katika utendaji wake.

“Hivi kama kweli nataka kuficha faili la Bunge nani anaweza kunizuia humu ndani?” alihoji Spika Sitta na kuongeza:

“Hizi ni taarifa za wabaya wangu, wanachofanya ni kuziweka kwenye internet kwanza halafu wanazisambaza kwenye vyombo vyao maalum, magazeti manne; gazeti la Tazama, Tanzania Daima na mengine mnayoyaona," alisema Spika na kuongeza:

“Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba mnipe ulinzi zaidi, hii vita ni ngumu na kubwa sasa. Ulinzi mnaonipa naona hautoshi,” alilalamika Spika Sitta na kuwaponda wanaomwandama kuwa hata iweje, ataendelea kushinda ubunge jimboni kwake na kuwa Spika kama bado atakuwa hai mwakani.

Alifafanua kuwa fedha wanazopeleka maadui zake jimboni kwake Urambo zinasaidia kuimarisha maendeleo, lakini hazitomng’oa madarakani.

"Wananchi wangu wanajua ninachokifanya jimboni kwangu, hata wakipeleka pikipiki bado nitashinda," alisema Sitta.

Mara kwa mara Spika Sitta amekuwa akidai kwamba anaandamwa na mafisadi ambao wanataka aache kufichua maovu yao.

Spika Sitta alisema hayo muda mfupi baada ya kumaliza kutoa mwongozo kwa mbunge wa Micheweni (CUF), Shoka Khamis Juma, kwamba chama fulani kina tabia ya kununua shahada za kura wakati wa chaguzi.

Katika mwongozo wake, Spika alimtaka mbunge huyo kufuta kauli yake bungeni kwa kuwa ushahidi aliotoa kuthibitisha kauli hiyo ni dhaifu.

“Madai ya Shoka ni tuhuma kama tuhuma zozote zinazotolewa na wanasiasa wengine,” alisema.

Akifafanua kuwa Shoka ameshindwa kuthibitisha tuhuma zake kwa kuwa ametoa ushahidi wa magazeti ambayo sio yote yanaweza kuaminika.

“Magazeti yanaweza kuwa chanzo cha taarifa kwa wabunge katika kuchangia hoja zao, lakini sio kigezo pekee cha kumwezesha Spika kutoa mwongozo,” alisema Sitta na kuendelea:

“Hivyo mheshimiwa Shoka hawezi kulindwa na kifungu namba 63 (2), kwa mantiki hiyo namtaka kwa kanuni namba 63 (1) afute kauli yake humu bungeni kabla ya kumalizika kikao hiki cha Bunge”.

Juni 12 mwaka huu mbunge huyo wa CUF alitamka bungeni alipokuwa akiuliza swali la nyongeza kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimekuwa na tabia ya kuiba shahada za kupigia katika maeneo ambayo kinaona hakiungwi mkono.

Naibu Spika Anne Makinda ambaye alikuwa anaongoza kikao cha Bunge siku hiyo, alimtaka mbunge huyo athibitishe kauli yake, naye alifanya hivyo Juni 17, mwaka huu kwa kuwasilisha kwa Spika nakala za magazeti yaliyoripoti uchaguzi wa Jimbo la Busanda.

Hata hivyo, Spika Sitta alisema kwa kuwa hakuna ushahidi wa hukumu kuhusu tuhuma hizo, madai ya Shoka ni tuhuma kama tuhuma zingine zinazotolewa na wanasiasa majukwaani, hivyo kumtaka afute madai yake.




CHANZO: Mwananchi

Nadhani sasa kuna umuhimu wa kuangalia kama Spika huyu wa Viwango na Spidi bado anastahili kuendelea na wadhifa wake ambao ni wa nne kitaifa.Natoa hoja hiyo kwa vile kuna kila dalili kuwa Spika Samwel Sitta sasa anaogopa kivuli chake mwenyewe.




Ni hatari kwa kiongozi wa kitaifa kama Spika kutoa madai mazito namna hiyo pasipo kuwa na uthibitisho wowote.Hivi hao mafisadi wanaohatarisha maisha yake ni akina nani?Nauliza hivyo kwa vile kwa mujibu wa maelezo yake inaonyesha anawafahamu hata kwa majina.Sasa tunapokuwa na kiongozi wa kitaifa ambaye pindi maisha yake yanapokuwa hatarini (kama unaamini anachosema) anakimbilia kuomba aongezewe ulinzi hadharani,then hapo kuna mushkeli.



Ni hatari zaidi kumsikia Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,taasisi tukufu yenye jukumu la kutunga sheria za nchi,akiuliza bila aibui wala uoga "Hivi kama kweli nataka kuficha faili la Bunge nani anaweza kunizuia humu ndani?” You can't be serious,Mzee wa Spidi na Viwango!Yaani unatuambia kuwa kwa wadhifa wako unaweza kuficha nyaraka muhimu za Taifa (mfano faili la Bunge) na hakuna mwenye uwezo wa kukuzuia?Nadhani unatafsiri vibaya madaraka yako.Uspika ni nafasi inayoongozwa kwa taratibu na sheria,za nchi na za Bunge unaloongoza.Sasa unapotuambia kuwa hakuna wa kukuzuia ndani ya Bunge kuficha faili (ukijiskia kufanya hivyo) unatuaminisha kuwa aidha huelewi mipaka ya kazi yako,au unadhani Uspika ni kuwa juu ya sheria za nchi na Bunge,au kulewa madaraka.



Tukiwa hapohapo kwenye hoja yako ya "hakuna wa kukuzuia...",na tukiamini kuwa ni kweli hakuna wa kukuzuia,je utalalamika kuwa mafisadi wanakuwinda wakikuzushia zengwe kwamba umeficha nyaraka muhimu zaidi ya faili la Bunge?Sawa utasema wanakuandama lakini ushawapa hoja kwamba "ukitaka kuficha faili la bunge hakuna wa kukuzuia".Well,wao wanaweza kuja na tuhuma kubwa zaidi ya kuficha faili.Laiti busara zingetumika,ungeishia tu kukanusha tuhuma za kwamba una mpango wa kuchoma moto ofisi za bunge,na sio kukurupuka kudai una uwezo wa kuficha faili la bunge pasipo kuwapo wa kukuzuwia.



Ni rahisi kwa Spika kuomba aongezewe ulinzi (kwa kigezo kuwa ulinzi alionao sasa hautoshi) kwa vile gharama za kuongezewa ulinzi zitabebwa na walipa kodi na si kutoka mfukoni mwa Spika.Hoja hii ya Spika Sitta pia inaweza kufanya tujiulize iwapo licha ya nafasi yake ya Uspika,Mheshimiwa Sitta pia ni mtaalam wa mambo ya ulinzi wa viongozi,na review aliyofanya katika protection anayopewa hivi sasa imempelekea kuhitimisha kuwa ulinzi alionao hautoshi.Hii ni sawa na kuwadharau professionals wenye jukumu hilo,ambao naamini wangetambua mapungufu hayo kabla hata ya Spika Sitta kutamka hadharani.



Lakini twende mbali zaidi kwenye hili la "ulinzi alionao Spika hautoshi"Je anaweza kututhibitishia japo tukio moja linaloashiria kutotosha kwa ulinzi alionao hivi sasa?Yaani kutuhumiwa kuwa anataka kuchoma moto ofisi za bunge, na "maadui zake kumwaga fedha jimboni kwake" vimekuwa matishio ya kiusalama yanayotosheleza kufikia uamuzi wa kumuongezea ulinzi?



Kichekesho ni kwamba wakati Spika akimtaka Mbunge wa Cuf (Mheshimiwa Shoka Hamis Juma) afute kauli yake kwa kuwa "ushahidi aliotoa-katika madai kuwa kuna chama flani kinanunua shahada wakati wa chaguzi-ni dhaifu",yeye mwenyewe anafanya kilekile cha kutoa madai dhaifu kuwa nguvu ya mafisadi inahatarisha usalama wake ilhali hajaweza kutoa uthibitisho wowote zaidi ya "kauli za kisiasa" kuwa maadui zake wanapeleka pesa jimboni kwake ili asirejee bungeni.Ana uhakika gani kuwa hao anaowaita maadui zake si wananchi wenye dhamira ya kuleta maendeleo katika jimbo hilo pasipo kuwa na ajenda za kisiasa?Au Spika Sitta anataka kutuambia kuwa ni yeye tu aliye na hatimiliki ya kupeleka misaada katika jimbo hilo?Jamani,yaani hadi maendeleo ya jimbo yanafanywa kuwa mithili ya maamuzi ya mtu binafsi!?



Kuna mengi ya kujadili kuhusu kauli za Spika Sitta,lakini lililo wazi ni kwamba nafasi anayojipachika ya ukinara wa mapambano dhidi ya ufisadi ni sawa na political conmanship.Kwa lipi hasa?Sio Sitta huyu aliyempa "kifungo" Zitto Kabwe kwa "kosa" la kumkalia kooni Karamagi kuhusu Buzwagi?Sio Spika Sitta huyu aliyetishia kumfungulia mashtaka Dkt Wilbroad Slaa pale mbunge huyo wa Karatu aliposhikilia bango kuhusu ishu za ufisadi?Ni lipi alilofanya Samweli Sitta,kama Spika wa Bunge la Jamhuri au Mbunge wa Urambo linaloweza kumjumuisha kwenye kundi la vinara wa mapambano dhidi ya ufisadi?Yaani Watanzania wenzake kutamani jimbo la Urambo imekuwa ufisadi?Au mtu kutamani nafasi ya uspika imekuwa ufisadi?



Lakini kwa vile siasa zetu kwa sasa zinaruhusu mambo ya ajabu kabisa kutokea,kauli hizi za Spika Sitta hazitawahangaisha wenye dhaman ya uchambuzi wa kauli hatari kama hizi na kuchukua hatua za haraka.Ni business as usual,kauli imetolewa,siku imepita,and life goes on!



Na kwa vile magazeti yetu yako bize zaidi kuripoti habari badala ya kuchambua mantiki ya habari husika,yayumkinika tutasikia makubwa zaidi ya kauli hizi za wanasiasa wanaoogopa vivuli vyao wenyewe.Na kwa vile kilio,kicheko,kuchafua hewa na hata kukoroma kwa mwanasiasa kunatosha kuwa leading news kwenye magazeti yetu,basi tutarajia vimbwanga zaidi.



Trust me,tutashuhudia vituko vingi zaidi na zaidi kadri siku zinavyoyoyoma kuelekea uchaguzi mkuu wa 2010.By the way,si ndio tunaelekea kile kipindi cha usanii wa kisiasa ambapo watu wazima hupiga magoti majukwani na wengine kutoa shikamoo hata kwa watoto wadogo alimradi wahakikishiwe kura?




16 Jun 2009



Wizara ya Fedha na Uchumi imesema, siasa za Tanzania ni nzuri na kuna mipango mizuri ya maendeleo ndiyo maana umasikini wa kipato unapungua. Hata hivyo Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Omar Yussuf Mzee amesema, bungeni mjini Dodoma kuwa, kuna watanzania wengi wanaishi kwa kula mlo mmoja. Kiongozi huyo wa Serikali amesema leo kuwa, umasikini ni mchakato, unapungua siku hadi siku.

Mzee ameyasema hayo wakati anajibu maswali ya Mbunge wa Viti Maalum, Magdalena Sakaya aliyetaka kufahamu ni kwa nini watanzani wengi bado ni masikini wakati nchi imepata uhuru miaka 48 iliyopita.

Mbunge huyo pia alidai bungeni kuwa, watanzania wengi bado ni masikini kabisa kwa kuwa hakuna siasa safi, na pia hakuna mipango mizuri ya kuwawezesha wananchi wapate maendeleo.

Naibu Waziri Mzee amewaeleza wabunge kuwa kuna umasikini wa aina tatu ukiwamo wa elimu, afya na kipato.Amesema, kama Tanzania isingekuwa na siasa safi na mipango mizuri ya maendeleo, takwimu zisingeonyesha kupungua kwa umasikini wa kipato nchini.


Amewaeleza wabunge kuwa, mwaka 1991, asilimia 21.6 ya watanzania wote milioni 24.8 walikuwa masikini kabisa. Kwa mujibu wa kiongozi huyo, mwaka 2001, Tanzania ilikuwa na watu milioni 31.9, asilimia 18.7 kati yao walikuwa masikini kabisa, na mwaka 2007, asilimia 16.5 ya watanzania milioni 38.3 walikuwa masikini kabisa.

Mzee amelieza Bunge kuwa, watanzania wengi bado ni masikini kwa kwa wengi wao ni wakulima wanaotumia jembe la mkono, bei za pembejeo za kilimo zimepanda, na pia mabadiliko ya hali ya hewa yanathiri uzalishaji kwa kuwa sehemu kubwa ya kilimo nchini hutegemea mvua. Ametaja sababu nyingine kuwa ni ukuaji mdogo wa sekta ya viwanda, wakulima kukosa mitaji, na pia ukosefu wa ajira.


CHANZO: Habari Leo

Wizi mtupu!

7 Dec 2008


UTATA wa zilipo fedha zilizorejeshwa na kampuni zilizoiba fedha katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA), umeendelea kuigubika nchi, baada ya kubainika kuwa fedha hizo hazijaingizwa kwenye mfuko ulioelekezwa na Rais Jakaya Kikwete wakati akilihutubia Bunge, Agosti 21 mwaka huu.

Fedha hizo ambazo ni zaidi ya sh bilioni 70, zilitakiwa ziende Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB), ambapo zingefunguliwa dirisha maalumu, lenye jukumu la kutoa mikopo kwa wakulima ambao kwa miaka mingi wamekosa fursa hiyo.

Uchunguzi wa Tanzania Daima Jumapili, umebaini kuwa fedha hizo zimehifadhiwa katika akaunti maalumu ambayo mpaka hivi sasa maelezo yake bado yamegubikwa na utata, kwa sababu kila ofisa wa Wizara ya Fedha na Uchumi aliyeulizwa juu ya akaunti hiyo, ameshindwa kutoa jibu linaloeleweka.

Tangu awali baadhi ya watu walionyesha wasiwasi wao kuhusu urejeshaji wa fedha hizo kama ni kweli zimerejeshwa au ilikuwa mbinu ya kisiasa ya serikali kutaka kuzima joto la wananchi, wapinzani na wahisani waliotaka fedha hizo zirejeshwe na watuhumiwa wafikishwe katika mikono ya sheria.

Watu hao waliweka wazi msimamo wao kuwa fedha hizo hazikurejeshwa bali ilikuwa ni janja ya serikali ili waweze kupata misaada kutoka kwa wafadhili ambao awali walitishia kutochangia bajeti ya serikali mpaka majibu sahihi na hatua za wizi wa EPA zichukuliwe.

Shinikizo hilo inadaiwa ndilo lililomfanya Rais Jakaya Kikwete kuamua kutengua uteuzi wa aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu, Daudi Ballali, pamoja na kuunda timu ya uchunguzi chini ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika, baada ya mkaguzi wa nje, Ernst & Young, kuthibitisha kuwapo kwa wizi katika akaunti hiyo, unaofikia kiasi cha sh bilioni 133.

Mkurugenzi wa Benki ya Rasilimali (TIB), William Mlaki, hivi karibuni alikaririwa na vyombo vya habari kuwa fedha hizo hadi sasa hawajazipokea.

Alisema inawezekana serikali inajiandaa kuwapelekea fedha hizo ambazo Rais Jakaya Kikwete alishaweka wazi dhamira ya serikali yake kuzipeleka TIB ili ziwasaidie wakulima.

“Mpaka sasa fedha za EPA, bado hazijaingia kwetu na si jukumu letu kuulizia fedha hizo zitakuja lini, kazi yetu ni kuzipokea na kuratibu zoezi la utoaji mikopo kwa wakulima,” alikaririwa Mlaki.

Kauli hiyo ya Mlaki, inazidisha utata kuhusu ukweli wa urejeshaji wa fedha za EPA ambazo uchotwaji wake unahusishwa na matumizi ya uchaguzi mkuu uliopita.

Inadaiwa kuwa mbinu za kuchota fedha hizo, zilifanywa na viongozi wa juu wa Serikali ya Awamu ya Tatu kwa kushirikiana na mwanasiasa na mfanyabiashara maarufu nchini ili zikisaidie Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu uliopita.

Hata hivyo, katika siku za hivi karibuni, tena kwa nyakati tofauti, Katibu Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba na Mkurugenzi wa Uchumi na Fedha, Amos Makala, wamekanusha chama chao kuhusishwa na wizi huo.

Mfanyabiashara huyo ndiye anayeaminika alikuwa mmiliki halali wa Kampuni ya Kagoda Agriculture Limited iliyochota sh bilioni 40, lakini hadi hivi sasa hajafikishwa mahakamani au kutajwa mbele ya umma.

Kutotajwa kwa mfanyabiashara huyo kunatokana na ukweli kuwa ndiye anayejua siri yote ya Kagoda na viongozi waliomuagiza kuzichota fedha hizo na hata matumizi yake pamoja na kujua nani kapata kiasi gani na kwa kazi gani.

Kwa hali ilivyo, Kagoda ndiyo kampuni inayoonekana kuitikisa nchi kama wamiliki wake watatajwa na kufikishwa mahakamani, kwani hawatakubali kushitakiwa peke yao bila kuwataja viongozi waliowatuma kufanya wizi huo.

Hali hiyo ndiyo iliyomfanya aliyekuwa Waziri wa Fedha, Zakhia Meghji, kutoa ufafanuzi kwa umma kuwa fedha zilizochotwa zilitumika kwa mambo ya usalama na si ufisadi kama ambavyo baadhi ya wanasiasa, akiwemo Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willbrod Slaa, walivyokuwa wakisema.

Msumari wa moto juu ya utata wa urejeshwaji wa fedha za EPA na ufisadi hivi karibuni ulishindiliwa na mfanyabiashara maarufu nchini na mwachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jafar Sabodo, ambaye alisema serikali inafanya mchezo wa kuigiza na haina nia thabiti ya kutatua matatizo ya rushwa.

Sabodo ambaye ni rafiki wa karibu wa marehemu Mwalimu Nyerere na mfadhili wa mfuko wa taasisi ya Mwalimu Nyerere na CCM, alifikia hatua ya kusema yuko tayari kukisaidia chama chochote cha upinzani katika uchaguzi ujao, kuiangusha CCM madarakani, kwa madai kuwa imeshindwa kuondoa tatizo la rushwa nchini.

Wachambuzi wa masula ya siasa wanadai kupandishwa mahakamani kwa mawaziri wawili ya serikali iliyopita Basil Mramba (Fedha) na Daniel Yona ((Nishati na Madini), ni mpango wa kuwasahaulisha wananchi juu ya mwenendo wa kesi ya EPA, hasa kuendelea kufikishwa mahakamani kwa watuhumiwa wengine.

Mpango huo uliasisiwa kutokana na joto la wananchi kutaka wamiliki wa Kampuni ya Kagoda inayohusishwa na wafanyabiashara, wanasiasa maarufu na wakongwe nchini, kuzidi kushika kasi kiasi cha kumfanya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuweka bayana kuwa joto hilo likizidi, wamiliki wake watajulikana.

Wadadisi hao wanaendelea kubainisha kuwa mpango huo kwa kiasi fulani, umefanikiwa, kwani watu walihamisha macho na masikio yao kutoka EPA na kuhamia kwa Yona na Mramba, ambao wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salam kwa kosa la kuisababishia hasara serikali ya zaidi ya sh bilioni 11.7, kwa kutoa misamaha ya kodi kiholela katika sekta ya madini.

Wakati wingu zito likiwa limetanda kuhusu mahali zilipo fedha za EPA, kuna tetesi kwamba fedha hizo ndizo zilizotumika kulipa madai ya walimu ambao miezi miwili iliyopita walitishia kugoma nchi nzima kushinikiza kulipwa fedha zao za malimbikizo zinazofikia sh bilioni 16.


Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.