17 Jan 2013


MIONGONI mwa matokeo ya kuyumba kwa uchumi wa Uingereza, ni mfumuko wa kampuni za mikopo ya muda mfupi ambayo hulipwa pindi mkopaji anapopata mshahara (payday loans).
Kushamiri kwa kampuni zinazotoa mikopo ya aina hiyo, kumechangiwa na ukweli kwamba taasisi nyingi zinazotoa mikopo ya ‘asili’ (traditional lenders), zimekuwa na masharti magumu ya kutoa mikopo kwa wateja wao.
Ingawa kampuni hizo za ‘payday loans’ zimekuwa kama mkombozi kwa wananchi wasioweza kupata mikopo kwingineko, viwango vyao vikubwa vya riba vimepelekea mjadala mkubwa huku baadhi ya taasisi za kutetea maslahi ya wateja zikiitaka Serikali kuongeza udhibiti wa taratibu za mikopo hiyo.
Kwa wastani, viwango vya riba vinavyotozwa na wakopeshaji hao ni kati ya asilimia 1,000 hadi 4,000. Mengi ya kampuni zinazotoa mikopo hiyo, hutoza riba kila siku, na matokeo yake ni kwamba mkopaji hujikuta akilazimika kukopa tena mara baada ya kumaliza kulipa deni la awali.
Kadhalika, wakopeshaji hao hufanya kila jitihada kuhakikisha kwamba mteja wao anaendelea kuwa ‘mtumwa’ wa kudumu wa mikopo yao ambapo humwandama kwa ofa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na ‘likizo’ ya malipo ambayo kimsingi hukuza kiwango cha riba hata maradufu ya kiwango cha awali.
Lengo la makala haya si kuzungumzia kuhusu kuyumba kwa uchumi wa Uingereza, ‘payday loans’ au kampuni zinazotoa mikopo ya aina hiyo yanavyonufaika na riba kubwa wanazotoza wateja wao, bali habari niliyoisoma katika gazeti moja la huko nyumbani, zikisema kwamba Shirika la Fedha Duniani (IMF) linaridhishwa na mwenendo wa uchumi wa Tanzania, na kwamba nchi yetu inaweza kukopa zaidi.
Mara baada ya kusoma habari hiyo ‘nilitwiti’ katika mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa ‘hivi sasa IMF imegeuka kuwa kama kampuni ya kimataifa ya ‘payday loans.’
Niliandika hivyo kwa sababu ni mwendawazimu pekee anayeweza kudai kwamba mwenendo wa uchumi wetu ni mzuri. Haihitaji japo kozi ya saa chache ya uchumi kutambua kwamba licha ya Tanzania kuwa moja ya nchi masikini zaidi duniani, pia hali za maisha ya Watanzania zinazidi kuwa ngumu siku hadi siku.
Lakini kwa vile IMF ni ‘wahuni’ kama kampuni za ‘payday loan’ ya hapa Uingereza, ambayo kwao cha muhimu ni faida bila kujali mzigo wanaombebesha mkopaji, pasi aibu, shirika hilo linanishawishi nchi yetu kukopa zaidi, kutokana na msingi wa kwamba ‘tunakopesheka’ ingawa tuna mzigo wa deni la ndani linalofikia Sh trilioni 22.
Niwarejeshe nyuma kidogo. Nimeshaandika mara kadhaa katika makala zangu kadhaa katika matoleo yaliyopita kwamba wakati mkoloni alikuwa na ‘excuse’ isiyokubalika ya kutuibia raslimali zetu, hakuna hata Mtanzania mmoja mwenye sababu ya kuihujumu nchi yetu.
Katika mtizamo huo huo, wakati ninaelewa kwanini IMF haijali kabisa kuchambua kwa undani hali halisi ya uchumi wetu, kwa vile kimsingi sera za IMF haina tofauti na zile za mkoloni, nilikerwa mno na kauli za wasomi wawili wa Kitanzania; Profesa Delphin Rwegasira na Profesa Humphrey Moshi.
Wakati Profesa Rwegasira alidai kuwa kuridhishwa huko kwa IMF kuhusu uchumi wetu kunaonyesha kwamba taasisi hiyo ina imani na mwenendo wa uchumi wetu, lakini akatahadharisha kuwa tunaweza kuishia kuwa na madeni makubwa zaidi. Kwa upande wake, Profesa Moshi alidai kuwa hiyo ni hatua nzuri kwa nchi kama Tanzania kwani inatoa fursa zaidi kwa sera na uhuru wa kuchagua sera.
Ingawa ninawaheshimu wasomi hawa, na ninatambua kwamba wanatumia haki yao ya kitaaluma na kikatiba kutoa mtizamo wao, lakini licha ya mimi kuwa si msomi kama wao, ninashindwa kuwaelewa wanapozichukulia porojo hizo za IMF kama hatua ya msingi kwa nchi yetu.
Kauli za wasomi hao, hazitofautiani na zile tunazosikia mara kwa mara kutoka kwa baadhi ya viongozi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), na hasa Gavana, Profesa Benno Ndulu, na viongozi wetu serikalini, na hasa Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk William Mgimwa, ambazo huambatana na takwimu za kuleta matumaini huku zikikinzana kabisa na hali halisi ya maisha mtaani.
Binafsi, ninaamini kwamba matumizi bora ya elimu si tu kuzingatia kanuni (theories) zilizopo vitabuni, ambazo mara nyingi hupuuza hali halisi ya jamii zisizo za kimagharibi, bali kutafsiri kanuni hizo kwa kuzingatia hali halisi katika jamii husika.
Ndiyo. Fedha za mikopo kutoka IMF na taasisi nyingine za fedha na nchi wafadhili, zinachangia kwa kiasi kikubwa katika bajeti yetu na miradi mbalimbali ya maendeleo. Lakini kanuni nyepesi na isiyo ya kitaaluma ya uchumi wetu, ni kwamba sehemu ya fedha za mikopo hiyo ndizo hizo zilizoko Uswisi kwenye akaunti za mafisadi.
IFM wanafahamu bayana kwamba nchi yetu ina mabilioni ya Shilingi yaliyofichwa na mafisadi huko Uswisi, na jinsi fedha hizo zingeweza si tu kupunguza haja ya nchi yetu kuendelea kukopa, bali pia zingeweza kuchangia kupunguza deni la ndani la Serikali na nakisi kwenye bajeti yetu.
Kwanini IMF inapuuza ukweli kuhusu uchumi wetu uliowekwa rehani mikononi mwa wafadhili wa nje na mafisadi wa ndani? Jibu jepesi ni kama lile la kwanini kampuni za ‘payday loans’ za hapa Uingereza, zinaendelea kuwabebesha mzigo wa madeni yenye riba kubwa wateja wake, hali inayowafanya waendelee kuwa mateka kwa kukopa na kulipa ili waendelee kukopa zaidi. Kwa lugha nyingine, ni kuendelea kwa mzunguko katili wa umasikini (vicious circle of poverty).
Kimsingi, kauli ya IMF haina tofauti na ile iliyotolewa na Waziri Mgimwa kuhusu deni letu la ndani la Sh trilioni 22, ya wamba ‘bado tunakopesheka.’ Busara kidogo tu zinapaswa kubainisha kwamba suala si kuendelea kuwa na uwezo wa kukopesheka, bali uwezo wa kulipa madeni hayo na hatimaye kuondokana na utumwa kwa kuishi kwa matakwa ya wanaotukopesha.
Nihitimishe makala haya kwa kuwakumbusha watawala wetu kwamba pamoja na ukweli kuwa hakuna nchi yoyote duniani inayoweza kujiendesha pasipo kukopa kutoka taasisi za ndani na nje ya nchi, deni la takriban Sh 500,000 (Sh trilioni 22 kugawanya kwa idadi ya sasa ya Watanzania-takriban milioni 45) analobeba kila Mtanzania, haliwezi kulipwa, achilia mbali kupunguzwa, kwa kukopa zaidi.
Njia pekee ni kutanguliza mbele maslahi ya taifa kwa kupambana na majambazi wanaohujumu uchumi wetu, kukubali kuishi kimasikini kwa maana ya matumizi ya Serikali kuendana na uwezo wetu, na pia kutohadaika na porojo za wakopeshaji kama IMF ambao kimsingi ustawi wao unatutegemea sisi kuendelea kuwa wateja wao.
Na kwa upande wa wasomi wetu, wito wangu kwao ni kujaribu kutafsiri yaliyoandikwa vitabuni kwa kuzingatia hali halisi ya nyanja mbalimbali katika Tanzania yetu. Uchumi wetu kwa mfano, ni zaidi ya takwimu, bali ni mamilioni ya Watanzania wasio na uhakika wa mlo ujao, raslimali zetu zinazotoroshwa kila kukicha, utashi wa kisiasa na kisera dhidi ya porojo za kibabaishaji katika kuikwamua nchi yetu kimaendeleo, na uelewa wa mfumo wa kinyonyaji unaotaka kuziona nchi masikini zikiendelea kuwa tegemezi daima.


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.