14 Apr 2013



WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda anaweza kujikuta katika wakati mgumu, baada ya kuumbuliwa na ripoti ya tume ya uchunguzi wa matokeo mabaya ya mwaka 2010, inayodaiwa hakuifanyia kazi na badala yake akakimbilia kuunda tume nyingine.


Ripoti hiyo ambayo imesambazwa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii, ikiwamo ule wa Jamii Forums, imekuja siku moja baada ya Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu kuwashawishi wabunge wampigie kura Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ya kutokuwa na imani naye, kutokana na kushindwa kumwajibisha Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa 



Katika ripoti hiyo ya mwaka 2011, iliyosambazwa kwenye mtandao wa Jamii Forum, na gazeti hili kuipata inabainisha upungufu wa wazi hasa kwa Serikali kwamba, uteuzi unaofanywa kwa viongozi mbalimbali wa kisiasa katika sekta ya elimu hauzingatii uzoefu, utaalamu, uwezo, uadilifu na uwajibikaji. 



Gazeti hili limebaini kuwa tume iliyokuja na ripoti hiyo iliongozwa na Profesa Sefue Mchome na utafiti wake ulifanywa kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali wa sekta ya elimu.



Hata hivyo, Serikali imeshutumiwa kwa kushindwa kuiweka wazi na namna hatua ilizochukua baada ya kupokea ripoti hiyo.



Baadhi ya watu waliotoa maoni yao walionyesha kushangazwa na hatua ya Pinda kuunda Tume kuchunguza kushuka kwa ufaulu kwa matokeo ya mwaka jana, ili hali tayari kulikuwa na ripoti nyingine ambayo ilikuwa haijafanyiwa kazi.



Kitendo hicho kimetafsiriwa kuwa kilikuwa na lengo la kuwahadaa wananchi ili kuwaonyesha kuwa anauchungu na anataka kulifanyia kazi suala hilo kumbe sivyo.



Ripoti hiyo ambayo ilijikita katika kufanya utafiti wa kushuka kwa elimu nchini, ulifanywa kwa ushirikiano kati ya TAMISEMI na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi (WEMU), ikihusisha Taasisi ya Elimu Tanzania na Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA).



Moja kati ya mambo ambayo yamebainika katika utafiti huo ni pamoja na sababu za kushuka kwa kiwango cha ufaulu wa Mtihani wa Taifa wa Kidato cha 4 mwaka 2010, ambazo ni masuala ya kimfumo ikiwemo upungufu katika usimamizi na uendeshaji wa elimu nchini. 



Maeneo mengine ni katika kujenga uwezo wa wasimamizi na watekelezaji wa mitaala, kuhakikisha upatikanaji wa vifaa bora na vya kutosha vya kufundishia, kujifunzia na uboreshaji wa majengo na miundombinu ambayo yanahitaji nguvu ya pamoja kati ya Serikali na wabia wake.



Katika moja ya mapendekezo yake Utafiti huo uliitaka Serikali 



kuona umuhimu wa kushirikiana na washirika na wadau wa elimu nchini, ili kuweza kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika sekta ya elimu.



Itakumbukwa kuwa hivi karibuni, Waziri Mkuu Pinda aliunda Tume kuchunguza kushuka kwa ufaulu kwa matokeo ya kidato cha nne, kitendo ambacho kilipingwa na baadhi ya wadau waliosema kuwa hakukuwa na haja ya kufanya hivyo, kwa sababu kila kitu kipo wazi.

0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.