Bunge lachafuka
Wednesday, 27 July 2011 21:31
WENJE ATOLEWA KWA NGUVU, MBUNGE CCM ANUSRIKA KUPIGWA
Neville Meena na Habel Chidawali, Dodoma
MBUNGE wa Nyamagana (Chadema), Ezekia Wenje, jana alijikuta akitolewa bungeni na askari (wapambe) wa Bunge waliotii amri ya Mwenyeviti wa Bunge, Sylivester Mabumba, aliyeongoza kikao siku hiyo.Katika tukio ambalo ni la kwanza kutokea tangu kuanza kwa Bunge la Kumi linaloongozwa na Spika Anne Makinda, Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM), alinusurika kupigwa na wabunge wa kambi ya upinzani baada ya kuwakejeli Chadena akisema waache mambo ya kitoto.
Mabumba alitoa amri ya Wenje kutolewa nje baada kukaidi amri ya Mabumba kumtaka akae chini mbunge huyo wa Nyamagana alipokuwa akiomba mwongozo, katikati ya mabishano yaliyokuwa yakiwajumuisha wabunge wengine wakati huo.Wakati Wenje akisisitiza kuomba mwongozo kwa maelezo kwamba jambo analotaka kusema "lina maslahi ya nchi", Mabumba ghafla aliwaita askari (wapambe) wa Bunge na kuwaamuru wamtoe nje kwa kukiuka kanuni za Bunge.
Kabla ya kuwaita askari hao, Mabumba ambaye ni Mbunge wa Dole alikuwa amemwamuru mara tatu Wenje akae chini, lakini hakutii akisema: "Nina jambo la dharura ambalo ni kwa maslahi ya Taifa".
"Sargent Ant Arms, mtoe nje mheshimiwa Wenje," alisema Mabumba na hapo askari watatu waliingia na kumtoa nje Wenje, tukio ambalo liliacha kukiwa hakuna utulivu bungeni.
Pamoja na kusindikizwa na askari wa Bunge, baadhi ya wabunge wa Chadema na NCCR Mageuzi walitoka nje wakimsindikiza Wenje.Walipofika nje ya ukumbi wa Bunge walianza kumlalamika kwamba, Mabumba ameshindwa kuongoza Bunge na kudai kuwa anaonyesha upendeleo wa wazi katika uendeshaji wa vikao vya chombo hicho.
Nje ya Ukumbi wa Bunge
Nje ya Ukumbi wa Bunge ilizuka tafrani nyingine iliyosababisha Mbunge Filikunjombe (CCM), kunusurika kupokea kichapo kutoka kwa wabunge wa Chadema na NCCR Mageuzi baada ya kuingilia mazungumzo yao wakati wanajadili suala la Wenje kutimuliwa ukumbini.
“Tatizo lenu ninyi wabunge wa Chadema mnaishia kuwa wabishi kila wakati, jambo ambalo linawapotezea heshima kwa wananchi,’’ alisema Filikunjombe na kuongeza: “Acheni mambo ya kitoto rudini ndani kuendelea na Bunge. Sio kila siku ninyi Chadema tu, watu wamewachoka.’’
Kauli ya ilikuwa kama kumwaga petroli kwenye moto, kwani kundi la wabunge wa Chadema na NCCR Mageuzi ambao kwa wakati huo wakiongozwa na Moses Machali (Kasulu Mjini NCCR), walimvaa kama nyuki mbunge huyo na kuanza kurushiana maneno makali.
“We mjinga kweli, hapa sio wabunge wa Chadema hata sisi wa NCCR-Mageuzi tupo tunachojadili ni maslahi ya nchi sio ushabiki wa vyama, toka hapa mshamba wewe,’’ alisema Machali.
Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Susan Kiwanga, alimwambia Filikunjombe aache hadithi za kijinga kwani wananchi wa eneo lake wanaporwa chuma, lakini yeye (Filikunjombe) anashindwa kuwatetea badala yake anarukia mambo yasiyomuhusu.“Tuondolee ujinga wako hapa, wananchi wako katika maeneo ya Liganga wanaporwa mali usiku na mchana unashindwa kuwatetea leo unapotuambia tuna akili ya kitoto, hivi unataka Watanzania wafe ili ninyi mshangailie,’’alisema Kiwanga.
Wabunge wengine waliomwandama zaidi Mbunge huyo ni, Machali (NCCR-Mageuzi), Peter Msigwa (Iringa Mjini-Chadema), Mariam Msabaha na Susan Kiwanga wote wa Viti Maalum (Chadema) ambao walimzingira mbunge huyo na kuanza kumrushia maneno ya kejeli.
Hali ilizidi kuwa mbaya baada ya wabunge wengine wa Chadema, Godbles Lema (Arusha Mjini), Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini) na Vicent Nyerere (Musoma Mjini) walipoingilia ugomvi huo na kutaka Filikunjombe awaombe radhi, lakini alikataa.Kama si busara iliyotumiwa na Mbunge wa Kondoa Kusini, Juma Nkamia (CCM) hali ingekuwa mbaya kwani idadi ya wabunge wa Chadema ilipozidi yalisika maneno kuwa mbunge huyo apigwe, ndipo Nkamia alipofika na kuokoa jahazi akimtaka Filikunjombe aondoke katika eneo hilo.
Maelezo ya Wenje
Wenje aliwaambia waandishi wa habari nje ya ukumbi wa Bunge kuwa kitu alichokifanya hakikustahili adhabu kama aliyopewa kwa kuwa alikuwa sahihi. '' Pale mimi nilikuwa sahihi kabisa kwani sikutaka kuzungumzia suala la Lissu bali nilikuwa nazungumzia suala la masilahi ya Watanzania wote. Ikumbukwe kuwa kuna samaki walioingizwa bila polisi kujua na sasa wako sokoni wananchi wanakula hiyo ni hatari, sasa mwenyekiti anasema kuwa nitoke hajui kanuni yule,'' alisema Wenje.
Mbunge huyo alisema kitendo cha Mwenyekiti kuamuru atolewe nje kwa amri ni kukiuka kanuni na kwamba hajui kwani aliposema suala la dharula ni pale kunapotokea vita si kweli. '' Kanuni ya 47 (1-3) ndiyo niliyotumia na inaniruhusu kabisa kuomba mwongozo huo, kwani wananchi wanaumia halafu tunaambiwa hadi kuwe na vita, kama si umbumbumbu ni nini basi," alihoji Wenje akiwa ameshika kitabu cha Kanuni za Bunge.Kwa upande wake Mbunge wa Arusha Mjini, Godbles Lema (Chedema) alisema kinachomsumbua Mwenyekiti ni kutokujua kanuni.
Chanzo cha mtafaruku
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) ndiye aliyeanzisha balaa ndani ya ukumbi wa Bunge baada ya kueleza kuwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Elimu), Kassim Majaliwa amesema uwongo bungeni.
Lissu alisema Majaliwa alipokuwa akijibu swali lake namba 313 kuhusu michango kwa wananchi, amedanganya kuwa wananchi hawalazimishwi kutoa michango hiyo na kusisitiza kuwa ana ushahidi unaothibitisha kwamba michango hiyo ni lazima.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haitumii nguvu katika kuwatoza wananchi michango hiyo, bali wanashirikishwa katika kuibua, kupanga na kuendesha miradi yao wenyewe,’’ alisema Naibu Waziri Majaliwa.Baada ya majibu hayo, Lissu alisimama na kulieleza Bunge kuwa Naibu Waziri alisema uongo huku akinukuu barua ya Mkuu wa Wilaya ya Singida iliyotolewa Mei 2,2005.
"Naomba kwanza niseme kwamba mimi namheshimu sana Mheshimiwa Naibu Waziri na kwa kweli huwa nakuwa mzito sana kusema Waziri amesema uongo. Lakini katika majibu haya naomba nitoe tamko kwamba, Mheshimiwa Naibu Waziri ameliambia Bunge hili uongo, na naomba nipewe nafasi ya kuthibitisha uongo huo leo leo, tena kwa ushahidi wa maandishi," alisema Lissu na kuongeza:
"Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niulize swali dogo la nyongeza".Kabla ya kuuliza swali hilo, Mabumba alisema: "Mheshimiwa samahani naomba... Mheshimiwa umekiri katika maelezo yako kwamba Waziri ameshindwa kukuridhisha, maelezo yake hayalingani na swali lako. Kwa hiyo hutakuwa na nafasi ya swali la nyongeza nimtake Mheshimiwa Waziri, No! Nikutake wewe unipe ukweli kuhusu suala hili".
"Tafadhali naomba uliambie Bunge hili ukweli wa suala hili na bahati nzuri umesema hapo ulipo uko tayari kutoa maelezo haya. Tafadhali nafasi ni yako," alihitimisha Mabumba.
Baada ya kupewa fursa hiyo, Lissu alisema Naibu Waziri, Majaliwa si kwamba ameshindwa kumridhisha na kusisitiza kuwa Majaliwa amesema uongo.
"Ndiyo maneno niliyoyatumia, …Naibu Waziri amesema uongo na uthibitisho ni kwamba mimi mwenyewe hapa Bungeni, nina barua ya tarehe 2/5/2005 iliyoandikwa na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Singida wakati huo, anaitwa Kepteni James Yamungu, ambayo kichwa chake cha habari kinasema; ‘Amri Na.1 ya Mkuu wa Wilaya ya Singida’ na inalazimisha wananchi kulipa michango".
Kabla hajamaliza kusoma barua aliyokuwa ameishika mkononi, Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi (CCM), aliomba mwongozo akisema kipindi hicho hakikuwa cha kutoa uthibitisho bali wabunge walipaswa kuendelea na mjadala wa maswali.Mwenyekiti alikubaliana na utaratibu huo, hivyo kumtaka Lissu awasilishe maelezo husika na kielelezo cha barua baada ya saamoja.
Hali ilibadilika
Hali hiyo ilimkera Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali, ambaye aliomba mwongozo wa Mwenyekiti na kutaka muda uongezwe kwa Lissu kabla ya kutoa uthibitisho wake.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, muda uliompa Mheshimiwa Lissu kutoa uthibitisho ni mfupi na kwa kuwa Lissu ni mbunge saa tano anatakiwa kuwa ndani ya ukumbi kuendelea na shughuli za Bunge naomba mwongozo wako,’’ alisema Machali.Mwenyekiti wa Bunge hakukubaliana na ombi la Machali na kusema kuwa hawezi kuomba mwongozo juu ya mwongozo hivyo akasema alichokizungumza ndicho kinatakiwa kutekelezwa.
Yalizuka mabishano kwa muda mrefu kati ya Machali na Mabumba ambayo yalimfanya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi, kuingilia kati na kuwataka wabunge kutokuchukulia jambo hilo kwa jazba.
“Unajua hapa wabunge hampaswi kuliona jambo hili kuwa ni kubwa kiasi hicho, kwani hata Lissu anaweza kuomba kwa maandishi kuongezewa muda na akaleta kwa wakati wake,’’ alisema Lukuvi.Hata hivyo, kulikuwepo na majibizano na ukali wa maneno kutoka kwa Mwenyekiti ambaye alimwambia Machali: “Unaongea maneno kama tuko klabu cha pombe, unatakiwa kujiheshimu na kuzungumza kwa utaratibu mheshimiwa mbunge’’.
Wakati hayo yakiendelea, Wenje alisimama akiomba mwongozo lakini alimriwa kukaa chini na baada ya kukaidi, Mabumba aliamuru atolewe nje.
Mabumba ajitetea
Akiahirisha kikao cha bunge jana mchana, Mabumba alitumia takriban dakika kumi kujitetea kuhusu hatua yake ya kumtoa nje Wenje kwamba, alifanya hivyo kwa mujibu wa Kanuni za Bunge baada ya mbunge huyo kukaidi amri yake.
"Kwa mujibuwa Kanuni za majadiliano, mtakubaliana na mimi kwamba, Mheshimiwa Wenje alikiuka kanuni hizo maana alikuwa akibishana na kiti na mimi sikuwa nimempa ruhusa ya kuzungumza," alisema Mabumba huku akiwataka wabunge kuzingatia kanuni za Bunge.Alisema kwa mujibu wa kanuni hizo, Wenje alipaswa kutohudhuria kikao kizima cha jana kama adhabu, lakini kwa kuwa alitii amri ya kutoka nje, alimpunguzia adhabu hiyo hivyo anaruhisi kuhudhuria kikao cha jana jioni.
"Kwa mujibu wa Kanuni zetu, Wenje alipaswa kukosa kikao cha siku nzima ya leo (jana), lakini kwa kuwa ametii amri ya kutoka nje na mpunguzia adhabu hiyo anaweza kurejea ukumbini kuhudhuria kikao cha jioni kuanzia saa 11," alisema Mwenyekiti huyo wa Bunge.Hata hivyo, alisema katika mazingira aliyomkatalia Wenje kutoa hoja yake, alikuwa sahihi, kwani haikuwa rahisi kufahamu kwamba hoja ya mbunge huyo ni tofauti na kile kilichokuwa kikiendelea wakati huo.
"Wakati mwingine mazingira huwa ni magumu sana, ni kwa vipi mtu angeweza kufahamu kwamba alichokuwa akitaka kusema Wenje ni tofauti na hoja ya Mheshimiwa Lissu, ilikuwa vigumu sana," alijitetea Mabumba
Wakati hayo yakiendelea,utoto mwingine umejitokeza Bungeni kama inavyoripotiwa katika habari ifuatayo
Saini ya Pinda yaghushiwa bungeni
Wednesday, 27 July 2011 21:32
Neville Meena na Habel Chidawali
VITUKO vya wabunge ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania vimezidi kuongezekana; sasa baadhi ya wabunge wanadaiwa kugushi sahihi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwa malengo ambayo bado hayajafahamika.
Kitendo cha kugushi sahihi ya Waziri Mkuu ndani ya ukumbi huo kunawaathiri zaidi wabunge wa upinzani, hasa wa Chadema ambao wamekuwa wakipelekewa ‘meseji’ za kuwadanganywa kuwa wanaitwa na Waziri Mkuu.
Juzi jioni kabla ya kikao cha Bunge kuahirishwa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alialazimika kuomba mwongozo wa Mwenyekiti kukemea kitendo hicho alichokiita kuwa ni cha kihuni.
Lukuvi asimama mara tu baada ya Bunge kumaliza kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika ambayo yalikuwa yalijadiliwa kwa siku mbili mfululizo.
“Naomba mwongozo wako kwamba, humu ndani imejitokeza tabia ambayo naona imezoeleka kidogo. “Kuna watu wanawaandikia wenzao meseji za kuwasumbua kwamba wanaitwa na mtu fulani halafu wanaweka sahihi na wakati mwingine haitokei,” alisema Lukuvi na kuongeza:
“ Nimeisikia hayo wiki iliyopita, lakini leo Mheshimiwa Joseph Selasini (Chadema) ameitwa kwa meseji inayodaiwa kuwa imesainiwa na Waziri Mkuu na hii nyingine ameitwa Mheshimiwa Leticia Nyerere (Chadema) kwamba anaitwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu wakazungumze maneno ya maana, lakini Waziri Mkuu hana habari na wamegushi sahihi yake,’’ alisema Lukuvi.
Waziri huyo wa Sera, Uratibu na Bunge alitaka mwongozo wa Mwenyekiti kama jambo hilo linaweza kufanywa na Wabunge, ndani ya Bunge kwa wabunge kugushi taarifa ambazo alisema nyingine na zinatisha.
Mwenyekiti wa Bunge George Simbachawene alikiri kuwepo kwa tabia hiyo ndani ya ukumbi wa bunge ambayo imekuwa ikifanywa na baadhi yao na kamba inaonekana kuota mizizi.
“Nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri, ni kweli kuna mtu amefanya hivyo na karatasi aliyoiandika ipo hapa, Kwa kweli siyo nzuri haionyeshi kama tupo serious (makini) na kazi,” alisema Simbachawene na kuisoma:
“Amemwandikia hivi, Mheshimiwa Joseph Selasini Mbunge, samahani nakuomba mara moja tuje tujadili suala moja muhimu ambalo ningependa kujua kutoka kwako. Ahsante. Mizengo Peter Pinda na sahihi”.
Simbachawene alisema Selasini alipokwenda kwa Waziri Mkuu alishindwa kusaidiwa kwa kuwa wakati huo Waziri Mkuu alikuwa makini kusikiliza hotuba ya Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika katika majumuisho yake.
Hata hivyo, mwenyekiti huyo alisema uongozi wa Bunge utafanya kila liwezekanalo kubaini ni nani mwenye tabia hiyo na kwamba ili kukomesha vitendo hivyo