21 Jun 2013


Kwa mara nyingine, Tanzania yetu imeshuhudia tukio la kigaidi lililopelekea vifo vya watu wasio na hatia. Jumamosi iliyopita, wakazi wa jiji la Arusha walikumbwa na janga la kigaidi baada ya bomu kurushwa katika mkutano wa kampeni za CHADEMA kwa ajili ya uchaguzi wa madiwani.
Kwa hesabu za haraka, tukio hilo la kigaidi ni la pili kutokea jijini Arusha kwa siku za hivi karibuni, na la tatu tukijumuisha na lile la mauaji ya Padre Evaristus Mushi huko Zanzibar.
Cha kusikitisha ni kwamba hadi wakati ninaandika makala hii, haki haijatendeka kwani licha ya kukamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa WATUHUMIWA wawili, mmoja kwa tukio la Zanzibar, na mwingine kwa tukio la kanisani Arusha, mwenendo wa kesi hizo na hisia miongoni mwa wananchi mbalimbali unaleta hisia hiyo ya haki kutotendeka na/au kuonekana imetendeka.
Lakini hata kama haki ingekuwa imetendeka katika matukio hayo mawili ya mwanzo, ukweli kwamba leo hii tunaongelea tukio jingine la kigaidi unamaanisha kitu kimoja tu: taasisi zetu za usalama zimezidiwa uwezo wa kukabiliana na tishio hilo linaloonekana kuzidi kukua la ugaidi. Niliwahi kuandika huko nyuma kuhusu mapungufu kadhaa katika taasisi zetu za usalama ambayo ninaamini kuwa yalipelekea taifa letu kushuhudia majanga hayo.
Na kama nilivyobashiri, japo niliomba Mungu aepushie mbali, kwamba pasipo hatua za haraka tunaweza kushuhudia vitendo vya kigaidi vikiendelea, kwa bahati mbaya (au makusudi?) mwishoni mwa wiki tumeona bayana mwendelezo wa matukio hayo.
Na japo nisingependa iwe hivyo, kuna uwezekano wa hali hiyo kuendelea kwa sababu tuliowakabidhi dhamana ya kupambana na ugaidi wameshindwa jukumu hilo muhimu.
Lakini kwa upande mwingine, tukizungumzia ugaidi, hisia za haraka zinaweza kuelekezwa kwa kesi inayomkabili Mkurugenzi wa Usalama wa CHADEMA, Wilfred Lwakatare, ambaye licha ya kuachiwa kwa dhamana na mahakama, Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai ameonyesha nia ya kupinga dhamana hiyo akitaka kiongozi huyo wa CHADEMA arejeshwe rumande.
Labda msomaji unaweza kujiuliza kama mie, hivi kipaumbele cha taifa letu kwa sasa ni kuendeleza kesi hiyo ‘ya kisiasa’ au kukabiliana na matishio halisi ya ugaidi ambayo tayari yameshapoteza maisha ya Watanzania wenzetu?
Haihitaji upeo mkubwa wa kufikiri kubaini kuwa kesi inayomkabili Lwakatare ni ya kisiasa zaidi, na ambayo kimsingi inapaswa kufutwa kwa sababu baadhi ya wabunge wa CCM wameshaitolea hukumu kwamba sio tu Lwakatare ni gaidi bali pia CHADEMA ni chama cha kigaidi.
Tukiweka kando ‘ishu’ ya Lwakatare na tuhuma za CCM kuwa CHADEMA ni chama cha kigaidi, binafsi nina maswali kadhaa ambayo labda kwa kuyaweka hadharani yanaweza sio tu kutupatia majibu lakini pia kuamsha tafakuri mpya kuhusu hatma ya nchi yetu kiusalama.
Baada ya matukio ya tukio la ugaidi huko Zanzibar na hatimaye Arusha, baadhi ya wananchi tulishauri viongozi husika serikali wawajibishwe. Hao ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi, Inspekta Jenerali wa Polisi Said Mwema, na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Rashid Othman. Swali: kwanini hadi sasa linatokea tukio la tatu la kigaidi viongozi hao hawajawajibishwi?
Katika hili, ni vigumu kukwepa kumtupia lawama Rais Jakaya Kikwete kwani yeye ndiye aliyewateua na pia ndiye mwenye mamlaka ya kuwawajibisha, tukiamini kuwa watendaji hao wamegoma kujiwajibisha wenyewe. Je itakuwa makosa kuhisi kuwa Rais Kikwete bado ana imani nao licha ya mapungufu yao ya wazi ya kiutendaji kazi?
Kwa vile watendaji hao wamegoma kuwajibika, na Rais haelekei kuwa na mpango wa kuwawajibisha, na kibaya zaidi, tayari kumeshatokea matukio matatu ya kigaidi, kwanini tusihisi kuwa usalama wa nchi yetu unazidi kuwa hatarini kwa sababu hakuna jitihada zozote za makusudi za kuhakikisha kuwa matukio ya ugaidi sio tu yanazuiwa bali yanakomeshwa kabisa?
Lakini pia tukio hilo la majuzi huko Arusha limekuja wakati Tanzania ipo kwenye ‘vita ya maneno’ na Rwanda kufuatia ushauri (wa nia njema tu) wa Rais Kikwete kwa Rwanda kuwa itafute suluhu na waasi wa kundi la FDLR ambao wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994-5.
Pamoja na kuafikiana na ushauri wa Rais Kikwete, lakini hivi nchi yetu haionekani ‘kituko’ kwa ‘kujifanya washauri wa amani na usalama wa Wanyarwanda’ ilhali sie wenyewe tunaishi kwa hofu ya matukio ya ugaidi ambayo hayana dalili ya kutotokea tena?
Kadhalika, nchi yetu imeamua kwa nia nzuri tu kuunga jitihada za Umoja wa Mataifa kusaka amani huko DRC. Lakini, pamoja na nina hiyo nzuri, hatuonekani ‘watu wa ajabu’ kwa kuelekeza nguvu zetu kusaka amani huko ilhali kwa mujibu wa matukio ya hivi karibuni, magaidi ‘wapo huru’ kuua Watanzania at will (watakavyo)?
Kingine kilichonikera sana ni ukweli kuwa lilipotokea tukio la ugaidi kanisani huko Arusha, tuliambiwa kuwa Rais Kikwete ameamua kukatisha ziara yake huko Falme za Kiarabu ili kuja kuwafariji wahanga wa tukio hilo. Muda huu ninapoandika makala hii, Rais yupo hapa Uingereza kuhudhuria mkutano wa G8.
Hivi kuna sababu zozote zinazomfanya Rais asirejee huko nyumbani kutoka na tukio hili? Je tukio la ugaidi kwenye mkutano wa CHADEMA huko Arusha lina umuhimu mdogo kuliko lile la kanisani ambalo lilimlazimu Rais kuahirisha ziara yake (japo kuna wanaodai alikuwa ameshamaliza ziara hiyo)?
Majuzi, akiongelea tukio hilo la ugaidi, Rais alidai, (namnukuu), “Mimi siamini kuwa Watanzania au wafuasi wa vyama vya siasa wanachukiana kiasi cha kufanyiana matendo ya unyama wa aina hii. Naamini kuwa hiki ni kitendo cha mtu au watu wasioitakia mema nchi yetu, watu ambao wanatafuta kila sababu ya kupandikiza chuki miongoni mwa raia, au makundi ya raia, ili nchi yetu iingie kwenye machafuko makubwa.”
Swali, je Kikwete haamini hivyo kutokana na hisia zake tu au ndio taarifa za kiusalama anazopatiwa kila siku zinavyomweleza? Lakini hata kama ni sahihi Rais kuamini hivyo, hivi kauli za Mwigulu Nchemba ambaye kuna ushahidi wa video unaomwonyesha akiwaambia wananchi waliokuwa wakimsikiliza kuwa wasipoichagua CCM watakufa na baada ya siku moja tangia atoe kauli hiyo kweli watu waliuawa kwa bomu?
Lakini pengine katika kuonyesha ‘ombwe’ la kiuongozi katika serikali ya Kikwete, wakati Rais anasema hayo, tamko la serikali lililotolewa na Waziri William Lukuvi linahitimisha kuwa, (namnukuu), “Katika siku za karibuni, zimekuwepo jitihada za makusudi za baadhi ya vyama vya siasa, makundi ya kijamii na watu binafsi kupandikiza chuki kwa raia dhidi ya vijana wetu wa Jeshi la Polisi, kuwafanya raia wawachukie askari, kuwafanya raia wasiwaamini askari, kuwafanya raia wasiwape ushirikiano askari na hatimaye kuwa na taifa ambalo halitawaliki.”
Sasa hapo tumwamini Rais Kikwete anadai haamini kuwa Watanzania au wafuasi wa vyama vya siasa wanachukiana kiasi cha kufanyiana matendo ya unyama wa aina hii, au Waziri Lukuvi ambaye anasema kwa hakika kuwa matukio ya ugaidi kama hilo la majuzi huko Arusha ni matokeo ya jitihada za makusudi za baadhi ya vyama vya siasa, makundi ya kijamii na watu binafsi kupandikiza chuki kwa raia dhidi ya polisi?
Lakini wakati jeshi la polisi likitangaza tume ya kuchunguza tukio hilo Arusha na kutangaza zawadi ya shilingi milioni 100 kwa atakayetoa taarifa kuhusu wahusika, tumeshuhudia dhihaka kubwa ikifanywa na Spika wa Bunge Anne Makinda kwa kutoona umuhimu wa kuahirisha bunge angalau kwa siku moja kwa heshima ya Watanzania wenzetu waliokufa au kujeruhiwa katika tukio hilo.
Inaelezwa kuwa Spika Makinda ameshindwa japo kumtumia SMS Mwenyekiti wa CHADEMA (Taifa) Freeman Mbowe kwa janga hilo (lakini Rais Kikwete anadai haamini kama kuna chuki baina ya wafuasi wa vyama vya siasa).
La kuchukiza zaidi ni ‘uhuni mkubwa’ uliofanywa na Katibu Mwenezi wa CCM Nape Nnauye ambaye amenukuliwa akidai kuwa inawezekana CHADEMA wanahusika na tukio hilo la kigaidi. Hii ni zaidi ya chuki ya kisiasa (ambayo Bosi wa Nape, Rais Kikwete, anaamini kuwa ipo); huu ni unyama wa hali ya juu. Kuna haja gani ya jeshi la polisi kuunda timu ya uchunguzi au kupoteza fedha za umma kwa dau hilo la shilingi milioni 100 ilhali tayari akina Nape wanawajua wahusika?
Nimalizie makala hii kwa swali hili, kwanini IGP Mwema adai jeshi la polisi litamchunguza Mwigulu kwa kauli yake kuwa wananchi wasipoichagua CCM watakufa (na kweli kesho yake baadhi wakauawa au kujeruhiwa kwa bomu) lakini YUPO HURU HADI MUDA HUU ilhali Lwakatare alikamatwa kwa tuhuma ‘nyepesi tu’ na sasa jitihada zinafanywa arejeshwe rumande baada ya kupewa dhamana?
Sio tu kuwa tunaelekea kubaya bali tumeshafika kubaya. Rais Kikwete alisisitiza hivi karibuni kuwa nchi haijamshinda. Je, kwa mwenendo huu wa magaidi kuangamiza maisha wanavyotaka tusemeje?


0 comments:

Post a Comment

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.