11 Jul 2013

WIKI iliyopita kulijitokeza video fupi mtandaoni inayomwonyesha Rais Jakaya Kikwete akizungumza kuhusu safari zake za mara kwa mara nje ya nchi. Kwa kifupi, katika video hiyo, Rais Kikwete alitetea safari hizo, huku akidai kwamba “hakuna nchi duniani ambayo mnaiendesha hamtoki nje, mmebaki palepale na mkadhani mtapata maendeleo...hiyo ni isolation...”
Aliendelea: “Suala kubwa ni mnakwenda nje kwa ajili gani, mnakwenda tu kutembea au mna malengo maalumu mnayafuata ambayo baada ya pale mnafuatilia?...”
Kadhalika, alieleza kwamba (kwake yeye) anadhani kuwa safari zote zimekuwa na umuhimu, na hatarajii kuwa Rais atakayefuata atasema Kikwete alikuwa anatembea sana, mie sasa sitembei... “ukitoka ndiyo wanakufuata. Na sisi masikini hivi nani atatufuata? Kwa shida gani?”
Vilevile Rais Kikwete alisema kuwa hata katika mataifa makubwa, marais wanatembea na kutolea mfano safari za marais Xi Jinping wa China na Barack Obama wa Marekani.
Naomba nipingane na maelezo hayo ya Rais Kikwete kwa sababu kuu moja. Kinacholalamikiwa mno kuhusu safari zake, ni ukweli kwamba ni nyingi mno kiasi kwamba pengine hata faida inayopatikana katika baadhi ya safari hizo, inaweza kutumika kugharamia safari nyingine, na huo ni mzigo kwa mlipakodi masikini wa Kitanzania.
Kama safari nyingi ndiyo chachu ya maendeleo, basi leo hii Tanzania yetu ingekuwa mbele kimaendeleo zaidi ya nchi kama Rwanda, Botswana, Ghana au hata Afrika kusini, kwa sababu marais wetu wamefanya safari za nje nyingi kuliko viongozi wa nchi hizo.
Ingawa ni kweli kwamba marais wa mataifa makubwa kama China na Marekani pia wanafanya safari za nje, lakini safari hizo ni chache ikilinganishwa na za Rais wetu, licha ya nchi hizo kuwa na uwezo mkubwa wa kiuchumi kiasi kwamba yayumkinika kuamini kuwa safari za viongozi wake zina athari ndogo tu kigharama (kama ipo at all).
Kadhalika, safari za viongozi kama Jinping na Obama, huenda sambamba na kusainiwa kwa mikataba mbalimbali ambayo huwa na manufaa zaidi kwa nchi hizo kuliko nchi zinazotembelewa.
Kimsingi, baadhi yetu tunazitafsiri safari hizo za viongozi wa mataifa makubwa kama zile zilizokuwa zinafanywa na ‘watangulizi wa ukoloni, kwa minajili ya kusaka malighafi za viwanda vyao, masoko ya bidhaa zao na sehemu za kuweka ‘reserve army of labour.’
Naomba isieleweke kuwa safari zote za Rais Kikwete hazina manufaa kwa taifa letu, la hasha! Kinachozua malalamiko ni wingi wa safari hizo, na ukweli kwamba mara nyingi si tu wananchi hawafahamishwi waliomo kwenye safari husika, bali pia hawajulishwi mafanikio ya safari hizo.
Ni nadra mno kusikia kwa mfano, Rais Kikwete akisema “kutokana na ziara yangu katika nchi fulani, tumeweza kupata soko la mchele tunaozalisha kwa wingi kule Ifakara na Mbeya.”
Sawa, sisi ni masikini na tunalazimika kuomba misaada kwa ajili ya maendeleo yetu. Lakini umasikini huo pia ni sababu ya kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, ikiwa ni pamoja na safari hizo za mara kwa mara ambazo kwa hakika ni mzigo mkubwa kwa taifa letu lenye uchumi duni.
Ingawa katika mazingira ya kawaida, ili utembelewe sharti nawe uwe unatembelea wenzako, kauli ya Rais Kikwete kwamba ‘ukitoka ndiyo wanakufuata’ inaweza kukinzana na ukweli kwamba wengi wa viongozi wanaokuja kututembelea, wanakuja kwa ajili ya maslahi ya nchi zao, na hata Rais Kikwete asingesafiri, bado kina Jinping na Obama wangekuja tu kwa vile wanatambua utajiri mkubwa wa rasilimali tulizonazo, ambazo kimsingi zingeweza kabisa kupunguza safari za mara kwa mara za nje ‘kutafuta maendeleo.’
Lakini pia kama nilivyoandika katika makala yangu ya toleo la wiki iliyopita ndani ya jarida hili, tatizo letu kubwa si upatikanaji wa misaada, bali matumizi sahihi ya misaada hiyo. Kwa hiyo, hata kama Rais Kikwete atakuwa safarini nje kila wiki na akarejea na rundo la misaada, itakuwa ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu iwapo mianya ya kufilisi misaada hiyo haitazibwa.
Katika lugha ya mfano, yayumkinika kuzifananisha safari za mara kwa mara za Rais Kikwete na zile za mtu ambaye anakwenda kuchota maji kisimani mara kadhaa, lakini akirudi nyumbani anayaweka maji hayo kwenye pipa linalovuja.
Kwa upande mwingine, kama tafsiri yetu ya ziara kubwa kama ya Jinping na Obama ni matokeo ya safari za mara kwa mara za Rais Kikwete nje ya nchi, basi ni wazi kwamba tunaweza kuishia kujigamba tu kuhusu ziara hizo pasi matunda yake kuonekana kwa mwananchi wa kawaida.
Pamoja na nchi zao kuwa na uhusiano mwema na Tanzania yetu, na hapa haimaanishi kwamba uhusiano huo mwema ni matokeo ya safari za Rais Kikwete, viongozi hao wa China na Marekani wanatambua uwepo wa rasilimali lukuki katika nchi yetu, hususan gesi na mafuta, na hawataki waachie fursa hiyo muhimu ya kujinufaisha kiuchumi.
Na ingawa sisi tunaweza kunufaika kutokana na ziara hizo, lakini tatizo letu kubwa ni wale mchwa wanaosubiria misaada ianze ‘kudondoka’ ili wamalizie mahekalu yao, waongeze idadi ya magari yao ya kifahari, na hata kuongeza idadi ya ‘nyumba ndogo’ zao.
Nihitimishe makala haya kwa kusisitiza kwamba tunaweza kupiga hatua kimaendeleo pasi na haja ya Rais wetu kusafiri mara kwa mara kwenda nchi za nje. Tuna Balozi zetu huko nje ambazo laiti zingetumika ipasavyo kutangaza vivutio tulivyonavyo, sambamba na kusaka fursa za kibiashara kwa nchi yetu, basi kusingekuwa na haja kubwa ya safari hizo za ‘kusaka maendeleo’ nje ya nchi.
Sababu za kupiga hatua kimaendeleo bila safari nyingi za nje, tunazo. Uwezo wa kupiga hatua kimaendeleo tunao. Kinachokosekana ni nia ya dhati ya kuiona Tanzania yetu ikipiga hatua kimaendeleo. Penye nia pana njia!


1 comment:

  1. nikweli kabisa katika imakala ulichokiandika ilikuwa ngumu kuona misaada au uchumi kukua zaidi tulion ukishuka na kuserereka kama maji yako kwenye mlima

    ReplyDelete

Categories

Blog Archive

© Evarist Chahali 2006-2022

Search Engine Optimization SEO

Powered by Blogger.